Shairi: Karibu Ngomani

Idd Ninga

Verified Member
Nov 18, 2012
4,902
2,000
KARIBU NGOMANI
Manju utamu wa ngoma, ingia ndani ucheze
Kuicheza ukigoma, siyo marimba ukaze
Ngoma siyo homa homa, mdundo tusiuwaze
Karibu tena ngomani, uone hali halisi.

Wale walojua ngoma, waganga na waganguzi
Sindano uliwachoma, ukawapa wauguzi
Hawajui ukasema, eti wao wapuuzi
Karibu tena ngomani, uone hali halisi.

Manju hukwepi lawama, hili lataka ujuzi
Lahitaji kuchutuma, si nguvu na ubaguzi
Mbwa kugeuka kima, hatofanana na mbuzi
Karibu tena ngomani, uone hali halisi.

Twawaza lijalo Juma, kwa jinsi ulivyokaza
Tatizo letu kusema, twaogopa tukiwaza
Mdomo tukiachama, viboko watucharaza
Karibu tena ngomani, uone hali halisi.

Ingali bado mapema, hadhira unaiuza
Kuipigania sima, ni wao kuwaumiza
Hapa wakataa jema, kijiji wakiunguza
Karibu tena ngomani, uone hali halisi.

Manju kuicheza ngoma, ni wazi unapuuza
Usiwaseme waroma, eti ngoma waikuza
Tunajuta tumekoma, kiti tulipokiuza
Karibu tena ngomani, uone hali halisi.

Tungelijua kusoma, majibu tusingejaza
Eti tatizo kuhema, dunia waishangaza
Mwanzo tuliweka koma, ona unatuburuza
Karibu tena ngomani, uone hali halisi.

SHAIRI-Karibu Ngomani.
MTUNZI-Idd Ninga,Tengeru Arusha
+255624010160
iddyallyninga@gmail.com
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Similar Discussions

Top Bottom