Kuibuka na kuzama kwa John Okello. Kutoka kwenye kitabu cha kwaheri ukoloni, kwaheri uhuru!

BuletAngle

JF-Expert Member
Apr 15, 2017
690
552
Mzee Selemani

John Okello, hapa nakumbuka walitoka watu, wametoka watu hapa wakenda Pemba. Kwa hali ya kiuchunguzi. Je, Pemba tunaweza kuwapata wenzetu tukaja kusaidiana hapa? Wakatupa motisha? Kule nakumbuka mtu wa mwanzo aliekwenda kule alikuwa Ibrahim Makungu. Alikwenda na Jaha Ubwa, Mdungi Usi. Watu watatu hao. Sasa walipokwenda kule, sasa wale Ma Afro-Shirazi magogo wa kule Pemba, wakawauliza, jamani e, vipi tunaweza kumpata kijana mshupavu huku wa kutusaidia hii kazi yetu sisi, au vijana washupavu hivi tunaweza kuwapata?

Sasa alikuwepo mzee mmoja Mkoani. Huyu akasema jamani mnajuwa nyinyi? Hapa yuko Mganda mmoja anachonga mawe huko. Huyu kijana naona kachangamka sana. Kachangamka sana! Sasa hatujuwi utaratibu wake hatuujuwi vipi. Sasa hapo mtu kama huyo sio anaingiwa tu ovyo ovyo. Panataka mbinu. Wakarudi wale kwanza. Kufika huku Mfaranyaki na Washoto wakasema “twende tukachonge mawe.” Wakenda Pemba. Kufika Pemba, wakaanza shughuli ya kuchonga mawe, sasa yule akiwa kama ni fundi wao. Wamechonga mawe pale, wamechonga, wamechonga, ile data wakamuelezea yule. Hii kazi gani hii? Utumwa gani huu? Pangelikuwa na wanaume wa kuipinduwa hii nchi…1

Lengo walilolikusudia ni kumvisha blangeti Okello kwa sababu yeye ni mgeni. Si mwenyeji. Sasa sisi tukitaka kutafuta sababu ya kujifunika tumvishe huyu. Huyu si Mtanganyika huyu. Ni Mganda! Mbali huko. Kwasababu leo Mtanganyika hapa akilizuwa balaa hili lazima atajulikana “Oh! Mwalimu umefanya chokochoko.” Lakini huyu, huyu anatoka Uganda huyu. Sasa watu watakuja kumuuliza Obote “vipi mambo haya?” Wewe Obote vipi mtu wako anakuja kufanya machafuko nchini kwetu. Sultani sasa atakuwa atapambana na Obote. Sio na Tanganyika.2

Bwana yule [Okello] kumueleza vile akasema “nyinyi wapumbavu, sisi tunazo dawa tunaweza kwenda kuzichukuwa hapo kwa Mau Mau, tukafanya mambo hapa yakajulikana yakawa kweli.” “Ah ewe bwana huwezi bwana. Mambo gani hayo? Unatufanyia kitu masihara tu bwana.” Akasema “bwana e hayo mambo yapo, tunaweza kuyafanya.” “Kweli?” “Kweli.” “Hebu fanya.” Akatoka Okello, akenda Nairobi. Kufika Nairobi akakutana na Mau Mau, wakampa dawa. Bwana eh, mnaweza kulifanya hili nyie lakini dawa hizi shote wote watakaoshiriki kwenye mapinduzi dawa hii sote mmoja mmoja uwapake. Unavowapaka dawa hizi, ina maana nyinyi mnawapumbaza wale watu wasijuwe. Japo kama watajuwa watadharau. Watadharau dharau. Okello akarudi Pemba. Kurudi Pemba kamkuta Washoto kaja Unguja. Kule kamkuta Mfaranyaki, vipi? Nimeleta. Umeleta nini? Hizi hapa. Dawa. Akamwambia sasa bwana wewe inabidi sasa tuondoke mimi na wewe twende Unguja. Wakaondoka, wakaja zao hapa.

Okello akakaa na mzee mmmoja sehemu za Bambi huku, pamoja na dawa zake. Kutwa nzima humkuti na mazungumzo na watu. Imekwenda kwenda ikabidi, akina Sefu Bakari, akina Natepe, akina Ingine, ndio wakaanza kusema, unajuwa nyie, sisi tumeshapata mtu wa kumfunika blangeti bwanaa! Vipi? Huyu hapa. Tumpeni cheo huyu. Tukimpa cheo huyu kwani iwe nini? Mambo yetu yakikaa sawa si basi! Si tunamwambia “chukua chako hichi, kwaheri.”

Okello sogea, vipi bwana wewe, masuala ya huyu Washoto na huyu Mfaranyaki. Mmekubaliana vipi nyie? Nimewaambia hakuna uzito. Lakini mimi nimewaambia, ngojeni mimi nikachukuwe dawa. Mimi nimechukuwa dawa. Zipo. Dawa hizi masharti yake? Akasema hizi dawa bwana, hizi dawa zinako-rogwa kwenye maji, wale watu siku ile khasa ya mapambano, wanamwagiwa mwagiwa hawa, wanajipakaa pakaa, tayari, halafu kuna dawa moja watu wanakunywa, wakishakunywa hiyo, suala limekwisha. Watu wanaondoka wanakwenda kwenye mapambano. Washakingika. Lakini shoti mfanye ngoma. Ngoma tunaweza kufanya fete, kubabaisha. Watakapokuja watu mjini kutoka mashamba watakuwa hawajulikani. Watakuwa wanaonekana wanakwenda kwenye sherehe, starehe na furaha.

Baada ya kupitishwa watu kuja kunako fete, hapo sasa ndo Kisasi na Okello, Mfaranyaki, huyu Kassim Hanga pamoja na Hasnu Makame waliambiwa “kaeni pembeni kabisa! Pembeni kabisa nyinyi. Msiingie huku, tuwachieni sisi kwa sababu nyinyi ndo chimbuko.”

Suala hili aliyekuwa akilishughulikia Kaujore. Kumalizika “jamani tumeshamaliza.” Sasa katika hao mmoja ile dawa akawa hakuipata, kama utaskia habari za chinichini, yuko mmoja alitoka Bomani akakimbia moja kwa moja mpaka Ndagaa akenda akasema “jamani huko mjini serikali imekwisha pinduliwa.” Ile dawa kwa sababu hakuipata. Lakini aliepata dawa bwana, hakupepesa hapa na pale. Hakupepesa hapa na pale. Khofu hamna. Mtakuwa khofu hamna. Hamuogopi kitu chochote. Hamuogopi kitu chochote. Na kwa kweli bwana. Leo we ufikirie, kweli tizama, mtu kuvunja mlango wa nyuma wa Bomani. Yule Kamanda yuko pale, watu wanapita pale, Kamanda yuko pale, hakuna anayemuona, mpaka kuja kumkabili sentry [askari wa zamu]. Si mchezo. Hapa kiinimacho hiki kilipita kikubwa sana. Hata ikabidi mambo yakaja yakaingia sura.

[Kwa upande wa Umma Party] Hanga ilikuwa kama ni kitu geresha kwa Abrahmani Babu. Siasa za Babu zilikuwa za Kikoministi za Kichina. Juu ya kuwa Mkoministi na siasa zake za Kichina, Hanga alisema, huyu vyovote itakavokuwa, wale ni wenzake. Kwa vyovyote itakavokuwa, damu nzito kuliko maji.3 Alisema hivo. Usifikiriye kama leo huyu Babu apigwe, Waarabu hawakubali. Hawatokubali, kwa sababu itakuwa aibu kwao. Watasema “ala! kwanini Mwarabu apigwe? Kaasi tu huyu chama cha Hizbu, anapigiwa kwanini. Hapana.” Hilo suala kwanza ndoto ya kumueleza Babu hamna. Asielezwe kwanza huyu. Babu, Ali Mahfudhi, na wenzao, hakuna suala namna hilo. Hii yote mambo ya Manamba, walikuwa hawayaelewi. Katika vikao vyote vilivopita hakuna mmoja aloshiriki katika Makomred. Hata sku moja.

Kwa sababu Komred siku ya Jumapili ndipo alivochukuwa bunduki kuumiza wenzake kujificha macho. Kujionyesha yeye kwa Mzee Karume au kwa Afro-Shirazi, yeye yuko bega kwa bega na Afro-Shirazi. Kujiaminisha. Kujikubalisha. Kwamba mimi hawa Waarabu sina imani nao. Na aliwaumiza kweli Babu. Jumapili bwana ndipo wale walipojuwa, mimi nikifanya hivi madam ile serikali imeshapinduka, wadhifa ntapewa na mzee Karume.

Huyu anafaa kupewa posti [cheo] kwa sababu aligombana na Hizbu na ataweza kutumika kuwazuwia kina Hanga na Othman Sharifu. Kilichokuwa kinatendeka mpaka Jumamosi usiku walikuwa hawakijuwi. Kabisa. Komred hakijuwi kabisa kwa sababu Hanga alizungumza “bwana, mtu damu nzito kuliko maji.” Sasa ukija ukitizama, Babu, Ali Mahfudhi, Badawi, nk, hawa wamezaliwa mshipa wa Kiarabu. Wazee wao Waarabu. Sasa leo mkija kuwazungumzia watakuwa na fikra hawa wawaze “je, wanotaka kupinduliwa hawa Waarabu. Sasa vita vikitokezea vitakuwa va Waarabu. Je, sisi tutanusurika?” Ikabidi pakafunikwa hapo. Wasiambiwe. Jumapili, kweli Komred walikuja Raha Leo kifua mbele.

Okello na watu wa Mkello

Family za Manamba wao wanajuwa. Lakini kwa sasa hivi wengi Wazanzibari wanajuwa kwamba Wamakonde bwana wameshiriki mapinduzi hapa. Wanafahamu kwamba wameshiriki na ndo watendaji wakuu hawa. Sasa familia ya Kimakonde au familia ya Kizanzibari, nadhani kiungo hiki madamu kinajulikana, sifikirii kwamba leo Mmakonde ataambiwa “wewe ndo muuwaji.” Au sifikirii atoke Mmakonde kumwambia Mzanzibari kwamba “wewe ndio muuwaji.” Sifikirii. Manake akisema kwamba “wewe ndio muuwaji” Mmakonde na yeye atasema “skiliza, mimi unaniambia muuwaji, huwezi kupewa cheo cha MBM [Memba wa Baraza la Mapinduzi], wewe lazima ulishiriki, sasa baba yako? Si alishiriki? Sasa ikiwa kama baba yako alishiriki basi na mimi baba yangu alishiriki, wewe na mimi basi jungu letu moja.” Kwa sababu nini, wazee wetu ndo waliokombowa kitu hiki. Sisi watoto haikutuhusu kitu. Ukinisema hivo, na mimi ntakwambia “na wewe!” Utata huu hapa itabidi utaondoka kwa sababu wote hawa wanajuwa. Hii hapa patakuwa hapana ngonjera. Hilo ndo liliopo.

Shina ndo lilotufanya sisi kutukusanya mahala pamoja. Baada ya hilo shina lenyewe kutueleza kwamba, jamanii, wasaidieni wenzenu kule hawawezi kufanya kitu. Kwanini wasifanye kitu? Akauliza yule bwana, Victor Mkello. Kwanini wasifanye kitu? Ndio. Kwa sababu ni jamaa ni watu walokuwa wanaelewana. Jamii moja hii. Mimi nilitembelea, nikaitazama Zanzibar nikenda nikaona, ndio Wazanzibari hawa, hawa Waswahili, na hawa Waarabu, lao moja Kwa sababu jamii hii, itikadi zao ni moja, mila yao ni moja, tafauti labda itakuwa ni kiutawala.4 Lakini ni watu waliokuwa wameingiliana. Akasema, nimetembea mjini na mashamba. Shamba ndo ndiko nlokofaidi. Nikaja nkaona “hawa wamekuwa ni kitu kimoja.” Sasa ndivo nilivoamua baada ya kukutana na mashina wenzangu. Suala lile nikaona mimi niamue nikuiteni nyie. Anasema Mkello maneno hayo.

Khamsini hatukufika. Sasa baada ya [Victor Mkello] kutuita akatupa ushauri “jamani kuna ndugu zenu nataka mkawasaidie. Wenyewe hawawezi.” “Hawawezi?” Hawawezi. Kwa nini hawawezi? Kwa sababu ile ni jamii ya mchanganyiko. Madam mchanganyiko itakuwa si siri. Lazima itatoka nje. Huyu ataweka siri, huyu atasema. Itakuwa hakuna mafanikio. Nyie mwende mkawasaidie ndugu zenu. Kukubali kwetu, suala tuloliuliza. Sisi tuna familia, halafu sisi wenyewe. Hili suala kama tunafanikisha tuna hongo gani? Tunalipwa vipi? Mimi [Mkello] sasa hivi siwezi kukujibuni. Lazima nende nikakutane na mashina yale kule. Tushauriane. Bahati nzuri, hata wiki mbili hazijafika, tukenda kule. Mashina ya huku yamentuma nende nikakutane na shina lile kule.

Manamba wamekubali kushiriki lakini suala waloniuliza nimeshindwa kulijibu. Hawa wanaweza kujiunga na suala hilo lakini watakuwa wapi? Na wakati wana familia zao nyuma? Kuna kupona, kuna kufa. Je hizi familia huku zitatizamwa na nani? Jimmy Ringo [Juma Maulidi Juma] alikata mkato moja kwa moja. Kwa sababu yeye anatoka kwenye shina. Akajibu moja kwa moja: “watahifadhiwa, na iko haki itatolewa. Haki zao zitatolewa wakifanikisha tu. Haki yake atapewa na familia yake itatizamwa. Heshima zenu zipo, hamtatupwa. Atakayekufa aelewe kuwa familia yake itatizamwa maisha.” Jimmy Ringo anasema. “Mmesikia?” “Tumesikia.”

Je, tamko hili mnalikubali au mnalikataa? Tukajibu kwamba ukituuliza “mmelikubali, mmelikataa” ina maana hapa unatwambia sisi tunaweza tukatae. Anasema, sasa niulize vipi? Mnavoona nyinyi, nikuulizeni vipi? Wewe lako la kufanya, jee kazi jee mmeikubali? Sisi wajibu wetu tukwambie tumeikubali. Je, huu mkataba mmeukubali? Sisi tumeukubali. Akasema hapo siwezi kurudia tena, kwa sababu nini, lile suala umenipa halafu limekurudia. Akasema aa! Uliza. Kwa sababu kila unapouliza ndipo unapopata maana.

Jamani, ndugu zenu ndo hawa, mmoja ni huyu hapa Jimmy Ringo. Je, hili suala, mmekubali kwenda kuwasaidia hawa ndugu zenu? Tumekubali, sawa. Je, hizi haki alizozizungumza huyu hizi, mmezikubali au na nyinyi mna masharti? Akasema, ehe! Sisi itabidi lazima tutowe masharti yetu. Waswahili hawa, sisi Wamakonde tunachanja uso, hawa hawachanji uso. Sisi wachanja uso wakati tunaposema “huyu anakwenda, anakwenda.” Lakini Waswahili watasema “yakhe, yakhe, yakhe.” Hafanyi kitu. Kwa hivyo tukubaliane hivi. Yule wa kule [Mkello] akasema sawasawa.

Nyinyi mnakwenda vitani ati, makubaliano ni lazima yawepo. Familia yako, mkataba huu lazima uwepo. Yule kule akachukuwa karatasi akatuandika majina tulokuwepo pale. Akatuandika majina. Alipokwisha, kilichofanyika, Jimmy Ringo, kila mmoja katika sie alitupa ngapi, shilingi ishirini, ishirini. Katoa katika wale. Tena siku hizo ishirini nyingi. Jimmy Ringo akazungumza kuwaeleza wale, “nitakuwa na imani kubwa sana, au tutakuwa na imani kubwa sana, tulioko Zanzibar, kuja kwenu sisi ndo itakuwa mafanikio yetu.” Na wale wakasema, “wakati wowote, saa yoyote, hata leo utatwambia twende, sisi tuko tayari.” Akasema Jimmy Ringo “tunakwenda kumalizia mipango, tukishamalizia mipango, ntakuja mimi, au atakuja mwenzangu mimi, au tutamuarifu huyu bwana [Victor Mkello].”

Sisi tulokuja huku Zanzibar tulikaa tukashauriana. Tulishauriana hivi. E bwana we, wale ndugu zetu wa Zanzibar, kila wakipiga kura wanakosa, kila wakipiga kura wanakosa. Wameamuwa kufanya mapinduzi. Maana ya mapinduzi tunayajuwa? “Si ndo yale yalioko Msumbiji? Sisi na Wareno? Hata tukaingia msituni? Si ndo haya? Si ndo wamekusudia hawa? Ehee! Tujuwe hivo. Manake msije mkafikiria kwamba kule tunakwenda kupiga miraba. Aa! Hatwendi kupiga miraba ya matuta. Kule tunakwenda, tukifika, tutakapoambiwa, kitanda hiki ingia ulale, au nyumba hii ingia ulale, bwana leo unakula muhogo, leo unakula sembe, shote tufahamu, suala litakuwa hilo. Na ahadi ndo imeshakuwa imekamilika hiyo. Tunakubaliana hivo? Tunakubaliana. Sote kwa pamoja.”

Mimi na yuko mwenzangu mmoja, tuliliendea lile shina letu, lile la kule Tanga. Tukamuuliza, “bwana we, mkataba umeshafungwa, kila kitu kimeshatengenezwa, umeandika majina, umefanya kila kitu. Barabara. Wewe, saini yako umetia?” Akasema “sijatia.” Tukasema “kama hujatia sisi hatwendi.” Akasema hakuna tatizo. Akachukuwa karatasi akatia. Baada ya kutia saini tumekaa, tumeendelea na shughuli zetu za kukata mikonge. Lakini huko jungu linatokota. Jungu linatokota. Siku moja alikuja kutuaga huyu [Mkello]. “Mimi nakwenda Zanzibar. Nakwenda Zanzibar kukutana na wenzangu wamenita.” Akaja Zanzibar.

Kufika Zanzibar wakakutana na mashina ya ndani kabisa. Wakazungumza, na yeye kule alichofanya, alikutana na watu hawa, Wamakonde watano tu, viongozi, sio wote, na akawaambia kwanini nakutana na nyinyi watu watano. Siri mliyopewa ni kubwa mno. Anasema, “mnaweza kuzungumza kilugha, lakini kuna wenzenu wengine wasiokuwepo katika gurupu hilo wanaweza kusikia lakini hatutaki yatoke nje. Na kama wanakuulizeni wenzenu, suala la kusema, kuna mipango kule inapangwa, lakini nnachokwambieni, baada ya wiki moja safari tayari. Mtakwenda nyie kule.”

Katika hao watano mmoja, Naruka, Tajiri, alikuwa akifanya kazi customZanzibar, Joseph Bhalo, Shindano, na mimi mwenyewe. Watano. Shindano kweli uhakika, kwa sababu alipigwa risasi jela, ubongo ukachanika huu. Mzee Karume akasema, hapana, huyu apelekwe Nairobi kwa matibabu. Sisi watano tukahamia Unguja. Nakumbuka Amboni alikuwepo Ndagaa, Joseph alikuwepo Ndagaa, yule wa custom [Tajiri] alikuwepo Mfenesini. Ina maana tulisambazwa sambazwa.

Sasa, Tajiri wakakutana na Khamisi Hemedi. Mimi nimeshachoka kulima. Je, pale pwani siwezi kupata kazi? Ngojea tufanye mipango. Kumfanyia mpango bahati nzuri akabahatika yule, ndo akenda pwani. Sasa yule wa Tanga [Mkello] alikuja kulisifu shina la hapa kuwa limefanya kitu busara. Kumchukuwa mmoja kumuweka custom atakuwa ni mpokezi wa hawa walioko Tanga. Kwa njia ya custom. Atakuwa anawapokea. Wageni wale wanafika pale anawapokea. Yeye anajuulishwa tu “ndugu zako hawa.”

Tumekaa hapa hata yalivokuwa mambo yanakaribia ikabidi wanakuja mmoja mmoja, kila anayekuja hapa, mbebaji ungo, Wamakonde hao, wamekuja kushughulika mambo ya miraba. Wanakwenda mashamba. Lakini shina la hapa linajuwa kinachotokea. Siku moja tulikuja kukutana na Jimmy Ringo, Kilombero. Siku hiyo ndo nilimuona Kaujore, Hanga, siku hiyo ndo nilimuona Twala. Walikuja viongozi kama wanne hivi, kuja kutuona na kutuambia “tulieni msiwe na wasi wasi.” Sasa walipotueleza akina Hanga pale, kidogo sisi tukatulia. Hanga alichofanya, anasema “mko pamoja au mko mbalimbali?” Tukasema “tuko mbalimbali.” Kama mko mbalimbali wewe itabidi uje Kijangwani. Ziko pesa ntakupeni, kiasi ishirini ishirini za chakula, kuendesha maisha, na kila kitakachopunguwa huyu itabidi aje pale, ndo kiungo. Huyu ndo kiungo wenu. Mmemkubali, tumemkubali. Bas. Kutoka siku hiyo viongozi wale mimi sikuwaona mpaka serikali inapinduka. Sisi tunaendelea na shughuli zetu lakini mimi nakwenda kule. Nikifika kule nikitokewa na shida napewa pesa.

Kwa maana kitu kikubwa nikifika kule ninachokionyesha ni kadi ya Afro-Shirazi tu. Huyo, Chairman [Mwenyekiti] wa Ndagaa huyo amekwenda kujenga taifa mahala fulani. Mpeni kiasi fulani huyo. Anapewa. Shina lilijenga huyu apitiye kwa njia hii. Blanketi sasa. Kafunikwa. Siku ilivodhihiri, tulikutana mmoja juu ya mmoja. Kikao cha tano kilichofanywa kwenye msitu wa Ndagaa ule, lakini uamuzi wa pamoja tuliamuwa na Victor Mkello alikuwepo kuja kuthibitisha na kuhakikisha, wamekamilika? Manamba wa Tanga hapa wamekamilika? Tulokuwa tumekuja sisi hapa tulikuwa ishirini na mbili.

Wenzenu wako njiani wanakuja [anasema Mkello]. Ishirini na mbili tulitoka kule. Kuna baadhi ya wenzetu kidogo waliingia mitini. Wakasema “njomba, kifo hicho!” Idadi yoteyote ni arubaini na nane. Ya Manamba waloingia hapa. Jimmy Ringo akasema “sasa hawa itatosha.” Mkello akauliza “wanatosha”. Tusiwafunguwe watu macho, “mbona Wamakonde siku hizi wanaingia sana hapa?” Tumekaa hapa tunalima. Tumejenga vibanda vetu va migongo. Tunaishi, bila ya wasiwasi. Hakuna mtu anatuuliza au kututuhumu. Manake watu wanajuwa kazi zetu sisi ni kulima. Na wengi wao kwa upande wa Waafrika walijuwa, hawa wamekuja kwa lengo kadhaa. Lakini sasa tuwaache kama walivyo. Wale walimaji tu wale.

Sasa, hata siku inawadia, kwamba bado wiki hii, moja, hili suala litendeke, palivuja siri, kuvuja siri Manamba hawakutajwa. Manamba hawakutajwa. Isipokuwa yule alievujisha siri Jamali Nasibu, kasema Afro-Shirazi inataka kufanya mapinduzi. Sasa siri ile ilikwenda kwenda mpaka ikaja kuonekana kama ni uwongo. Watu wakaingia kazini. Kwa sababu ndani ya polisi mle Afro-Shirazi wamo. Wakenda kucheketa. Ikabidi hapo Jamali hakuulizwa kitu. Akawa ni wa kutengwa tu kwenye mashughuli. Ikabidi watu wakafanya shughuli zao, hata zilipokuja kukamilika, tukapokewa mjini kutoka Ndagaa, tukapelekwa kwa Yusuf Himidi. Hata Yusuf Himidi akatuonyesha, hapo kuna magari mabovu hapo, hebu waficheni waficheni kwenye hayo magari mabovu. Baada ya nyumba moja ya Mgoni huyo, kujaa hiyo nyumba.

Suala linalonisikitisha mie, na wenzangu wengi wamekufa, familia zao hazijulikani. Kinachonisikitisha nini? Mimi huku ndo nimepinduwa, bendera ile pale inapepea, nimepata nini? Eh! Karume katoa shilingi arubaini na nane, zilikuwa khamsini, mbili za risiti, nikipata arubaini na nane. Ndo nikaona hakuna faida ya kuandika historia. Mimi nitapata nini? Mimi kazi yangu itakuwa ni ileile kazi ya zeze. Nitapata faida gani? Lakini leo imebidi nikueleze ukweli kwa sababu iliniuma nikueleze ukweli baada ya kukukimbia. Suala la Manamba hilo hapa. Idadi yote ni tisini na mbili. Kutoka Manamba mpaka hawa wa hapa. Jeshi lenyewe. Tisini na mbili. Katika hawa tisini na mbili, Mfaranyaki na Okello, walikuwa ndani ya gari ya polisi, kawapa Antoni Kisasi, na ndani yake akiwemo askari. Wanazunguka. Sasa askari wao kama wanajuwa tu alikuwemo askari, na ndani wamo askari wawili. Okello na Mfaranyaki, wao wanafanya patrol. Ulipofika wakati yule askari alivuwa gwanda akavaa nguo zake za kawaida.

Okello alifahamu sana kuhusu Manamba. Sana. Mwisho lakini baada ya tukio. Okello kwa BiKazija hakufikishwa. Kwa sababu huyu ni Mganda. Tunamuamini kweli lakini sasa kumuamini kwetu tunamuamini vipi?5 Haiwezekani hiyo! Lakini kina Kaujore, Saidi Washoto, Sefu Bakari, Ingine, wakijuwa kuwa Manamba walikuwa wameingia. Ni ndugu zenu. Jamani Manamba wameingia. Wako mashamba huko wanalima. Ndo hapo ndipo utakapoona, Wamakunduchi walishindwa kushirikishwa kwa sababu Ameir Tajo kuwa bega na bega na Mfalme. Wakasema hapana. Huyu atasema huyu. Kwa sababu huyu Shekhe. Anapewa kilemba kikubwa sana. Kusini suala hili lisizungumzwe.

Kiini cha John Okello—J. J. Mchingama

Walompa Okello ile hadhi ni kina Sefu Bakari, Natepe, akisaidiwa na akina Kaujore, Saidi Washoto. Sefu na Natepe ndo walomkabidhi. Sasa zilipomalizika zile shughuli ikawa moja kwa moja na yeye akajivika kile kilemba kwa sababu alipewa basi ni changu kwelikweli. Anataka kuingilia sasa amri zote za serikali. Mpaka zipitie kwake. Ikabidi apewe masaa ishirini na nne Zanzibar kuondoka. Akaondoka akenda zake Kenya. Kenya akafuatwa na waandishi wa habari wanataka kujuwa habari za mapinduzi yalitokea vipi. Hakuwa anaeleza misingi. Akasema tu, tulikusanyika na mapanga na marungu basi tukaingia bomani. Ndio. Lakini source, chimbuko nini? Hakueleza. Hata kwenye magazeti mengi tu. Jambo hilo hawakulipata.

Akaenda Uganda ambako ndo asili yake. Kwao. Ni mu Acholi huyu. Kabila la Acholi la Uganda. Alipokwenda kule, kabla hajafanya lolote, akakutana na waandishi wa habari wengi. Wakimhoji lakini hakutowa cha msingi. Nakumbuka gazeti fulani nililisoma, anatembelea shule, yeye huyo, baada ya kutimuliwa hapa [Zanzibar]. Anatembelea hospitali, wagonjwa. Uganda huko. Pale, inasemekana serikali ikaanza kushtuka. Huyu mtu kaingia karudi kwao, lakini mbona anaanza kujiweka ufahari namna hii? Kuna nini hapa? Unaona hiyo? Sasa ikawa hakuna njia isipokuwa wamvute sasa. Wamvute karibu (vicheko). Wakamwambia bwana wewe huko ulishiriki mapinduzi na nini. Akasema “ndio.” “Sasa kule wewe kama uliongoza mambo haya ulifikia cheo gani?” Akasema “Field Marshall.” Wenzetu wanajuwa kuna taratibu. U-field Marshall huwezi kuufikia kama hujapigana na taifa. Ukashinda taifa. Mfano kama Samora Moses Machel. Amepata U-field Marshall baada ya kulishinda taifa la Kireno. Kwa sababu alikuwa anapigana na taifa. Hukipati kienyeji, kiholela. Hapana, hapana. Lazima umefikia level [mustawa] ya kupigana na taifa ukalishinda.

Sasa huyu bwana wakaona, basi kama ulikuwa Field Marshall itabidi uingie jeshini. Wakamuingiza jeshini. Huko habari nilizokuwa nimezipokea alikuwa ni platoon commander. Kamanda alikuwa akiongoza platoon moja, ya watu thalathini labda kitu kama hivi. Sasa pale yule akaona mimi nimetoka rank[cheo] ya “Field Marshall” Zanzibar leo nakuja kupewa platoon commanderndo manake nini? Akadanganywa. Palikuwa na udanganyifu fulani wa kumpozapoza. Baadae akaambiwa wewe nenda, kasomee kulinda mpaka wa Kenya na Uganda. Kapelekwa sehemu inaitwa Busia. Mji wake unaitwa Mbale. Basi alipofika kule wakafanya mbinu wakamuuwa. Akafa. Wakamzika hukohuko. Wala hawakumrudisha kwao Acholi ambako kwenye asili ya kabila lake. Baada ya kumuuwa wakamzika hukohuko na hazikutangazwa habari zake. Zikawa kimya moja kwa moja. Mpaka hii leo.

Okello alikuwa halijuwi chimbuko. Pengine angelikuweko katika kamati ile ya mapinduzi yenyewe akajulikana muandalizaji nani kwa uandalizi wote wa mapinduzi yenyewe, akamjuwa fulani na fulani ndo wenzangu. Hiki kitu alikuwa hakijuwi. Waliopika mpango huu walipanga wao wenyewe lakini kwa kutumia mbinu wakasema “wewe bwana njoo! Unajuwa kuna kitu fulani hichi kafanye hivi.” Kama kungetokea jambo lolote pale la kufichuka hao wote wangeliruka wangelimuachia mpira yeye na asingekijuwa cha kueleza nani alikutuma, nani mulipanga nae. Asingejuwa. Na ndio maana aliendelea kutokujuwa chimbuko hasa, nani na nani waliopanga huu mpango. Yeye alikuwa ni kama mtu aliekuwa ameokotwa tu akapewa ule umbele na yeye akaupokea. Kwa kuona Waswahili wenzangu hawa wameniambia hivi akaupokea. Lakini kiini, nani na nani walioandaa, hakujuwa.

Kiini, ni kuna watu katika jeshi la polisi wakijuwa hizi habari. Bahati mbaya sasa hivi wameshatangulia mbele ya haki. Kwa mfano mzee mmoja wa Kijaluo akiitwa Thomas Tete. Alikuwa akijuwa mpango huu. Kuna mzee mmoja wa Kimwera akiitwa Anthon Musa Shamwingo, alikuwa katika jeshi la polisi, alikuwa akijuwa. Kuna Juma Maneno [Muheza]. Kuna Edington Kisasi, alikuwa anajuwa hizi habari kwa upande wa jeshi la polisi. Ambao wao walikuwa wakiungana moja kwa moja na akina Sefu Bakari, Kaujore, na Natepe. Hawa ndo walokuwa wana siri hizo. Na wao ndo walikuwa wakisema, nani na nani tutawapata wa karibu wa kuweza kuungana nao.

Mngereza nahisi alikuwa halijuwi kwa sababu kujuwa kwake angelilipata kutoka kwa hawa ambao walikuwa katika jeshi la polisi na ndio wakubwa. Lakini hawa walimficha Mgereza. Hawajamwambia Muingereza. Kufahamu kwangu mimi hivo. Walikuwa hawakumwambia Muiengereza. Wakumwambia Mueingereza ni Edington Kisasi, Anthon Musa, na Thomas Tete. Hawa ndo walokuwa wamelishikilia wakati ule jeshi la polisi.6

Hawa ndo walokuwa wepesi wa kumwambia lakini hawa kwa vile walikuwa wameungana na huku hawakuweza kumwambia na kama walikuwa wanamwambia ilikuwa ni udanganyifu, sio ule uhakika. Pengine kumwambia kama kuna rumours [uvumi] hivi, labda, tuweke standby [tahadhari]. Kuna wasiwasi hali lazima tuweke standby. Vitu kama hivi. Lakini kiini kuwa kutafanyika hivi alikuwa hajuwi.7

Unajuwa wakati mwengine nahisi kwamba mara nyingi Afro-Shirazi ikitaka kufanya jambo lake walikuwa wakiwatumia sana Youth League. Kama ni suala likitokea jambo lolote kwamba ni vijana hao wamefanya fujo na vijana kimataifa hukumu zao zinakuwa tafauti. Wakiwatupia vijana. Hata kama lile jambo wata-kuwa wamelifanya watawatupia wale vijana waonekane Youth League. Wanajitowa wao. Nasema hivo kwa sababu kulikuwa na maktaba ya Mmarekani ilikuwepo hapo Kikwajuni ile nyumba ya Ubalozi wa Msumbiji sasa. Lakini kutoka na michezo walokuwa wakionesha pale, wao kina Sefu Bakari ndo walokuwa wakiwatuma vijana kwenda kutupa mawe pale, kwenda kufanya fujo pale. Yule Mmarekani akalalamika kwamba mimi naonyesha filamu hizi kufanya burudani kwa vijana hasa pale kipindi cha Apollo 11.

Akasema “wewe si unajuwa vijana tabia zao? Kwenu si mnao vijana?” Mpaka mwisho ikaamuliwa kwamba bora wahame pale, watakufanyieni fujo. Akahamishwa pale akapelekwa Mji Mkongwe. Kwa hivo walikuwa wanatumia trick [ujanja] hizo kutumia Youth League kwamba vijana mara nyingi ni ulimwengu mzima wanaeleta fujo sana.

Kina Babu, mapinduzi, nnavofahamu mimi, wamefahamu alfajiri yake, ila wao walikuwa na maandalizi ya kufanya mapinduzi kwa njia zao wenyewe. Kwa sababu walipofukuzwa kutoka ZNP wakaunda chama cha Umma Party na walikuwa na wanafunzi wao ambao walikuwa wamechukuwa mafunzo ya kijeshi. Bila ya shaka walikuwa na maandalizi yao lakini maandalizi haya wamekuja kushtukizia asubuhi. Wakaona na sisi tukitaka hichohicho ili kitokee. Madam yameshatokea mapinduzi ambayo sisi tulikuwa tumeshajiandaa, basi tujiunge moja kwa moja. Wakaunga mkono moja kwa moja. Lakini kiini cha kabla hawakushirikishwa. Lakini baada ya kuwa wameunga mkono na kweli ule udhalilishaji wa ZNP dhidi ya kina Abdurahman Babu, wakawa wao kama kundi moja na ASP. Na wao wakawachukuwa moja kwa moja wakawapokea. Ndo maana baadhi yao wakapata nafasi ya kuwa Memba wa Baraza la Mapinduzi (MBM) kwa kutokana na kuunga kwao mkono. Hawakuwa katika kiini. Kiini kilikuwa watu separate [mbali] na wao kabisa.

Mimi suala hili la mchujo kwa kweli nafahamu kwamba wao walitaka Waafrika wenye asili ya kutoka bara walijuwe suala hili peke yao bila ya kumshirikisha mtu yoyote wa Zanzibar. Mzaliwa wa Zanzibar. Hilo kwanza. Na ndio mana utakuta pale kuna Saidi Washoto Myamwezi. Umeona hivo. Kuna Kaujore ni mtu wa wapi, Tunduru pale. Sefu Bakari Mdengereko. Hafidh Suleiman ni wa hapa lakini nafikiri katika masuala hayo hakuingizwa zaidi. Kina Ibrahim Makungu hawa wamekuja mwishonimwishoni lakini kiini cha siri ya mwisho ilikuwa hivo. Nafikiria hivo, sina hakika ya kutosha. Lakini mchujo ulikuwa uko wazi. Kwa sababu tukiwaambia hawa wengine wameowana na kuzaliana na Waarabu.8 Hatokubali shemegi yake au mwanawe akauliwe. Ataona uchungu japo kuwa hakubaliani na matendo yale lakini hatokubaliana kuona family yake inakufa. Kwa sababu vitendo vina mauwaji. Haya ashtukie yametokea bas. Asijuwe mapema. Hiyo ilikuwepo. Ndo mchujo nnaoufahamu mimi, kwa ufahamu wangu mimi.

Kwa kabila letu sisi Wamakonde tuna mambo ya kuigiza sana. Ukenda mahakamani kuna mtu anaitwa Bwana Shauri anaeshauri mahakama, basi mama wa Kimakonde anajiita mimi Bwana Shauri. Pesa shilingi mia, basi mwanamke anasema mimi “bwana mia.” Ni watu wenye kuigiza sana majina. Wepesi wa kuchukuwa majina. Akikuta kitu cha ajabu tu hivi kinatajwatajwa sana yeye yuko tayari akichukuwe. Anabadili jina lake la asili sasa hivi, akirudi kwao anasema jina lile nimeliacha naitwa fulani. Hii ni tabia ya Wamakonde. Kwa hivo Mzee Amboni Matias anaweza kuwa ameitwa kwa hivo tu. Amboni kweli ni mji, kuna yale mapanga pia, Amboni. Yalikuwa yakitolewa kwa ajilii ya shamba lile la Amboni. Yanaitwa mapanga ya Amboni kwa shughuli za kukata mkonge. Kwa sababu yale mapanga ni makali basi na yeye atajita “Amboni.” Ni sifa ile. Mie ni “Amboni.” Huyo Tajiri pengine nyumbani alikotoka jina lake si tajiri. Lakini kufika hapa, bwana kuna tajiri mmoja pale, alaa, kumbe yule tajiri, manake ni mwenye pesa. Basi na yeye anajita “Tajiri” ili apendwe na wasichana. Amboni, mkali, Tajiri ni mapesa japo hana.

Turudi kulekule kwenye mazungumzo yetu, kama kulikuwa na plani [mipango] hizo mimi kwa kweli sizielewi hili suala na halimo katika kichwa changu na wala katika historia. Mimi nakubali kwa sababu hata siku hiyo, nakumbuka, kulikuwa na tetesi tetesi lakini si za uhakika. Lakini saa kama hizi za jioni tukiwa pale Makadara. Tuliitwa vijana wote wa Kimakonde tulokuwa tukifanya kazi kwa Wahindi humu majumbani, kukosha vyombo, kulea watoto, sijui nini, wote tuliitwa Makadara kwenye ofisi ya FRELIMO. Wao wanajuwa hicho kitu, kwa muda mrefu, na siku ile kwa kutwa nzima wanazo hizo habari lakini hawakutaka kulitowa. Wa kike na wa kiume. Hata wale wanofanya kazi za dangurodanguro wakaitwa. Tukaambiwa bwana, kuanzia sasa hivi vijana nyote hamna ruhusa kulala peke yenu. Mtalala jengo hili. Kwa sababu hali ya nchi leo si nzuri. Mmesikia, tumesikia. Tunakwambieni msiondoke.

Mimi nakumbuka nilikuwa napenda kukaa palepale Mwembeladu palikuwa na duka moja la Muhindi. Huyu Muhindi alikuwa akijifanya yeye ana asili ya Msumbiji. Kwa hivo Wamakonde wengi walikuwa wanakwenda pale, nafikiri ulikuwa ni mvuto wake. Kwa hivo mimi nilikuwa napenda sana kwenda pale. Sijui kwa njia gani au vipi alikuja akapata fununu huyu Muhindi. Akaniuliza kama nimesikia kutakuwa na fujo. Nikamwambia mimi sijui.

Basi nikarudi. Saa kama hizi akaja babangu akanambia nimekuja kukwita twende nyumbani kwa sababu wenzako kuku wanakula kule wanamaliza. Kamchukuwe kuku wako umle. Kumbe yeye anajuwa anataka kuniondowa kiujanja. Siku ile kukawa na ngoma nzuri sana ya Kimakonde sehemu za Jumbi. Siku ile ya mapinduzi. Na mimi na appointment [miadi] zangu za ujana kule kwenye ngoma. Nikamwambia baba leo siji huyo kuku nitakuja mla Jumapili kwa sababu leo nataka kwenda ngomani. Akasema leo usende ngomani. Wenzako kule kuku kaka zako wanamaliza. Juzi yule kala wawili, yule mmoja jana kachinjwa, huyu nikasema hata, huyu muachieni mwenzenu kwa hivo twende. Nikamwambia mimi leo hapana. Akaniona mgumu. Akaniita pembeni. Sikiliza. Ninachokwambia leo hali ya nchi hii si nzuri. Huenda vikatokea vita. Mimi nilivokuja nimekuja kamili. Amevaa shuka na hilo panga la Amboni amelichomeka kwa ndani. Akakunja shuka akanionyesha panga. Kalinowa sawasawa. Unaliona panga hili? Mimi sirudi tena nyumbani ila wewe rudi nyumbani, mimi nimepona sawa, nimekufa utaongozana na wazee wako. Kama ananiaga.

Nikamwambia baba, mimi mwanamme. Kwenda kuniungamanisha mimi na wanawake nikakae niwachunge wanawake wewe unakwenda kufa mimi sikubali. Utakapo kufa wewe ndo nitakapokufa mimi. Kwa hivo mimi sikubali. Tufatane wote. Yule baba akaona hapa amefanya makosa kuitoa hii siri. Kumbe sasa imekuwa ni kero kwake. Kwa hivo yeye akasema kama ni hivo nisubiri nende kwa Haji Tumbo nikanunuwe kiteweo ili tuje tuambatane tuondoke. Nikamwambia kiteweo cha nini na nyumbani kuna kuku? Nimembana zaidi pale! Kidogo nilijitahid machachari. Akasema aa, yule kuku wa kwako wewe lakini huyu samaki nakwenda kununuwa sisi tule. Yule wa kwako. Nikamwambia haya nenda. Nakusubiri basi. Hakurudi tena yule. Ikawa sasa mambo yangu nimeshayapata mara tatu. Kutoka kwa baba yangu, Makadara ofisi ya FRELIMO na kwa yule Mhindi.

Kumbe ile ngoma inayofanywa Jumbi nayo ni mkusanyiko wa kuwakusanya wanawake na watoto tu lakini wanaume watu wazima wote wanakuja zao kwenye kazi. Mimi mshipa umenishika. Lazma niende kule. Wikiendi [mwisho wa wiki] itanipita! Sasa na wenzangu fulani wakawa wamejitokeza. Twendeni bwana, si tutarudi? Ah! Twende, twende. Tulikuwa watu watano. Wakati huo baiskeli zinakodishwa. Shilingi mbili mpaka kesho asubuhi. Tukenda kukodi baiskeli zetu. Safari, Jumbi! Kufika kule ngoma wanawake wengi lakini wanaume hamna! Wanaume ndo tumekwenda sie tu pale. Kufika saa sita tukaona upuuzi huu. Bora turudi zetu. Tukarudi. Tunafika Fuoni polisi, saa nane za usiku, tukakuta road block [kizuwizi cha njia]. Mnakwenda wapi? Tunakwenda mjini. Kufanya nini? Sisi tunafanya kazi kwa Wahindi. Huku mnatoka wapi? Tunatoka kwenye ngoma. Hiyo ngoma inamuhusuni nini? Sisi watoto wa Kimakonde. Mmoja akasema tuwekwe ndani, tuzuwiliwe. Mmoja akasema hapana, waachie. Watakaloliona watakuja kutwambia kuliko kuwazuwia hapa linalotendeka huko hatulijuwi. Road block [kizuwizi cha njia] imeshafungwa pale. Kuna gari moja inatoka shamba inakuja spidi kali sana. Ilipofika pale kumurika ikakuta kile kizuizi haikujali, ikavunja poo! Ikapita tu. Kwa sababu yule askari alikuwa na tochi, akamurika ndani ya gari na kutaka kuisoma ile namba. Kwa jicho langu niliwaona watu waliokuwemo mle, wamevaa weusi mtupu na hata miili yao wamejisinga weusi mtupu. Gari ikaondoka! Lakini wako kimya.

Basi tukaja zetu mpaka meli tano Fuoni. Kufika Fuoni, ndo tunasikia sasa risasi zinalia. Jamani turudini. Tumeambiwa na wale askari wale. Aah! Turudi vipi bwana. Twendeeni! Tukafika Mwembe Njugu. Tunafika Mwembe Njugu saa kumi na moja za alfajiri ndo kinachukuliwa kituo cha Ngambo police station. Hapapitiki. Risasi mtawalio mmoja. Ikabidi tena tukimbilie Mwembe Matarumbeta. Mwembe Matarumbeta ni opposite [inakabiliana] na Ziwani barracks [kambi ya jeshi la polisi]. Nako kule kuna marisasi yanaangukia hapa. Na la mgambo likatoka pale, mwanamme nje, mwanamke ndani. Ndo tuko nje. Ikabidi sisi tuwache baiskeli ndani ili kumfata mzee wetu pale. Tukawacha baiskeli, sisi tukarudi tuka join [tukajiunga] kuelekea Raha Leo. Tayari nayo Ziwani ishachukuliwa. Pale tunakutana na John OKello. Asubuhi hiyo. Mapema!

Ukifika hapo “unajuwa bunduki?” “Najuwa au sijuwi.” Basi kama hujuwi shika “kama unakuta Mwarabu piga yeye.” Okello anasema. Kilugha chenyewe cha Kigandaganda cha kuvunjavunja tu. Sasa likatokea lorry moja. Lina mapanga, lina mamishare, mapinde. Nikaona ile ndo jadi yangu. Mimi nikawacha bunduki nikenda kuchukuwa upinde nikaona ni silaha naiamini kuliko bunduki. Tukajiunga pale, tunapakiwa wapi, mahala flani kuna Mwarabu anafanya fujo. Tunakwenda. Pengine tunakutana nao, pengine tayari tumeshamuuwa au tushamchukuwa. Tunarudi wapi, twende Kipange, mara twende huku. Hivyo, ikawa vurugu. Kwa hivo inawezekana kwamba kama kuliweko vitu hivyo, nataka kukubaliana kwamba hili gari nloliona alfajiri linapita pale Fuoni, usiku ule wa saa nane, inawezekana pengine katika hawa watu waliokuja kuandaliwa kutoka huko Tanga. Sijui. Inawezekana hivo.9 Lakini kwa ufasaha hasa kusema kwamba kuna watu walitoka sehemu nje ya Zanzibar kuja kufanya hivo ndo itakuwa mara yangu ya kwanza kuisikia. Watu wengi hawaijui. Inawezekana ilikuwa high level [inajulikana na daraja la juu la uongozi].

Mimi najuwa katika kambi za mkonge makabila yalokuwa yameshamiri: Warundi, Wamakonde, nk. Wananyaruwanda ndo walokuwa sana katika kambi za mkonge. Myamwezi alikuwa sio fani yake. Mmasai alikuwa sio fani yake. Ila wako wale Wakwami walikuwa wanashiriki lakini sio sana. Kama nilivosema siku ile. Haya mambo yanakwenda kwa level [kwa daraja ya cheo]. Wewe unaweza kupewa kitu ufahamu hichi. Usitake kukijuwa kengine. Na yule na ajuwe pale, asitake kujuwa kwengine. Huwezi kuyajuwa yote.

Mimi kwa level [daraja] hizo na miaka hiyo sijui. Kwa sababu huyu Tajiri Fundi kwa upande mmoja mimi alikuwa ni mzee wangu wa karibu kifamilia. Na wanawe wapo ambao wao mimi ni ndugu zangu. Wapo hapohapo Shakani. Tulikuwa tunaongea sana hata katika Jumuiya ya Wanamsumbiji sikukumbuka katika historia yake alikotokea. Na sisi nakumbuka tulimkuta na yeye Fundi Tajiri na alikuwa mpinzani wa FRELIMO hata kwenye shughuli za jadi, kama jando, yeye alikataa akaamuwa kuwachezea watoto wake kwa mila za Kizanzibari. Kawapigia beni na tarab kwa kupingana na FRELIMO. Mpaka 1975 ulipopatikana uhuru wa Msumbiji ndo aka-surrender [akasalimu amri], akaja upande wetu. Kuna Mzee Thomas ambaye bahati mbaya alifariki hivi karibuni alitokea Tanga vilevile lakini hakuja kwa njia hizo naye pia alikuwa against na FRELIMO, na watu walokuwa wakisupport ASP ni chama cha FRELIMO. Hao wengine kwanza walikiita chama chao Afro-Shirazi Makonde. Michango yao wakiwapa Mzee Thabit Kombo na Mtoro Rehani Kingo. Na FRELIMO iliposhamiri wakawaruka [wakawalia pesa zao]. “Wafateni wenzenu. Kwa nini msiwe na wenzenu?” Ndo hao kina Tajiri Fundi, kina Thomas Kalawone, na wengi wengine tu. Lakini kama Mzee Amboni alikuwa FRELIMO. Joseph Bhalo FRELIMO na mwaka 1974 alienda Msumbiji baada ya FRELIMO kupata madaraka, bado uhuru kamili, ndo alipoondoka Joseph Bhalo kwenda Msumbiji kwa kuitwa na viongozi wa kule ili kwenda kuangalia hali ya madaraka inavopatikana.

Kuibuka kwa Mzee Karume—Mzee Issa Kibwana

Mzee Karume alikuwa na mawasiliano na watu watatu katika jeshi la mkoloni. Alikuwa na mawasiliano kwanza na Edington Kisasi. Alikuwa na mawasiliano na Anthon Musa. Alikuwa ana mawasiliano na Juma Maneno. Huenda wakawemo na wengine lakini mie nisitambuwe. Nazungumza kile kitu nnachokitambua. Sasa wale walikuwa maisha siri ya yale maboma wanampa yule. Halafu akaweka, kwamba wale watu wake wa kuwatumia, siri zake ndani ya maboma yale. Nadhani hata tulipoingia katika boma la Mtoni mtu wa kwanza wa kumtafuta Anthon Musa kwa sababu ule ufunguo wa armoury [ghala ya silaha] alikuwa nao yeye. Mawasiliano yalikuwa mnakwenda mahala fulani mkishamaliza vilevile vidogovidogo huku mlangoni mpenye mumtafute fulani ndo mwenye ufunguo wa silaha. Tunakwenda pale kwa kujuwa kuwa fulani ndo mwenye ufunguo. Na wanokwenda Bomani wanajuwa nani mwenye ufunguo.

Hawa watu [akina Hanga] walikuwa wasomi. Karume si msomi. Karume kasoma umaarufu wake ndani ya vyombo tu baharini. Lakini usomi wa ndani ya vibuku, vitabu hivi, hayumo. Sasa Karume kichwa chake kilikuwa kinafanya kazi akili ya kuzaliwa. Anajuwa kitu kinachokuja usoni kwake ni kibaya na anajuwa kitu kinachokuja usoni kwake ni kizuri. Sasa wale japo kama walishiriki ndani ya mapinduzi yale lakini alitambuwa kabisa hawa kuja ndo maji yangu mie.10

Nasema kwa kujuwa ndo nkakwambia kuwa mie nlikuwa karibu naye mtu yule. Alijuwa kabisa. Maana kuna saa ingine huita hasa. Humwita Idi Bavuai, humwita Juma Maneno, humwita Sefu Bakari, kina Kisasi, wote huwaita pale. Huwaambia hasa “mnajuwa nyie, kula mkikaa kuna watu wengine mkizungumza mambo ya masilaha yenu watu wengine msiwaambie. Au kunakuja chombo chenye silaha watu wengine msiwaambie. Muwe na akili. Kwa sibabu bado maadui tunao hapa. Kama si wewe mie, kama si huyu, huyu. Huja tukapoteza maisha yetu kabla hatujajuwa ulimwengu uko vipi.” Sasa mtu wa kwanza wa kutambua lile suala analolizungumza Mzee Karume, Waziri Kiongozi wa kwanza—Ramadhani Haji. Ramadhani Haji haraka aliijuwa siri ya Mzee Karume. Jibu lake anamwambia “hakika na mie natambua. Kuna kitu kwanza huyu Hanga anakuja vibaya sana kwa sababu wewe hujui kusoma kwanini ukawa kiongozi. Hujui kusoma utakuwa vipi kiongozi. Umtizame sana mtu huyu. Halafu kuna mtu wewe unampendelea saana mambo yako kumpa. Huyu kwako wewe si mzuri. Kuna kitu anataka kwako wewe. Sisi tunavoona. Au tuwachie sisi tufanye shughuli zetu.” Jibu lake “ntakupangeni. Mimi mwenyewe ntakupangeni halafu ntakupeni kazi.” Wakachaguliwa watu ishirini na tano, wakapelekwa wapi? Hapoo, pakiitwa Kambi ya Jitegemee. Kambi ile wamechaguliwa watu ishirini na tano makusudi wana kazi yao maalum huja nayo Mzee Karume akaja akawapa, ikiwa usiku ikiwa mchana waifanye. Jambo la kwanza kabisa kabisa kabisa kabisa akawaambia mtizameni Hanga. Akawaambia “mtizameni mtu huyu. Huyu mtu mbaya sana. Mbaya sana. Mtizameni sana mtu huyu.” Wakamwambia “basi nyamaza.” Hakujulikana kapelekwa wapi. Wao wanapeleka ripoti, “bwana kazi yako tumeshamaliza hii.” Kule wale viongozi wabaya wabaya wale wanasema “Mzee Karume anauwa.”

Sasa na kwa kujuwa na mwenyewe ile wanavokwenda kula masaa wale watatu hawabaguani: Abdalla Kassim Hanga, Abdul Aziz Twala, na Saleh Saadalla. Na Othman Sharifu. Ramadhani Haji anamwambia “watu hawa watizame sana.” Jibu “nyota yangu, uso wangu, maelekezo yangu weye, weye pamoja na [Saidi] Idi Bavuai. Nilindeni.” Wewe utakuwa sehemu ya jeshi, Bavuai atakuwa sehemu ya usalama, akisaidiana na Ibrahim Makungu. Kawaambia “hiyo kazi yenu nyie. Kama kuniua nyie, kama kunilinda nyie.” Wote hao wacha kidogo pembeni lakini Idi Bavuai yuko mbele. Halafu baadae akaitwa “Sancho,” Hafidh Selemani. Yeye huyu ndo akimwambia “Mzee wewe, tizama bwana weye, usiweke watu wabaya wako matakoni mwako. Wacha tukulinde. Usitwambie sisi wapumbavu. Hata!” Ndo akapewa jina hilo “hili Sancho hili.” Kitu kibaya chochote, haraka wanakwenda kumuambia Mzee na yeye anawaambia “nakuwachieni wenyewe.” Jibu lake “nakuwachieni wenyewe.” Basi wale wanatimiza.

“Sancho” kuwa karibu na Mzee Karume, “Sancho” ni mtu mkweli. “Sancho” ni mtu shujaa! “Sancho” ni mtu asieogopa mtu. Hata kama mrefu kama mbuyu, midam anataka kuzungumza kitu cha halali anamzungumza. Hamuwekei mtu kinyongo. Anamwambia hapo masuala yake alonayo, akimaliza hapo basi. Hamuwekei kitu hapa (moyoni). Sasa Karume kile kitu alikuwa ndo ugonjwa wake. Hiyo ndo sifa alokuwa nayo “Sancho” na Karume kuwa jirani yake. “Sancho” akizungumza kitu, Karume anakaa nacho siku tatu, ya nne anamwita. “Umefikiri siku ngapi kitu hiki?” “Ah, kimentokezea tu kwa vile nataka mawazo.” “Haya tukaye tufanye utafiti mimi na weye, au tumdokezee mtu atusaidie mawazo.” Anamuuliza. Madokozi yake anakwenda kwa Ramadhani Haji, au anakwenda kwa Saidi Idi Bavuai, au kwa Saidi Washoto. Kutafuta mawazo. “Sancho” mchango wake wa mapinduzi, yule alikuwa ni mwanaharakati mkubwa katika sehemu ya mapinduzi. Ni mwanaharakati mkubwa kama tulivorudi kwa yule,Tete. Anakaba kitu. Hakitoki nje. Kwa vile mchango ule wa mapinduzi, ikizungumzwa ndani ya baraza lake yule Mzee Karume, yule mmezaji sana siri ile. Haitoki. Pia alikuwa dereva mzuri sana wa Afro-Shirazi.

Halafu Ibrahim Makungu. Kawekwa na Karume awe mkubwa wa usalama, Unguja na Pemba. Unampelekea kitu Ibrahimu, “bwana kuna suala hivi hivi hivi.” Anakuuliza “umeliona weye au umesikia na mtu?” Sasa umpe ukweli. Nimesikia na mtu au nimeliona mwenyewe. Anakwambia “niachie.” Hakuulizi umesikia kwa nani. Aa. Niachie, hiyo kazi yangu mie mwenyewe. Ibrahim Makungu hendi mahala popoote anakwenda bar kwenda kunywa. Nyie mnaweza kumaliza chupa kumikumi yeye chupa moja ile hajaisha. Kumbe kuna mzigo wake anautafuta pale. Kama kweli neno ulilolisema anakwenda mdokolea mtu pale. Anajuwa hicho kitu changu kinakuja. Sasa analipeleka kwa yule mzee la uhakika. Mzee naye yumo kwenye uchunguzi wake. Mzee hakusoma lakini kama tulivosema, kichwa chake kinafanya kazi kweli. Hawezi kumbana mtu kama kile kitu si sahihi. Kwa vile kipenzi chake kwa yule bwana kwa kazi zake. Anazozifanya anazifanya kwa uhakika. Analomwambia ni kweli.

Ibrahimu alikuwa ana mchango mzuri kwenye mapinduzi. Kwa sababu Ibrahimu kwenye mchango wake wa usalama alitafuta vitu vizuri saana ndani ya usalama katika mabaraza yale kwa ajili kwamba kuna kitu kinatakiwa. Sasa yeye yumo ndani ya mabaraza yale. Kutafuta. Hiki kitu kimevuja au hakijavuja. Na kama kimevuja ntakipata wapi. Kama hakikuvuja ntakipata wapi. Na kazi yake kubwa kukaanga samaki na kuuza gongo sasa pale alikuwa anayapata mengi sana. Pale alikuwa anayapata mengi. Basi ilikuwa hiyo. Mchango ule anaoupata pale anautuwa. Sasa kuutuwa kule yule Mzee haufanyii kazi. Kwanza yumo kwenye mapekuzi. Alikuwa na mchango mzuri sana. Saidi Idi Bavuai alikuwa yule mkulima. Yule mpanda bangi. Shambani kwake kulikuwa na bangi tupu. Sasa anamwita “Bavuai e, mbona shambani kwako watu hawafiki kuna nini? Wewe shambani kwako umefuga majibwa tu, majibwa tu.” Kwani majibwa ya Sultani aliyachukuwa yeye ati. Anasema Bavuai “sikiliza Mzee Karume. Mimi bwanaa, mimi mpendaje mzuri sana kwako wewe. Mimi walinzi wangu wauza bangi na mimi napanda bangi. Nyumbani kwangu kote imeenea bangi. Mikarafuu kidogo kuliko bangi. Na ndizi. Kula penye mgomba pana mche wa mbangi. Sasa ukitaka kujuwa ulimwengu ulivo kamatana na watu hao. Usikutane na walevi wa pombe. Walevi wa pombe wanalewa wanaanguka hawajuwi la kusema. Lakini mlevi wa bangi anasema!”

Mzee Kaujore kipenzi wa Karume tena wala usimsengenye kwa Mzee Karume! Hata! Mchango wake akikutana naye yeye kazi yake kuuwa. Mzee Kaujore. Akizungumza kitu anamwambia “ah! Sasa kama wale kina fulani ya nini kuwaweka duniani?” Halafu hutowa bunduki lake lile. Akalitizamaa! “Ah, masikini.” Basi palepale humwambia “ushakupiga mshipa wa kutaka kuuwa watu. Bwana usende kuuwa watu majiani huko. Leo wazimu wako uwache.” “Ah, Mzee hapana bwana.” Ala, mara ushasikia kapiga watu msikitini. “Mzee Kaujore keshapiga watu, mleteni mleteni. Wewe Mzee Kaujore si nlikwambia bwana! Unafanya nini? Serikali yako, unakwenda uwa raia kwa nini?” Humuonya yule mpaka anarudi. Mpaka akawa mzuriii! Kawa mzuri mwishoni lakini karibuni pale motomoto ya mapinduzi alikuwa Mzee Kaujore kama hajauwa hajafurahi. Kabisa! Hajafurahi!

Washoto alikuwa yeye, hana makuu sana. Washoto ilikuwa kazi yake yeye alikuwa Shekhe. Watu wakizozanazozana wakisema twende kwa Mkuu wa Mkoa kufika pale “mnawazimu. Muozesheni huyu.” Unaozeshwa palepale. Washoto ndo ilikuwa kazi yake. Alikuwa ana maingiliano na watu. Alikuwa habaguwi huyu nani, huyu nani.


Kamati ya Watu Ishirini na Tano

Vitisho vilikuwa vikubwa baada ya mapinduzi kwa sababu wangelivamiwa. Hilo Komred walikuwa wameliweka tayari bwana. Komred alikuwa tayari kuipinduwa serikali. Sasa ndo utakuta baraza [la mapinduzi] lilikuwa na nguvu. Linozungumzwa harakaharaka anapewa Mzee Karume. Akipewa Mzee Karume anapeleka kule tulikozungumza. Kwa kamati yake ile. Ingelikuwa bila ya muungano Komred angeliichukuwa nchi. Na asikari kutoka Mombasa wangetuvamia pia. Ndo ukaona umuhimu wa kuwa na shirikisho la Afrika ya Mashariki.

Kamati ya watu ishirini na tano ikiongozwa na Kanali Tete.11 Humjui. Alikuwa Jaluo moja huyo sawasawa na Mzee Anthon Musa. Cheo chao walipewa siku moja katika ukoloni. Alikuwa msasi sana wa nguruwe. Huyo ndo alopewa kambi hiyo. Tete, akiitwa. Huyo ndo alokuwa kiongozi wa kundi hilo la watu ishirini na tano.

Suala la mapinduzi Mzee Karume alikuwa akilijuwa lakini kulikuwa na mchezo baina yake yeye na wasomi. Sanaa! Wasomi walikuwa hawamuamini na yeye alikuwa hawaamini. Lilikuwa suala la nani atamzidi kete nani. Hicho ndo kitu chenyewe lakini Karume ndo mwenye mapinduzi khasaa. Kwa sababu shabaha zote zile za kuwafukuza Waengereza anazijuwa Karume. Wale wote wengine fikra hizo walikuwa hawanazo. Zile kaziwaza mwenyewe na kazitenda mwenyewe. Na tumepata njia ya mapinduzi kwa Karume. Sasa kama kuna mtu anasema hakushiriki mapinduzi huyo namkatalia. Moja kwa moja. Karume ndo mshiriki mkuu wa mapinduzi. Ndo mpangaji mkuu wa mapinduzi halisi. Yeye ndo alotupa mlango kuondoka Mgereza. Tusingefanikisha. Hata kidogo. Tusingefanikisha. Hiyo hakika. Ntasema mpaka kesho kutwa.

Kulikuwa na kamati ya watu ishirini na tano nje ya Baraza la Mapinduzi. Baraza la Mapinduzi linajuwa kwamba kuna kamati yetu fulani ndo yenye shughuli zake. Wao wakisikia kitu wanapeleka kule. Baraza la Mapinduzi linampelekea Karume. Kuna kitu hivi, hivi, hivi. Yule ndo analijuwa Baraza lake la kulipa kazi. Asikudanganye mtu bwana. Mtu asikudanganye. Hawa wasomi, huyu si msomi, lakini huyu mwenyewe khasa wa mapinduzi.

Wale wote wako nje ya Baraza la Mapinduzi. Wote! Kamati hii aliiunda mwenyewe Karume baada ya mapinduzi ilipoanza ile chokochoko.12 Hata lile Baraza la Mapinduzi kamati ile wanaiogopa. Kwa sababu wanajuwa wazi kuwa kamati hii hata sisi wanaweza kutuchukuwa. Kabisa, kabisa. Ilikuwa serious hiyo kamati. Hii ilikuwa siri ya mwenyewe kabisaa! Tena hao watu walikuwa, huyu Tete huyu, hayuko mbali. Saa ishirini na nne wako hivi (pamoja).

Mzee Tete kafa. Kafa kazini. Anthony Musa kafa kastaafu kazi. Anthony alikuwemo kwenye kamati ya watu ishirini na tano. Katika wakubwa wakubwa, Tete, Anthony Musa, na Juma Maneno. Mshauri Mkuu “Sancho.” Kwa sababu yule mtu alichaguwa makatili matupu. Mtu kama Sefu Bakari anajuwa tu lakini hayumo. Kwa mambo ya chini kwa chini “Sancho” alikuwa na nguvu kuliko Sefu. “Sancho” ofisi yake ilikuwa kwa “Bwa Mkwe” [Hassan Mandera] katika Kamati hiyo ya watu ishirini na ngapi hiyo. Yeye kucheka kwake anachekea tumboni, lakini mdomo wake kuinua, “he, he, he”, hata. Akifika anakwambieni “tumeambiwa kuna kazi, kazi ifanywee! Sasa mnaijuwa wenyewe. Kwaherini.” Anaripoti “bwana kazi yako nishatimiza huko, tena wewe tusikilize tu ulimwengu ulivo.” Memba wa Baraza la Mapinduzi wakijuwa “nikifanya kitu fulani hapa hawa watu wakiipata taarifa hii mimi naondoka. Tena kuondoka kwenyewe si kama wanantowa ndani ya baraza. Hata. Naondoka roho yangu! Kwa vile aa. Midam nataka ugari aa. Yamalizikie hapohapo.”

Yule Mkenya. Kanali Tete, Mkenya. Lakini siri ya mapinduzi anaijuwa vizuri sana pamoja na huyu Anthony Musa. Tangu mwanzo inakwenda siasa wale wanaitambuwa. Aliletwa na Mgereza hapa. Tete alikuwa pamoja na Lazaro. Halafu anavoitambuwa, huyu mtu, madhubuti moyo wake kuficha siri. Hakuwa mropokwaji. Yeye ukizungumza, anakwambia kesho anakwenda saka nguruwe. Ndo kazi yake. Hujui, hujui, hujui. Utamkuta katika baraza zake, anakuja Miembeni pale, kwa ajili “jumaapili hii tunakwenda saka wapi?” Hujui! Hujui. Bwana, mazungumzo yake yeye na wasasi. Huwezi kumtilia shaka hata mara moja. Anakwambia mahala fulani pana mbwa fulani, na mbwa huyo bwana “heeee! Nikimpata mie huyo raha sana.” Hiyo ndo kazi yake. Wakitaka kufanya fujo kule Baraza la Mapinduzi basi wanaambizana “jamani ee! Lakini mnaijuwa nyie kamati ya Mzee Karume? Pengine wengine wako hapahapa!”

Kamati hiyo ikikutana pahala padogo saana. Tena katikati ya mji. Polisi ya Kisima Majongoo unaijuwa? Sasa ile ilikuwa nyumba na nyumba yake [Karume] si ilikuwa pale pale? Sasa pale mazungumzo yao mle, Karume mchezaji bao. Utakuta hapa pana bao, hapa pana karata, hapa pana nini, hapa pana keram. Mle ndani mle. Kumbe wana yao wanakula. Hawamshitui mtu. Akitoka pale “je, unaona! Nimeshakufunga leo. Utafanya nini. Huna pesa wewe. Wacha nikupe pesa ukatumie kwa sababu nimekufunga sana.” “Wewe ngoja, tutaonana kesho. Mzee wewe leo unakujanifunga namna hii? Kesho tutaonana.” “Mawee! Umekwisha we! Kamata, katumie!” Yule bwana, sisi, au nikisema, mimi, ningekuwa nimetimiza miaka ishirini mpaka ishirini na tano na yule bwana, mimi nisingelifanya kazi ya mtu yoyote.

Mimi namkumbuka mzee Karume, kipenzi wa watu. Hukaa nikainama hasa, kwamba, Karume ni kipenzi wa watu. Karume hakusema huyu mwanangu, huyu mjukuu wangu, huyu fulani. Aa! Karume alipenda msema kweli. Mtu yoyote anozungumza na yeye anozungumza ukweli yeye anamtambuwa, basi yule anampenda Karume. Karume hakutaka wewe ukae kitako ukambughudhi mtu au ukamsengenya mtu. Hata. Ukimsengenya mtu kesho atakuweka na yule “bwana we hebu nambie yale maneno ulosema jana. Huyo hapo. Sema yale ulosema jana.” Utaona haya. Husemi. Hivo ndo alivokuwa yule kiumbe.

Anatoka hapaa, anakwenda Dar es Salaam anakwenda cheza bao na Mzee Nyerere. Sisi tunasema wanacheza bao kumbe kule wana lao wanatafuna. Akija huku humsikii. Mara anakwambia “natoka Dar es Salaam. Si bora tukaungana? Sisi wadogo hapa, watu hawa wazaliwa saa ingine ni watu wabaya. Watakuja kutugeuka hawa. Bora tuungane na serikali kubwa.” Akituzungumza sie. Kwa kukuogopa hapa [Zanzibar]. Aliwajuwa hawa watu eti bwana we! (anasema mbio mbio). Alijuwa. Hawa bwana, wabaya!13

Ubaya wake watageuza watu kuwa wanapendana binafsi na yeye ubinafsi alikuwa hataki. Watu wote walokuwa Zanzibar, Mnyamwezi wake, Mmakonde wake, wote walio hapa ni wake, midam wanazungumza kitu sawa. Sasa watakuja watu wabaguzi wa watu itakuwa si nchi tena. Tutaharibikiwa. Na itakuwa mapinduzi, mara tatu, mara nne. Itakuwa mara fulani, mara fulani. Bora nijitie hapa [Tanganyika]. Kakubaliana na watu hawa nnokwambia ni jirani zake. Fulani, fulani, jamaa mnaonaje tukafanya hivi? “Ah! Hivyo ndivyo.”14

Sasa wale mabotea wanotaka kufanya uharibifu hawajui washike wapi. Akiuliza mtu hapa “jamani, khasa serikali iko wapi? Atakwambia serikali iko Tanzania. Sisi hapa tawi tu hapa. Sasa wewe unayo nguvu ya kuingiliana na kule? Huwezi.” Wakaingia hao akina Makomredi kutaka ubabaifu. Karume akenda. Fulani unajuwa anafanya hivi anafanya hivi. “Ngojea, ngojea. Hapo hapo. Ngoja hapohapo.” “Fulani we, njoo! Naona nyinyi nafasi zenu hapa kwa serikali sasa hivi ilivosimama, nafasi zenu cheo kimoja kina watu kumi, ishirini, thalathini. Hakuna anaojifaraguwa.” Siasa ya Nyerere hiyo. Tena kafurahi mwenyewe kapigwa transfer [uhamisho]! Kumbe jungu lishapita pale. Anakuja tambuwa baadae! Yuko mbali na Zanzibar, hana base [jukwaa la wafuasi]. Sina hivi sina hivi na huko nliko nna cheo lakini nafatwa. Haya, mkuu wa jeshi Tanzania Bara! “Bwana hapa vyeo vote, kula cheo kina watu kumi, kumi na tano, bara huko hakuna nafasi?” “Ah, nafasi ziko. Nani nimchukuwe?” Kwanza akaanza kuchukuliwa Yusuf Himidi akapelekwa Tabora.

Kamati ya watu isihirini na tano ilikuwepo na ilikuwa na nguvu ile kwa mwenyewe, hayati Karume. Kafa yeye na ile imekufa. Kwa sababu ya yeye ilikuwa na mtetezi. Huna hata kitu kimoja cha kwenda kumgusa katika kamati yake ile. Kafa yeye hamnahamna, na kiongozi wa kamati, Tete, kafa. Na msaidizi kafa. Na wengine kwenye Baraza la Mapinduzi. Wale wote wamekufa mfululizo tu. Anakufa huyu, anakufa huyu, anakufa huyu. Likawa halina nguvu na sasa hivi ndo haliko kabisa. Wenyewe wamo humu. Tena ukikaa wanakwambia hasa “masikini, kufa kwa baba Karume, e Mungu! Mungu muweke mahala peponi.” Wanaomba dua hilo. Katuwacha maskini. Maskini. Maskini sie. Leo mie si mtu wa kusema “e bwana, hebu nigaie nauli nende zangu Mbweni hapo bwana. Hebu nigaie nauli nende zangu Mahonda. Sie. Hata! Sie kabisa!”


Mapinduzi Yasiofahamika

Sherehe za mapinduzi, ile kumbukumbu tu lakini mwenye kujuwa hasa hamna. Kwa sababu ingelikuwa wanaijuwa historia ilee, mpaka sasa hivi wanamapinduzi wamo japo kama wamebakia kidogo. Wale wangechukuliwa kama siku ile ya sherehe za mapinduzi wakawekwa mahala hasa. Wageni wanokuja wakaonyeshwa “jamani hawa ndo wenyewe wanamapinduzi.” Sasa hivi hawajulikani. Hata. Hawajulikani.

Kitu kilichodharaulisha historia ya mapinduzi ni ubinafsi! Ubinafsi. Leo mimi mkata maji. Unanchukuwa mimi ndo nnoijuwa historia ya hapa. Leo unaweza ukansogeza hapo nikafanya historia. Nikufanyie historia wewe ulozaliwa hapa? Hatuwezi kukubaliana. Huyu ataniponda mimi ntakuwa sijulikani. Kumbe wewe ndo ungepata masilahi yako. Leo unantupa mie, utaipata wapi siri ya mapinduzi? Utaipata wapi?

Alikuja jamaa mmoja kutoka Cuba tena akaja kwangu. Nimezungumza nayehistoria ilee, kapiga picha na nini. Alikuja kwa marehemu Athumani Bapa. Sasa Bapa hajui, ikawa kaniletea mie. Kwani [Athmani] Bapa hajui ndo akanileta kwako. [Ali Omar] Lumumba hajui ndo akakwita wewe mzee… Na wewe [mwandishi wa kitabu hiki] umenita mie hujui ndo mana ukanita mie. Na mimi siri yangu hasa, sikukupa pale. Sikutowa. Kwa sibabu wewe hutaki faida kwangu. Mimi sitaki faida kwako. Kwa sababu mimi mwenzio nimetembea nao wanamapinduzi. Kina mzee Kaujore, kina nani, huko tumekwenda kula mananasi mwitu. Na mpaka hivi nnavokwambia ukenda kulekule Ikulu kuna picha yetu maalumu ya mapinduzi. Hawataki kuitowa. Ukenda utakuta hasa. Huyu si fulani, mbona hapa kawa kizee na sasa hivi kijana huyu? Kumbe kwa ule uchungu wa kutafuta nchi. Nilikuwa na manywele shetani hafai. Mimi sina ndevu nilikuwa na ndevu.

Unajuwa, utakuta watu wa mapinduzi, lao moja, lakini kuna siri. Mimi inaweza kuwa kuna baadhi ya siri sizijuwi na huyu baadhi ya siri hii haijuwi. Lakini sasa basi. Inatokana na nini? Ufuatiliaji. Hilo suala, kwa mimi, sikatai, sikubaliani nalo, kwa sababu. Sikuona, wala sikulisikia, nalisikia hapa kama kuna Wamakonde na makabila mingine kutoka bara yamekwenda Zanzibar kwa ajili ya kushiriki katika mapinduzi. Lakini humo mote ninamotembea humo, sijalipata. Inawezekana. Kwa sababu sisi ni watu. Kwa sababu mimi baada ya mapinduzi, nimekaa miaka yangu miwili, mwaka wa tatu mimi nikatoka, niko nje tu. Urusi, China, wapi huko. Sasa matokeo ya huku nyuma, nisije nikayapinga kumbe yapo. Au nisije nikayakubali na mie sijayaona. Kwa sababu nikiyakubali mtu atanambia “hebu nihadithie.” Ntahadithia vipi? Hili suala mimi nnavolisikia Wamanamba, Manamba huchukuliwa huko kwenda kukata mkonge. Hili nasikia huko bara. Kuna Manamba wamechukuliwa mahala fulani, Kisarawe, Shimo la Mungu, nk, wamepelekwa Ngerengere kwa ajili ya kukata mkonge shamba la Mzungu fulani Mjerumani. Kuna Manamba Wanyakyusa wamechukuliwa wapi wamepelekwa Ngerengere kukata mkonge. Hili nnajuwa. Myakyusa alichukuliwa Manamba, Mmakonde alichukuliwa Manamba, lakini sio kwa sehemu za huku Zanzibar. Sehemu za bara kukata mkonge. Katika mashamba ya mkonge hili natambuwa.

Wanaweza walikuwa Manamba wametoka kule wamekuja hapa kabla ya mapinduzi. Lakini tafauti yenyewe ni kwamba nini, kukosa kuelewana kwamba hawa wamekuja hapa tunawaona tu wanalima kwenye nini… Si sawa sawa hapa tumetowa hadithi moja, Baraza la Mapinduzi, kamati ya watu ishirini na nne walikuwa hawawatambuwi. Na kama wanatambuwa, wanajuwa kama kigengi hiki ni cha nini? Ilikuwa hawakielewi. Na hili lilikuwa Baraza la Mapinduzi zima lakini kigengi hichi hawakijuwi. Na hiyo ya Manamba inawezekana au haiwezekani.


Machano, Makame, na Joseph

Hili suala sahihi kwa sababu kuwa sahihi, hivi sasa tunavozungumza kuna watu hawa wa hapa [Zanzibar] na watu wanotoka bara hawaaminiani mpaka kesho kutwa. Hata wakiwa ni Waisilamu. Chimbuko lake liko hivii. Anotoka bara la Afrika anamwambia huyu mtu wa Zanzibar “weye bwana, Mwenye Enzi Mungu kakujaalia tu ule kwenye serikali hii lakini mapinduzi yake huyajuwi. Wewe kama ulikuwa mdogo babako alijificha mvunguni. Suala hili lote waloungana ni wale wenye kulijuwa ndo walofanya kazi hii. Leo ukinambia mimi kwamba mimi ni mbara sijulikani hapa utakosea. Mimi ndo nlokupa mwega kupata serikali wewe hata ukawa mtu. Leo unanibaguwa mimi si mtu tunakubaliana. Kwa sababu wewe unasema mtoto wako waziri au babako waziri. Ndo unalinda hiyo. Mimi sina baba waziri lakini ndani ya mapinduzi mimi ndo mwenyewe. Sasa hilo suala ndo watu unaona mtu wa hapa anojuwa suala hilo anajuwa ‘alaa, huyu anaanza kuleta ubaguzi.’ Sasa utaona atakwambia ‘hapana, hebu tuliwache suala hili. Tuliwache. Tuingie kwenye chama chetu kinasema hivi, kinasema hivi.’ ”

Chuki itasimama kwa hawa wenye kupata mavyeo hapa na nini, watawachukia wabara. Hiyo uhakika. Hiyo hakika kwamba haya mambo ya hawahawa wabara na kumbe wamezungumza ukweli, wao ndo wenye kufanya shughuli hizi. Hawa wa hapa watafanya chuki.

Kitabu kitaleta chuki lakini hakileti chuki kwa sibabu kuna watoto wetu sisi, wajukuu zetu sisi, wanapata hii historia, sasa kitabu kile wale watasuta Wewe unajuwa nini? Hiki kitu halali. Leo hapa kinazungumza hiki. Hakuna mbara hakuna wa wapi. Wote wameshiriki kwenye shughuli hizi kwa manufaa yetu. Ngao hiyo sasa ndo itakayoweka bayana. Sasa tuungane tufanye shughuli zetu za kuijenga Zanzibar yetu. Hakuna chuki hapa. Atakaefanya organisation kwamba wewe mbara hii inaeleza hivi hivi hivi, atamwambia “Hata. Kwanini? Tazama, hapa, panaeleza hivi. Kabila hili, kabila hili, kabila hili, viongozi hawa na hawa, wa Kiafrika, mbona waliungana kwenye suala hili kwa umoja? Leo kwanini sisi tubaguwane?” Hakileti sura mbaya kitabu. Kinaleta upendo suala hili. Kwa vichwa vetu sisi wazee tunopotea kitaleta upendo kwa watoto zetu wale wasomi, kila atosoma akaona historia ilivo ataona hawa watu walishirikiana hawa. Ushirika wao mmoja, baba, mama, walikuwa pamoja hawa. Kwa vile na sisi hebu tukamatane kwenye suala hili kwa upendo. Isipokuwa Jazeera, Pemba, watakuja kujiuliza. Hakuna alieshirikishwa hasa baada ya Shamte kusema “hata mkinipa utume sitoshirikiana na nyinyi.” Wangekubali kuwa kitu kimoja Zanzibar kusingelikuwa na mapinduzi.

Bwana hili lifanyie mpango litokee! Saana. Safi kabisa. Litokee! Watoto zetu ambao ni Wazanzibari watapata mbegu za kutembea. Watapata nguvu ya kuzungumza. Wanakaa wawili, wanakaa wawili. Pengine wote wako chuoni au skuli, wamesoma wakaona “Ah! Bwana we, kwanini tukaanza kuchukiana mimi na wewe? Wewe babako si huyu hapa? Mimi babangu si huyu hapa? Sasa walipokutana walikuwa wakitafuta nini? Si walitafuta serikali. Serikali si ndo hii? Mbona hawa hawakubaguwana, tubaguwane mimi na wewe? Hata! Tufuate hii bwana. Hii inatuongoza.” Hatima utakuta hii Zanzibar hakuna tena mpasuko.
 

Nnangale

JF-Expert Member
Jul 20, 2013
2,664
1,360
okello alidhurumiwa baada ya mapinduzi angelipwa kama wakukodiwa na siyo kutupwa bila msaada wowote.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

1 Reactions
Reply
Top Bottom