Serikali yasema inatekeleza mikakati ya msamaha ya Dawa kwa Wagonjwa wenye changamoto ya Akili

Serikali yasema inatekeleza mikakati ya msamaha ya Dawa kwa Wagonjwa wenye changamoto ya Akili

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
4,783
Reaction score
14,975
Serikali imesema inaendelea kutekeleza mkakati mahsusi wa kuhakikisha wagonjwa wa afya ya akili wanapata dawa bure au kwa gharama nafuu, kwa kuzingatia Sera ya Afya ya Mwaka 2007, sura ya 5, sehemu ya 4, ibara ya 1 hadi 3, inayotoa mwongozo wa utoaji wa huduma kwa watu wenye magonjwa ya muda mrefu.

Akijibu swali la Stella Ikupa Alex (Viti Maalum), Mei 20, 2025 Bungeni jijini Dodoma, kuhusu mkakati wa Serikali wa kutoa dawa bure kwa wagonjwa wa akili, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa Serikali inazingatia hali ya kiuchumi ya mgonjwa au mlezi wake kabla ya kutoa msamaha wa gharama za matibabu.

Dkt. Mollel amesema mfumo huu unatekelezwa kupitia ushirikiano wa karibu kati ya Maafisa Ustawi wa Jamii walioko hospitalini na watendaji wa kata kutoka maeneo wanakoishi wagonjwa husika. Mfumo huu huruhusu tathmini ya kijamii kufanyika ili kubaini uwezo wa mgonjwa au familia yake kuchangia gharama za matibabu, na iwapo wanastahili msamaha.

“Lengo kuu ni kuhakikisha hakuna mgonjwa wa akili anayekosa dawa kutokana na hali ya kipato,” amesema Dkt. Mollel, akibainisha kuwa Serikali inahimiza ufuatiliaji na uratibu madhubuti wa huduma hizi hasa katika maeneo ya vijijini ambapo mahitaji ya huduma za afya ya akili ni makubwa.

Aidha, Naibu Waziri ameeleza Serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa muhimu za afya ya akili katika vituo vya afya na hospitali za rufaa nchini, sambamba na kutoa mafunzo kwa watoa huduma ili kuongeza uelewa na ufanisi wa utoaji wa huduma hizo.

Serikali inaendeleza jitihada za kuhakikisha huduma za afya zinakuwa jumuishi na zinafikia kila Mtanzania bila ubaguzi, hasa wale walio katika mazingira magumu na wasio na uwezo wa kifedha.
 
Back
Top Bottom