elivina shambuni
JF-Expert Member
- May 31, 2018
- 461
- 295
SERIKALI imefuta miliki ya mashamba matatu ya Mkomazi Plantantions, maarufu MOA, yaliyoko Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga kutokana na kukiuka masharti ya uendelezaji.
Imeelezwa kuwa moja ya masharti yaliyokiukwa ni mashamba hayo kutoendelezwa na hayajalipiwa kodi ya pango la ardhi. Uamuzi huo ulitangazwa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipozungumza na wananchi wa Mayomboni wilayani Mkinga alipokwenda kutatua mgogoro wa muda mrefu katika eneo hilo.
Mashamba yaliyofutiwa ni yenye hati Na. 9780 na ukubwa wa ekari 14,688, shamba Na. 4268 lenye ekari 804 na shamba lenye hati Na. 9781 lenye ekari 246. Kutokana na uamuzi huo, jumla ya vijiji 10 vyenye kaya 3,236 zenye wakazi 16,450 zitanufaika na uamuzi wa serikali kutokana na wananchi wake kuvamia mashamba hayo na kufanya maendelezo ya kujenga makazi, shule na kuendesha shughuli za kilimo cha mazao ya kudumu na ya muda mfupi.
Vijiji vilivyonufaika na uamuzi wa serikali ni Kilulu-Dunga, Zingibari, Mwaboza, Mwakikoya, Mhandakini, Nkanyeni, Sigaya, Mayomboni, Ndumbani na Moa. Akizugumza wakati wa kutangaza uamuzi huo, Waziri Lukuvi alisema uamuzi wa kufuta mashamba hayo matatu unafuatia maombi yaliyotumwa kwa Rais John Pombe Magufuli ya kutaka kufutwa mashamba hayo kutokana na kutoendelezwa na wamiliki wake kwa muda mrefu.
Alisema Rais ameridhia maombi hayo kwa kuwa serikali imekuwa ikisisitiza utekelezwaji wa Sheria ya Ardhi Na. 4 ya Mwaka 1999 inayotaka uendelezaji wa mashamba ambayo yamemilikishwa katika maeneo mbalimbali nchini. Waziri huyo pia aliagiza kufanyika upimaji katika vijiji vyote 10 na kuainishwa mipaka ya vijiji hivyo na kupatiwa hati ili wananchi wanaoishi kwenye vijiji hivyo wasibughudhiwe.
Lukuvi pia alitaka maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya uwekezaji katika shamba yaliyofutwa kuachwa kwa ajili ya shughuli hiyo ikiwamo mwekezaji wa Katani, Azka International Tanzania mwenye ekari 500 pamoja na maeneo ya viwanda.Katika hatua nyingine, Waziri Lukuvi aliagiza kufanyika uhakiki wa mashamba mengine ya Kwa Mtili Estates Co. Ltd yaliyoko Mkinga mkoani Tanga ambayo alibaini ekari 58 pekee ndiyo zilizoombwa kufutwa kwa Rais kutokana na kutoendelezwa huku mmiliki wake ikidaiwa kumiliki ekari 2,841.
Hatua hiyo inatokana na Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Obed Katonge, kueleza kuwa Kwa Mtili Estates Co Ltd inalo shamba lenye ukubwa wa ekari 2,841 tofauti na inavyoonekana katika kumbukumbu za ofisi ya Msajili wa Hati Kanda ya Kaskazini ambazo ni 58.
Lukuvi aliagiza wataalamu wa ardhi kutoka Kanda ya Kaskazini kufanya uhakiki huo katika kipindi cha mwezi mmoja na kumpa taarifa ya uhakiki huo mwisho wa mwezi ujao na pale itakapothibitika kuna ujanja uliofanyika wa kumwongeza mmiliki wa shamba hilo, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika. Mbunge wa Mkinga, Dustan Kitandula, aliishukuru serikali kwa kusikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wanaoishi eneo la shamba lililofutwa la kutaka kurejeshewa ardhi yao waliyokuwa wakiitumia kwa shughuli mbalimbali. Alisema mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa Mkinga na wamiliki wa mashamba ya Mkomazi Plantantions Co. Ltd ni wa muda mrefu na anaamini uamuzi wa serikali umepeleka furaha jimboni kwake.