Serikali haina hoja juu ya uwezo huu wa Mahakama | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali haina hoja juu ya uwezo huu wa Mahakama

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mzee Mwanakijiji, Apr 15, 2010.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Apr 15, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Na. Lula wa Ndali Mwananzela (Raia Mwema)  KATIKA kesi hii inayoendelea nchini, ambayo imedumu kwa muda mrefu, masuala makubwa mawili yanatarajiwa kutolewa uamuzi na Mahakama ya Rufani.
  Kwanza, ni suala la mgombea binafsi/huru kuweza kushiriki katika chaguzi mbalimbali nchini. Suala hili tayari limeshatolewa uamuzi mara kadhaa huko nyuma ambapo mahakama zote zilizosikiliza suala hili zimekubalina kuwa hakuna hoja ya kikatiba au kisheria inayoweza kumzuia Mtanzania kugombea endapo ametimiza sifa za msingi zinazomruhusu vile vile kupiga kura.  Suala hili la haki ya wagombea huru/binafsi kuruhusiwa kushiriki chaguzi zetu nimeshaliandikia kwa muda mrefu miaka kadhaa iliyopita, na siyo kusudio langu kulizungumzia katika makala hii.


  Suala la pili, hata hivyo, ni kubwa zaidi na ambalo naamini ni la msingi sana (rejea mahojiano yangu na Waziri Phillip Marmo) ni hili linalohusu uwezo wa Mahakama zetu nchini kutengua sheria pale ambapo sheria inaonekana kupingana na Katiba na kutokana na hilo ni uwezo wa mahakama kutengua kipengele cha Katiba pale ambapo kipengele hicho kinapingana na kipengele kingine cha katiba.
  Hapa yapo mambo mawili yaani la sheria kupingana na Katiba na lile la kipengele cha Katiba kupingana na kipengele kingine cha katiba.  Kuelewa mgawanyo wa mihimili
  Ni muhimu kwanza kuelewa nadharia zinazoongoza tawala za kidemokrasia duniani. Kuna nadharia kadhaa ambazo ndizo zinaunda msingi wa tawala za kidemokrasia na kubwa kati ya hizo ni mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili ya serikali (separation of powers), uhuru wa kutoa maoni (freedom of speech), uhuru wa habari – kupata na kutoa (free press), uhuru wa imani (religious freedom) na ushiriki wa wananchi katika utawala – aidha moja kwa moja au kupitia wawakilishi wao.  Katika hayo naomba nichukue hilo la kwanza; yaani mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili ya serikali.  Kama tunavyofahamu serikali inaundwa kwa mihimili mitatu; yaani Utendaji (Rais na wote wanaotekeleza majukumu mbalimbali kwa mujibu wa sheria na ofisi zao – mara kwa mara tunawaita hawa ni “serikali”), Mahakama; yaani Jaji Mkuu na vyombo vyote vinavyoshughulikia suala la upatikanaji na utoaji wa haki na Bunge; yaani Spika na wabuneg na vyombo vyote vinahusiana na mchakato wa kutunga sheria na usimamizi wa serikali pamoja na ushauri.
  Katika demokrasia vyombo hivi vitatu vinahusiana sana na wakati huo huo vinaachiana madaraka mbalimbali. Wakati wowote vyombo hivi vinapogongana au kushindwa kufanya kazi kwa pamoja, basi, demokrasia yenyewe inakuwa mashakani.
  Hivyo, utaona Rais anaapishwa na Jaji Mkuu, Jaji Mkuu anateuliwa na Rais, Rais anaweza kuondolewa na Bunge, na Rais anaweza kuvunja Bunge (siyo wakati wowote apendavyo) n.k.
  Kutokana na mahusianao haya, nadharia mpya ambayo ni sehemu ya nadharia ya mgawanyo wa madaraka ni nadharia ya kusimamiana katika mihimili hii.  Nadharia ya kusimamiana kwa mihimili (checks and balances)
  Kwa wengi wetu tunafahamu nadharia hii kama uwiano wa madaraka (balance of powers) kati ya mihimili. Hata hivyo uwiano wa madaraka siyo lazima uwe umetengeneza mfumo wa kusimamiana. Kwenye “balance of powers” mihimili hii mitatu inaachiana madaraka ili kuzuia mhimili mmoja kuwa na madaraka makubwa zaidi au kuwa na madaraka yote.
  Kwa mfano, hapo zamani za enzi wafalme walikuwa ndiyo wenye madaraka yote; yaani watawala, waamuzi na wenye kutunga sheria za jamii zao. Katika demokrasia yenye mfumo wa kijamhuri kama ya kwetu, Rais hawezi kuwa ndiyo Jaji Mkuu hata kama angependa, au Jaji Mkuu kuwa ndiyo Spika wa Bunge au wabunge kuwa ndiyo majaji hata kama wangependa wawe hivyo!  Jambo hili ni muhimu kulielewa kwa sababu ndiyo msingi wa hoja ambayo ningependa kuiweka ieleweke.  Kwamba katika utawala wa demokrasia siyo tu kuwa mihimili ya dola imegawanywa; bali pia imepeana uwezo wa kusimamiana ili kuhakikisha mhimili mmoja hautendi juu ya mhimili mingine au kuinuka juu ya wananchi ambao ndio msingi wa madaraka yote ya kutawala.
  Katika nchi za kidikteta na kibabe unaweza kusikia kuwa zipo mahakama, Bunge na Rais lakini hivi vitatu kwa kweli vinakuwa ni vyombo vya geresha tu kwani nguvu kubwa iko kwa rais ambaye anaweza kufanya lolote.  Vyombo vyote lengo lake ni mwananchi
  Katiba yetu inasema hivi “lengo kuu la serikali ni ustawi wa wananchi”. Hii ina maana serikali yetu haiwezi kuweka lengo la “kuwanufaisha wawekezaji”, “kufurahisha nchi wahisani” au kundi jingine lolote lile nje ya wananchi wa Tanzania.
  Ni muhimu kutambua na kuelewa kuwa lengo la serikali ni kumtumikia mwananchi. Tutafanya makosa makubwa tukifikiria kwamba kuna lengo jingine lolote la serikali. Mahali popote duniani serikali inaposhindwa kumtumikia mwananchi, basi, serikali hiyo inapoteza uhalali wake na wananchi wana haki ya kuiondoa kwa njia za kawaida za sanduku la kura au pale ambapo wananchi wanaona kuwa serikali haiwezi kutengeneza mazingira ya uchaguzi huru na wa haki kufanyika, basi, wananchi wanayo haki ya kuasi dhidi ya serikali na kuiondoa hata kwa nguvu.  Siamini kama tumefikia mahali pa kutumia njia nje ya Katiba za kuiondoa serikali madarakani; kwani bado pamoja na udhaifu wake vyombo vyetu vya demokrasia vinafanya kazi.


  Tukielewa lengo hili la kutumikia wananchi hatuna budi pia kukubali kuwa serikali (Mahakama, Bunge na Rais) ni lazima wanapofanya maamuzi yao, matendo yao, sheria wanazotunga n.k ni lazima vilenge kumnufaisha mwananchi wa Tanzania.  Wakati wowote chombo kimojawapo kinapoenda kinyume na lengo hili chombo hicho ni lazima kisahihishwe na pale inapopasa kibadilishwe. Hivyo, Rais na watendaji wengine kazi yao ni kutekeleza mambo ambayo wananchi wamewakabidhi kuyatekeleza aidha kwa kupitia makubaliano ya uchaguzi, kuagizwa na Bunge au kuamuliwa na Mahakama.
  Mahakama ikisema mtu fulani afungwe miaka 20 ni serikali ndiyo inatekeleza hukumu hiyo, Bunge likisema iundwe Idara ya Wanyamapori, basi, ni watendaji (executive) wanaotekeleza suala hilo.


  Bunge kwa upande wake linapewa jukumu la kawaida la kutunga sheria. Hili linafanywa kwa njia ya kawaida pale ambapo watendaji (rais na wenzake) wanapotaka kuwa na uwezo wa aina fulani, au kupewa chombo fulani. Hivyo, Rais hawezi kukurupuka tu na wenzake wakaamua kujianzishia taasisi wanazozitaka wao bila ya sheria za Bunge (ukiondoa yale ambayo wao wamepewa uwezo kuyafanya kisheria) na Bunge ndilo linapanga fedha za kutumiwa na mihimili hiyo mingine.  Mahakama kwa upande wake ina jukumu moja kubwa nalo ni kuhakikisha kuwa mwananchi anapata haki yake. Rais na Bunge hawawezi na hawapaswi kuwa waamuzi wa haki za wananchi, wanataka wazilinde na kuzisimamia na pale ambapo wananchi wanaona wanapotezewa haki zao wanatakiwa kukimbilia mahakamani.


  Mahakama ndiyo mwamuzi wa haki
  Katiba yetu inasema hivi: “Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na Mahakama na vyombo vinginevyo vya Mamlaka ya Nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria” (Ibara 13:1) na vile vile “Mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa mikononi mwa Idara ya Mahakama na Idara ya Mahakama ya Zanzibar, na kwa hiyo hakuna chombo cha Serikali wala cha Bunge au Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki.” (Ibara ya 107A:1).


  Vipengele hivyo ni muhimu sana kuvielewa linapokuja suala la uwezo wa mahakama kutengua sheria au hata kipengele kingine chochote kile cha Katiba. Ni muhimu kuvielewa kwa sababu swali lililo mbele ya Mahakama ya Rufaa inahusu mambo yote mawili; yaani haki ya wagombea binafsi na uwezo wa mahakama.


  Haki yako ikivunjwa au kunyimwa ukimbilie wapi?
  Kama tungekubali hoja za serikali ni wazi kuwa mwananchi akiona serikali inamminyia haki zake aende Bungeni kutaka Bunge lirekebishe! Kwamba, kama serikali inatenda jambo fulani lenye kutishia haki zako kama binadamu na kama raia usiende mahakamani bali umtafute mbunge wako ili aende Bungeni waweze kufanya mabadiliko ya sheria.
  Dhana hii ni potofu na ya kipuuzi (absurd). Miaka yote tumewasikia viongozi wa CCM wakiwahimiza watu wanaodai kuwa wamevunjiwa haki zao kuwa waende mahakamani iweje leo watuambie twende Bungeni?


  Haki ya kuchaguliwa imezuiliwa
  Walipoamua kulazimisha kuwa wagombea wote wa nafasi za kisiasa ni lazima wawe ni wale wanaosimamishwa na vyama vya kisiasa, serikali ya CCM ilichezea na kutupa mbali haki ya mwananchi kuchaguliwa na kushiriki katika uongozi wa nchi yake. Walivunja Ibara ya 13:1 ambayo inatangaza kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria, na walivunja kipengele cha 2 cha ibara hiyo hiyo ambacho kinakataza serikali kutunga sheria au kuchukua hatua ambayo itakuwa ni ya kibaguzi kwani utaratibu wao unawapendelea watu wa kwenye vyama vya siasa na kuwazuia watu wasio na vyama kushiriki katika siasa za nchi yao.  Dhana ya kupitiwa na Mahakama (Judicial Review)
  Sasa hili naamini ndilo msingi wa Ibara ya 30:5 na ni muhimu ni nukuu kwa kuweka msisitizo. “Endapo katika shauri lolote inadaiwa kwamba sheria yoyote iliyotungwa au hatua yoyote iliyochukuliwa na Serikali au mamlaka nyingine inafuta au inakatiza haki, uhuru na wajibu muhimu zitokanazo na ibara ya 12 hadi 29 za Katiba hii, na Mahakama Kuu inaridhika kwamba sheria au hatua inayohusika, kwa kiwango inachopingana na Katiba ni batili au kinyume cha Katiba, basi, Mahakama Kuu ikiona kuwa yafaa au hali au masilahi ya jamii yahitaji hivyo, badala ya kutamka kuwa sheria au hatua hiyo ni batili, itakuwa na uwezo wa kuamua kutoa fursa kwa ajili ya Serikali au mamlaka nyingine yoyote inayohusika kurekebisha hitilafu iliyopo katika sheria inayotuhumiwa au hatua inayohusika katika muda na kwa jinsi itakavyotajwa na Mahakama Kuu, na sheria hiyo au hatua inayohusika itaendelea kuhesabiwa kuwa ni halali hadi ama marekebisho yatakapofanywa au muda uliowekwa na Mahakama Kuu utakapokwisha, mradi muda mfupi zaidi ndio uzingatiwe.”


  Ibara ya 12 hadi ya 30 ni ibara ambazo zimewekwa chini ya kundi la “Haki na Wajibu Muhimu”. Mafungu haya yanalinganishwa na Orodha ya Haki za Msingi (Bill of Rights) ya Wamarekani ambayo inalindwa kama lulu ya thamani kubwa.  Haki za Watanzania zinatambuliwa na Katiba katika sehemu hiyo na ni jukumu la serikali na vyombo vyote kuhakikisha kuwa haki hizo zinalindwa na kuhifadhiwa. Kama taifa la watu walio huru hatuwezi na hatupaswi kumuacha mtu, chama, kikundi, au jamii yoyote ya watu kutishia haki hizi. Ni haki ambazo tunaweza kuziita ni takatifu (sacred).
  Serikali au chombo chochote kwenye nchi hii hakiwezi kuchezea haki za wananchi kwa sababu haizipendi au zinatishia uwepo wa serikali hiyo au maslahi ya chama fulani cha kisiasa. Wakati wowote chombo, idara, au taasisi yoyote inaingilia haki na wajibu wa mwananchi ni haki ya wananchi kukimbia mahakamani kuzuia chombo hicho na kupata ulinzi.
  Ni kutokana na hili nchi mbalimbali za kidemokrasia zimekubali nadharia kuwa mahakama zina uwezo wa kuingilia kati maamuzi, mipango na hatua za serikali pale zinapoingilia uhuru na haki za wananchi na kupima mambo haya kwa mwanga wa katiba.
  Kwa maneno mengine, mahakama zina uwezo wa kuamua kama tendo, uamuzi, sheria, au jambo fulani linalofanywa au lililoamuriwa kufanywa na Bunge au Urais kama linakubaliana na Katiba au pale ambapo mahakama inasema kuwa jambo hilo ni kinyume na Katiba, basi, kwa kadri ambavyo mahakama imesema jambo hilo linakuwa limetenguliwa na kufutwa.
  Kwenye nchi kama Marekani ambapo nadharia hii imeota mzizi katika utawala wao wa sheria, mahakama ikishatoa uamuzi huo jambo hilo haliwezi kutekelezwa tena isipokuwa kama kuna rufaa mbele.  Ni nadharia hii ndiyo msingi wa ibara ya 30:5 tuliyoiona hapo juu. Hivyo, wale wanaosema kuwa mahakama haina uwezo wa kuamua jambo, sheria, au uamuzi wa serikali na kuupima kama linakubaliana na Katiba hawajui wanachosema au kwa makusudi wanataka tukubali uongo kama ukweli.


  Kutengua sheria au kipengele cha Katiba kwa Katiba?
  Ni rahisi zaidi kwa mahakama kutengua sheria au kipengele fulani cha sheria kwa kutumia Katiba. Na ni rahisi vile vile kusema kuwa uamuzi au hatua fulani ya serikali ni kinyume na Katiba.  Kwa mfano, Bunge likiamka siku moja na kutunga sheria inayosema kuwa kuanzia sasa hakutaruhusiwa kuwepo kwa dini yoyote nchini Tanzania na Rais akaridhia na ikawa sheria, wananchi watakimbilia mahakamani na kudai kuwa serikali imevunja Katiba kwa sababu Katiba inatambua haki ya wananchi kuwa na imani na dini zao. Hivyo, mahakama inaweza kutangaza kwa urahisi tu kuwa sheria hiyo mpya ni kinyume na Katiba na papo hapo sheria hiyo inakosa nguvu au kwa muda ambao mahakama itakuwa imeweka kwa serikali kujisahihisha.  Hata hivyo, hili siyo rahisi pale ambapo serikali badala ya kutunga sheria inaamua kuingiza kwenye Katiba kitu ambacho kinapingana na haki zile za msingi. Yaani, serikali inatambua kuwa ikitunga sheria juu ya jambo hilo inaweza kufutwa kwa hiyo inaamua kuliingiza jambo hilo kwenye Katiba.


  Hivi ndivyo ilivyofanya kwenye suala la mgombea binafsi mara ya kwanza; kwani wakati wanasubiri kusikiliza rufaa ambayo wameipoteza, serikali ikaenda Bungeni na kufanya mabadiliko ya Katiba kwa kutumia sheria namba 34 ya 1994 (Mabadiliko ya 11 ya Katiba) na kuingiza kwenye Katiba kitu ambacho hakikuwapo mwanzoni kwa uwazi huo.  Mabadiliko hayo yakafanya ni lazima kuwa wagombea wote wa ngazi zote ni lazima wawe wanatokana na vyama vya kisiasa, na matokeo yake ni mara moja kufuta wagombea huru na binafsi. Hili lilimkorofisha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na kuita kuwa ulikuwa ni uamuzi wa kipumbavu – nakubaliana naye.  Mbinu hii ikikubaliwa ni hatari kwa demokrasia
  Sasa kama tutakubali kama serikali inavyotaka kuwa jambo likishaingizwa kwenye Katiba haliwezi kupitiwa (judicial reviewed) na mahakama matokeo yake yatakuwa ni yale yale. Serikali itaanza kukwepa kuleta sheria na itakuwa inafanya mabadiliko ya haraka ya Katiba na kuziba midomo wakosoaji. Hili halipaswi kukubaliwa.  Jukumu kubwa, basi, kwa mahakama katika kesi hii siyo suala la wagombea binafsi; kwani hili ni rahisi na mtu yeyote anayeelewa misingi ya demokrasia anaweza kutabiri kwa urahisi tu kuwa Mahakama ya Rufani itakubali hukumu mbili za huko nyuma ambazo zote zilikubali uwepo wa wagombea binafsi.  Suala gumu zaidi ni hili la mahakama kutengua kipengele cha nyongeza cha Katiba ambacho kinapingana na vipengele vya awali au kinatishia haki za msingi. Kutokana na haya naomba niseme yale ninayoweza kuyatabiri kwa uhakika yatatokea na yanapaswa kutokea.
  Mahakama ya Rufani:

  1. Inapaswa kutambua haki ya kila Mtanzania kushiriki katika uongozi wa nchi yake kwa kuchagua na kuchaguliwa bila ya kulazimishwa kusimamishwa na chama cha siasa akiwa ametimizi masharti ya msingi ya kugombea;
  2. Uamuzi wa Mahakama ya Rufani huko nyuma uliotoa muda wa kutosha kwa serikali kujiandaa kwa kuweka mazingira ya wagombea huru/binafsi kushiriki unasimama na hakuna haja ya muda wa nyongeza. Hukumu ya Jaji Manento ilikuwa wazi kuwa “kuanzia sasa (2005) hadi uchaguzi mkuu ujao mdaiwa” awe ameweka mazingira na miundombinu ya kuhakikisha kuwa wagombea huru nao wanashiriki. Serikali imepewa zaidi ya miaka minne na kiujumla zaidi ya miaka kumi kuingiza wagombea binafsi. Walikuwa na nafasi katika chaguzi ndogo zilizopita kufanya mazoezi ya suala hili na hawakutaka.Mahakama ya Rufani isiwadekeze.
  3. Mahakama itangaze wazi kabisa kuwa inayo mamlaka na uwezo wa kutosha kabisa kupitia jambo, sheria, matendo yoyote ya chombo chochote cha serikali pale mambo hayo yanadaiwa kugongana na Katiba au haki za msingi za wananchi. Vinginevyo, tutaruhusu wanasiasa waanze kufanya mambo bila kujali matokeo yake kwa haki za wananchi.
  4. Kwa vile gharama zozote kubwa ambazo zinaweza kutokea kwa kuingiza wagombea binafsi sasa hizi ni gharama ambazo zingeweza kuepukwa miaka mitatu iliyopia basi mahakama isikubali hoja ya gharama na muda kuwa ni kizuizi cha wagombea binafsi. Endapo mahakama itaamua kuchelewesha kuruhusu wagombea binafsi kwa madai kuwa serikali itaingia gharama zaidi basi itakuwa imezawadia uzembe na kutokuwajibika. Kama serikali isingetaka gharama za ziada ingetekeleza hukumu ya mahakama kwani tayari wanajua wameshapoteza kesi hii mara mbili. Hizo gharama zitakuwa ni funzo kwa serikali kutii mahakama kwenye masuala ya msingi bila kudharau na kupuuzia kama walivyofanya.
  5. Endapo licha ya kutoa maamuzi hayo hapo juu serikali itakataa kutii mahakama, basi, Jaji Mkuu na majaji wote wa Rufaa nchini watapaswa kujiuzulu nafasi zao mara moja ili kutokuwa sehemu ya utawala usioheshimu Katiba.
  Kesi hii ni muhimu kwa haki za wananchi, uhuru wa mahakama na uwezo na madaraka ya mahakama. Kinyume cha hapo ni kukaribisha utawala wa kibabe.
  Ni matumaini yangu kuwa mahakama itafikia uamuzi ambao ni wa kihistoria, ni muhimu kwa demokrasia na ambao utalinda haki za wananchi wetu na kuwapa kinga Watanzania kutoka katika kucha ndefu zilizochongwa za mikono mirefu ya serikali.


  lulawanzela@yahoo.co.uk
   
 2. Kamakabuzi

  Kamakabuzi JF-Expert Member

  #2
  Apr 15, 2010
  Joined: Dec 3, 2007
  Messages: 1,497
  Likes Received: 81
  Trophy Points: 145
  Umetufundisha na kutufafanulia mengi katika katiba. Asante sana.
  Naamini uamuzi wa mahakama hautakuwa tofauti sana na ulivyoeleza.
   
 3. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #3
  Apr 15, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Kamakabuzi.. ndio maana nimeshangaa yule Profesa kujenga hoja zisizo na msingi kabisa.. na kama kuna wanafunzi waliopitia chini yake wenye msimamo kama huo basi tuna matatizo makubwa zaidi.
   
 4. M

  Msee Lekasio Member

  #4
  Apr 15, 2010
  Joined: Mar 25, 2010
  Messages: 73
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nakbaliyana kabisa na huyu nduku mwandishi Lula kwamba mahakama lasima iangalie kesi hii kwa usito unaostahili. Sababu ni kwamba KAMA mbinu chafu iliyotumiwa na sirkali ya kurekebesha katiba ili ikisi matakwa ya watawala itakubaliwa, itakuwa imewafungulia mdhango wa udikteta na huko mbedheni sitakuja kujitokesa cases sa aina hii nyingi kwani mbusi ikisoea kudha ndisi haichi....
   
 5. Rufiji

  Rufiji JF-Expert Member

  #5
  Apr 15, 2010
  Joined: Jun 18, 2006
  Messages: 1,710
  Likes Received: 161
  Trophy Points: 160
  Lula , shule uliyoipiga hapo ni kubwa sana ! Mungu akubaliki. Mimi baada ya kusoma nusu tuu, nikaona siifaidi vizuri. Nikaamua niiprint then nikaenda Starbucks nikaanza kuisoma taratibu huku nikishushia na gahawa.

  Sidhani kama watu ambao ni close-minded wanaweza kukuelewa unasema nini , hoja ulizozijenga zinasimama zenyewe. Lula, umezichambua branches za government mpaka nikapata hasira, hii article yako ni kama kisu cha moto kinachopitishwa juu ya siagi. Haya ndiyo tunayoyaita mapambano ya fikra.
   
 6. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #6
  Apr 15, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Rufiji.. ni vizuri tunavyofanya hivi kwa kutoa michango yetu ya kifikra kwa namna hii..
   
 7. Mag3

  Mag3 JF-Expert Member

  #7
  Apr 15, 2010
  Joined: May 31, 2008
  Messages: 9,094
  Likes Received: 6,188
  Trophy Points: 280
  Mwanakijiji, pamoja na mahakama kuwa na nguvu ya hoja, serikali yetu ina hoja ya nguvu katika dola na bunge. Serikali imekamata mpini wakati mahakama pamoja na kujitahidi kutoa haki ni wazi imekamata makali kwani serikali itahakikisha katiba kama ilivyo inailinda katika maamuzi yake kupitia bunge. Swali hapa ni kifanyike kitu gani serikali yetu tuliyoiwekwa madarakani inapoamua kumnyima haki ya msingi mwananchi kwa kutumia katiba hiyo hiyo iliyotakiwa kuilinda hiyo haki. Mpaka hapo katiba itakapofanyiwa mabadiliko ya msingi, mchezo utakuwa ni huo huo na ni juu yetu wananchi tutakapoamua kusema basi, hatukubali tena - bahati mbaya wananchi ni hao hao wanaoiangusha mahakama.
   
 8. Kiby

  Kiby JF-Expert Member

  #8
  Apr 15, 2010
  Joined: Nov 16, 2009
  Messages: 5,202
  Likes Received: 1,007
  Trophy Points: 280
  Mwanakijiji ahsante sana, unajua mtu unaweza kuwa na utusi utusi katika jambo fulani, lakini unapopata ufafanuzi kama huu wa MwK milango yote ya fahamu inafunguka na kupewa uwezo wa kutambua kinagaubwaga namna serikali inavyoweza kupoteza haki yake ya kutawala kwa kukaribisha udikiteta tene kwa makusudi. Ni uelewa kama huu unaoweza kuwapa raia ujasiri wa kuiondoa serikali yao kimabavu ikiwa serikali yenyewe imeamua kuukanyaga utawala wa kisheria na kutokuziheshimu haki za wananchi zinazoainishwa na katiba. BE BLESSED MWK!
   
 9. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #9
  Apr 15, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Mag3.. kwenye pendekezo hili ni: 5. Endapo licha ya kutoa maamuzi hayo hapo juu serikali itakataa kutii mahakama, basi, Jaji Mkuu na majaji wote wa Rufaa nchini watapaswa kujiuzulu nafasi zao mara moja ili kutokuwa sehemu ya utawala usioheshimu Katiba.
   
 10. Kaa la Moto

  Kaa la Moto JF-Expert Member

  #10
  Apr 15, 2010
  Joined: Apr 24, 2008
  Messages: 7,666
  Likes Received: 164
  Trophy Points: 160
  Mwanakijiji umewakamata hawa wajinga wanaotufanya watanzania wote majuha. Na hasa huyu mtu Waziri Phillip Marmo kwangu ni adui kabisa wa demokrasia. Mbabe, dikteta, ambaye anadhani hakuna siku ataulizwa na kizazi cha watanzania kwa nini alichezea katiba yetu.
  Ndege mjanja unaswa katika tundu bovu. Iko siku hata kama si leo.
   
 11. N

  Ngekewa JF-Expert Member

  #11
  Apr 15, 2010
  Joined: Jul 8, 2008
  Messages: 7,730
  Likes Received: 23
  Trophy Points: 135
  Hapana la kushangaza kabisa kwa vile Serikali ni CCM na CCM ni Serikali. Hivyo Watanzania tutategemea nini kutoka kwa CCM isiyotaka Demokrasia? CCM na TANU huko nyuma zimekuwa siku zote kutaka kuona Watanzania wanaongozwa wakiwa kama kondoo wa kafara. Kwa kipindi cha miaka yote ya Uhuru wa Tanzania lini wananchi waliwahi kuwa waamuzi wa mambo yao? Tulishuhudia Ujamaa ambao mwisho wake uliwanufaisha tabaka la Viongozi, na baada ya kuondoka Ujamaa tulishuhudia kunufaika kwa Wafanyabiashara na Viongozi.
  Kuja kwa vyama vungi tukitegemea ukombozi lakini CCM imekuwa ikiibana Demokrasia. Hili la mgombea binafsi lingeweza kuwa tishio kwa CCM lakini kwa vile wao ndio wao watalitupa hili. Hebu angalia Kesi ya Serikali na analetwa mtumishi wa Serikali ( Mkurugenzi wa Mashtaka wa Zanzibar) atowe ushauri wa kesi inayoikabili serikali, hapa pamekaa sawa?
   
 12. O

  Ogah JF-Expert Member

  #12
  Apr 16, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 6,229
  Likes Received: 71
  Trophy Points: 145
  Kuna "vipofu"...............rigid minds hawawezi kuelewa huo uchambuzi hata siku moja...............halafu wanatuita wananchi "mabwege".......na eti tunachagua viongozi wabovu..........muddo sik!
   
 13. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #13
  Apr 16, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Ogah.. I believe..hukumu itakayotolewa itawashtua CCM kuliko wanavyotarajia.. uchaguzi hauahilishwi; wagombea binafsi wataruhusiwa na mahakama itadai uwezo wake wa judicial review..
   
 14. Edson

  Edson JF-Expert Member

  #14
  Apr 16, 2010
  Joined: Mar 7, 2009
  Messages: 9,202
  Likes Received: 719
  Trophy Points: 280
  palamagamba aliniudhi sana
  sijui u prof wake alipateje, alijennga hoja dhaifu ile mbaya pale mahakamani
   
 15. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #15
  Apr 16, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Kwa kweli ndio sababu ya kuandika hii makala.. kwa sababu kama profesa anaweza kujenga hoja isiyo na kichwa wala mguu tena mbele ya Mahakama ya Rufaa basi tatizo letu limeongezeka kwa kiasi kikubwa zaidi ya tunavyofikiria..
   
 16. W

  WildCard JF-Expert Member

  #16
  Apr 16, 2010
  Joined: Apr 22, 2008
  Messages: 7,477
  Likes Received: 70
  Trophy Points: 145
  Mwanakijiji,
  Wale "marafiki" wa mahakama akina Prof Palamagamba Kabudi, Dr Jwan Mwaikusa na mwanasheria kutoka Zanzibar wameivuruga sana kesi hii. Wameweka mambo ya Muungano humo, wamelikuza sana Bunge,..... Serikali inashinda kesi hii.
   
 17. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #17
  Apr 16, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  serikali haiwezi kushinda; kama mahakama itafanya maamuzi kwa kutegemea marafiki wa mahakama serikali inaweza kushinda; lakini kwa vile ni hukumu ambayo inapitia hukumu za huko nyuma.. ni lazima wataangalia reasoning ya Kisanga na Manento na kuona kama ina makosa kisheria. Linapokuja suala la uwezo wa mahakama kuingilia kati haki ya mwananchi inapochezewa na serikali hakuna mahakama yoyote katika nchi ye kidemokrasia inayoweza kurule in favor ya serikali. As a matter of fact.. kama hujawahi kusikia maneno makali dhidi ya serikali basi yatakuwa kwenye hukumu hii..

  NInachoogopa ni kuwa serikali inaweza kufanya gross defiance ya mahakama kwa kwenda Bungeni kupitisha sheria kwa (kama walivyofanya awali) ambayo itafanya ni vigumu kwa mgombea binafsi kushiriki!! Yote itategemea mahakama kama itasimamia hukumu ya manento au itaammua kuwapa leeway ya aina fulani.
   
 18. Pascal Mayalla

  Pascal Mayalla JF-Expert Member

  #18
  Apr 16, 2010
  Joined: Sep 22, 2008
  Messages: 24,560
  Likes Received: 18,289
  Trophy Points: 280
  Mzee Mwanakijiji, ni suala moja tuu ndilo linalosubiriwa kutolewa uamuzi na sio mawili. Suala lenyewe ni la uwezo wa Mahakama Kuu kwenye masuala ya Katiba, yaani High Court Jurisdiction, ina nguvu zinazoitwa inherent powers kuhusiana na jambo lolote.

  Suala la Mgombea binafsi lilishaamuliwa na Mahakama Kuu, serikali haikukata rufani kupinga kulichoamuliwa na Mahakama Kuu, bali imekata rufani kupinga uwezo wa Mahakama Kuu kuamua ilichoamua.

  Hivyo uamuzi wa sasa, labda wataamua kutoa uamuzi wa kukazia hukumu ya Mahakama Kuu, tena Jaji Mkuu akiamua kuuma kama Lord Denning, anaweza akaisulubu serikali kwa Contempt of the court kwanini haikufanya chochote kutekeleza hukumu halisi, hata kama ilikata rufani, kwa vile rufani zote ni probability, baada ya hukumu, utekelezaji huanza unless kama serikali ingeomba 'Stay Order', kusitisha utekelezaji, kitu ambacho serikali haukufanya. Kukata rufani pekee siyo 'Stay Order'.
   
 19. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #19
  Apr 16, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Pasco.. suala hilo la pili linaathiri moja kwa moja suala hilo la kwanza.. kimsingi wagombea huru/binafsi watasimama na kuanguka kutokana na uamuzi wa suala hilo la pili. Sivyo?
   
 20. w

  wasp JF-Expert Member

  #20
  Apr 16, 2010
  Joined: Aug 19, 2009
  Messages: 206
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Asante sana Mwanakijiji kwa kutuelimisha. Mimi pia nilimshangaa sana yule Professor wa UDSM aliyeunga mkono hoja ya serikali. Lakini huyu naye anatafuta ulaji (he is an opportunist) kutoka kwa Mungwana ili apewe kitengo cha ulaji. Nasikia wajanja kwa kuona mizengwe yake walimjima hata kuwa Advocate.
   
Loading...