SEHEMU YA 11...
Chuoni wakajua, watu wengi wakashangaa, sarafina hakutakiwa kuwa na mtu kama David, mwanaume huyo alikuwa mtu wa wanawake, aliwafunua wanawake wengi chuoni hapo, aliwafanya alivyotaka, wanawake wengi walilia kwa ajili yake, wengi walitoa mimba kwa kuwa alikuwa akizikataa, kitendo cha Sarafina kuwa na mwanaume huyo ilionekana kuwa kama marudio ya maisha ya wasichana wengine kwamba naye angepatwa na balaa kama yaliyowapata wanawake wengine.
“Sarafina! Ninakupenda, ninakupenda sana,” alisema David huku akimwangalia msichana huyo machoni.
“Nakupenda pia!”
“Ungependa twende wapi?”
“Maisha Basement! Nimesikia kuna wasanii, Diamond na Ali Kiba watapanda jukwaani kwa pamoja kutambulisha ngoma yao mpya. Jamani! Nawapenda wale mpaka naumwa!” alisema Sarafina huku akimwangalia David.
“Hakuna shida!”
Maisha ya starehe yakamteka msichana huyo, alikwenda huku na kule akila raha, kwake, kila kitu kilionekana kuwa chepesi kwa kuwa tu alikutana na mwanaume aliyekuwa tayari kumpa kiasi kingi cha fedha kwa ajili ya kufanyia mambo yake.
Hakutaka kumfikiria Richard, kila alipokuwa akimuona chuoni hapo, alimuonea huruma, alionekana kuwa mwanaume mwenye maisha duni, mwanaume ambaye alitakiwa kupata zali la mentali kumpata mwanamke mwenye pesa ili ayaendeleze maisha yake, kwake, kwa jinsi alivyomwangalia Richard, alionekana kuwa naye mbalimbali kama mbingu na nchi.
Maisha yaliendelea, kila siku walikuwa watu wa kula raha. Sarafina alibadilika kwa asilimia mia moja, hakuwa yule Sarafina wa zamani, yule mshamba mshamba ambaye hata kufika Mlimani City aliogopa.
Alikuwa na bwana mwenye pesa kidogo ambaye aliyafanya maisha yake kuwa na mteremko. Hakuwa akiingia sana darasani kama kawaida, muda mwingi alikuwa akilala kwani kwa nyakati za usiku alikuwa akitoka sana na kwenda klabu.
Baada ya miezi miwili ya starehe Sarafina akaanza kuona mabadiliko, yale mapenzi aliyokuwa akiyaonyesha David yalionekana kupungua. Hakuwa mtu wa kumpigia simu kama ilivyokuwa zamani, hakuwa mtu wa kumtumia meseji kama kipindi kilichopita.
Je, nini kitaendelea?