Lowassa, Nape wawekwa kiporo
na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
KIKAO cha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC), kimeweka kiporo baadhi ya ajenda zake nyeti, ikiwamo ile inayogusia suala lenye utata la mradi wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wake wa Vijana (UVCCM), ambalo linatishia umoja na mshikamano miongoni mwa viongozi wa CCM.
Hoja ya mradi huo, iliyoibuliwa na mwanasiasa chipukizi ndani ya UVCCM, Nape Nnauye, anayewatuhumu Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la UVCCM, Edward Lowassa, Mwenyekiti wa umoja huo anayemaliza muda wake, Dk. Emmanuel Nchimbi na Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Francis Isaac, kwa kuiingiza jumuiya yao katika mradi usio na tija wala masilahi kwao.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya kikao hicho cha CC kilichokutana juzi zinaeleza kwamba, suala hilo sasa linatarajiwa kujadiliwa Jumanne ijayo na uamuzi kuhusu mradi huo mzima utafikiwa kabla ya mapendekezo ya Kamati Kuu kupelekwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho tawala (NEC), kwa maamuzi siku hiyo hiyo.
Suala hilo la ujenzi litajadiliwa kwa kupitia mapendekezo yaliyotolewa na timu ya wanasheria wa chama hicho ambao walipewa kazi ya kuvipitia upya vipengele vyote vilivyo katika mkataba huo ambavyo vimekuwa vikilalamikia na wana UVCCM kadhaa, akiwamo Nape.
Taarifa kutoka ndani ya CC hiyo zinaeleza kuwa, ajenda nyingine muhimu ambayo iliwekwa kiporo juzi ni ya kupitia majina ya wanaowania uongozi ndani ya jumuiya za chama hicho, ambapo sasa ajenda hiyo itajadaliwa Jumanne ijayo mjini Dodoma, kabla ya maamuzi kufikiwa ndani ya NEC.
Hata hivyo, kabla ya vikao vya CC na NEC, havijakabidhiwa majina ya wanaowania nafasi za uongozi, Baraza Kuu la UVCCM, linatarajia kupitia majina hayo katika kikao chao kitakachofanyika Jumapili wiki hii kutokana na kile ambacho kimeelezwa na baadhi ya wajumbe hao kuwa ni uamuzi wa kushinikizwa.
Uamuzi wa kufanyika kwa kikao hicho cha Baraza Kuu la UVCCM unakuja baada ya kuwapo kwa taarifa za awali zilizokuwa zikidai kwamba, kilikwama kufanyika mapema kwa madai kwamba umoja huo ulikuwa umekwama kifedha.
Mbali ya Nape, waombaji wengine katika uchaguzi huo wa UVCCM unaoendelea kuvuta hisia za watu kila kukicha ni Benno Malisa, Zainab Kawawa, Mohammed Bashe, Said Mtanda na Suleiman Muhsein, Jerry Slaa, Hamad Masauni, Issa Haji Ussi, Anthony Mtaka, Said Mtanda, Haule Pangisa, Samuel Marero, Stephen Deya, Geofrey Mwankenja, David Manoti, Mussa Mnyeti, Edson Lubua, Mwamini Lusingu, Asmah Kalokola, Marco Zablon Allute, Harold Adamson, Adila Hilal Vuai, Ashura Ismail, Rashid Masalaka na Raha Ahamada.
Wanaowania uteuzi wa nafasi ya makamu mwenyekiti ni Happy Mahava, Raha Ahamada Ally, Riziki Pembe Juma, Michael Bundala, Rabia Hamid Shaka, Nuru Mohammed Ahamed na Twaha Ally Muhaji.
Vyanzo vyetu vya habari kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu, kilichokuwa chini ya Uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, zilisema kuwa CC ilishindwa kumaliza ajenda zake kutokana na sababu mbili, mosi ni muda mwingi uliotumika kujadili suala la hadhi ya Zanzibar na kasoro za Muungano.
Vyanzo vyetu vya habari ndani ya kikao hicho, zilisema hoja hiyo ilitumia muda mwingi kutokana na mgawanyiko wa kimitazamo kutoka kwa wajumbe.
Sababu nyingine ya kutomalizika kwa ajenda 19 za kikao hicho, inaelezwa kwamba ilitokana na ugeni wa Rais wa Chama tawala cha ANC cha Afrika Kusini, Jacob Zuma, ambaye alikuwa na mazungumzo na Rais Kikwete.
"Kwa hiyo ajenda zingine hazijaguswa kabisa na kikao kimeahirishwa na sasa kitafanyika mjini Dodoma Septemba 9, kabla ya kikao cha Halmashauri Kuu (NEC), kinachotarajiwa kufanyika Septemba 9 hadi 10 mwaka huu," alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Kwa mujibu wa habari hizo zilizothibitishwa na wajumbe wengine tofauti, ajenda ya mradi wa jengo haikupata nafasi kabisa ya kujadiliwa licha ya shauku ya baadhi ya wajumbe kutaka ijadiliwe ili kubaini ukweli wa tuhuma dhidi ya Lowassa, Dk. Nchimbi pamoja na viongozi wengine ndani ya jumuiya hiyo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, alithibitisha kuwa kikao hicho hakikumaliza ajenda zake na kwamba kitaendelea tena mjini Dodoma.
"Siwezi kutoa maazimio ya CC jana, kwa sababu kikao bado kinaendelea, ila hatujajadili jina la Nape, kwa sababu kikao hicho ni kikubwa na cha kitaifa, hivyo hakiwezi kujadili jina la mtu," alisema Makamba bila kuingia kwa undani wa ajenda zilizojadiliwa.
Kwa hatua hiyo basi, suala la mkataba wa mradi huo ambao katika siku za hivi karibuni umezua maneno mengi ndani ya chama hicho tawala, litajadiliwa mjini Dodoma kabla ya suala hilo kupelekwa kwenye kikao hicho kupata baraka za NEC.
Nape ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mwanasaiasa wa siku nyingi, Moses Nnauye, kwa mara ya kwanza alitoa hoja ya utata wa mradi huo, saa chache tu baada ya kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo inayompa fursa mshindi kuwa mjumbe wa vikao vya kimaaamuzi vyenye nguvu kubwa ndani ya chama hicho tawala, Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Katika madai yake, Nape alimshutumu moja kwa moja Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa umoja huo, Edward Lowassa na viongozi wengine wa juu wa UVCCM kwa kuingia katika mkataba huo ambao alisema hauna masilahi yoyote ya maana kwa umoja huo.
Tangu Nape atoe tuhuma hizo, hali ya mambo ndani ya CCM na hususan katika UVCCM imekuwa ni ya vuta nikuvute, ikiwagawa viongozi waandamizi ndani ya chama hicho tawala katika makundi mawili.
Kundi la kwanza ni lile linalomuunga mkono Nape likijumuisha wakongwe kadhaa wa siasa za CCM (majina tunayo) ambao wanakiona kitendo cha mwanasiasa huyo kijana kuwa ni cha kijasiri na ambacho kinapaswa kuungwa mkono na kila mwanachama wa chama hicho.
Miongoni mwa watu wanaomuunga mkono Nape katika siku za hivi karibuni wanadaiwa kuwa wamekuwa wakifanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kwamba; ‘kijana wao' huyo anashinda uteuzi wa uenyekiti wa UVCCM kwa gharama zozote.
Kundi la pili katika msigano huo ni lile linalomuunga mkono Lowassa, likiwajumuisha wanasiasa kama Makamba, ambao wamekuwa wakimtaja Nape kuwa kijana anayejaribu kujenga hoja ili kujihalalishia ushindi kwa gharama zozote zile.
Habari kutokana ndani ya CCM zinaeleza kuwa, wanasiasa wanaounda kundi hili ambalo linamuungamo mkono Lowassa na Nchimbi wameshaanza kupanga mikakati ya kuhakikisha wanamuengua Nape katika mchuano huo, wakitumia hoja mbalimbali, zikiwamo zile wa umri wake kuzidi miaka inayotakiwa kwa mtu kugombea nafasi hiyo.
Wana CCM walio katika kundi hilo ambao baadhi yao wamepata kufanya mahojiano na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, wamekuwa wakimuelezea Nape kuwa mwanasiasa mzushi na mtu anayetumiwa na kundi la wazee kadhaa wa ndani ya chama hicho wenye lengo la kuhakikisha wanawaengua watu wote walio karibu kisiasa na Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye atakayekuwa mwenyekiti katika mchakato huu wa leo.
Katika hoja zake, Nape amenukuliwa akisema kwamba, mkataba huo ulipitishwa kinyemela hata kabla haujafikishwa kwenye vikao vya juu vya CCM kwa maana ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho ili kupata baraka za mwisho.
Vipengele vingine ambavyo Nape analalamikia ni kuhusu uhai wake kwani kinasema mwekezaji ataendesha mradi huo milele huku jumuiya hiyo ikipata asilimia 25 na mwekezaji asilimia 75.
Kasoro nyingine anazozitaja Nape katika tuhuma hizo ni pamoja na ile ya kukiukwa Sheria ya Ardhi (kiwanja), kuhamishwa kwa wabia kabla ya shughuli yoyote ya ujenzi kuanza.
Utaratibu ni kwamba, kabla hatua hiyo haijachukuliwa, sharti Kabidhi Wasihi Mkuu wa Serikali, atoe kibali kwa ajili ya uhamisho wa aina hiyo.
Mkataba wa mradi huo unaosomeka kwa kichwa kisemacho ‘Development Agreement', ulisainiwa Januari 2 mwaka 2007 kati ya UVCCM na makampuni mawili ya M.M. Integrated Steel Mills (MMISML) na Estim Construction Company Limited (ECCL).
Mkataba huo pia hauelezi kiasi cha uwekezaji kutoka kwa wabia ambacho kinaweza kutumika kuelezea mgawo wa asilimia 25 ambayo inadaiwa UVCCM, watachukua.
Aidha, mkataba huo hauna ufafanuzi wa matumizi na mapato hatua kwa hatua, jambo ambalo linaonyesha kutokuwa makini au kuashiria ghiliba katika mahusiano ya wabia.
Vilevile mkataba hauelezi iwapo ubia ni wa miliki ya pamoja au itaundwa kampuni tofauti ya kuendesha kitega uchumi.