SoC03 Saidia katika kutulinda Tembo wa Afrika

Stories of Change - 2023 Competition

Damaso

JF-Expert Member
Jul 18, 2018
1,590
2,089
Naitwa Bonte ni tembo ninayeishi kwenye hifadhi ya taifa ya Serengeti, Tanzania, ni miaka kumi sasa tangu mama na baba yangu walipoteza maisha mara baada ya kuingia kwenye mtego uliotegwa na majangili, Huu ni ujumbe wangu kwa binadamu;
IMG_1252.jpg


Naomba muendelee kutulinda sisi tembo wa Afrika, zamani za kale idadi ya tembo tulikuwa ni zaidi ya mamilioni katika sehemu mbalimbali za bara la Afrika pamoja na Asia, lakini katikati ya miaka ya 1980 idadi yetu ikaanza kuporomoka kwa kasi kutokana na ujangili bila kusahau uvamizi wa binadamu katika maskani yetu. Mpaka sasa tumebakia Tembo wachache sana katika nchi za Afrika, kwa sababu majangili hutuvamia na kutuua kwa ajili ya nyama yetu pamoja na kuchukua pembe zetu nzuri za ndovu.
IMG_1259.jpg


Tambua kuwa tupo aina mbili za Tembo wa Afrika, Tembo wa Savannah ambao hawa ni tembo wakubwa na ndio wanyama wakubwa duniani, wakiwa na urefu wa mita nne kutoka chini mpaka juu pamoja na uzito wa kilogramu zipatazo 7,500 mimi pia hapa ni Tembo wa Savannah.
IMG_1258.jpg
IMG_1264.jpg


Tembo wa namna hii tunajitambulisha kwa masikio yetu makubwa yaliyopinda kwa nje, na Tunapenda sana kuishi kwenye uwanda wenye nyasi haswa upande wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, nashukuru sana kwa jitihada za wananchi na serikali za nchi za Kusini mwa Afrika idadi yetu imeanza kuimarika.

IMG_1265.jpg
IMG_1255.jpg

picha kwa hisani ya Wikipedia.

Aina ya pili ya tembo wa Afrika ni Tembo wa Msituni kisayansi wamepewa jina la Loxodonta Cyclotis, hawa ni wapwa zangu wanaopatikana huko Afrika ya Magharibi, bibi alipenda sana kunisimulia mambo mengi sana kuhusu wapwa zangu. Wao ni tembo wa tofauti kidogo na sisi tembo wa Savannah, wao ni wadogo na wana rangi iliyokoza zaidi, huku masikio yao yakielekea chini na wanapatikana zaidi ukanda wa Magharibi na Afrika ya Kati haswa kwenye misitu mikubwa ya Afrika ya kati na Magharibi.
IMG_1257.jpg



Hawa wapwa zangu ndo tembo walio kwenye hatari zaidi ya kupotea kuliko sisi tembo wa savannah, kwa sababu kuu mbili. Mosi ni ujangili ulioshamiri pamoja na kupoteza makazi yao, takwimu zinasema kuwa ni nchi tatu tu za Magharibi mwa Afrika ndizo zenye Tembo hawa zaidi ya 300,000, huku nchi zingine zikiendelea kupambana kuendeleza jitihada za kuwalinda ndugu zangu kutokupotea. Ripoti kutoka Kenya zinasema kuwa kwa mwaka 2012 tu ndugu zangu zaidi ya 384 walipoteza maisha kutokana na ujangili, pia ndugu zangu wa Namibia wao waliopoteza maisha kwa mwaka 2016 walikuwa ni 101.
IMG_1266.jpg


Nilipata kusimuliwa na Mama kuwa soko la Pembe za ndovu lilianza kukua kwa kasi sana karne ya 20 na wanafamilia wengi walipoteza maisha kwenye mikono ya majangili, wakati huo ndipo babu na bibi yangu walipouawa kikatili. Baba aliniambia kuwa Pembe zetu ni bidhaa ya thamani sana na hutumika kwenye mapambo ya kifahari, na bidhaa nyingi zinazotumiwa na binadamu, matokeo ya biashara hii yalipelekea kuvunwa kwa zaidi ya tani 20 mpaka 1000 za pembe za ndugu zangu kati ya mwaka 1950 mpaka 1985.
IMG_1267.jpg


Miaka minne baadaye biashara ya kimataifa ya Pembe zetu ikazuiliwa, tangu hapo kukawa na mauzo ya Pembe hizo kwa uangalizi mkubwa haswa kutoka nchi za Afrika ya Kusini ambazo zilikuwa na ndugu zangu wengi wenye Pembe zilizokuwa na thamani kubwa kwenye soko, lakini bado soko liliendelea kuwafanya majangili waendelee kusaka ndugu zangu. Kulifanyika utafiti wa masoko 22 ya Pembe za ndovu kwa bara la Afrika pamoja na Asia, ikaonekana wanahitaji tembo zaidi 12,000 kila mwaka ilikuweza kulisha masoko hayo.


Migogoro kati ya binadamu na tembo pia imepelekea tembo tukose makazi ambayo binadamu wanayavamia, maeneo haya binadamu huyageuza na kuyafanya kuwa mashamba kwa ajili ya mazao pamoja na sehemu ya makazi yao. Babu zangu walioko Afrika Magharibi katika karne ya 20 walipungua kwa zaidi ya 95%, huku kwa upande wa Afrika ya kati, tembo wengi wanapoteza makazi Kutokana na tabia ya binadamu ya kukata misitu na kuchoma moto ili kuandaa mashamba.

Kwa wale tuliopata nafasi ya kulindwa hatufiki 20%, ambao tunaishi kwenye hifadhi na maeneo ya maalumu. Wengine hujenga majengo kama mahoteli kwenye misitu ambayo ndo nyumbani kwetu, na tunaporudi nyumbani huwa hatusahau njia tulizopita kamwe, kwa sababu Tembo tuna ubongo mkubwa na ubongo mzito kuliko mnyama yoyote na ndio unatuwezesha kuwa na kumbukumbu nzuri hata kwa miaka 100.

Shangazi yangu aliniambia kuwa wakati mwingine hukutana na miundombinu yha vyuo ikiwa imejengwa, na wao hupata hofu wakiona tunapata kufuata njia zetu za asili.
Wakulima wengine wakorofi sana, wanapanda mazao ambayo kwetu ni chakula kitamu sana, tena wakati mwingine pembezoni mwa hifadhi, unakuta mkulima amepanda maboga, matikitiki maji na mbogamboga. Kaka yangu mkubwa tu Nambe anakula zaidi ya kilo 300 kwa siku moja, hii ni sawa na 4% mpaka 7% za uzito wake, pia tunakula matunda, mizizi, mimea, pamoja na magome ya miti.



Baadhi ya watu wanaotulinda hutumia sindano za nusu kaputi kutuchoma endapo tukivamia mashamba ya binadamu, na endapo wataalamu wakiwa hawapo basi maafa makubwa hutokea, kwani wakulima wanaweza kutuvamia kwa silaha na kutudhuru na hata kutua, na kuna baadhi ya ndugu zangu hupata hasira kwa wepesi na wanalipiza kisasi kwa kuwajeruhi na hata kuwaua binadamu.

Uchitah Bonje, ni mtaalamu wa wanyama anayetuhudumia nilimsikia akisema kuwa serikali imeanzisha mradi na mpango mkakati wakishirikiana na binadamu katika kutulinda ila bado wanalifanyia kazi zaidi. Ndugu zangu waliopo Kenya kwenye makazi ya Amboseli, na Tsavo wanadai kuwa hawaingii tena mashambani kwa sababu wanakutana na kamba ambazo zinakuwa na pilipili na zinawasha sana. Tembo tuna uoni hafifu, hivyo tunatumia harufu na sauti kujiongoza kwenye maamuzi yetu, hii inawezekana kutokana na masikio yetu makubwa na yenye usikivu mkubwa.

Tuna uwezo wa kipekee wa kutembea mpaka kilomita 195 kwa siku moja, huku kwenye mbio tuna mwendokasi wa kilomita 40 kwa saa hivyo hata binadamu hawezi kunikimbia endapo nikiamua kumfukuza vyema. Mpwa wangu Totu, anayeishi huko kwenye hifadhi ya Taifa ya Mikumi ana uwezo wa kukimbia kwa mwendokasi wa kilomita 35 huku Mjomba Goka, kwa sababu ya uzee yeye hukimbia kwa mwendokasi wa kilomita 10 tu.
Nakuomba uendelee kunilinda mimi pamoja na wanyama wengine, nitafurahi sana kama nitakuwa nikikuona ukija kuniona kwenye hifadhi, nitafurahi sana endapo watoto wangu wakija kuishi huru pasipo hofu ya kufanyiwa ujangili, Asanteni sana.

Nilinde mimi Bonte pamoja na ndugu zangu wengine!
 

Attachments

  • IMG_1254.jpg
    IMG_1254.jpg
    22 KB · Views: 2
  • IMG_1259.jpg
    IMG_1259.jpg
    66.7 KB · Views: 2
Back
Top Bottom