ACT Wazalendo: Serikali iwafute machozi wananchi dhidi ya kadhia ya Tembo nchini

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,988
Chama cha ACT Wazalendo hakiliridhishwi na kasi ya Serikali katika kushughulikia matukio ya tembo kuvamia makazi, kuharibu mali (mazao) na kutishia usalama wa wananchi nchini. Tangu mwaka 2021 vilio vya wananchi wanaoishi pembezoni au maeneo yanayozunguka hifadhi au mbuga za wanyama kama vile Selous, Nyasaka, Mkomazi na Biharamulo vinazidi kuongezeka kufuatiwa na kuibuka kwa wimbi kubwa la uvamizi wa Tembo.

Tembo wamekuwa na athari kubwa kwa wananchi ikiwemo uharibifu wa mali zao (mashamba, mazao, mifugo na makazi), kujeruhiwa na vifo. Vilevile, kukatisha masomo kwa wanafunzi kwa hofu ya kudhuriwa au kuuawa. Pia, kufufuka kwa matukio ya ujangili unaotokana na visasi baina ya wanajamii na wanyamapori.

Idadi ya matukio na vijiji vinavyovamiwa na tembo inazidi kuongezeka kila uchao. Kwa utafiti tulioufanya kwenye baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi yanaonyesha kama ifuatayo;

Nachingwea peke yake kumetokea vifo 5 kati ya mwezi Machi-April 2023 katika vijiji 8 vya wilaya hiyo (Namapwia 3, Ngunichile 1, Namikango 1, Lionja A na B) na vijiji zaidi ya 5 mazao yao yameharibiwa sana. Hali ipo kama hivyo kwa maeneo ya Same, Kilwa, Katesh-Manyara, handeni na Liwale ambapo vifo, majeraha na uharibifu mkubwa wa mazao umefanyika na kuacha wananchi wa maeneo hayo katika hali mbaya.

Aidha, wananchi wanalalamikia viwango vidogo vya fidia (vifuta jasho na machozi) za uharibifu unaofanywa na tembo. Viwango vya sasa kwa mujibu wa kanuni ni shilingi 200,000 kwa aliyepata majeraha yasiyo ya kudumu na shilingi 500,000 kwa majeraha au kilema cha kudumu. Fidia ya shilingi 100,000 kwa ekari kwa wale ambao mazao yao yameharibiwa na wanyama pori na shilingi 1,000,000 kwa mwananchi aliyeuwawa na wanyama.

ACT Wazalendo tunatoa rai kwa Serikali kuongeza idadi ya askari kwenye vijiji vyote vinavyokabiliwa na changamoto za uvamizi wa Tembo nchini ili kusaidia kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza.

Pili, Serikali ifanye utafiti wa idadi ya tembo na tabia zao ili kama imeongezeka sana kuanza kuvunwa ili kupunguza uvamizi wa mara kwa mara.

Tatu, Serikali itenge na isimamie ipasavyo matumizi bora ya ardhi hususani kati ya shughuli za kilimo na ufugaji ili kudhibiti wafugaji kwenda maeneo ya makazi ya Wanyama pori.

Nne, Serikali ianzishe mfuko wa fidia ya wanyamapori ili kuwa na chanzo cha uhakika na uwezo wa kulipa kwa haraka na zitungwe kanuni za wazi za fidia zinazoendana na uharibifu unaofanywa na sio kifuta machozi kama ilivyo sasa.

Tano, Serikali iongeze jitihada katika kutoa elimu ya matumizi ya njia za asili za kukabiliana na tembo.

Imetolewa na;
Ndg. Anthony Ishika
X: @AnthonyishikaTZ
Naibu Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii
ACT Wazalendo.
25 Oktoba, 2023
 
Back
Top Bottom