Muda huu saa tisa kamili usiku 3:00 huwa kuna maelfu ya watanzania walio macho kwa kukosa usingizi kutokana na mambo mbalimbali. Nimeanza KUANDIKA
Napenda niwashukuru kwanza wale mliochangia comment zenu hapa. Wale mliowafahamu wazi wazi baadhi ya watu niliowataja hapa, kama vile marehemu mkongwe Jongo. Wale ambao najua kama nikiendelea kuweka wazi mambo watanifahamu kabisa, na jamaa wote mnaoshiriki pamoja nami hapa ahsanteni sana.
Sipendi niache baadhi ya issue zenye kunifanya niwe na huzuni wakati nikikumbuka yaliyopita huko. Jina X kama upo hapa unaweza kunifahamu, bado nakumbuka msisimko nilioupata baada ya miaka tisa ya panda shuka za ajabu na taarifa yako ya kifo cha binti mrembo sana moyoni mwangu. Sasa ni zaidi ya miaka 22 na bado ahadi yangu ya kuliona kabuli na kwenda kulia kwa sauti kubwa na machozi mengi sijaitimiza, lakini kwa hapa nilipo sasa naahidi sitalala kimya milele kabla ya kutimiza ahadi ya moyo wangu.
( NAKUWA NA WAKATI MGUMU SANA KUANDIKA, MUDA MWINGI MACHOZI NASHINDWA KUYAZUIA)
Basi baada ya siku ya nne ya kuusikilizia upepo, hao tukaondoka na gari ya mzigo, tuliyokuwa tunaisubili na ilitufanya tuongeze siku moja mbele mbadala wa siku tatu tulizopanga. Sisi hatukuacha alama kabisa ya wapi tulipotokomea, hii ilikuwa tofauti kabisa na vijana wengine ambao japo waliacha taarifa kwa rafiki zao na vijiweni huko. Kilichotufanya tuwe hivi nadhani ni hadaa za vipindi vya televisheni hasa zile movie za Lino lensi yule jamaa aliyekuwa pikpik kuubwa na minywele kibao, Isidingo pia ilichangia pakubwa kutupa moja na mbili katika maswala ya ujanja ujanja tofauti na vijana wengine ambao nadhani kwa wakati huo wazee kumiliki Panasoniki au Hitachi haikuwa jambo la mchezo.
Mdogo mdogo tumebanana kwenye kichwa cha gari, nakumbuka ustaarabu wa ndugu

utingo wa lile gari. Kipindi hicho kiukweli nilikuwa sijui kabisa na sijawahi kufika hata hapo kimara. Kwa watu walioishi ukanda wa bandali kule watanielewa. Hivi mtoto wa kurasini kimala unafuata nini hasa kipya wakati huo???
Labda kwa wale waliokuwa wanapita huko kwenda mikoani kwao na wazee wao nyakati za likizo.
Sasa hofu, furaha ya safari, mashaka na wasi wasi vyote vilikuwa vinapita pita tu hovyo ovyo kichwani. Safari ya usiku na magari ya mizigo sio mchezo, tena unapoenda haupajui. Tuliimaliza dsm bila kujua, safari sasa pwani hiyo gari mdogo mdogo, kwa maelezo ya utingo tukaingia mkoani morogolo na kidogo kuanzia hapo tukaanza kuenjoy mazingira mazuri ya njiani huko.. .. Huku baadhi ya vipande vya barabara vikipitika kwa shida shida yaani.
Wenzangu hawakupata bahati sana ya kushangaa nje maana walikaa ndani kidogo mafichoni nyuma ya kibin huko, safari ikaendelea taratibu sana kutokana na ubovu wa gari na vipande korofi vya barabara. Kufika mbele mbele huko mara gari inaanza kuchemsha, lile gali lilikuwa kimeo sana muda wote spana mkononi.
Kwa kipindi kile yale maeneo gari lilipo pata hitilafu sikuwa nayajua kabisa. Ila kwa sasa ni pale kwenye mitelemko ya iyovi kama nipo sahihi..huku kibariidi tukikisikia kwa mbali, utingo anatuambia tutafurahia shoo tukifika juu huko Iringa na Mbeya. Sasa hatukubeba nguo yoyote zaidi ya tulizo vaa ni kwa sababu kama mbili tatu hivi. Moja ni kutogundulika kila hisi nyumbani wakati tunatoka, pili tuliamini huko tunakoelekea kuna mavazi bora zaidi na tatu hatukuwa tayali kuona tunaibiwa chochote au kupoteza kitu, na kwa urahisi wa safari tulipendelea kuwa free bila mzigo wowote hadi tufikapo.
Hatukuwa na passport wala nyaraka yoyote ile. Hata dereva na utingo hawakuwa wakijua kama tunampango wa kwenda nje.
Asubuhi kabisa majira ya saa nne hivi safari ikaendelea baada ya chombo kupoa poa pale, tukapita ruaha mbuyuni kwa mara ya kwanza, aisee maeneo ni mazuri sana yanavutia sana, hapo baridi linaongezeka taratibu taratibu, safari hadi mlima kitonga chini kabisa gari ikabuma kimoja...
Aisee uzuri wa kuadithiwa nenda ukajionee. Japo barabara haikuwa bora sana kama hii leo lakini mazingira yalikuwa na mvuto zaidi ya hii leo.. Sisi kazi ilikuwa kufikicha mikono kwa kibaridi na kushangaa shangaa milima na vingedere watu maeneo yale... Muda kidogo ulivyoenda ndipo kwa msaada wa dereva tuliombewa lifti kwenye gari ya mastista lililokuwa linaishia sehemu moja hivi inaitwa mafinga.
Basi ndani ya gari ilikuwa tumsifu yesu kristu kibaooo.. Navile udogoni tuluwahi kutumikia kanisani ndo ikawa kama gari yetu na sisi ni wanafamilia pamoja nao. Kuna sehemu gari ilisimama tukapata chai pale kwa hisani ya ndugu zetu wa kiroho na safari ndefu ikaendelea. Tatizo ilikuwa wale masister walikuwa na maswali mengi mno, hadi unatamani gari ifike ushuke na wala haifiki. Rafiki yangu alipewa sweta baada ya kuzibuliwa miswali kibao na kuwa anaijibu papo kwa hapo.
Tulifika hapo mwisho wa lifti mafinga na baridi ilitulegeza kweli kweli, wale jamaa wanaishi ndani ya friji aisee, tulivutiwa sana na ka- harufu fulani hivi sijui kanatokana na nini hasa, maana DSM hatukuwai kabisa kukaskia, yaana harufu flani nzuri ya hali ya hewa.
Hatukua na mapepe na haraka sana hapo, pia hatukuitaji kupoteza pesa nyingi hapo. Basi kuna sehemu majamaa yamewasha moto karibu kabisa na stend tukajumuika nao kuota moto. Yaani walipotuona tu wakajua hawa jamaa wageni huku, maana mgeni hajifichi ugenini. Watu wa kule sio wabaya kabisa wana roho nzuri na wakalimu sana,
Baada ya muda kidogo tuliulizia ulizia namna ya kupata usafiri hapo wa kutufikisha jijini mbeya. Na kutokana na mionekano yetu ya kitown town kila mtu alikuwa anataka kuwa mwenyeji wetu..
Haikuwa rahisi kupata gari ya mizigo pale japokuwa zilikuwa nyingi zinapita hapo.
Basi kutokana na maelezo ya mwenyeji wetu ilibidi tulale hapo siku hiyo na tungeondoka kesho yake asubuhi na magari ya kiwanda cha karatasi yatakayopita mapema hapo kuelekea mikoa ya juu huko.
Kwa msaada wa mwenyeji wetu tukapata guest moja ya bei nafuu hapo na tukarundikana humo humo kwa hisani ya mwenyeji wetu.
Aisee lile baridi sio mchezo tulipitiwa na usingizi hadi saa tatu hivi au nne kabisa
Nje ukungu, maji hayashikiki, ukiyanawa usoni mikono inakufa ganzi, mafua si mafua yaana tabu tupu ni mwendo wa kutetemeka tu.
Tukaona hapa hapatufai kabisa na sio sehemu salama kwetu. Shida sasa tumeshachelewa kuvizia yale magari tuliyo elekezwa.
(Saa 5:34 nimefikia hapa, tunaendelea baadae kidogo baada ya kutoka kanisani)