Safari Kuelekea Ikwiriri Tamasha la Bi. Titi Mohamed

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,925
30,273
SAFARI KUELEKEA IKWIRIRI TAMASHA LA BI. TITI
Juma hili kuelekea Tamasha la Bi. Titi lilikuwa na shughuli nyingi kwangu.
Ingia toka ya waandishi na makamera yao ya TV yakishushwa kutoka kwenye magari ikawa jambo la kawaida nje ya nyumba yangu.

Napokea simu baada ya simu.

Haukupita muda nikapokea mwaliko kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuniomba nihudhurie tamasha la Bi. Titi Ikwiriri, Rufiji.

Safari imeanza mchana saa nane.
Jua kali sana lakini gari ina kiyoyozi.

Baada ya kuutoka mji na kupita Mbagala nahisi kuwa sasa ndiyo tunaanza safari hakuna tena magari ya kupishana barabarani.

Ndani ya gari mzee ni mimi peke yangu wote waliobakia watatu ni vijana wadogo sana.

Sasa wameniweka kati na maswali ya historia ya uhuru wa Tanganyika.

Hawa ni wahitimu wa vyuo vikuu wananieleza kuwa toka walipoanza kusoma na kunisikiliza katika mahojiano kuhusu Bi. Titi wamepigwa na na butwaa kwani historia ninayoieleza mimi wao hawakupata kufundishwa si sekondari wala vyuoni.

Hawa Sykes ni nani?

Mbona kila uliitaja TAA, TANU na Nyerere hawa nao utawataja?
Bi. Titi vipi tunaanza kumsikia sasa?

Hii ikawa fursa kwangu kutoa darsa la historia ya kuundwa kwa TANU 1954 na kikao nyumbani kwa Ally Sykes Mtaa wa Kipata kuhusu usajili wa chama.

Kikao hicho kilikuwa cha watu watatu, Abdul Sykes, Ally Sykes na Julius Nyerere.

Bi. Zainab mke wa Ally Sykes alikuwapo.kikao kile kama msikilizaji mama mwenye nyumba.

"Hii barabara tunayopita ya Kilwa Road ilikuwa inaishia Mtoni kwa Aziz Ally."
Naanza kuhadithia.

"Kutoka pale hapakuwa njia ya kuweza kupita gari ila baiskeli na wenda kwa miguu.

Aziz Ally ndiye aliyefungua njia kuweza gari kupita hadi Mbagala kwa kupitisha gari lake kwenye njia hiyo ya baiskeli na miguu kwani mke wake mmoja alimjengea nyumba Mbagala."

Kufika hapa nikawarejesha nyuma kwenye kikao cha Abdul na Ally Sykes na Julius Nyerere nyumbani kwa Ally Sykes Kipata.

Nyerere alifikisha taarifa kuwa msajili kakataa kuisajili TANU kwa kuwa chama hakikuwa na wanachama.

Kikao kile kiliamua Said Chamwenyewe asafiri kwenda Rufiji kuitafutia TANU wanachama.

"Mwaka wa 1954 hii Kilwa Road haikuwa hivi ina lami ni udongo mtupu wakati wa Masika barabara haipitiki.

Said Chamwenyewe alisafiri kwa baiskeli kutoka Dar-es-Salaam hadi Ikwiriri akisimama kila kijiji kuandikisha wanachama wa TANU.

Analala kijiiji kimoja asubuhi anaendelea na safari.

Kile kikao cha Kipata kilikuwa mwezi Julai na ilipofika Novemba ndipo TANU ikawa imekamilisha orodha yake ya wanachama wengi wakiwa wametoka Rufiji."

Vijana hawakunipa nafasi ya kusinzia njia nzima nasomesha historia ya TANU na kujibu maswali

Tumeingia Ikwiriri kiza kimetanda na moja kwa moja tukaenda ofisi ya Mh. Mohamed Mchengerwa Mbunge wa Rufiji na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Ofisi ilikuwa imezingirwa na watu wake kwa waume wamevaa sure za CCM.
Jambo lililotokea hapo lilinishangaza.

Huyu mtu mimi sikuwa namjua.

Akanisalimu kwa bashasha anawanadia watu, "Huyu ndiye Mohamed Said anaesomesha historia ya TANU...kadi namba moja Julius Kambarage Nyerere, kadi namba mbili Ally Sykes, kadi namba tatu Abdul Sykes...kadi ya Nyerere imeandikwa na Ally Sykes.

Watu wametuzunguka mimi na wenzangu na jamaa yangu anaendelea kubonga...

Sote tumeshangaa.
Pale nilipokuwa nimesimama nikamweleza Bi. Titi.

"Ilikuwa kama kesho TANU wana mkutano jioni Bi. Titi na wanawake wenzake watakutana nyumbani kwa Abdul Sykes kupanga ni wanawake wafanye kuhamasisha wenzao kuja mkutanoni na vipi wachangamshe hadhira.

Nisingetoka pale nilipozungukwa kama Mheshimiwa Mchengerwa asingekuja pale kutulaki.

Picha ya mwisho chini ofisi ya Mh, Mohamed Chengerwa ikiwa imezungukwa na wananchi waliofika katika Tamasha la Bi. Titi.

Picha ya kwanza juu khanga yenye picha ya Bi. Titi na picha ya pili ni i Bi. Halima Mzee mtoto wa pekee wa Bi. Titi.

Picha zinazofuatia ni Mwandishi na Mh. Mchengerwa Waziri wa Utamaduni,
Sanaa na Michezo.


320645738_714836729847444_727405088902227394_n.jpg
320620500_513090590796606_6755257824797412759_n.jpg
320668179_461551276166157_7756039967299530175_n.jpg
320698853_1383361832201522_1240700776049779900_n.jpg
 
Back
Top Bottom