Sababu ya wananchi kususia vikao serikali za mitaa

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Wakati vumbi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 likiwa bado halijatulia, baadhi ya wenyeviti wa mitaa na vijiji nchi nzima wanashindwa kuitisha mikutano ya kila robo mwaka kutokana na wananchi kudaiwa kuisusia.

Mbali na wananchi kususia mikutano hiyo katika baadhi ya mitaa na vijiji kwa madai hawakuwachagua viongozi hao, sehemu nyingine wanadai viongozi hao hawana uhalali wa kisiasa, kutokuwapo kwa bajeti za vikao na wengine wakihofia michango.

Katika uchaguzi huo wa mwaka 2019 ambao ulilalamikiwa na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani kuwa uligubikwa na madudu mengi, CCM ilishinda kwa karibu asilimia 99, huku ikizoa mitaa yote 4,262 nchini. Uchaguzi mwingine wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika 2024.

Katika uchaguzi huo wagombea wa CCM walipita bila kupingwa katika vijiji 12,028, vitongoji 62,927 na mitaa 4,207, baada ya wagombea kutoka vyama vya upinzani kuenguliwa kwa sababu mbalimbali.

Hata hivyo, pamoja na ushindi huo, uchunguzi wa gazeti hili katika mikoa mbalimbali nchini umebaini baadhi ya wenyeviti wa mitaa na vijiji, hawajaitisha mikutano ya kila baada ya miezi minne kama sheria na kanuni inavyowataka.

“Kuna makundi kama matatu. Wapo wenyeviti kweli wanaitisha mikutano kila robo mwaka kama kanuni zinavyotaka, lakini lipo kundi linaitisha wanakuja wachache sana na lipo kundi halijaweza kabisa kuitisha mikutano,” kilisema chanzo chetu kimoja.

Chanzo hicho kilieleza kuwa licha ya baadhi ya wenyeviti kutoitisha mikutano hiyo, baadhi wamekuwa wakighushi mihutasari ya vikao na kupeleka kwa watendaji na baadaye kwa wakurugenzi wa halmashauri.

“Lakini ukiwauliza wananchi wanadai kutofahamu mikutano hiyo na sababu ni makovu ya uchaguzi huo, wanaodai wananchi hawakuwachagua,’’ kilifafanua zaidi chanzo chetu.

Uchunguzi uliofanyika katika mikoa na miji ya Moshi, Arusha, Mbeya, Pwani, Bukoba, Katavi, Morogoro, Mwanza, Kigoma na Musoma, umethibitisha uwepo wa changamoto za uitishwaji wa mikutano hiyo kadiri sheria inavyotaka.

Kauli ya Serikali

Akizungumzia wenyeviti hao kutoitisha mikutano, Naibu Katibu Mkuu Tawala za Mitaa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ramadhani Kailima alisema mamlaka ya kuwawajibisha wasiofuata kanuni yapo mikononi mwa waliowachagua.

Kailima alisema utaratibu wa kufanya mikutano na kusoma mapato na matumizi upo kisheria, hivyo kila aliyechaguliwa anatakiwa kufanya hivyo.

“Wananchi wanatakiwa kutambua wajibu wao, kama mikutano haiitishwi siyo jukumu la Tamisemi, huku ni mbali sana, wanapaswa kuandika barua kwa mtendaji wa mtaa kuomba mikutano,” alisema Kailima.

Alieleza kuwa ikiwa mtendaji hawasaidii, wanapaswa kwenda kwa mtendaji wa kata, ofisa tarafa na mwisho kwa mkuu wa wilaya ambaye ni mtu wa mwisho kwao.

Hata hivyo, alisema kwa mwenyekiti wa kijiji, mtaa au kitongoji atakayewajibishwa na wananchi ikiwemo kuondolewa au kusimamishwa, pia rufaa yake inaishia kwa mkuu wa wilaya ambako atakwenda kueleza kama aliondolewa kimakosa.



Hali ilivyo Moshi, Arusha

Diwani wa Kiborloni, Manispaa ya Moshi (Chadema), Frank Kagoma, alidai katika baadhi ya mitaa mikutano inaitishwa kwa kusuasua na kwingine haiitishwi na kuna ambayo inaitishwa lakini wananchi wanaojitokeza hawazidi 20.

“Sio watu waliochaguliwa na wananchi ndio maana hata wakiitisha mikutano wananchi wanaipuuza na hilo sio hapa kwangu tu, ni tatizo la maeneo mengi. Wewe uliza wananchi kama kila robo mwaka kuna mikutano,” alisema Kagoma.

Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Moshi, Raymond Mboya ambaye amewahi kuwa Meya wa Manispaa ya Moshi (2015-2020), alisema haoni mikutano ya kikanuni ikiitishwa katika mtaa anaoishi wa Kibo.

“Sio hapa kwangu tu, ni karibu Manispaa nzima. Kuna visingizio vya baadhi ya wenyeviti eti wakiitisha mikutano wananchi hawaji au wanakuja wachache, lakini sheria iko wazi usipoitisha wananchi wanatakiwa kukung’oa,” alisema Mboya.

Hata hivyo, Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscus Tarimo alisema kwenye mtaa wa Mawenzi anakoishi na mtaa jirani wa Makongoro, ameshuhudia vikao vikifanyika akisema ili ufanye mkutano wa maendeleo wa kata (WDC), ni lazima vikao vya mtaa vianze.

Mwenyekiti wa zamani wa mtaa wa Relini katika Manispaa ya Moshi, Athman Mmbaga alisema mwanzoni mwaka 2020 aliwahi kuona mkutano mmoja uliofanyika karibu na Machibya, baada ya hapo hajawahi kusikia matangazo.

Katibu wa CCM mkoa Kilimanjaro, Jonathan Mabhia alipoulizwa alisema hajapokea malalamiko yoyote, lakini atafuatilia kufahamu kama tatizo hilo lipo na walirekebishe, kwani walishatoa maelekezo kwa wenyeviti kufanya mikutano hiyo.

Mkoani Arusha, baadhi ya viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji ambao walichaguliwa katika uchaguzi huo, wanadaiwa kutoitisha vikao na wengine kutoonekana katika ofisi zao.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili mkoani humo na kuthibitishwa na baadhi ya wananchi, watendaji wa kata na viongozi wa kisiasa walisema kukwama kwa mikutano hiyo, kumechangiwa na sababu nyingi, ikiwamo wengi kutokubalika katika maeneo yao, kutokuwa na fedha za kuitisha vikao na baadhi ya wananchi kususia.

Mjumbe wa serikali ya kijiji cha Engorika wilayani Arumeru, Laki James alisema katika kijiji chao chenye vitongoji vinne vya Rikoyani, Mbalaka, Muruve na Kainat, hakujawahi kufanyika mkutano kwa zaidi ya mwaka sasa.

Celina George, mkazi wa kijiji cha Engorika alisema hajawahi kuhudhuria kikao cha kitongoji kwani kiongozi ambaye alichaguliwa, amekuwa haonekani kwa muda mrefu na hawaelewi anakabiliwa na changamoto gani.

Ofisa mtendaji wa Kata ya Kilimatembo, wilayani Karatu, Birangu Silo alisema katika kata yake, kuna baadhi ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji wanafanya vikao na wengine hawafanyi, akisema hiyo ni changamoto tangu wachaguliwe.

Mwenyekiti wa kamati ya madiwani wa jiji la Arusha ya huduma za jamii, elimu, afya na uchumi, Isaya Doita alisema tayari wamebaini mikutano mingi ya mitaa haifanyiki katika kata mbalimbali katika jiji la Arusha kutokana na sababu kadhaa, ikiwepo viongozi waliochaguliwa kuogopa vikao na wananchi kutohudhuria.

Katibu wa Chadema mkoa Arusha, Reginald Masawe alisema zaidi ya asilimia 80 ya viongozi wa vitongoji na mitaa ambao walichaguliwa, hawaitishi vikao kwa sababu hawakuchaguliwa kihalali na wananchi.

Kwa upande wake, Katibu mwenezi Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa Arusha, Gerald Munisi alisema wanafuatilia taarifa za kutofanyika mikutano ya vijiji na vitongoji na ambao hawafanyi hatua za kinidhamu zitachukuliwa.

Kanda ya Ziwa

Katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, tatizo la vikao vya kikanuni kutoitishwa liliibuliwa na wakazi wa vijiji vya kata za Sigunga na Uvinza, waliodai kutosomewa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha wanazochanga kwa miradi.

Mkazi wa kijiji cha Uvinza kata ya Uvinza, Abdul Said alisema: “Binafsi huwa natoa michango kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, lakini hakuna vikao wala mikutano ya kusomewa taarifa ya mapato na matumizi.’’

Mariam Jabir, mkazi wa Kata ya Sigunga alisema kitendo cha viongozi wa mitaa kutoitisha vikao siyo tu kinaibua hisia ya matumizi mabaya ya fedha, bali pia kinawanyima wananchi fursa ya kuibua na kupanga miradi ya maendeleo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Ruchugi, Ramadhani Kayugilo alitaja mwingiliano kati ya mamlaka za mitaa na idara nyingine za Serikali kuwa miongoni mwa changamoto zinazokwamisha mikutano ya kila robo mwaka katika maeneo yao.

“Tunashindwa kuitisha vikao vya kuibua miradi, kusoma mapato na matumizi kutokana na taarifa nyingi kutokamilika kwa sababu ya mwingiliano kimamlaka na wakati mwingine masuala ya kisiasa,” alisema Kayugilo.

Diwani wa Uvinza, Aloka Mashaka alikiri uwepo wa changamoto ya vikao vya kikanuni vya kila robo mwaka kutofanyika katika vijiji vya Ruchugi na Uvinza kutokana na misuguano miongoni mwa viongozi kwa misingi ya itikadi za kisiasa.

Diwani wa Sigunga, Augustino Lugagala alisema awali kata hiyo ilikumbwa na changamoto ya vikao vya kikanuni kutofanyika kutokana na baadhi ya vijiji kutokuwa na watendaji, hali sasa ni shwari baada ya watendaji kupatikana.

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hanafi Msabaha alisema ofisi yake kwa kushirikiana na uongozi wa halmashauri ya wilaya imeitisha vikao viwili vya wenyeviti na watendaji wa vijiji na mitaa kuwaelekeza majukumu yao, ikiwemo kuitisha vikao.

Changamoto ya vikao kutofanyika pia imeripotiwa jijini Mwanza ambako Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyanza kata ya Mkolani, Barnaba Chonji alisema tangu aingie madarakani, ameitisha vikao viwili pekee vya kikanuni, hali inayofifisha fursa ya wananchi kuibua, kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Katika vikao viwili nilivyoitisha, wananchi walijitokeza; lakini tatizo linalotukabili ni kukosa fedha za kutekeleza miradi,” alisema.

Mkazi wa mtaa huo, Hellen Kennedy aliziomba mamlaka za juu za Serikali kufuatilia utendaji wa viongozi wa mitaa, ikiwemo suala la vikao vya kikanuni na utoaji wa taarifa ya mapato na matumizi.

“Tangu mwaka 2020, nimehudhuria kikao kimoja pekee cha mtaa wangu, licha ya sheria kuelekeza vikao vinne kwa mwaka; ni muhimu viongozi wa juu wa Serikali kuanzia halmashauri, wilaya na mkoa wafuatilie suala hili,” alisema Hellen.

Mikoa mingine

Mkazi wa kijiji cha Makorongo wilayani Chemba Mkoa wa Dodoma, Rashidi Ndwata alisema mikutano ya kusomewa mapato na matumizi, haifanyiki kwa sababu wenyeviti hawajiamini, akihisi hilo linatia mashaka juu ya matumizi.

Alisema tangu mwaka jana viongozi wa kijiji chao na watia saini wamekuwa na matumizi mabaya ya fedha, lakini wanapoitwa wanaogopa kujitokeza hadharani, jambo lililochangiwa na mazingira ya namna walivyochaguliwa.

Akijibu tuhuma hizo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hamisi Daniel alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo, kwani mambo mengi yanapikwa na watu wasiotaka maendeleo na kwamba siasa siyo lazima mikutano.

Mmoja wa wenyeviti katika Kata ya Berege wilayani Mpwapwa ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alisema wanafanya kazi katika kipindi kigumu, kwani maeneo mengi wananchi hawawaamini, na anatamani muda wa uchaguzi ufike.

“Ndugu yangu mimi natamani muda ufike tukabidhi au tugombee na wenzetu tuwashinde ili tupate uhuru, lakini kwa sasa tunaongoza kwa aibu kubwa, hatuna sauti na vijana ndiyo tabu,” alisema akiomba kutokutajwa jina lake.

Jijini Dodoma, Mkazi wa Mtaa wa Swaswa, Jumanne Ally alisema hajawahi kusikia kuhusu mikutano ya mitaa tangu uchaguzi ufanyike mwaka 2019.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Njedengwa, Daimu Haji alisema kwa kawaida wanapaswa kuitisha mikutano kila baada ya miezi mitatu, lakini kwa mtaa wake wamekuwa wakiitisha hata kabla ya kipindi hicho.

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema wamekuwa wakipokea taarifa za vikao vya mitaa kutoka kwa watendaji.

Huko Morogoro, Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Simu A kata ya Mjimpya, Saidi Mkwinda amesema kila baada ya miezi mitatu kuanzia mwaka 2019 wamekuwa wakiitisha mikutano ya wananchi kujadili mambo mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Ally Machela alisema katika halmashauri hiyo mikutano ya hadhara ambayo ipo kisheria imekuwa ikifanyika kwa kila robo ndani ya mwaka.

Lakini hali inaonekana kuwa tofauti kwa mkoa wa Mbeya ambapo inaelezwa mwitikio wa wanachi kuhudhuria mikutano hiyo ni mkubwa kama ilivyo kwa mkoa wa Pwani na kwamba mikutano hiyo imesaidia kuibua miradi ya maendeleo.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom