11th February 2010 (Ippmedia)
Balozi wa Rwanda nchini, Fatuma Ndagiza, akifurahia jambo na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika makao makuu ya IPP, jijini Dar es Salaam jana.
Balozi wa Rwanda nchini, Fatuma Ndangiza, amemwomba Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, kuhamasisha wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani kwenda kuwekeza nchini humo.
Aliyasema hayo jana ofisini kwa Mengi ambako walikutana na kuzungumzia mambo mbalimbali yanayohusu uhusiano wa Rwanda na Tanzania.
Balozi alisema Rwanda imejitahidi kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na imekuwa ikiwapokea kwa mikono miwili watu wanaokwenda kuwekeza nchini humo.
Wewe ulikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) hivyo unaushawishi mkubwa, tunaomba utusaidie kuwaeleza Watanzania na wawekezaji wengine duniani kuwa Rwanda kuna fursa nzuri za uwekezaji na mazingira yameboreshwa, tumeondoa kabisa ukiritimba na hatuvumlii hata kidogo vitendo vya rushwa, alisema.
Alisema serikali ya nchi hiyo imekuwa mwiba kwa wala rushwa kwani haina mchezo kabisa na watu wanaopata tuhuma za aina mbalimbali.
Alisema watumishi wa umma wanapoingia madarakani Sheria inawataka wataje mali zao na wanapotoka pia wanatakiwa kufanya hivyo na wasiofanya hivyo wanachukuliwa hatua hali.
Alisema kuonyesha kuwa serikali haina mzaha katika suala hilo, hivi karibuni iliwasimamisha kazi kwa miezi sita watumishi 130 ambao hawakutaja mali zao na watalazimika kulipa faini.
Balozi Ndangiza alimsifu Mengi kwa kuwekeza kwenye vyombo vya habari ambavyo alivielezea kuwa ni sauti ya wanyonge.
Watu wengi wanaogopa kuwekeza kwenye vyombo vya habari, wanapenda kuwekeza sehemu ambayo inafaida ya harakaharaka lakini wewe kwa kweli umesaidia sana jamii katika upatikanaji wa habari na sisi tunapata habari nyingi sana kutoka Tanzania kupitia kituo cha ITV na EATV na tunakuomba uje uwekeze kwetu Rwanda, alisema.
Kabla ya kuja Tanzania mwishoni mwa mwaka jana nilikutana na Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, wakaniambia ukienda Tanzania mtafute Mengi ni rafiki yetu na tunapenda aje kuwekeza Rwanda, ndiyo maana nikawa natafuta nafasi ya kukutana na wewe, alisema.
Kwa upande wake, Mengi alisema wakati nchi zinahamasisha uwekezaji kutoka nje, wawekezaji wa ndani nao lazima wawekewe mazingira mazuri na wapewe moyo.
Alisema imekuwa kawaida kwa nchi za Afrika kuwakaribisha kwa mikono miwili wawekezaji kutoka Ulaya na Marekani lakini wale wanaotoka kwenye nchi zao hawathaminiwi ipasavyo.
Wawekezaji wazalendo ni muhimu sana na ndiyo nguzo kuu ya uchumi maana ukitokea mtikisiko wa uchumi wawekezaji wa nje wanaondoka zao lakini wazalendo wanabaki, hapa Tanzania mwaka jana kulikuwa na wawekezaji wengi waliokuwa wakitafiti madini lakini ulipootokea mtikisiko wakaondoka, alisema.
Mengi alisema Rwanda ni mfano wa kuigwa kwa kukaribisha wawekezaji vizuri na imepiga hatua kubwa kiuchumi katika kipindi kifupi.
Niliwahi kwenda Rwanda kutafuta fursa za uwekezaji, kweli mlinikaribisha vuzuri sana, mimi na kwa niaba ya wafanyabiashara wenzangu nawapongeza sana kwa hatua kubwa mliyofikia maana mmefanya maajabu makubwa, alisema.