Ruaha mto uliolipiza kisasi cha kifo cha Mtwa Mkwawa 1898

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,263
RUAHA MTO ULIOLIPIZA KISASI CHA KIFO CHA MTWA MKWAWA 1898

Katika askari mamluki walitoka Mozambique kuja German Ostafrika kuja kupigana katika jeshi la Wajerumani dhidi ya Mtwa Mkwawa na Abushiri bin Salim majina yao yanafahamika.

Majina haya yamefahamika kwa sababu mtoto wa mmoja wa hawa askari ndani ya jeshi la Wajerumani alinyanyua kalamu akaandika maisha yake.

Katika kuandika maisha yake akaeleza historia ya watu muhimu sana katika historia ya Tanganyika kama Hermann von Wissman, Chief Mohosh wa Inhambane, Mozambique, kijiji cha Kwa Likunyi ambae Tanganyika alikuja kujulikana kama Affande Plantan.

Hawa ni wageni walioingia Tanganyika wakiwa wamebeba bunduki.

Katika kuhadithia historia hii amehadithia historia ya Abushiri na vita vyake dhidi ya Wajerumani na vita vya Wahehe chini ya kiongozi wao Mkwawa dhidi ya hao hao Wajerumani.

Aliyeandika historia hii kama nilivyodokeza ni mtoto wa mmoja wa hawa askari ndani ya jeshi la Wajeruamani.

Jina la huyu mtoto ni Kleist Sykes aliyezaliwa mwaka wa 1894.

Wakati vita hivi vinapiganwa Kleist alikuwa mtoto mchanga wa mikononi akiishi Pangani na mama yake mwanamke wa Kinyaturu jina lake Kwema.

Wakati Mkwawa anajiua mwaka wa 1898 baada ya kuona kuwa Wahehe wameshindwa vita vile Kleist alikuwa na miaka minne.

Katika historia hii aliyoandika Kleist Sykes haya niliyoeleza hapo juu ndiyo historia aliyoanza kuandika mwanzo wa mswada wake akimtaja baba yake na sababu zilizofanya aondoke kwao kijiji cha Kwa Likunyi Inhambane kuja Tanganyika mwaka wa 1874.

Jumla ya hawa Wazulu mamluki waliokuja Tanganyika na Wissman ni 400 na Wanubi walikuwa 600.

Katika hawa Wazulu 400 ambao Kleist kawataja ni Affande Plantan na Chakullan.

Affande Plantan kamtaja kwa kuwa ndiye aiyemlea baada ya kifo cha baba yake.

Sykes Mbuwane baba yake Kleist alipotoka Pangani kwenda vitani kupambana na Abushiri Bagamoyo, Pangani na Kalenga hakurejea.

Mzulu mwingine ambae Kleist kamtaja ni Chakullan ambae alimuoa mama yake Bi. Kwema baada ya kya kifo cha mumewe Kleist Mbwane.

Mzulu mwingine ambae anafahamika kama mmoja katika wale askari 400 wa Kizulu ni Machakaomo.

Machakaomo mimi nilikuja kumjua kwa kumsikia kwa kuwa alikuwa anaishi Mtaa wa Kipata na mwanae Hassan Machakaomo alikuwa mtu maarufu na kiongozi wa Yanga katika miaka ya 1940 hadi 1950.

Mkasa huu wa kifo kifo kilichotokea Ruaha nimekieleza katika kitabu cha Abdul Sykes:

''Historia ya ukoo wa akina Sykes inarudi nyuma kiasa cha zaidi ya miaka 100 hivi.
Katika miaka hiyo yote ukoo huu umeweza kuhifadhi historia yake kupitia kwa Kleist Sykes mwenyewe ambae yeye alijifunza historia ya kabila lao kutoka kwa mlezi wake, Affande Plantan.

Kleist akawa ndiyo mtu wa kwanza katika ukoo huo kuandika asili yao na yote aliyoyatenda katika uwanja wa siasa.

Affande Plantan alimlea Kleist katika nyumba yake baada ya kifo cha baba yake Sykes Mbuwane kutokea huko Ruaha wakati wakirudi vitani baada ya kumshinda Chifu Mkwawa.

Sykes Mbuwane aliona ng’ombe wakivuka Mto Ruaha na akadhani maji hayakuwa na kina kirefu.

Ng'ombe walikuwa wamewateka vitani kama ngawira.

Akihisi kuwa angeliweza kuvuka kama ng'ome wamevuka, Kleist na wenzake wakajaribu kuvuka na wote wakasombwa na maji na kuzama.''

Wenyeji wanaoishi kando kando ya mto Ruaha wamenifahamisha kuwa Mto Ruaha hauendi kwa kasi ila wakati wa mvua za masika.

Ikiwa hivi ndivyo inaelekea vita na Mkwawa ilimalizikia majira ya masika wakati Mto Ruaha unateremesha maji kwa wingi na maji haya ya masika ndiyo yaliyowazamisha Wazulu wale pamoja na Sykes Mbuwane.

Ikiwa ni kisasi basi Mkwawa alilipiwa kisasi chake dhidi ya Wazulu hapo Ruaha.
Leo nimeupiga picha Mto Ruaha na ni huo hapo juu na picha hii nimeupiga Ruaha upande wa Iringa.

Kwa kuhitimisha napenda kusema kuwa kwa hakika lau kama tuna deni kubwa kwa Kleist Sykes kwa historia hii lakini Chief Mohosh au Affande Plantan yeye ndiye aliyemfunza Kleist historia hii.

Tuna deni kubwa zaidi kwake.

Picha: Mto Ruaha, Chief Adam Sapi Mkwawa mjukuu wa Chief Mkwawa na fuvu la babu yake, Mwandishi na Chief Adam Abdul Mkwawa kitukuu cha Chief Mkwawa.

Lakini huu si mwisho wa historia ya Mkwawa kugusana na historia ya Sykes.

Wajukuu wa hawa watu wawili Abdul Sykes na Chief Adam Sapi Mkwawa watakujakutana nusu karne baadae si kama maadui bali kama ndugu wazalendo wakipambana na ukoloni wa Mwingereza.

Ikitokea fursa In Shaa Allah nitaeleza hawa vijana wawili walifanya nini Kalenga ndani ya ngome ya Chief Mkwawa babu yake Chief Adam Sapi na chini ya pua ya Gavana Edward Francis Twining.



1656188426528.png
 
Mto ruaha ni silent killer unaweza zani maji hayatembei na hayapigi kelele kamwe ukiweka mguu tu umeisha
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom