Robert Heriel Mtibeli
JF-Expert Member
- Mar 24, 2018
- 21,340
- 51,891
RIWAYA: WAKALA WA SIRI
Mtunzi; Robert Heriel
0693322300
Episode 01
MAABARA YA BORETI.
Jokofu maalumu kwa ajili ya kuchunguzia maiti lilikuwa limezungukwa na Madaktari bingwa wa maswala ya uchunguzi, ndani yake ilikuwepo maiti iliyofungwa kwa karatasi jeupe la nailoni. Ilikuwa ni maabara ya kuchunguza maiti za watu ambao walikufa vifo tata au kuuawa. Kitaalamu maiti za namna hii huitwa 'cadaver' (tamka Kadava). Cadaver ni mwili wa binadamu aliyekufa ambao hutumiwa na Madaktari wa uchunguzi kubaini sababu ya kifo cha mhusika. Pia Cadaver hutumiwa na Wanafunzi wa utabibu, wanafizikia wanaojifunza Anatomia kubaini magonjwa, kutoa tishu au viungo kwa wanadamu waliokuwa hai. Walikuwa Madaktari saba waliokuwa katika maabara wakifanya uchunguzi wa maiti iliyokuwa mbele yao juu ya meza, huku wao wakiwa wameizunguka. Daktari mmoja alikuwa yupo mbele ya Madaktari wengine. Huyu ndiye alikuwa Daktari Mkuu wa uchunguzi huo. Walivalia makoti meupe ya kidaktari yaliyofika mpaka magotini. Pua zao waliziziba na barakoa ya puani ya kufanyia upasuaji (surgical mask) nyeupe huku kichwani wakiwa wamevaa kofia maalumu za kufanyia upasuaji (surgical cap). Mikononi walikuwa wamevaa Gloves nyeupe kwa ajili ya kujikinga na hatari yoyote ya maambukizi endapo ingetokea.
Pembeni ya lile Jokofu lenye maiti kulikuwa na meza ndogo yenye ukubwa wa mita mbili, ambapo juu yake kulikuwa na sinia kubwa lenye mikasi, visu na vifaa vingine maalumu vya upasuaji. Juu ya dari kulikuwa na Taa ndefu iliyokuwa inamulika na kukifanya chumba kile kiwe na nuru ya kutosha kabisa. Daktari Mkuu aliisogelea ile maiti kisha akalifungua lile karatasi la Nailoni jeupe lililokuwa limezungushwa kwenye ile maiti. Sasa Maiti ilikuwa uchi kabisa bila ya nguo wala ile nailoni. Wale Madaktari sita wengine walisogea zaidi karibu na Daktari mkuu wote wakiutazama ule mwili. Daktari Mkuu alipeleka mkono wake kwenye macho ya ile maiti akalifungua jicho moja la ile maiti. Akatazama kwa muda kisha akalifunga. Akapeleka macho yake mpaka iliposhingo ya ile maiti, kisha akaigusa kama mtu anayepima jambo. Kisha akatoa. Madaktari wengine walikuwa wakimtazama Daktari mkuu jinsi anavyofanya. Daktari Mkuu akasogea mpaka lilipotumbo la ile maiti. Kisha akalishika na kulibinya kidogo huku akitazama mdomoni mwa ile maiti. Akabinya mara tatu kwenye tumbo la ile maiti. Akaacha. Akaagiza kifaa maalumu, kitambo kidogo akaletewa kifaa kilichofanana na mpira akakishika mkononi. Kisha akafungua mdomo wa ile maiti akatazama kwa makini. Kisha akaufunga.
"Embu binya tumbo la hii maiti mara tatu" Daktari Mkuu aliongea huku akichomeka kile kifaa kama mpira Mdomoni mwa ile maiti huku akiziba pua ya ile maiti. Kisha Daktari mwingine alisogea na kubinya tumbo la ile maiti mara tatu. Kitendo hicho kilifanya hewa ijae kwenye kile kifaa cha mpira kilichobandikwa mdomoni mwa ile maiti. Kisha Daktari Mkuu akasogea mahali zilipo sehemu nyeti za ile maiti. Ilikuwa maiti ya mwanaume. Hapo akaushika uume wa ile maiti akaubinya ukatoa maji maji. Kwa upesi akapewa na Daktari mwenzake kioo maalumu akakinga yale maji maji yaliyotoka kwenye uume wa ile maiti. Kisha walimalizia kwa kuufanyia mwili Scanning(tamka Skani). Alafu wakachukua dawa fulani wakapaka ile maiti na kuifunga na lile lile karatasi la Nailon jeupe la awali.
"Nadhani kazi itakuwa imekamilika. Sasa twendeni tukachukue vipimo kwenye hizi sampo tuone tatizo lilikuwa ni nini" Daktari mkuu wa uchunguzi aliongea miwani yake ikiwa imeshikiliwa na pua yake pana kama pua ya ng’ombe
"Sasa nyie mnaweza kurudi nyumbani hii kazi nitaimaliza mwenyewe. Kesho asubuhi tukutane Room 66 kwa ajili ya kuwapa mrejesho" Daktari Mkuu aliongea akiwatazama Daktari wenzake ambao nao walikuwa wakimtazama. Walitingisha vichwa vyao kuashiria kukubaliana na kauli yake, kisha wote wakatoka mule kwenye ile maabara na kuondoka kwenda makwao wakimuacha Daktari Mkuu hospitalini.
Ilikuwa yapata mida ya saa saba za usiku wakati Daktari mkuu akiwa yupo ofisini kwake ambapo ni Room 33, akifanya uchunguzi kwenye zile sampo alizozipata kutoka katika ile maiti kule maabara. Alichukua Darubini(Microscope) kifaa maalumu cha kimaabara kinachotumika kuangalia viumbe wenye maumbile madogo yasiyoonekana kwa macho. Alichukua yale maji maji aliyoyatoa kwenye uume wa ile maiti ambayo aliyalebo kama Sampo B. Kisha akaanza kufanya uchunguzi. Daktari alishtuka kile alichokiona kwenye Darubini. Alitoa macho kama mtu aliyeshangazwa na kile alichokuwa amekiona. Alipeleka macho yake tena kwenye darubini kuangalia sampo B. Aliacha tena. Kisha akachukua kalamu na kuanza kuandika kwenye kitabu kuhusiana na kile alichokiona katika hatua ya awali ya uchunguzi wake. Akiwa anaandika punde akasikia kitasa cha mlango wa ofisi yake kikicheza. Hapo akaacha kuandika akatazama Mlangoni, akaona bado kitasa kinacheza.
" Devis...! Devis.." Aliita jina la Mlinzi wa zamu wa siku hiyo ambaye alikuwa anaitwa Devis. Kwa muda ule alijua fika kuwa eneo hilo wapo wawili, yeye na Mlinzi, Devis.
Hata hivyo hakuna aliyemuitikia ingawaje kitasa bado kilikuwa kinacheza. Alinyanyuka kuelekea mlangoni, alipofika mlangoni alikumbuka bastola yake aliyokuwa ameiacha kwenye droo ya meza. Akarudi kuichukua. Tayari alikuwa na mashaka. Hali ilie haikuwa ya kawaida kwake kwani tokea aanze kazi Hospitalini humo haikuwahi kutokea jambo kama hilo. Alipokishika kitasa kikaacha kucheza. Akafungua na funguo mlango ukafunguka. Hamadi! Alishtuka akaanguka chini. Loooh! Alikuwa ni Popo Mkubwa aliyempiga usoni baada ya yeye kufungua mlango. Hapakuwa na mtu mwingine kwenye ile korido zaidi ya yule popo aliyempiga usoni, Yule popo alianza kuranda randa kwenye ile korido ambayo ilikuwa ndefu yenye milango mingi na mwanga wa taa. Daktari Mkuu alitembea kwa hatua fupi fupi huku akiangalia nyuma na mbele kwenye ile korido kuona kama ataona mtu lakini hapakuwa na mtu, na korido yote ilikuwa kimya mno. Kwenye ile korido kwa juu kulikuwa na taa moja ambayo kulikuwa na wadudu wadogo wadogo na vipepeo waliokuwa wanaruka kufuata mwanga . Daktari alitembea huku akijaribu kuita Devis mkononi akiwa kaishika vyema Bastola yake.
"Shiiti! ni mawenge ya usingizi? Mbona hakuna mtu wala dalili ya kuwa na mtu korido hii?"
Daktari Mkuu alipuuzia, aliona huenda ni usingizi ndio ulikuwa unamchanganya, Akaamua kurudi ofisini kwake, Room 33.
Alipokuwa akirudi mara alishtuka baada ya macho yake kuona jambo geni chini kwenye sakafu. Aliona karatasi ya rangi nyeupe ikiwa pale chini. Alishangaa ni kivipi alipita pale pale na hakuiona. Hata hivyo alijipa sababu kuwa huenda ni kutokana muda ule alikuwa na hofu, ukizingatia pia katarasi ile ilikuwa nyeupe. Aliiokota na kuigeuza upande wa nyuma ambapo alishangaa kuona picha ya ile maiti kwenye ile karatasi. Chini yake kukiwa na maandishi ya kitaalamu yenye alama nyingi za kikompyuta. Wasiwasi ulimuingia, nani aliyekuwa kaiangusha ile karatasi. Kwa nini ipo pale. Daktari alishika tena Bastola yake vizuri akageuka huku na huku lakini bado korido ilikuwa tupu ikimtazama.
Aliichukua ile karatasi akaenda nayo moja kwa moja ofisini kwake. Alipofika ofisini kwake alishangaa kukuta mabadiliko ya kuogopesha. Alishangaa kuona Darubini ikiwa imehamishwa kutoka pale alipokuwa ameiacha akaikuta ipo juu ya kabati wakati yeye alikuwa ameiacha juu ya meza. Akiwa anajiuliza maswali yaliyomfanya mwili wake kusisimkwa na kuhisi kuna hali isiyo ya kawaida inayoendelea, punde alihisi kitu kikigusa kichwa chake kwa nyuma huku sauti nzito isiyo na mzaha ikisema;
" Ukijaribu kuleta ujanja wowote nitapasua kichwa chako. Tulia hivyo hivyo tafadhali"
Hapo Daktari akaona tayari yupo chini ya mikono hatari. Maisha yake yapo hatarini.
************
Siku iliyofuata wa kwanza kufika katika hospitali ya Boreti alikuwa ni Dokta Festo. Ilikuwa ni kawaida kwa Dokta Festo kuwahi asubuhi na mapema. Hata Wafanyakazi wengine wa hospitali hiyo walimzoea kwa tabia yake ya kuwahi asubuhi . Dokta Festo aliingiza gari lake baada ya kufunguliwa na Devis ambaye ndiye aliyekuwa Mlinzi wa zamu.
" Mambo Vipi Devis" Dokta Festo alimsalimia Devis huku akifunga mlango wa Gari lake.
"Salama Kabisa. Naona kama kawaida yako"
" Hahaha! Acha maneno yako Devis. Kazi ni nyingi, usipowahi huwezi zimaliza"
" Kweli kabisa. Kama Watanzania wengine wangekuwa kama wewe, nchi hii ingefika mbali sana"
Wote wakacheka kisha Dokta Festo akaondoka kwenda ofisini kwake akimuacha Devis akifunga geti.
Ofisi ya Dokta Festo ipo Room 22 ambapo yeye ni Daktari wa Mfumo wa Neva.
Moja kwa moja aliingia kwenye jengo la hospitali ambapo alichukua uelekeo wa upande wa kushoto, Kulikuwa na korido ndefu yenye milango mingi. Kisha alifika sehemu yenye ngazi inayopandisha ghorofani akapanda, akatokea juu ilipo ghorofa ya kwanza. Akatembea kidogo kisha akasimama mbele ya mlango uliaondikwa Room 22, chini yake yalikuwepo maandishi yaliyosomeka NEUROLOGIST.
Alitoa funguo mfukoni kisha akaufungua ule mlango akaingia ndani. Alipoketi aliwasha Kompyuta iliyokuwa mezani. Kisha akawa anaandika jambo fulani. Ghafla aliacha kuandika baaada ya kukumbuka jambo. Alitoka upesi upesi moja kwa moja mpaka aliposimama mbele ya mlango ulioandikwa Room 33, chini yake yalikuwepo maandishi yalisomeka SURGEON GENERAL (ambaye ni Daktari Mkuu wa Upasuaji).
Dokta Festo alibisha hodi mara tatu lakini kulikuwa kimya. Alikishika kitasa cha mlango akakitekenya, Mlango ukafunguka. Akaingia ndani. Alishtuka kuuona mwili wa Daktari Mkuu ukiwa umelala chini kama Maiti.
" Dokta Beatus! Dokta...! Doktaa! Amka..! Nini kimetokea?" Dokta Festo aliita huku akimtingisha Dokta Beatus ambaye ni Daktari Mkuu wa hospitali hiyo, aliyekuwa amelala pale chini kama maiti.
" Devis..! Devis... Ooh! Shiiit! Nini hiki tena" Dokta Festo alimuita mlinzi lakini sauti yake haikutosha kumfanya Mlinzi asikie. Alitoa simu akabinya binya huku akiwa kachuchumaa pale chini alipokuwa amelala Dokta Beatus.
"Ndio Devis,. Njoo haraka huku juu. Dokta Beatus kapatwa na tatizo. Fanya haraka" Dokta Festo alikata simu baada ya kuwasiliana na Mlinzi, Devis. Dakika mbili hazikuisha Mlango ulifunguliwa na Devis aliingia.
" Kuna shida gani Festo?"
" Mwenyewe ndio nashangaa. Nimefika nimemkuta Dokta Beatus kalala hapa chini"
" Hee! Shida itakuwa nini? Vipi umeangalia kama ni mzima?"
Devis aliongea akiwa tayari amesogea alipochuchumaa Dokta Festo.
" Mapigo yapo chini sana" Dokta Festo alisema.
" Huenda alipatwa na shinikizo la damu" Devis aliongea akimtazama Dokta Festo aliyekuwa akimkagua Dokta Beatus aliyekuwa amelala pale chini.
" Tumbebe tukamlaze kwenye wodi ya Staff"
Dokta Festo aliongea na mara moja zoezi la kumbeba Dokta Beatus likaanza. Walimbeba mpaka ilipo Wodi maalumu ya Staff ambapo wafanyakazi wa Hospitali hiyo wakipatwa na matatizo hulazwa hapo.
"Habari za asubuhi Dokta Binamungu. Upo wapi? ahaa! Sawa. Fanya hima. Dokta Beatus amepoteza fahamu. Wee njoo tutaongea huku yote"
Dokta Festo alikata simu, alimtazama Dokta Beatus aliyekuwa amefumba macho pale kitandani walipomlaza. Devis alitoka upesi upesi baada ya kusikia honi ya gari kwa nje. Walijua aliyefika ni Dokta Binamungu ambaye ni Daktari mwenye cheo cha pili baada ya Dokta Beatus. Kitambo kidogo Dokta Binamungu alifika kwenye wodi ya Staff ambapo Dokta Festo alikuwepo akiwa anauchunguza mwili wa Dokta Beatus.
"Habari Festo. Poleni sana. Kwani imekuwaje?" Dokta Binamungu alisema.
" Tumeshapoa. Hata sielewi Binamungu. Kama unavyoona. Dokta Beatus tumemkuta amepoteza fahamu ofisini kwake"
" Jana si tuliagana na alikuwa mzima wa Afya kabisa au alikuambia anaumwa?"
" Hakuniambia kama anaumwa. Lakini mbona alikuwa sawa tuu" Dokta Festo alisema huku akimfungua jicho moja Dokta Beatus.
" Aisee! Kwa hiyo bado hujabaini tatizo ni nini?"
" Ndio nilikuwa namfanyia uchunguzi hapa. Ila nimegundua kuna kitu hakipo sawa"
" Kitu gani hiko? Lakini si atakuwa salama?"
Dokta Binamungu aliongea kwa hofu.
" Sumu..!"
" Imefanyaje? Dokta Festo mbona unanitisha"
" Sumu ndio imemfanya apoteze fahamu"
" Umewezaje kujua hilo?"
Dokta Binamungu aliongea akimtazama kwa makini Dokta Festo.
" Embu fungu macho yake utagundua hilo"
Dokta Festo alisema, Binamungu akafungua jicho moja la Dokta Beatus.
" Beatus anawezaje kujipulizia Sumu"
Binamungu aliongea akifunga jicho la Dokta Beatus.
"Lazima kuna kilichojificha. Hapa kuna jambo halipo sawa. Alafu hata ile maiti tunayoichunguza si unajua mazingira yake yalivyotata"
Dokta Festo aliongea akitazamana na Binamungu.
" Kwa hiyo unataka kusema kuna msaliti kati yetu? Mimi sidhani"
" Hudhani! Hatupo hapa kudhani. Hii kazi ni kubwa na ngumu. Usaliti kutokea ni kawaida"
Dokta Festo aliongea kwa ukali kidogo.
" Hivi umesahau mimi ni nani kwako? Umesahau nakuuliza? Unamfokea nani sasa? Festo unataka kunipanda kichwani?"
" Samahani Mkuu. Nimeghafilika. Haya mambo yanachanganya"
" Chunga adabu yako. Mimi ndio nimekuleta hapa. Sawa..?"
" Sawa Mkuu"
Kimya kidogo kilitokea wakati wawili hao wakigombana huku Dokta Beatus akiwa kalazwa akiwa hajitambui kitandani.
" Jana niliacha Wallet yangu kule Maabara. Embu kaniletee" Dokta Binamungu alisema akatoka na kumuacha Dokta Festo akiwa amesimama akimtazama Dokta Beatus aliyekuwa amefumba macho.
Dokta Festo naye akafuatia kutoka kisha akaenda moja kwa moja Maabara kuchukua Wallet aliyoagizwa na Boss wake. Alipofika alishtushwa mno mpaka akasahau alichokuwa ameagizwa. Hakuiona ile maiti waliyoifanyia uchunguzi jana usiku. Alitoka upesi akakimbia mpaka kwa Dokta Binamungu.
" Dokta.. Dokta.. Mwili haupo. Cadava haipo" Dokta Festo aliingia ofisi ya Binamungu kwa papara akihema kwa pupa kama Panya aliyekoswa na mtego.
" Unasema nini Festo?"
" Cadava haipo" Bado anahema kwa pupa.
" Unauhakika kuwa haipo Festo. Embu acha mzaha"
" Nimefika pale... Nikashangaa jokofu lipo tupu bila ya mwili"
Festo aliongea akiwa anakiwewe. Dokta Binamungu alitoka bila kusema chochote, Festo naye akamfuata nyuma nyuma, Wote wakaelekea Maabara.
"Tumekwisha! Nani atakuwa amechukua huu mwili?" Binamungu alisema,
" Devis anakesi ya kujibu. Yeye analinda nini ikiwa maiti zinaibiwa humu ndani"
Binamungu alisema tena huku akiangaza macho yake mule ndani. Dokta Festo hakuwa na majibu.
" Huu mlango uliukuta wazi?" Binamungu aliuliza.
" Hapana, Niliukuta umefungwa. Nilifungua kwa funguo ulizonipa" Festo alijibu.
" Mimi na Dokta Beatus ndio tunafunguo za maabara hii. Embu twende huku" Binamungu aliongea, wakatoka. Moja kwa moja waliingia chumba maalumu cha Mitambo ya Kamera ambacho ni room 44. Hapo wakafungua Mtambo maalumu wa kukusanya video na picha zote zilizorekodiwa kwa usiku mzima.
" Haufunguki bila Nywila(Password) Shiit" Binamungu aliongea huku akitazama kioo kikubwa cha ule mtambo ambacho kilimtaka aweke Password.
" kuna njia nyingine naweza kuufungua huu mtambo bila hata hiyo Password" Festo alisema akimtazama Binamungu.
" Embu ifanye hiyo njia haraka haraka tuone kilichotokea usiku"
"Nadhani tungemsubiri Mr. Darmian kuliko kufanya hivi bila ruhusa yake" Festo aliongea kwa sauti ya kuogopa lakini akijua kile anachosema yupo sahihi.
" Hivi wewe Unaakili kweli? Yaani tumsubiri mtu ambaye hatujui leo kaamkaje. Embu fungua huo mtambo. Mimi si ndio mkuu wako? alafu tangu lini nikikupa maelekezo unapinga, haya fungua upesi" Binamungu alifoka na kumuamrisha Dokta Festo afungue ule Mtambo wa Kamera.
Festo alikosa chaguo ikabidi afungue ule mtambo wa kurekodia Video na picha za eneo la hospitali. Dakika tano mtambo ulifunguka. Na video zikaanza kuonekana.
" Rudisha kuanzia mida ya saa saba za usiku baada ya sisi kuondoka" Binamungu alisema, Kisha Festo akafanya kama alivyoagizwa.
Video ilimuonyesha Dokta Beatus akifanya vipimo vya zile Sampo walizozitoa kwenye ile maiti. Waliona pia Dokta Beatus akishtuka baada ya kuona kitasa kinacheza.
" Embu chezesha upande wa kwenye korido tuone aliyekuwa anachezea kitasa" Binamungu alisema na Festo akafanya kama alivyoagizwa.
Wakashtuka kumuona Mtu aliyevalia nguo nyeusi akiwa kaufunika uso wake kama Ninja. Punde walimuona akitoka upesi pale mlangoni na kuingia chumba kingine. Alivyomalizikia walimuona Dokta Beatus akifungua mlango akishangaa huku na huko kwenye ile korido. Hakuona mtu. Waliona kila kitu mpaka Dokta Beatus alivyorudi ofisini kwake akakuta Darubini yake imehamishwa na kuwekwa kwenye Kabati. Hatimaye walishtuka kuona yule mtu aliyevaa kininja akitokea kwa nyuma akiwa kamuwekea Bastola kichwani Dokta Beatus.
" Hamtaweza kufanikiwa Kukwamisha mipango yetu"
Walimsikia yule mtu akimuambia Dokta Beatus.
" Ninyi ni akina nani? Mnataka nini?" Dokta Beatus aliuliza.
" Sio kazi yako kujua mimi ni nani"
Yule mtu aliyevaa kininja alimjibu Dokta Kwa dharau.
" Mnataka nini kwangu?" Dokta Beatus aliongea, lile jitu likamzaba kofi la kichwa, Dokta beatus akadondoka chini. Kisha kwa wepesi yule mtu aliyevalia kininja akatoa kitambaa kutoka katika mfuko wa suruali yake, akamziba Dokta Beatus puani. Matukio yote haya yalikuwa yanaonyeshwa kama mkanda wa filamu kwenye ule mtambo wa kurekodia, Wakina Dokta Binamungu na Festo walibaki wamepigwa na butwaa kwa yale waliyokuwa wanayaona. Kila mmoja alitamani amjue mtu yule aliyevalia kininja kuwa ni nani. Walitamani ile baroka aliyoivaa usoni idondoke na sura yake iwe dhahiri lakini hilo halikutokea.
Punde mtambo ulimuonyesha yule mtu akimuachia Dokta Beatus baada ya kuona amepoteza fahamu. Kile kitambaa bila shaka kilikuwa na sumu ya kumfanya mtu azirai. Yule mtu alielekea mahali ilipo Darubini kisha akachungulia kama alivyokuwa anafanya Dokta Beatus, akaacha. Kisha alichukua zile Sampo A na B na kuziweka kwenye mfuko mweusi alioutoa katika mfuko wa suruali yake. Alipomaliza, alianza kukagua kagua ofisi ya Dokta Beatus mahali ilipokabati. Alichakura chakura mafaili kisha akayarudishia vizuri kama alivyo yakuta.
Akasimama kama mtu anayetafuta kitu alichokisahau au kama mtu ambaye hataki kusahau jambo. Hapo akaona kijitabu juu ya meza, kilikuwa kimefunguliwa na katikati ilikuwepo kalamu. Yule mtu aliyevalia kininja akainama kisha akasoma kilichopo kwenye kile kitabu. Akachana ile karatasi akaiweka kwenye mfuko wa Suruali. Dokta Binamungu na Festo waliyaona hayo yote. Walitulia ungedhani wanatazama filamu ya kusisimua. Ukimya wao uliashiria jambo moja. Nalo ni udadisi na uchunguzi wa hatua zote za mtu yule. Walimuona yule mtu Ninja akitoka kwenye ofisi ya Dokta Beatus lakini walishangaa kumuona akirudi haraka kama mtu aliyesahau jambo. Hii iliwafanya wavute umakini wao kumtazama kuona ni kitu gani alichokuwa amekisahau.
Yule mtu Ninja alifika ilipomeza akaishika Darubini kama mtu anayeikagua. Jambo hilo Walilielewa akina Dokta Binamungu na Festo. Walijua alichokuwa anakitafuta mtu yule. Sura zao zilibadilika mno, ni kama walikuwa wakiomba dua yule mtu asifanikiwe. Lakini dua lao lilikuwa kama dua la kuku ambalo katu halimsogelei Mwewe.
Yule mtu alibinya sehemu fulani kwenye ile Darubini, kikatoka kitu mfano wa Chipu.
" oooh! tumekwisha. Tupo uchi jamani. Sijui itakuwaje" Dokta Binamungu aliongea akiwa kachanganyikiwa huku uso wake ukiendelea kumtazama yule mtu Ninja kupitia video ya ule mtambo. Yule Ninja alitoka, moja kwa moja alielekea ilipomaabara.
" Huyu mtu aliwezaje kujua kwa urahisi mahali maabara yetu ilipo? Hii inawezekanaje?"
Itaendelea episode 02
Simulizi ya MLIO WA RISASI HARUSINI ipo sokoni.
Pata Nakala.
Kitabu Tsh 15,000
softcopy Tsh 8,000
Namba za miamala;
0693322300
Robert Heriel
Airtelmoney
0758216209
Robert Heriel
M-PESA