Riwaya ya Kijasusi: Mlio wa Risasi Harusini

Ahsantee 🤗


🙏🙏🙏🙏

Pitia na humu

 
hadithi haina uhalisia baadhi ya matukio, japo wacha niendelee kuisoma labda italeta uhalisia
 
Hii riwaya mwenye nayo kaisusa, ndioo tatizo la riwaya zinaletwa humu utasubiri weeee hola
 
MLIO WA RISASI HARUSINI ( Episode 04)
Mtunzi: Robert Heriel
WhatsApp 0693322300



ILIPOISHIA.
Yule mtoto wa watu alikuwa kanyamaza kama kondoo anayesubiri kukatwa mkia. Mwili wa Sajent Warioba ulimsisimka na kufa ganzi alipomuona yule Mama akivua ile
chupi na brazia akabaki kama alivyozaliwa. Akamuona yule mtoto akishindwa kuungalia mwili wa yule Mama. Kweli dunia imeisha. Akafikiri. Punde, Sajenti akasikia kitu kigumu kikimpiga kichwani na hapo hapo giza likavamia macho yake na ukungu ukazisonga fahamu zake. Akadondoka chini akapiga kichwa dirisha kutokana na kupigwa na kitu kizito. Jambo hilo lilimshtua yule Mama na mtoto waliokuwa mule ndani. Yule Mama akalisogelea dirisha na kufunga pazia.


ENDELEA....


Fahamu zikamrudia. Alishangaa kujikuta kalala kitandani ndani ya chandarua akiwa katundikiwa dripu kwenye mkono wa kulia. Mwanga hafifu wa bluu uliangaza katika chumba kile. Akajigeuza kwa tabu akashindwa. Alisikia maumivu makali kwenye kichwa. Akaangalia pembeni kidogo akaona meza kubwa yenye makopo na maboksi yenye madawa. Akagundua muda ule ulikuwa usiku lakini hakujua ni usiku wa saa ngapi. Akajaribu kukumbuka yaliyotokea. Alikumbuka alikuwa ndani ya gari akiwa na Ismaiya ambaye alikuwa ndiye dereva. Sasa akajua kuwa walikuwa wamepata ajali. “Hapa ni wapi? Ismaiya wangu yuko wapi?” akawaza. Lakini alijikuta akikata tamaa ya uwezekano wa Ismaiya kupona kutokana na kuwa aliyekuwa akiwafuatilia ni Adele. Robert akafikiri kuwa kama Ismaiya angekuwa amepona basi Adele alikuja akammalizia kwa kumpiga risasi. Alifikiri hivyo akiona katika mawazo yake; akamuona Adele akilisogelea gari lililopinduka akamkuta Ismaiya akiwa ameumia vibaya akiwa hoi taabani. Adele hakumuonea huruma Ismaiya. Akampiga risasi. Robert alishtuka! Kumbe yalikuwa ni mawazo yake mabaya na wala halikuwa tukio halisi. Usingizi ulimchukua tena mpaka asubuhi. Akazinduka. Muda huu chandarua ilikuwa imeondolewa na ile taa ya bluu ilikuwa imezimwa. Akaangalia kwenye ile meza akamuona mtu aliyemgeuzia mgongo akiwa anafanya jambo ambalo hakuwa analiona. Robert alitamani mtu yule ageuke ili amuone. Mtu yule alikuwa kavaa koti jeupe kama daktari. Punde mlango ulifunguliwa na sura ya Adele ilijitokeza. Robert akashtuka kumuona Adele ingawaje kwa upande wa Adele haikuwa hivyo. Yeye alitabasamu. Yule mtu aliyevalia koti jeupe akasalimia, Adele akamjibu kwa ufupi huku akienda kitandani alipolala Robert .

"Mume wangu Robert nilikuwa nakuombea upone" Adele akasema.

Adele akafurahi kumuona Robert akiwa yupo hai baada ya kuzimia kwa zaidi ya masaa thelasini. Aliomba usiku na mchana ili Robert aweze kupona. Sijui alimuomba Mungu yupi ilhali kaiba mchumba wa mwenzake. Sijui alimuomba Mungu yupi ikiwa yeye ndiye chanzo cha kifo cha Ramla. Labda mungu wa sangoma. Hivyo ndivyo alivyokuwa akiwaza Robert baada ya kumsikia Adele aliposema alikuwa akimuombea kwa Mungu. Punde mlango ulifunguliwa. Robert alishtuka kumuona mtu aliyekuwa akiingia. Mapigo ya moyo yakakimbia kwa hofu. Hakutaka jambo lile litokee. Lakini ndio basi tena lilikuwa limetokea. Mbele yake alisimama Mama yake akiwa analia. Macho yake yalilowa tepetepe kwa machozi. Uso wake ulikuwa mwekundu kwa kulia. Robert akamtazama Mama yake kisha akamtazama na Adele aliyekuwa akimbembeleza Mama mkwe wake asilie. Adele alijua kwa kufanya hivi angeuteka moyo wa Mama yake Robert. Aliamini kuwa kama akiuteka moyo wa Mama mkwe basi pasingekuwa na pingamizi lolote kwa Robert. Mama Robert akamsogelea Robert kitandani. "Mwanangu, dunia umeikosea nini? Umeikosea nini dunia?" aliongea kwa kigugumizi kutokana na kusumbuliwa na kwikwi.

"Baba yako walimuua. Wanataka kukuua tena na wewe?" Mama aliongea kwa uchungu sana.
Mama Robert aliona maisha ya mtoto wake yanaingia katika shimo refu lenye giza. Akakumbuka siku ya harusi yake jinsi wale watu wa Ismaiya walivyokuja kumteka Robert. Alikumbuka siku ya harusi ya mtoto wake jinsi alivyomuona Ramla akidondoka chini kwa kupigwa risasi. Akahuzunika kuona siku ya harusi ya pekee kwa mwanaye ikigeuka kutoka siku ya furaha kwenda siku ya kilio.

*************************************************​




Ilikuwa ni siku yake ya kwanza tokea alipopata ajali kupata nguvu ya kuweza kuamka kitandani. Hiyo ni baada ya kulala kitandani kwa miezi sita. Leo alijisikia nguvu kidogo ya kuweza kuamka na kutembea katika kile chumba. Akaamka akatembeatembea pale chumbani akiwa pekee yake. Akaenda mlangoni akakitekenya kitasa lakini mlango ulikuwa umefungwa. Akatembea kidogo kuelekea lilipo dirisha akachungulia kwa nje. Akagundua kuwa kile chumba alichokuwepo kilikuwa kipo ghorofa ya tatu. Akatupa macho yake akaona nyumba nyingi za aina mbalimbali. Hakujua kuwa ulikuwa mji gani lakini hakutaka kuamini kuwa pale ni Dar es salaam kutokana na kuwa mandhari ya eneo lile lilikuwa na miinuko miinuko ya hapa na pale. Alijua kuwa jiji la Dar es salaam kwa sehemu kubwa ni tambarare na kama ni miinuko ipo sehemu chache hasa maeneo yaelekeayo Goba. Chini kabisa alimuona Adele akiwa amepumzika pamoja na mtu mmoja ambaye hakuwa anamfahamu. Walikuwa wakinywa juisi ya chungwa kwa mrija. Aliwaona wakiongea na mara kadhaa walikuwa wakicheka. Akafikiri ni namna gani ataweza kutoroka mule ndani. Robert hakutaka hata mara moja aendelee kukaa mule ndani kama mfungwa. Alitaka atoroke akamtafute Ismaiya mwanamke aliyekuwa akimpenda kuliko kitu chochote kile. Lakini donge lilimshuka kooni baada ya kufikiri kuwa upo uwezekano mkubwa kuwa Ismaiya alikuwa amekufa. Akiwa anafikiri hivyo punde mlango ulifunguliwa na Adele akaingia ndani akiwa amebeba juisi ya kopo. Akamsogelea Robert na kutaka kumkumbatia lakini Robert akamzuia kwa mkono. "Usinikumbatie. Nambie Ismaiya yupo wapi?" Robert akasema akimsukuma Adele hali iliyofanya Adele aangushe lile kopo la juisi.

"Wee shetani haunisikii..! Mke wangu yupo wapi?" Robert akafoka kwa sauti hali iliyofanya kile chumba kiwe na uhai.

"Honey. Calm down. Wewe bado unaumwa" Adele aliongea kwa sauti ya mtu mwenye kujali.
"nani honey wako eeh! Nani? Siwezi kuwa na shetani kama wewe" Maneno hayo ya Robert yalimchoma sana Adele. Aliumia kusikia mtu ampendaye akimuita shetani. Lakini lawama zote akampelekea Ismaiya. Aliamini Ismaiya ndiye chanzo cha mambo yote yale. Adele aliamini kuwa huenda Robert alikuwa amelogwa na Ismaiya. Adele aliwahi kusikia kuwa mwanaume akipewa limbwata akili yake yote inakuwa imevurugwa. Muda wote anakuwa anamuwaza mtu mmoja. Hivyo ndivyo alivyokuwa anaamini Adele.

"Sikiliza Robert . Hata kama hunipendi mimi nakupenda" Adele akasema huku akimtazama Robert kwa macho ya kumaanisha.

"Mimi sioni tabu kupigana kufa kupona kwa ajili yako. Robert mimi nitakufa kwa ajili yako" akameza fumba la mate kisha akaendelea.

"Maisha yangu nimeamua kuyahatarisha kwa ajili yako . Nakupe...eenda Robert " Adele aliongea kwa sauti iliyochanganyika na kilio huku akipiga magoti kumbembeleza Robert . Magoti yake yalikanyaga juisi iliyokuwa imemwagika kutoka katika lille kopo hata hivyo hakujali. Alichojali ni kuuteka moyo wa Robert.

Robert akabaki ameduwaa akimtazama Adele. Unajua nini. Adele ni mwanamke aliyebarikiwa lugha na sauti yenye kushawishi. Alikuwa ni mwanamke mwenye uwezo wa kuigiza onyesho lolote ambalo angepewa na muongoza filamu. Sembuse onyesho hilo la mapenzi yake kwa mtu ampendaye. “Robert naomba unisamehe. Nimegundua bila wewe maisha yangu hayawezekani. Wewe ni kama pumzi yangu. Ndio maana na kuvuta uingie ndani yangu na sitaki nikutoe. Wewe ndiye roho yangu. Ndio maana nakupigania ili mtu mwingine asikuchukue. Tafadhali Robert ..." Adele akaendelea kulalama akiwa amepiga magoti akiishika mikono ya Robert . Akakumbuka jambo. Akasimama mbele ya uso wa Robert wakawa wanatazamana.

"Njoo huku" akasema huku akigeuka kuelekea mlangoni. Alipofika mlangoni akageuka tena kuona kama Robert alikuwa akimfuata. Lakini haikuwa hivyo. Robert alikuwa amesimama akimtazama tuu.

"Honey twende basi" akasisitiza. Robert akapiga hatua polepole kumfuata Adele pale mlangoni. Wakapita kwenye korido ndefu kisha wakaingia kwenye chumba cha lifti. Adele alibonyeza kitufe kilichoandikwa G yaani ground. Dakika moja walikuwa wamefika chini kabisa. Adele akataka kumshika mkono Robert lakini Robert alikwepesha mkono. Wakatembea bila kuongea mpaka waliposimama mbele ya mlango ambapo Adele alichukua funguo na kufungua ule mlango. Ilikuwa ni sebule kubwa yenye samani za kisasa kutoka uturuki. Masofa yalizunguka kijimeza cha kioo ambacho ndani yake kulikuwa na samaki wa urembo waliokuwa wakiogelea. Pia kulikuwa na luninga kubwa ya kisasa ya lg ikiwa imebandikwa ukutani. Juu ya luninga kulikuwa na saa kubwa ya ukutani iliyokuwa ikionyesha ni saa tisa mchana. Pia kulikuwa na midoli midoli iliyofanya sebule ile izidi kuvutia. Adele alimkaribisha Robert ambaye alikuwa amesimama akishangaa mandhari ya sebule ile. Hakutaka kukaa alibaki amesimama akimtazama Adele aliyeenda kuwasha luninga. Punde luninga ikaonyesha msafara wa watu waliobeba jeneza wakiwa wanaimba nyimbo za mazishi. Akagundua kuwa ule ulikuwa ni msiba wa kikristo kutokana na kuwaona wanawake wakiongozana na wanaume kwenda makaburini kuzika. Punde akamuona Mama yake Ismaiya akiwa analia. Alishtuka sana. Akili ilimkimbia na hisia za huzuni zikamzunguka. Hakutaka kujiongopea kuwa ule ulikuwa ni msiba wa Ismaiya mpenzi wake. Angewezaje kujiongopea ikiwa alimuona Mama yake Ismaiya akilia kama mtoto mdogo. Kilio kile kilimuambia jambo moja tuu kuwa kinachomfanya mtu alie vile ni tukio la kuondokewa na mtu ampendaye. Asingejiongopea tena alipomuona baba yake Ismaiya akiwa kavaa suti nyeusi na miwani nyeusi huku uso wake ukiwa na dalili zote za kuomboleza. Moyo wake ulikufa ganzi na kupondeka pondeka alipomuona mdogo wake Ismaiya aitwaye Evelyne akiwa amebeba msalaba ulioandikwa jina la mpenzi wake Ismaiya. akatazama mahali palipoandikwa siku aliyozaliwa na siku aliyokufa akagundua kuwa ilikuwa imepita miezi sita tokea Ismaiya afariki. Walimfikisha makaburini ambapo tayari kaburi lilikuwa limeshachimbwa. Mchungaji aliendesha mazishi na muda wa kuliingiza jeneza ndani ya kaburi ulikuwa umewadia.

"Tafadhali msimzike jamani. Msimzike! Subirini nyie watu" Robert akasema kama mtu aliyechanganyikiwa, muda wote machozi yalikuwa yanatoka. Robert akahisi uchungu mkali moyoni mwake ukipita kama kichomi. Wakati huo Adele alikuwa akimtazama kama mtu asemaye kuwa umeshajua alipo Ismaiya.

"Wewe ndiye uliyemuua Ismaiya. Wewe ni muuaji" Robert akamgeukia Ismaiya akimtazama kwa chuki. "Sikuwa na lengo la kumuua Ismaiya. Nilikuwa na lengo la kukupata wewe. Bahati mbaya rafiki yangu Adele aliumia sana siku ile. Alijeruhika vibaya sana. Hali iliyopelekea kupoteza maisha siku ileile" Adele akasema. Machozi laini yalilamba mashavu yake huku mdomo wake ukianza kutetemeka. Jambo hili lilimfanya Robert amuonee huruma. Maneno ya Adele yalimuingia akilini. Akawaza huenda ni kweli Adele hakuwa na lengo la kumuua Ismaiya kama alivyosema bali ilitokea tu bahati mbaya. Akakumbuka jinsi Adele na Ismaiya walivyokuwa marafiki walioshibana ungesema ni ndugu wa damu. Walikula pamoja. Walilala pamoja. Walikuwa wakivaa nguo zinazofanana mithili ya wachezaji wa mpira. Walivaliana viatu kutokana na miguu yao kulingana. Walitamani kuvaliana nguo lakini hilo halikuwezekana kutokana na kuwa Ismaiya alikuwa na makalio makubwa kumzidi Adele.

"Siwezi kumuamini shetani. Siwezi nasema" Robert akabwatuka huku akimsogelea Adele aliyekuwa ameangalia chini. "Umemuua Ismaiya kwa ufedhuli wako. Alafu unasema bahati mbaya. Unataka kuniletea uongo wako wa kipuuzi! Unafikiri nitakuamini eeh!" Robert akasema kwa sauti ya juu mdomo wake ukiwa umeukaribia uso wa Adele aliyekuwa bado ametazama chini kwa aibu.

"Ramla naye utasema bahati mbaya eeehe! Alafu ati unaongea upuuzi wako. Ati unanipenda..." Robert akasema kwa sauti ya chini huku akimzunguka Adele ambaye alikuwa kasimama palepale akiwa ameangalia chini. Alifika nyuma ya mgongo wa Adele akasogelea sikio lake. Kisha akaanza kuongea kwa sauti ya kunong'ona kwenye sikio la Adele.

"Adele umeutonesha moyo wangu. Umeusagasaga umekuwa kama unga. Umemuua mpenzi wangu. Adele kwa hili sitokusamehe. Umevuka mipaka ya uvumilivu wangu. Nitakuua kifo cha maumivu makali kwa mkono wangu" akavuta pumzi kidogo na kumeva fumba la mate.

"Adele sitokusamehe" hapa akapayuka kwa sauti hali iliyomshtua Adele kutokana na sikio lake kushindwa kuhimili mawimbi ya sauti iliyotolewa na Robert.





*************************************************​



Kilikuwa ni chumba chenye giza totoro. Punde taa ya chemli ikawashwa hali iliyopelekea giza kukimbia. Aliyekuwa ameiwasha ile taa alikuwa ni mtu mweusi tii kama mkaa. Alikuwa ameshika ndoo ya maji ya baridi yenye barafu ndogondogo. Akamtazama Sajenti Warioba aliyekuwa bado hajazinduka akiwa amefungwa kwenye nguzo akiwa ananing'inia. Akammwagia yale maji ya baridi pwaaaah! Hali iliyofanya akili za Sajenti Warioba kumrudia. Sajenti Warioba alipumua harakaharaka kama mbwa panya aliyekoswa na mtego. Yale maji ya baridi ndio yaliyomfanya apumue hivyo. Alihisi baridi ikiingia mwili kwake. Yule mtu mweusi akamsogelea Sajenti Warioba akiwa kashika mjeledi. Akamchapa tumboni kwa nguvu. Sajenti Warioba akasikia uchungu sana lakini alijikaza. Yule mtu mweusi kama msudani akakunja uso wake kidogo kisha akaanza kumcharaza mijeledi hovyohovyo Sajenti Warioba. Sajenti alitoa sauti za uchungu akilia kama mtoto mdogo. Maumivu aliyokuwa anayasikia yalikuwa makali mno. Ndani ya dakika tano Sajenti Warioba alikuwa yupo hoi akiwa kachakaa. Mwili wake ulivuja damu kutokana na mikwaju mikali aliyoipata. Alihisi maumivu makali sana. Donge kubwa la uchungu lilipita kooni mwake likasababisha koo kukauka. Akahisi kiu ya maji. Lakini asingethubutu kumuomba yule mtu mweusi katili aliyekuwa akifurahi maumivu yake.

"Wewe ni nani. unatoka wapi?" yule mtu mweusi tii akamuuliza Sajenti Warioba huku akijifuta jasho usoni mwake. Usijiulize jasho linatokana na nini. Unafikri kazi aliyoifanya ya kumcharaza mijeledi Sajenti ilikuwa ni ndogo. Alimchapa haswa mpaka akachakaa. "Wee mbuzi si ninakuuliza… Wewe ni nani?" yule mtu mweusi mwenye roho mbaya akamuuliza huku akimpiga ngumi ya uso iliyochana mdomo wa Sajenti. Kama ni ngumi basi Sajenti Warioba alikiri ile ilikuwa ngumi. Uchungu wake hakuweza kuufananisha. Akalamba mdomo wake uliokuwa ukivuja damu.

"Nitakuua wewe kenge. Unajifanya mgumu ehhe! Hahahaha! Hapa utasema tuu" yule mtu mweusi aliongea kwa majigambo huku akicheka kwa dharau. Yule mtu mweusi asiye na jina akaondoka kwenye kile chumba akarudishia mlango. Sajenti Warioba akaona afadhali. Aliona ni muda wa kupumua baada ya kipigo kikali. Kumbe alikuwa anajidanganya. Alishangaa kumuona yule mtu akifungua mlango na kuingia ndani akiwa kabeba kikopo kikubwa kama kikopo cha mafuta ya kimbo. Yule mtu mweusi akasogea pale alipokuwa Sajenti Warioba. "Wewe si unajifanya mbishi! Hapa utasema" aliongea hivyo huku akifungua kile kikopo. Mule ndani ya kikopo kulikuwa na siafu wengi mno. Siafu wale walikuwa na hasira kama wamevutishwa bangi. Yule mtu akawamwaga kwenye kichwa cha Sajenti. "Mamaaa! Ooooh! Watoe! Watoe! Nitasema yote. Watoe niseme" Sajenti Warioba alipiga mayowe kama mbwa koko aliyepigwa jiwe na wahuni. Wale siafu walimshambulia usoni. Wengi waling'ang'ania puani. Wengine masikioni, wengine walitaka kuingia ndani ya matundu ya pua na masikio.siafu wawili walishikilia kipande cha mdomo kilichopasuka kutokana na kupigwa ngumi kali na lile jitu jeusi lisilo na huruma. Sajenti Warioba ilibidi afunge mdomo ili siafu wasiingie mdomoni. Hata hivyo wapo siafu wachache ambao aliwafungia ndani ya mdomo. Walimng'ata ulimi na fizi. Pia aliyafumba macho yake ili wale siafu wasimdhuru machoni. Hata hivyo wale siafu walikuwa ni wajeuri na wakatili kama yule mtu mweusi mwenye roho mbaya kama shetani. Sajenti Warioba hakuwahi kupata maumivu makali kama yale. Awali aliwahi kung'atwa na nyuki lakini maumivu yake hayakuzidi maumivu ya kung’atwa na siafu. Hata hivyo aling’atwa nyuki mmoja na leo ni kundi la siafu wakatili wenye sumu kali wa yule bwana mweusi kama jinamizi. Akatamani kuwaondoa na mkono lakini mikono yake ilikuwa imefungwa. Akalia sana wakati yule mtu mweusi akiwa amewasha sigara yake na kuanza kuvuta. Alikuwa akivuta alafu ule moshi akawa anampulizia Sajenti usoni. Jambo hilo lilikuwa linawakera wale siafu. Ni kama ndio alikuwa akiwaambia muumeni zaidi na zaidi. Nao walifanya kama yalivyo mawazo yake. Sajenti Warioba alihisi uvumilivu ukimshinda. Akahisi kamba za uvumilivu wake zikilegea. Alikumbuka kuwa moja ya kazi ya askari Polisi tena mpelelezi kama yeye ni kulinda siri hata ikibidi kufa. Lakini leo siafu walimdhibiti vilivyo. Tayari siafu wengine walikuwa wametoboa mlango wa jicho karibu na kope. Mmmh! Sajenti Warioba alipoona hivi akajua asipofanya kitu macho yake yatafikiwa na kutobolewa na wale siafu wabaya wa mtu yule asiye na jina. "Wewe mtu! Watoe niseme" Sajenti Warioba akasema kwa kupagawa kutokana na siafu wengine kuingia mdomoni baada ya kuachia mdomo wake wazi.

"Hahaha! Nilikuambia utasema tuu. Sasa sema hivyo hivyo. Wewe si unajifanya nunda" yule mtu akasema huku moshi wa sigara ukitoka puani. "Naitwa Aidan Kaaya. Ni ndugu yake na yule mtoto niliyekuwa namchungulia pale dirishani" Sajenti Warioba akasema akimdanganya yule mtu mweusi. Sajenti Warioba aliamua kutumia jina hilo kutokana na alivyomuona yule kijana. Alivyomuona alifanana na watu wa arusha kama sio kilimanjaro. Lafudhi yake pia aliisikia na kuifananisha na watu wa arusha au wachaga. Hivyo kutumia jina la ukoo wa kaaya alijua siyo rahisi kuwa mbali na ukweli. Maneno hayo yakamfubaza kwa upesi yule mtu mweusi. Kutokana na ukweli kuwa yule kijana aliyekuwa na lile jimama chumbani, alikuwa akitokea arusha. Ingawaje ukoo wake haukuwa ni kaaya bali ni Laizer.

"Anaitwa nani huyo kijana" yule mtu mweusi aliuliza huku akimpulizia moshi wa sigara Sajenti Warioba kuwashtua siafu waliokuwa kama wamelegeza midomo yao. Jambo hilo likaamsha mchecheto kwa wale siafu. Wakamng'ata kwa ukali zaidi. Swali hilo alijua ni mtego, Akikosea jina la yule kijana ni wazi angeonekana muongo. Akatafuta koo maarufu za arusha akalipata jina la Laizer. "Anaitwa Nickson Laizar na mimi ni mjomba wake" Sajenti Warioba alimjibu huku akijitahidi kutingisha kichwa chake akijaribu kuwadondosha wale siafu waliokuwa wakimng’ata lakini hakufanikiwa. Jibu hilo likamfanya yule mtu mweusi kuamini kidogo maneno ya Sajenti Warioba ingawaje yule kijana hakuwa akiitwa nickson bali alikuwa akiitwa Joseph Laizer. Alijua huenda yule kijana alibadili jina siku ile walipomteka. Yule mtu mweusi akatoka mule chumbani. Hali iliyomfanya Sajenti Warioba kupiga kelele akimuita aje amtoe wale siafu. Hata hivyo yule mtu mweusi alikuwa kama kaziba masikio kwa pamba. Alitoka na kupotea. Punde mlango ulifunguka. Yule mtu mweusi akaingia akiwa na yule Mama wa makamo aliyekuwa amevua nguo mbele ya kijana Joseph. Nyuma yao alikuwepo Joseph Laizer. Moyo wa Sajenti Warioba ukaingiwa na upepo wa hofu. Akahisi anaenda kuumbuka. Akajua kama yule kijana akiulizwa na akasema hamjui basi huo ndio utakuwa mwisho wa maisha yake.

"Dogo Joseph, unamjua huyu mtu hapa" yule mtu mweusi mwenye sura mbaya aliongea akimnyooshea mkono Sajenti Warioba. Joseph akamtazama kwa kitambo. Pia Sajenti Warioba alikuwa akimtazama Joseph kwa huruma. Alijua muda ule Joseph ndiye alikuwa ameshikilia hatma ya maisha yake. Kimoyomoyo alikuwa akimuambia Joseph. " wewe Joseph, sema unanifahamu. Nakuomba. Nitakutoa humu. Sema unanijua tafadhali" yalikuwa ni mawazo ya Sajenti Warioba aliyekuwa akitazamana na Joseph. Joseph akanyanyua mdomo lakini kabla hajafanya hivyo Sajenti Warioba akaropoka.

"Wewe Mama hivi huoni aibu kumuwekea mtoto mdogo kono lako kwenye bega lake. Embu toa huo mkono" Kitendo cha Sajenti Warioba kuongea hivyo kiliamsha hasira za yule mtu mweusi na lile jimama. Wakamsogelea na kuanza kumpiga. Yule mtu alimpiga ngumi nyingi za tumbo hali iliyomfanya Sajenti Warioba kutapika damu. Jambo hilo likamfanya Joseph amuonee huruma. Sajenti Warioba alifanya hivyo makusudi kutokana na kuona kuwa Joseph alitaka kusema hamjui. Hii ilikuwa nafasi ya kuweza kumpa ishara Joseph kuwa aseme anamjua. Joseph akamtazama Sajenti jinsi alivyokuwa akitoa udenda wa damu mdomoni. Aliyatazama yale makovu mabichi ya mijeledi aliyochapwa Sajenti. Akawatazama wale siafu wabaya waliokuwa wakiushambulia uso wake. Huruma ilimuingia. Alijua kuwa Sajenti Warioba hakuwa na kosa lolote. Kimya kidogo kikatokea huku jibu la Joseph likisubiriwa kama filimbi ya mwisho katika mpira.

"Kohoo! Kohoo!" Joseph akakohoa kama mtu anayesafisha koo lake. Kitendo cha Joseph kukohoa kilimshtua sana sajent. Akajua sasa muda umefika wa yeye kusomewa hukumu yake. Alimtazama Joseph kwa huruma zote. Joseph alikuwa ameangalia chini tayari kwa kutoa maamuzi.
"Namfahamu" Joseph akajibu akiinua uso wake kumtazama yule mtu mweusi katili asiye na huruma. Jibu hilo lilimfanya sajent Warioba kushusha pumzi nzito mithili ya bata dume. Yule mtu mweusi akachukua ule mjeledi akaanza kumchapa nao tena Sajenti Warioba. Muda huu alimchapa mpaka akapoteza fahamu.



SURA YA PILI


Ilikuwa ni mtaa wa gizaasali uliopo mbezi beach ambapo Adelle alikuwa ameikodisha. Wakiwa ndani ya nyumba hiyo ya kisasa Adele akaagiza bodaboda amletee chakula. Ndani ya dakika kumi na tano bodaboda alikuwa getini akiwa kabeba chakula. Adele akaandaa chakula mezani akiwa kavalia nguo nyepesi iliyoonyesha nguo yake ya ndani. Alivaa makusudi nguo hiyo ili aitege akili ya Robert aliyekuwa amelala kwenye sofa. Adele alikuwa akimkata kijicho upembe Robert kuona kama anamuangalia. Alimshuhudia Robert akiyakodolea macho mapaja yake kwa hamu kubwa. Jambo hili lilimfurahisha sana Adele. Alijua kuwa Robert ni mwanaume asingeweza kuruka mitego yake. Adele akaanza kuimba nyimbo za kwao huko tanga.

"ooh mimi ni wako. Ooh kila kitu changu chako. Miguu mpaka kichwa vyote vyako. Siyo upaja wala macho mpenzi pakua kwa lako jiko"Adele kwa nyimbo na misemo alishindikana miaka mingi iliyopita. Aliimudu vyema sanaa ya ushairi na semi. Aliimba wimbo huo kwa sauti nyororo ya kumlaza simba mwendapole ambaye alikuwa akimtazama. Wakati akiimba pia alikuwa akinengua akikichezesha kiuno chake laini kilichoshikiliwa na shanga za kidigo. Looh! Kama ni mtego huyu alikuwa fundi wa mitego. Hakuna mwanaume ambaye angetegwa na Adele asiingie kingi. Robert aliduwaa alipoona kiuno cha Adele kikizungushwa kwa madeko na madaha. akamtazama Adele ambaye alikuwa anamuangalia macho yakiwa yamelegea huku ameung'ata mdomo wake kidogo. Adele jamani! Adele wewe. Adele kiboko ya wanaume. Siyo kwa madaha hayo. Ungedhani ni mlimbwende wa kimataifa anayetumbuiza jukwaani. Robert akahisi mwili ukipata hisia za mapenzi. Mapigo ya moyo yalibadilisha miondoko yake. Yalikuwa yakikimbia lakini kila yalipojaribu kukimbia ndivyo mitego ya Adele ilivyokuwa inayafukuzia. Adele alikuwa amesimama mbele ya Robert akiwa kashika sahani yenye vipande vya nyama ya kuku. Akamsogezea Robert mdomoni ili amlishe. Masikini Robert wa watu alikuwa kaduwaa. Akashtuka kipande cha nyama kikigusa mdomo wake. Akashusha pumzi kama mtu aliyemaliza mbio ndefu.

"Acha! Nitakula mwenyewe" Robert akaongea akikwepesha mdomo wake. Adele akatabasamu kisha akamkabidhi Robert ile sahani yenye vipande vya nyama ya kuku. Hakuwa na wasiwasi. Moyoni alisema; kuku wangu manati ya nini. Haha! Labda siyo mimi Adele mtoto wa kidigo. Akaenda kuwasha luninga kubwa ya bapa. Aliiwasha kisha akaenda chumbani. Akarudi akiwa kashika flash mkononi. Akaichomeka na punde muziki ulianza kuimba. Akamtazama Robert kisha akatabasamu kama ilivyokawaida yake. Robert alikuwa akila nyama kama mtu ambaye hajala muda mrefu. Ni kweli kabisa. Ni zaidi ya miezi saba imepita nyama haijaingia katika mdomo wa Robert . Hii ni kutokana alikuwa amelazwa kwa muda mrefu akiwa hoi kitandani. Jambo hili ndilo lililomfanya Robert azishambulie zile nyama. Adele akaenda kwenye jokofu akatoa chupa mbili za redwine akammiminia kwenye glass na kumpelekea. Hapa alijua kuwa tayari alikuwa amemaliza kazi. Akasimama mbele karibu na luninga jambo hili alilifanya makusudi kumziba Robert aliyekuwa akitazama muziki uliokuwa unaendelea. Kisha akaanza kucheza kidogokidogo kufuatana na mdundo wa muziki. Robert sasa aliacha kuiangalia luninga akawa anamuangalia Adele. Adele alijua kucheza buana. Aliwashinda hata wale waliokuwa kwenye luninga. Hii ndio ilimfanya Robert amuangalie. Punde uliingia muziki kutoka kabila la warazamo. Hapa ndipo kasheshe lilipokuwa. Adele alikata mauno duniani haijawahi kutokea. Robert akakiri moyoni kuwa hakuwahi muona mcheza ngoma kama Adele. Kumbukumbu zake hazikumuonyesha kama aliwahi kuona mtu achezaye kama Adele.

Ilikuwa ngoma ya kizaramo alimaarufu kama gombesugu. Ilikuwa ngoma haswa inayohitaji mchezaji ajue kukata mauno. Adele hilo alilimudu kwa asilimia zote. Adele akajibinua makalio yake na kuyatikisa tikitikitikitiki... Mama weee! Robert akapumbazika akawa amebaki ameshika kipande cha nyama mdomoni asijue akipeleke mdomoni au akirudishe kwenye sahani. Alinata mithili ya sanamu la michelini. Mdomo wake ulibaki wazi huku macho akiwa kayatoa nje. Alishangaa jinsi makalio ya Adele yalivyokuwa yakitikisika huku shanga kiunoni zikicheza ukutiukuti. Huyo ndiye Adele mtoto wa kidigo. Mwanamke aliyeshindikana sokoni kwa mkopo na kwa pesa mkononi. Muda wa kulala ulifika. Hata hivyo pamoja na mbwembwe zote za Adele lakini Robert hakutaka kulala naye. Angeweza vipi kulala na mwanamke aliyesababisha kifo cha mtu ampendaye. Angeweza vipi kulala na mwanamke aliyesababisha yeye kupata ajali nusura apoteze maisha. Hilo aliliona ni jambo ambalo kamwe lisingewezekana.

"Honey tulale wote kwa leo. Hatutafanya chochote" Adele akasema.

"Hilo haliwezekani Adele. Nielewe" kimya kidogo kilitokea wakati Adele anamtazama Robert bila kuongea lolote.

"Mimi naondoka. Naenda kulala kwangu".
"Haa! Unaenda wapi usiku huu. Muda umeenda sana mume wangu"

"Mimi siyo mume wako. Nimekuambia usiniite hivyo"

"Jamani kwani ni kosa kukuita hivyo, Anyway tuachane na hayo. Basi utalala chumba kile. Nami nitalala hiki. Sawa!"
Adele akasema akimuonyesha Robert vyumba vya kulalia. Robert akaondoka kwenda kwenye chumba alichoonyeshwa na Adele. Adele alimfuata nyuma nyuma kama bata na watoto wake. Alipofika chumbani Robert alishangaa kumuona Adele nyuma yake.

"Adele nimechoka. Nahitaji kupumzika"

"nimekuja kukuaga mpenzi. Mwaaah"
Adele akasema kisha akamkumbatia kwa nguvu na kumbusu Robert katika shavu lake kwa lazima. Robert akamsukuma hali iliyofanya Adele apepesuke. Adele akatabasamu kisha akasema. "Nakupenda mume wangu. Ulale salama" Maneno hayo aliyatoa akidengua kisha akaondoka. Robert akaenda kufunga mlango na funguo ili kukwepa kero za Adele. Aliingia bafuni kuoga kisha akatoka. Akajilaza kitandani. Mawazo mengi yakamjia. Aliwaza juu ya yote yaliyokuwa yametokea. Alikumbuka siku ile ya harusi ilivyokuwa imependeza lakini baadaye ikageuka kilio. Alimkumbuka Ramla aliyekuwa mshenga wa Adele jinsi alivyopigwa risasi. Kumbukumbu hii ilimtia uchungu sana. Moyoni alijisemea; nisamehe Ramla hukuwa na hatia yoyote. Akamkumbuka Ismaiya mwanamke aliyekuwa anampenda kuliko jambo lolote lile duniani. Alikumbuka alivyodanganywa na Adele kuwa Ismaiya alikufa kwenye ajali ya ndege ya malaysia. Punde uso wake ulikunjuka kwa tabasamu. Ni kutokana na kumbukumbu ya walivyokuwa wakifanya mapenzi na Ismaiya mara ya mwisho wakiwa maeneo ya Bunju. Akakumbuka jinsi walivyofurahiana. Kila mmoja alimchezea mwenzake kwa kadiri alivyoona inampendeza. Lakini tabasamu liliyeyuka alipoikumbuka ajali iliyosababishwa na Adele aliyerusha risasi kwenye gari lao likapinduka. Mwisho machozi yalimtoka alipoona jeneza la Ismaiya likibebwa kwenda makaburini.. Hiyo yote ilikuwa kumbukumbu. Akamuona Ismaiya akiwa anachuma maua kwenye bustani iliyokuwa kwenye uwanda wa tambarare akiwa kavaa dera na mtandio. Moyo ulilipuka. Akaogopa sana. Robert akapiga hatua kumsogelea huku akimuita.

"Ismaiya! Ismaiya!" Ismaiya akageuka na alipomuona Robert akatabasamu.

"Ismaiya mpenzi. Nilidhani umekufa kumbe upo hai mpenzi?" Robert akasema huku akipiga hatua kumfuata Ismaiya aliyekuwa umbali wa mita kumi.

"Mimi sijafa. Penzi letu ndio limekufa" Ismaiya akajibu akiwa ameshika ua zuri lenye rangi ya njano ya papai. Punde Adele akatokea kwa nyuma na kumchoma Ismaiya kisu cha mgongo. Robert akashtuka. Kumbe alikuwa akiota. Robert alijikuta yupo kitandani jasho likiwa linamtoka huku akipumua kwa pupa. Ni ndoto hiyo mbaya iliyomfanya ashtuke usingizini. Hata hivyo tayari kulikuwa kumekucha miale ya jua ilikuwa ikirandaranda katika chumba kile. Ndege walikuwa wakiimba nyimbo za sifa kuikaribisha siku nyingine mpya.

Robert akaenda kuoga. Akiwa bafuni alimsikia Adele akibisha hodi.

‘'Nipo bafuni. Nakuja adele" Robert akasema. Akamaliza kujiandaa akaelekea sebuleni ambapo alimkuta Adele akiwa kajilaza kwenye sofa akiangalia luninga. Adele alipomuona Robert akaamka na kumkumbatia kwa nguvu sana. Akamlazimisha denda mpaka akafanikiwa kubadilishana ndimi na Robert . Jambo hili likaibua hisia kali za mapenzi kwa Robert . Adele alijua ile ndio nafasi pekee ya kuonyesha ufundi wake. Alijua kama ataipoteza ile nafasi basi asingepata nafasi ingine. akamshika Robert kwenye maeneo yake nyeti kwa ustadi wa hali ya juu huku wakiendelea kupeana asali ya mdomoni. Hali ya Robert ikazidi kuwa mbaya. Hamu ya mapenzi zikamzidi nguvu. Akajikuta akimuachia nafasi Adele ambaye alionekana kukamia. Adele akamsukuma Robert kwenye sofa na kwa haraka aliwahi ilipo zipu ya suruali akaifungua na kupeleka suruali chini. Sasa Robert alibakiwa tuu na pensi ya ndani. Ulikuwa wakati mzuri wa Adele kuchota asali katika mzinga. Robert alikuwa amepagawa mno. Mbaya zaidi ni kuwa Adele hakuwa amevaa kitu chochote ndani isipokuwa kanga nyepesi. Jambo hili lilizidisha uhondo kwa Robert.

"Mimi sijafa ila mapenzi yetu ndio yamekufa" Robert alikumbuka maneno ya Ismaiya aliyoyaota usiku wa jana. Maneno hayo yalimrudisha kwenye akili yake. Akamsukuma Adele kwa nguvu chini, kanga aliyoivaa Adele ikachomoka kiunoni akabaki uchi kama alivyozaliwa. Adele hakuamini kama hatua aliyofikia; Robert angeweza kufanya vile. Kwa hatua ile alijua tayari mtego wake umefanikiwa lakini haikuwa hivyo, Robert alikuwa ni mtu makini na mwenye msimamo thabiti linapokuja suala la mapenzi. "Hutanidanganya kama kipindi kile Adele" Robert alimuambia Adele huku akimbetulia mdomo kwa dharau. Adele bado alikuwa pale chini akiwa amejishika kiuno kama mtu aliyeumia. "Ulinidanganya Ismaiya alikufa kwenye ndege ya malaysia. Leo hutanidanganya"

Robert akasema huku akiamka kwenye sofa. Akavaa suruali yake iliyovuliwa na Adele.

"Nikudanganye kipi. Kwamba Ismaiya hajafa? Nitakupeleka kwenye kaburi lake ili uamini" Adele akasema kwa hasira akiwa bado palepale chini. "Kumbe hakufa kwenye ndege si ndio wee kenge? Hivi wewe mwanamke huyo shetani uliyenaye anakulipa nini mpaka ufanye mambo yote haya?" Robert akadakia kabla Adele hajamaliza kuongea. Maneno hayo Adele hakuwa na lakujibu. Akabaki amemtazama tuu Robert. "Twende kwenye kaburi la Ismaiya. Usije ukawa hata hili umenidanganya. Amka twende" Robert akasema huku akienda ulipo mlango wa kutokea.

"Sasa kama Ismaiya hajafa tunaenda kwenye kaburi la nani? Si umesema mimi ni muongo. Basi hakuna haja ya kwenda” Adele alipoona Robert amemkata jicho la hasira akasema; “Sawa subiri nikavae nguo ili twende maana unavyoniangalia”

"Kavae unasubiri nini hapo chini?"
. Adele akaamka pale chini na kujifunga kanga yake iliyochomoka baada ya kusukumwa. "Basi kunywa chai nikienda kujiandaa" Adele alimuomba Robert aliyekuwa akimtazama kwa hasira. Maneno hayo yalimpoza kidogo Robert lakini hayakumshawishi.

"Sina haja na chai. Namtaka Ismaiya wangu" Robert alibwatuka kama mlevi. Kisha akaendelea. "Nakupa dakika tano. Hujamaliza naondoka"

"Yamekuwa hayo tena. Sawa nakuja"
Adele alijibu huku akienda chumbani kujiandaa.

Wakafika kwenye makaburi ya kinondoni na moja kwa moja Adele alimpeleka lilipokaburi la Ismaiya.

"Hapa ndipo alipopumzishwa rafiki yangu kipenzi Ismaiya" Adele akasema huku akipiga magoti kwenye kaburi la Ismaiya. Akasujudu akachota mchanga kwenye mikono yake akalia. "Maiya kipenzi changu. Nisamehe kwa niliyokufanyia rafiki yangu. Nimekukumbuka sana"
Adele akasema huku akilia kwa sauti ya kwikwi. Akiwa kavaa baibui jeusi lenye vishikizo kwa mbele. Kichwani amevaa lemba na miwani ya rangi nyeusi. Huku masikioni akiwa amevaa hereni za mduara zenye rangi ya dhahabu. Robert akasimama mbele ya msalaba wa kaburi la Ismaiya ambapo akaona jina la Ismaiya na umri aliozaliwa na tarehe aliyofariki. Aligundua kuwa Ismaiya ni kweli alikufa siku ileile waliyopata ajali. Robert akajikuta akitoa machozi bila kujua. Akalia sana. Alijiona yeye ndiye chanzo cha kifo cha Ismaiya. Alijua bila yeye Ismaiya leo hii angekuwa hai. Mbaya zaidi Ismaiya alikufa kwenye tukio la kutetea penzi lao. Alikufa akirusha risasi kuwashambulia watu waliotaka kumtenganisha na yeye. Alikuwa akikimbiza gari akikiwakimbia watu wanaotaka kumtenga naye. Yote hayo Robert alikuwa akiyawaza. Lakini alishindwa kukikimbia kifo ambacho kimemtenganisha naye daima.

"Kifo njoo hapa nikupige. Njoo hapa. Kama wewe ni kidume. Njoo....." Robert akapayuka kwa sauti huku akivuta ule msalaba kama anayetaka kuung'oa.

"Kama ungekuwa na nguvu si ungenichukua mimi eeh...! Mbona ukamchukua msichana wa watu. Kifo njoo hapa" akasema huku akiuangalia msalaba kana kwamba msalaba ndio hicho kifo alichokuwa akikiita. Kuna muda alikuwa anaunyooshea ule msalaba kidole. Adele aliona jinsi Robert alivyokuwa anauchungu na kuchanganyikiwa. Akajuta kwa tukio alilokuwa amelifanya, lililoondoa uhai wa rafiki yake kipenzi. Lakini majuto siku zote ni mjukuu. Kaburi la Ismaiya bado lilikuwa halijajengewa. Lilikuwa na maua machache. Robert hakuona ua lake katika kaburi la mpenzi wake. "Ona! Ona! Ona sasa. Kaburi la mtu ninayempenda halina hata ua langu. Maiya.. Maiya mama yangu...eee" Akaanza kulia tena huku akishika maua yaliyowekwa juu ya kaburi la Ismaiya. Akatoa ua moja baada ya ua jingine huku akilia kwa uchungu. Punde akanyanyua ua moja na jambo lisilotarajiwa likajitokeza. Kilianguka kipande kidogo cha karatasi lilichokunjwa vizuri. Adele naye alikiona. Adele alitaka kukiokota lakini Robert alikuwa mwepesi zaidi yake. Akawahi. Kisha akakifungua. Ile karatasi ilikuwa inamandishi ya wino mweusi yenye hati ya Ismaiya. Wino mweusi uliashiria huzuni na maombolezo. Robert akaanza kusoma wakati Adele akimsogelea karibu na bega lake kwa nyuma.

"Kwako Robert mpenzi. Nimeondoka sitorudi tena. Nimeondoka bila kuagana na wewe kipenzi changu. Nimeenda mahali usikofika. Mapenzi yangu yataisha kwako siku jua likiacha kuangaza. Nitakupenda hata kama sikuoni tena. Nilijitahidi kupigania penzi langu. Ilikuwa haki yangu kukupigania. Lakini... Lakini.. Laki..ni mwenzangu amenishinda. Roobert. Kifo kilimsaidia. Kifo hiko mume wangu kilimsaidia" Robert aliweka kituo akaanza kulia. Yalikuwa maneno makali aliyoyasoma kwenye ile karatasi ambayo aliamini yalikuwa yametoka kwa Ismaiya. Kisha akaendelea kusoma; "Mimi nimekimbia bila kupenda. Mwenzangu alisaidiwa na kifo. Mimi sikuwa na wakunisaidia. Baki salama mume wangu kipenzi. Tutaonana baadaye. Eu te amo ternamente mimi Ismaiya"

"Nakupenda pia mke wangu"
Robert aliyajibu maneno yaliyokuwa yameandikwa Eu te amo ternamente ambayo ni lugha ya kireno yakimaanisha nakupenda sana. Robert alimkamata Adele na kumpiga vichwa vitatu mfululizo. Hali iliyomfanya Adele apige kelele.

"Unaniua! Unaniua Robert " Robert hakujali akaendelea kumpiga akichanganya ngumi na mateke. Adele akaongeza mayowe akiomba msaada.

"Nakuua leo Adele. Nenda ukamlete Ismaiya" Robert akafoka huku akimpiga ngwala Adele ambaye alidondoka chini kama gunia la chumvi. Alimpiga mateke ya tumbo mpaka Adele akaanza kutoa damu za mdomoni huku sauti ikianza kupungua. Punde kundi kubwa la watu lilikuwa likija huku likimrushia mawe Robert.

Robert alipoona watu wanakuja akajua anaweza kuuawa na watu wale. Akamuacha pale chini Adele na kuanza kukimbia. Mawe yalikuwa yakimkosakosa huku akisikia wakiimba mwizi! Mwizi! Kamata mwizi huyo. Robert akaongeza kasi lakini wale watu nao walikamia. Walimfukuza kama paka shume jizi lililoiba nyama ya mabaharia. Bahati haikuwa yake. Alipigwa jiwe la kichwa akadondoka chini. Aliona kizungu zungu na kichwa kilikuwa kizito sana. Akili yake ikamuambia; walimuua Ismaiya na wewe sasa wanakuua. Kimbia Robert . Alijikaza akaamka na kuendelea kukimbia huku akipepesuka. Damu zilimtoka kichwani zikalowesha shati alilokuwa amelivaa. Akaingia kwenye uchochoro mmoja wa mitaa ya kinondoni iliyozunguka yale makaburi. Lakini bado alisikia wale watu waliobeba mawe wakisema mwizi! Mwizi wakija huku wakitupa mawe. Robert akahisi nguvu zikiwa zinamuisha baada ya damu nyingi kuvuja. Masikini Robert akapigwa jiwe jingine la mgongo lililompeleka chini. Hata hivyo alijikaza akaamka. Alijua kama atajilegeza siku ile ndio ingekuwa mwisho wa maisha yake. Akakaza mbio lakini za kujikokota. Alipiga kona akaona nyumba ambayo mlango upo wazi. Akatoma ndani moja kwa moja akaingia chumbani bila hodi mpaka uvunguni.

Kule uvunguni alisikia vishindo vya wale watu waliokuwa wakimkimbiza wakipita huko nje. Moyo wake ulikuwa unadunda sana. Alimuomba Mungu amuepushe na watu wale ambao walitaka kumpiga kwa mawe. Ghafla akasikia wale watu wakimuuliza mwanamke mmoja huko nje.

"Habari za asubuhi Mama. Hujaona mtu yeyote aliyejeruhiwa akikimbia?"

"Mtu akikimbia! Mimi sijaona mtu njia hii" Yule Mama alijibu huku akiwa ameshtushwa na maswali ya wale watu. Robert akiwa chini ya uvungu aliendelea kuomba Mungu wale watu waondoke pale nje. Mungu siyo Athumani wala siyo selemani. Aliwasikia wale watu wakiondoka. Akashusha pumzi nzito mithili ya kobe mzee. Ni kama alikuwa amebeba mzigo mzito. Punde alisikia maji yakimwagwa kwenye pipa lililokuwa sebuleni alipokuwa yule mwanamke. Hapo akajua kuwa yule Mama alikuwa ametoka kuchota maji. Akahisi kichwa kikimzunguka. Macho yakaingiwa na giza zito. Hatimaye alipoteza fahamu.

ITAENDELEA

Jipatie simulizi yote ya MLIO WA RISASI HARUSINI Softcopy kwa Tsh 3,000/= Kitabu Tsh 10,000/=

0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel
Duuh riwaya nzuri ila mpangilio wa matukio sio mara inaenda miezi saba mbele mara inarudi nyumaa kwa afande aliotekwa
 
Back
Top Bottom