Riwaya: UCHU

Waandishi wa kiwango hiki tanzania wamekwisha kitabu kina miaka lakini bado kitamu. Njama, kikomo, kikosi cha kisasi ah musiba pumzika.
 
UCHU
BIBIANE-II

Willy Gamba alimkuta Col. Rwivanga
anakula chakula. Alipomuona Willy
alionekana kufurahia "Nimekusubiri sana
mpaka nikaamua bora niendelee na
chakula maana ni zaidi ya saa nne sasa
na unajuwa mimi nakula mara moja tu
kwa siku, njaa ilikuwa inauma sana", Col.Rwivanga alijitetea.
"Usijali Kamanda", Willy alijibu huku
akielekea jikoni kuchukua sahani na kisha akaketi kwenye meza pamoja na Col.Rwivanga na kupakuwa chakula.
"Hiki chote kilikuwa chako peke yako",
Willy alimkejeli Col. Rwivanga.
"Hapana, nilijuwa tu utanikuta nakula",
Col. Rwivanga alijibu huku akicheka. Willy alichota kijiko cha kwanza na kukitia mdomoni, chakula kilikuwa wali na mchemsho wa nyama.
"Lo, mpishi ni wewe?".
"Kwani vipi?".
"Kitamu sana chakula hiki", Willy alijibu.
"Wapi, na wewe una njaa vilevile, upishi wangu mimi ni mchemsho tu".
"Hapana si njaa ila wali umepikwa vizuri na nyama ya mchemsho, napenda sana mimi", Willy alieleza.
"Ehe vipi huko, umewakuta?".
"Bwana nimewakuta wale mapadri na
nimewekwa shule hasa, na sasa hivi
naijua historia ya utawala wa nchi vizuri sana kuanzia kabla ya ukoloni".
"Wacha bwana".
"Nakuambia wale mapadri wanaijua nchi
hii kuliko viganja vya mikono yao", Willy alimweleza Col. Rwivanga, kisha
akamgusia kwa muhtsari mambo muhimu
aliyoelezwa.
"Kumbe hili swala la Akazu hata hawa
wazee wanalifahamu sana?", Col.
Rwivanga aliuliza baada ya maelezo ya
Willy.
"Sana, na wamesema bila hawa watu
kukamatwa hakuwezi kuwa na amani
katika nchi hii".
"Hilo ni kweli kabisa na sisi tunalijua na ninafikiri ndio walio nyuma ya hili swala la kutaka kukuua maana hawa watu wana mahusiano dunia nzima na pesa nyingi.
Hivyo, tunajua wanajipanga kuja
kutuhujumu, hilo tunajua. Ila hatujui kwa sasa hivi wanafanya shughuli zao kutoka wapi. Nia yetu imekuwa ni kuimarisha
serikali yetu, halafu ndipo tuangalie
habari yao", Col. Rwivanga alieleza.
"Ni sawa, lakini mimi nafikiri jambo hili mgelishughulikia sasa hivi wakati bado nao wamechanganyikiwa, lakini mkisubiri watakusanya nguvu halafu itakuwa shida tena", Willy alishauri.
"Kutokana na matokeo ya siku hizi mbili
nasi tumeshituka sana, maana
inaonekana hawa watu bado wana watu
ndani ya serikali yetu na wameanza
kutuhujumu. Kama unavyosema, nasi
tumeamua kulishughulikia mara moja
swala hili na tutakuwa na mkutano na
makamanda wote wa jeshi pamoja na
baraza la mawaziri kesho saa moja na
nusu asubuhi", Col. Rwivanga alieleza.
"Hivyo itakuwa vizuri. Ingawaje mimi kazi
iliyonileta haikuwa ya mapambano, lakini
kwa sababu wao ndio wamenianza na
mimi naomba ruksa yako unilinde mbele
ya wakubwa wako, kwani nataka nami
kwa kiasi fulani nijuwe habari ya watu
hawa na vipi wameamua kutaka
kuniangamiza. La maana hasa nataka
nijuwe nani hasa anahusika na kutaka
kuniua mimi. Hilo Col. Rwivanga
ningependa sana unipe hiyo nafasi
nifanye kazi yangu", Willy alijieleza.
"Ni sawa lakini tungeomba na sisi
utufahamishe kila hatua unachofanya ili
tuweze kukusaidia itakapobidi kwani
ukweli ni kuwa kazi hii ni yetu na wala si yako", Col. Rwivanga alijibu.
"Asante Col. Rwivanga. Vipi yule
msichana wa jana usiku, Bibiane umepata
habari zake?".
"Ahaa, ndio nilikuwa nakusubiri nikueleze.
Hivi usingewahi ungenikuta nimeshaenda
kumfuata. Huyu msichana inasemekana
ni mkalimani, anajuwa lugha kama nane
hivi na amekuwa akifanya kazi serikalini kama mkalimani hivyo, alikuwa akisafiri
na Rais au mawaziri ama maafisa
wakubwa wa serikali wanaposafiri nje ya
nchi na vilevile ndiye aliyekuwa
mkalimani wa serikali kama wageni
wasiojuwa kifaransa wakija nchini hapa.
Inasemekana wakati wa mauaji yeye
hakuwepo. Alikuwa Nairobi, lakini ni kati ya watu wa kwanza kabisa kurudi na
amekaa katika nyumba yake aliyokuwa
akiishi toka zamani mtaa uleule wa Silas Biniga, lakini nyumba ya nne mbele kwenye kona watu wamekuwa hawana
wasiwasi nae kwani inasemekana ana
asili ya Kitutsi ingawa ni chotara na uzuri wake watu wengi wameuchukulia tu kuwa huenda ni chakula ya wazee. Kwa hivyo hakuna ambaye amediliki kumgusa. Hivyo nataka nikajuwe habari zake", Col.Rwivanga alieleza.
"Hapana, usiende wewe, maana wewe ni
afisa wa ngazi za juu na unajulikana hapa la pili wewe ni mwanajeshi. Kazi hii ni ya mpelelezi kama mimi. Tatu, nina kisasi
naye. Naomba uniachie, usiku huu lazima
nitapambana naye kama bado yuko hapa
mjini na nitakujulisha habari zake
baadae".
"Sawa Willy, kazi kwako, mzee naye
alinieleza ndio zako hizo ikibidi msichana au mrembo".
"Zamani siyo sasa, sasa nimestaafu
maana nimeoa lakini kwa msichana kama
yule ambaye hatishiki na mtu kuuawa,
nataka mimi mwenyewe nijuwe habari
zake. Habari ulizonazo ni kwamba bado
yuko mjini?".
"Jioni hii ameonekana akiendesha gari
lake aina ya MB 190E. Na hilo ni gari lake hata kabla ya mauaji na kabla sisi
hatujaingia hapa. La ajabu si sisi wala si Intarahamwe aliyegusa gari lake, ni jambo la kushangaza na limefanya nitaka
kujuwa huyu binti vipi mambo yake".
"Basi niachie maMBO yake utayapata. Si
bure huyU binti ni mtu hatari, na hatari sana".


ITAENDELA
 
BIBIANE - III

Baada ya Col. Gatabazi kumwelezea mipango yote kama walivyokuwa wamepanga na Jean, Nkubana aliomba gari ili akawachukuwe wenzake na kuanza kazi ya kumsaka Willy. Col.
Gatabazi aliwapa gari aina ya Landrover
110 ya Jeshi ambayo hutumika kwa ajili
ya wageni wa Serikali. Kwa sababu ya
kazi maalum iliyokuwa ikiwakabili,
kutokana na unyeti wa kazi hiyo, Col.
Gatabazi aliwaachia gari hilo waendeshe
wenyewe. Nkubana alikwenda, moja kwa
moja akawaamsha wenzake, baada ya
mazoezi makali, walioga na kupata
chakula pale hotelini, kisha wakaanza
kazi ya kupeleleza habari za Willy
Gamba.
Kutokana na maelezo waliyokuwa
wamepewa na Col. Gatabazi, mara moja
walijua kuwa Willy yuko Meridien Hoteli, mara baada ya kupata namba ya chumba chake cha kulala waliamua kwanza
wakafanye shughuli nyingine ili wasubiri wakati mzuri wa kupambana na Willy Gamba ambaye pia walikuwa wakimhofia kwa kiasi fulani.
Baada ya kupanga vyema mipango yao
ya kuhakikisha wanamuua Willy Gamba
usiku huo. Walirudi hotelini wakapata
kinywaji kidogo kwa ajili ya kujiweka safi.Ilipotimia saa nne hivi usiku wakaamua kwenda kwa wote kwa Col. Gatabazi kwa ajili ya mikakati ya ziada. Ni wakati huo walipokuwa wakielekea kwa Col. Gatabazi
ndipo walipokaribia kuligonga gari la Willy Gamba bila wao kujuwa kuwa ndiye mtu anayepanga kumuangamiza usiku huo.
Kwa kasi ileile, gari hilo liliingia nyumbani kwa Col. Gatabazi, aliyekuwa nje ya nyumba yake akitafakari jinsi Willy alivyokuwa akiwanyima usingizi.
alipowaona akawapokea kwa tabasamu
kisha akawaongoza hadi kwenye sebule
ya nyumba yake.
"Vipi mmepata habari zozote kuhusu Willy Gamba?", Col. Gatabazi aliwauliza baada tu ya kuketi kwenye makochi.
"Habari za Willy zote tunazo, huyo
tutaanza biashara yake, atakuwa
marehemu baada ya saa sita usiku",
Nkubana alijibu kwa majidai na kujiamini.
"Nasema tena lazima muwe makini sana,
huyo mtu ni hatari sana, na amri ni
kwamba mara hii isishindikane,
akionekana tu ua mara moja", Col.
Gatabazi alisisitiza.
"Col. tafadhali usitutishe na huyo mtu
wako, atakuwa hatari gari mbele yetu! Vipi una matatizo nini Col. Gatabazi?",
Nkubana alijibu kwa mshangao huku
vijana wake wote wanne wakicheka kwa
dharau.
"Acha wasiwasi mzee, kazi ya Willy
hesabu imeisha, amezoea kucheza na
wafanzi leo atakutana na waalimu wa
kazi", Felician alimhakikishia Col.
Gatabazi.
"Ehe, Bibiane umemtaarifu kuwa
tutakwenda nyumbani kwake leo?",
Nkubana aliuliza.
"Bibiane ana taarifa zenu, na wakati ndio huu, twendeni basi mara moja, hiyo gari acheni hapa maana anakaa ileile nyumba yake", Col. Gatabazi alijibu.
"Ahaa, kweli gari tuache tu hapa,
tutalipitia wakati wa kwenda mjini",
Felician alijibu.
"Haya twendeni anatusubiri, lakini mjuwe kutokana na mipango ilivyo mimi
nitawaacha pale nyinyi mtaendelea nae",
Col. Gatabazi aliwaelza.
"Sawa hamna tabu", wote walijibu kwa
pamoja na kuondoka kuelekea kwa Bibiane.


ITAENDELEA
 
BIBIANE -- IV

Wakati Willy anafika nyumbani kwa
Bibiane. Col. Gatabazi alikuwa
akifunguliwa lango la mbele nyumba hiyo
akatoka na kuondoka akihofia matatizo
aliyokumbana nayo kwa Luteni Biniga.
Willy alichukuwa hadhari kubwa sana
maana alichukuwa vifaa vya kazi si
mchezo. Kwa vile nyumba ya Bibiane
ilikuwa kwenye kona ya barabara mbili,
Willy alibana kwenye kona moja na
kuchungulia mbele ya nyumba na kuona
lango likifunguliwa. Alimuona mtu mmoja
akitoka na kukatisha barabara na
kuelekea kwenye uchochoro na
kutokomea. Willy alirudi nyuma kidogo na
kuhisi kuwa sehemu ile ndiyo ilikuwa
nyuma ya nyumba hii. Kwa hadhari sana
alikwea ukuta uliozungishiwa vyuma
vilivyochongoka juu. Kwa vile Col.
Rwivanga alimweleza kuhusu hilo. Willy
alikuwa amejitayarisha vizuri kabisa kwa lolote. Alikwea na kuchungulia ndani, baada ya kuangaza vizuri macho yake aliweza kuona kivuli cha mtu amebana kwenye ukuta wa nyumba hii karibu na upande wa pale alipokuwa yeye. Mtu huyu
alikuwa amebeba bunduki kubwa. Hivyo,
Willy alihisi ni mlinzi wa pale nyumbani.
Baada ya muda kidogo, Willy alimuona
mtu mwingine anakuja akitokea upande
wa mbele kuja upande huu ambao huyu
mwingine alikuwa amebana. Willy
alijining'iniza juu ya ukuta kwa nje ili asionekane huku macho yake yakiwa
usawa wa ukuta. Yule mtu alikuja moja
kwa moja mpaka usawa wa yule
mwingine alipokuwa amesimama.
"Unataka sigara?", yule aliyekuja eneo hilo
alimuuliza mwenzake.
"Sitaki, hao jamaa ndani si wamalize
mambo yao haraka ili waondoke na sisi
twende zetu, maana hapa tunapoteza
muda na huku kazi yenyewe bado", yule
wa pili ajibu.
"Mbona kama una wasiwasi, vipi
unaogopa?".
"Kwanini nisiogope, mimi si binadamu
bwana?".
"Acha woga wewe, wajuwa Kaisari
alisema watu waoga mara nyingi hufa
kabla ya tarehe ya vifo vyao kufika,
komaa mtoto wa kiume", mwenzake
alisema kwa kujiamini.
"Bwana, hebu nenda kalinde sehemu yako
na umwambie huyo Nkubana aharakishe
kutoka sehemu hii".
Baada ya kuelezwa, yule mtu aliyekuja
sehemu hii kutoka mbele aliondoka
kimyakimya kurudi kule alikotoka huku
mwenzake akimsindikiza. Willy akatumia
nafasi hiyo. Kama tumbili aliukwea ule
ukuta haraka sana. Kufumba na
kufumbua akaruka juu ya vile vyuma na
kujitosa ndani bila hata kusababisha
kishindo na kujibanza kwenye ukuta. Kwa
vile Willy alikuwa amevaa nguo nyeusi
pale alipokuwa amejibanza ilibidi
umsogelee karibu sana ndipo uweze
kumtambua maana upande huu wa
nyumba hapakuwa na mwanga. Mara
akamsikia yule mlinzi akirudi upande
wake, kutokana na mazungumzo
aliyokuwa ameyasikia alihisi hawa nao
bila shaka walikuwa kundi lilelile kama
alilopambana nalo kwa Luteni Biniga. Bila
shaka walikuwa wamekuja kwa malipo
kwa huyu mwanamke. Willy alijitayarisha
na kujibanza kwenye ukuta utafikiri
buibui. Yule mtu alikuja akinyata taratibu
utafikiri alikuwa amehisi kitu. Willy
alikuwa amebana kwenye kona kabisa ya
upande wa pili wa nyumba. Huyu mtu
alipofika hapo tu, kama Simba
anapomrukia Swala, Willy alimtia kabali
kwa nguvu zake zote. Yule mtu hakuweza
hata kuguna maana kabali ile ilikuwa kali,
na huku akitumia utaalam kumuua
kimyakimya kwa kumnyonga, Willy
alimuua yule mtu. Kisha, alimvuta mpaka
kwenye ua wa nyumba na kumvua shati,
akavua lake na kuvaa la yule mtu kwani
ukubwa wa mwili na urefu walikuwa
wanalingana. Akatwaa silaha yake ya AK
47 'Machinegun' ya Kirusi na kuelekea
mbele.
Alipofika kwenye kona ya mbele, Willy
alimuona yule mtu mwingine akichungulia
dirishani, si mbali na aliposimama Willy.
Willy alikohoa kidogo na yule mtu
akageuka kuangalia. Alionyesha ishala ya
kumwita. Na yule, akijuwa fika kuwa
alikuwa mwenzake, alikuja haraka bila
hadhari. Alipokaribia, na kwa ajili ya giza
aliamini ni yule mwenzake, alianza
kusema, "Huko ndani naona mambo
yanaa...", kabla hajamalizia sentesi yake,
Willy alimrukia na kumpiga karate ya
shingo na kumuua palepale. Alianguka
chini kwa kishindo, na Willy alipomrukia
pale chini akammaliza. Baada ya Willy
kumkagua alimkuta na Bastola mbili,
moja yenye kiwambo cha sauti na
nyingine ya kawaida. Vilevile alimkuta na
kisu ambacho ukikibonyeza kinachomoka
na kutoka urefu wa nchi tisa. Kile kisu
kilikuwa silaha hatari sana ikitokea watu
wanapigana huku mmeshikana. Willy
alijihisi mtu mwenye bahati kwani silaha
kama hii kama ingebidi kumenyana bila
kujuwa kuwa mtu anayo anakuondoa
duniani haraka sana.
Sasa Willy alikimbia mbele kuangalia
kama kulikuwa na mtu mwingine, lakini
hakukuwa na kitu. Alipozunguka upande
mwingine tena hakuna kitu. Kisha
akachukua dakika chache kuhakikisha
kuwa hakuna hatari nyingine, na
alipohakikisha ndipo alipokwenda pale
dirishani alipokuwa anachungulia yule
mtu wa pili. Dirisha lile lilikuwa sebuleni
na lilikuwa wazi kidiogo. Pazia la dirisha
lilikuwa limerudishiwa kidogo kiasi
kwamba ungeweza kuona ndani na
kusikia maneno yote yaliyokuwa
yanazungumzwa.
Willy alishangazwa kuwaona wanaume
watatu na mwanamke mmoja ambaye
mara moja alimtambua kwani alikuwa
Bibiane. Hawa wanaume wote walikuwa
wametoa Bastola zao wakizungumza na
yule mwanamke. Wawili walikuwa
wamesimama na mmoja ameketi kwenye
kiti kilichokuwa kinaangaliana uso kwa
uso na alichoketi Bibiane.
"Nakwambia hivi, sisi tumetumwa kuja
kukuua na huyo huyo bwanako Jean.
Faida yako kwake imesisha sasa wewe ni
mzigo na yeye hataki kubeba mzigo", yule
aliyeketi alimweleza yule mwanamke huku
akionyesha kwenye sura yake maudhi na
usongo wa ajabu.
"Wewe unatania. Jean! hawezi kusema
hivyo. Kwa yote niliyomtendea na jinsi
tunavyopendana, Xavier sema jingine
kama wewe na Col. Gatabazi mmeamua
kuniua basi niuweni, msimsingizie Jean,
Jean ni wangu wa kufa na kuzikana",
Bibiane alijibu huku akionyesha sura ya
hofu maana aliwajuwa hawa jamaa ni
wauaji.
"Wanawake ni watu wa ajabu. Epa", yule
mtu ambaye Bibiane alimwita Xavier
alimwita mmoja wa wale waliosimama.
"Eee", yule mtu alijibu kwa woga vilevile.
"Siku zote nakwambia wanawake ni
wajinga, wewe huamini. Huyu anafikiri eti
Jean alikuwa anampenda, Jean alikuwa
anamtumia tu kama chombo. Kwanza
alikuwa anakutumia kwa mambo yake ya
kazi zake za kumwingizia pesa na pili,
anapokuwa huku Afrika alikuwa akijisaidia
kutimiza haja zake za kimwili; hata siku
moja hajawahi kukupenda. Pale tu wewe
na Col. Gatabazi mlipomweleza kuwa
wewe umemwona Willy Gamba na Willy
Gamba kukuona mara moja alijuwa Willy
Gamba atakutafuta na akikupata utatoa
siri, na ukitoa siri si ndiyo mambo yetu
yameisha! kwa hiyo, mara moja ametoa
hukumu ya kifo kwako na sisi tumekuja
kutekeleza amri. Kwa kweli ni uhalibifu
kwa kiumbe kizuri kama wewe kuuawa,
lakini wewe sasa ni mzigo kwetu nasi
hatubebi mzigo," Xavier alieleza.
Kwa maelezo haya Bibiane alijua kweli
hukumu imetoka kwa Jean na huo ndio
ulikuwa mwisho wake. Pamoja na ujuzi
wake wote wa kupigana hakuthubutu
mbele ya Xavier na wenzake kwani
aliwajuwa vizuri, walikuwa wabaya mara
kumi yake, na alijuwa kuwa hao
hawabembelezeki hivyo, alikata tamaa na
hasira zikampanda dhidi na Jean na
machozi yakaanza kumtoka.
"Ukionana naye mwambie atakufa kifo
kibaya sana. Nami naamini kuwa huyo
Willy Gamba anayemuogopa kweli ndiye
atakayenilipia kisasi", Bibiane alisema
huku akitetemeka kwa hasira.
Xavier alisimama na kurudisha kiti chake
nyuma. Bibiane naye akataka kusimama.
"Hapana, kaa hapohapo, usilete ujanja
hapa. Huyo Willy baada ya muda si mrefu
mtaonana ahera, nasikia huko watu
huonana tena. Hamtapishana zaidi ya
masaa mawili na yeye atakuwa
marehemu kama wewe".
Willy, ambaye alikuwa anasikia na kuona
yote haya akiwa dirishani, alipoangalia
usoni mwa yule aliyeitwa Epa, akajuwa
huyu ndiye akayemuua Bibiane. Aliangalia
nafasi aliyokuwa, akajuwa angeweza
kumpiga risasi Epa na yule mwingine,
lakini si Xavier. Kwa vyovyote Xavier
angemmaliza Bibiane, lakini hakukuwa na
njia. Hawa walikuwa ni wauaji wataalam,
tena huenda wa kulipwa. Hivyo, ilikuwa ni
afadhali kwake kupambana na mmoja
kuliko watatu na kwa maajabu ya Mungu
angeweza kumponyesha Bibiane ambaye
akili yake ilimweleza kuwa angeweza
kuwa mtu muhimu kwake.
Xavier alimkonyeza Epa. Yeye akavuta kiti
na kuanza kugeuka. Bibiane akafumba
macho, lakini kabla Epa hajafyatua risasi,
palepale Willy akiwa dirishani na mikono
yake yote ikiwa na Bastola, alimpiga
risasi ya kichwa Epa na yule mwingine
kifuani, na Bibiane akajirusha nyuma ya
kiti, Nkubana kama umeme akamimina
risasi dirishani. Lakini Willy alikuwa tayari
amejitupa chini na kujiviringisha na kisha
kuchukua AK 47 akamimina risasi kama
hamsini hivi kumtia kiwewe Nkubana.
Haya mambo yote yalitokea haraka sana
kama kufumba na kufumbua. Nkubana
alipoangalia akajuwa Epa na Karekezi
walikuwa wamekufa na hakujuwa
wamezungukwa na watu wangapi.
Alijirusha kwenye dirisha upande wa pili
ambalo lilikuwa la kioo kitupu na
kuangukia nje na kisha kujiviringisha
tena. Bibiane alichukua Bastola
iliyodondoka kutoka kwa Epa na kujaribu
kumpata Xavier lakini naye alijitosa nje
akaurukia ukuta wa mbele kwa nanma ya
ajabu na kuangukia uapnde wa
barabarani. Willy alipokimbia upande ule
wa pili ili kumuwahi Nkubana alikuwa
amechelewa, Xavier naye alikuwa ndio
anaishia baada ya kuruka ule ukuta.
Bibiane alipoinuka pale alipokuwa
amejitupa kumfuata Xaviar akajikuta
anaangalia kwenye mdomo wa AK 47.
"Tupa silaha yako mama, uko chini ya
ulinzi", Willy alimweleza Bibiane.
"Aheri ya Musa kuliko ya Firauni, Bila
shaka wewe ni Willy Gamba".
"Naamini wewe ni Bibiane".
Willy alimshika mkono Bibiane na bila
hata kumwelezana wanaelekea wapi,
wakakimbia kwa tahadhari kuwa kutoka
eneo hilo kabla askari na watu wengine
hawajafika kuangalia kilichotokea hapo
kwani mlio wa risasi za Ak 47 ulikuwa
umetikisa eneo hilo na kusikika vibaya
sana wakati huo wa usiku.

ITAENDELEA COL. NI AFISA WA JESHI
MWENYE CHEO CHA KANALI
 
duh mambo matamu sana aisee. technician msaidie kidi kudi kurusha mambo bwana. kuisoma kidogodogo inasumbua sana
 
Kwa kweli anatutesa nimekuwa kila muda ninaangalia kama ametupia du kweli utamu kolea.

nyarema wacha kabisa. kila nikitingwa na kazi, nikipata upenyo natupa macho jf. sasa ni utumwa. inabidi tuwasihi wengine waje wamsaidie huenda ametingwa na Kaiser.

willy gamba 1 na technian msaada wenu tafadhali
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…