U C H U
TAFUTA UKWELI II
Baada ya Musoke na Willy Gamba
kuondoka nyumbani kwa Temu, kila mtu
alitawanyika kuelekea kwenye hoteli yake.
Malisa aliyekuja kwenye mkutano huo
akitokea Dar es Salaam, alikuwa amefikia Hoteli ya Sabasaba. Alijulikana sana katika kundi la wasomi na kiserikali alikuwa mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania kuwepo Umoja
wa Afrika. Hata maafisa wa ngazi za juu
serikalini mara nyingi walitafuta ushauri kwake kila walipotaka kuzungumzia swala la Umoja wa Afrika.
Malisa alikuwa msomi na Mhadhili wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika
kitivo cha Sayansi ya Jamii. Mara hii
alipokuwa anakuja kwenye mkutano huu
Arusha, Afisa mmoja wa ngazi za juu
kabisa serikalini alimwomba amweleze
mazungumzo na makubaliano ya
mkutano wao, kwani serikali ilipenda
kujuwa mambo gani PAM inafikiria
kuhusu tatizo la Rwanda ili serikali nayo iweze kusaidia. Huyu Afisa wa serikali alimpa namba zake za simu za nyumbani na kumwomba ampigie baada tu ya mkutano.
Malisa alipofika Hotelini tu, ikawa yapata saa kumi na mbili na robo, alichukua ufunguo wa chumba chake mapokezi na kueleka chumbani. Alipofika chumbani alimwomba opereta wa simu pale hotelini ampatie simu ya Dar es Salaam na
kumpa namba.
"Subiri kidogo nitakuita", opereta
alimwambia.
"Haya asante, lakini nifanyie haraka
maana nataka kutoka nina miadi", Malisa
alimwomba opereta.
"Sasa hivi", aliambiwa.
Baada ya muda si mrefu simu iliita
chumbani kwa Malisa.
"Hallo".
"Namba yako ya Dar es Salaam inaita",
opereta alijibu.
"Haya asante", na akaunganishwa na
namba hiyo ya Dar es Salaam ambayo
iliendelea kuita.
"Hallo", mtu aliitikia baada ya muda
kidogo.
"Hapa ni Arusha, mzee yupo?", Malisa
aliuliza.
"Yupo, subiri".
Na baada ya muda kidogo akasikia,
"Hallo, nani mwenzangu?".
"Malisa hapa, shikamoo".
"Marahaba, habari ya huko?".
"Salama".
"Vipi mkutano".
"Tumemaliza".
"Ehee, hebu nipe maazimio yenu kwani
wazee huku wana shauku ya kusikia".
"Haya tega sikio nikueleze, mambo ni
mazuri sana", Malisa alijibu na
kumweleza mambo yote tokea mwanzo
mpaka mwisho.
"Hizo ni habari njema", yule afisa alijibu na kuendelea. "Willy Gamba ni kijana wetu na ni mtu shupavu. Kwa hakika ataifanikisha hiyo kazi. Na mimi
nitawaeleza wazee naamini wataridhika
na hatua mliyochukuwa. Mnajua sisi
kama serikali ni vigumu kuchukua hatua
yoyote dhidi ya nchi nyingine, lakini nyinyi
mkiwa umoja usio wa kiserikali mnaweza
kutusaidia sana kwa mambo kama haya.
Willy amefikia wapi?".
"Yuko hoteli ya Impala chumba namba
212. Huenda mzee si vizuri kumpigia simu
sasa hivi tu atashituka", Malisa alijibu.
"Na kweli, ingawa ni kijana wetu basi
tuache nyinyi muendelee nae. Asante
sana kwa kazi nzuri, na mwanzo mzuri,
watu wenye uchungu na Afrika kama
nyinyi ndio mtakaoisogeza Afrika mbele
katika kuleta maendeleo wakati tukielekea
katika karne ya sayansi na teknolojia.
Asante sana", yule afisa wa serikali alijibu
na kukata simu.
Bila kujua alichokuwa amefanya, Malisa
alifurahi sana kusikia sifa alizozitoa mtu
huyu mashuhuri katika serikali ya
Tanzania, kwa umoja wao. Minongono
mingi jijini Dar es Salaam ilikuwa ni
kwamba afisa huyu, ambaye watu wengi
walipenda kumwita kwa kifupi tu kama
'JKS' alitegemewa kugombea Urais baada
ya muda wa Rais wa sasa kumalizika.
Baada ya kukata simu ya Malisa tu, JKS
alipiga simu nyingine. Mara hii ilikuwa
simu ya masafa marefu, alipga Paris,
Ufaransa. Na mara moja ikaitikiwa.
"Hallo, naomba kuzungumza na Jean
Yves Francois".
"Subiri kidogo", alijibiwa.
"Hallo Francois, nani anaita?".
"Yaani huwezi kutambua sauti".
"Ah JKS. Ehe, nipe habari".
"Habari nzuri, sijui wewe huko?".
"Huku salama, tunasubiri tu kwa hamu
kusikia Umoja wa Mataifa mahakama ya
mauaji ya Rwanda ianze lini".
"Nasikia itaanza miezi minne ijayo huko
Arusha".
"Aha, majina?", Jean aliuliza.
"Majina ni yaleyale mpaka sasa".
"Kwa hiyo upande wa watu wetu hakuna
aliyeguswa?".
"Bado kabisa, ila kumetokea hali ambayo
inaweza kutuletea madhara".
"Hali gani?", Jean alihoji kwa shauku.
"Unakumbuka niliwahi kukueleza juu ya
chama kiitwacho kwa kifupi PAM?",
alimwuliza.
"Nakikumbuka na nimekitafiti vilevile
kujua msimamo wake. Wanachama wake
wanapigania umoja wa waafrika ili kuleta
haraka uhuru wa watu weusi dhidi ya
ukoloni mambo leo, ili watu weusi
waweze kujiamulia mambo yao wenyewe.
Na vilevile walikuwa mojawapo ya
makundi yaliyotoa shinikizo katika
mkutano wa Arusha ili mgogoro wa
Rwanda umalizike kwa njia ya amani.
Hata mkutano wa Algers, walikuwepo
wawakilishi wao, niliwaona maana
nilikuwepo. Haya sema watu kama hawa
wanaweza kuleta madhara gani?", Jean
aliuliza.
"Wanaweza kuleta madhara makubwa
sana", JKS alimjibu na kisha akaanza
kueleza kwa kirefu jinsi Malisa
alivyomweleza, na hatua ambazo tayari
zilikuwa zimechukuliwa.
"Huyu Willy Gamba ni hatari, anaweza
kuchambua kila kitu mpaka akafikia
ukweli unaweza kukugusa hata wewe",
JKS aliasa.
"Lililopo ni kuzuia asiende", Jean alijibu.
"Tutamzuia vipi na hayuko chini yetu?",
JKS aliuliza.
"Mbona huelewi, kwani maiti inasafiri?".
"Aha, sasa nimekuelewa, lakini hiyo ni
kazi kubwa", JKS alijibu.
"Hiyo ni kazi ndogo kabisa, si umeeleza
kuwa mtu wako ameeleza kuwa leo huyo
Willy Gamba analala Arusha. Hotel ya
Impala na chumba amekupa namba zake,
au sikukuelewa vizuri?", Jean aliuliza.
"Ni sawa kabisa, alinipa kila habari bila
kuelewa maana yake, na mimi
aliponieleza sikuelewa habari hiyo
itakuwa muhimu", JKS alijibu.
"Hiyo ilikuwa muhimu sana. Unakumbuka
kuwa tuna watu wetu kule Arusha, ambao
walikuwa wasafiri na Rais aliyeuawa,
lakini kwa ajili ya ujumbe wa Rais wa
Burundi hawakwenda na wapo kule
Arusha kama wageni wa serikali yako?",
Jean aliuliza katika hali ya kukumbusha.
"Hao! hata juzi nilizungumza na kiongozi
wao maana alikuwa ametokea Ngala
kwenda makambi ya wakimbizi wa
Rwanda kwa ajili ya kuwachukuwa vijana
kumi muhimu ambao waliingia Tanzania
baada ya kufunga kazi kule Rwanda.
Alikuwa anataka msaada wangu kwa ajili
ya makazi, nami nimewafanyia mpango
katika nyumba za mashirika ya serikali
pale Arusha na sasa wako salama
salimini", JKS alijibu.
"Hiyo ni kazi nzuri sana. Kwa kazi hiyo na
kwa habari ulizonipa leo, nitapeleka dola
za kimarekani elfu ishirini kwenye akaunti
yako kule Uswisi, kufika kesho jioni pesa
zitakuwa zimeingia. Na kama kazi hii ya
usiku ikifanikiwa dola zingine elfu ishirini
zitapelekwa", Jean alimweleza JKS.
"Asante sana, nami nitafanya kazi kwa
upande wangu. Nitampigia simu kiongozi
wao hapo Arusha, Bwana Phillipe
Habimana, atume vijana wawili waimalize
hiyo kazi. Umeshatoa agizo, na agizo lako
litatimizwa", JKS alijigamba.
"Oke, vizuri; unajuwa vijana wetu wana
ujuzi wa hali ya juu, na swala la kuua
kwako si swala tena la maana
wameishaua sana kiasi kwamba kuua
kwao sasa ni sawa na kunywa chai", Jean
alijibu huku akiangua kicheko cha kejeli.
"Tena sana, juzi tu kwenye kambi huko
Ngala wamemaliza kuua vikaragosi
vinavyojipendekeza kwenye serikali mpya,
kwa kuwashawishi wakimbizi waanze
kurudi ili ionekane serikali ya sasa
imeshaleta amani na usalama Rwanda ili
iweze kuungwa mkono na jumuia za
kimataifa. Ni baada tu ya kumaliza hiyo
kazi ndipo Phillipe alipokwenda
kuwachukuwa kwa msaada wangu. Hivyo,
nikiwaagiza leo, hakika huyu Willy
ajihesabu ni marehemu maana bado
wana mori kabisa", JKS alijibu.
"Haya basi, nipigie simu kesho, baada ya
kumaliza hiyo kazi. Na kama ukisikia
habari zingine zozote, fanya kama
kawaida na mimi nitafanya kama kawaida
yangu", Jean alijibu na kukata simu.
Jean na JKS walikuwa wanafahamiana
yapata miaka mitano sasa. Uhusiano wao
ulianza wakati JKS alipokuwa na wadhifa
wa kuamua juu ya ununuzi wa silaha
mbalimbali zilizokuwa zinahitajiwa na
serikali ya Tanzania. Jean Yvers Francois
alikuwa kijana bado yapata miaka
therathini na minane, na alikuwa tayari
mfanyabiashara maarufu sana duniani.
Alikuwa akifanya biashara ya kuuza
silaha katika nchi zinazoendelea, na
alimudu sana kupata biashara hiyo kwa
urahisi kwa vile watu wengi walisema
kuwa alikuwa mtoto wa kiongozi wa ngazi
za juu kabisa katika serikali ya Ufaransa.
Kwa kutumia wadhifa wa baba yake na
umaarufu aliokuwa nao baba yake katika
nchi zinazoendelea, kijana huyu hakukosa
biashara hii ya silaha na biashara
nyinginezo zilizokuwa zikipita mbele yake.
Lakini vilevile alinong'onwa kuwa, kijana
huyu alijua kuwazawadia waliompa
biashara, hasa viongozi wa ngazi za juu
katika nchi za Kiafrika. Kutokana na sifa
hii ya kutoa asilimia kumi na zawadi
zingine, kijana huyu alikuwa akitafutwa na
biashara badala ya yeye kuzitafuta hata
ikasemekana kwamba viongozi
fulanifulani wa nchi za Kiafrika iliwabidi
wazungumze naye kwanza kabla
hawajatoa maamuzi yoyote muhimu ya
kibiashara.
Kwa hiyo, wakati JKS alipoagizwa na
serikali ya Tanzania kutoa zabuni ya kisiri
kwa makampuni yanayotengeneza silaha,
mara moja alimtafuta Jean, maana
viongozi wenzake walishawahi
kumweleza kama angetaka kunufaika na
wenzake pia wanufaike basi Jean ndiye
alikuwa mtu wa kuwasiliana naye. Ingawa
wakati huo walikuwa hawafahamiani,
lakini JKS alikuwa tayari ana anuani ya
Jean kutoka kwa rafiki zake. Hivyo
hakusita, akawasiliana naye. Ni baada ya
kuwasiliana naye na kufanya biashara ya
kwanza ndipo urafiki wa karibu sana
ulipoanza kati yao.
Kwa vile Ufaransa ilikuwa na uhusiano wa
karibu sana wa kiserikali na serikali ya Rwanda, Jean alijikuta ana uhusiano wa karibu sana na uongozi wa serikali ya nchi hiyo kuliko ilivyokuwa serikali za nchi nyingine za Kiafrika alizokuwa
akifanya nazo biashara. Inasemekana
kuwa, kwa njia moja ama nyingine, Jean
ndiye aliyekuwa mshauri mkuu wa
uongozi huo na hakuna uamuzi wowote
uliofanyika bila yeye kuhusishwa.
Kiuchumi, Jean alimiliki njia zote muhimu za uchumi wa Rwanda kwani uongozi wa serikali ya Rwanda ulimpa uwezo wa kufanya biashara yoyote aliyoitaka nchini humo, na uongozi huo ulinufaika kwa kujilimbikizia mali, na kumwachia anyonye jasho la wananchi wa Rwanda kwa kununua mazao yao yote kwa bei rahisi na kuwauzia bidhaa kwa bei ghali.Kwa jinsi hii Rwanda ilimtajirisha Jean na viongozi wa serikali isivyo kifani. Na ndio
sababu wakati wa mkutano wa
kusuruhisha pande zote za mgogoro wa
Rwanda mjini Arusha, Jean alikuwepo.
Inasemekana alimtumia sana JKS
kujaribu kuipotosha serikali ya Tanzania ili isione ukweli wa mambo ulivyokuwa Rwanda kutokana na urafiki wao wa karibu uliotokana na kupeana bakshishi. Baada ya Jean kukata simu, JKS alitafuta kitabu chake cha simu na kutafuta simu ya Phillipe Habimana kule Arusha. Baada ya kuipata alimpigia simu.
"Hallo Habimana".
"Habari za leo", JKS alijibu na mara moja Phillipe akaitambua sauti.
"Nzuri mzee, shikamoo".
"Marahaba, sikiliza kwa makini, nina kazi nataka vijana wako wakaifanye usiku huu, tafadhali sitaki makosa ya namna yoyote yafanyike kwani yanaweza kuleta madhara kwa suala lenu zima.
Nimeshazungumza na Jean.
JKS alitoa maagizo yake kwa kirefu na
akamalizia.
"Narudia tena, mtu huyu ni hatari sana;
vijana wako wasifanye mzaha wakafikiria
ni mtu wa kawaida, si wa kawaida,
hadhari yote ichukuliwe".
"Hamna matatizo mzee, hesabu kazi
imekwisha, tuonane kwenye msiba wa
Willy Gamba", Phillipe alijigamba.
ITAENDELEA