UCHU
NGUVU YA RUSHWA--III
Simu ilipoita Jean alikuwa amelala. JKS
alikuwa amemweleza kuwa vijana
walikuwa wamefika salama na kazi ya
kumsaka na kumuua Willy Gamba ilikuwa
ifanyike usiku ule. Alikuwa amefikiria jinsi
Bibiane angeshangaa sana baada ya
kuelezwa kuwa Jean ndiye aliyetoa amri
ya yeye kumuua. Jean alikuwa mtu
aliyefurahia uovu, alikuwa mtu katili
afadhali ya mnyama. Alifurahi kusikia mtu
akipata maumivu, na hapo ndipo roho
yake ilipopata faraja. Pamoja na miaka
yoye sita aliyokaa na Bibiane, utafikiri
walikuwa mtu na mke wake, yaani mume
na mke, bado alipomweleza Col. Gatabazi
kuwa lazima Bibiane auawe moyoni
mwake hakusikia masikitiko.
Kilichomfurahisha na kumridhisha ilikuwa
ni pesa na nguvu ya pesa, na si mapenzi.
Jean aliabudu pesa kwani aliamini kuwa
pesa ndizo zilizompatia uwezo alionao
duniani.
Kwa kutumia pesa, Jean aliweza
kuwakamata wakuu wa nchi nyingi
duniani, hasa katika Afrika na Asia, lakini
vilevile viongozi wa ngazi za juu katika
serikali za nchi za Ulaya. Alipata kila
alichokitaka kwa kutumia pesa. Hivyo,
simu ilipolia alijua analetewa habari
njema za kuuawa kwa Bibiane na Willy
Gamba maana alikuwa amesema alikuwa
amesema wakishauawa aelezwe. Kila
alipopewa taarifa ya kuuawa kwa mtu
alipata faraja ndani ya moyo wake, Ndio
sababu maelfu ya Watutsi walipouawa
alisikia raha isiyo kifani. Hakika mtu huyu
alikuwa mgonjwa, tena mgonjwa sana!.
"Jean", aliitikia kwenye simu.
"Col. Gatabazi hapa".
"Sema Col. Gatabazi".
"Kazi imeharibika".
"Nini?".
"Kazi imeharibika. Vijana wote
wameuawa. Bibiane yuko hai na
ameokolewa na Willy Gamba. mimi na
Nkubana tunaondoka kwenda Kibunda,
hatuna muda maana wakati wowote
wataanza kutusaka, afadhari tuyaandae
majeshi yetu tayari kwa vita", Col.
Gatabazi alimwambia Jean.
"Ilikuwaje", Jean aliuliza kwa sauti ya
kukata tamaa. Col. Gatabazi alimweleza
kwa ufupi kama Nkubazi alivyomweleza.
"Basi tuonane kesho Goma, saa tisa
mchana nitakuwa huko, natarajiwa kuja
na ndege yangu, lakini nitampitia rafiki
yetu Kinshasa", Jean alieleza na kukata
simu kabla hata Col. Gatabazi hajajibu
kitu.
Jean alipokata simu ya Col. Gatabazi,
alitumia muda huo kupiga simu Zambia,
Zaire, Afrika Kusini, Angola, Kenya na
kumalizia Tanzania.
"Umenipata JKS?", Jean alimuuliza JKS
baada ya kumweleza yote yaliyotokea na
maelekezo mengine huku JKS akipatwa
na shinikizo la damu.
"Nimekupata", JKS alijibu kwa sauti ya
kutetemeka.
....ITAENDELEA....