SIRI
season 3
Episode 20
Mtunzi. Patrick CK
HAIFA – ISRAEL
Saa nane kasoro dakika
ishirini kwa saa za
Israel,mlango wa chumba
alimolazwa Edger kaka
ulifunguliwa na watu watano
wakaingia wakiongozwa na
mmoja aliyevaa koti la
daktari,wawili wakabaki
mlangoni.Edger alikuwa
amelala fofofo yule jamaa
mwenye koti la daktari
akamuamsha.
“Edger amka uzungumze na
wageni wako” akasema yule
jamaa aliyevaa koti la kidaktari.Edger akafumbua
macho na kukuta kuna watu
mle chumbani akainuka na
kukaa akafikicha macho ili
aweze kuona vizuri. Miongoni
mwa watu wale alikuwemo
mwanamama aliyejitanda
ushungi kichwani.
Baada ya Edger kuinuka na
kukaa watu watatu wakatoka
mle chumbani na kuwaacha
watu wawili tu.Yule
mwanamama akavua ule
ushungi aliokuwa amejitanda
na uso wa Edger ukachanua
kwa tabasamu pana “Mama ! akasema Edger na
kuinuka akaenda kumkumbatia
mama yake
“Edger ! Akasema
mwanamama yule ambaye ni
Habiba Jawad.Walikumbatiana
kwa dakika mbili halafu Edger
akapeana mkono na mtu
aliyekuwa pembenmi
“Sayid Omar,nafurahi
kukuona” akasema Edger
“Pole sana Edger” akasema
Sayid.Edger akawakaribisha
wageni wake katika sofa
lililokuwamo mle chumbani “Mama nimefurahi sana
kukuona.Ahsante kwa kuja
kunitembelea” akasema Edger
“Hata mimi nimefurahi sana
kukuona Edger.Imenilazimu
kufanya kila niwezalo kuja
kukuona
mwanangu.Nimeumizwa sana
na hawa washenzi waliotaka
kuyaondoa maisha
yako.Ninakuahidi kwamba wote
walioshiriki katika jaribio hili la
kukuua tutawasaka na hakuna
atakayebaki salama.Najua ni
mtandao mkubwa wa maadui
zako ambao hawalali wakipanga mipango ya
kukuangamiza” akasema
Habiba Jawad
“Jaribio lao
limeshindwa.Hali yangu ni
nzuri kwa sasa” akasema Edger
“Edger napenda pia
kukuhakikishia kwamba kwa
sasa kuwa na amani kwani uko
salama.Kama alivyosema
Habiba mtandao wa maadui
zako ni mkubwa na walituma
watu wao kukufuata hadi huku
kutafuta namna ya
kukumaliza.Watu waliotumwa
kukufuatilia walitega vifaa humu chumbani kwako bila
wewe kujua.Walitega kamera za
siri na walikuwa wanaangalia
kila unachokifanya,vilitegwa
vifaa vingine pia ambavyo
viliweza kunasa mawasiliano
yako yote uliyokuwa
unayafanya na kuwatumia
wakuu wao.Ni mtandao
mkubwa uliowahusisha pia
watu wakubwa serikalini lakini
taarifa nzuri ni kwamba tayari
tumekwisha ubaini mtandao
huo na tayari hatua za haraka za
kuuondoa zimeanza na hivi
tuongeavyo vijana wako kazini wakiendelea na kazi ya
kuusafisha na hatabaki mtu
yeyote tutahakikisha wote
tumewasafisha” akasema Sayid
Omar
“Nashukuru sana Sayid kwa
kuweza kulitambua hilo kwa
haraka kwani mimi sikuwa na
mawazo kama wangeweza
kunifuata hadi huku.Unaweza
ukanitajia baadhi ya watu
waliomo katika mtandao huo
niwafahamu? akauliza Edger
“Hapana Edger sintaweza
kukutajia kwa sasa lakini
ninachoweza kukushauri ni kuwa makini sana.Kuanzia sasa
usimuamini mtu yeyote
yule.Yule unayemuamini ndiye
huyo atakayekuingiza kwenye
shimo la moto hivyo jaribu
kuchagua watu wachache wa
kuwaamini na kuwaweka
karibu.Mipango yako
usimueleze mtu ambaye hauna
imani naye.Umenielewa Edger?
Akauliza Sayid
“Nimekuelewa Sayid”
akajibu Edger
“Edger” akaita Habiba
“Naam mama” “Hiki kilichotokea kimezidi
kutupa sababu ya wewe
kugombea urais.Hadi sasa
tayari umekwisha jenga maadui
wengi na mtandao wao unazidi
kutanuka na kila uchao
wanapanga
kukuangamiza.Wakati umefika
kwa wewe kugombea
urais.Hatuna tena muda wa
kusubiri kwani tunavyoendelea
kuvuta muda na kusubiri zaidi
maadui zako wanaendelea
kujipanga zaidi namna ya
kukuangamiza.Edger
tumekuandaa kwa muda mrefu kwa ajili ya nafasi hiyo na
mpaka hapa tulipofika
maandalizi yetu yanakwenda
vizuri.Tayari umekwisha
tengeneza wafuasi wengi
ambao ndio mtaji mkubwa kwa
mwanasiasa kushinda
chaguzi.Nguvu yako ni kubwa
na unazidi kuwapa hofu maadui
zako.Kwa upande Fulani
ninawashukuru hawa
waliofanya jaribio hili la kukuua
kwani wametufanya na sisi
macho yetu yafumbuke zaidi na
kung’amua kwamba wakati
umefika.Ninashukuru Edger kwa kukubali kugombea urais
kwani ile mipango yetu yote
inakwenda kutimia” akasema
Habiba
“Mama sikuwa nimepanga
kugombea urais kwa wakati
huu,mipango yangu ilikuwa
nigombee baada ya miaka
mitano ijayo lakini kwa hili
lililojitokeza na kwa ushauri
nilioupata kutoka kwa Sayid
nimeamua kugombea urais
katika uchaguzi mkuu ujao.Uko
sahihi kwamba tayari
nimekuwa na maadui wengi na
wanaongezeka kila uchao na njia pekee ya kuweza
kuwashinda maadui zangu ni
kwa kuwa rais.Nina uhakika
mkubwa wa kushinda uchaguzi
kutokana na mtaji mkubwa wa
wafuasi nilio nao.Tayari
nimejenga jina kubwa na
wananchi wengi wananiamini
na nina hakika nitashinda kwa
ushindi mkubwa. Lakini
…”akanyamaza kidogo
“Lakini nini Edger?akauliza
Habiba
“Nimeamua nitagombea
kupitia chama cha upinzani cha
Democratic ambacho tayari mazungumzo yamekwisha anza
ili niweze kujiunga nao”
“Hapana Edger” akasema
Habiba
“Hautagombea urais kupitia
chama cha upinzani.Utagombea
urais kupitia chama
chako.Kuhama chama
kunaweza kuzusha maswali
mengi,utaonekana u mroho wa
madaraka.Kampeni za rais ni
gharama kubwa hivyo basi kwa
vyama vidogo kama hicho
unachotaka kuhamia lazima
kitachunguzwa sana namna
kilivyoweza kugharamia kampeni na wanaweza
wakagundua mambo ambayo
hatutaki yajulikane.Ukiwa ndani
ya chama chako hakuna
atakayeweza kukuhisi chochote
kwani kampeni zako
zitagharamiwa na chama chako
ambacho ni kikubwa na kina
rasilimali za kutosha hivyo basi
utaendelea kugombea urais
lakini kupitia chama
chako”akasema Habiba Jawad
“Mama hayo uyasemayo
ninayafahamu na hata mimi
ningependa sana kugombea
urais kupitia chama changu lakini kuna tatizo ndiyo maana
nikafikiria kuhama chama”
“Kuna tatizo gani
Edger?akauliza Sayid Omar
“Tatizo ni kwamba nguvu
yangu kubwa iko nje ya
chama.Ndani ya chama sina
nguvu kubwa na sina uhakika
kama ninaweza kuteuliwa na
chama kugombea.Kuna
mchuano mkubwa ndani ya
chama vigogo wenye nguvu
wakichuana nani achaguliwe
kupeperusha bendera ya chama
katika uchaguzi mkuu
ujao.Kama nguvu yangu ingekuwa kubwa chamani
ningekubaliana nawe mama
lakini nguvu yangu kubwa iko
nje ya chama ndiyo maana
nikafikiria kuhama chama na
kujiunga na chama kingine ili
niweze kutumia nguvu yangu ya
nje kushinda urais.Nikiwa ndani
ya chama changu
ninawahakikishia kwamba
sintaweza kufika kokote”
akasema Edger
“Edger wasi wasi wangu ni
kwamba kuhama chama
kutakupunguzia mvuto.Ushauri
wangu ni kwamba endelea kubaki ndani ya chama chako
ila unachohitaji ni kuunda timu
yenye nguvu ambayo
itakuwezesha wewe uweze
kuteuliwa ndani ya chama
kupeperusha bendera katika
uchaguzi mkuu ujao wa
rais.Tutaunganisha baadhi ya
vigogo wenye ushawishi
chamani na watakubali kwani
kinachoongea ni fedha.Tuachie
sisi suala hilo tutalishughulikia
lakini achana kabisa na
mipango yoyote na vyama
pinzani.Utagombea urais kupitia chama chako na
utashinda” akasema Habiba
“Mama nimeamua
kugombea urais kupitia chama
cha upinzani kwa sababu mimi
ndiye niliye ndani ya chama na
ninafahamu kinachoendelea
ninafahamu fitina zilizopo
ndani ya chama hivyo naombeni
mkubaliane nami nijiunge na
chama cha upinzani.Msihofu
kitu kwani ninao mtaji mkubwa
wa wafuasi na kokote
nitakakoenda watanifuata.Wote
wanafahamu namna
ninavyoikososa serikali na kupambana na mafisadi ndani
ya chama changu na
wananiunga mkono.Kitendo cha
mimi kuwekewa sumu pia
kitakuwa ni kigezo kikubwa
sana cha mimi kuhama chama
na nitakapowaeleza wananchi
wataniamini” akasema
Edger.Habiba na Sayid
wakatazamana kwa muda kisha
Habiba akasema
“Tunakwenda kulijadili
suala hili tuone ipi itakuwa njia
bora zaidi ya wewe kugombea
urais aidha ukiwa ndani ya
chama chako au ukiwa nje ya chama.Jibu tutakalopata
tutakujulisha.Edger nimefurahi
nimekuona na yawezekana
hatutaweza kuonana tena
kwani usalama wetu ni mdogo
sana hapa Israel lakini
tutaendelea kuwasiliana kama
kawaida” akasema Habiba na
kumkumbatia Edger
wakaagana.
“Sayid ameniambia
kwamba walitumwa kuja
kunichunguza ni watu wangu
wa karibu,ni akina nani
hao?Watu nilio nao karibu hapa
hospitali ni Olivia na Judy je kuna mmojakati yao ametumwa
kunichunguza?Nahisi labda
anaweza kuwa Judy kwani
sidhani kama Olivia anaweza
akafanya hivyo.Yeye ndiye
aliyenileta hapana kuokoa
maisha yangu.Nilishuhudia
vifaa vile vilivyotolewa humu
chumbani vilivyotegwa
kunifuatilia nina hofu kama
wameweza kunasa mawasiliano
yangu na Sayid wanaweza
wakaniharibia kabisa mipango
yangu yote ya kuwania
urais.Wakigundua kwamba
Sayid ni mfadhili mkubwa wa kikundi cha IS jina langu
litachafuka mno na kitakuwa ni
kifo changu cha kisiasa.Sitaki
siri yangu ijulikane hadi hapo
lengo langu litakapotimia.Sayid
amenihakikishia kwamba
wanalifuatilia suala hili na
mtandao wote
wataufagia.wanatakjiwa
wafanye haraka sana kuufagia
mtandao huu kabla hawajaleta
madhara” Kichwa cha Edger
kilikuwa na mawazo mengi
sana baada ya Habiba na Sayid
kuondoka pale hospitali TEL AVIV – ISRAEL
Saa tatu za asubuhi katika
chumba kimoja ndani ya jengo
la makao makuu ya shirika la
ujasusi la Israel Mossad, watu
wanne walikuwa ndani ya
chumba cha mikutano
wanamsubiri mkurugenzi mkuu
wa shirika hilo kwa ajili ya
kikao muhimu.Mkurugenzi
mkuu ambaye alikuwa njiani
akitokea nyumbani kwake
aliwasili ndani ya muda mfupi
baada ya kupewa taarifa
kwamba anahitajika kwa jambo muhimu la usalama wa
taifa.Yitzhak Zamir mkurugenzi
mkuu wa Mossad alipowasili
katika chumba kile akaomba
wajielekeze moja kwa moja
katika kile kilichowakutanisha
pale kwani alikuwa na
mazungumzo na waziri mkuu
saa tano asubuhi.
“Mkurugenzi tumelazimika
kukuita hapa asubuhi hii
kuhusiana na suala muhimu”
akasema David Shiloah na
kumfanyia ishara Yair aendelee
kutoa maelezo “Siku chache zilizopita rais
wa Tanzania alimpigia simu
waziri mkuu na kuomba
mgonjwa wake ambaye ni
mbunge wa bunge la jamhuri ya
muungano wa Tanzania
aliyekuwa mahututi,aruhusiwe
kuingia hapa nchini kupata
matibabu.Kutokana na
mahusiano mazuri kati ya
Tanzania na Israel waziri mkuu
alitoa maelekezo kwa mgonjwa
huyo kuruhusiwa kuingia nchini
kutibiwa na alipoletwa hapa
nchini alipelekwa Haifa katika
hospitali ya Rambam.Wakati wakimpatia matibabu
madaktari waligundua kwamba
mbunge alipewa sumu.” Yair
akanyamaza kidogo halafu
akaendelea
“Dr Olivia Themba kutoka
hospitali kuu ya moyo nchini
Tanzania ambaye ndiye
aliyeambatana na mgonjwa
huyo alimjulisha spika wa
bunge la jamhuri ya muungano
wa Tanzania suala hilo la Edger
kuwekewa sumu na spika
akamjulisha waziri
mkuu.Inahisiwa sababu ya
kutaka kuuawa kwa mbunge huyo ni chuki za kisiasa kwani
amekuwa ni mahiri sana katika
kufichua ufisadi unaofanywa
nchini mwake hasa na watu
wakubwa serikalini hivyo
amejijengea maadui
wengi.Baada ya kupata taarifa
kuwa Edger aliwekewa sumu
waziri mkuu wa Tanzania
aliamua kuchukua hatua za
kumlinda kwa kuhofia kwamba
watu waliotaka kumuua
wangeweza kumfuata hata kule
Israel kummalizia.Nina urafiki
na waziri mkuu wa
Tanzania,aliwahi kunisaidia kupata hifadhi Tanzania kwa
muda wa mwaka mmoja
nilipokuwa nawafuatilia wale
magaidi waliokwenda kujificha
Zanzibar.Kutokana na urafii
wetu alinipigia simu akaniomba
nimsaidie mmoja wa vijana
wake ambaye atamtuma hapa
Israel kumlinda
Edger.Niliwasilisha suala hili
kwa kiongozi wangu David
nikamueleza na yeye akanipa
ruhusa na kufanya
hivyo.Nilifanya maandalizi na
Dickson alipokuja hapa
nilimpeleka katika ile hospitali akiwa kama mgonjwa kutokea
nchini Zimbabwe.Dickson
aliweka kamera za siri katika
chumba cha Edger na aliweza
kuona kila kinachofanyika
ndani ya chumba kile.Usiku wa
kuamkia jana watu wawili
mwanamke na mwanaume
waliingia ndani ya chumba cha
Edger lakini hawakuweza
kuongea naye kwa kuwa
alikuwa amelala fofofo.Dick
alinitumia picha za mwanamke
yule akinitaka nimsaidie
kumtambua na nilipomuona tu
nilistuka baada ya kumuona mwanamke yule ni Habiba
Jawad”
“Habiba Jawad? Yitzhak
akastuka
“Ndiyo mkurugenzi”
akajibu Yair
“Mna uhakika ni
mwenyewe Habiba
Jawad?akauliza Yitzhak.
“Ndiyo mkurugenzi.Tuna
uhakika ni mwenyewe”
akasema Yair na kutoa picha
kutoka katika faili lililokuwa
mbele yake akampatia
mkurugenzi wake akazipitia
“Endelea” akasema Yitzhak “Aliposhindwa kuzungumza
na Edger,Habiba alimuachia
ujumbe uliokuwa katika
bahasha.Dick aliichukua
bahasha ile akakuta kuna
namba za simu ambazo Edger
alielekezwa apige.Alinipigia
simu na usiku ule ule bila
kupoteza muda nilifika pale
hospitali.Tuliamua kupiga
namba zile za simu Habiba
alizomuachia Edger ili
kufahamu mahala
alipo.Nilifanikiwa kupata simu
ambayo ingetusaidia kufahamu
mahala aliko Habiba na Dick akaitumia kupiga zile namba
alizoacha Habiba lakini baada
ya simu kupokelewa Habiba
aligundua kwamba yule hakuwa
Edger akakata simu haraka
hivyo hatukuweza kujua mahala
alipo.Hakukata tamaa Dick
aligundua kwamba Edger
alikuwa anatumia kompyuta
yake kuwasiliana na watu wake
muhimu kwa kutumia mtandao
wa Skype hivyo siku iliyofuata
Dick akafanikiwa kuipata
kompyuta ya Edger na
kugundua kwamba amekuwa
na mawasiliano na Sayid Omar” “Sayid Omar bin
Abdullah?akauliza Yitzhak
“Ndiyo mkurugenzi.Edger
amekuwa na mawasiliano
naye”akajibui Yair
“Sasa nimepata picha
nzuri.Kwa mujibu wa taarifa za
uchunguzi tulizonazo ni
kwamba Habiba na Sayid ni
washirika wakubwa na Sayid
anatumiwa na Habiba katika
kufadhili kikundi cha IS
ambacho kinaendeleza harakati
zake sehemu mbalimbali
duniani.Kama huyo Edger ana
mawasiliano na Sayid na akatembelewa hospitali na
Habiba hii inatuhakikishia
kwamba huyo mbunge ana
mahusiano ya karibu sana na
watu hao.Inashangaza sana kwa
mbunge huyo kuwa na
mahusiano na watu hawa
hatari.Serikali ya Tanzania
wanafahamau chochote
kuhusiana na suala hili? Idara
ya ujasusi Tanzania
wanafahamu kama mmoja wa
wabunge wa nchi yao ana
mahusiano na watu
wanaofadhili mtandao wa
IS?akauliza Yitzhak “Hapo ndipo penye tatizo
mkurugenzi.Dick alitumwa na
waziri mkuu wa Tanzania kuja
kumlinda Edger kwa siri na
suala hili limejitokeza wakati
akiendelea kutimiza jukumu
lake la kumlinda Edger na
hajamueleza mtu yeyote nchini
Tanzania.Nilimshauri
asimjulishe mtu yeyote bali
tuendelee kufanya uchunguzi
na kufahamu kinachoendelea
kati ya Edger na hawa watu wa
IS.Kwa bahati mbaya sana kabla
hatujafika mbali na uchunguzi
wetu Edger amefariki dunia” “Amefariki? Yitzhak
akashangaa
“Ndiyo amefariki dunia jana
usiku na inadaiwa kwamba
chanzo cha kifo chake ni
kupanda ghafla kwa shinikizo la
damu lakini hizo ni sababu tu
naamini kabisa Dick ameuawa
na IS.Nina uhakika waligundua
kwamba alikuwa anamfuatilia
Edger na
wakamuua.Kulithibitisha hilo
waziri mkuu wa jamhuri ya
muungano wa Tanzania ambaye
ndiye aliyemtuma Dick kuja
hapa Israel kumlinda Edger naye pia ameuawa asubuhi ya
leo katika mlipuko wa bomu
lililotegwa nje ya ofisi
yake.Naamini kabisa kwamba IS
ndio waliofanya shambulio hilo
kwa ajili ya kuficha siri ya Edger
isigundulike.Waligundua
kwamba Edger amekuwa na
mawasiliano na waziri mkuu
hivyo wakaamini kwamba
lazima atakuwa amemueleza
kuhusiana na Edger kukutana
na Habiba hivyo wakalazimika
kuwaua wote” akasema Yair
“Habiba Jawad amekuwa
akimtumia Sayid Omar kufadhili kikundi cha IS
ambacho kimekuwa
kinaendesha mauaji ya watu
ndani ya ardhi ya
Israel.Nimeshangazwa na
kitendo cha watu hawa wawili
kuingia nchini mwetu bila ya
mamlaka kufahamu na kuwatia
nguvuni.Nalazimika kuamini
kwamba kuna watu ndani ya
serikali ambao wamewasaidia
watu hawa kuingia humu nchini
na hadi kufika hospitali
kuonana na Edger.Uchunguzi
mkali sana unatakiwa kufanywa
katika hili na kuwabaini hawa watu wanaoshirikiana na IS”
akasema Yitzhak kwa ukali
“Kitendo cha huyu mbunge
kukutana na watu hawa wawili
kinadhihirisha wazi kwamba
wana mahusiano ya karibu na
ninahisi kwamba yawezekana
naye akawa ni mwanachama wa
kikundi cha IS kwani kikundi
hiki kina wanachama wengi na
wamekuwa na wakipandikiza
watu wao ndani ya serikali
mbali mbali na ninaamini hata
ndani ya serikali yetu wana
watu wao ndiyo maana watu
hawa wawili Habiba na Sayid wameweza kuingia nchini Israel
bila mamlaka kuwa na
taarifa.Ninashawishika kuamini
kwamba huyo mbunge naye ni
mmoja wa watu
walipandikizwa na IS ndani ya
serikali ya Tanzania.Nini
mnafikiria kukifanya?akauliza
Yitzhak
“Tumelifikisha kwako suala
hili tunasubiri maelekezo yako
mkurugeni” akasema
David.Yitzhak akatoa sigara
akawasha na kuvuta mikupuo
kadhaa halafu akasema “Tunamuhitaji sana
Edger.Tumekuwa tunawatafuta
Sayid na Habiba kwa muda
mrefu na huyu anaonekana ni
mtu wao wa karibu sana hadi
wamehatarisha usalama wao
kwa kuingia hapa Israel kuja
kumtembelea hospitali.Hiki
walichokifanya
kinatuhakikishia kwamba huyu
ni mtu wao wa muhimu sana
hivyo basi tukimpata
atatusaidia kwanza kufahamu
walipo Habiba na sayid na pili
kufahamu mambo mengi ya IS
pamoja na mipango yao mbali mbali.Tuanze mikakati ya
kuhakikisha kwamba
tunampata huyu kijana.Yair
utasimamia hili zoezi.Weka
watu pale hospitali ambao
watafuatilia kwa karibu kila
kinachoendelea kwa huyu
jamaa.Chunguzeni watu
anaokutana nao na kama
akionekana Habiba au mtu
mwingine yeyote
watakayemtilia shaka basi
wakujulishe haraka sana”
akasema Yitzhak na kumgeukia
David “David nataka iandaliwe
operesheni maalum ya kumpata
Edger.Nataka ufanyike
uchunguzi kujua lini Edger
atarejea nyumbani
Tanzania.Operesheni kubwa
iandaliwe ya kwenda
kumchukua Edger nchini
Tanzania muda mfupi
atakapowasili akitokea huku
Israel.Nasema ni operesheni
nzito kwa sababu nataka
Tanzania na dunia nzima wajue
kwamba Edger amefariki
dunia.Huyu ni mtu muhimu
sana kwetu na serikali ya
Tanzania haipaswi kufahamu
chochote kuhusu operesheni hii
kubwa tunayokwenda
kuifanya.Uwezo wa kufanya
operesheni kubwa kama hiyo
tunao kwani shirika letu la
ujasusi ni shirika kubwa na
lenye uwezo mkubwa kabisa wa
kufanya chochote katika nchi
yoyote duniani. Tumekwisha
fanya operesheni kubwa katika
nchi mbali mbali duniani na
hatujawahi kushindwa hivyo
basi hatuwezi kushindwa pia
katika operesheni hii.Hii ni
operesheni muhimu sana na ipewe uzito
mkubwa.Ninakwenda kuonana
na waziri mkuu nitazungumza
naye kuhusu suala hili ili atupe
kibali chake na nitakaporejea
nataka nikute mpango maalum
umekwisha andaliwa namna
operesheni hii
itakavyoendeshwa” akasema
Yitzhak na kuwaachia jukumu
lile David na Yair kuandaa
operesheni ile ya kumpata
Edger