SEHEMU YA KUMI NA TATU
GIZA LA USIKU
-------------
Walichokisikia hakikufanana kabisa na walichokitarajia asilani.
Ni huyuhuyu kijana, mdogo kiumbo ambaye wasingeshindwa kumdhibiti kama tu wangepata nafasi hiyo.
Lakini walikuwa tayari wamezidiwa hatua moja mbele, akawazidi maarifa na akili.
Wako chini matumbo yao yakiikumbatia ardhi na mikono yao wote ikiwa ndani ya pingu moja ya chuma kila mmoja.
"Kukamatwa sio kuhukumiwa. La hasha! Hivi ni vitu viwili tofauti kabisa." Kwa sauti yake ileile ndogo na ya utaratibu yule kijana aliyejitambulisha kwa majina ya Tito Ngeze akawanong'oneza.
"Ninachokitaka kwenu ni taarifa tu! Mnieleze nyinyi ni kina nani na ni nani aliyewatuma kumtafuta huyu kijana kwenye mitaa ya mji huu!" Akaweka kituo na kuruhusu upande wa kujitetea utoe sera zake.
Wakiwa bado hawaamini kama ni wao wako chini na wako mbele ya askari huyu wa polisi wakapiga kimya kwa sekunde kadhaa kisha wakajikusanya kwa kubebana na wakajikalisha vyema pale mavumbini. Matundu mawili ya pingu moja yakifurahia kuimiliki mikono yao kila mmoja kwenye tundu lake. Wamebanwa kwenye kona ya vichochoro wasivyoweza kuvifahamu. Wakagundua kuwa wamekamatika haswa!
"Tusikilize afande!" Sanga akawa wa kwanza kutoa sauti yake.
"Kama wenzetu wakitukuta hivi ndani ya hii pingu. Sidhani kama utaliona jua la kesho asubuhi!" Akaweka pumziko kwa kumtazama Tito Ngeze, akiyapima maneno yake kama ni kweli yamemuingia.
"Naelewa...naelewa. Na ninajua kuwa niko na watu hatariahi sana mbele yangu. Na mimi hata sihitaji tufikishane mbali." Akawajibu na kuchuchumaa mbele yao akiwa umbali wa mita moja na nusu kutoka kwao.
"Kwanza naombeni picha yake huyo mlioagizwa mumtafute!"
Bila kusita Kassim akajipekua na kuibuka na picha ndogo aliyoirusha ardhini kwa jeuri. Tito akaiokota na kuitazama kwa sekunde kumi kwa umakini mkubwa.
"Siku nzima ya leo nimekuwa kwenye mitaa takribani minne ya mji huu. Na wamepita vijana ambao wanaisambaza hii picha kwa kuulizia taarifa juu ya huyu mtu!" Akaweka pumziko kisha akaendelea,
"Nimejaribu kufanya utafiti nikagundua kuwa wao sio askari polisi wa mji huu. Na wanatumia kivuli cha kuwa askari ili tu wapate kila taarifa wanayohiitaji kwa haraka!
Jambo zuri zaidi ni kwamba taarifa hii bado ni mbichi sana na haijafika kituoni."
Alipofika hapa akaiweka picha ile kwenye mfuko wa sweta lake jeusi alilokuwa amelivaa. Kisha akawatazama vijana wale nyusoni.
Haikujulikana kama alikuwa akiwaona kwenye kiza kile au la lakini yeye alizidisha umakini wake kwao.
"Nimewafatilia tangu pale bar, nikawaona namna mnavyopanga mipango yenu. Nikawashuhudia namna mlivyoondoka na wale vijana wawili. Nikawashuhudia mpaka mnaingia zahanati na kuzua taflani. Nikagundua kuwa hata nyie ni moja kati ya wale vijana ambao mnazunguka na hii picha mkihitaji kupata data!" Akaweka pumziko na kumeza funda la mate.
"Sitaki kuwachoma....na kwanza mimi ni mtu mkarimu sana. Nataka tu kufahamu ukweli uliopo nyuma ya hii picha na zaidi ya yote nyinyi ni kikundi gani haswa!" Akaweka kituo.
"Bro!" Kassim akawa wa kwanza kumjibu.
"Maelezo tuliyonayo ni mengi sana. Nadhani kwanz awe tufungue pingu, halafu utafahamu kila kitu! Nakuhaidi hilo..."
Lilikiwa jibu la kimtego na likaambatana na ombi la kimtego pia.
Tito Ngeze hakutaka kunasa kwenye mtego ule,
"Hivi unajua kuwa haya ni maongezi kati ya polisi na mhalifu? Umeona wapi eti askari akamfungua mhalifu eti kwanza wakubaliane halafu nd'o amfunge tena. Hapo nitakuwa namtukana Kopro aliyenipa mafunzo yangu kwenye kozi!"
Sanga akakohoa kidogo kisha akamjibu,
"Wewe tuamini tu. Sisi mbona hatuna baya wala!" Jibu lake likashuhudia teke kali lililofyatuliwa na kutua juu ya nyuso zao kwa zamu. Midomo na pua zao vikaungana kuonja maumivu yale kwa pamoja.
"Msitake niwaumizeni aisee. Halafu wala sitaki kuwahusisha askari wenzangu wengine kwenye hili. Nataka tu kujua nyinyi mmetumwa na nani. Na kwa nini mnamtafuta huyu kijana!"
Hawakuwa na sababu ya ziada kukataa kumpa ushirikiano. Sanga na Kassim wakajikusanya kwa pamoja na kutoa maelezo juu yao , aliyewatuma na kiasi gani kawahaidi.
Walitamka yote japo hawakuwa na jibu halisi juu ya ni kwa nini kijana yule pichani ambaye ni Feruzi anatafutwa.
Walichoambiwa wao ni kumleta akiwa hai tena kama ikiwezekana awe anatabasamu kabisa.
Walikuwa vijana wa mitaani tu ambao walikusanywa na kuhaidiwa kiasi kikubwa cha pesa kama tu wangefanikisha kufahamu alipo Feruzi na kama ikiwezekana wamlete akiwa hai. Wakamtaja kuwa aliyewatuma ni mtu maarufu na tajiri mkubwa tu pale mjini, Aliyefahamika kwa jina la Brown Kizito al-maarufu kama Bosi Mzito kama alivyojulikana na wengi.
Ulikuwa msako wa siku moja tu na walitakiwa wote waripoti kwenye eneo ambalo walipanga naye. Ni hapo ambapo angewalipa kulingana na matokeo ya msako wao.
"Kikundi chenu kilikuwa na jumla ya watu wangapi?" Tito akawauliza,
"Kama kumi na tano tu bro! Sio wengi sana hata!" Sanga akamjibu.
Tito akabaki kimya akiyapima maelezo yao. Mazungumzo yao yalikuwa ya kirafiki na Tito Ngeze alikuwa msikilizaji mzuri kabisa, jambo liliwafanya Sanga na Kassim wajenge imani yao kwake. Wakasahau kuwa aliyeko mbele yao ni askari polisi, wao wakamchukulia kama bro.
"Nadhani ni muda wenu wa kulala usingizi mzito kidogo halafu nitawaamsha baadaye!" Tito Ngeze akatamka huku akisimama taratibu.
"Usingizi?!...Kulala?" Kassim akamuuliza.
Hakujibiwa, badala yake ndani ya sekunde sita tu wote walikuwa wakiona giza na hawakutambua kilichokuwa kinaendelea.
Hii ni baada ya Konstebo Tito Ngeze kuwagusa maeneo kadhaa ya fahamu kwenye miili yao kwa mapigo yake mepesi na ya haraka. Akijua kuwa endapo tu akiwagusa katika maeneo hayo, watapoteza fahamh kwa muda fulani.
Akawafungua pingu na kuwaburuza akiwapeleka katika eneo alilolijua yeye. Shahidi pekee walioshuhudia hili ni zile kuta zilizokuwa zimewainamia. Utulivu mkubwa ukafuata huku kile kimya cha shetani amepita kikatanda eneo hili.
********
Hatua kadhaa alizozipiga zilimuwia chungu sana. Aliwaza mambo mengi sana kichwani mwake. Tayari amaeshampoteza rafiki yake ambaye hakujua kama ni kweli ameuwa au ni mzaha tu.
Akabaki katika kilio huku macho yake yakitiwa ukungu na upofu kwa machozi yaliyoulowanisha uso wake.
Maumivu ya kifo cha rafiki yake yakachanganyikana na maumivu ya kupotelewa na pesa zake alizokuwa amepewa kama zawadi.
"Zawadi gani hii sasa? Zawadi gani ambayo imekuwa laana?!" Akajiuliza akiwa anazipiga hatua kuelekea mbali alikokujua yeye mwenyewe.
Akapata wazo la kufika pale nyumbani kwake. Lakini machale yakamcheza kuwa pale sio mahala salama tena kwake.
Baada ya kufikiri kwa kuda mrefu, akaamua kupuuza machale haya na akaanza kupiga hatua kuelekea nyumba yake ilipokuwa.
Ghafla akaikumbuka simu yake na akaitoa mfukoni. Alipoibofya ili iwake akagundua kuwa namba ngeni takribani sita tofautitofauti pamoja na moja ya Mtemi, zilikuwa zimempigia.
Alipoona kuwa hata ya Mtemi ilimtafuta na hakupokea wasiwasi ukajijaza tena kwenye koo lake. Jambo lililomfanya ameze funda la mate kwa woga.
Wanataka nini tena hawa? Alijiuliza.
Na muda ambao namba ile ilimtafuta ulikuwa umepishana na wakati huu kwa dakika kumi pekee. Hapo akagundua kuwa aliiweka simu ile katika mfumo wa kuita bila kutoa sauti yaani 'silent mode'.
Akazipuuza zile nyingine na akaamua kuipigia ile namba ya Mtemi. Sauti nyororo ya mwanadada ndani ya simu ikamkumbusha kuwa hakuwa na salio la kutosha kuipigia simu ile na ikamshauri achukue mkopo ambao utamuwezesha kupata salio.
Wakati huu alikuwa ameikaribia nyumba aliyokuwa akiishi, akakata kona na kugeuza kuyatafuta maduka ya karibu ambayo angeweza kununua vocha maalumu ili aongeze salio kwenye laini ya simu yake.
Muuzaji alimuhuumia huku akiwa na mashaka machoni mwake, alipepesa huku na kule huku akimkagua Feruzi mavazi yake kwanzia juu mpakaa chini.
"Oyah mangi eeh! Vipi tena mbona unanichekicheki tatizo nini mzee? Kama unanipa vocha nipe bhana mi nisepe!" Feruzi akaamrisha kwa jazba.
"Hamna kaka! Kwani hujasikia taarifa yoyote ile leo kukuhusu bro?!" Kwa sauti ya chini mangi akauliza.
"Taarifa gani?"
"Kuna watu wanakutafuta mdogo wangu! Sijui ni askari wale...wanasema we ni haini na haramia!"
Mapigo ya moyo yakaongeza kasi na woga ukamvaa upya kijana Feruzi. Upesi akachukua vicha yake na kuondoka katika duka lile lililokuwa na mwanga mkubwa wa taa iliyomulika kwa fujo.
Mungu wangu! Ilimtoka Feruzi.
"Ina maana mpaka askari wameshanifahamu? Vipi kama wameshafika mpaka nyumbani kwangu?!" Akajiuliza akiwa anajiahughulisha kukwangua vocha yake kwa kucha zake yeye mwenyewe.
Akanakiri namba zake na kuongeza salio kwenye simu yake,
Kisha upesi akaipigia namba ile ya Mtemi huku akinyata kuisogelea nyumba yake kwa tahadhari.
Simu iliita bila kupokelewa. Ikakata!
Akapiga tena, wakati huu alishuhudia kinachoendelea pale nyumbani kwake kwa makini akiwa amejificha. Simu ikapokelewa,
"He..ha.halooo! Shikamoo bro!" Akasalimia.
"Ulikuwa wapi Adam Feruzi Adam!?" Likaanza swali kabla ya salamu yake kujibiwa.
"Nilikuwepo tu bro!"akajibu kwa wasiwasi.
"Na sasa hivi uko wapi?!" Sauti ile nzito ikauliza.
"Kwangu..nipo kwangu!" Akajibu.
"Fanya haraka utoke hapo sasa hivi! Kuna watu wanakuja kukuteka! Kajifiche kadri unavyoweza."
Aliyoyaongea mtu yule ndani ya simu yalishabihiana na aliyoyaona Feruzi. Mbele ya chumba chake walisimama wanaume wanne ambao tayari wamefanikiwa kuvunja mlango wa chumba chake, wamepekua kila kitu ndani na wamepata baadhi ya vitu walivyovihitaji baada ya kumkosa yeye,
Mmoja wao akapaza sauti akisema,
"Nampigia hapa mpaka sasa hivi lakini namba yake inatumika. Sijui anaongea na nani huyu mwanaharamu!!"
Akayakumbuka maneno ya Mangi dukani. Na akapigia mstari hisia zake kuwa anatafutwa na polisi. Aliogopa sana.
Lakini sauti ile ndani ya simu ikaendelea,
"Hawa wanaokutafuta sasa hivi ni watu hatari sana Adam Feruzi Adam. Wakikukamata tu watakujeruhi mpaka wapate kile wanachokitaka! Wanaua, wanasaga, wanakoboa na kuteketeza kabisa uhai wa mtu yeyote yule endapo tu watataka."
Kauli hizi tata zikazidi kuwa mwiba wa sumu kwenye nyama za Feruzi.
"Bro niende wapi sasa? Eh? Wewe ndiye umeniharibia maisha yangu, ukamuua rafiki yangu na sasa ona naandamwa kama mhalifu. Nimekukosea nini lakini?!" Feruzi akalalama kwa sauti yenye machozi na manung'uniko.
"Vipi ile zawadi yangu ya leso nzuri yenye mchanganyiko wa maua mekundu kwenye nyeupe. Uliitunza vizuri kweli au uliitupa ovyo?"
Hili swali likaleta mzizimo kwenye mwili wa Feruzi. Na kama miujiza vile, mmoja kati ya wale wanaume akatoka na leso ile ndani ya chumba akiwaonyesha wenzie.
"Mnaona? Huyu kiumbe ni muuaji huyu! Lazima atiwe nguvuni mpaka afikishwe kwenye vyombo vya dola!"
Feruzi akatoa macho yake na hata majirani baadhi waliokuwa wakishuhudia kilichofanywa na vijana wale waliojulikana kaama askari waliweka mikono yao vinywani na wengine vichwani wakishangaa!
"Kama uliijali zawadi yangu na kuitunza vizuri, basi umeokoka Adam Feruzi. Lakini kama hukuijali we ukatupa tu, basi Mungu akusaidie!" Simu ikakatwa.
Alichokiona na alichokisikia vyote vilishirikiana kuiumiza nafsi yake. Akauona mlango wa jela ukimuita na akakiona kitanzi kmcha kunyongwa kwa kosa la mauaji kikitabasamu kumpokea.
Kitambaa chenye ramani zisizoeleweka za damu kavu kilikuwa hadharani kimemulikwa kwa mwanga mkali wa taa.
Yeye kajibanza mafichoni.
Giza la Mungu likishindana na taa za mzungu,
Feruzi anatafutwa!
ITaendelea kesho!!