Saturday, December 12, 2015
Maseypr kwa 9:06 AM
SALAMU KUTOKA KUZIMU
SURA YA TANO II
Unono, huyu alikuwa mwanamke wa makamo, mfupi kiasi, mnene wa kutosha, mweusi kupindukia, mama huyu alikuwa mmoja kati ya watu wengi walioshuhudia ajali hii ya mtu kuuawa kwa bomu. Mama huyu alikuwa miongoni mwa umati huo, kama wananchi wengine alisema hili na kusikiliza lile, macho yake yakifanya kazi ya kutazama kwa hofu tukio hilo pamoja na polisi kadhaa, ambao walikuwa katika pilika pilika za kukusanya mabaki ya marehemu huyo.
Kichwani Unono alikuwa na mawazo tofauti, nje kabisa ya tukio la msiba huo uliotokea eneo hilo. Alikuwa na mawazo mchanganyiko wa matatizo ya kiuchumi na mapenzi. Mama huyu alihisi kuwa sehemu hiyo ingeweza kumfanya apate ufumbuzi wa tatizo lake moja ama yote mawili yanayomtatiza.
"Usiku..." aliwaza moyoni mwake.
Kimaumbile, Unono hakuwa na umbo la kuridhisha wala hakuwahi kujidanganya kuwa ana sura nzuri. Ukweli huo alikuwa ameubaini tangu enzi za usichana wake alipojiona akikua miongoni mwa vijana wa kiume ambao walionekana kumwepuka kama jini na kumtazama kama jinamizi. Wakati huo huo aliambulia kuwaona wenzake wakifuatwa na vijana wa kiume na kubembelezwa kama malaika, wakipewa lugha tamu na matendo ya kimapenzi. Ndipo alipoanza kujitathimini katika kioo.
Akagundua kuwa pamoja na kuwa na sura mbaya, Alitisha na kuchukiza kwa jinsi alivyojengeka kama kilema ingawa hakuwa na kasoro yoyote kimaumbile. Hivyo maisha yake yaliyofuata aliishi akifahamu kabisa kuwa tunu ya kuzaliwa mwanamke yeye isingemsaidia kama wanawake wengine. Aliamini kuwa katika maisha yake lazima atoe jasho ili aweze kuishi.
Jasho lake alilitoa kwenye vilabu akiwauzia wanywaji makongoro ya ng'ombe ambayo aliyanunua machinjioni na kuyachemsha kwa maji na chumvi. Sura yake haikumtendea wema katika biashara yake. Mwanamke huyo aliyekuwa na tama zote za kike, alipata mume wa kufariji kwa kwa bahati. Na alipompata, ilikuwa mhali mwanaume huyo kumrudia. Naye Unono hilo halikumshangaza kamwe kwani hilo lilikuwa jambo la kawaida katika maisha yake. Hayo yalimtokea kwa nadra sana. Hivyo siku nyingi Unono alikuwa mhitaji. Ndipo akabuni mbinu za kutembea sehemu fulani fulani usiku, sehemu ambazo alikuwa na matumaoni ya kukutana na wanaume ambao nafsi na hali zisingewaruhusu kuchunguza. Walevi wachelewao kurejea majumbani kwao usiku, wazururaji wasio na makazi maalumu, na walinzi wanaokesha wakilinda nje usiku, hawa ni miongoni mwa wateja ambao Unono aliwahi kuwapata ili kutimiza haja zake. Baadhi waliwahi hata kumpatia pesa.
Kwa hivyo Unono akakusudia kujaribu bahati yake kwenye eneo hili lililolipuliwa na bomu. Hangekosa kufua dafu pale. Askari mmoja ama wawili wasingekosa kuwekwa hapa kwa ajili ya kulinda mazingira. mmoja wao asingekosa kumtupia maneno iwapo angecheza vema karata yake. Na hata wawe wote wawili angebabaishwa na nini angestahimili. Eti kakosa mapenzi ya mume kwa muda mrefu sasa. Ni mawazo hayo yaliyomfanya Unono afunge biashara mapema na kurejea nyumbani. Aliogaa, akajipaka mafuta yake yenye harufu nzuri, mafuta ambayo aliyanunua kwa shingo upande. Alivaa baibui lake jeusi bila vazi lingine lolote mwilini.
Alijikuta akiingiwa na wasiwasi. Alikuwa peke yake, katikati ya kiza katika eneo ambalo mchana huo lilikuwa la maafa. Akawaza kurudi, lakini alijikongoja hadi alipofika kando ya vifusi vya jumba hilo. Alitupa macho kila upande, hakuonana dalili yoyote ya mlinzi. Baada ya mizunguko kadhaa, aliamini kuwa sehemu hiyo haikuwa ikilindwa. Akasononeka moyoni.
Mara likamjia wazo jingine. Yawezekana katika jumba hili mlikuwa na vitu vya thamani ambavyo angevichukua na kuviuza! Wazo hili likamtuma Unono kuanza kuchungulia, akashika kile na kujipenyeza pale. Alipata mwanya ambao ulimwingiza ndani ya kifusi hicho. Mikono yake iliendelea kupeleleza kwa makini, macho yakifanya juhudi kutazama.
Ghafla Unono aligusa kitu ambacho kilimshitua. Kitu chenye dalili ya uhai. Nyoka? alijiuliza baada ya kuutoa haraka mkono wake. Baada ya kutulia kwa makini, aligundua kuwa alichogusa ni mwili wa binadamu. Ugunduzi wake ulimshitua zaidi. Maiti nyingine! aliwaza akiinuka na kuanza kuondoka.
Kisha ushujaa ukamwingia na kumfanya ahairishe safari yake na kuuinamia mwili huo kwa uchunguzi zaidi.
ITAENDELEA 0784296253