RIWAYA : SALA YA SARAH
MTUNZI : ALEX KILEO
SEHEMU YA SITINI NA TISA.
ENDELEA..................
Taita alienda mpaka hospitali na kwenda katika wodi aliyolazwa mlinzi wake wa getini, alimkuta tayari fahamu zimemrejea,
"ni nani aliyekuwa ndani ya nyumba kabla nyumba haijawaka moto?" Taita aliuliza moja kwa moja bila hata kumjulia hali mlinzi,
"nyumba haijawaka moto?, nyumba ipi?" Mlinzi aliuliza kwa maana wakati nyumba
ikiungua yeye alikuwa amepoteza fahamu kwa hiyo hakuna anachojua,
"wewe vipi?, hujui kuwa nyumba imeungua?" Taita aliuliza kwa hasira,
"mzee mimi nilipigwa na mwanamke ambaye simjui, nikspoteza fahamu, kwa hiyo sijui kitu kingine kilichoendelea" Mlinzi wa getini alijibu na kumfanya Taita ajiulize huyo mwanamke ni nani?
"huyo mwanamke yupoje?" Taita aliuliza,
"ana mwili wa wastani, ana nywele ndefu na ni mweusi" Mlinzi alijibu na kumfanya Taita ajiulize huyo mtu ni nani? Kwa maana Sarah hayupo hivyo, Sarah ni mwenye kiasi na mwili wake ni mwembamba,
"sasa huyo mwanamke alikuwa anataka nini? Au alikupiga tu bila sababu?" Taita aliuliza,
"alikuwa anamuulizia Trigger, na Trigger alinizuia nisiruhusu mtu aingie ndani, kwa hiyo nikagoma kumruhusu huyo mwanamke kuingia, ndio akanipiga" Mlinzi alijibu,
"Trigger alikuwa ndani?" Taita aliuliza kwa wasiwasi,
"ndio, alikuwa na wanaume watatu ambao alikuwa amewateka" Mlinzi alijibu na kumfanya Taita achanfanyikiwe, maana alizidi kuvurugwa na asijue ni nani aliyeungua,
"wapoje hao wanaume?" Taita aliuliza,
"mzee mmoja na vijana wawili" Mlinzi alijibu na kumfanya Taita ageuke na kuondoka, maana aliona mlinzi anamvuruga tu.
*************
Sajenti Minja fahamu zilipomrudia, sehemu ya kwanza aliyofikiria kwenda ni katika kambi ya Taita, maana hali aliyoiacha haikuwa hali salama.
Sajenti Minja alisimamisha boda boda iliyomchukua mpaka eneo lile la kambi ya Taita, aliukuta umati wa watu ukiwa unatawanyika baada ya moto kuwa umezimika, hata kikosi cha zimamoto hakukikuta, kilikuwa kimeshaondoka, kilichomshangaza Sajenti Minja ni Kukuta ile nyumba ikiwa imeteketea kabisa wakati yeye aliiacha ikiwa nzima kabisa, sasa swali alilojiuliza ni ule moto ni wa kuwashwa na mtu au umetokea bahati mbaya?
"aisee ndani ya nyumba kulikuwa na mtu kweli?" Sajenti Minja alimuuliza dada mmoja aliyekuwa jirani nae,
"wameukuta mwili wa mtu" Yule dada alijibu kwa huzuni,
"mwanamke au mwanaume?" Sajenti Minja aliuliza,
"wameukuta wa mwanaume" yule dada alijibu na kumfanya Sajenti Minja ahisi huenda Sarah ameamua kumchoma moto Trigger.
Sajenti Minja akatoka pale na moja kwa moja akaenda kwa Dokta Innocent Malle, akamkuta akiwa na Kijana wake, Sajenti Minja akawajulisha wanatakiwa wahame pale kwa muda kwa ajili ya usalama wao. Kisha Sajenti Minja akachukua gari yake na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Taita, akaingia moja kwa moja mpaka ndani na kumkuta Vin akiwa amekaa sebuleni huku akiwa bize kubonyeza simu,
"mzee yupo wapi?" Sajenti Minja aliuliza baada ya kuingia,
"ametoka, vipi?" Vin aliuliza,
"mzee nadhani yupo hatarini, muda wowote Sarah anaweza kumdhuru" Sajenti Minja aliongea,
"kwanini unasema hivyo?" Vin aliuliza,
"Sarah ametoka kumuua Trigger muda si mrefu, tena kile ni kifo kibaya" Sajenti Minja aliongea kwa masikitiko,..
.
.
..
"mzee nampigia hapokei simu, ila sitokubali Sarah amuue, nitamlinda mzee kwa nguvu zote, yule ni baba yangu hata kama sio wa halali" Vin aliongea kwa ukali,
"ila mimi hapa nimekuja kumkamata mzee wako, kwa maana baada ya kufuatilia kila kitu kuhusu vifo vya wazazi wako na Sarah nadhani nimeshakusanya ushahidi wa kutosha wa kumtia hatiani mzee wako" Sajenti Minja aliongea,
"hapana, hiyo kesi si inanihusu mimi kama mwenye wazazi waliouawa? Basi nasema nimemsamehe Taita, sitaki umkamate" Vin aliongea kwa ukali,
"usichukulie hasira, hii kesi ilifunguliwa na familia ya baba yenu, kwa hiyo mwenye uwezo wa kuifunga hii kesi ni babu yenu tu, pia nadhani endapo nitamkamata Taita, itakuwa salama kwake kwa kuwa kukaa kwake urahiani ni kukaa karibu na kifo, kwa maana inakuwa rahisi kwa Sarah kumfikia" Sajenti Minja alijaribu kumueleza Vin,
"hapana, usitumie kigezo hicho kumtia hatiani mzee wangu" Vin aliongea kwa kujiamini, na kipindi hicho Taita alikuwa amerudi na amekaa nyuma ya mlango akisikiliza maongezi kati ya Vin na Sajenti Minja.
"usibishane na sheria wewe, na hakuna mtu ambaye yupo juu ya sheria, Taita lazima nimkamate na akajibu mashtaka" Sajenti Minja aliongea kwa kujiamini pia,
"kwa ushahidi Upi?" Vin alihoji,
"ngoja nikujibu kwa kifupi tu, Sarah amenipa ushahidi wa maneno yote aliyoongea Harry kabla hajafa, pia kuna mtu anaitwa Strategic, amenipa maongezi yake na Trigger, aliyarekodi kupitia lap top yako, pia leo muda mfupi kabla Trigger hajafa, aliongea ukweli wote wakati akiwa ametuteka'" Sajenti Minja aliongea na kumfanya Vin achoke,
"Strategic nae amekupa ushahidi? Mbwa wangu mwenyewe leo amening'ata?" Vin aliongea kwa upole na wakati huo sasa Taita aliamua ajitokeze sebuleni,
"Trigger amekufa? Au nimesikia vibaya?" Taita aliuliza huku akimtazama Sajenti Minja,
"ndio amekufa, na wewe upo hatarini pia" Sajenti Minja alijibu,
"mzee ebu ondoka nchini, ikiwezekana chukua hata ndege ya kukodi muda huu" Vin alimwambia Taita,
"hiyo haiwezekani, mzee upo chini ya ulinzi" Sajenti Minja aliongea huku akimuangalia Taita,
"kwa kosa gani?" Taita aliuliza kwa dharau,
'"kwa mauaji yaliyotokea miaka ishirini iliyopita, uliua familia ya Isack kwa kuiteketeza na moto" Sajenti Minja aliongea,
"mzee, huyu anatuvuruga tu, mzee ingia ndani uangalie vitu muhimu na uondoke haraka, hii nchi haifai tena" Vin aliongea kwa msisitizo na kufanya Taita aanze kwenda chumbani kuchukua vitu vyake muhimu,
"simama mzee" Sajenti Minja aliongea huku akiichomoa bastola yake na kumuelekezea Taita, Vin akaona akifanya uzembe mzee wake atakamatwa, Vin akarusha teke nw kumpiga Sajenti Minja, Sajenti Minja akapepesuka, kisha Vin akaokota mto wa kochi na kuurusha kuelekea kwenye mkono wa Sajenti Minja, mto ukaipiga ile bastola na kudondoka chini, Vin akachomoa bastola yake na kumuelekezea Sajenti Minja,
"mzee harakisha uondoke" Vin aliongea baada ya kumzidi ujanja Sajenti Minja.
Taita akaingia chumbani na kisha alirudi sebuleni baada ya muda mchache huku mkononi akiwa na begi dogo,
"Vin mwanangu tuondoke" Taita aliongea huku akimtazama Vin,
"mzee wewe nenda, kwa hali ilivyo hapa, nikishusha bastola chini utakamatwa" Vin alimwambia Taita,
"mpige risasi huyo ili tuondoke, sitaki nikuache mwanangu" Taita aliongea kwa upole.
"hapana mzee, siwezi kumpiga risasi, cha muhimu wahi kuondoka na uende mbali, ukifika nitaharifu" Vin aliongea ila Taita aliweka msimamo waondoke wote, Vin alimbembeleza na mwisho Taita akakubali kuondoka, alimsogelea Vin na kumbusu katika paji la uso wake, kisha akageuka na kuanza kuondoka,
"mzee, ondoka peke yako, usimuamini mtu yoyote, hata Strategic" Vin alimsisitizia Taita ambaye aliitikia kwa kichwa na kisha akageuka na kutoka nje, sebuleni akawaacha Sajenti Minja ambaye alikuwa mateka wa Vin.
"elewa kuwa hili unalofanya ni kosa, unamsaidia muharifu kutoroka" Sajenti Minja alimwambia Vin ambaye alikuwa ametulia na bastola yake mkononi,
"sawa, acha nifanye kosa kwa ajili ya kumsaidia mtu anayenipenda" Vin alijibu na kumfanya Sajenti Minja acheke.
Baada ya nusu saa ya kumshikia bastola Sajenti Minja, Vin aliamini baba yake atakuwa ameshaondoka na kufika mbali, Vin akateremsha bastola na kuitupa chini, kisha akanyoosha mikono juu kujisalimisha kwa Sajenti Minja.
Sajenti Minja akashangaa, ila kwa haraka akamkimbilia bastola na kuikota, kisha akamfuata Vin na kumfunga pingu, kisha akaanza kutoka nae nje.
Alivyotoka nje, Sajenti Minja akatoa simu mfukoni na kumpigia Sarah, aliona huyo ndio mtu mzuri ambaye anaweza kumsadia kumkamata Taita kwa muda huo.
Sajenti Minja akatoa akapiga simu,
"sarah naomba unisikie kwa umakini mkubwa, nina ushahidi wa kutosha wa kumtia hatiani Taita, sasa basi hapa nipo kwake, Taita amenitoroka na nahisi ameelekea uwanja wa ndege, fanya ukamuangalie na ukimpata nitaharifu, usimfanye chohote" Sajenti Minja aliongea kwa kusihi,
"kama mmeamua kumfungulia kesi sawa, ngoja niende kumuangalia" Sarah aliongea kwa utulivu na kukata simu.
Muda huo wa jioni ndio muda ambao Sarah alikuwa amefika nyumbani kwake kutoka katika kambi ya Taita. Baada ya Sarah kupokea taharifa hizo kutoka kwa Sajenti Minja, alichofanya ni kuingia ndani na kubadili nguo, alivaa suruali nyeusi na koti jeusi la kike, kisha ile mask yake akaitia ndani ya mfuko wa koti, kisha akamuaga Dokta Pendo na babu yake na kuondoka zake huku akifurahi kitendo cha Sajenti Minja kuamua kumfungulia kesi Taita, aliamini haki itatendeka.
Ilimchukua muda mchache tu kwa Sarah kufika nje ya majengo ya Kiwanja cha ndege, aliamua kutumia usafiri wa boda boda kwa maana ndio ulikuwa wa haraka. Sarah alivyofika nje aliangaza kila upande aone kama anaweza kuiona gari yoyote ya Taita, kwa maana alikariri asilimia tisini ya magari ya Taita. Baada ya kuangalia kwa muda, hakuweza kuona gari katika eneo hilo.
Sarah hakuwa na uhakika kama ni kweli Taita anaweza kuwa yupo au hayupo, mwisho akajiaminisha huenda Taita labda alikuja na gari nyingine ambayo Sarah haijui, Sarah akaamua aingie ndani ya jengo huku akiamini labda Taita yupo ndani, ila wakati akiinua mguu ili aanze kuelekea ndani, alishuhudia gari ya Taita ikiegeshwa, Sarah akasita na kuanza kuifuata kwa kujificha ficha, na kwa kuwa giza lilikuwa linaanza kushika kasi, haikuwa rahisi kwa Taita kumtambua Sarah kwa urahisi.
Taita akafungua mlango, akashuka na begi lake, mara ghafla akawekewa bastola kichwani na Sarah,
"rudi ndani ya gari mjomba" Sarah aliongea huku akimuangalia, Taita akataka kupiga kelele, Sarah akamuwahi kwa kumpiga ngumi kali ya kisogo, Taita akalegea na kuanguka, Sarah akamuingiza ndani ya gari kisha akamvua koti la suti na kulichana, kisha akatengeneza kamba na kumfunga mikono, kisha akamfunga kwa kumuambatanisha na kiti cha gari, Sarah akaingia kwenye gari na kuliondoa.
Baada ya muda mchache Taita akazinduka na kujikuta na kamba mwilini,
"unaenda kuniua?" Taita aliuliza,
"hapana, nakupeleka polisi ili sheria ifuate mkondo wake" Sarah alijibu na kumfanya Taita acheke,
"sheria za nchi gani? Sheria za hii nchi zinafuata mkondo wa pesa, wewe unadhani nikipelekwa mahakamani nitafungwa" Taita aliuliza huku akicheka,
"utafungwa tu, ushahidi si upo" Sarah alijibu,
"ningefungwa siku nyingi tu kwa maana hata madawa ya kulevya nimekamatwa nayo mara nyingi tu, ila naachiwa, we unadhani serikali inaweza kumfunga mtu anayoisaidia fedha za kufanya mambo yao?" Taita aliuliza kwa dharau na kumfanya Sarah sasa abadili muelekeo wa gari, aliona ni kweli Taita hawezi kufungwa.
Sarah aliendesha gari mpaka nyumbani kwa Taita, kisha akashuka na kumkuta mlinzi yupo getini, Sarah akampiga mlinzi na kumfanya apoteze fahamu, Sarah akamshusha Taita na kumuingiza ndani, akamfunga kwenye kiti kama alivyomfanya Trigger, kisha yeye akakaa kwenye kochi,
"kazi nzuri" Taita aliongea huku akitabasamu,
"sipo hapa kwa ajili ya kuongea, nimekuja kuitimisha agano" Sarah aliongea huku akivaa kinyago chake,
"agano? Agano uliwekeana na nani?" Taita aliuliza,
"unaikumbuka ile sala niliyoomba nikiwa mdogo? Leo hii inatimia" Sarah aliongea huku akisimama,
"unawaka kama moto? Ebu waka nikuone" Taita aliongea kwa dharau na kumfanya Sarah atanue mikono yake, kisha akaikutanisha na moto ukatokea kwenye viganja vya mikono yake, Taita akashangaa,
"umeona sasa?" Sarah aliuliza huku akicheka na kumfanya Taita ashikwe na bumbuwazi, Sarah akamsogelea Taita na kuuweka ule moto kichwani, Taita akaanza kuungua, Sarah akawa anamtazama tu namna Taita anavyoangaika, kisha Sarah akauzima ule moto,
"moto ukiwaka kichwani utakufa mapema" Sarah aliongea na kisha akaanza kuchana makochi ya sofa na kuanza kumfunga nayo Taita mwilini, aliporidhika akawasha moto, Taita akaanza kuungua na kipindi hicho Sarah akaanza kuwasha moto kwenye kila chumba, nyumba nzima ikawa na moto sasa, Sarah akarudi na kumuangalia Taita namna anavyoungua.
Mkononi kwa Sarah alikuwa na pete ambayo ndio ilikuwa inatoa moto, alipewa na jeshi kama silaha pindi awapo kwenye hali ngumu.
****************
Sajenti Minja alifika polisi huku akiwa na vin, akamuingiza kwenye ofisi yake kwa ajili ya kumuhoji, ila kabla hawajaanza mahojiano, alifika mlinzi wa getini kwa Taita na kuwapa taharifa kuwa Taita ametekwa na mtekaji amejifungia ndani ya nyumba, Sajenti Minja akataka aende ila mkuu wa polisi akamzuia,
"kila siku unashindwa kumkamata huyo dada, leo hiyo kazi nitafanya mimi" Mkuu wa polisi aliongea kisha akatoka na askari katika gari tano, wote walikuwa na silaha.
Wale askari walifika mpaka nyumba kwa Taita na kukuta nyumba nzima inawaka moto na katika dirisha la sebuleni alisimama Sarah akiwa anawaangalia, kisha alivyoona ni askari, Sarah akashusha pazia.
Askari wakaamua watoe tangazo kuwa mtu yoyote aliyepo ndani ajisalimishe, lakini Sarah hakutaka atoke, badala yake alikuwa anatafuta njia ya kutoroka.
Sarah akatokea mlango wa nyuma, ila alipofungua mlango tu akakoswa na risasi, akagundua ameshazungukwa kila upande, Sarah akarudi mpaka dirishani na kutoa bastola yake, alikuwa ameshapaniki kwa kitendo cha kukoswa na risasi, Sarah akafyatua risasi iliyompiga askari mmoja na kuanguka chini.
mkuu wa polisi akaamuru vijana wake waishambulie, polisi wakaanza kufyatua risasi kuelekea dirishani, moja ikampata Sarah kifuani na kuanguka chini, huku risasi nyingine zilimpiga Taita aliyekuwa anafuka moshi baada ya moto kumteketeza, baada ya zile risasi kumpiga Taita, alikufa pale pale juu ya kiti.
Nje mkuu wa polisi akawaamuru askari wawili wasogee dirishani wakaangalie kama wamemuua mtekaji, wale askari wawili wakasogea mpaka dirishani, ila Sarah akawapiga risasi na wakafa palepale.
Mkuu wa polisi akaamuru tena washambulie, askari wakapiga tena risasi mfululizo na mbili zikampiga Sarah, moja ilimpiga Sarah mkononi na nyingine ikampiga kwenye mbavu, Sarah akaanguka chini na bastola ikamtoka, Sarah akawa anapumua kwa shida huku akiwa na mawazo ya kujisalimisha, kwa maana aliona ameshazidiwa, aliona akiendelea kupambana atafia ndani kwa kuwa alishazungukwa.
Kwa upande wa nje, mkuu wa polisi aliomba msaada wa jeshi, aliamini inawezekana mtu wanaepambana nae sio wa kawaida, na muda huo Vin na Sajenti Minja walikuwa wanawasili.
Vin alivyoona hali ilivyo, alianza kulia tu, aliamini Taita hawezi kuwa mzima kwa namna ule moto ulivyokuwa unawaka.
Baada ya muda mchache, wanajeshi walifika, wakawaambia askari warudi nyuma, kisha wao wakakaa mstari wa mbele, na amri ikatolewa kuwa lazima huyo mtekaji auawe kwa maana ameshaua askari watatu, wanajeshi wakajipanga kushambulia, na walikuwa na mabomu ya sumu, ndio walipanga kuyarusha ndani.
Sarah aliweza kuona kila kitu kupitia dirishani, alikata tamaa, aliona njia bora ni kujisalimisha,
Wanajeshi wakarusha bomu, likaingia kupitia dirishani, kisha wakasubiri kwa muda, mara ghafla mlango wa mbele ukafunguliwa, akatoka Sarah mikono ikiwa juu, ila kutokana na amri waliyopewa wanajeshi, walianza kumpiga risasi nyingi mfululizo na asilimia tisini ya hizo risasi zilimpiga kuanzia kichwani mpaka shingoni.
Sarah akapiga magoti, lakini bado waliendelea kumpiga risasi, mwisho Sarah akaanguka chini na kukata roho huku kile kinyago chake kikimuachia na kuanguka pembezoni mwake.
Kiongozi wa jeshi akaonesha ishara na wanajeshi wakaacha kupiga risasi, kisha kiongozi wa jeshi na polisi wakaisogelea ile maiti na kuigeuza, risasi zilikuwa zimemuharibu vibaya uso wake, alikuwa hatizamiki mara mbili.
Vin alikuwa analia huku akisikitika kuwapoteza watu wawili kwa wakati mmoja, yaani Taita, na Sarah ambaye ni dada yake.
Sasa askari wote wakaruhusiwa kwenda kuuangalia ule mwili, hapo Sajenti Minja ndipo akapata nafasi ya kuuangalia ule mwili,
"umekufa, ila hukustahili kufa, ungeachwa hai ili ulisaidie taifa, ni mtu muhimu sana wewe" Sajenti Minja aliongea kwa huzuni, kisha akaondoka huku akicheka.
Vin aliendelea kulia huku akiiangalia ile cheni ya Sarah shingoni, hakika ilimuuma, aliendelea kuuangalia ule mwili wa dada yake uliokuwa umelala chini,
"tuondoke, una kesi ya kujibu" Sajenti Minja alirudi na kumchukua Vin ambaye alikuwa na uchungu mkuu.
Huku nyuma mwili ule ulichukuliwa na kwenda kuhifadhiwa, huo ndio ukawa mwisho wa Sarah na Taita.
**********ITAENDELEA***********
the Legend☆