Riwaya: Sala ya Sarah

Riwaya: Sala ya Sarah

RIWAYA : SALA YA SARAH

MTUNZI : ALEX KILEO

SEHEMU YA ISHIRINI NA NANE.

ILIPOISHIA..................

Sajenti Minja akaamua atumie akili ili kuweza kuikamata ile gari, akaendelea kuikimbiza kwa nusu saa, akafanikiwa kuipita kisha akaisimamisha kwa ghafla gari yake katikati ya barabara, ile Range Rover nayo ikaminya breki, Sajenti Minja akawasha tochi yake na kummulika dereva wa ile gari, alikuwa ni Dokta Pendo, tena alikuwa na hofu tele.

Sajenti Minja akachomoa bastola yake na kushuka ndani ya gari,

"telemka chini, Mikono ikiwa juu" Sajenti Minja aliongea huku bastola yake akimuelekezea Dokta Pendo, hapo Dokta Pendo akazidi kuchanganyikiwa, akashuka kwenye gari.

"mpo wangapi kwenye gari na mmebeba nini?" Sajenti Minja aliuliza lakini Dokta Pendo hakujibu, ni machozi tu yalimtoka,

"wewe mwanamke si nakuuliza?" Sajenti Minja aliongea kwa ukali, lakini Dokta Pendo hakujibu, aliendelea kulia kimya kimya, sasa Sajenti Minja akahisi ndani ya gari kuna kitu na ndio maana yule dada analia, Sajenti Minja akalisogelea gari na kufungua mlango wa nyuma kwa nguvu.......

**********ENDELEA*********

Sajenti Minja alikutana na teke kali lililotua kwenye mkono wake wenye bastola, bastola ikamdondoka, alichofanya Sajenti Minja ni kuushika mguu wa Sarah na kumvuta nje kwa nguvu, Sarah akatoka kama mzigo na kupigizwa chini, kwa kuwa hakuwa na mask, alichofanya alitoa kitambaa na kujifunika kuanzia puani na kushuka chini.

Sajenti Minja hakufanikiwa kumuona vizuri Sarah, ila Sajenti Minja aliruka juu kumuelekea Sarah, Sarah hakutaka kupoteza muda, alimsubiri Sajenti Minja atue chini, alipotua alikutana na mateke ya haraka haraka ya mbavuni na Sajenti Minja akajikuta ameinama baada ya kuhisi maumivu kwenye mbavu, Sajenti Minja alipoinama tu, akapigwa ngumi tatu za kisogoni na kuanguka chini, alipoteza fahamu pale pale, leo Sajenti Minja alipigwa kiurahisi sana, mpaka Sarah mwenyewe akashangaa, hakutegemea kushinda kiurahisi vile.

"iondoe hiyo gari yake hapo barabarani" Sarah alimwambia Dokta Pendo ambaye alielekea mpaka ilipokuwa gari ya Sajenti Minja na kuiondoa barabarani, kisha akarudi alipokuwa amesimama Sarah,

"itabidi niwe dereva muda huu" Sarah aliongea huku akiingia kwenye gari yake na Dokta Pendo akaingia kushoto mwa gari,

"mzee bado hajahamka" Dokta Pendo aliongea huku akimuangalia Taita aliyekuwa amelala nyuma ya gari,

"huyo kuamka ni mpaka kesho, hiyo sumu niliyomnusisha sio nzuri, inachukua masaa mengi kutoka mwilini" Sarah alijibu,

"sasa shoga yangu, mi nadhani unirudishe nyumbani tu" Dokta Pendo aliongea,

"wewe hata huogopi? Hujaona tulivyowakuta wakikuwinda pale kama mnyama?" Sarah aliuliza kwa mshangao,

"nirudishe nikachukue nguo zangu tu ili nihame pale, sina mpango wa kuishi pale" Dokta Pendo aliongea,

"hapo sawa" Sarah aliongea huku akiongeza mwendo wa gari yake,

"na yule uliyepambana nae kule ni mmoja wao?" Dokta Pendo alimuulizia Sajenti Minja,

"yule ni askari" Sarah alijibu katika sauti tulivu,

"askari???? Sasa mbona umempiga? " Dokta Pendo aliuliza kwa mshangao,

"pale sijampiga, nilichofanya ni kujilinda, kanuni za kijeshi zinasema ni bora ujilinde huku ukiwa unashambulia" Sarah alimjibu Dokta Pendo,

"kanuni za kijeshi? kwani wewe ni mwanajeshi?" Dokta Pendo alihoji,

"hapana, ila najua mambo mengi ya kijeshi" Sarah alijibu huku akiegesha gari yake mtaa ule ule anapokaa Dokta Pendo, ila alipaki mbali kidogo ingawa nyumba aliiona vizuri.

"subiri kwanza nikaikague nyumba yako" Sarah aliongea Kisha Sarah akatelemka na kuelekea kwenye nyumba ya Dokta Pendo kwenda kuikagua, alienda kiuangalifu mpaka alipofika mlangoni, akachomoa bastola yake na kisha akagonga hodi, lakini hakujibiwa, akarudia tena kugonga hodi na hali ikawa ile ile, akasukuma mlango na mlango ukafunguka, akaingia ndani na kukuta hakuna mtu, akaikagua nyumba yote mpaka chooni pia hakukuta mtu, akaridhika na ukaguzi wake, Sarah akatoka nje na kuelekea kwenye gari,

"unaweza kwenda, ila mimi naondoka, Wewe cha kufanya ni kukusanya vitu vyako haraka na kuondoka" Sarah aliongea,

"usijali shoga yangu, situmii hata muda mrefu" Dokta Pendo alijibu kisha wakaagana na Sarah, Sarah akawasha gari na kuondoka zake.

Safari ya Sarah iliishia nyumbani kwake, akaingiza gari ndani ya geti na kisha akafungua mlango wa nyuma wa gari, akamtoa Taita, hakuwa na uwezo wa kumbeba, alimburuta mpaka ndani, akamuingiza ndani ya chumba chake cha siri, kisha akamfunga mikono na miguu, na mdomoni alimziba na plasta nzito ambayo ilimzuia Taita kutoa sauti endapo atarejewa na fahamu zake.

Baada ya kujiridhisha na hayo, Sarah alielekea sebuleni, alifikia kujitupa kwenye kochi kisha akatabasamu,

"sasa wao wameshika makali, mimi nimeshika mpini" Sarah aliongea peke yake huku akitabasamu, aliamini kufanya kabisa kwa kitendo kile cha kumshika Taita, basi tayari ameshaiweza kambi yote ya Taita, aliamini kinachofuata ni kuwaendesha tu kimabavu.

Sarah akasaula nguo pale pale sebuleni, kisha akaingia bafuni kujiswafi mwili, alitumia nusu saa ndani ya bafu, kisha alitoka na kuingia chumbani kwake, akavaa nguo za kulalia, kisha akatoka na kuelekea sebuleni, akaelekea kwenye friji na kutoa pakiti ya maziwa, akapitia kwenye kabati na kuchukua glass, akaelekea kwenye kochi kisha akawasha runinga, Sarah aliimaliza siku yake vizuri.

*************************

Sajenti Minja alikuja kuzinduka huku akiwa na maumivu sehemu za mbavu na kisogoni, hizo ndizo sehemu alizoshambuliwa na Sarah.

Sajenti Minja alipozinduka akatupa macho kushoto na hakuona kitu isipokuwa alama za matairi ya gari, alipotupa macho kulia aliweza kuiona gari yake ikiwa imewekwa pembeni ya barabara, akaisogelea na kuikagua kama kuna chochote kibaya, hakuona kitu chochote kibaya, Sajenti Minja akaingia ndani ya gari yake na kukaa huku akijishika kichwa kutokana na maumivu pia mawazo.

"huyu binti ni nani? mara ya pili hii tunakutana kiutata utata tu" Sajenti Minja alijiuliza mwenyewe huku akiangalia kama funguo ya gari yake ipo,

"huenda kweli ni mwanajeshi" Sajenti Minja aliongea kisha akawasha gari yake na kuiondoa kwa kasi.

Safari ya Sajenti Minja iliishia nyumbani kwake, hakutaka hata kupoteza muda, alipofika nyumbani kwake aliingia chumbani na kuwasha laptop yake kisha akaandika mambo yote aliyoyajua kuhusu huyo binti aliyemshambulia dakika chache zilizopita, kwake yeye aliamini huyo binti ni mtu mbaya sana, aliamini huyo binti anastahili kufuatiliwa kwa jicho la karibu sana.

*********************

Dokta Pendo hakutaka kabisa kuhama nyumbani kwake, na pia aliamini kuwa kundi la Taita alitomfanya kitu, kwa hiyo baada ya kuachwa na Sarah, alichofanya yeye ni kwenda moja kwa moja kuoga, alipotoka kuoga alitoka nje na kwenda kununua chakula, alirudi ndani na kula kisha akalala zake huku akibaki na maswali mengi kumuhusu Sarah, hakujua ni mtu wa aina gani, ni mtu mbaya au mtu mwema? Hakupata jibu sahihi, alichoamua ni Kulala usiku huo.

********,********

Asubuhi palipokucha, Dokta Pendo alidamka mapema na kujitayarisha kwa ajili ya kuwahi kazini, maana alikuwa na wasiwasi wa kufukuzwa kazi baada ya kutokwenda kazini katika siku iliyopita na hakutoa taharifa.

Dokta Pendo alitoka na kuchukua bajaj iliyompeleka mpaka kazini kwake, alipofika alielekea moja kwa moja ofisini kwa bosi wake, alipoingia alimsabahi,

"jana mbona hukuja kazini?" boss wake alimuuliza kwa ukali,

"nilikuwa na matatizo" Dokta Pendo alijibu kwa unyekekevu,

"taharifa ulimpa nani?" Boss wake aliendelea kumbana kwa maswali,

"kwa aina ya matatizo niliyoyapata ilikuwa ngumu kupata muda wa kuja hapa kazini na kutoa taharifa" Dokta Pendo alijibu,

"ni matatizo gani hayo?" Boss wake alimuuliza,

"nilitekwa, kuna mtu alinivamia juzi usiku na kuniteka?" Dokta Pendo alitoa jibu lililomuogopesha boss wake,

"na nani?" Boss aliuliza kwa mshangao,

"hata sijamjua mpaka sasa, maana aliniteka akiwa amejifunga kitambaa usoni na alinipa dawa iliyonifanya nipoteze fahamu, nilizinduka jana usiku na nilikuwa nipo ufukweni" Dokta Pendo alidanganya,

"basi kama ni hivyo, nenda katoe maelezo polisi kwanza, alafu ndio sisi tukupokee" Boss wake alimwambia,

"sawa, nashukuru" Dokta Pendo aliongea huku akinyanyuka na kuelekea nje, akachukua usafiri uliomfikisha mpaka kituo cha polisi, alipofika alienda mpaka kaunta na kumkuta askari akiwa amekaa eneo, akamueleza shida yake, yule askari hakuwa na uwezo wa kuisikiliza ile kesi, akamuonesha ofisi ya kwenda.

Dokta Pendo akaenda mpaka kwenye mlango mmoja, akagonga hodi, akaitikiwa kisha akafungua mlango ili aingie, alipofungua mlango tu alishtuka, maana mwenye hiyo ofisi ni Sajenti Minja,

"karibu ukae" Sajenti Minja alimkaribisha, Dokta Pendo hakuongea kitu ila alienda kukaa alipotakiwa kukaa, aliamini Sajenti Minja amemsahau,

"za tangu jana usiku?" Sajenti Minja aliongea huku akitabasamu na kumfanya Dokta Pendo ashtuke,

"sio nzuri" Dokta Pendo alijikaza na kujibu kwa sauti ya upole,

"naona umekuja kujisalimisha" Sajenti Minja aliongea huku akiandika andika mambo yake,

"sijaja kujisalimisha, nimekuja kutoa taharifa" Dokta Pendo alijibu,

"taharifa zipi?" Sajenti Minja aliuliza huku akiacha kuandika na kumuangalia Dokta Pendo,

"kuhusu yule dada uliyenikuta nae jana, aliniteka na kuniamrisha niendeshe ile gari yake, kuna mwingine alikuwa amemteka na alikuwa amekaa nae siti ya nyuma" Dokta Pendo aliongea,

"baada ya hapo?" Sajenti Minja aliuliza huku akiwa hamuamini kabisa yule mwanamke,

"baada ya kukamilisha kazi yake aliniachia" Dokta Pendo alijibu,

"alikuacha bila ya kukudhuru?" Sajenti Minja aliuliza,

"aliniacha kirafiki tu na kaniomba nisije kutoa taharifa polisi, pia nikamkubalia kuwa rafiki yake" Dokta Pendo aliendelea kutoa maelezo ambayo Sajenti Minja aliyaona ya kitoto tu.

"una namba yake ya simu?" Sajenti Minja alimuuliza,

"hapana" Dokta Pendo alijibu na kisha Sajenti Minja akacheka,

"sasa ndio rafiki gani hata namba yake ya simu huna? Unafanya kazi?" Sajenti Minja alimuuliza,

"ndio, mimi ni daktari wa hospitali binafsi" Dokta Pendo alijibu,

"vitambulisho vyako viko wapi?" Sajenti Minja aliuliza huku akiwa amemkazia macho, Dokta Pendo akatoa vitambulisho vyake na kuviweka juu ya meza, Sajenti Minja akaviokota na kuanza kuviangalia,

"sasa tukubaliane jambo moja, nitakupa namba yangu ya simu, huyo rafiki yako ukimuona popote unipe taharifa" Sajenti Minja aliongea huku akimrudishia Dokta Pendo vitambulisho vyake,

"sawa haina shida" Dokta Pendo alijibu,

"sawa unaweza kwenda" Sajenti Minja aliongea,

"natakiwa nipewe karatasi ambayo itaonesha kama nimekuja polisi kutoa maelezo, bila hivyo itakuwa ngumu kukubaliwa kurudi kazini" Dokta Pendo aliongea, kisha Sajenti Minja akachukua karatasi na kuiandika na kisha akampatia Dokta Pendo.

"asante" Dokta Pendo aliongea huku akiipokea ile karatasi kisha akaondoka zake, akarudi hospitali na kumpelekea boss wake kile kikaratasi alichopewa polisi, boss wake akamruhusu akaendelee na kazi.

**************

Mishale ya saa mbili usiku, Sarah alikuwa eneo la hospital akikagua kama Dokta Pendo ameenda kazini, kwa bahati nzuri aliweza kumuona Dokta Pendo akitoka, akamkimbilia na kumsalimia,

"umehamia wapi shoga yangu?" Sarah alimuuliza,

"sijahama shoga, nipo pale pale" Dokta Pendo aliongea na kufanya Sarah ashtuke,

"huogopi hata hali ya usalama wako?" Sarah aliuliza,

"hawatanifanya kitu shoga, mimi mwanamke bwana, nina mbinu za kupambana nao" Dokta Pendo aliongea huku akitabasamu,

"ingia kwenye gari nikupeleke, ila huame pale shoga, sio pazuri pale" Sarah alimsisitiza Dokta Pendo huku wakiingia kwenye gari,

"usijali shoga yangu, kuwa na amani tu" Dokta Pendo aliongea wakati Sarah akiondoa gari eneo la hospital,.

Ndani ya gari waliendelea na maongezi yao, ila kitu ambacho Sarah hakukijua ni kuwa muda huo Dokta Pendo alikuwa akichat na Sajenti Minja, alikuwa akimtaharifu kuwa yupo na Sarah na alimtaharifu kuwa muda huo wanaelekea nyumbani kwake yeye Dokta Pendo, Sajenti Minja akahakikishia kuwa anakuja muda sio mrefu.

Sarah alipofika mtaa ule anaokaa Dokta Pendo, aliiegesha gari yake mbali sana na nyumba ya Dokta Pendo, alifanya vile kwa sababu za kiusalama.

Wakatelemka na kutembea mpaka mlangoni kwa Dokta Pendo,

"karibu shoga" Dokta Pendo alimkaribisha Sarah,

"Mimi mwenyeji hapa shoga yangu" Sarah alijibu huku akitabasamu na pia alikuwa akiingia ndani. Wakaelekea sebuleni na kuanza kuongea, ila muda wote Dokta Pendo alikuwa akichat,

"ngoja nikakuchukulie soda" Dokta Pendo aliongea huku akinyanyuka,

"acha tu, usijisumbue" Sarah aliongea,

"sio vizuri bwana" Dokta Pendo aliongea huku akitoka nje.

Baada ya dakika mbili aliingia Dokta Pendo na soda mkononi, akaenda kukaa pembeni ya Sarah, mara ghafla mlango ukafunguliwa, alikuwa ni Sajenti Minja, Dokta Pendo akanyanyuka haraka na kukimbilia nyuma ya Sajenti Minja.

Sarah akabaki ameganda vile vile, hakutaka kugeuza sura yake mbele ya adui,

"hahaha atimaye leo nimekupata ukiwa huna mask usoni, geuka basi niione sura yako mrembo" Sajenti Minja aliongea huku akicheka na muda huo bastola ilikuwa mkononi, Sarah hakuwa na ujanja, alibaki akisali moyoni mwake Mungu amuepushe na kikombe kile............................

*********ITAENDELEA**********

the Legend☆
 
RIWAYA : SALA YA SARAH

MTUNZI : ALEX KILEO

SEHEMU YA ISHIRINI NA TISA

ILIPOISHIA.....................

Baada ya dakika mbili aliingia Dokta Pendo na soda mkononi, akaenda kukaa pembeni ya Sarah, mara ghafla mlango ukafunguliwa, alikuwa ni Sajenti Minja, Dokta Pendo akanyanyuka haraka na kukimbilia nyuma ya Sajenti Minja.

Sarah akabaki ameganda vile vile, hakutaka kugeuza sura yake mbele ya adui,

"hahaha atimaye leo nimekupata ukiwa huna mask usoni, geuka basi niione sura yako mrembo" Sajenti Minja aliongea huku akicheka na muda huo bastola ilikuwa mkononi, Sarah hakuwa na ujanja, alibaki akisali moyoni mwake Mungu amuepushe na kikombe kile............................

*********ENDELEA**********

Sarah aliendelea kuganda vile vile huku moyoni mwake akiamini amechezewa mchezo, na wala hakujisumbua kuwaza ni nani aliyemchezea huo mchezo, aliamini ni Dokta Pendo, taratibu aliamini ameshashikwa leo mtegoni ila akajiapiza endapo atapelekwa polisi, atatoroka ila akirudi uraiani, Dokta Pendo atakuwa mmoja kati ya watu wataopata patashika kutoka kwake.

"ina maana husikii nilichosema?" Sajenti Minja alihoji huku akiikoki bastola yake, Sarah akanyoosha Mikono juu, akasimama huku akijiandaa kugeuka, ila pasipo kutegemea kikasikika kishindo kizito Kama mtu amepigwa na kitu kizito, ndipo Sarah alipogeuka haraka, akamkuta Sajenti Minja akiwa yupo chini amepoteza fahamu na wakati huo Dokta Pendo akiwa amesimama huku ameshika kipande kikubwa cha jiwe,

"ondoka shoga yangu, kimbia shoga" Dokta Pendo aliongea huku akimtazama Sarah na kufanya Sarah abaki na mshangao huku akijiuliza kama Dokta Pendo ndio alimuitia askari, ni kwanini amsaidie?

"nikiondoka si utabaki hatiani?" Sarah alimuuliza Dokta Pendo,

"shoga wewe nenda tu, sitokosa cha kumdanganya" Dokta Pendo aliongea huku akiwa anamtazama Sarah,

"dah, nina maswali mengi kwa hiki ulichokifanya leo" Sarah alizungumza huku akiwa bado amesimama,

"utaniuliza siku nyingine, sasa hivi ondoka tu shoga yangu, huyu asije akaamka yakawa mengine tena" Dokta Pendo aliongea kwa hamaki,

"sawa, nashukuru kwa yote uliyonifanyia leo" Sarah aliongea kisha akatoka ndani ya nyumba ya Dokta Pendo na kumuacha akimpepea Sajenti Minja.

Baada ya dakika kumi za kuondoka kwa Sarah, Sajenti Minja alipata fahamu na kumkuta Dokta Pendo akiwa amevaa gloves huku pembeni kukiwa na chupa ndogo ndogo za dawa pamoja na pamba zilizokuwa na damu. Shati alikuwa ameondolewa na jirani yake kulikuwa na feni iliyokuwa ikimpuliza.

Sajenti Minja ndio akakumbuka tukio gani lililokuwa likiendelea hapo, akapeleka mkono wake kisogoni akasikia maumivu na pia akahisi amefungwa bandeji,

"ni nani alinipiga kisogoni?" Sajenti Minja alimuuliza Dokta Pendo,

"kwanza pole, wakati umemshikia bastola yule dada, kuna mwanaume ameingia na tofali na kukupiga nalo, alafu amemchukua yule dada ameondoka nae" Dokta Pendo aliongea kwa huruma, lakini maneno yote yalikuwa ya uongo,

"wewe hawajakudhuru?" Sajenti Minja aliuliza,

"kwa kweli hajanidhuru" Dokta Pendo aliongea,

"huyo mwanaume umeshawahi kumuona kabla?" Sajenti Minja aliuliza,

"ile sura ndiyo naiona leo, ila nikikutana nae mahala popote nitamkumbuka" Dokta Pendo aliongea na wakati Sajenti Minja alikuwa akiinuka,

"silaha yangu ipo wapi? au wameichukua?" Sajenti Minja alimuuliza Dokta Pendo,

"hiyo hapo chini ya meza" Dokta Pendo alijibu na kisha Sajenti Minja akainama na kuichukua, akaiweka kiunoni,

"kama nilivyokwambia kule ofisini, ukimuona tena huyu mwanamke au huyo mwenzake aliyekuja kumuokoa, nijulishe" Sajenti Minja alimkumbusha Dokta Pendo,

"usijali Kaka yangu, nitakutaharifu" Dokta Pendo alijibu, kisha Sajenti Minja akatoka zake nje huku akiwa amejishika kisogoni.

Sajenti Minja alivyotoka tu, Dokta Pendo akaenda kumchungulia kwa dirishani na kushuhudia Sajenti Minja akiingia kwenye gari yake na kuiondoa.

"mbona Sarah mtu mwema tu? Au hata kama ana ubaya wake hajawahi kunifanyia mimi, aliniteka na akanipa sababu za kuniteka, nikamuelewa na akanirudisha salama, sasa kwanini nimsababishie matatizo?" Dokta Pendo alijiuliza mwenyewe huku akiwa bado yupo pale dirishani.

Baada ya kukaa kwa muda pale dirishani, akaamua aende zake chumbani.

Akafika na kuvua zile nguo alizitoka nazo hospitali, kisha akaingia bafuni kuoga.

**********************

Usiku huu Sarah alirudi nyumbani kwake huku akiwa hamuamini kabisa Dokta Pendo, ingawa alimsaidia ila alipanga kujihadhari sana mbele ya Dokta Pendo ingawa alitaka kujenga urafiki ili amuamini ila aliamua kukaa nae mbali.

Mawazo hayo yote alikuwa anayawaza huku akiwa juu ya sofa ndani kwake. Ila kumbuka siku nzima ya leo hajaingia katika chumba chake cha siri kumuona Taita, aliyafanya yote kwa makusudi kwa ajili ya kumtesa Taita na njaa, aliamini kufanya hivyo kunaweza kumpa nafasi nzuri ya kumuuliza Taita na kujibu vizuri kutokana na njaa ambayo atakuwa nayo mjomba ake huyo.

Sarah akaitoa bastola yake na kuiweka juu ya meza, kisha akavua raba zake.

"hata leo sitoenda kumuona, acha akae na njaa ili aone watu masikini wanavyotesekaga na njaa" Sarah aliongea kisha akamalizia na sonyo kali, akanyanyuka kwenye kochi na kuingia chumbani kwake kwenda kupumzika.

********************

Asubuhi Sarah aliamka mapema na kufanya mazoezi kama kawaida yake, hutumia masaa mawili kufanya mazoezi mchanganyiko, baada ya hapo akaenda bafuni kujiswafi mwili wake, bafuni hutumia saa moja.

Akishatoka bafuni huenda sebuleni na kuwasha runinga, kisha huangalia taharifa ya habari na mambo mengine ya kisiasa, hapo pia hutumia saa moja na nusu, kisha huzima runinga na kuwasha radio kwa ajili ya kusikiliza mziki laini ambao hutumika kumuweka vizuri akili yake.

Ilipofika saa tatu na nusu, aliingia jikoni na kuandaa kifungua kinywa, baada ya dakika thelathini alimaliza na kwenda kwenye kabati na kutoa kikombe, akarudi jikoni na kumimina maziwa kwenye kikombe, akapakua na tambi na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba chake cha siri, ambapo alimfungia Taita.

Alipofungua tu mlango wa kile chumba, akawasha taa na kumfanya Taita afunge macho kutokana na macho yake kukosa mwanga kwa muda mrefu.

Sarah akaingia na kuvuta kiti kisha akakunja nne na kuanza kula huku akimuangalia tad Taita,

"husikii njaa?" Sarah alimuuliza Taita ambaye alikuwa akimuangalia kwa tabu,

"wewe Sarah we ndio wa kunifanyia hivi?" Taita aliuliza huku akimtazama Sarah,

"leo ndio umejua mimi naitwa Sarah? Si uwa unaniitaga malaya? Uwa nafurahi zaidi ukiniita malaya" Sarah aliongea huku akitabasamu,

"wewe ni mwanangu, kipindi nakuita malaya nilikuwa bado sijakutambua" Taita alijijitea

"nina maswali mawili tu kwako, la kwanza, kwa nini umemteka babu yangu?" Sarah aliuliza,

"nilimteka kwa sababu nilitaka nionane na wewe" Taita alijibu,

"haya tumeshaonana, ulitaka kuniambia nini?" Sarah aliuliza swali Lake la pili,

"nilitaka nikuombe msamaha kwa kile kilichotokea miaka kumi na tisa iliyopita" Taita alijibu,

"kwanza kabla hatujaendelea zaidi, nahitaji nyumba ya babu yangu mliyoichoma moto ijengwe" Sarah aliongea kisha akanywa maziwa,

"hiyo nyumba ikijengwa ndio utaniachia?" Taita aliuliza,

"ndio, endapo nyumba itajengwa nitakuachia" Sarah alijibu na kumfanya Taita atamani hata nyumba ijengwe ndani ya siku moja,

"kwanini nisinunue nyingine kwa jina la babu yako?" Taita aliuliza

"ni wewe tu, ili mradi babu yangu akitoka apate pa kuishi" Sarah alijibu,

"nisaidie simu niongee na Trigger" Taita aliongea,

"unataka kuongea nae nini?" Sarah alimuuliza,

"nataka nimwambie afanye hiyo kazi ya kununua hiyo nyumba leo hii hii ili mimi niwe huru" Taita aliongea,

"ngoja nimpigie" Sarah aliongea huku akiitoa simu yake mfukoni na kupiga namba ya Trigger, Trigger alipopokea, Sarah akampa simu Taita, Taita akaanza kuongea kwa kujuliana hali na kijana wake huyo kisha akamsisitiza sana akachukue pesa bank,

"nikachukue shilingi ngapi?" Trigger alimuuliza Taita,

"akachukue shilingi ngapi?" Taita akamuuliza Sarah,

"million sitini, nadhani nyumba ya million sitini itakuwa bomba zaidi" Sarah alimjibu Taita,

"Trigger akatowe million sitini" Taita alimpa jibu Trigger,

"alafu nazipeleka wapi?" Trigger akauliza,

"kanunue nyumba popote" Taita alijibu,

"lete hiyo simu" Sarah aliongea huku akimpora Taita simu,

"wewe mtumwa wa Taita, hiyo pesa inabidi unikabidhi usiku wa leo" Sarah aliongea na Trigger baada ya kumpora simu,

"sawa, tukutane wapi?" Trigger alijibu kwa sauti tulivu,

"nitakuambia baadae, ila naomba msifanye ujanja ujanja wowote, vinginevyo nitammaliza bosi wenu" Sarah Alimwambia Trigger,

"amini hakuna ujanja wowote utakaofanyika, ukija unachukua pesa yako na kuondoka" Trigger alijibu kwa upole, kisha Sarah akampa simu Taita na kumwambia awatahadharishe vijana wake wasifanye kitu chochote cha tofauti pindi atakapoenda kuchukua hiyo pesa usiku.

"Trigger huyu Sarah atakapokuja kuchukua pesa naomba msimgeuke wala msimshike, maana huku roho yangu nimeiweka rehani" Taita alimsihi Trigger,

"hatutakuwa na shida, aje na achukue huo mzigo" Trigger alijibu kisha Sarah akampora Taita simu na kobonyeza kitufe cha kukatia mawasiliano.

"hilo la Kwanza likiisha bila shida, kuna la pili" Sarah aliongea huku akinyanyuka kwenye kiti,

"la pili lipi tena? Si baada ya kupata pesa utaniachia?" Taita aliuliza,

"sio baada ya kupokea pesa, baada ya kupata nyumba ndio nitakuachia" Sarah aliongea huku akiondoka, na kumuacha Taita asijue la kuongea, baada ya muda Sarah alirudi akiwa na chakula na kukiweka mbele ya Taita, kisha akamfungua kamba.

"kula mjomba, nitarudi baadae" Sarah aliongea kisha akazima taa na kutoka zake nje akimuacha Taita akiwa hana la kuongea.

******************

Muda wa saa tano usiku, Sarah akiwa amevaa kikazi aliegesha gari yake, kisha akashuka na kutembea mwendo wa dakika ishirini na kuingia kwenye jengo moja la ghorofa ambalo halijakamilika.

Alipanda mpaka juu ya ghorofa na kumkuta Trigger akiwa ameshika begi jeusi kubwa,

"naona umekuwa sasa" Trigger aliongea huku akimuangalia Sarah,

"nimefuata pesa, sihitaji habari nyingine" Sarah aliongea huku akiwa amesimama,

"chukua hizi hapa" Trigger aliongea na kumtupia Sarah lile begi, Sarah akalidaka na kuanza kuondoka. Wakati akiwa amepiga hatua tatu, mbele yake waliibuka vijana kama ishirini wote wakiwa na bastola, alipogeuka nyuma akakuta vijana wengine wengi wakiwa wamesimama na Trigger na wote wana bastola,

"wewe unadhani mjanja nani kati yetu na wewe?" Trigger aliuliza huku akiijaza bastola yake risasi............

**********ITAENDELEA************

the Legend☆
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom