RIWAYA : SALA YA SARAH
MTUNZI : ALEX KILEO
SEHEMU YA THELATHINI NA NNE
ILIPOISHIA.................
Sarah alivyofika eneo hilo, alishuka kwenye gari na kuanza kukagua mazingira yale kama kuna mtu yoyote anaweza kuwepo kwenye mazingira yale, alijiridhisha hakuna mtu na pia akiwa amejiaminisha kuwa hata yule aliyekuwa akimfuatilia hawezi tena kufika hapo, Sarah alienda kwenye mlango wa nyuma wa gari yake na kuufungua, akamtoa Taita, kwa kuwa hakuwa na nguvu ya kumbeba, alichofanya ni kumbingirisha tu, alimsukuma mpaka kwenye mtelemko uliopo mwishoni mwa dampo, kisha akauachia hapo mwili wa Taita ukiwa unaseleleka kuelekea bondeni, Sarah akawa amechuchumaa akiuangalia namna unavyobingirita,
"dah, sijapenda, amekufa kirahisi sana" Sarah aliongea peke yake kisha akisimama, alipogeuka nyuma akakuta mtu akiwa amesimama kama hatua kumi kutoka alipo yeye na alikuwa akimuangalia, ila kutokana na giza lile ilikuwa ngumu kuonana sura, Sarah akajipapasa kiunononi kuiangalia bastola yake, hakuikuta, akakumbuka ameisahau ndani ya gari, wakati Sarah akiendelea kutafakari huku akijiuliza yule mtu ni nani usiku ule, pembeni ya yule mtu akaongezeka mtu mwingine, Sarah akachoka kabisa, na muda huo wale watu wawili wanaume wakaanza kupiga hatua kuelekea alipo Sarah, Sarah alipotazama nyuma kuangalia njia nyingine, bahati mbaya hakukuta njia, njia ilikuwa moja tu, ambayo ndiyo hiyo iliyo mbele yake na ubaya kuna wanaume wawili walikuwepo wanamfuata.............
*********ENDELEA*********
Sarah akaanza kurudi nyuma huku hofu ikimzidi,
"sister saula, hili chaka uliloingia sio" kijana mmoja aliongea kwa sauti nyembamba iliyotokea puani na kumfanya Sarah ajue kuwa huyo ni teja,
"fasta kabla hatujakugeuza bucha" kijana wa pili aliongea huku akivuta panga kutoka kiunoni mwake.
"ngojeni, mnataka nini?" Sarah aliuliza huku akirudi nyuma,
"toa kila kitu sister" kijana wa kwanza alijibu huku akiwa karibu kabisa na Sarah, Sarah akapiga hesabu za haraka haraka kisha kwa kasi ya ajabu akamruka kijana wa kwanza na kutua mbele ya kijana wa pili yule mwenye panga, yule kijana akabaki na mshangao kwa namna Sarah alivyofanya,
"habari yako" Sarah aliongea huku akimuangalia yule kijana kisha Sarah akaachia teke kali lililomkuta yule kijana usawa wa shavu, yule teja akaenda chini na panga likamtoka mkononi, kisha Sarah akapiga sarakasi ndogo na kuokota lile panga kisha akageuka nalo na kumkuta yule kijana mwingine akija kwa kasi huku akiwa na bisibisi mkononi, Sarah akapiga hatua moja kumuelekea kisha akamuwekea panga shingoni kama anataka kumchinja,
"shida nini baba?" Sarah alimuuliza huku akitabasamu, lakini yule kijana hakujibu kitu, alikuwa akitetemeka tu, Sarah akatoa panga shingoni kwa yule kijana kisha akalitupa panga chini na kuondoka zake kwa mwendo wa haraka na kuwaacha wale vijana wakimuangalia tu huku wasiamini kile walichofanyiwa.
Sarah akaelekea kwenye gari lake na kuingia kisha akaliondoa kwa fujo kurudi nyumbani kwake huku akifungua mziki mzito ndani ya gari.
Sarah alifika nyumbani kwake na kukimbilia kwenye kioo na kujiangalia usoni kama amedhurika na mapigo ya Aisha, hakuona jeraha lolote,
"mpumbavu yule, amekariri pigo la aina moja tu, siku nyingine namuua ili huyo Harry apate fundisho" Sarah aliongea huku akielekea kwenye chumba chake cha siri na kukisafisha kisha akaelekea bafuni kuoga huku akiisubiri siku mpya ambayo aliamini itakuja na habari mbaya kumuhusu Taita.
**************.
Aisha alishtuka asubuhi akiwa amelala sakafuni huku akiwa na maumivu na damu baadhi ya sehemu za mwili,. Aisha akajivuta na kusimama, alijitahidi kuinuka ingawa alihisi mwili ukimuuma, akaenda kukaa kwenye kochi na hapo ndipo kumbukumbu zikamrejea juu ya tukio lililomkuta mpaka akafikia katika hali aliyokuwa nayo muda huo,
"kumbe yule mwanamke ni mwendawazimu" Aisha aliongea baada ya kukumbuka alichofanyiwa na Sarah, na hapo akahisi mlango ukigongwa, Aisha akanyanyuka na akauendea mlango kwa tahadhari sana huku mkononi akiwa na bastola yake, nae mgongaji hakuchoka kugonga mlango, aliendelea tu, na safari hii alizidisha nguvu ya ugongaji.
Aisha akausogelea mlango kisha akaangalia na kugundua upo wazi, akapiga hatua tatu nyuma na kuishika vizuri bastola yake, aliielekezea mlangoni,
"karibu, mlango upo wazi" Aisha aliongea huku macho yakiwa mlangoni, mlango ukafunguliwa na kisha mgongaji akaingia ndani,
"wewe ni mimi, usipige risasi" Harry aliongea baada kuingia ndani na kukutana na mdomo wa bastola,
"kumbe ni wewe boss, nilijua yule malaya amerudi tena" Aisha aliongea huku akikaa kwenye kochi, Harry akamtazama sura yake na kuona jinsi ilivyokuwa nyekundu, Harry hakupata tabu kugundua kuwa sura ya Aisha kuwa vile ni kutokana na kipigo,
"nani, Sarah?" Harry aliuliza,
"ndio huyo huyo" Aisha alijibu huku akiangalia pembeni,
"alikuja muda gani?" Harry aliuliza,
"muda mchache baada ya nyinyi kuondoka" Aisha alijibu,
"hujamuua?" Harry aliuliza swali la kizembe,
"wewe mjinga nini, ningekuwa nimemuua ungenikuta nimeshika bastola namna ile?" Aisha aliuliza kwa jazba baada ya kuhisi Harry anamdhiaki,
"ilikuaje sasa?" Harry aliuliza,
"ameingia hapa na nimemdhibiti vizuri tu, ila nimefanya kosa dogo ndio amefanikiwa kunikimbia" Aisha aliongea,
"umemdhibiti au alikudhibiti? kama wewe uliyemdhibiti upo kwenye hali hiyo, je huyo aliyedhibitiwa yupoje?" Harry aliuliza,
"naona imani imepungua kwangu, ni bora niachane tu na kazi yako kama huniamini" Aisha aliongea,
"nakuamini sana Aisha, ila naona kama kazi imekuwa ngumu kwako ila unashindwa kukubaliana na hilo jambo" Harry aliongea,
"mzee unatakiwa utulie, kazi naifanya mimi, nikishindwa nitakurudishia pesa yako uliyonipa hawali" Aisha aliongea kwa jeuri,
"basi yaishe, tunatakiwa kuondoka muda huu, maana hapa sio kwetu" Harry aliongea huku akinyanyuka kwenye kochi na Aisha nae akasimama kisha wakatoka zao ndani ya ile nyumba ya Dokta Pendo na wakaondoka zao.
**** *********
Dokta Pendo alikuwa bado amefungiwa kwenye chumba kidogo ambacho hakikuwa na hewa ya kutosha, na isitoshe alikuwa amepigwa sana kutokana na kiburi chake cha kutosema ukweli kuhusu njia ya kumshika Sarah, Dokta Pendo alikuwa Hoi bin taaban, hawezi kutembea, miguu ilikuwa imevunjwa na Trigger, Dokta Pendo alibakiwa na sauti ya kuongelea,
"ujue mimi nitakuua, sifanyi utani, nipe namba za Sarah" Trigger aliongea huku akiwa amevaa vest iliyokuwa na damu sehemu kubwa,
"niue tu, maana hicho ndicho kilichobakia, niue, unasubiri nini!?" Dokta Pendo aliongea kwa uchungu huku akilia, Trigger akamrushia konde zito na kumpiga Dokta Pendo ngumi ya mdomo, Dokta Pendo akapiga kelele za maumivu,
"kuua ni jambo dogo tu kwangu, tena kwa mtu jeuri kama wewe uwa nafurahi sana ninapokuua" Trigger aliongea huku akitoa tabasamu la kifedhuli bila kujali maumivu anayoyapata Dokta Pendo,
"najua wewe ni muuaji mzuri, na ndio maana mkamuulia Sarah wazazi wake na pia mkamteka babu yake" Dokta Pendo aliongea kwa hasira, alishaamua liwalo na liwe,
"kumbe mnakaaga na kuongea hayo mambo eeh?" Trigger aliuliza huku akiokota kipande cha nondo, alipania kumpiga nacho Dokta Pendo kichwani,
"Niue, nimalize nikapumzike" Dokta Pendo aliongea huku akikilaza kichwa chake sakafuni, alishajikatia tamaa. Trigger akakinyua juu kile kipande cha nondo, Trigger alidhamiria kummaliza Dokta Pendo, Trigger aliinyanyua nondo juu, kisha akawa anajiandaa kuishusha kichwani kwa Dokta Pendo,
"wewe vipi? Usimpige bwana" Harry aliongea huku akiingia mule ndani, aliongozana na Aisha,
"ana kiburi sana, ananijibu hovyo" Trigger aliongea huku nondo ikiwa bado ipo hewani,
"sasa ukimuua si ndio utaharibu kabisa, utakuwa umeharibu mtego wetu" Aisha aliongea huku akimtazama Trigger,
"Trigger hizo bangi unazotumia kwa sasa hazikupeleki vizuri, unakuwaje sijui, yaani hujielewi kabisa" Harry alimlaumu Trigger,
"kumuacha huyu itakuwa kosa kubwa sana" Trigger aliongea huku akiwa bado anaonesha hasira za wazi kwa Dokta Pendo,
"Aisha ebu mchukue huyo dada na umpeleke kule chumba kingine" Harry aliongea kisha Aisha akaenda sehemu alipo Dokta Pendo na kumnyanyua, cha ajabu Dokta Pendo alishindwa kusimama, alikuwa akilia tu,
"Boss, huyu miguu hana tena, tayari imeshavunjwa" Aisha aliongea huku akimtazama Harry,
"dah, Trigger bangi unazovuta sasa hivi zinakukataa, unakuwa kama kichaa, yaani hueleweki kabisa" Harry alimlaumu Trigger ambaye alikuwa akivaa fulana yake,
"huyu sio wa kuwekwa ndani, tuangalie namna ya kumfikisha hospitali" Aisha aliongea kwa huruma,
"huyu tukimpeleka hospitali itakuja kuwa shida kwetu akipona" Trigger aliongea kwa hasira,
"Aisha ebu toka nje mara moja" Harry aliongea huku anamuangalia Aisha, Aisha akaenda zake nje, ingawa alihisi kuna jambo baya linaweza kutokea juu ya Dokta Pendo. Aisha akaenda zake nje,
"wewe unataka tufanye nini? " Harry alimuuliza Trigger,
"huyu afe tu, hakuna njia nyingine" Trigger alijibu,
"usimuue, maana hapo alipo tayari hana uwezo wa kuishi hata siku mbili, cha msingi ni kwenda kumtupa tu" Harry alitoa ushauri,
"sawa, hilo nalo ni wazo zuri" Trigger aliongea,
"sawa, usiku utafanya hivyo" Harry alimwambia Trigger,
"poa" Trigger aliongea kisha wakawa wamemaliza kwa mtindo huo, wakaachana na kila mmoja akaelekea kwenye jukumu lake.
*******************
Asubuhi hii ilimkuta Sajenti Minja akiwa ofisini kwake na mawazo yalikuwa juu ya ile gari nyeusi ambayo inamilikiwa na mwanamke ambaye alimchukulia ni hatari sana, na mbaya zaidi usiku uliopita aliweza kuiona hiyo gari na alijaribu kuifukuzia lakini hakuipata.
Akiwa kwenye mawazo hayo, alishtuliwa na simu yake iliyokuwa inaita, alipotupia macho kwenye kioo cha simu, alikuta jina la bosi wake, akapokea simu haraka,
"naam mkuu" Sajenti Minja aliongea kikakamavu,
"nenda eneo la dampo kuu, kuna mwili wa mtu umeokotwa" Mkuu wa polisi aliongea na kukata simu.
Sajenti Minja akainuka na kutoka mpaka kwenye gari yake, akaingia na safari ya kwenda dampo kuu ikaanza, ilimchukua dakika kumi kufika dampo kuu.
Alishuka na alikuta kuna askari wengine wakiwa eneo hilo, na ndani ya gari walikuwa wameupakia mwili. Sajenti Minja akawasalimu wenzake, kisha akatupia macho kwenye ule mwili, ndipo alipomuona mtu mzima akiwa amelala, alikuwa ni Taita, ila Sajenti Minja hakuweza kumjua kwa kuwa mwili wa Taita ulikuwa umevimba.
"mmepata habari yoyote kuhusu huu mwili?" Sajenti Minja aliuliza,
"kuna vijana wawili wanadai walimuona mtu aliyekuja kuutupa mwili" askari mmoja alijibu,
"wako wapi?" Sajenti Minja aliuliza,
"wale pale waliokaa pale" askari aliongea huku akiwaoneshea kidole,
"kwanini mmewaacha sasa?" Sajenti Minja aliuliza kwa ukali,
"tumewaona ni mateja, tukahisi wanataka pesa tu" askari alijibu,
"wajinga kabisa nyie, huo ndio ushahidi, niwakute ofisini kwangu wale vijana" Sajenti Minja aliongea huku akielekea mahali ilipo gari yake, kisha akaiwasha na kuondoka.
***************/****
Sajenti Minja alirudi ofisini kwake na kuwakuta wale vijana wakiwa nje ya ofisi yake wakimsubiri, Sajenti Minja akawasalimia kisha akawataka waingie ofisini,
"bila kupoteza muda, mnaweza kunieleza chochote kuhusu ule mwili uliookotwa kule dampo kuu?" Sajenti Minja aliuliza huku akiwatupia jicho,
"sisi tuliona gari nyeusi kali, ikipaki, kisha tukamuona mwanamke akishuka na kwenda kufungua mlango wa nyuma wa gari na kumtoa mtu na kwenda kumtupa" Teja wa kwanza alielezea, kipindi chote Sajenti Minja alikuwa amesisimka mwili kutokana na maelezo ya huyo Teja, kwani mtu anayezungumziwa ndiye yule yule anayemtafuta.
"huyo mwanamke mlifanikiwa kumuona kwa karibu?" Sajenti Minja aliuliza,
"tulimuona vizuri ingawa kulikuwa na giza, Maana tulimfuata" Teja wa kwanza alijibu,
"Mimi mpaka gari yake naijua, nimeikariri vizuri tu" Teja wa pili aliongezea,
"namba za gari yake umezikariri?" Sajenti Minja aliuliza,
"sio namba, ile gari nimeikariri tu, range Rover nyeusi" Teja wa pili alijibu,
"majina yenu" Sajenti Minja aliuliza huku akiwaangalia,
"mi naitwa Juma John" Teja wa pili alijibu na Sajenti Minja akaandika,
"andika salum dengo" Teja wa kwanza akajibu na kisha Sajenti Minja akaandika,
"mnaweza kwenda, ila mkimuona huyo dada au mkiiona gari yake, mje mnipe taharifa, nitawapa pesa" Sajenti Minja aliongea,
"usijali kamanda, tutakutimbia tukimdekshia" Teja wa kwanza aliongea huku wakitoka nje na kumuacha Sajenti Minja akiwaangalia huku akitabasamu.
Wale mateja wakatoka mpaka nje ya ofisi, na wakati huo Sarah alikuwa akiegesha gari yake nje ya ofisi za polisi. Wale mateja wakamuona,
"mzeebaba, yule dada si yule pale" Teja wa kwanza aliongea huku akimtazama Sarah aliyekuwa akatelemka kwenye gari,
"ndio yeye, hata gari ndio lile lile" Teja wa pili alijibu,
"wewe baki hapa mtazame anapoelekea, mimi ngoja nikamtonye kamanda" Teja wa kwanza aliongea huku akielekea ofisini kwa Sajenti Minja. Alipofika aliingia moja kwa moja ofisini, mpaka Sajenti Minja akashtuka,
"Baba kama zali, huyo demu Aliyefanya unyambilisi nae ndio anaingia kituoni, yupo hapo nje" Teja alitoa taharifa iliyomsisimua Sajenti Minja,
"yupo nje?" Sajenti Minja aliuliza kama hakusikia vile,
"Babu tuwahi, tusipoteze muda" Teja aliongea huku akigongesha mikono kwa msisitizo.
Sajenti Minja akanyanyuka na kuanza kuelekea nje, huku yule teja akija kwa nyuma yake na mwendo wake wa kutembea bega moja likiwa chini...........
*********ITAENDELEA**********
the Legend☆