SEHEMU YA MWISHOO
Bunduki ilikuwa haipo katika kiwambo cha kuzuia sauti
ilitoa mlio mkubwa sana baada ya Rama kufyatua.
Alikuwa amefyatua hewani
Mama Jose akaanguka chini, akawa amemwangukia
Jose. Jose akaanza kulia.
Kilio chake kikapenya katika masikio ya Rama…..
Akajikuta anaishiwa nguvu, akaishusha bunduki yake
chini.
Akakimbilia alipokuwa mama Jose akamkwapua mama
Jose huku akiwa makini kabisa kumtazama Sajenti
asije kuzua balaa lolote.
“Rama… sajenti aliita, “ kisha akaendelea “sio muda
huu Rama, sio muda huu hatuwezi kuzungumza lakini
elewa kuwa hili ni pumbazo….” Alitaka kuendelea
kuzungumza lakini ghafla akapokea pigo maridhawa
kutoka kwa Rama. Lilikuwa pigo ambalo hakulitarajia,
teke kali likatua katikati ya miguu yake.
Sajenti akatoa kilio kikubwa haswa cha uchungu.
“Nyamaza mwanangu!!” Rama alimbembeleza Jose
aliyekuwa akitokwa na kilo kikubwa bado.
“Rama hebu nisikilize kidogo!” alisihi sajenti. Rama
akamtazama lakini hakusema neno lolote.
“Rama unalodhani si sawa hata kidogo, tuondoke eneo
hili si salama kwetu hata kidogo. Tazama Rama
ningekuwa na nia mbaya nisingefyatua risasi na
kumuua huyo bazazi aliyetaka kukumaliza, kwanini
nisimwache akuue ili nifanye hayo unayowaza kuwa
nilikuwa nafanya!! Rama kuwa mwanaume imara sina
nifanyalo na mkeo, nimekuwa nikimlinda…”
alizungumza kwa kufoka sajenti.
Rama akaanza kuingiwa na yale maneno, na palepale
sajenti akatokwa na teke kali la haja likaipiga ile
bunduki ikarushwa mbali.
Rama aliyekuwa amebeba mtoto akataka kuikimbili
lakini tayari Sajenti alikuwa ameokota bunduki yake
kisha akamwonya Rama asipige hatua zaidi.
“Kwa hiyo unataka kuniua ili umfaidia mke wangu
sajenti…” alizungumza kinyonge.
“Niue lakini usimwache mwanangu hai.. tuue sote.
Ubaki na mwanamke wako..” alimalizia Rama.
“Rama mimi ni mtu mzima, unajua kuhusu familia
yangu Rama.. nimewahi kukueleza hapo kabla familia
yangu ni kitu cha muhimu kupita kitu kingine duniani,
Rama nipo hapa kwa sababu tu nimetakiwa kuwepo
sijawahi na wala sina mpango wowote wa kushiriki
dhambi hii unayonitamkia. Rama mtandao wa Vonso
umechachamaa, ni hawa waliotaka kukuua dakika
kadhaa nyuma, Rama hatupo sehemu salama. Simama
kama mwanajeshi weka haya mambo kando!” akasita
akameza mate kisha akatoa amri.
“Ninazungumza kama mkuu wako wa kazi sasa, mpatie
mtoto mama Jose kisha pick up the gun tunaingia
vitani!!”
Ilikuwa sauti ya amri haswa Rama akatii!
Lakini ni kama alichelewa sana kutii, walijikuta
wamezungukwa na watu wanne wenye silaha nzito
kabisa.
Hakuna ambaye alithubutu walau kufyatua risasi
kutoka katika bunduki yake.
Wakatekwa na kufungwa vitambaa vyeusi usoni,
wakapakiwa katika gari na watu wasiowajua.
Ndani ya gari sajenti alimlaumu Rama kwa kuendeshwa
na hisia zaidi kuliko uhalisia
_____
MWAKA 1965, Visiwani Zanzibar.
ILIKUWA imepita miaka miwili bada ya mapinduzi ya
Zanzibar yaliyofanya kisiwa hiki kuwa huru kutoka
katika utawala wa mwarabu.
Waarabu ni moja kati ya watu ambao hawakufurahia
kabisa jambo hili kwa sababu walizoea kuishi katika
kisiwa hicho. Lakini si waarabu pekee wapo waswahi
wachache ambao pia hawakufurahia jambo hili.
Mmoja kati ya waswahili hao alikuwa ni Sameer bin
Alafat ambaye baadaye alibadili jina lake na kujiita
Vonso Almeida, jina alilotunukiwa na mtawala wake
ambaye ni mwarabu.
Huyu alikuwa ananeemeka kutokana na uwepo wa
waarabu, aliwafanyia kazi na kuwanyenyekea
walivyotaka na kujikuta akiipata ridhiki yake kiulaini
sana.
Kuna waswahili walikuwa wakimchukia lakini hakujali
kwa sababu kila mmoja alikula kwa jasho lake.
Kitu cha msingi ni kwamba katu hakuwahi kuvujisha
siri zozote alizojua kuhusu harakati za kuusaka
uhuru.
Waarabu walimpenda kwa sababu ya unyenyekevu
wake, na hata baada ya uhuru walimuuliza iwapo yupo
tayari basi waende naye Oman.
Vonso akakubaliana nao.
Aliyazoea mazingira ya Oman upesi sana na ni huko
alipujifunza mengi kuhusu waarabu, aligundua kuwa ni
watu wasiopenda kufanya kazi za mikono, badala yake
wanapenda kufanyiwa kila kitu.
Hizi kazi yeye aliziweza na aliamini kuwa wazanzibari
wengi tu wanaziweza kwa sababu walizoea suluba za
utumwa.
Akiwa ametimiza umri wa miaka thelathini mnamo
mwaka 1975 akiwa sawa kabisa na waarabu wa Oman,
Vonso alianza kuwatafutia neema wazanzibari
wenzake. Kila akienda Zanzibar anaondona na
wanaume watano na wasichana watano na kuwapeleka
Oman kufanya kazi ambapo walikuwa wanapata malipo
mazuri kabisa.
Waarabu wenginje waliposikia juu ya hili na wao
wakaanza kumsumbua Vonso awatafutie wafanyakazi.
Hatimaye mwaka 1980 Vonso akafungua kampuni yake
ya kusaidia watu kupata ajira akaiita Vonso Almeida!.
Kampuni hii ilimwingizia kipato, lakini pia ukawa
mwanzo way eye kupumzika na kuwaacha watu
wengine wasafiri kwenda Tanzania bara na visiwani
kusaka wanaohitaji kufanya kazi nje ya Tanzania.
Kuna tetesi zilianza kuvuma miaka ya 1985 ambazo
zilimtesa sana Vonso ambaye ni mcha Mungu!
Alisikia kuwa kuna baadhi ya vijana wake wanachukua
rushwa ya ngono kwa wanawake kabla ya kuwafikisha
Oman ambapo wanakuja kufanya kazi.
Alilikemea jambo hili lakini hakutajiwa muhusika,
kampuni nayo ikazidi kuwa kubwa!
Mnamo mwaka 1990 kesi zikawa nyingi sana za
unyanyasaji, sasa haikuwa kutoka kwa waswahili peke
yao bali waarabu kwenda kwa waswahili.
Vonso alikuwa anawaheshimu sana waarabu kwa jinsi
walivyomtunza kuanzia uvulana hadi anakimbilia uzee
wake.
Kuliko kuzua mabishano nao, akaamua kung’atuka
katika kiti chake cha ukurugenzi.
Akawaambia maneno yake machache sana, wenzake
ambao wote walikuwa wanamzidi kisomo.
“Kama mnalofanya mnalijua ni dhambi na mnalificha
huku mkiendelea kulifanya wallah! Nawaapia mwenyezi
Mungu atawahukumu siku moja…!
Wasomi wakacheka wakampuuza!
Vonso akaondoka lakini hakuwakabidhi hati wala
katiba ndogo ya kampuni yake.
Akarejea Tanzania bara badala ya Zanzibar, akaanza
kufanya ujenzi na kisha akahamia nyumbani kwake
maeneo ya Kitunda akatulia tuli akajisahaulisha kabisa
kama aliwahi kuwa na kampuni kubwa kabisa iliyokuwa
inamuingizia pesa.
Na ili asahau zaidi juu ya ile kampuni, alipotua pale
Kitunda akajitambulisha kwa jina la David Magea!
Wakamzoea kwa jina la mzee Magea.
Maisha yakaendelea!
Miaka inakatika na sasa yupo mikononi mwa akina
Geza usiku wa manane pakiwa na hekaheka juu ya
kampuni yake inayojishughulisha na biashara ya
utumwa wa kisasa.
Si kijana tena sasa ni mzee!
Maelezo ya Vonso yaliwagusa sana Inspekta na Geza,
wakamuuliza maswali mawili matatu.
Akaelezea kila alichokuwa anakitambua.
Geza akamwagiza Inspekta waende kuwahifadhi mahali
Vonso na mjukuu wake ili wao waingie kazini moja kwa
moja.
Ikawa hivyo!
_______
MAKUTANO YA PUMBAZO
KIMYA kilikuwa kimetanda haswa, na giza lilikuwa
limetawala. Baadaye taa ikawashwa…
Mateka kadhaa wakaonekana wakiwa na vitambaa
vyeusi usoni.
Hakuna mateka aliyepewa nafasi ya kujitetea zaidi ya
kuitwa jina lake na anapoitika anasogezwa mbele zaidi
katika foleni.
Liliitwa jina la Ramadhani, akaitwa Sajenti Pilipili,
akaitwa Mama Jose, akaitwa Jose yule mtoto
akawekwa peke yake huku analia, hakuna aliyejali,
akaitwa mzee Fidelis, akaitwa Rabitt Sungura, lakini
hakuwa amepatikana bado.
Kisha kikafua kitendo cha bunduki kuandaliwa kwa ajili
ya kuwaondoa katika uso ule wa dunia kwa kosa la
aidha kugundua juu ya harakati za chimbo la mauti
ama namna yoyote ile.
“Geza….. chukua wawili na mimi nachukua wawili wale
wenye silaha…” alinong’ona inspekta Zay B kutokea
katika kona waliyokuwa wamejificha wakiwa
wameingia mapema zaidi kuliko kundi lile la watu
wengi… alipomgeukia Geza aligundua kuwa Geza
alikuwa akibubujikwa na machozi.
Ilikuwa mara yake ya kwanza kabisa kumuona Geza
katika hali ile hakuweza kuhoji kwa sababu muda
ulikuwa unazidi kwenda.
Inspekta akahesabu hadi tatu kisha akafyatua risasi
akiwaangusha wale wawili lakini Geza alimfyatua
mmoja tu na hakutumia risasi tena akatoka mbio
kutoka katika lile ficho.
Inspekta akabaki kuduwaa ni nini kilikuwa kinamsibu
Geza.
Geza akajirusha na kumkamata yule bwana aliyediriki
kumshika yule mtoto na kumweka katika orodha ya
wanaostahili kufa bila kujali kilio chake. Alikibamiza
kichwa cha yule bwana chini mara kadhaa akaamka
naye akajirusha naye chini.
Kwa kifupi Geza aliua kwa hasira kali zaidi kuliko mara
zote alizowahi kuua.
Baada ya hapo alisimama akiwa amelowa damu.
“Sina mtoto lakini ole… ole kwa atakayediriki katika
hii dunia kumnyanyasa mtoto mdogo mbele yangu..”
alisema huku akimsogelea Jose, akamfungua kile
kitambaa cheusi na kumkumbatia.
“Ba…. Ba….” Jose alisema kwa sauti ya kitoto
toto….
Zay b akatokwa machozi.
Baada ya dakika kadhaa Zay B alikuwa anapiga saluti
ya heshima mbele ya Sajini Pilipili.
Rama alikuwa amekumbatiana na mkewe huku
wakihofia kumwomba Geza awapatie mtoto
aliyeonekana kumzoea na kumpenda tayari.
Fahamu zilikuwa zimerejea kwa mzee Fidelisi na
dereva wa bodaboda, wao walikuwa wakijiuliza kulikoni
na hakuna aliyewajibu.
“Vonso ni mtu hatari sana..” Sajenti alisema, Geza
akacheka kwa sauti…. Hii ilikuwa mara yake ya
kwanza kutokwa na kicheko kikubwa vile.
Inspekta Zay B akaelezea kwa kifupi juu ya Vonso na
hapo akampa pole Rama kwa yaliyomsibu.
“Mbona uliniacha nikatekwa Zay B” Rama alihoji.
“Nilipokupungia mkono nilikuwa nimetekwa tayari…
tumshukuru Mungu kuwa tupo hai.” Alijibu kwa sauti
tulivu yenye mahadhi ya Zanzibar.
Rama akatabasamu.
_____
Mwili wa Rabbit Sungura ulikutwa katika ufukwe wa
bahari ya hindi jijini Dar es salaam ukiwa ulishapoteza
uhai muda mrefu sana.
Nchi za Tanzania na Oman zilishirikiana kikamilifu
kuwatia nguvuni wote waliohusika katika mkakati huu
wa kiuaji.
Maafisa wa uhamiaji walikamatwa kwa fujo katika
msako huo, huku wengine wakikutwa na hatia.
Wahusika katika mpango huu walifikishwa mbele ya
sheria, wale wa Tanzania walihukumiwa maisha jela
huku wale wa Oman wakihukumiwa kunyongwa.
Wakati haya yanatokea familia ya Rama pamoja na ile
ya Aneth kwa pamoja walikuwa wanasheherekea upya
harusi ya watoto wao hawa.
Watu baki kadhaa akiwamo Nasra walijumuika pia
katika hili
Yaliyopita si ndwele ndo walivyosema!!
Geza kama kawaida yake, alipotea katika uso wa
wanadamu na kuendelea na maisha yake mbali kabisa
na jiji la Dar es salaam, hakuwepo hata katika ule
mgao wa zawadi kubwa waliyotunukiwa wote
walioshiriki katika kung’amua uozo huu wa miaka
kumi.
Sajenti Pilipili na Inspekta Zainabu walipandishwa
vyeo, huku IGP akirejeshwa kazini baada ya
kupelelezwa na kuonekana hausiki na hakujua juu ya
mwanaye kushiriki katika mkakati ule.
Umoja kati ya Oman na Tanzania ukazidi kukua
maradufu huku ulinzi ukiimarishwa zaidi ili tukio kama
hili lisiweze kutokea tena asilani.
Ile siku IGP anarejeshwa kazini alipokea ujumbe
kutoka katika namba mpya.
“Ujue hadi leo sijalipia zile bia pale baa
walipokunywawale mademu! Mtume Pilipili
anapafahamu wanadai kama elfu sita mia tano hivi!
Msalimie Zay B mwambie tutakutana tena”
Mtuma ujumbe hakuandika jina lake, lakini IGP
alijikuta anatabasamu.
“Vipi mkuu!” alihoji sajenti akiwa pamoja na IGP.
“Geza kanitumia ujumbe….”
Wakajikuta wanacheka kwa pamoja, safari hii wote
walikuwa wanamjua vizuri!
Na huu ndo mwisho wa riwaya hii ya Pumbazo.
Ni Tungo kutoka kwa mwandishi George Iron Mosenya,
tungo hii ni haikuwa na nia yoyote mbaya kwa jamii
yoyote ile.
Ikiwa kwa namna moja ama nyingine imevunja amani
ya nafsi yako.
Ninakuomba radhi!