SIMULIZI.... PENZI CHUNGU
MWANDISHI.. HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010
SEHEMU YA 31
"Habari zenu jamani" Mama Bruno alisalimia.
"Nzuri" wote waliitikia.
"Hapa tuna agenda kuu moja tu, hakuna kufungua kikao wala kufunga kikao, agenda ni kumuua Suto Sutani kwa njia yoyote ile na haraka iwezekanavyo, kikao hiki ni kwa ajili ya kupanga mipango kujua tunaanza vipi na tunamaliza vipi. Lakini tuhakikishe Suto Sutani anakufa !" Mama Bruno alisema kwa kirefu.
"Mpango siyo kumuua Suto, mpango kwanza ni kujua Suto Sutani yupo wapi kwa sasa, Suto Sutani amekuwa mwiba mkali sana, jeshi la Polisi lenyewe linahaha usiku na mchana kumsaka Suto. Sasa sisi tunapanga kumuua, tutamuonea wapi, hapa tujipange kumtafuta kwanza, ili tujue anaishi wapi" Manka nae alichangia.
"Ni kweli kabisa Manka. Kujua Suto Sutani yuko wapi ni kazi ngumu kuliko tunavyofikiria, jeshi la Polisi lenyewe limeshindwa kuvumbua kitendawili hiko mpaka leo wanahaha kumsaka Suto, mama Bruno kama unadhani kazi ya kumuua Suto ni rahisi, unajidanganya mama, Mimi ndiye naziona nyuso za maaskari zilivyo na woga, Inspekta Jasmine mwenyewe tunayemuamini wananchi wote, huku nchi ikimtegemea, anastuka ukimtajia jina la Suto Sutani, Veronica mimi najuta kujiingiza katika kadhia hii, pesa zenu haramu zimeniponza, kuitumia vibaya kalamu yangu kumeniponza, sijui... ."
"Nyamazaaaaa...huu siyo wakati wa kulaumiana, siyo wakati wa kulalamika, kama pesa ushachukua, kama kalamu yako ushaitumia vibaya, lakini ushukuru bado upo kazini, bado ni mwandishi wa gazeti la Dumizi, sisi tumekosa kazi Veronica, kutokana na Suto, kutokana na pesa unazoziita haramu. Cha muhimu hapa ni kutafuta namna ipi tunampata Suto Sutani na kumuua, basi !" Beji aliyasema maneno hayo kwa hasira. Na wengine wote walitikisa vichwa, ishara ya kukubaliana nae.
"Eeh tunafanyaje sasa" Dungu kwa mara ya kwanza alichangia.
"Naona mnagombana sana, kumkamata Suto na kumuua siyo tatizo kabisa. Suto atamatwa na atauwawa!. Kumkamata Suto ni kazi ndogo sana kwa Kurwa na Doto. Kwakuwa mmetushirikisha katika hili hakuna litakaloshindikana. Mnastaajabu Polisi kushindwa, Polisi hawana akili za kutufikia sisi, Kulwa na Doto" Kurwa kijana mpya katika kikao kile alisema kwa kujigamba.
Sasa kikao kilipata uhai, Kurwa alirejesha hali ya kujiamini kwa wanakikao.
"Tunaanzaje sasa msako wetu?" Dungu aliuliza.
"Mwelekeo wetu unategemea mwelekeo wa Polisi, lazima tujue Polisi wanahisi Suto yuko wapi,nasi tunaelekea huko. Kwa hilo tunategemea sana mchango wako Veronica, ukaribu wako wa Polisi utatusaidia sana. Lazima tuhakikishe Suto anakufa kabla hajaingia mikononi mwa Polisi, Polisi wakimkamata tu, atakutajeni ninyi, nanyi mtaangia matatani. Lazima tuwe makini, na tufanye kazi kwa haraka mara mbili au tatu zaidi ya Polisi. Kulwa alieleza kwa kirefu.
" Tunawategemea sana jamani" Manka alisema kwa sauti yenye uwoga.
"Usijari, tutafanya kazi mliyotutuma kwa haraka sana"
Mama Bruno alifunga kikao, kila mtu akiwa na matumaini mapya, huku wakisubiri taarifa toka kwa mwandishi Veronica Baro, ili Kurwa na Doto wakafanye kazi.....
ITAENDELEA. ........