NITAKUPATA TU
SEHEMU YA 011
Alikuwa akitizamana na midomo miwili ya bastola. Washikaji wakiwa katika umakini wa hali ya juu. Teddy hakuamini kile alichokuwa akikitizama. Akataka kujaribu kumuuliza Jimmy kinachoendelea, lakini sauti haikutoka, akabaki akiitizama midomo ya bastola ambayo ilikuwa umbali mfupi kutoka usawa wa paji la uso wake. Akili yake ikaganda, ikashindwa kufanya kazi kwa wakati, mzigo umepotea, harafu tena anashikiwa bastola! Hilo likamchanganya kama sio kumshangaza. Akakitamani kitendo kile kiwe ndoto, lakini bado haikuwa hivyo. Mzigo haukuwepo na kibaya zaidi alikuwa akitizamana na midomo ya bastola. Akainamisha kichwa chini akijaribu kukiamini kile kinachoendea pale. Kwa mara nyingine akainua kichwa kutizama tena, lakini safari hii hakukiona kile ambacho alikiona mwanzo. Hakuwa akitizamana tena na midomo ya bastola, hapakuwepo na watu wawili waliokuwa wameshika bastola. Walipotea na kutokuonekana kabisa. Mbele ya macho yake alisimama Jimmy pekee. Hata Jimmy hakuwa yule wa tabasamu. Huyu alionekana kuchanganyikiwa na hata kukata tamaa. Uso ulikunjamana kwa hasira, sasa alikuwa akimtizama Teddy kwa macho yake makali. Uso wake ulikuwa ukiongea kifo, macho yake yalikuwa yakiitangaza shali. Kila alipokuwa akimuangalia Teddy mishipa ya hasira ilikuwa ikizidi kuharibu taswira yake. Alikuwa akihitaji kuongea na Teddy. Alitambua teddy hakuwa mhusika wa kilichotokea, alimjua tena na pia aliufahamu uaminifu na hata msimamo wake. Asingeweza kukifanya kile. Hilo likampa ugumu kuongea, kitendo cha watu wao kumnyooshea Bastola kilimpa wakati mgumu sana. Alimjua fika katika medani ya mapambano, alimjua fika katika medani ya mapigano, huyu alikuwa ni zaidi ya Jean Claude Van Damme na hata zaidi ya Don Yen na Hata Jet lee. Kitendo cha kumnyooshea bastola ni kumkosea sana. Hilo likamfanya Jimmy awe mnyenyekevu mbele ya mwanadada huyu. Lakini kile alichokitegemea hakikuwa hivyo.uso wa teddy haukuwa katika masihara tena, alimuangalia Jimmy kwa macho yenye maswali lukuki. Akatamani kuongea neno moja lakini hakuipata nafasi hiyo. Teddy alisimama na kupiga hatua bila hata kumuangalia Jimmy. Alitembea akitoka katika jumba lile akiwa ni mwenye hasira sana. Aliuhisi mchezo mzima kuchezwa na watu wake hao ili kumzunguka. Hilo hakuwa tayari kuliona likitokea. Alikuwa tayari kumuua yoyote katika hilo. Alishakubali kumuua masimba sababu ya mzigo ule, sasa kwa nini hawa wanataka kunizunguka?
Lilikuwa swali ambalo lilikivuruga na kukichanganya kichwa cha teddy. Bado Jimmy hakuweza kuongea kitu. Bado jmmy alikuwa akimkodolea macho. Teddy akakiinua kichwa chake kwa mara ya pili kisha kumuangalia tena jimmy. Macho yake yalikuwa yakiongea kitu kingine kabisa. Hakuwa teddy yule mrembo na mwenye tabasamu, huyu alikuwa teddy tofauti kabisa. Bado hakuyaondoa macho yake usoni kwa Jimmy. "Huu ndio Wema wangu? Haya ndio malipo ya kuwasaidia mzigo wenu? Umenisahau mimi ni nani? Umesahau kuwa ninauwezo wa kuwaua kwa muda mfupi tu? Sasa naomba uniambie ukweli, nataka kuujua mzigo uko wapi na nani ameuondoa hapa. Usipokuwa mkweli maiti yako itakutwa humu ndani. Aliongea teddy akimuangalia jimmy pasipo kupepesa macho bastola ikiwa mkononi. Jimmy alijikuta midomo ikimkauka, akajikuta mate yakishindwa kupita kooni. Alimtizama teddy machoni kwa muda mrefu akitamani kuongea kitu. Hakupata neno la kuongea, alijikuta akianza kutetemeka. Jimmy leo alikuwa akimuogopa teddy.
Akaona kukaa kimya kutasababisha makubwa. Kwa sauti ya uoga akaanza kuelezea kila kitu tokea waliporudi na kuikuta maiti ya mlinzi, akaeleza walivyoingia ndani wakishuhudia mzigo wao ukiwa haupo. Hakuficha chochote kile. Baada ya Jimmy kumaliza kuongea teddy hakuongea kitu. Alipiga hatua mpaka nje pale ulipolazwa mwili wa mlinzi yule. Akaufunua na kuuangalia kwa makini. Cha kwanza kukiona ni jeraha shingoni kwa marehemu yule.
"Masimba!" Lilikuwa neno pekee kutoka kwa teddy. Hili likamfanya jimmy aliekuwa amesimama nyuma kidogo ya teddy asogee na kuonyesha kushangazwa. "Masimba aliingia hapa na ndiye aliefanya hiki kitu. Na kama kweli ni yeye alieuchukua mzigo, itabidi uwasiliane na mwamvita muda huu, ili watakapo kutana ajue anatakiwa kufanya nini." Aliongea teddy akitoka pale akionyesha ni mwenye mawazo.
*********
Ulikuwa usiku wa saa mbili na nusu pale simu ya Masimba ilipotoa sauti kuonyesha kulikuwa na ujumbe mfupi wa maneno. "Upo wapi Masimba? Uliuliza ujumbe ule. Masimba akatulia kwanza kujipa muda wa kufikiria.
"Nipo nyumbani!" Alijibu nakutulia tena.
'Bila shaka utakuwa upo tayari kwa sasa kukutana na mimi?" Ujumbe mwingine ukaonyesha kuuliza.
"Yeah! Naomba tukutane Ngamia Pub kigamboni, nadhani panafaa kwa aina ya maongezi yetu.". Alituma ujumbe huo ambao ulipokewa kwa ukimya wa muda mrefu. Kwa mtu aina ya Masimba aliutambua ukimya ule. Aliutambua kwa maana moja. Mwanamke yule alikuwa akifanya mawasiliano na watu wengine, watu ambao alitambua lazima watakuwa wameshaanza kuelekea sehemu ya mkutano wao. Hakuwa na shaka kwa kuwa Charty John alikuwepo sehemu ya tukio akimuangalia kila aingiaye na kutoka. Hakuwa na shaka kuhusu hilo.
Muda mfupi alikuwa akiingia maliwatoni, akajimwagia maji, kisha kutoka na kuyaendea mavazi yake. Baada ya kuvaa na kujiangalia akachukua bastola zake mbili revolver colt na dernng up automatically na kuziweka sehemu yake. Baada ya kumaliza hapo akaweka vitu vyake sawa pale ndani. Muda mfupi alikuwa akiliacha jumba lake akielekea sehemu ya tukio akiwa katika tabasamu la aina yake. Siku zote alipenda kucheza na watu wa aina yake, alipenda kucheza na watu walioupenda mchezo ule. Alitaka kumalizana na hawa kisha kurudi kwa teddy. Alitaka kumfanya kuwa wa mwisho.
*****
Sehemu kubwa ya eneo hili la mjimwema lilikuwa limechangamka watu wakionyesha kuifurahia siku hii. Muziki ilikuwa ukisikika, muziki ambao ulikuwa ukiwa burudisha vijana kwa wazee. Sehemu yote ilikuwa katika hali ya kupendeza na hata kuvutia. Charty alikuwa pembeni kabisa macho yake yakiwa busy kutizama kila tukio linaloendelea hapo. Muda mfupi akaiona gari aina ya Toyata ikisimama eneo la maegesho. Macho yake yakavutiwa na watu walioshuka kwenye gari ile. Hayakuvutiwa kwa uzuri wa mavazi yao ama sura zao, bali alivutiwa kwa kuwa ndio wale aliowaona mchana wakimfuatilia masimba. Hilo likamuweka kwenye utayari. Muda mfupi akamuona mwanamke yule akiingia pale, alikuwa katika mavazi ya aina yake. Sketi fupi ilioishia juu ya magoti kwa juu kabisa. Sketi ya kubana na kusababisha mistari ya chupi aliovaa kuonekana kwa uwazi zaidi. Wateja wote wakageuka kutizama kule alipokuwa akitokea mwanamke yule. Miluzi ikasikika na shangwe kutamalaki. Wakati mwanamke yule akiendelea kuwahenyesha wanaume na kuzivunja shingo zao, masimba ndio kwanza alikuwa akiwasili eneo la tukio, bastola mbili zikiwa kiunoni, akitembea kuelekea pale pale.
Kesho