RIWAYA: MTUTU WA BUNDUKI
SEHEMU: 7
_____
ILIKUWA TAYARI IMEKWISHATIMIA saa tano na robo usiku wakati nilipowasili kwa mara ya pili nyumbani kwa John Varma, nyumba namba 102 eneo la West Point kandokando ya jiji la Monrovia. Baada ya kumkosa jioni ile nilikuwa nimeamua kutafuta baa ya karibu na eneo lile ambapo nikiwa humo niliburudika na kauli nzuri za wadada warembo waliovaa sketi fupi wenye maumbo na sura za kuvutia, wahudumu wa baa ile iliyokuwa mtaa wa pili nyuma ya mtaa aliokuwa akiishi John Varma. Lengo langu hasa likiwa ni kupoteza muda wakati nikiendelea kumsubiri John Varma huko alipokuwa ameenda arejee nyumbani. Sasa nilikuwa mbali na kelele za muziki wa baa ile na maongezi ya walevi ambayo mengi yalijikita katika kuzungumzia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika pale Liberia usiku wa jana.
Mara hii niliutazama mlango ule wa nyumba namba 102 katika ghorofa ya nne huku nikiwa nimezama kwenye tafakuri. Shauri langu sasa lilikuwa ni katika kutaka kufahamu kama John Varma angekuwa tayari amerudi mle ndani au lah!. Usiku huu nyumba zote katika korido ile zilikuwa gizani na zaidi ya pale utulivu wa eneo lile ulinitia wasiwasi. Usiku huu mvua ilikuwa imeanza kunyesha na kama siyo jaketi nililolinunua njiani wakati nikija pale kwenye kitongoji cha West Point huwenda ningekuwa nikitaabika vibaya na baridi ile kali ya usiku.
Kwa tahadhari nikatega sikio langu pale mlangoni kujaribu kusikia sauti ya kitu chochote mle ndani lakini hapakuwa na kiashiria chochote cha uwepo wa mtu le ndani na hali ile ilinishangaza sana. Nikasogea na kujaribu kuchungulia mle ndani kupitia dirishani hata hivyo sikuambulia kuona chochote kwa vile giza zito lilivyokuwa limenawiri mle ndani. Kilipita kitambo kifupi nikiichunguza ile nyumba kwa makini kisha nikaanza kugonga pale mlangoni. Mara hii nilikuwa makini zaidi katika kugonga kwa kukwepa kuwashtua majirani au mtu yeyote ambaye angekuwa eneo lile. Hata hivyo pamoja na ufundi wangu wote wa kugonga lakini sikujibiwa. Nilipogonga kwa zaidi ya mara nne bila ya kujibiwa nikahisi ni kama niliyekuwa nikipoteza muda. Hivyo kwa msaada wa funguo zangu za kazi nikafyatua kitasa cha mlango ule na kuzama ndani taratibu huku bastola yangu tayari ikiwa mkononi.
Mara baada ya kuingia mle ndani na kuufunga ule mlango nyuma yangu nikasimama kwa utulivu kuishughulisha milango yangu ya fahamu. Kwa kufanya vile nikasikia kelele za muungurumo wa jokofu na mshale wa saa ya ukutani iliyokuwa imetundikwa sehemu fulani katika sebule ya ile nyumba. Sikuhisi mjongeo wowote wa kiumbe hai wala sauti ya mkoromo wa mtu aliyeko usingizini hivyo nikachukua kurunzi kutoka kwenye mfuko wa koti langu na kuiwasha nikianza kumulika mle ndani.
Nilikuwa nimetokezea kwenye sebule kubwa ya nyumba ile. Niliona seti moja ya makochi ya mbao yenye mito kuizunguka meza fupi ya mti wa mkaratusi katikati ya sebule ile. Upande wa kulia niliona kabati kubwa la vyombo vya dongo pembeni ya mlango wazi kuelekea kwenye ukumbi mdogo wa kulia chakula wenye meza ya umbo duara iliyozungukwa na viti sita. Nilipofika katikati ya ile sebule upande wa kushoto nikaona korido fupi iliyokuwa ikipakana na milango mitatu ya vyumba. Nilipofika pale nikasimama na kuupima utulivu. Bado sikuweza kusikia sauti ya kitu chochote hivyo nikapiga hatua zangu kwa tahadhari kupeleleza ule ukumbi wa chakula uliopakana na dirisha dogo linalotazama na chumba cha jiko kwa upande wa kulia.
Sikuona kitu chochote hivyo nikarudi pale sebuleni na kuanza kupeleleza kwa makini zaidi. Kwa kufanya vile nikaiona simu ya mezani juu ya stuli iliyofunikwa kwa kitambaa cha kufuma kwa mkono kwenye kona ya sebule ile. Ukutani nikaona picha nzuri za kuchora kwa mkono na nyingine zikimuonesha John Varma akiwa katika maeneo tofauti. Kulikuwa na redio ndogo ya bendi sita ya Hitach katika meza ndogo ya mapambo yenye ua dogo la kitenge. Mandhari yale yalikuwa safi na tulivu sana.
Hatimaye nikaondoka eneo lile kwa tahadhari na kuifuata ile korido ya kuelekea vyumbani huku bastola yangu ikiwa mkononi. Loh! sikuwa nimeona vizuri gizani hivyo nikajikwaa kwenye kona ya korido ile mahali kulipokuwa na ndoo ya bati. Ile ndoo ikajigonga ukutani na kusababisha ukulele mle ndani. Nikashtuka sana na kuzima kurunzi yangu mkononi huku nikisikiliza. Kikapita kitambo kirefu bila mtu yoyote kujitokeza kwenye ile korido na hapo nikapata mashaka kuwa huwenda mle ndani hapakuwa na mtu. John Varma alikuwa bado hajarudi nyumbani kwake?. Nikajiuliza bila kupata majibu.
Hata hivyo nilitaka kupata hakika juu ya hisia zangu hivyo nikaanza tena kunyata kuelekea vyumbani kufanya uchunguzi. Sikufika mbali mara nikahisi nyuma yangu kulikuwa na mtu. Hofu ikanimeza haraka huku kijasho chepesi kikininyemelea maungoni. Mara hii nikapanga kugeuka haraka kwa hila lakini sikufanikiwa kwani nilijikuta nikitulizwa kwa mkuno wa chuma baridi kisogoni.
“Usijaribu kuleta hila yoyote John. Tupa bastola yako chini tafadhali!”. Sauti kavu ya mwanaume kutoka nyuma yangu ikanionya.
“Wewe ni nani?”. Nikamuuliza yule mtu nyuma yangu.
“Paye Dolo. Nimekuwa humu ndani nikikusubiri kwa muda mrefu”
“Ulikuwa unanisubiri mimi?”. Nikamuuliza yule mtu baada ya kugutuka kuwa alikuwa amechanganya mahesabu.
“Ndiyo. Nilikuwa nakusubiri wewe kwa muda mrefu humu ndani hadi nikaanza kukata tamaa kuwa umekwishatokomea. Lakini Mungu siyo Athumani kwani hatimaye umeingia kwenye kumi na nane zangu”. Yule mtu nyuma yangu akajigamba.
“Unasema ulikuwa humu ndani ukinisubiri kwani mimi na wewe tulipeana miadi ya kuonana?”. Nikamuuliza yule mtu huku taratibu nikigeuka kumtazama lakini sikufanikiwa kwani kabla sijafanikiwa vizuri kugeuka nikashtukia nikichapwa kofi baya shingoni na hapo moto wa maumivu ukasambaa haraka shingoni.
“Sasa mbona unanipiga?”. Nikamuuliza yule mtu.
“Sijakwambia ugeuke nyuma kwanini ujitie kiherehere?”
“Okay, samahani sana mkuu lakini bado hujanijibu swali langu”
“Swali gani?”
“Kama tumepeana miadi hadi ulalamike kutumia muda mrefu kunisubiri humu ndani”
“Acha maswali yasiyo na msingi wewe tumbili”. Yule mtu nyuma yangu akanionya huku akianza kunipekua mwilini. Alipomaliza akafanikiwa kuchukua bastola yangu.
“Una shida gani na mimi hadi univamie kibabe namna hii?”. Nikamuuliza yule mtu na mara hii nikagundua kuwa alikuwa hamfahamu vizuri John Varma. Ni kama alikuwa ametumwa kumshughulikia mtu asiyemfahamu vizuri kwani vinginevyo alipaswa kutofautisha sauti yangu na ya John Varma.
“Idara yetu ya ujasusi inakuhitaji”. Yule mtu akavunja ukimya.
“Ndiyo mnivizie ndani kwangu usiku wote huu kwani simu yangu hamuijui?”. Nikamuuliza yule mtu nikijitia mimi ndiye John Varma.
“Tumekuwa tukipiga simu yako mara kwa mara lakini haipokelewi”
“Sikuwepo nyumbani”
“Na ndiyo maana nikaamua kukufuata mwenyewe hapa kwako John”
“Idara ya ujasusi inanihitaji kwa jambo gani?”
“Utusaidie kutueleza mahali alipo mzee Amara Konneh”
“Sifahamu alipo”
“Com on, acha kudanganya John, hakuna yoyote anayeweza kukuamini kwa maneno yako. Kama hutozungumza ukweli idara haitalaumiwa kwa kifo chako”. Yule mtu akanionya huku akivuta kilimi cha bastola yake kuiruhusu risasi kuingia kwenye chemba.
“Mnadhani kuniua mimi ndiyo utakuwa ufumbuzi wa haja yenu?”
“Huwenda lisiwe suluhisho lakini angalau hutoweza kutudanganya tena”
“Kwani nimewadanganya nini?”
“Mara hii umesahau kuwa wewe ndiye uliyetuhakikishia kuwa Amara Konneh na familia yake pamoja na yule kijana mgeni wangekuwa wamekimbilia Gissie na kumbe siyo kweli?”
Maelezo ya yule mtu nyuma yangu yakanizindua, akili yangu ikaingiwa na taharuki baada ya kung’amua kuwa JohnVrama ndiye aliyewaelekeza wale wanajeshi kutuwekea mtego wa barabarani usiku wa jana wakati tukitoroka kuelekea Gissie. Kwa kweli nilijihisi kuishiwa nguvu.
“Lakini mimi sikuwadanganya?”. Nikajitahidi kujitetea.
“Huwenda ukawa na nafasi nyingine ya kujitetea lakini hapa siyo mahala pake. Nimetumwa kukukamata na kukufikisha kwa wakuu”
“Kwa kosa gani nililofanya?”
“Hata mimi sijui”. Yule mtu nyuma yangu akanikata kauli kisha kwa wepesi usioelezeka mikono yangu ikashikwa na kuzungushwa kwa mtindo wa ajabu na wakati nikitaka kufurukuta tayari nikajikuta nimeshapigwa pingu mikononi. Paye Dolo alikuwa mtu hatari wa kuogopwa kwa namna alivyofanikiwa kunidhibiti kwa kasi ya umeme wa radi. Kisha akanisukuma na kunitanguliza mbele huku kasiba ya bastola yake ikikodolea macho kisogo changu kwa nyuma.
Sasa tulikuwa tumebadili uelekeo. Paye Dolo alikuwa nyuma yangu akiniongoza kuelekea nje na hapo nikajua kuwa kulikuwa na mipango kamambe ya kuniteka na kunifikisha huko kwa wakuu wake wa kazi. Kwa kweli sikuwa tayari kufikishwa popote na kwa mtu yoyote usiku ule, iwe kwa watu salama au wasio salama. Hivyo wakati nimetangulizwa mbele nikawa makini sana kufanya tathmini juu ya mazingira mazuri ya kuchoropoka kwenye mtego ule.
Sasa tulikuwa karibu kuufikia ule mlango wa sebule kuelekea nje. Kuona vile nikakusanya nguvu kisha kwa tukio hatari la kushtukiza, kufumba na kufumbua nikajitupa ukutani na kukita miguu yangu kisha nikajitupa kunyumenyume na kumvamia Paye Dolo nyuma yangu. Kwa nguvu ile niliyoitumia sote tukapiga mweleka na kuanguka chini. Lakini kwa mimi ambaye nilikuwa nimefungwa pingu mikononi tukio lile lilikuwa hatari zaidi. Bastola ya Paye Dolo ikamponyoka mkononi na kuangukia kusikojulikanana huku na mimi nikijiviringisha kando. Paye Dolo naye kuona vile akajiviringisha sakafuni kunifuata huku akinitupia mapigo hatari ya kareti na mateke kunishambulia. Hata hivyo aliambulia patupu kwani mchezo wa gizani niliupenda sana kwa vile ulimpunguzia adui umakini. Nikaendelea kujiviringisha hadi kwenye kona ya sebule ile hapo nikaukita mguu wangu kisha nikajibetua kwa mtindo hatari wa sama soti kusimama.
Loh! ilikuwa kabla sijapata mhimili vizuri Paye Dolo akanichapa teke hatari la tumbo lililonivuruga vibaya na kunitupa nyuma. Nikaangukia kwenye kochi moja la pale sebuleni na kulivunja vipandevipande huku maumivu makali yakisambaa mwilini. Hata hivyo nikawahi kujizoazoa pale chini na kusimama. Paye Dolo akanifikia tena, akatupa ngumi tatu makini kichwani lakini nilizikwepa kama mchezo na hivyo zikakata upepo na kumpunguza nguvu. Kuona vile Paye Dolo akabadili mtindo na kunitupia pigo baya la kareti shingoni, pigo lile likanipunyua kidogo lakini nikafanikiwa kulikwepa. Kisha nikakusanya nguvu na kumtandika kichwa cha pua na kuupasua vibaya mwamba wa pua yake huku akipiga mweleka mbaya na kuanguka chini. Nikamuwahi pale chini na kumchapa teke la korodani na hapo akapiga mguno na kubweka kama mbweha lakini aliwahi kusimama na kunijia kwa kasi ya kimbunga.
Nilijaribu kumzuia lakini sikufanikiwa na hapo nikajikuta nikichapwa pigo baya la kareti mbavuni na maumivu yake yakanipelekea niachie mguno mkali wa maumivu. Nikayumba hovyo nikirudi chuma na kabla sijapata mhimili vizuri Paye Dolo akanichapa teke la kifua lililonitupa chini na kunilambisha sakafu. Kwa kweli nilisikia maumivu makali sana kifuani kama niliyepigwa na tofali huku nikikohoa hovyo. Paye Dolo hakuniacha na mara hii akaongeza kasi zaidi akinijia kwa mapigo ya mateke ya haraka ambayo nilijitahidi kwa kila namna kuyapangua kwa mikono yangu iliyofungwa pingu.
Nilipohisi kuwa Paye Dolo alikuwa mbioni kuishiwa nguvu nikajitupa sakafuni kumfuata na kabla hajaishtukia hila ile nikazungusha mguu wangu sakafuni na kumchota mtama uliompaisha vibaya hewani. Alipoanguka chini akatua juu ya ile meza fupi ya pale sebuleni na kuivunja vipandevipande. Kiuno chake kikapata hitilafu huku mkono wake mmoja ukivunjika vibaya na hapo akapiga yowe kali la maumivu. Paye Dolo hakuwa na namna ya kufanya hivyo haraka akachomoa kisu kiunoni kwake na kunitupia lakini hakuwa na shabaha makini hivyo kisu kile kikanikosa na kwenda kukita kwenye mbao ya juu ya dirisha.
Kisu cha alichonirushia almanusura kinipate kifuani lakini nikawahi kukikwepa kisha nikajitupa chini kujiviringisha kumfuata katika mtindo wa zigizaga hali iliyompelekea ashikwe na kiwewe katika namna ya kunidhibiti. Wakati akiendelea kushangaa nilipomfikia nikamchapa teke la tumbo na alipoanguka chini nikamrukia na kumtundika kabari ya miguu ya mtindo wa judo. Paye Dolo akajitahidi sana kufurukuta kwa vile alikuwa ni mtu mwenye nguvu nyingi hivyo tukaanza kuepelekana huku na kule hata hivyo sikumuachia.
Kumdhibiti mtu mwenye nguvu kama Paye Dolo ilihitajika kazi ya ziada hivyo nguvu zikaanza kuniishia. Nilipoona anakaribia kuchomoka kwenye kabari ile matata nikamuongezea kabari nyingine ya shingoni nikitumia pingu zangu mkononi na mara hii sikumpa Paye Dolo nafasi ya kuomba maji kwani niliikaza mikono yangu kisawasawa. Jicho likamtoka pima kama mjusi aliyebanwa na mlango, mishipa ya kichwa ikamtuna huku jasho likimtoka. Nilikuwa nimemdhibiti vizuri hivyo akaanza kutupa mikono na miguu yake huku na kule kujitetea. Hivyo pakatokea patashika ya aina yake pale sebuleni lakini sikumuachia. Hali ilipozidi kuwa mbaya Paye Dolo akajitutumua na kusimama na mimi huku nimemng’ang’ania shngoni kisha akanibwaga chini. Sote tukaanguka chini lakini bado sikumuachia kwani kabari yangu ilikuwa ni zaidi ya tumbili aliyenasa kwenye mtego wa nyati.
Muda mfupi baadaye nikamuona Paye Dolo akianza kuishiwa nguvu na kupunguza kutapatapa pale sakafuni nilipomng’ang’ania na hatimaye akatulia. Bado sikumuachia hadi pale nilipojiridhisha kuwa tayari alikwisha kata roho. Taratibu nikaondoa ile kabari ya pingu shingoni mwake na kujitupa kando huku nikihema hovyo kutafuta pumzi iliyokuwa mbioni kuniishia. Mikononi nilisikia maumivu makali sana kwani vifundo vya viganja vyangu vilikuwa vimechubuka vibaya kufuatia ile kabari niliyomtundika Paye Dolo shingoni.
Niliendelea kujilaza pale sakafuni kwa kitambo hadi pale hali yangu ilipoanza kuwa nzuri hapo nikasimama na kumsogelea Paye Dolo pale chini alipolala. Nilipompekuwa mifukoni nikamkuta na funguo za ile pingu aliyonifunga mikononi hivyo nikachukua ile funguo na kufungua ile pingu nikiitupilia sakafuni pale sebuleni. Kisha nikaendelea na upekuzi wangu mifukoni mwake. Nilipomaliza upekuzi ule nikawa nimefanikiwa kumfahamu vizuri Paye Dolo kuwa ni mtu wa namna gani.
Kupitia kitambulisho chake nilichokikuta kwenye wallet yake ya ngozi ya nyegere kwenye mfuko wa nyuma wa suruali yake ya dengrizi nikagundundua kuwa Paye Dolo alikuwa shushushu au afisa usalama kutoka katika idara kuu ya ujasusi ya taifa ya pale Liberia iliyofahamika kwa jina la NSA-National Security Agency. Serikali ya mapinduzi ya kijeshi iliyojitwalia madaraka kwa mapinduzi ya kijeshi baada ya kuvamia Ikulu na kumuua rais William Tolbert ilikuwa imemtuma kumtafuta John Varma, dereva wa aliyekuwa waziri wa ulinzi, mzee Amara Konneh. Baada ya kukosa kumkamata mzee Amara Konneh, jitihada zilikuwa zimeelekezwa katika kumtafuta John Varma kama mtu wa karibu wa mzee Amara Konneh ambaye angeweza kuwafahamisha mahali alipo. Bahati mbaya sana Paye Dolo baada ya kuandaa mtego wake mle ndani nikawa nimenasa mimi na siyo John Varma, mtu aliyekuwa amemkusudia. Hii ilimaanisha kuwa Paye Dolo aliwahi kufika na kuingia mle ndani kwa siri kisha akajificha na kumsubiri John Varma ajitokeze. Niliwaza.
Baada ya kumaliza kufanya upekuzi wangu mle ndani bahati mbaya sana sikuwa nimeambulia kitu chochote cha maana. Muda uliendelea kusonga bila John Varma kujitokeza kwenye maskani yake na hali ile ikanitia wasiwasi kuwa huwenda nilikuwa nikipoteza muda wangu bure mle ndani baada ya kuhisi kuwa John Varma angekuwa tayari ameshtukia juu ya kuwindwa kwake na wanausalama wa serikali ya mapinduzi ya kijeshi hivyo alikuwa ameamua kutorokea kusikojuliana. Mawazo hayo yakazidi kuzamisha matuamini ya kumpata Max na pesa alizokimbia nazo. Kwa kweli nilijihisi kutaka kupata muda wa kuzidi kutafakari zaidi kwani kufuatia kumkosa John Varma mle ndani mipango yote ilikuwa imevurugika.
Hatimaye nikaamua kutoka kwenye ile nyumba kwa kuhofia kukutwa na wanausalama wengine na hivyo kujiingiza upya kwenye matatizo. Mvua ilikuwa imeanza kunyesha hivyo nilipofika chini ya lile jengo la ghorofa nikaamua kujifunika kwa kofia ya jaketi langu baada ya kuhisi baridi kali ikinishambulia kichwani. Wakati nikitembea kwenye korido ya nje ya lile jengo la ghorofa sikuona mtu yeyote, pikipiki au gari likikatisha mitaani na hapo nikatambua kuwa ile amri ya jeshi ya kutokutembea mitaani kwa raia mara baada ya kutimia saa kumi na mbili na nusu ilikuwa imezingatiwa kikamilifu. Hivyo nikajionya kuchukua tahadhari huku mara kwa mara nikigeuka nyuma kuchunguza kama kungekuwa na mtu yeyote ambaye angekuwa akinifuatilia nyuma yangu. Sikumuona mtu yeyote kwa vile giza lilivyokuwa nene lakini sikuacha kujipa hadhari.
Ukweli ni kwamba sikujua ni wapi nilipaswa kuelekea kwa usiku ule kwa vile sikuwa na mwenyeji mwingine yeyote pale jijini Monrovia. Wazo la kuelekea katikati ya jiji la Monrovia likanijia haraka baada ya kuamini kuwa nikiwa huko ningeweza kupata baa moja iliyochangamka usiku ule na kuzamia humo huku nikipanga vyema mikakati yangu. Lakini hilo halikutimia kwani wakati nikiwa nimezama kwenye tafakuri ile mara ghafla nikashtukia nikipigwa na kitu kizito nyuma yangu kichwani. Loh! lilikuwa pigo sana na hapo nikayumba hovyo karibu ya kuanguka chini huku nikiupeleka mkono wangu kwenye mfuko wa koti langu kuifikia bastola.
Hata hivyo sikufanikiwa kwani wakati nikigeuka nyuma kutazama ni kitu gani kilichokuwa kikinitokea nikajikuta nikikabiliana na pigo lingine baya mbele ya kichwa changu. Muda uleule macho yangu yakaingiwa na giza zito, mdomo wangu haukuweza tena kuzungumza neno hata pale nilipofungua kinywa changu kupiga yowe la kuomba msaada. Bastola yangu mkononi ikaniponyoka na kuanguka chini, miguu yangu ikalemewa ghafla na uzito wa kuogopesha na hivyo kunipelekea nijihisi kama mlevi wa pombe kali. Nikaendelea kujikaza huku nikiinama kuiokota bastola yangu pale chini ilipoangukia lakini sikufanikiwa kwani pigo la tatu kichwani likafanikiwa kunibwaga chini na kulala chali na baada ya pale sikufahamu kilichoendelea.
_____
NILIYAFUMBUA MACHO YANGU kwa taabu baada kumwagiwa ndoo mbili za maji baridi yenye harufu mbaya ya shombo ya samaki. Nikazinduka na kutazamatazama huku na kule sehemu ile. Nikagundua kuwa nilikuwa sehemu ngeni kabisa katika maisha yangu. Tukio lile likaambatana kizunguzungu kibaya na hisia za maumivu makali yaliyoamshwa upya kichwani mwangu. Nilipomwemwesa macho yangu vizuri nikagutuka kuwa mikono na miguu yangu ilikuwa imefungwa kwenye kiti cha chuma kilichokuwa mbele ya meza kubwa. Nyuma ya meza ile kwenye kiti aliketi mwanaume mmoja mwanajeshi mwenye cheo cha Luteni Kanali kama cheo chake begani kilivyojieleza.
Niseme sijapata kuona mwanaume mrefu na mweusi kama yule katika pilikapilika zangu huko nyuma kwani mwanga hafifu wa mle ndani uliniwezesha kidogo kuyaona macho na meno yake wakati alipokodoa kunitazama. Tathmini yangu ya haraka ikanitanabaisha kuwa mtu yule hakuonekana kuogopa kitu chochote hapa duniani zaidi ya kupenda kutoa roho za watu. Ingawa mtu yule alijitahidi kutabasamu lakini hali ile haikufanya sura yake mbaya kurudisha matumaini wala macho yale yenye unyama na chuki kutangaza amani.
“Loh! masaibu gani tena haya?”. Nikajisemea kimoyomoyo huku nikitembeza macho yangu kutazama huku na kule.
Tulikuwa kwenye chumba kikubwa kishichokuwa na dirisha lakini chenye kuta imara. Katikati ya chumba kile ndiyo kulikuwa na vile viti tulivyoketi na meza kubwa ya chuma iliyotutenganisha katikati. Juu ya meza ile ilining’inizwa balbu ya umeme wa mwanga hafifu kutoka katika dari ya chumba kile. Nilipoendelea kuchunguza nyuma ya yule kamanda wa jeshi kiasi cha umbali wa mita zisizopungua tano nikauona mlango mkubwa wa chuma uliofungwa. Sikuweza kugeuka nyuma kwa vile nilivyokuwa nimefungwa mikono na miguu kwenye kile kiti lakini nilihisi kuwa huwenda kulikuwa na mtu au watu ambao ndiyo wangekuwa wamehusika katika kunimwangia yale maji baridi ili kunizundua. Mle ndani kulikuwa na utulivu kana kwamba tulikuwa kwenye chumba cha mtihani wa taifa na hali ile ilinipasha tumbo joto.
Fahamu zilikuwa zimenirudia baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani na mtu nisiyemfahamu mara baada ya kutoka kupambana na Paye Dolo kule nyumbani kwa John Varma, kitongoji cha West Point. Hofu ikazidi kuiteka nafsi yangu wakati macho yangu yalipoweka kituo kutazama pale mezani. Nikaiona bastola yangu iliyotenganishwa na kiwambo maalum cha kuzuia sauti, risasi nne zilizotolewa kwenye magazini, pingu niliyotumia kumnyongea Paye Dolo, pasipoti yangu ya kusafiria ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na karatasi ya viza ya kuniruhusu kukaa pale nchini Liberia kwa muda wa mwezi mmoja na nusu.
Pale juu ya meza nilipochunguza vizuri hofu ikaongezeka zaidi baada ya kuiona nembo kubwa ya NSA-National Security Agency, shirika la ujasusi la Liberia. Sasa sikuwa na shaka yoyote kuwa nilikuwa nimefikishwa kwenye makao makuu ya shirika la ujasusi la Liberia kuhojiwa. Kijasho chepesi kikaanza kunitoka maungoni.
Yule mtu mbele yangu alipojiridhisha kuwa nilikuwa nimerudiwa vizuri na fahamu akaondoa kofia yake ya kijeshi kichwani na kuiweka pale juu mezani na hapo nikapata kuuona upara wake uliong’aa na kusukwasukwa na mishipa ya damu kama mizizi ya kitunguu. Yule mtu akakohoa kidogo kusafisha koo lake na hatimaye kuvunja ukimya huku akiegemeza mikono yake mezani na kunitazama.
“Ni vizuri sasa tukafahamiana. Jina langu naitwa Lansanah Dagosseh, mwanajeshi mwenye cheo cha Luteni Kanali katika jeshi la mapinduzi hapa Liberia. Lakini vilevile mimi ni mkurugenzi wa upelelezi wa idara ya usalama wa taifa ya hapa Liberia, NSA-National Security Agency”. Yule kamanda akamaliza kujitambulisha na kupisha tafakuri ya kimya huku akinitazama. Nikajua alitaka kusikia kutoka kwangu lakini sikuwa na cha kuongea. Alipoona muda unayoyoma bila mimi kujitambulisha akaamua kuvunja ukimya huku akinitazama.
“Wewe ni nani?”
“Najiona mateka katika sehemu nisiyoifahamu”. Nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama yule kamanda mbele yangu.
“Jina lako tafadhali!”. Yule kamanda akanikatisha huku amanikazia macho. Baada ya kufikiri kidogo nikaona kuwa hapakuwa na haja ya kudanganya kuwa mimi ni nani kwa vile pasipoti na viza yangu vilijieleza.
“Jina langu naitwa Tibba Ganza, raia wa Tanzania”
“Umefuata nini hapa Liberia?”
“Nimekuja kwenye matembezi tu”
“Kumtembelea nani?”
“Kutembelea nchi yenu na vivutio vyake, bahati mbaya sana kabla sijaanza matemebezi yangu ndiyo nikapigwa kichwani na wahuni. Sasa ndiyo nimezinduka nashangaa kujikuta humu ndani nimefungwa mikono na miguu namna hii”
“Umefikia sehemu gani hapo Monrovia?”
“Kumbe hapa ni Monrovia?”. Nikamuuliza yule kamanda huku nikijitia hamnazo, hata hivyo sikuona tashwishi yoyote usoni kwa yule mtu mbele yangu.
“Nijibu swali langu tafadhali!”
“Oh!, samahani sana kwa kukawia kukujibu bwana mkubwa. Nilikuwa nimepanga kufikia Bella Casa Hotel na ndiyo nilikuwa njiani kuelekea huko wakati nilipokutwa na masaibu haya. Loh! wahuni wa mjini kweli siyo watu”
“Uchunguzi unaonesha kuwa uliwasili uwanja wa ndege wa James Spriggs Payne Airfiled saa 10:30 asubuhi siku ya juzi ukitokea Ibadan nchini Nigeria. Unaweza kunieleza muda huo wote tangu ulipowasili hapa Monrovia ulikuwa ukikaa wapi?”. Yule kamanda akaniuliza huku akinitazama kwa udadisi na swali lile likanipelekea nigutuke huku kijasho chepesi kikianza kunitoka. Sasa nilianza kuona hatari kubwa mbele yangu kwa namna shirika la kijasusi la Liberia lilivyokuwa limepiga hatua katika kupata taarifa zangu.
“Muda wote huo nimekuwa nikishinda kwenye baa mbalimbali za hapa jijini Monrovia kabla ya mapinduzi ya kijeshi kufanyika”. Maelezo yangu yakampelekea yule kamanda anitazame kwa kejeli hata hivyo hakutia neno. Baada ya kitambo kifupi cha ukimya mle ndani hatimaye nikamuona yule kamanda taratibu akiegemea kiti chake kustarehe. Kisha akaingiza mkono kwenye mfuko wa gwanda lake na kuchukua pakiti ya sigara. Humo akatoa sigara moja na kuibana kwenye kingo za mdomo wake kisha akajiwashia mche ule wa sigara kwa kiberiti cha kasha. Baada kuvuta pafu mbili akaupuliza moshi mbele yangu na kurejea kwenye maongezi.
“Umesema umekuja hapa Monrovia kutembea?”
“Ndiyo”. Nikaitikia
“Ungewezaje kukaa muda wote huo hapa Monrovia wakati huna pesa?”
“Pesa zangu zote zimeibwa na wahuni walionishambulia kichwani”. Nikadanganya.
“Na hii bastola mali ya jeshi la Liberia uliokutwa nayo unaweza kuniambia uliipata wapi?”
“Sijawahi kumiliki bastola achilia mbali kuitumia”. Nikajitetea.
“Kwa hiyo vijana wangu ni waongo?”
“Kwani vijana wako ndiyo walionivizia na kunipiga kichwani?”. Nikauliza nikijitia sielewi vizuri somo.
“Bado hujapigwa ila walichokifanya ni utaratibu wa kawaida kabisa wa kumkamata mhalifu”. Yule kamanda akasisitiza huku akilazimisha tabasamu kuumbika usoni pake.
“Huu ni utekaji na uvunjaji wa haki za binadamu. Nikiamua ninaweza kuwafungulia mashtaka ya kidiplomasia kwa unyanyasaji kwani nimefuata taratibu zote za kuingia nchini mwenu na sijafanya uharifu wowote”. Nikaendelea kujitetea hata hivyo nilikuwa na matumaini makubwa kwa vile nilikuwa na hakika kuwa hakuna mtu aliyekuwa akinifahamu kama mimi ni jasusi hatari wa kuogopwa.
“Tunayo haki ya kumkamata mtu yeyote, awe mgeni au mzawa ambaye mienendo yake inaonekana kutishia usalama wa nchi yetu. Huwa sipendi kumuona mtu analeta masuala ya siasa kwenye mambo ya msingi”. Yule kamanda akanionya huku akiendelea kuvuta sigara yake taratibu.
“Ni kwa vipi mienendo yangu imetishia usalama wan chi yenu?”. Nikamuuliza yule kamanda na baada ya kutoa sigara yake mdomoni na kukung’uta majivu kando akavunja tena ukimya.
“Mmoja wa vijana wangu amekuona ukitoka kwenye nyumba namba 102 iliyopo kitongoji cha West Point. Mkazi wa nyumba hiyo anaitwa John Varma, huyu ni mtu hatari katika kutishia usalama wa nchi ambaye tumekuwa tukimtafuta kwa muda mrefu. Mtu wetu mmoja amekutwa ameuwawa kwa kunyongwa kwa pingu shingoni kwenye nyumba hiyo wakati mwenyeji wake hafahamiki alipo. Je, tunawezaje kukutenganisha na tuhuma hizi?”. Yule kamanda akaniuliza na mara hii akinikata jicho kali la utafiti.
“Siwafahamu hao watu wote uliowataja na wala sijawahi kuyasikia majina yao hata kwenye matangazo ya vifo redioni. Nawezaje kuingizwa kwenye tuhuma za mauaji ya mtu nisiyemfahamu?. Nadhani ingekuwa busara kumtafuta mkazi wa hiyo nyumba na kumuuliza. Mimi ni mgeni nipo hapa kufurahia matembezi yangu na siyo kuvunja sheria”
“Tazama viganja vyako”. Yule kamanda akaongea kwa utulivu. Haraka akili yangu ikatumbukia tena mtegoni na mara hii nikahisi kuwa nilikuwa nimekutana na mtu makini na mwenye hila nyingi za masuala ya usalama katika kucheza vizuri na saikolojia ya mtu. Loh! ile michubuko ya pingu kwenye vifundo vya viganja vyangu wakati nikimnyonga Paye Dolo kule West Point nyumbani kwa John Varma ilikuwa imeniumbua. Nikameza funda la mate kujipa utulivu huku nikiichunguza ile michubuko viganjani mwangu. Nilipoinua macho yangu kumtazama yule kamanda tayari nilikuwa nimetengeneza hila.
“Sioni kitu labda mnifungue mikono”
“Viganja vyako vimekutwa na michubuko ya pingu. Sina shaka yoyote kuwa pingu hizo ndiyo zilizotumika kumnyongea Paye Dolo kwenye nyumba namba 102 kule West Point”
“Sasa kamanda huoni kuwa taarifa zenu zina mkanganyiko?”. Nikaingiza hoja.
“Kwa vipi?”. Yule kamanda akaniuliza kwa udadisi.
“Kama mimi nashukiwa kumuua Paye Dolo kwa vipi natuhumiwa kumnyonga kwa kutumia pingu wakati inasemekana nilikuwa na bastola. Huoni kuwa risasi ndiyo ingelikuwa njia rahisi zaidi ya kuhitimisha uhai........ wiki ijayo
Shunie naomba uwatagi wengine wooooote wadau wa adithi. Au yeyote atag watu