SEHEMU YA MWISHO
Kuna mambo mengi ya kukera katika huu ulimwengu, huyu linamkera hili na mwenzake lile. Ilimradi tu dunia haina usawa siku zote.
Mapenzi yameishikilia dunia kwa asilimia kubwa, kati ya maumivu kumi utakayosimuliwa ama kusimulia basi mawili kati ya hayo chanzo chake ni mapenzi.
Inasumbua sana akili kwa muda mrefu unapoyaamini maneno ya mtu na kufikia hatua ya kumkabidhi maisha yako ukamuelezea kila kitu kuhusu wewe kumbe mwenzako anayasikia na kuyapuuzia huku akijifanya kuyaremba maneno yako na neno lake moja tu, ‘nakupenda’.
Mwisho wa siku anakuacha na kwenda zake baada ya kupata kile alichokuwa anakihitaji.
Hali hii huzua hofu ya mapenzi na chuki hata kwa wasiotakiwa kubeba lawama.
Maumivu ya mapenzi yanaweza kukubadilisha na kuwa mwanadamu nje lakini mnyama hatarishi sana katika moyo wako.
KITENDO cha Chopa kumsaliti Nkozi miaka kadhaa iliyopita kilimuathiri sana binti yule wa Kinyarwanda, alikuwa mtu wa kulia kila mara masomo yalimuwia magumu sana.
Marafiki zake wawili yule binti wa kisomali na binti wa kitanzania ambaye ni Sofia hawa ndio waliokuwa wakimtuliza.
Alipokuja kuwaeleza kuwa kilio chake sio tu kwa sababu ya kuachwa katika mataa na Chopa bali kiumbe ambacho Chopa amekiacha katika tumbo lake.
Chopa alimuacha Nkozi akiwa yu mjamzito!!
Marafiki wale wakamshauri sana Nkozi kuwa aitoe mimba ile kwa sababu kuzaa mtoto asiyekuwa na baba kwa hali ile ya kimaisha lilikuwa tatizo kubwa sana.
Nkozi ambaye ile ilikuwa mimba yake ya kwanza kabisa aliufikiria uamuzi wa rafiki zake na kuamua kufanya walichomshauri.
Mimba ikatolewa na hapo akakata mawasiliano kabisa na Chopa alifanya vile ili aweze kumsahau.
Akiwa palepale chuoni ukiwa ni mwaka wa pili alikuja kugundua kuwa kuna tatizo analo, akajaribu kutafuta ushauri kwa madaktari bingwa.
Mwisho wa siku akaambiwa kuwa kizazi chake ni kibovu, na kiliharibiwa ile siku aliyokuwa anatoa mimba.
Taarifa hizi zikakianzisha kilio upya, akamkumbuka Chopa na ahadi zake hewa.
Akajenga chuki ya hali ya juu.
Ni katika kipindi hiki ambacho Sofia aliondoka kwenda kusomea mambo ya upelelezi na mapigano nchini Cuba.
Nyuma akawaacha Nkozi na rafiki wa kisomalia.
Msomali huyu ndiye ambaye baadaye aliijenga dhana ya kisasi katika kichwa cha Nkozi akamsimulia mikasa kadhaa juu ya kisasi.
Nkozi akajikuta anahitaji kumyoosha chopa kwa mambo yote aliyomfanyia lakini alijiwekea ahadi kuwa ikiwa atamkuta Chopa hayupo katika mahusiano yoyote yale atamsamehe kwa maneno lakini akimkuta yupo katika furaha ya penzi na yeye akiwa anaemia tu kwa kusalitiwa na kisha kupoteza kizazi basi ataipata ya motomoto.
Shughuli ikaanza yule binti wa kisomali akamuunganisha Nkozi na mtandao alioufahamu unaohusika na kesi ambazo haziwezi kusikilizwa mahakamani.
Kesi kama ya Nkozi.
Ilikuwa upesi sana akapewa majibu kuwa Chopa na mchumba wa mtu na muda wowote ule wamepanga kuoana.
Nkozi hakufikiria mara mbilimbili akatoa tamko kuwa Chopa avurugwe vibaya mno bila kuumizwa mwili bali akili yake.
Mipango ikaenda sawa, wakati huo Nkozi hana mahaba na mwanaume yeyote yule zaidi ya kuyafanya mapenzi kuwa biashara.
Biashara iliyokuwa inalipa haswa kutokana na umbile lake la kuvutia sana.
Ikawa kama alivyotamka, Chopa akajikuta akitupwa gerezani akipewa hukumu isiyokuwa na kichwa wala miguu lakini miaka mitatu ilihusika.
Ikiwa haijakatika miaka mitatu, Nkozi aliyekuwa masomoni Nairobi nchini Kenya anaelezwa kuwa Chopa yu uraiani, anaamua kumfuatilia tena. Lakini safari hii zile hisia zilizojizika za muda mrefu zinaibuka tena, hisia za chuki iliyokithiri juu ya wanaume.
Anatoa agizo Chopa ahifadhiwe sehemu maalumu ili aje kumuadabisha mwenyewe.
Anafunga safari kutoka Nairobi anapewa maelekezo ya jinsi ya kufika eneo la tukio.
Anapofika anakumbana na hili balaa.
Sasa anatazamana ana kwa ana na Chopa lakini pia anakutana na Sofia rafiki yake kipenzi.
Sasa wanamtazama Chopa anayetia huruma, ule ukarimu wake wa kuwapakia katika lori lake miaka ya nyuma na kisha kumpatia Nkozi pesa kwa ajili ya malazi, wakamtazama kisha Nkozi akayasahau aliyopanga kufanya juu ya Chopa badala yake akahoji kulikoni.
Pocha akaelezea tena jinsi Chopa alivyowasaidia watu wengi gerezani wasionewe, Nkozi akakumbuka ukle moyo wa Chopa wa enzi zile, Sofia naye akakumbuka uchangamfu na maneno ya Pocha siku anawasafirisha kwenda Dodoma bila kuwabughudhi!!
Nani atamfunga paka kengele?
Hili likawa ni swali kwa yeyote ambaye anaweza kuanza kumuhukumu Chopa.
Tz 11 aliyekuwa kimya wakati wote alizungumza maneno machache tu.
“Kwanza wewe dada sijui ndio Sofia, nakupigia saluti... upo vizuri umenihenyesha... pili wanasema ukitaka kumuua nyani ni kosa la jinai kumtazama usoni,. Nyinyi mmetazama tayari, kama ni heri basi haya mambo yaishie hapahapa.... pia wewe Chopa katika haya uliyopitia jifunze mambo mengi ya kuzingatia.... kubwa ni kuwa makini na usiwe mtu wa kupuuzia mambo..... nilikutumia ujumbe kukupa tahadhari hata kabla haujakamatwa usiku ule lakini ulikuwa unapuuzia....” alimaliza Tz 11 kisha akatoka nje akiwaacha wajuanao kuendelea na mazungumzo yao.
_____
LUCAS alifika nyumbani kwake akiwa hayupo sawa kabisa, alipotoka alikuwa ameacha tatizo na huku anapoingia anaenda kuambiwa tatizo. Alikuwa anatembea lakini akili ilikuwa ipo nukta chache kabla ya kumruka.
Alifika nyumbani kwake majira ya saa kumi jioni, alipokelewa na mkewe alimuuliza kuna tatizo gani limetokea hadi akapewa taarifa ile ya dharula arejee nchini Tanzania.
“Mama na baba ni wazima eh!” alihoji huku akionyesha kupagawa waziwazi.
“Wazima tu... nadhani tatizo ni mpango wa kando...” mkewe alimjibu huku akimpokea begi lake.
“Mpango wa... ndo nani huyo aaah! Ndo kitu gani hicho...” aliuliza hovyohovyo.
“Karibu ndani mume wangu....” Christina alimsihi mumewe.
Naam! Akaingia na kukaribishwa sebuleni na Edwin pamoja na mkewe. Walikuwa watulivu sana, wakamsalimia...
Lucas alibabaika wakati anawajibu ile salamu yao. Alijiuliza kichwani mwake kuwa je wale wamekuja kuna tatizo wanataka kutatuliwa ama wamekuja kuzua tatizo jipya.
Hakupata majibu, akachukua nafasi katika kochi!!
Kimya kikatanda kama dakika mbili nzima nadhani kila mmoja alikuwa akisubiri mwenzake aanze kuzungumza, mama caro ambaye walau ndo alikuwa na hali njema katika moyo wake alianzisha mauzungumzo ambayo wao watatu walikuwa wameyaongea vizuri kabisa hapo awali.
Mama Caro alizungumza kwa utaratibu kabisa hadi alipofikia suala la Lucas kuwa na mahusiano na mtoto wake, kwa hilo Lucas alikuwa mkali akalikataa waziwazi, ni hapo ambapo urafiki uliingia ndoa, Edwin alipandwa hasira akatoka alipokuwa ameketi akamvamia Lucas na kumtandika ngumi chini ya jicho lake, ukageuka ugomvi mkubwa na wa kuachanisha walikuwa wanawake, hii ilileta ugumu sana Lucas alitwangana na Edwin. Watu wazima hawa waliangushana chini huyu akimpiga mwenzake hapa na yeye anajibu kwa pigo jingine.
Mkewe Lucas alipoona huu ugomvi hautenganishwi kwa hali ya kawaida, upesi akakimbia ndani akaufungua mlango kisha akarejea na kile kilichofanya ugomvi ukafikia mwisho.
Alirejea akiwa na mtoto....
Lucas alikodoa macho yake na hakuamini kabisa kile alichokuwa anakishuhudia mbele yake alikuwa anamuona mtoto ambaye siku kadhaa nyuma alipotea jijini London na sasa anakutana naye ndani ya nyumba yake, mtoto ambaye alizaa na Caro mtoto wa rafiki yake.
Kufikia hapo sasa Lucas alipiga magoti na kuomba msamaha kwa kila aliyekuwa pale ndani, Edwin hakutaka kumsikiliza, akiwa amechanika mdomo wake aliondoka na kumsisitiza Lucas kuwa asahau kabisa kama waliwahi kuwa marafiki.
Mume ameondoka mke abaki kufanya nini?
Mama Caro naye akafuata nyuma akimwendea mume wake.....
Ndani wakabaki wanafamilia na yule mtotro mgeni aliyefikishwa nchini Tanzania kwa njia za kimafia baada ya Christina kuamua iwe hivyo ilimradi tu kumuonyesha mume wake kuwa hakuna siri ya kudumu katika dunia hii.
Lucas alilia sanma huku akijutia kila alichokifanya lakini aliomba tu adhabu kubwa ya kupewa ni kusamehewa na hakuna kingine. Maana alikuwa amejiadhibu tayari kwa yote aliyopitia.
“Mpigie simu mke mwenzangu mwambie asihangaike mtoto yupo Tanzania kwa mama yake mkubwa...” Christina alizungumza huku machozi yakimlenga lenga.
Kauli ile ilimuumiza sana Lucas....
“Lucas, ni nini hiki umenifanyia na utu uzima huu lakini eeh! Ni nini?” alihoji Christina huku akishindwa kabisa kujizuia kuangua kilio.
Lucas alitamani sana kumbembeleza lakini akili yake ilikuwa imeganda hajui la kufanya.
____
MAMBO HADHARANI.
Simu kutoka Tanzania ilimueleza Caro kuwa hana haja ya kuendelea kubaki London ni heri arejee Tanzania kukabiliana na ukweli.
Simu hiyo alipigiwa na mama yake mzazi ambaye alimueleza kuwa hata mtoto anayehangaika kumtafuta huko London basi yupo Tanzania.
Caro akaona kweli hakuna haja ya kuendelea kubaki nchi za ugenini wakati mtoto wake yupo Tanzania.
Alifanya safari ya haraka sana lakini hakusafiri peke yake aliambatana na mtu mwingine kutoka nchini uingereza.
Alipokelewa uwanja wa ndege na mama yake ambaye bado alikuwa yu jijini Dar es salaam pamoja na mume wake.
Lucas hakutaka kuzungumza na mtoto wake kwa sababu alijua jazba aliyokuwanayo na alihofia huenda anaweza kufanya jambo baya, kitendo cha Caro kufanya mahusiano ya kimapenzi na Lucas rafiki yake kilikuwa kimemtonesha moyo wake vibaya mno.
Caro alizungumza na mama yake kwa kirefu sana akimuelezamazingira yote jinsi yalivyokuwa.
Maelezo ya caro yalikuwa na kitu kipya alichokuwa amekificha kwa siku nyingi sana huku akimini kuwa itafika siku ya kukiweka wazi.
Mama Caro akaenda kumueleza mumewe juu ya hilo jambo.
Jambo hilo likawafanya kwa mara nyingine tena wafunge safari kwenda nyumbani kwa Lucas.
____
Wakati wawili hawa wakikusudia kwenda nyumbani kwa Lucas. Upande mwingine wa shilingi Pocha alikuwa amekinai kuishi maisha ya mashaka, tangu atolewe gerezani na mzee Bosco alijiona hana amani kabisa kwa sababu mtu aliyemsababisha aende gerezani bado hakujua ni nini hatma yake, alizungumza na Chopa kwa kirefu akaelezea kusudio lake la kwenda nyumbani kwa muheshimiwa ambaye alihusika katika kumpeleka gerezani ili aonane naye wazungumze kama ni msamaha na amuombe ilimradi tu aanze maisha mapya akiwa na amani tele.
Ili kulifanya jambo lile liende vyema alimsihi Sofia waambatane naye ili lolote litakalokwenda kinyume aweze kuwasaidia.
Sofia akakubaliana nao na wakaipanga siku ya kwenda nyumbani kwa huyo mbunge ambapo Pocha alikuwa akipatambua vyema.
Siku ikafika ya kuchambua pumba na mchele ili kila mtu aweze kubaki huru.
Walitumia usafiri wa daladala hadi wakafika mahali walipotakiwa kupanda bajaji.
Wakaenda hadi nyumbani kwa yule muheshimiwa, walipofika getini wakajieleza kwa kina kuwa wanahitaji kuonana na muheshimiwa, mlinzi akadai kuwa ana wageni wengine wa muhimu sana na hawezi kuonana na mtu yeyote.
“Chopa na Pocha hakuna harufu mnaisikia.... kuna harufu naisikia halafu naifananisha...” Sofia aliwauliza wenzake, wakatikisa vichwa kukataa.
Lakini harufu ile ilikuwa imembadilisha Sofia kabisa, ni kama kwa dakika kadhaa alikuwa ameondoka katika eneo lile kifikra na kwenda mbali sana. Alikuja kushtuliwa na Chopa aliyemwambia kuwa mlinzi amewataka waketi mahali kusubiri ruhusa zaidi.
Wakaenda jirani na nyumba ile na kuketi katika viti!!
Pocha alikuwa akiwaza juu ya usalama wake na Sofia akiwaza juu ya harufu aliyoinusa... ni Chopa pekee aliyekuwa hana mawazo sana.
Zaidi alikuwa akimuwaza Nkozi!! Hakumuwaza kwa mabaya wala hofu.
Baada ya kimya cha muda mrefu mara vilisikika vishindo ndani ya nyumba, na mara kelele za wanawake wakilia kuomba msaada zilisikika.....
Sofia alitamani kuingia ndani lakini hakuwa na ruhusa ile.
Akiwa bado vilevile mara zile kelele zilizidi kuja nje... ni kama kulikuwa na ugomvi mkubwa.
Hatimaye ule ugomvi ukahamia nje ukisindikizwa na sauti za akina mama.
Wale watu waliokuwa wanapigana walipofika tu nje watu wawili Pocha na Sofia walimtambua mmoja mmoja.
Pocha alimtambua mheshimiwa mbunge Lucas Kazioba huku Sofia akimtambua William Mackzube.
Wakabaki kutazamana Sofia asiamini alichokuwa anakiona mbele yake, William mackzube amefata nini nchini Tanzania tena bila kumwambia wakati wanawasiliana mara kwa mara.
“Carooo!!” mara Chopa naye akasimama wima alikuwa amempata wa kumtambua.... baada ya kwenda gerezani na hatimaye kutoka anakutana na Caro katika mazingira asiyoyatarajia.
Ule ugomvi ukaishia pale, William Mackzube akamuuliza Sofia imekuwaje yupo pale, Sofia naye akamuuliza amekuja lini Tanzania.
Mara caro naye akadakia.
“Wililiam huyu ni nani?”
William akashikwa na kigugumizi.
Wakiwa bado katika kushangaana mara akatoka yule mtoto wa Caro.
Upesi Sofia akaichukua simu yake akaitazama ile picha ya mtoto akamtazama na yule mtoto mbele yake.
“Nilikwambia William huyu ni mtoto wako ukapinga vikali... haya yapo wapi? Sofia alizungumza huku akimtuhumu William.
Sasa siri zote zilikuwa nje, ukweli ulikuwa mchungu sana kuumeza lakini ilibidi tu kuupokea, William alikuwa ndiye baba halali wa mtoto Bryan, wakati Caro anajihusisha na Lucas alifanya vile ili kupata pesa ya kumwongoza katika maisha yake pamoja na kumsaidia mpenzi wake William Mackizube aliyekuwa na hali mbaya kiuchumi, kwa pamoja walikubaliana kumbambika ile mimba Lucas ilhali haikuwa kweli.
Lucas alikuwa na tatizo la kizazi!!
Uhakika huu ukamfanya muheshimiwa Lucas apoteze fahamu palepale.
“Kumbe William ulinifanya mimi MPANGO WA KANDO!!” Caro hatimaye alizungumza baada ya kugundua kuwa kumbe William Mackzube ni mchumba wa Sofia ambaye alikuwa pale pamoja na akina Chopa.
“Caro yaani miaka michache hivyo ukashindwa kunivumilia..... nimemuumiza msichana wa watu Nkozi aliyenipenda kwa sababu yako, tazama sina hata cha kumpooza hawezi tena kuzaa... Caro nd’o upo hivyo kweli..... kumbe yawezekana hata kipindi nipo nawe ulinifanya MPANGO WA KANDO bila mimi kujua...” sasa ilikuwa zamu ya Chopa kulalamika akimtazama Caro machoni.
Caro alikumbwa na aibu.....
“Na muheshimiwa akiamka kutoka katika kuzimia mkumbusheni kuwa mimi naitwa Pocha ni yule kijana ambaye alinipeleka gerezani kisa tu MPANGO WA KANDO wake aliyekuja kutengeneza simu nikazifumania picha zao. Nilidhani kuwa wakati ule nilifanya makosa kumbe kufuga mpango wa kando ni tabia yake” Pocha naye alizungumza lake
Mzee Edwin alimshika mkono wake mkono akamchukua na Bryan kisha akazungumza.
“Naondoka na mtoto wangu pamoja na mjukuu wangu, hakuna hata mtu mmoja aliyekuja kumtolea mahari, ambaye ana maanisha kumuona mwanangu apatafute nyumbani aje tuzungumze.....” alimaliza kuzungumza akaondokana mkewe.
Huku nyuma wakabaki Sofia, Pocha, Chopa, Wiliam, Christina na muheshimiwa Lucas akiwa amepoteza fahamu.
Sofia akawaomba Pocha na Chopa waondoke, hakutaka kumsikia kabisa William Mackzube msaliti.
____
KIHITIMISHO
Ilianza kama utani, Pocha akajinadi kuwa yeye hana mpango wa kando wowote ule, Sofia akachukulia utani. Lakini sura ya Pocha ikamaanisha alichokuwa akikisema hatimaye Sofia akautua ujasiri wake kando akaangukia katika mikono hatari katika kufungua namba za siri zozote zile duniani.
Sofia akaangukia kwa pocha.
Chopa hakuwa na cha kumlipa Nkozi zaidi ya kulifufua penzi lao. Hawakuwa na uwezo wa kupata mtoto lakini waliamua kuianza ile safari tena.....
Caro hakutaka kuolewa na hakutaka kumsikia William, wazazi wake wakasikiliza alichotaka mtoto wao. William alipomtafuta walimpuuzia, akalazimika kurejea uingereza katika shughuli zake.
Fahamu zilimrejea Lucas na kujikuta yupo hospitali alipopata tiba vyema na kurejea nyumbani. Alikutana na mlinzi tu getini.
Mlinzi akampatia ujumbe aliouacha mkewe.
“Siwezi kuwa na mwanaume niliyemvumilia kwa miaka mingi huku nikijua kuwa ni yeye mwenye matatizo halafu ananisaliti akijiona yeye ni bora zaidi, nimeondoka naenda kutafuta mtoto na watu wanaojua kuzaa sio wewe hayawani”
Ulikuwa ujumbe kutoka kwa mkewe, ujumbe ambao haukuwa umedhibitiwa ili usisomwe na mtu mwingine hivyo kwa namna yoyote ile yule mlinzi lazima tu aliusoma.
Jambo hili lilimfadhaisha sana Lucas akatamani kama siku zingerwejea nyuma ili asifanye upuuzi alioufanya kujihusisha kimapenzi na Caro ambaye alimbambikia mimba isiyokuwa yake akaihudumia kwa mapenzi mazito, akamsomesha mtoto wa mwanaume mwenzake akajiona yeye ndiyo baba kumbe hakuna kitu.
Ule usemi wa mwisho wa ubaya ni aibu ukamwangukia mbele yake hakuweza kuukwepa ule mwisho aliouona.
Aliwaza na kuwazua huku akipiga hatua kuelekea ndani. Hakuna lililokuwa sahihi kufanya kwa wakati ule.
Akaingia moja kwa moja hadi chumbani kitandani akameza dawa za kutuliza maumivu ya kichwa.
Akasinzia hadi aliposhtuka siku iliyofuata na kukuta simu yake ikiita.
Alikuwa ni Prisca katibu muhtasi wake, akaitazama kwa muda kabla ya kuipokea.
“Haujambo Prisca!”
“Sijambo bosi shkamoo, ulikuwa umelala?”
“Nimelala hadi sasa Prisca si unanisikia au?” alijibu kwa jazba kidogo.
“Kwa hiyo hata magazeti hujayasoma?” Prisca aliuliza.
“Magazeti? Kuna nini kwenye magazeti.....” alihoji, sasa alikuwa anazungumza vizuri na hofu yake ikasikika waziwazi.
“Hebu ngoja nikusomee hili nililonunua.... “ akasikika Prisca akizifungua kurasa.
“Kumbe tatizo ni mtoto chanzo cha mheshimiwa Lucas kuukacha ubunge... mkewe atibua kila kitu aamua kuachana naye akazae pengine.... aelezea machafu yote ya muheshimiwa....”
Lucas hakutaka kusikiliza zaidi akaikata simu, alipokata simu kwa prisca ilikuwa furaha. Kama kawaida yake umbea haudumu katika kifua chake, alikuwa ameutua tayari.
Baada ya kukata simu ya Prisca, Lucas hakuwa na haja tena ya kupokea simu ya mtu mwingine.
Alimfikiria Edwin walipotoka na urafiki wao... akajiona aliyelaaniwa kwa kitendo alichofanya cha kutembea na mtoto wake.
Nafsi ikamsuta akaona hana njia nyingine ya kujisafisha bali njia moja tu.. kukimbia!!
Kweli alitii wazo hili na akafanya maamuzi....
Baada ya siku tatu, mwili wake ulikutwa chumbani kwake ukiwa unaoza na kutoa harufu.
Alikuwa amekufa baada ya kunywa sumu!!!
Hizi ndizo zilikuwa mbio zake alizoziita sahihi baada ya kukumbwa na mambo mabaya mfululizo.
Edwin rafiki yake kipenzi alisimamia taratibu zote za msiba, akamzika rafiki yake huku akiwa amemsamehe kabisa.
Caro hakuhudhuria mazishi yale na Christina vilevile.......
Kifo cha Lucas kikahitimisha ule msemo usemao kuwa hakuna marefu yasiyokuwa na ncha.
Nami mwandishi wako George Iron Mosenya nimeifikia ncha.....
Ikiwa kuna sehemu yoyote ambayo nimeenda kinyume usisite kunishauri
TAMATI!!!!