RIWAYA; Mpango wa kando

mzaramo

JF-Expert Member
Sep 4, 2006
6,371
5,183
RIWAYA: MPANGO WA KANDO
NA: George Iron Mosenya

SEHEMU YA 1

KADRI karandinga lilivyokuwa linazidi kushika kasi ndivyo akili yake nayo ikazidi kuamini kuwa hakuwa katika ndoto tena bali ni kweli alikuwa ameveshwa pingu katika mikono yake na alikuwa ametoka kuhukumiwa kwenda jela kwa miaka mitatu kwa kosa ambalo hata apewe utulivu mkubwa kiasi gani hawezi kulielezea, alishtakiwa kwa jina tofauti kabisa na kosa asilolijua hata kidogo. Alilalamika mahakami pale kuwa huenda amefananishwa na mtu mwingine lakini akaletewa ushahidi uliomuacha mdomo wazi na hapo masikio yakasikia sauti ya muhukumu ikisema kuwa ataenda jela kwa miaka mitatu na adhabu ya viboko kumi na viwili, sita wakati wa kuingia na sita wakati wa kutoka.
Alijaribu kujitikisa tena huenda alikuwa yu ndotoni lakini badala ya kushtuka kutoka ndotoni akashtushwa na maumiuvu baada ya kunaswa kibao na mtu aliyekuwa pembeni yake.
Ajabu yule mtu baada ya kumnasa kibao hakusema neno lolote bali akaendelea kuimba wimbo alioujua yeye mwenyewe katika namna ya kulazimisha kitu asichokiweza.
Baada ya kuimba imba kwa sekunde kadhaa akamgeukia.
“Nimekunasa kibao kwa sababu ulinitikisa nikiwa naimba wimbo wangu mzuri!!” alimweleza kisha kama ambaye hajamaliza ama anayesubiri kujibiwa alimtazama tena na kuzungumza.
“Hii ni mara yako ya kwanza kuja jela?”
“Ndio.. ni mara ya kwanza!!” yule bwana alijibu....
“Oooh! Karibu sana katika ulimwengu, samahani kwa kile kibao nilidhani wewe ni mwenyeji wa huku... naitwa Crispin sijui mwenzangu...” alizungumza huku akiwa anatabasamu.
“Naitwa Chopa!!” alijibu kwa kifupi.
“Doh! Kuna jamaa ana jina kama lako huko jela... sijui ni Chopa na yeye ama vipi. Ipo siku utakutana naye kama umenyeshewa mvua nyingi... aam! Kwani umenyeshewa mvua ngapi?” bwana aliyejitambulisha kama Crispin alimuuliza Chopa.
Chopa asiyejua nini maana ya mvua alibaki kushangaashangaa.
“Hujui mvua ulizonyeshewa jamaa!! Au dharau...”
“Sijaelewa maana ya mvua..” Chopa alijibu kiuoga. Yule bwana alicheka sana, kitendo kile cha kucheka kikasababisha harufu mbaya kutoka katika mdomo wake ianze kumbughudhi Chopa hata kabla hajaingia gerezani bado.
“Mvua ni miaka uliyohukumiwa....”
“Mitatu!” alijibu kwa ufupi.
“Ahaa! Kama ni miaka mitatu basi unaweza ukaonana naye, ujue tupo wengi sana kule hivyo ni ngumu sana kuwajua watu kwa majina..... halafu hata ukionana naye bado haina maana kwa sababu na yeye ni ndaro tu kama mandaro wengine...”
“Ndaro... ndaro ni nini!!”
“Alaa! Najisahau sana najiona kama nazungumza na mkongwe mwenzangu... ndaro ni fala ama mchovu asiyekluwa na sauti na ukiwa ndaro ni rahisi sana kugeuzwa malkia wa selo...” akasita akamsogelea Chopa sikioni na kumalizia, “Ukiwa malkia maana yake unawaniwa na wanaume na atakayefanikiwa anakuoa....”
Maneno haya ya maudhi yalimkera sana Chopa na wakati huo gari lilikuwa limefikia mlango wa gereza.
Bado Chopa alitaka kuamini kuwa ile ilikuwa ndoto lakini ukweli ulikuja pale alipocharazwa viboko sita vya nguvu, ikiwa ni mwanzo wa kuitumikia adhabu yake ya miaka mitatu gerezani.
Adhabu kwa kosa asilolitambua kabisa!!!
Baada ya viboko vile na kisha kupewa mavazi kama mfungwa rasmi, akamkumbuka mchumba wake Carolina, akakumbuka alivyomuona mara ya mwisho pale mahakamani akibubujikwa na machozi kumshuhudia mpenzi wake katika hali ile.
Akakumbuka mambo mengi kati yao, eti mpango wao wa kuoana ndani ya miezi sita mbele ilikuwa imemezwa na utata ule wa ajabu!!
Chozi la uchungu likamdondoka.
Mlango wa selo ukafunguliwa akaingia akiwa mgeni kabisa!!!


______

HALI ya Caro kiafya ilikuwa imedhoofu sana, mama yake alikuwa mtu wa kwanza katika familia kugundua kuwa mtoto wake hakuwa sawa katika upande wa afya ya mwili na mawazo pia. Macho yake alijaribu kuyaficha lakini bado yalionekana kuvimbiana.
Mama yake hakutaka kulilazia damu hili jambo, siku hiyo akamfuata Carolina chumbani kwake. Alimkuta akiwa analia sana na hapo ni punde tu baada ya kuingia akitokea alipotokea.
Mama alimfuata na kumkumbatia begani, akamfuta machozi na kisha akamuuliza nini kinamkabili.
Hii haikuwa mara ya kwanza kumuuliza swali hili tangu amuone akiwa katika hali ya sintofahamu, lakini siku hii alitaka majibu ya ukweli.
“Caro mimi ni mama yako, hakuna mwanamke yeyote hapa duniani aliyeupitia uchungu wa kukuzaa wewe Caro ni mimi tu! Zungumza na mimi binti yangu, sema mama anakusikiliza!!” mama aliongea kwa sauti iliyojaa hekima na upole sana kwa mwanaye.
Ni kama sauti ya mama ilizidisha uchungu kwa binti yake, Caro akaangua kilio kikubwa ikawa kazi ya mama kumbembeleza hadi akatulia.
“Mama! Mama.... Chopa wangu mama.... Chopa wanguu....” alizungumza huku akiugulia kwa sauti iliyotawaliwa na kilio.
“Chopa... Chopa amefanya nini tena..... ” alihoji mama yule mtu mzima.
“Chopa amefungwa mama, wamempeleka jela miaka mitatu leo mama.. leo hii Chopa amefungwa!” alishindwa kuzungumza kikawaida alikuwa anazungumza huku analia.
Mama alizidi kumtuliza na hapo Caro akaelezea juu ya mkasa uliomkumba Chopa, mkasa usioelezeka na kueleweka kwa sababu hata Caro mwenyewe hakuweza kuuelezea vizuri!!!
Mama alimpooza lakini ilikuwa sawa na bure!!
Siku hii ikawa mbaya sana kwa caro. Ikafuata siku ya pili na kuendelea, hali yake ikazidi kuwa mbaya. Hakuwa akienda kazini tena.... alikuwa ni mtu wa kulia tu ama kubaki ameduwaa kama mwenye utindio wa ubongo.
Japokuwa mama mtu hakuwahi kumuona Chopa hata siku moja, kila siku akiishia kupewa ahadi na mwanaye huyo lakinui alikiri kuwa huenda mwanaye alikuwa katika mikono salama sana. Kwa sababu alikuwa anapata afya na alikuwa mwenye furaha na amani mara zote.
Hivyo kitendo hiki cha Chopa kushtakiwa na kisha kupelekwa gerezani hakika kiliondoka na vyote alivyokuwanavyo!!
Hali ilipofika pabaya ikalazimika baba mtu apigiwe simu akiwa Mwanza kikazi, akasafiri upesi hadi jijini Dare s salaam ili aweze kushuhudia kwa macho hicho anachosimuliwa na mke wake, kwamba mtoto wake wa katikati na pekee wa kike alikuwa katika hali mbaya sana.

Kweli ilikuwa zaidi ya alivyokuwa anaelezwa, Caro hakuwa yule aliyemfahamu. Kwanza alikuwa amepungua sana uzito na kukondeana mwili. Alikuwa anayeelekea kupoteza uwezo wake wa kufikiri maana kuna maswali alikuwa akiulizwa anajibu anavyojua yeye na kisha kuja kujirekebisha baadaye.
Hii haikuiwa hali nzuri, baba akajaribu kuwasiliana na wanasaikolojia akawaleta pale nyumbani kwa ajili ya kumtazama Caro.
Baada ya juma moja wakaelezea kuwa mtoto wao anaathirika ubongo wake kwa sababu ubongo wake unafanya kazi kubwa ya kuusaka ukweli ambao haiwezi kuujua kamwe.
“Mtoto wako anautesa ubongo wake kwa sababu anataka kujua chanzo cha Chopa kutupwa gerezani na hakuna sehemu yoyote ya kuupata ukweli huo zaidi ya kumuona Chopa na amueleze, na kama mnavyosema kuwa imekuwa ngumu sana kuonanana Chopa kwa ambazo na nyinyi hamzitambui basi hii hali ikiendelea hivi kwa muda mrefu huyu mtoto mtampoteza kutoka katika ulimwengu wa wenye akili timamu!!” alizungumza yule mwanasaikolojia ambaye pia ni tabibu.
“Dokta unataka kumaanisha kuwa Caro anaweza kuchanganyikiwa?”
“Hapana simaanishi kuchanganyikiwa maana hapa alipo tayari amechanganyikiwa... namaanisha atakuwa mwehu wa kiwango cha juu!!” alijibu bwana yule kana kwamba lile ni tatizo dogo.
Baada ya jibu lile mama Carolina akasikika akianza kulia, mume wake akamtuliza na kumweleza kuwa kulia hakusaidiii kitu chochote kile jambo la msingi wamsikilize mtaalamu.
“Aaah! Kwa hiyo ndugu zangu, wazazi wenzangu...huyu mtoto anatakiwa afanyiwe maarifa upesi sana... sijui ni kipi kinaweza kufanyika kwa sasa lakini nipeni muda nitafakari ni kitu gani tufanye kumsaidia mtoto huyu.... poleni sana bwana na bibi Mtembei!!!” alimaliza na kuwaaga huku akiwashika mikono kwa zamu.
______

Majuma kadhaa yalikuwa yamekatika, siku hii baada ya kufanya kazi kuanzia asubuhi hatimaye muda wa chakula ulifika. Chopa alipanga foleni ndefu akifuata utaratibu, siku hii njaa ilikuwa imemsumbua sana na hakika japokuwa chakula cha gerezani kilikuwa kibovu bado alikitamani ili tu aweze kuitibu njaa yake.
Tatizo lilikuwa moja ambalo lilimkera na si yeye tu hata wenzake aliowasikia kwa ukaribu walikuwa wanannung’unika.
Yaani wao walipanga mstari kwa muda mrefu lakini kuna watu ambao walikuwa wanakuja moja kwa moja na kuchukua chakula bila kufuata foleni.
Chopa alipoona foleni haisogei kabisa alimwomba mfungwa mwezake, wa mbele na wa nyuma kumtunzia nafasi yake ili aweze kutoa malalamiko kwa askari magereza.
“Bro acha tu, tumeshalalamika kila mwaka lakini hakuna mabadiliko wanajuana nao hao...” bwana mmoja alimwambia Chopa huku akijilazimisha kutabasamu.
Chopa alisita kidogo kisha akaamua kwenda hivyohivyo kushtaki. Yule askari magereza badala ya kuisikiliza shida yake akamuuliza ana miaka mingapi gerezani. Chopa hakujibu yule askari magereza akakisoma kibandiko katika nguo yake.
“Yaani wewe hata miezio sita huna gerezani unalialia kisa chakula... una akili wewe... au nd’o wale walioingia humu kwa kesi ya kuiba kuku.” Alimjibu kwa kebehi.
“Nenda kwenye foleni bwana mdogo chakula kipo kingi utakula na hata usipokula leo bado hautakufa, au kama ukifa itakuwa vyema hautamalizia kifungo chako tena utakuwa huru!!”
Majibu yale yalimkera sana Chopa akajawa na hasira lakini akalazimika kurejea kwenye foleni.
Akiwa pale kwenye foleni alimuona yule askari magereza akiongea na wafungwa wawili na kisha wale wafungwa wakamtazama Chopa kwa pamoja.
Chopa akatambua kuwa yule askari kuna kitu alikuwa amewaambia juu yake.
Punde baada ya maongezi yale wale mabwana wawili wakatoweka machoni mwa Chopa.
Baada ya kama nusu saa wakatokea tena, safari hii walikuwa wamebaki watu wanne tu ili Chopa aweze kufikiwa zamu yake ya chakula.
Wale mabwana wakafika na kumuita kando Chopa. Chopa akawajibu kuwa ni heri achukue chakula kwanza halafu atawasikiliza.
“Oya nenda kawasikilize watemi hao...” jamaa aliyekuwa nyuma yake akamnong’oneza.
Chopa hakujibu!!
“Tumekuita!!” wakasema kwa pamoja wale mabwana. Chopa akawatazama , kisha akaenda upesi kuwasikiliza ili ikiwezekana aiwahi foleni.
“Tumekuona ulipojipenyeza katika foleni, umewapita wenzako waliopanga foleni muda wote wewe umefika na kujiingizaingizatu!! Kwa hiyo kuliko kukikosa chakula kabisa unaombwa kurudi nyuma kabisa ufuate foleni....” bwana mmoja mfupi aliyejazia kiasi fulani alizungumza kwa dharau tele.
Chopa alistuka sana , jinsi alivyokuwa ametulia katika mstari kwa zaidi ya masaa mawili halafu anaambiwa eti aliingilia.
“Bro utakuwa umenifananisha mkuu, mimi nipo hapa tangu saa ngapi sijui, nilitoka kidogo tu kumuuliza jamboyule askari...” akataka kuonyesha hakumuona huyo askari....
“Kuna askari alikuwa hapa... halafu nikarudi.” Alijitetea Chopa.
“Kwa hiyo kumbe basi mimi ni fala wa kutupwa, macho yangu hayaoni nimekufananisha si ndohivyo...” alihoji.
Chopa akageukia foleni na kugundua kuwa alibaki mtu mmoja ili aweze kuhudumiwa. Akaondoka na kuingia katika foleni ili aweze kupata chakula ambacho alikihitaji mno.
Kitendo alichofanya kikawaacha wafungwa wengine midomo wazi ni kama kuna kitu walikuwa wanajua kuhusiana na hao watu wawili.
“Mpishii! Usimpe huyo bwana chakula...” sauti ya yule mwingine mrefu iliamrisha. Chopa akageuka na kuwaona wale mabwana sasa wakianza kumsogelea, wakati huo ndo kwanza m,pishi alikuwa ameupakua ugali anahitaji kumuwekea Chopa katika sahani.
Akili ya Chopa ikafanya kazi upesi, jinsi walivyokuwa wanamsogelea ikamkumbusha baadhi ya matukio wakati huo akifanya kazi ya ubaunsa katika kumbi za starehe.
Hakuwa na mwili mpana lakini Chopa alikuwa anawakabili vyema wateja wasumbufu.
Na hii ilikuwa chanzo cha yeye kukutana na mchumba wake Caro!!
Kwa sababu alikuwa na njaa alitambua wazi kuwa akitumia viungo vyake wale mabwana watambana vibaya!!
Akabaki ametulia huku jicho lake likiwa limeona kitu tayari!
Wale mabwana wakamfikia na kwa sababu alishaitambua shari mbele yake akaona ni heri iwe alivyopanga!!
Ilikuwa ni kitendo cha sekunde moja, akaukwapua ugali wa moto uliokuwa umepakuliwa katika sahani ya mpishi!!
Akautuliza moja kwa moja katika uso wa yule bwana mrefu kisha akatokwa na teke moja kali sana likatua vyema katika kifua cha yule mfungwa mfupi.
Akawaacha wanaugulia kila mmoja akilia kivyake.
Wafungwa waliokuwa kwenye foleni na kandokando walikuwa kimya kabisa wasiamini kile walichokuwa wanakiona!!
“Nipakulie chakula!!” sasa akamgeukia mpishi!!!
Mpishi akatii!
Akampakulia!!
Wakatia anaondoka pale akamuona tena yule mtu mfupi akija mbiombio. Bila kuuweka ule ugali chini na mboga yake, Chopa akatokwa na teke jingine hili la sasa kali kuliko lile la kwanza, likamtupa mtu mfupi chini, sasa wafungwa wakatambua kuwa Chopa hakuwa anabahatisha wakaanza kushangilia!!
“Ukiendeleza huu ujinga wako hukumu yako itaisha hivi karibuni, nitakuua ukatumikie kifungo kaburini. Waambie na wenzako kuwa sipendi masihara!!” Chopa akainama pale chini na kumkoromea mtu mfupi. Kisha akaondoka zake!!!

_____
 
SEHEMU YA PILI

CHOPA mwenye ghadhabu moyoni lakini uso wake ukionekana kukifurahia kile chakula cha gerezani alikuwa akiyakata matonge makubwa makubwa na kuyachocya katika maharage ambayo yalikuwa hayachovyeki kutokana na kuwa yanashabihiana na maji kabisa... na hayakuwa yameiva vizuri na kama hyiyo haitoshi yalikuwa yamejaa wadudu.
Chopa alikuwa akiikunja sura yake kila alivyotaka kumeza tonge.
Akiwa anaendelea na safari ile ya kuyakata matonge na kumeza, alipokuwa ameketi alikuja mfungwa mwingine akiwa na sahani yake akaketi huku akiendelea kula kidogo kidogo, alikuwa anaangalia mbele pasi na kumtazama Chopa machoni lakini alikuwa nazungumza naye.
“Kamanda... wakikuuliza nini chanzo cha ugomvi sema walitaka kukugeuza bibi, hapo kidogo adhabu itapungua lakini ukisema ukweli tu utalimishwa heka tano peke yako au utapewa adhabu ya kukata mbuyu.....” Yule bwana alipomaliza kuzungumza yale alisimama na kuondoka zake bila kuaga bila kumtazama Chopa machoni!!
Maneno ya yule bwana hayakuonekana na maana hadi ilipofika wakati wa kuhesabiwa ili kila mmoja arejee katika selo yake.
Chopa alishangaa kuona anatengwa!!! Wenzake wote wakaingia yeye akabakizwa nje.
Milango ya selo zte ikafungwa, akabaki yeye pamoja na askari magereza wawili.
Akiwa wima bado hajui nini kinaendelea mara ghafla alipigwa ngwala akadondoka chini.
“Unajifanya kuwa tunalingana tumesimama na wewe umesimama....” alifoka bwana mmoja na kisha akaruka ghafla na kurusha mkono ili amnase kofi Chopa.
Chopa akapangua lile kofi!
Balaa likaanzia pale, akatajiwa kosa kuwa anajaribu kumpiga askari magereza.
Kwa kosa hilo atachapwa viboko vine.
Ikawa hivyo, Chopa akalambwa viboko vine vya nguvu!!
Hapo sasa akaulizwa ni kwa nini amepigana na wafungwa wenzake wakati wa chakula.
Upesi Chopa akalikumbuka jibu aliloandaliwa na yule mfungwa ambaye hakuwa akimjua kwa jina.
“Waliniambia maneno mabaya, waliniambia watanifanya mke wao!!” Chopa alijibu kwa kulalamika.
“Sasa ulipoambiwa hivyo ndio ukapigana!!” akatupiwa swali jingine. Akajitetea kuwa hajapigana bali alijaribuy kujitetea walipotaka kumlazimisha zaidi.
Naam! Jibu hili likawa ponapona yake!!
Mlango ukafunguliwa akaruhusiwa kuingia ndani huku akipewa onyo kali!!
Chopa aliingia ndani akaanza kugusagusa sehemu yenye upenyo aweze kupita.
“Kamanda!” ile sauti ya mchana ule ikamuita..... akajongea hadi alipoitwa!!
“Vipi umepona?” alimuuliza.
Chopa akaelezea kilichotokea, yule bwana akamwambia amshukuru Mungu kwani hapo ni sawasawa na amesamehewa tu!!
“Naitwa Pocha walizoea kuniita Mr. P nilipokuwa mtaani unaweza kuamua kuniita vyovyote....” hatimaye yule bwana akajitambulisha.
“Umesema unaitwa Pocha mimi naitwa Chopa almanusura tufanane majina..... ujue wakati naingia niliambiwa na bwana mmoja wa kuitwa Crispin kuwa kuna mtu nafananae majina.. nadhani ni wewe....”
Ikawa mkasa kwa mkasa wakatajiana makazi yao huko uraiani na kidogo wakagusia kesi zilizowaweka humo ndani.
huu ukawa mwanzo wa ukaribu kati ya Chopa na Pocha!!

_____

KITENDO cha kuzungumza na Pocha na kukumbushiana kwa kilaupande chanzo cha kutupwa gerezani kulimfanya Chopa aamke akiwa na mawazo mengi, kichwa kilimuuma sana kwa sababu hakuwa na jibu sahihi la chanzo cha yeye kutupwa gerezani akihukumiwa kukaa humo miaka mitatu.
Katika kumbukumbu zake hizi zilizomletea maumivu ya kichwa alishindwa kuelewa iwapo ni ugeni wake katika mambo ya mahakama na hizi kesi ama ni vipi lakini alijiona kama aliyeonewa kwa kutopewa nafasi walau ya kumtafuta mtu wa kumtetea.
Alipofikiria juu ya mtu wa kumtetea akawakumbuka marafiki pamoja na baadhi ya ndugu zake waliokuwa hapo mjini, ni kweli hawakuwa wengi na hawakuwa na uwezo lakini halahala jama damu ni nzito kuliko maji!!
Lakini sasa unakaribia mwezi mzima hao aliodhani wangeweza kumtetea hawajawahi hata kuja kumjulia hali akiwa gerezani.
Hawa hawakumuumiza sana kichwa aliyemuumiza kichwa alikuwa ni Caro. Inawezekana vipi mchumba wake waliyependana hadi wakati huo hajaenda kumwona gerezani, mara ya mwisho alimuona akiwa kwenye karandinga kupelekwa gerezani.
Kwa mchanganuo huo, Chopa akakiri kuwa katika huu ulimwengu ukiwa matatizoni unakuwa peke yako lakini ukiwa salama unakuwanalo jopo kubwa sana la marafiki!!
Chopa akaamua kusahau kuhusu kupata msaada, wazo lake likarejea juu ya usiku ule wa kukamatwa!!!
Akakumbuka kuwa siku nzima kuna mtu asiyemfahamu alikuwa akimtumia jumbe za ajabuajabu katika simu yake.
Akimpigia anakata, kisha anatuma tena ujumbe mwingine ambao Chopa aliamini wazi kuwa mtumaji alikuwa anakosea namba.
Lakini sasa akiwa gerezani anaona kuwa bwana yule hakuwa anakosea nambari bali alikuwa sahihi kabisa.
Chopa akajisikitikia kwa kuzipuuzia jumbe zile!!
“Lakini si ningekuwa mjinga yaani saa tano usiku mtu ananiambia niondoke nyumbani niende mbali kabisa na nisirudi kabisa nyumbani kwangu wakati huohuo Caro alikuwa njiani anakuja kulala nyumbani kwangu, hakika nisingeweza kufanya ule ujinga!! Ni kweli imenigharimu sana lakini kuna uonevu umetanda katika hili!!!” Chopa alizungumza kwa sauti kiasi huku akiwa anafyeka kipande alichopangiwa kufanya kazi siku hiyo.
“Chopa wa Chopa!!” ilikuwa sauti ya Pocha yule rafiki yake mpya wa gerezani.
Kwa mara ya kwanza akageuka na kumtazama kwa makini usoni mwake, alikuwa yu mjanja mjanja sana haikuhitaji akili nyingi kulifahamu hili.
“Usiache kufyeka hawakawii kutucharaza bakora hawa!!” Pocha akamuonya Chopa ambaye alitaka kujisahau.
Bila kusubiri Chopa akatii, wakaendelea kufyeka huku wakibadilishana soga hapa na pale.
“Jana uliniambia kuna mzito mpaka atoke madarakani labda na wewer ndo utatoka una maana gani??” Chopa alimuuliza swahiba wake yule.
“Aisee hausahau.... anyway mimi nilikuwa fundi simu hadi nilipokamatwa na kutupwa humu,eti nikabambikwa kesi ya wizi kwa njia za mtandao..... ila kiukweli ishu haikuwa wizi sema ujanja ujanja wangu uliniponza. Ujue kaka mimi hapa kuna kitu fulani hivi nahisi nimejaliwa, sijui ni machale sijui ni nini katika akili na mikono yangu ila kuna uhusiano fulani wa kipekee. Na ninakuhakikishia mimi nikitoka humu nahakikisha sikai hapa bongo tena, bongo majungu sana.....” Alizungumza Pocha huku akiendelea kufyeka kwa juhudi. Yaani ni kama walikuwa hawasemezani lolote.
“Yaani mimi katika kuunda simu, nikajikuta kuwa hizi simu hizi za kisasa hizi zinazofungwa kwa loki ya michoro ‘patterns’ basi we unaweka pateni zako mi ukinipa nikijaribu kama mara nne tu nishatibua kila kitu. Mwenyewe siwezi kuelezea hata inakuwaje.... basi bwana si unajua mjini kila kitu biashara bwana. Mtu akiniletea simu nitengeneza hasahasa wakinadada na akina mama, mi nafungua natazama picha nikikutana na picha za kibiashara nazitoa....”
Chopa akaingilia kati na kuuliza, “Picha za kibiashara nd’o zipi maana we nawe una maneno mageni kweli!!”
“...Picha za kibiashara ni zile mtu kajipiga akiwa mtupu ama amepiga na bwana yake wakiwa watupu mi naziuza kwenye magazeti ya udaku..... walikuwa hawanilipi pesa nyingi sana lakini ikafikia siku sasa ya mimi kuwa mjanja na kudai malipo makubwa na ninakuapia Chopa hilo dili lilikuwa dili langu la mwisho kabisa na nisingethubutu tena kufanya mchezo ule.....”

_____

___POCHA ANASIMULIA___

KIMVUAMVUA kilichonyesha katika jiji la Arusha kilipunguza mizunguko ya watu kuingia na kutoka mjini. Hali hii ilisababisha baadhi ya biashara kuzorota....
Kibanda cha kutengeneza simu na kuuza bidhaa ndogondogo kilichomilikiwa na Pocha ama maarufu kama Mista P. Kiliishiwa kukaliwa na marafiki waliokuwa wakijikinga wasinyeshewe mvua. Kwa mpita njia angeweza kudhani ni wateja wamemjalia Pocha hivyo wangeweza hata kumwonea tamaa. Lakini uhalisia aliujua Pocha mwenyewe. Tangu asubuhi alikuwa hajapata dili lolote la maana la kumwingizia pesa. Walau pesa ya kula tu!!
Na hapo mchana alikuwa amekopa chakula kwa mama muuza akiwa ameahidi kulipa jioni.
Majira ya saa kumi na dakika kadhaa jioni alikuja mteja, kama masihara vile Pocha alimuita kuanzia mbali. Mteja akaingia mtegoni, akamchangamkia na hatimaye akasema kuwa ana tatizo la simu yake anahitaji amesahau pateni zake anahitaji simu yake iflashiwe.
Pocha akaichukua ile simu na kuitazama vyema sana, ilikuwa simu ya maana sana na aliyeileta alioneka akuwa sio mmiliki halisi wa simu ilea ma la basi amenunuliwa na bwana yake mwenye pesa.
“Hii hapa elfu ishirini na tano mama!” Pocha aliinadi bei yake huku akiendelea kuitazama simu ile.
Bei ile ikamshtua yule mwanamama,ni kama hakuamini na hapo palikuwa na mawili aidha ilikuwa kubwa sana ama ilikuwa chini sana tofauti na matarajio.
“Na inatengemaa baada ya muda gani maana sitaki ilale!” alihoji kwa utulivu.
“Mara ya mwisho simu ya mtu kulala kwangu ilikuwa mnamo mwaka alfu tisa mia na tisini na mbili.... tofauti na hapo sijawahi kulaza simu ya mtu hapa dadangu!!” Pocha alipiga domo na kusababisha kila mtu kuangua kicheko.
Kasoro yeye tu ambaye hata tabasamu halikumtoka!!
Yule dada akalipia shilingi elfu kumi na kuahidi kuwa akikamilisha hilo zoezi anamlipa kiasi kilichosalia.
“Sasa kaka lakini si wanaflash kwa kutumia Kompyuta wewe hata kompyuta huna...” mwanamama alihoji huku akimpatia ile pesa.
“Mama, ubongo wa mwanadamu una akili mara bilioni moja kuliko kompyuta, Mista P ana ubongo uliotimia.” Sasa alijibu huku akitabasamu na kuikunja ile pesa.
“Kama kweli ubongo una akili kuliko kompyuta naomba basi uiflashi hiyo simu halafu namba zangu zisipotee kutoka humo...”
“Hilo tu, ukija andaa shilingi elfu kumi nyingine ya ziada... Mista P naitibu kama unavyotaka, yaani mimi hata simu ikivunjiika kioo naweza kuunganisha kwa kutumia ubongo wangu na sio gundi....joo baada ya saa zima mama” alijitapa Pocha na kuzidisha vicheko kwa watu.
Mwanamama akajiondokea huku akiwa hana imani ya kutosha na hili lilionekana usoni.
Punde baada ya kuondoka.
Akaitazama simu ile akatulia kwa muda akaitazama katika kioo chake na kisha akauruhusu mkono wake ufanye kama ufanyavyo kila siku.
Akapitisha michirizi ya kwanza ikakataa, akatulia akapitisha michirizi ya pili napo ikagoma. Wakati huo mvua ilikuwa imekatika na wale watu waliojazana pale kijiweni walikuwa wameondoka na kubaki watatu tu.
Hawa walikuwa wakimtazama Pocha huku wakimshangaa sana kwanini amepokea pesa ya watu wakati ni kweli hawezi kuiflashi ile simu!!
Pocha hakuwajibu, sasa alikuwa anajaribu michirizi ya tatu.
Akaipeleka mikono kama akili ilivyotaka.
Akafikisha mwisho, ikafunguka.
“Hureeeeeeeey!! Pesa mfukoni, na pesa hii imethibitishwa kwa matumizi halali kwa ajili ya Pocha... Mista P.” Pocha akatokwa na mayowe huku akiikunjua ile pesa na kweli ilikuwa imethibitishwa kwa matumizi halali kwa sababu tayari alikuwa ameifanya kazi.
Pocha akaondoka akiwa mwenye furaha moja kwa moja akaenda kulipa deni la chakula, akapita dukani akalipa deni la vocha aliyokopa.
Kisha akarejea ofisini mwake.
Tofauti na simu nyingine ambazo kitu cha kwanza akifanikiwa kutoa loki kifuatacho kinakuwa kutazama picha, kwenye hii alichelewa kufanya hivyo!
Na ilikuwa kama bahati mbaya sana akajikuta ameingia kwenye yasiyomuhusu.
Awali zilikuwa picha za kawaida tu, lakini mara akaanza kukutana na picha za ajabu ajabu, alikuwa ni yuleyule mwanamke akiwa na mheshimiwa mbunge wa jimbo mojawawapo la kaskazini, walikuwa watupu kitandani. Sijui kama ni mtu aliwapiga picha ama walikuwa wameiseti simu ili iwapige zile picha.
Pocha alipagawa, upesi akaondoka pale ofisini kwake na kuelekea kwa rafiki yake jirani ambaye yeye anamiliki kompyuta. Huku akazifyonza katika namna ya kunakiri zile picha zote. Kisha akarejea ofisini kwake na wakati huo yule mama alifika.
Pocha mwenye tabasamu akampatia simu yake huku akimweleza kuwa ndio kwanz amemaliza.
“Ukanitangaze mama waambie kuna jamaa anaitwa Mista P. Anatibu simu zote bila kupoteza namba...” wakati anatoa tambo hizi yule mama alikuwa anaduwaa asiamini kila alichokuwa anakiona mbele yake.
Kweli simu ilikuwa imetolewa loki na ilikuwa sawa kabisa.
Akalipia ile huduma na kuaga.
Alipoondoka POCHAnaye akafunga ofisi muda mfupi baadaye. Akaenda kwenye ile kompyuta na kuziweka zile picha katika santuri (CD).
Akaondoka zake kwenda kufanya biashara.
Safari hii akalitangaza dau lake mapema kabisa katika gazeti la udaki akawatumia moja ambayo haiwaonyeshi wakiwa watupu na kisha akasema kuwa anazo nyingine nyingi sana zinazouzika sana.
Lile gazeti likavutiwa na ile biashara!! Lakini halikuwa tayari kutoa ile pesa kwa awamu moja....
Wakamtumia nusu na yeye akatuma picha nusu!!

“Ujue Chopa kila sehemu kuna wakuda... yaani wakuda hawakosekani kila kona. Nahisi kuna mwandishi ambaye anamjua huyu mzito, basi akamvujishia zile picha.
Aisee nikajidanganya kuwa kuna siri baina ya watu wawili, tena sio wawili eti siri kati ya raia na gazeti la udaku. Kesho yake nikaingia kazini... ilwe nafika tu askari hawa hapa.... wakaninyaka.
Sijawahi kuruydi tena uraiani Chopa... na nilipigwa vibaya mno hadi niseme wapi pengine nilizihifadhi zile picha.... nikasema kila zilipokuwa lakini hawakuniamini wakaona jambo jema ni kuninyamazishia humu gerezani. Nd’o maana nakwambia mimi hadi kutoka humu ni mpaka muheshimiwa aamue ama afe na ninaombea afe kwa sababu maamuzi hawezi kutoa hivi karibuni maana anahofia kuwa huenda ninazo picha nyingine. Kwa hiyo huu ndo mkasa wangu kaka.”
Alimaliza kusimulia Pocha na kumwacha Chopa akiwa anayeduwaa, aliduwaa kwa sababu alikuwa akisikia tu kuwa wanaokwenda jela sio wote wenye hatia.
Sasa alikuwa amekutana na ukweli wenyewe.
Ila bora huyu alikuwa analijua lililomsababisha awe jela. Ila yeye Chopa hakuna alilokuwa akilijua hii ilimtesa sana.....


______
 
SEHEMU YA 3

1995, Mwanza Tanzania.

Marafiki wawili waliokuwa wamesoma wote shule ya msingi na ile ya upili mjini Mwanza na hatimaye kuwa kati ya wanamwanza wachache kuchaguliwa kujiunga na chuo kikuu cha Dar es salaam.
Lucas Kazioba na Edwin Mtembei!
Kama masihara vile alianza Mtembei kwa kumshawishi Luca wachukue fomu za kugombea ubunge. Luca aliduwaa sana kwa sababu hakuamini kama ingekuwa rahisi sana kama mwenzake alivyokuwa anawaza....
Kadri siku zilivyosogea mbele na jambo lile kuzungumzwa kisomi zaidi hatimaye wakakubaliana kuwa mmoja achukue fomu ya ubunge na mwingine fomu ya udiwani ilimradi tu isijekutokea siku moja wakajikuta majukwaani wakikandiana kwa sera tofauti.
Edwin yeye alikuwa amewahi kuwa kiongozi katika serikali ya chuo kikuu cha Dar es salaam lakini Luca ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza hivyo alikuwa akijifunza mengi sana kupitia kwa Luca.
Hata kuzungumza aliiga kwa Edwin!!
Siku zikaenda na kufikia siku ya kuchukua fomu, awali walikuwa wamekubaliana mmoja achukue fomu ya udiwani na mwingine fomu ya ubunge lakini lilipobaki juma moja kwa ajili ya kuchukua fomu Luca alitoa wazo jipya, kwa sababu yeye hakuwa vizuri sana katika kuzungumza mbele ya watu basi safari hii iwe ya Edwin halafu yeye atajaribu miaka ijayo. Lakini wazo lake halikuishia hapo akasema atachukua fomu kupitia chama cha upinzani ilimradi ajifunze siasa tu!!
“Aaah! Sasa wakikuchagua itakuwaje si nd’o yale ya kupondana jukwaani?” Edwin Mtembei alimuuliza Luca.
Luka alijibu kimasihara kabisa kwanza aliuponda sana upinzani kuwa kamwe hautakuja kuwa bna mbunge hata mmoja katika bunge la jamuhuri!! Hii ni kwa sababu huu ulikuwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi na hakuna aliyetarajia maajabu yoyote kutoka kwa upinzani!!
Majibu haya yakamshawishi Edwin akakubaliana na uamuzi wa Lucas rafikiye.

Mambo yakaenda kama walivyopanga!!
Baadaye yakabadilika kama masihara, Edwin hakuchaguliwa na chama tawala lakini Luca akasimamishwa na upinzani ili awanie jimbo lile ambalo Edwin alipanga kuliwania.
Walikutana kujadili na Edwin akaapa kuwa atakuwa na Luca bega kwa bega katika kampeni zake.
Kiasi fulani Edwin alikuwa na pesa kumpita Luca hivyo alitumia pesa zake kusaidia usafiri na matangazo ya hapa na pale ili kuwavuta watu katika kampeni za Luca. Awali alifanya kwa siri ili chama alichotangazia nia kisijue hali ilivyoendelea mbele akajiweka wazi kuwa anamuunga mkono mgombea wa chama pinzani!!

Ikawa kama ndoto ya hayawani!!
Ndoto isokuwa na dalili ya kuwa kweli, lakini hatimaye Luca akampiku aliyekuwa mgombea wa chama tawala kwa kura za kumtosha kuwa mbunge wa jimbo lao.
Haya yote aliyaweza kwa sababu Edwin alikuwa anatumia muda wake mwingi kumkaririsha Luca maneno ya kuwashawishi wananchi.
Wananchi wakamuelewa na kumpigia kura zao.
Yule aliyedhani hawezi kuwa hata diwani wa kata,akabadilika na kuwa muheshimiwa Lucas Kazioba.
Miaka mitano baadaye akahamia chama tawala kwa sababu alizodai kuwa upinzani unababaisha!!!
Hiyo ilikuwa mnamo mwaka 2000.
Uamuzi huu ulipokelewa kwa shingo upande kabisa na rafiki yake Edwin am,baye hakuchukua tena fomu za kuwania ubunge kwa sababu hakutaka kukabiliana na rafiki yake wa muda mrefu!!!
Maisha yakaendelea.

_____

Dodoma, Tanzania
Septemba, 2011

Yalikuwa yamepita masaa manne tangu mgeni aliyekuwa amekuja kwa ajili ya kuonana na muheshimiwa mbunge alikuwa akingoja.
Awali alikuwa akitarajia kuwa punde tu baada ya taarifa kumfikia muheshimiwa basi walau atatoka na kumjulia hali na kumweleza ni kitu gani kilikuwa kinaendelea.
Lakini haikuwa hivyo, hili jambo lilimkwaza sana kwa sababu alikuja pale si kama mwananchi wa kawaida bali alikuwa ni mtu wa karibu pia kwa muheshimiwa.
Hatimaye uvumilivu ukamshinda, akaenda tena pale mapokezi na kumuita yule katibu muhtasi na kumuuliza.
“Ulimwambia jina langu na akakusikia kabisa ama?”
Katibu muhtasi alibetua midomo yake mikubwa iliyojazwa rangi nyekundu, akageuza na macho yake juu na chini kisha akamjibu.
“Kila mtu ana jina babangu... na bosi hajasema anasikiliza mtu kulingana na jina lake hapa.” Alimaliza kujibu akaiweza sawa blauzi yake.....
“Aaah! Samahani dada, sina maana mbaya namaanisha kuwa ukimwambia jina langu walau ataujua na uzito wa shida yangu kwa sababu niliwasiliana naye hapo kabla...” yule mgeni alijiongoza asije kutawaliwa na hasira aliyokuwa ameihifadhi kifuani mwake akajibu kwa utulivu.
Kama ilivyokuwa awali dada yule alianza kwa kubetua midomo yake na kisha akageuza macho yake juu na chini kana kwamba ile ni njia mojawapo ya kujiandaa kujibu maswali.
Safari aliongezea jingine la kukwaza nafsi, alikuwa anatafuta ‘big g’ akaitafuta vyema kisha akaiweka katika ulimi wake na kuipuliza ikapasuka na kutoa kisauti cha kukera.
“Sasa kamamuliwasiliana naye hapo kabla mbobna usiwasiliane naye tena sasa hivi... we vipi babangu.” Alijibu kwa sauti iliyojaa maudhi.
Hili sasa yule mgeni likawa zito sana kwake.
“Mpumbavu wa adabu wewe shenzi kabisa, nina mtoto kama wewe umri sawa kabisa shenzi kabisa.... hiyo midomo yako kama ndo ilikupa kazi basi wewe na bosi wako hamna akili...jinga kabisa hili... mi ni mtu mzima vibinti kama wewe vijinga vijinga nilikuta navyo miaka mingi iliyopita na nitamsubiri hapa bosi wako aje akueleze mimi nilikuwa nani lilipokuja sualala wajinga wajinga kama wewe.... lione macho kama shetani!! Unaona kila mtu anayekuja katika hili dirisha anawaza ngono tu kama unavyowaza wewe.... wajinga nyie nd’o mnasababisha wabunge wetu walalamikiwe kuwa wanafata ngono Dodoma.... na laiti kama ungekuwa hapa nje ningekuchapa viboko na usingekuwa na popote pa kushtaki......” aling’aka yule mgeni ambaye kweli umri ulikuwa umeenda lakini alikuwa bado imara sana.
Ukali wake na matusi yote aliyomrushia yule binti yalikuwa dawa tosha kwa yule katibu muhtasi.
Dada akawa mnyonge kabisa, sasa hakubetua tena midomo wala kuzungusha macho badala yake alikazania kwenye neno moja tu.
“Nisamehe baba yangu..... basi yaishe baba yangu!!”
Baada ya takribani dakika tano ya songombingo lile akatoka aliyekuwa na mamlaka ya juu ya ofisi ile.
“Edwin!! Nini kinatokeatena hapo..” alihoji muheshimiwa mbunge!!
“Lucas intavyuu zako za kutafuta wafanyakazi anasimamia nani, huyu mjinga mjinga siku ukipata muda mueleze mimi ni nani na nilikuwa nani.....” alifoka Edwin! Muheshimiwa Lucas akamtuliza, akamshika bega na alipofika pale dirishani akatoa kauli ambayo ilimaanisha alichokuwa akizungumza Edwin dhidi ya yule dada.
“Vero, kesho sihitaji kukuona hapa..... afandee! Hakikisha huyu binti anakaguliwa vizurui kabla ya kuondoka hapa ndani. Si mfanyakazi tena katika ofisi hii!!” ilikuwa sauti kali ya Muheshimiwa!!
Kamamasihara dharau zikamtokea puani Vero!!
Akaipoteza kazi.....

Walipofika nje waliingia katika gari la muheshimiwa mbunge na Edwin hakusubiri wazungumze sana akamueleza kuwaamsikilize shida yake,
Lucas akawa msikivu kama alivyokuwa siku zote kwa Edwin!
Edwin akaelezea tatizo linalomkabili binti yake, akajieleza kwa kirefu sana kama lilivyokuwa na kisha akaelezea wazo lake.
“Nahitaji Lucas kama yawezekana na ninaamini inawezekana kabisa, nisaidie huyu mtoto walau akakae nje ya Tanzania hata kwa miezi miwili tu.... ujue Caro ndo binti yangu wa ujanani na sina binti yeyote... nisijieleze sana historia ya caro unajua mwenyewe nampenda sana yule mtoto. Eti sasa hivi daktari ananiambia eti Caro akiachwa kama alivyo anaweza kuwa mwehu au tahira wa kiwango cha juu kabisa aaargh!!” Edwin alishindwa kuzungumza akaanza kulia.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kabisa Lucas kumuona swahiba wake akitoa machozi hadharani.
Nafsi ilimuuma sana!!
“Sasa Edwin unacholia nini eeh! Si umeshakuja huku kwangu na umesema unachohitaji niache basi na mimi niongee au? Tulia bwana Edwin!!” Lucas alimbembeleza rafiki yake wa muda mrefu.
Baada ya Edwinkutulia kidogo hatimaye Lucasa alizungumza nakutoa kauli yake.
“Edwin rafiki yangu unayenijua kupita marafiki zangu wengi, umenisimamia katika shida zangu mara nyingi sana na sihitaji kuzihesabu hizo mara nyingi ili nijue najihusisha katika hili kwa kiwango gani, tatizo lako ni langu nakumbuka hata caro alivyozaliwa tukiwa mwaka wa kwanza chuo tulihangaika wote kumbeba mama caro hadi hospitali, sasa hata hili siwezi kukuachia peke yako. Kajipange huko Mwanza ukiwa tayari niambie nimfuate caro lini.... nampeleka Caro London!! Sitaki ujinga kabisa linapokuja suala lako Edwin!! Nasema hivi nampeleka caro London... nini miezi miwili bwana nasema atakaa huko miezi sita kama tatizo bado halijaisha nampeleka Amsterdam Uholanzi huko...... Edwin wewe ni wangu. Haya sasa lipo la kukufanya ulie tena?? Kama lipo niambie!!” alimaliza kuongea vyema rafiki yule wa kweli.
Edwin akabaki mdomo wazi, wakati yeye akiwaza kuwa patakuwa na mlolongo mrefu katika kusaidiwa shida yake na akiwa anawaza walau Caro aende kuishi kampala ama Mombasa anashangaa huyu bwana anakusudia kumpeleka caro London!!
Alibaki akitokwa machozi ya furaha, akatoa shukrani za dhati na kwa mara chache kati ya nyingi wanazowasiliana akamuita kwa kutumia cheo chake.
Mheshimiwa Lucas Kazioba!!

_______


TANGU Pocha amuulize Chopa kuwa yawezekana ile kesi yake na hatimaye kuhukumiwa kwenda gerezani yaweza kuwa mpango wa kando, katu hakuwahi kumfafanulia nini maana ya mpango wa kando, zaidi alimweleza kuwa amegundua kuwa chanzo sio mpango wa kando huenda ni mambo mengine tu!!
Chopa akachoka kumsisitiza kwa sababu hata kama angejua sababu ya kufungwa hakuwa na namna ya kutoka gerezani.
Akaamua kupuuzia kujua maana ya lile neno.
Siku zikaenda hatimaye ukawa mwaka mmoja gerezani, Chopa sasa alikuwa yu mzoefu kabisa na hakujali kuhersabu siku kama alivyokuwa anafanya zamani hizo.
Alishazoea sasa kuwa hakuna wa kuja kumtembelea pale gerezani, hivyo ndugu zake ni wafungwa wengine wenzake alionao humo ndani.
Kama kawaida ukiwa mtetezi wa wanyonge unakuwa mtu wa watu, na hili lilikuwa kwa Chopa. Alipendwa sana.
Kama walivyonena wazee wetu wa zamani wenye maarifa walisema kuwa ni kawaida kabisa kuwa vizuri kamwe havidumu!!
Mwaka wa pili ulivyoanza pale gerezani, wakiwa wanapata chakula Pocha alimwomba Chopa wazungumze kidogo.
Chopa akatega sikio kumsikiliza......
“Chopa nina taarifa moja mbaya sana inayonisumbua kichwa changu.....” akasita kisha akapiga tonge moja la ugali.
“Mmoja kati yetu humu ndani anakaribia kuondoka, sasa sijui anaondoka kwa misingi ipi. Sijui ni kifo, sijui anahamishwa gereza, sijui ni msamaha wa raisi ama vipi?” alizungumza kwa majonzi Pocha.
“We nani amekwambia.....” Chopa aliuliza kwa makini.
“Mikono na akili yangu, nilikuwa nachora kitu fulani nikajikuta naingiwa na fikra hizo na mahusiano kati ya akili yangu na mikono nilikueleza pale mwanzo kuwa nayaheshimu sana.... sasa naomba na wewe uheshimu pia. Kama ikitokea kweli tunatenganishwa iwe kwa kifo, kuachiwa huru ama vinginevyo napenda nitumie fursa hii kukueleza kuwa umekuwa na umuhimu sana katika maisha yangu, na zaidi kama ni kuondoka kwa kifo naombea niwe mimi...” Pocha alisema akiwa anamaanisha.
“ Kwa nini wajiombea mambo mabaya Mista P”
“Chopa kabla haujaja hapa gerezani kuna wajinga wawili walikuwa wamekaribia kunifanya mke wao... najua kwa nguvu walizonazo halafuy eti wewe usiwepo watanioa wale. Hakuna kitu sipendi kama kufanywa hivyo, we mwenyewe si unawaona waliofanywa hivyo walivyo kwa sasa.....” alizungumza kwa majonzi sana.
“Tunalala nao selo moja ama...” Chopa aliuliza. Pocha akatikisa kichwa kukubali.
“Tukiingia kulala nionyeshe nitafanya kitu kizuri tu!”

____
 
SEHEMU YA 4

Walipoingia katika selo zao Pocha akafanya kama alivyoagizwa...
Chopa akawabana watu wale huku akiwaeleza kuwa yeye ni mtu wa usalama wa taifa hivyo ikitokea ameondoka pale ndani wakijifanya kumsumbua Pocha watakiona cha mtema kuni......
Aliwabana katika maana halisi ya kuwatia adabu!!

Ikawa giza na kulipopambazuka alikuwa ni Chopa aliyetolewa gerezani, na hakuna aliyejua wapi amepelekwa!!
Kitendo kile kikamfanya Pocha ajiulize mara mbilimbili juu ya uhusiano wa akili yake na mikono yake.
Na ni vipi atumie uhusiano huu katika kujiweka katika hali nyingine ya kimaisha!!
Akaamua kulishughulikia hilo jambo.

Majuma mawili baadaye akapambana aweze kuonana na mkuu wa gereza!!!
Akafanikiwa kuonana naye akamuelezea alichopanga kumweleza akiamini kuwa kitakuwa na manufaa kwa upande wake............

______

KWANZA ilianza simu ya mkononi, iliita kwa muda mrefu kiasi. Mwenye simu akaitazama katika kijicho cha kuchungulia kana kwamba anaepusha kumtambua ni nani aliyepiga ile simu. Ilikuwa kama alivyodhani mpiga simu alikuwa yuleyule asiyetaka kuipokea simu yake. Haikuwa kwa sababu ya madeni ama ubaya wowote lakini nafsi ilikuwa ina mashaka labda kuna lolote baya limefichuka tayari.
Baada ya simu ya mkononi kuacha kupokelewa simu ya mezani ilianza kuita. Ilikuwa nambari ileile inampigia.
“Prisca!! aliita kwa sauti ya wastani na baada ya sekunde kadhaa mbele yake alikuwa amesimama msichana aliyevalia nadhifu!
“Bee muheshimiwa!! Yule binti aliitikia wito.
“Pokea hii simu mwambie kuwa nipo katika kikao tangu asubuhi sijarejea ofisini....” alitoa maelekezo yale kivivu kabisa.
Yule binti alitii, lakini alipoufikia mkonga ana kutaka kuunyanyua simu ilikuwa imekatika tayari.
“Naona amekata!” alijieleza Prisca.
“Ok! Namba ya dada wa Airport si unayo, mwambie anifanyie utaratibu wa tiketi ya kwenda London baada ya masaa arobaini na nane mwambie azingatie sana na isishindikane!! Nenda ukawasiliane naye sasa hivi, mimi natoka... nitakachochukua kwako ni tiketi na sio maneno” alizungumza kwa ukali kiasi wakati huo anasimama.
“Mh! Bosi wangu huyo safari zaidi ya raisi wake!!” Prisca alisema kiutani huku akitabasamu, hii haikuwa mara yake ya kwanza kumtania bosi wake huyo.
“Whaat! Mpumbavu nini, tangu lini umeanza kazi ya kunipangia safari, nakuuliza we binti nilikuajiri hapa kuanza kunihesabuia mara ngapi au kutimiza yale ninayokuagiza... shwain kabisa....kwa hiyo mi nikisafiri kuliko raisi wangu inakuumiza nini, ul;itaka usafiri wewe au.. haya basi kuwa mbunge mimi niwe sekretari wako... hovyo kabisa... nipishe hebu nipite.. pishaa!! Mambo ya Lucas naomba umuachie Lucas mwenyewe bastard!!” alibwatuka muheshimiwa mbunge akimuacha katibu muhtasi wake akiwa haamini anachokiona mbele yake na kukisikia, hii ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwa bosi wake huyo kumfokea na kumtukana namna hii. Bosi huyu alikuwa mtani wake sana.

Muheshimiwa Lucas Kazioba alipiga hatua kubwa kubwa akatoka nje akiwa amebeba koti lake la suti. Alipofikia gari lake akaanza kujipekua huku na kule huku akizungumza peke yake.
Alipekua kila kona, na mara akapata wazo kuwa huenda anachokisaka kwa fujo zote hizo amekisahau ofisinii ile anageuka ili arudi anamuona Prisca akijongea kwa hekima zote na adabu kumuendea akiwa amezishikilia funguo za gari za bosi wake.
Fadhaiko likamuandama muheshimiwa akajisikia vibaya sana kwa maneno aliyomuambia binti yule lakini bado binti hakuweka kinyongo akatambua kuwa amezisahau funguo akampelekea.
“Prisca... nisamehe mama yangu, nimevurugwa kupita maelezo nadhani unanijua si mtu wa kutukana na kufoka kama nilivyofanya nakuomba sana unisamehe....” Lucas aliyasema yale huku aibu zikiyatawala macho yake, lakini pia sauti yake ilikuwa imechoka sana. Bila shaka kuna jambo zito lilikuwa linamkabiri.
“Usijali muheshimiwa Lucas, sisi ni wanadamu na kamwe siku huwa hazilingani...nimelielewa hilo na nimeyasahau yote palepale. As long as hujanipunguza mshahara basi yote yaliyobaki huenda nilistahili...” Prisca alijibu huku akijilazimisha kutabasamu.
Maneno ya Prisca yakamchoma Mh. Lucas, na sasa hakutaka kuomba tena msamaha kwa maneno, akamsihi Prisca asubiri kidogo. Akafungua gari lake na kunyofoa bahasha moja ya rangi ya dhahabu!!
“Pokea hii.... haina maana yoyote mbaya nimejisikia tu. Hii itakusaidia kuwa maikini wakati unazungumza na dada wa airport kuhusu tiketi yangu, si unajua wanavyokera watu wa airport... sasa hii ni kinga ya kutokwazika. Basi baadaye!!” akapanda kwenye gari bila kusubiri asante ya prisca!!
Lucas alipoondoka upesi Prisca akaifungua ile bahasha, akahesabu zile pesa kana kwamba anahakikisha wakati hakutajiwa kiasi sahihi ni ngapi.....
Ilikuwa mshahara wake wa miezi miwili, shilingi laki tisa!!
Prisca alisahau kabisa kama alitukanwa na bosi wake.
Amakweli pesa sabuni ya roho!!
Lakini Prisca alikuwa wa tofauti kidogo, licha ya pesa zile kumsahaulisha matusi ya bosi, lakini kile kitendo cha bosi kuitaka safari ile ya haraka huku akiwa amepagawa hakukipuuzia hata kidogo alihisi kuna jambo zito linamkabili bosi wake.
Umbea ni kama rangi ya ngozi jama unaweza kujifanya umeuacha lakini likitokea tukio la kuhusu umbe utajikurta umeshiriki tu!!!
Prisca hakuiacha asili yake!!
Akairejea fani yake!!!
Laiti kama angeikumbuka ile kauli ya umbea hauna posho abadani asingejihusisha tena na umbea.... lakini hakuukumbuka usemi ule.
Ni kawaida ya vijana wa kisasa kuwapuuzia wahenga!!!
Prisca naye alikuwa kijana.

_______


Desemba, 2013
Mara, Mugumu Serengeti

__MTU HURU__

Lango la gereza lilifunguliwa, takribani mwaka mzima uliopita lango lile lilipofunguliwa yeye na wenzake walikuwa wameveshwa bangili zisizopendeza machoni kuzitazama na usiombee kuzivaa.
Walikuwa wameunganishwa kwa pingu, na kama si pingu basi walikuwa wamewekwa katika karandinga huku ulinzi ukiwa mkubwa sana.
Lakini siku hii alikuwa huru kabisa, alisindikizwa hadi getini, hapo alikuwa amekabidhiwa pesa kiasi sawa na ujira wake kwa kulitumikia gereza. Akapewa na ziada ya usafiri kwa sababu hapo awali alihamishwa kutoka gereza la Ukonga Dar es salaama kabla ya kupelekwa Kiomboi Singida na hatimaye gereza la mahabusu la Mugumu Serengeti!!
Gereza pekee katika wilaya ile.

Alipiga hatua kama sita kisha akapiga goti chini akainama akainyanyua mikono yake juu akaanza kumshukuru Mungu huku akilia kilio kikuu kwa sauti ya chini kiasi lakini machozi yakibubujika kwa kasi.
“Mungu! Mimi si mtiifu sana kwako, sikumbuki kama nimekutumikia kwa muda mrefu lakini kwa uweza wako wewe nipo hai na huru leo... ninayo mengi ya kukushukuru lakini naomba nikukabidhi kwako wenzako waliobaki katika gereza hili moja kati ya magereza mabovu niliyowahi kuyashuhudia katika mapito yangu, Baba iamshe serikali ifike huku na kuuimarisha ukuta wa gereza hili kabla haujawaangukia waja wako, waamshe wabunge waje kutazama huu mrundikano katika gereza, waamshe wanasheria waje kuwatetea waliofungwa kimakosa ama kwa kuonewa.... na kuu la msingi baba nipunguzie hii hasira ama la kam,a hii hasira haitafutika katika moyo wangu, naomba unisamehe baba kwa sababu sitatulia kabla ya kumtafuta yeyote yule aliyehusika katika mpango huu.... mpango wa kunipotezea dira ya maisha yangu.....”
Alikaa kimya akiwa ametulia pale chini kwa muda akiamini kuna wapiti njia kadhaa wanamshangaa lakini hilo halikumuumiza kichwa.
Akasimama hatimaye hakujihangaisha kujifuta vumbi!!
Akageuka kulitazama lango la gereza ambalo lilikuwa limefungwa tayari. Akatikisa kichwa na kulazimisha tabasamu, alipopiga hatua nyingine mbele akajisemea.
“Asante raisi kwa msamaha huu kabla ya kukimaliza kifungo changu, najua sikustahili wapo waliostahili kusamehewa..... ila asante”
Akamaliza na kujifuta machozi kisha akapiga hatua kuelekea popote anapoweza kuelekea.
“Babaa... baba!” alisikia sauti ya mwanamke ikimuita.
“Tacho hano mona wane.. tacho ulaghere! Weii mona wane....” mwanamke yule alizungumza kikabila.... yule mtu huru hakuelewa anachomaanisha lakini ishara ya mkono ni kama alikuiwa akimuita.
“Wewe ni wa huku kwetu...” yule mama alimuuliza huku akionyesgha huruma ya hali ya juu.
“Hapana mama..shkamoo, mimi si wa huku..”
“Aaah! Nilidhani ni mkurya, nilikuita uje ule chakula mtoto wangu, aaah! Ona walivyokuchubua chubua....aaah! gereza hili gerezaaa lilimmeza mtoto wangu wakampiga akafia huko eti kisa alimtukana balozi... aaargh!” mama akashindwa kuzungumza akaanza kutokwa machozi.
Na wakati huohuo akaifungua chupa ya maziwa ambayo alikuwa anauza kama biashara akammiminia mtu huru. Yule bwana akapokea na kunywa, maziwa yale yalimchangamsha na kumtia nguvu.
“Unaitwa nani?” alimuuliza wakati anamalizia kunywa yale maziwa.
“Naitwa Manfred Gregory!!”
“Mnifureti!!” alijari8bu kutaja jina lile yule mama... lafudhi ya kikurya ilikuwa ikimsumbua.
“Niite CHOPA!!” mtu huru akabadilisha jina ili kumrahisishia yule mama.
“Chopa.. eeh! Pore mwanangu, sasa usiangarie nyuma usitazame sijui nani alikuweka ndani sijui nani alikudhurumu haki yako we kapambane na maisha tu. Yariyotokea uyasahau sawa mwanangu!!” mama alimsihi Chopa.
Chopa akakubaliana na yule mama ambaye ‘R’ na ‘L’ zilikuwa tatizo kwake.
Akamshukuru kwa maziwa kisha akaondoka, akatembea hadi alipoipata nyumba ya kulala wageni!!
Akaipata ya bei ya kawaida akaingia humo. Akaoga tena kwa mara nyingine, hapo awali alioga gerezani kabla ya kutoka rasmi!!
Wakati anaoga akawa anakumbuka juu ya siku yake ya mwisho uraiani!
Siku aliyokamatwa na kisha kutupwa gerezani akisomewa shtaka la kughushi vyeti feki na kujipatia kazi asiyostahili hivyo alikuwa anashtakiwa na jamuhuri ya muungano wa Tanzania.
Kesi hii ilimfanya asite kidogo kuoga, akaanza kuzungumza peke yake.
“Yaani mimi nimeishia kidato cha nne, nikapata daraja la pili, halafu anatokea mtu anasema nimeghushi vyeti?? Kazi yenyewe bora ingekuwa inaingiza milioni nyingi, yaani kazi ya mshahara laki na nusu chakula na usafiri juu yangu, anakuja mtu ananipeleka gerezani... hivi hii ni haki?? Eeh! Ni haki hii?” alijiuliza mwenyewe.
Alipomaliza kuoga akakiendea kioo kikubwa kilichokuwa kimebandikwa ukutani.
Hapa ndipo Chopa alilia kama mtoto tena..
Mwili wake ulikuwa na mabakamabaka, ngozi yake ilikuwa hovyo kabisa, akageuka na kujitazama mgongoni.
Ilitisha sana hali aliyokuwanayo, mfanowe ngozi yqa punda aliyebebeshwa mzigo kwa muda mrefu akachubuka na kuacha jeraha na mwenye punda asijali hayo akaendelea kumbebesha mizigo.
Chopa alilia sana na hii hali aliyoitazama kwa macho yake mwenyewe ikamfanya azidi kuifikiria kesi yake.
Na hapo akazikumbuka tena zile jumbe alizotumiwa kabla ya kuingia gerezani.
Akaukumbuka ujumbe wa kwanza.
“SIKU ZAKO ZINAHESABIKA SI UNAJIFANYA MJUAJI! TUTAONA MJUAJI NANI KATI YA MTU HURU NA ANAYEENDA KUUPOTEZA UHURU.”
Huu ulikuwa ujumbe wa kwanza siku ile asubuhi, ujumbe alioupuuzia kwa kuamini kuwa umekosea njia.
Chopa alihangaisha sana kichwa chake, akawafikiria ndugu zake. Eti hakuna hata mmoja aliyefika gerezani kumjulia hali.....
Akamfikiria Caro mchumba wake, eti na yeye kwa miaka hiyo miwili hakuwahi kwenda japo kumsalimia!!
Kichwa kilimuuma sana alipoyafikiria haya, kujiepusha na haya akajirusha kitandani. Godoro laini lisilokuwa na hiyana likampokea, akalivuta shuka na kujifunika.
Nadhani haitakiwi kuendelea kusimulia kilichotokea!
Miaika miwili hujalalia godoro lililo katika mazingira mazuri halafu unajikuta eneo kama hilo......
Zilihitajika kelele za milio ya risasi kumwamsha mtu huru huyu, Chopa!
Wakati Chopa analala usingizi wa samaki aitwaye Pono....
Mahali pengine nchini Tanzania kulikuwa na majadiliano mazito!
Kuna mtu huru mwingine alikuwa anaongezeka!

______
 
SEHEMU YA 5

Dar es salaam!!

AWALI bibie Christina au maarufu kama mama Lucas alikuwa anadhani ni utani mumewe alipomtumia ujumbe kwa njia ya simu na kumueleza kuwa ana mpango wa kuachana na siasa haraka iwezekanavyo.
Christina aliamini kuwa huu ni utani kwa sababu mumewe ambaye raisi alikuwa na kila dalili ya kumpa uwaziri eti leo hii aseme anataka kuacha siasa.
Aliujibu ujumbe ule kwa kicheko tu! Kisha akapuuzia.
Majira ya saa nane mchana mumewe alirejea nyumbani akionekana kuwa hakika ana jambo zito kichwani mwake.
Alifika na kuingia chumbani moja kwa moja, Christina ambaye alikuwa mbunge viti maalumu alifuata nyuma na kuingia chumbani alipoingia mume wake.
“Una nini muheshimiwa!!” alimuuliza, ikiwa ni kawaida yao kuitana cheo hicho wanapokuwa nyumbani.
“Kama nilivyokuandikia ujumbe ule ninamaanisha nilichokwambia, nahitaji kuwa mtu huru!!”
“Mtu huru??” aliduwaa Christina mkewe Lucas Kazioba!!
“Ndio nahitaji kuwa mtu huru nifanye mambo yangu, miaka yote hii kuanzia mwaka 1995 nadhani sasa niwaachie nyie, na jimbo langu la Nyamagana achukue mtu mwingine, ujue siasa ni kama mbio za vijiti tunapokezana unapochoka na kumpatia mwenye nguvu!!” alijibu Lucas kwa sauti iliyopooza.
“Mume wangu, hebu acha masihara basi.... uache siasa wakati raisi amekuahidi uwaziri na ndiyo ilikuwa ndoto yako mpenzi wangu!!” mke wa Lucas alihoji huku sasa aklimshika mumewe begani.
“Siutaki tena huo uwaziri acha awape watu wengine, yaani hata nikiambiwa kuwa 2015 ni mimi nitagombea uraisi kwa tiketi ya chama sitakuwa tayari, sio tu najivua madara hapa naacha siasa kabisa. Nitabaki kuwa mshauri tu kwa vijana wanaotaka kujiunga na siasa!!” alisisitiza Lucas....
Sasa Christina ambaye alikutana na mume wake huyu bungeni mnamo mwaka 2007 na kuanzisha mahusiano na hatimaye kuoana mwaka 2009, alianza kuamini kuwa Mh. Lucas hakuwa na masihara hata kidogo.
Akabaki kimya asijue la kusema. Akiwa kimya bado, mumewe alizungumza tena kama kumaliza ule mjadala.
“Panapo majaliwa kesho kutwa alfajiri nitakuwa aidha ndani ya KLM ama EMIRATES nakimbia London mara moja..... sasa mi napumzika naomba uniamshe saa kumi.” Akamaliza mazungumzo yale huku akiaga kwenda London kama anayeenda soko la jirani hapo kununua bilinganya na matembele.
Mh. Christina Lucas alichoka!!!
Mumewe alikuwa amebadilika ghafla mno.

_____

FAHAMU zilimrejea tena Chopa majira ya saa kumi na moja jioni, maziwa aliyopewa na yule mama mkarimu wa kikurya yalimfanya alale vyema bila tumbo kumpigiza kelele za kuomba chakula.
Lakini majira hayo ya saa kumi na moja tumbo lilianza kulalamika kuwa yale maziwa yalikuwa yamemalizika.
Chopa akaamka na kuingia bafuni kujimwagia maji tena, kisha akatoka kwenda nje kutafuta chakula na kukata tiketi ya basi kwa ajili ya kwenda Arusha siku inayofuata.
Hii ni baada ya kuambiwa kuwa hakuna mabasi yaendayo Dar es salaam moja kwa moja, hivyo ilikuwa ni lazima aunganishe!!

SIKU ambayo Chopa anafanya safari yake ya kwenda Arusha ndani ya jiji la Dar es salaam mheshimiwa Lucas naye alikuwa katika maandalizi ya mwishomwisho kwa ajili ya kuruka kwenda nje ya nchi.

______

LONDON, Miaka miwili nyuma (2011).

Ilikuwa safari yake ya kwanza kabisa kwa usafiri wa ndege.
Ikiwa ingekuwa safari ya kutoka Mwanza kwenda Dar es salaam pekee ilikuwa ya kihistoria kwake, vipi kuhusu safari ya kutoka Dar es salaam kuelekea katika mojawapo ya majiji yanayozungumzwa zaidi duniani.
Jiji la London!!
Hakika kuna baadhi ya matatizo hayatatuliwi na wanasaikolojia, badala yake yanatatuliwa na mazingira.
Caro alikuwa hajawahi kuota kuingia katika ulimwengu huu.
Mheshimiwa Lucas alimfikisha Caro nyumbani kwake na kumtambulisha kwa mkewe ambaye tayari walikuwa wamejadiliana naye kuhusiana na matatizo yanayomkumba binti huyo. Hivyo makubaliano ya kumsaidia waliyapanga wote wawili.
Baada ya siku mbili za mapumziko Lucas akaongozana na Vero kuelekea jijini London.
Walitumia ndege ya shirika la Emirates.
Ilikuwa safari ndefu sana lakini kwa Caro ilikuwa safari ya kushangaza mno, uso wake ulionyesha mshangao ule na hamu zote za kutua jijini London.
Wakati Caro akiuliza maswali ya hapa na pale na Lucas akimjibu kiufasaha, hatimaye Vero alipitiwa na usingizi.
Ni hapa ambapo Lucas alijikuta akipatwa na kumbukumbu za kipuuzi sana ambazo alijaribu kuzipuuzia lakini ziliendelea kumuandama.
Kwanza aalijisemea, “hawa watoto wa kike hawa wanawahi kweli kukua, kaone haka katoto”
Alisema hayo huku akiweka picha mbili katika kichwa chake, picha ya kale katoto kadogo Caro kalikozaliwa mnamo mwaka 1992 wakati huo wakiwa chuoni mwaka wa kwanza na rafiki yake kipenzi Edwin.
Baadaye Caro akafikisha miezi miwili hatimaye mwaka.......
Akaukumbuka utani waliokuwa wakirushiana na Edwin, Lucas alimwambia Edwin kuwa amezaa mtoto mrembo sana hivyo apambane sana kusoma ili aje apate kazi nzuri amlinde mtoto wake, Edwin naye akamwambia Lucas afanye upesi azae mtoto wa kiume ili siku moja amuoe Caro na urafiki wao ili amlipishe mahari kubwa sana ya kumkomoa.
“Yaani Luca ukileta mtoto wako anataka kuona huyu malikia wangu nakuhakikishia kuwa nitakufilisi, yaani nakutajia mahali hata milioni mbili”
Luca akaukumbuka usemi huu akajikuta akitabasamu, aliifikiria milioni mbili ya wakati ule wakiwa wanasoma ilivyokuwa pesa kubwa yenye thamani akaifananisha na ya wakati uliopo akasikitika sana.
Maisha yakaendelea hatimaye Caro akafikisha miaka kumi, Luca akazidi kumsifia Edwin kuwa hakika kwa caro amelamba dume!!
Si tu alikuwa mrembo bali hata darasani alikuwa vizuri!!
Alipomaliza kumfikiria caro wa enzi zile akamtazama Caro aliyeketi pembeni yake, caro mwenye umri wa miaka kumi na tisa mwaka huo 2011.
Macho ya Lucas yakaanguka katika kifua cha yule binti, akazikumbuka enzi zile kakiwa katoto kalikuwa kanatembea kifua wazi na hakuna aliyejali, sasa aliuona mzigo mdodo wa embe dodo changa zilizoota katika upande wa kifua chake katika namna ya kupendeza.
Kisha akafumba macho yake na kukumbuka maumbile ya nyuma ya binti yule.
Akapandisha macho yake hadi katika midomo ya Caro, hapa sasa akajikuta akimeza mate ya matamanio bila ya kutarajia.
Akauchukua mkono wake na bila kutarajia akamgusa Caro shavuni!!
Caro akashtuka kutoka usingizini. Mheshimiwa Lucas akajikuta akitokwa na swali la kipuuzi.
“We Caro hivi ulikuwa umelala au?” alimuuliza kizembe!
Caro akajibu hapana!!
Lucas alijaribu kuzikabili hisia zilizomwandama lakini zilikuwa zimekuja kwa nguvu kubwa sana iliyousukuma moyo wake katika namna ya kushindwa kujizuia.
Alijilazimisha kuukumbuka urafiki kati yake na Edwin ili aweze kumchukulia Caro kama mtoto wake lakini hata hii haikusaidia.
Mara akamtazama tena Caro aliyesinzia, na hapo akakumbuka kuwa kuna bwana aitwaye Chopa ambaye yupo gerezani akitumikia kifungo cha miaka mitatu, eti huyo bwana ndiye ambaye ana mamlaka ya kuzitoa nguo za caro na kumfanya vyovyote atakavyo.
Hili jambo likamkera sana mheshimiwa mbunge na kuhisi huyo bwana ambaye hamjui hata sura yake, hana hadhi ya kummiliki Caro.
Akavihesabu vidole vyake.
“2011, 2012, 2013, 2014 mh! Bado sana kutoka kwake!!” akajisemea baada ya kuihesabu hukumu ya Chopa.

SANDERSON HOTEL, LONDON

Jiji la London ni mojawapo ya majiji yenye uwingi wa Hoteli za kisasa nyingi zakiwa ni za hadhi ya nyota nne na tano.
Jiji hili lina jumla ya hoteli elfu moja na mia sita, na katika orodha hiyo hoteli ya Sanderson ni ya arobaini kwa ubora.
Wakati akiwa Tanzania mheshimiwa mbunge tayari alikuwa amefanya mawasiliano kwa ajili ya kuandaliwa chumba kwa ajili ya usiku huo atakaofika London.
Ilikuwa kama a,livyoagiza, alipotua uwanja wa ndege akapokelewa na gari kutoka hoteli hii.
Kuanzia pale uwanja wa ndege ungeweza kugundua ni kiasi gani hii hoteli ilikuwa na huduma za kisasa. Kujali mteja na kwenda na muda!!
Kufikia chumbani huku hapasimuliki, kuanzia sehemu ya kulala hadi bafu la kuoga.
Vyote hivi vilikuwa vigeni sana kwa Caro.
Ilianza kama masihara, wakala pamoja wakazunguka hapa na pale na kisha ukafika usiku wa muheshimiwa mbunge aidha kukabilianana tamaa iliyomuandama ama kutii kiu yake na liwalo na liwe.
Muheshimiwa mbunge alitumia faida ya goli la ugenini, Caro yu mgeni jijini London akiwa anashangaa kila kitu anachokiona.
Siku hiyo walilala chumba kimoja, kila mtu akiwa katika kitanda chake.
Usiku huo ukapita salama kabisa, ukaja usiku wa pili na wa tatu katika hoteli hiyo ambayo kila panapoitwa asubuhi basi shilingi lakini nne za kitanzania zinakuwa zimeteketea.
Hivyo kwa siku tatu zilikuwa ni milioni moja na laki mbili, sahau kuhusu kufuru nyingine wanazofanya wakienda kutembea kati kati ya jiji la London.
Hatimaye ikawa siku ya tano, muheshimiwa mbunge akaamua iwe itakavyokuwa.
Akatumia ule usemi wa mtoto wa mwenzio mkubwa mwenzio.
Caro akiwa kuku mgeni na kamba yake mguuni muheshimiwa akarusha mpunga kuku akaufuata.
Ikawa usiku wa namna yake, muheshimiwa alijua itakuwa kuwa jambo la aibu sana mbele ya rafiki yake iwapo atagundua kilichotokea.
Hivyo akaamua kutumia umafia. Akamwekea Caro kilevi katika kinywaji, Caro akabwia bila kujua. Usingizi ukamkumba.
Mheshimiwa Lucas akamwingilia Caro kimwili pasi na hiari ya yule binti!!
Palipopambazuka Caro alijikuta chumbani peke yake kama alivyolala usiku uliopita.
Muheshimiwa alifika pale baadaye sana na kujifanya asiyejua lolote, lile hata na alikuwa wa kwanza kumweleza Caro kuwa huenda hali ya hewa imemfanya awe mnyonge kama alivyokuwa siku hiyo.
Siku hiyo alipelekwa chuo cha mambo ya ushonaji, fani ambayo alikuwa anipenda. Muheshimiwa akalipia gharama zote na kisha akamuaga Caro kuwa anarejea Tanzania.
Kabla hajaondoka alimsihi sana akizungumza na baba yake asimueleze hali ya kualala chumba kimoja, akatumia lugha ya kiutu uzima.
“Caro nisingeweza kulipia laki nane kwa usiku mmoja kwa vyumba viwili, najua haipendezi kulala chumba kimoja lakini naamini unaelewa!! Wewe ni binti mkubwa unaweza kuchanganua.... nimejitahidi nilipoweza.” Akamsihi na ikawa hivyo.
Baada ya hapo ikawa ni tabia kila akisafiri kuja London anatumia ujanja uleule kumuingilia Caro kimwili.
Hatimaye baada ya mwaka mmoja Caro akainasa mimba!!
Hii ilibadili kila kitu!!
Muheshimiwa akamtamkia Caro waziwazi kuwa anahitaji awe naye kimapenzi......
Tofauti na alivyodhani kuwa caro atamkatalia alishangaa anakubaliwa upesi tu!

______
 
SEHEMU YA 6

WAKATI ULIOPO.(2014)

LUCAS alifika nchini uingereza akiwa mtu asiyekuwa na raha kabisa, alifikia hoteli ileile ambayo miaka kadhaa nyuma alikuwa akilala na Caro.
Usiku huu hawakutumia tena vitanda viwili, bali kitanda kimoja wakiwa kama mtu na mpenzi wake, kitanda kingine alilala kiumbe mwingine kabisa asiyejua hata nini maana ya afrika na Tanzania kwa ujumla.
Huyu alikuwa ni Bryan, mtoto wa Caro na Lucas.
Mtoto ambaye hata wazazi wa Caro walikuwa hawamjui, kwa sababu alimfanya kuwa siri kubwa sana, siri kati yake na muheshimiwa mbunge!!
Lakini pia kulikuwa na siri nyingine, siri iliyofananana bomu la nyuklia ambalo likilipuka halina simile linaua maefu kwa makumi elfu!!
Usiku huu walijadili mambo mengi sana na hatimaye muheshimiwa akamueleza Caro kuwa ameamua kuachana na siasa ili apate muda mrefu wa kumlea mtoto wao hukohuko London.
Uamuzi huu Caro aliupinga kwa kumueleza muheshimiwa Lucas kuwa kitendo cha yeye kuacha kazi na kisha kuwa na safari za mara kwa mara jijini London zinaweza kusababisha mkewe akashtuka na hata wazazi wake wakashtuka kuwa kuna jambo linaendelea.
“Pia Lucas tambua nilikueleza na tukakubaliana kuwa Chopa akitoka gerezani utakuwa mwisho wa mahusiano yetu, sasa huoni kama utaniharibia?” Caro alihoji.
Lucas akatulia akimtazama kwa muda kisha akamueleza jambo ambalo awali hakuwahi kumueleza.
“Caro ujue ni kwamba wewe ni msichana wangu wa kwanza kabisa kushiriki naye mapernzi nje ya ndoa yangu, na nilijua kuwa ni bahati mbaya tu. Lakini kupitia usaliti huu nimegundua jambo moja kubwa sana ambalo limeiathiri akili yangu kwa kiwango kikubwa mno.
Hivi haushangai Christina nimemuoa wakati wewe ukiwa sijui form two vile, ulikuwa mdogo sana eti hadi leo hajawahi kushika mimba zaidi ya kuniambia aliwahi kubeba mimba yangu kisha ikaharibika..... umri unaenda eti sina hata mtoto wa kujisifia mtaani akiona baba yake natema pointi bungeni, au mtoto wa kutaniwa kuwa babako ameongea pumba leo bungeni...... sasa sio hisia tena mke wangu ana matatizo ya kizazi na kama hiyo ndivyo, nimempata mtoto niliyekuwa namtamani siku zote kwanini nisitumie muda mwingi kuwa naye......” aliweka kituo.
“Lucas, usinambie eti unataka kumuacha mkeo...”
“Nilimuacha tangu niliposhuhudia tumbo lako likizidi kukua na ulipokubali kwa hiari yako kuwa mpenzi wangu...” Mheshimiwa alijibu.
Caro akachoka na kujilaza kwenye kitanda.
Mazungumzo yalichukua muda mrefu na kamwe msimamo haukubadilika Lucas alikuwa ameamua iwe atakavyo.
Walilala huku Caro akimweleza Lucas kuwa anataraji kusafiri kwenda Tanzania kuwasalimia wazazi wake kwani ilikuwa imepita miezi miwili hajaenda.
Lucas akamkubalia kwa sababu haikuwa mara ya kwanza kufanya hivyo!!
Alikubali bila wasiwasi wowote kwa sababu alijua kuwa bado mwaka mmoja Chopa atoke gerezani hivyo hakuna namna yoyote ya wawili hawa kukutana.
Ni usemi usiobadilika kila siku kuwa, laiti kama tungelijua lijalo na tungezificha nyuso zetu ili lisituumbue usoni!!
_____

ASUBUHI majira ya saa nne, tayari Chopa alikuwa amekabidhi chumba katika nyumba ya kulala wageni alipokuwa ameuweka ubavu wake kwa usiku ule alioingia jijini Dar es salaam.
Sasa alikuwa hana tofauti na vijana wengi wa mjini, alikuwa amevalia suruali yake ngumu aina ya ‘jeans’ iliyoukamata vyema mwili wake na juu alikuwa amejivisha fulani nyekundu isiyokuwa na maandishi ya aina yoyote ile, chini alivaa makubadhi!! Hii ni baada ya bei ya kiatu kumshinda!!
Alipanda daladala akiwa mkimya kabisa, alienda hadi maeneo ya Makumbusho, akachepuka mitaa kadha wa kadha hadi akaifikia ile nyumba ambayo kabla hajaenda jela palikuwa nyumbani kwao Caro mchumba wake.
Alikuwa akiombea sana amkute Caro. Nia ikiwa moja tu amuulize ni kwanini amemtenga kwa miaka miwili mfululizo pasi bna kukanyaga gerezani alipokuwa amefungwa!
Alipofika pale alikutana na sura ngeni machoni pake, akalazimika kuulizia na hapo akaelezwa kuwa anaowaulizia walihama mwaka mmoja na nusu uliopita na walihamia jijini Mwanza lakini hakuna hata mtu mmoja aliyefahamu eneo rasmini walipohamia.
Chopa akashusha pumzi zake kwa nguvu sana huku akiwa amejishika kiuno. Waliomjibu wakaendelea na shughuli zao.
Naye alipokosa lolote la kuuliza akageuka kurejea alipotoka, alipita mitaa miwili zaidi akaiona nyumba ambayo ilikuwa haina mabadiliko sana, nyumba ile zamani aliwahi kuishi rafiki yake Caro. Na mara nyingi alikuwa akikutana na Caro eneo lile kwa ujanja ujanja kuwa ameenda kumsalimia rafiki yake.
Chopa akajaribu kuvuta kumbukumbu ya jina la yule rafiki yake Caro lakini jela ilikuwa imemvuruga vibaya mno hakuna alichokuwa anakumbuka.
Alijiuliza iwapo aende ama asiende, moyo mmoja ukamsukuma mwingine ukamvuta.
Akachukua maamuzi ya kwenda, akalifikia geti na kugonga mara tatu, hatimaye mlango ukafunguliwa na mwanamke mtu mzima kiasi akiwa amebeba mtoto mgongoni.
Chopa akampa salamu zake na kisha akajaribu kuulizia kwa kadri alivyodhani anaweza kueleweka.
“Sasa kaka unamuulizia mtu ambaye hata jina lake humjui unamaanisha niwaambie nyumba nzima watoke nje ili uwakague au? Maana sikuelewi mara ananifanana mimi mara sijui nini....” yule mama akamuuliza huku akionekana wazi kukwazika na uwepo wa kijana yule.
Chopa hakuridhika akaendelea kusihi, yule mama akamwambia aendelee kukaa pale nje na kuwakagua wanaoingia na kutoka mle ndani huenda akamuona anayemfananisha.
Alimpa jibu lile kisha akaondoka.
“Mama samahani nimemkumbuka anaitwa Victoria, ni Victoria.” Chopa akamsihi yule mama.
Mama yule akageuka upesi.
“Umesema...”
“Anaitwa Victoria yeah ni Victoria sidhani kama nimekosea.. anafanana na wewe sana tu..” Chopa aliendelea kuzungumza akiwa amechangamka.
Yule mama akapiga hatua mbili zaidi kumkaribia Chopa.
“Unamtakia nini huyo Victoria...”
“Aaam! Si kwa ubaya mama yangu....”
“Sijakuuliza iwapo ni kwa wema au ubaya na hata ingekuwa kwa ubaya bado usingesema ungedanganya tu!!” alijibu kwa kujiamini.
“Aaah! Ni siku..ni miaka mingi sijaonana naye walah! Nahitaji kumsalimia tu...ni miaka mingi” Chopa akamjibu.
“Haya nimwambie nani anamuita...”
“Sijui atanmikumbuka... lakini mwambie Manfredy asipoelewa mwambie Chopa wa caro!!” alijibu huku uso wa tumaini ukijengeka katika muonekano wake.
Asalaale!! Yule mwanamke akakodoa macho yake, akapiga hatua zaidi kumsogelea Chopa. Hali hii ikamshtua Chopa... yule mama alikuwa anataka kusema neno lakini hakuweza kusema.
Alipomfikia Chopa alimkumbatia kwa nguvu sana kisha akamuachia.
Chopa alimtazama yule mwanamke, alimshuhudia akiwa katika mvua ya machozi....
“Chopa shemeji yangu pole Chopa...ona ulivyokonda Chopa... ona ulivyobabuka ngozi Chopa aaah! Walikuonea Chopa shemeji yangu.......”
Sasa Chopa aliweza kumtazama vizuri zaidi yule mwanamke aliyekuwaakimfananisha na Victoria....
Hakuwa amefananisha bali aliyekuwa mbele yake alikuwa ni Victoria mwenyewe.
Wakakumbatiana kwa mara nyingine, huku Chopa akimsihi Victoria asiendelee kulia sana kwa sababu sasa yupo huru na kinachotakiwa ni kuyatazama maisha katika jicho jingine na si kwa kutazama yaliyopita.
Victoria alimkaribisha ndani Chopa walizungumza kwa muda mrefu sana juu ya maisha yalivyoenda kasi katika ulimwengu wa uhuru aliouacha.
Chopa alilalamika sana kuwa Caro alimtupa moja kwa moja na kamwe hakwenda kumsalimia gerezani.
“Chopa shemeji yangu yaani Caro usimlaumu kabisa, amepambana yule akatafuta wakili akatafuta sijui vitu gani, mwisho anakuja kuambiwa mara umehamishwa gereza mara hauruhusiwi kuonana na mtu.... wamemtesa sana kimawazo hadi akaugua hakuwa akijitambua tena.... mara ya mwisho nadhani ni mwaka juzi mwanzoni hivi niliwasiliana naye akasema kuwa yupo Mwanza lakini muda wowote ule anaweza kwenda nje ya nchi.... akaniambia atakuja dar tutazungumza kirefu... lakini ikawa bahati mbaya alipokuja dar mimi nilikuwa nipo chumba cha kujifungulia. Hivyo alipiga sana simu na kutuma sanja jumbe lakini mimi sikuwa na fahamu maana nilijifungua kwa upasuaji. Nilikuta tu ujumbe wake akinisihi vile vitu vyako nikutunzie ipo siku utatoka yeye anaondoka....” alimaliza kusimulia kwa uchungu Victoria.
“Vitu gani tena.... na pole sana kwa uchungu wa uzazi uliopitia” Chopa alizungumza huku dhahiri akionekana kuwa na kiherehere cha kujua ni nini kiliendelea zaidi.
“Yaani huwezi amini mama alikuwa ananishangaa kweli nilivyokuwa mkali mtu akitaka kugusa huo mzigo.” Alizungumza huku akisimama kuelekea ndani, Chopa akabaki kusubiri.
Baada ya kama dakika mbili Victoria alirejea.
“Vipi unalikumbuka hili?” alimuonnyesha begi dogo. Chopa akafikiri na kusema kuwa halikumbuki.
Victoria akatikisa kichwa kusikitika.
“Ujue shem jela kuna mambo mengi sana yanaudhi, yanatibua akili na kukufanya ujione wewe si mwanadamu. Kushuhudia wafungwa wanakufa, kushuhudia wanaume wakigeuzwa wanawake, na mambo mengine mengi yasiyosimulika. Nisamehe bure lakini ukweli ni kwamba asilimia 70 ya mambo niliyoyaacha huku duniani hata siyakumbuki kabisa.....” Chopa alizungumza kwa sauti tulivu sana huku akionekana kuzidiwa na hisia za alichokuwa anasimulia.
Victoria akampatia lile begi na kumwambia kuwa humo kwenye begi kuna baadhi ya vitu ambavyo Caro alimsihi sana avitunze na kumpatia akitoka gerezani.
Chopa akalifungua begi.
“Mh! Hivi hii ndio ile simu yangu au?” aliuliza Chopa huku akicheka.
“Ona na hii ni ile saa, aah! Masikini hii saa alininunulia Caro wangu hii naikumbuka halafu wewe ndo uliniletea siku ile....” Chopa aliitazama ile saa kwa muda chozi likamdondoka.
Victoria naye ikawa hivyohivyo!!
“Hii simu ni nzima kweli?” alizungumza kama anayejiuliza.
“Juzi tu nimetoka kuichaji, Caro aliniambia niwe naichaji isije ikfa...”
Chopa akaiwasha, kweli ikawaka na ikaandika maneno ambayo yalimkumbuisha mbali sana.
“LIWAKE JUA, INYESHE MVUA SITAKUBADILIKIA C WA C”
Maneno yale aliyaandika Caro katika simu yake na simu ya Chopa pia. Wawili hawa walizoea kuitana C wa C yaani akiita Caro anamaanisha Chopa wa caro na akiita Chopa anamaanisha Caro wa Chopa.
Baada ya maneno yale simu ikaomba michirizi ya siri ya kuifungua.
Chopa akajaribu kwa mara ya kwanza ikagoma, akajaribu ya pili hakufanikiwa kitu.
“Shem! Ombea sana jela ibakie kuwa hadithi tu katika maisha yako na familia yako.... yaani huwezi amini nimesahau password!!” alizungumza kwa masikitiko huku akijilaza katika kochi katika namna ya kuegemeza kisogo chake hivyo akawa anatazama darini.
“Halafu shem nimeiona hii simu nd’o nimekumbuka vizuri sasas kuwa ni mojawapo kati ya kitu ninachokihitaji sana kwa sasa...”
“Basi hapo huna ujanja itabidi uiflashi” Victoria akatoa ushauri.
“Hapana Shem hii nikiiflashi kila kitu kitapotea kutoka humu kuna namba ya mtu na meseji zake, naamini huyu mtu anajua kwanini mimi nilipelekwa jela.... huwezi amini hadi sasa sijui kwanini nilifungwa gerezani...”
“Shem hayo yamepita tena umesema wewe mwenyewe basi hapo la msingi ni kutazama mbele....”
“Hapana Viki, naweza kusema yameisha je nikianza kutazma mbele halafu huyu mtu anichukue tena na kunipeleka gerezani patakuwa na maana gani, natakiwa kuwa mtu huru katika maana halisi ya kuwa huru...... siwezi kuishi maisha haya ya mashaka shem acha nimjue tu, nikishamjua wala sitazua mengine.” Alisimamia msimamo wake Chopa.
“Mh! Sasa hapo ndo mtihani, hakuna fundi wa kukutolea hizo loki bila kupoteza hizo namba na meseji.”
Aliposema vile mara Chopa akasimama wima, akarusha ngumi hewani kama mtu anayeshangilia akarukaruka juu kana kwamba amefunga goli.
“POCHAAAAAAA!!!” Akapiga kelele za wastani. Akiwa mwingi wa furaha.
“Una nini wewe Pocha nd’o nani?”
“Mtaalamu wa kutoa loki ya simu yoyote ile bila kupoteza namba wala kupoteza meseji yoyote ile.....” Chopa alizungumza na kisha kumwagia sifa kemkem Pocha.
Na hapo akaaga kuwa anaeneda kuona uwezekano wa kuonana naye. Akachukua namba za simu za Caro na kumsihi kuwa atawasiliana naye kwa lolote lile.

Chopa akaondoka na kuelekea gereza la Ukonga.
Huko akafanya mazungumzo pale ofisini na kujieleza shida yake, akadai anamuulizia ndugu yake ambaye hajui amefungwa gereza gani. Lakini ameelekezwa kuwa ni hapo Ukonga ndipo amefungwa.
Akaulizwa jina lake akataja jina moja tu la Pocha.
Ilikuwa ngumu sana kupata msaada kwa kutaja jina moja tu. Lakini bado walipekua jina lile kwa utulivu lakini hakuna jina lililofanania lile katika orodha ya wafungwa wote pale Ukonga!!
Alipewa daftari akajihakikishia hadi katika orodha ya wale wanaotumikia vifungo vya maisha hapakuwa na jina Pocha!!

Chopa akaaga na kuondoka akiwa mnyonge kabisa, ile furaha yake yote ikayeyuka!!!
Alitembea kwa mwendo mrefu kiasi, akajihisi kichwa kinamuuma sana. Akauona mti wenye kivuli akakusudia kujipumzisha kwa muda pale, akalifungua tena begi lake na kupekua hapa na pale vitu vya ziada ambavyo Caro alimuhifadhia.
Alijikuta akitabasamu alipokutana na kadi zake za benki. Alimfikiria sana Caro na kukiri kuwa yule alikuwa ni binti wa kuigwa, alikuwa ni yule asiyesahau fadhila na anayeona mbali.
“Sijui zimefungiwa?” alijiuliza.....
Baada ya kupumzika kwa muda akataka kupanda daladala, lakini akajikuta akicheka mwenyewe kwa sababu yeye alikuwa ni mzururaji hakuwa na sehemu rasmi ya kwenda sasa kulikoni kupanda daladala, akanuia kulala hukohuko Ukonga siku hiyo.
Kwa sababu muda ulikuwa bado unaruhusui akaamua azurure kidogo.
_____
 
SEHEMU YA 7

MAHALI FULANI JIJINI NAIROBI.

Simu ya dada mmoja iling’ara kumaanisha kuwa ilikuwa inaita aliitazama namba ile na kuitambua kuwa ilikuwa ni mpya katika simu yake.
Aliipuuzia kwa mara ya kwanza, ikapigwa tena kwa mara ya pili na ya tatu bado hakuipokea alikuwa ametingwa na shughuli nyingi sana za kimasomo akiwa chuoni.
Simu ile safari hii ilipokea ujumbe, akabofya ukafunguka.
“POKEA SIMU NI MUHIMU. TZ 11”
Ujumbe ule ulimshtua sana na aliufahamu umuhimu wa huyo bwana mwenye kitambulisho TZ 11 (TZ eleven) katika simu yake.
Upesi akaacha kila alichokuwa anakifanya, akatoka njea na kuingia msalani. Alipoufunga mlango tu, simu ile ikaita akaipokea upesi.
“Yupo huru ameingia benki maeneo ya Ukonga, Dar Es salaam jioni hii ya leo. Nakusikiliza wewe sasa!” sauti ile ya kike ilimuuliza kwa utulivu sana. Binti yule aliduwaa sana na badala ya kujibu akatupa swali.
“Imekuwaje mapema hivi si ilitakiwa kuwa next year ama?”
“Kuna haja gani ya kujadili juu ya goli ulilofungwa.... tafadhali jadili unasawazisha vipi ama hutaki kusawazisha jiandae kutoa sababu za kujitetea kwa nini umefungwa...” sauti ya mwanamke kutoka upande wa pili ilijibu kwa ukali kidogo.
“Hakikisha unamfuatilia kwa ukaribu....utanipa taarifa zake kwa juma moja.”
“Akaunti yangu ni ileile sijaibadilisha, tanguliza nusu ya malipo ya kazi hii.” Akamaliza upande wa pili na kukata simu, akimuacha yule binti aliyekuwa pale msalani kwa lengo la kuongea na simu pekee akijikuta ameshikwa kweli na tumbo la kuhara!!!


MTAFUTANO!

Giza lilikuwa limetanda tayari, Possian Clement alikuwa chumbani kwake akiwa mbele ya kioo akijitazama. Alilitazama tumbo lake jinsi lilivyokuwa limenona kwa sababu ya kitambi.
Alitikisa kichwa huku akitokwa na tabasamu la karaha, alisikitika kwa sababu kile kitambi kilikuwa kimekuja bila idhini yake na alikuwa amechelewa kupambana nacho na hakuweza tena kupambana nacho kutokana na mazingira aliyokuwa akiishi.
Alitambua wazi kuwa hata afanye mazoezi kutwa mara tatu bado lile tumbo linalomning’inia haliwezi kuondoka kwa sababu alikuwa akiishi katika mazingira ya kuridhika sana mjini Dodoma.
Mbaya zaidi alikuwa akiishi kama mwanamke anayemtegemea mwanaume kwa kila kitu maishani mwake, watu hawa hujulikana zaidi kwa jina la ‘golikipa’.
Possian hakuyazoea haya maisha kabisa lakini hakuwa na budi kutii bila shurti hadi pale muda utakapofika wa kusimama yeye kama yeye tena.
Si kwamba alikuwa yu mtoto mdogo la! Alikuwa ni mtu mzima apataye miaka thelathini na mbili.
Lakini wakati wake wa kusimama yeye kama yeye ulikuwa haujafika bado.
Alipomaliza kujitazama kwenye kioo, alitoa shati lake kisha akajinyoosha kitandani huku akikwepesha macho yake ili asilione tumbo lake.
Ni kweli kutolitazama haimaanishi lingeondoka katika mwili wake lakini ingesaidia kuliondoa katika fikra zake.
Akiwa amejilaza pale kitandani usingizi ukampitia bila kutarajia, lakini usingizi ule haukudumu kwa muda mrefu kabla hajakurupuka na kujikuta amesimama wima jasho likimtoka huku akizungumza peke yake. Maneno yake yakiambatana na kile kilichokuwa katika fikra zake.
Kilikuwa kitu cha kutisha kwa kiasi kikubwa japokuwa hakuwa na ushahidi nacho lakini ni mambo mengi ameyafanya pasi na kuwa na ushahidi na yalikuwa yanaleta uhakika baadaye.
Hakuweza kulala, akauitazama saa yake ilikuwa ni saa mbili na nusu usiku, akavaa shati lake na kutoka pale chumbani.
Akaenda sebuleni ambapo alimkuta Sofia, binti mkubwa katika familia ile ambaye mara kwa mara huwa haonekani nyumbani, lakini hizo mara chache ambazo huonekana basi huwa karibu naye walau kimazungumzo ya hapa na pale.
Possian alifika na kuketi akitazamana ana kwa ana na binti yule mrembo wa haja aliyejengeka mwili wake vizuri katika mvuto wa kike.
Sofia alikuwa amejikita katika kutazama filamu iliyokuwa inaendelea.
“Possian vipi mbona jasho!”
“Nina matatizo makubwa Sofia na ni wewe unayeweza kunisaidia, ni wewe pekee Sofia na si wakati mwingine bali ni wakati huu...”
Sofia akaachana na filamu akaweka umakini kumsikiliza Possian.
Kuona vile Possian akaendelea kuzungumza.
“Sofia kuna rafiki yangu kipenzi yupo katika matatizo makubwa sana!!”
“Rafiki? Wewe unaye rafiki gani tena wakati hauwasiliani na mtu yeyote nje ya nyumba hii!!”
“Dada Sofia nakuomba sana unielewe kadri uwezavyo kwa sababu manenio nitakayokueleza hayana uzito sana kiushahidi na yanaweza kuwa kama vituko tu. Nakusihi sana usiyachukulie kama kituko.” Alisihi Possian na kisha akaanza kujieleza kinagauubaga akijitahidi kutilia mkazo anayoyasema.
Alitumia dakika saba kujieleza kwanza juu ya yeye ni nani.
“Mh! Umesema jina lako maarufu ni nani na kwanini sasa unaitwa Possian hapa....”
“Sio kwamba Possian sio jina langu, nilizaliwa nikiitwa Possian Clement Haule.... lakini nikiwa darasa la saba mwalimu wa kiingereza kubna simulizi alitusimulia na ndani ya simulizi hiyo kuna jina alilitaja la kiingereza nasi tukatokea kulipenda mno. Niliporudi nyumbani jina lile likagoma kunitoka kabisa, nikajikuta nalitazama jina langu bila kujua kwa nini nalitazama sana na hapo nikaliona lile jina alilotutajia mwalimu. Kesho yake nikaenda ubaoni wakati mwalimu hajaingia nikachukua chaki nikaandika Possian Clement haule... kisha nikanyofoa herufi katika kila jina.. na hapo nikaandika ubaoni POCHA!!
Tangu wakati huo jina langu la kuzaliwa likasahaulika hadi ukubwani kila anayenifahamu ananifahamu kwa jina la Pocha!!” alijibu kwa utulivu wa hali ya juu. Sophia akajikuta akitokwa na tabasamu lililovutia.
“Nimelipenda sana jina lako jipya Mr. Pocha!! Haya umesema kuwa una uwezo wa kutoa loki kila aina ya simu..... nihakikishie na hilo kisha nitakusikiliza sasa juu ya hilo lililokuleta... hii hapa simu yangu, nakupa dakika kumi na tano unitolee loki.... ukimaliza tutaongea....”
“Fanya dakika tatu Sofia ili tuzungumze juu ya hii shida yangu! Tafadhali” Pocha aliomba.
Jibu la Pocha lilimshtua Sofia, yaani mtu kapewa mtihani badala aombe kupewa muda mrefu anaomba muda upunguzwe..... mtu wa aina gani hii.
“Haya sawa” akamkubalia huku akipandisha mabega juu kana kwamba anaupuuzia uwezo wa Pocha.
Pocha akaichukua simu ya Sofia, akaitazama kwa sekunde kadhaa kisdha akauweka sawa mkono wake......
Hazikuwa dakika tano ile awamu ya kwanza tu simu ya Sofia ikaachia!
Yule dada aliruka mbali kana kwamba Pocha alikuwa amemtekenya pasi na hiari yake.
“Possian we Possian..nani amekupa password zangu..eeh! nani?” alihoji Sofia lakini kwa Pocha hata hakuwa ameshtushwa na jambo hili.
“Sofia naomba basi tuzungumzia hili jambo langu kama una uwezo wa kunisaidia tafadhali nifae....” alimsihi. Sophia akiwa katika mshangao bado aliketi asiamini kile kilichotokea, aliichukua simu yake kutoka mikononi mwa Pocha.
“Bado Pocha bado.... ujue nina simu mbili.....haya hii hapa nyingine... ifungue. Hii hautaweza hata kwa dawa najua..... nikupe muda gani?” alimuuliza, badala ya kujibu Pocha ambaye damu ilikuwa ikimchemka vyema alikwapua ile simu, akaishika akatulia kwa sekunde kadhaa akapiga mchapuo wa kwanza akakosea, Sofia akaanza kumcheka.
Akaenda ya pili hola... Sofia akaonekana kufedheheshwa akiwaza ni wapi aliitoa namba yake ya siri ya simu yake kubwa.
Wakati anawaza haya akiwa ameacha kumtazama Pocha kwa kuamini kuwa hataweza kuipatia namba ya simu ile nyingine alishangaa Pocha akimuuliza.
“Huyu mtoto hapa juu ni wako.. maana mnafanana kweli”
Sophia alipogeuka alikuwa simu imefunguliwa tayari.
Mdomo ukamfunguka!!
Sasa alikiri kuwa mbele yake palikuwa kiumbe moja wa ajabu sana... huenda ni wa ajabu kupita yeye mwenyewe anavyojidhania!!
Sasa alimsikiliza shida yake vizuri.
“Umesema Chopa... Chopa ni nani?” Sofia akamuuliza Pocha.
Pocha akajieleza kuiwa amekumbwa na hisia kuwa Pocha yupo huru lakini yupo matatani tena, tena matatizo makubwa sana ambayo yanamnyemelea ili kumuharibia tena maisha yake.
Pocha akamsimulia Sofia juu ya utata wa kesiya Chopa hadi kuishia kutupwa gerezani bila kuijua kesi yake huku akinyimwa hata uhuru wa kutembelewa na ndugu na marafiki.
Maelezo ya Pocha yakamuingia vyema Sofia.
Akamwambia Pocha kuwa alfajiri wataondoka kuelekea huko Ukonga anapodai kuwa hisia zimemtuma kuwa Chopa anapatikana.
Sofia alikuwa ameamua kuucheza mchezo huu akiwa na matumaini ya kujifunza kitu zaidi katika masomo yake.
Masomo ambayo yalikuwa yanamfanya asionekane nyumbani mara kwa mara.
Wakati Sophia na Pocha wakiagana na kwenda vyumbani kulala.
Kiumbe mwingine alikuwa kitandani akiukosa usingizi kwa sababu ya mambo yaisyomuhusu anayojilazimisha yamuhusu!!
_____

YALIKUWA ni majira ya saa nne usiku, kwake hakuona kama usiku ulikuwa umeenda sana. Alikuwa amejikita katika simu yake.. mara kuwapigia marafiki zake mara kuwapigia ndugu zake.
Alikuwa akizungumza nao kwa muda mrefu huku akiwakatia walipojaribu kumpigia simu.
Na ilifikia hatua hata asipoulizwa shida anajifanya kuulizia shida ilimradi tu aweze kujiweka katika nafasi ya kutoa msaada.
Huyu hakuwa mwingine bali ni Priska yule katibu muhtasi wa mheshimiwa Lucas. Alikuwa akiwashwa na zile pesa alizopewa kama bakhshishi na bosi wake baada ya kumfokea pasi na sababu ya msingi.
Alimaliza kuwapigia watu simu aliokuwa anawakumbuka kichwani, na hapo alikuwa amejilaza tu7 akiwasubiri rafiki zake waje kumpitia waende mahali kuzitumia pesa zile, wakati anaendelea kutafuta majina mengine ya kuwapigia simu akakutana na jkina alilolihifadhi na kisha kulisahau.
Hili jina alilihifadhi “KWANINI”
Akatabasamu baada ya kulitazama jina lile akabofya kitufe cha kijani. Simu ikaita hadi ikakatika, akapiga tena safari hii ikapokelewa na mwanamke.
Alipogundua ni mwanamke akakata!!
Akang’ata kidole chake na kufikiria kuwa kama kweli anataka kuujua umbe basi ni heri atumie nambari ya tofauti ili aweze kuupata ama kuusambaza bila kujulikana.
Akajipekua na kutoa kadi yake nyingine ya simu!
Akaiweka katika simu ile na kumpigia yule mwanamama.
Simu ikapokelewa, mama yule aliongea akionekana dhahiri kuzidiwa na usingizi.
“Mama unalala sana nd’o maana wenzio kila kukicha wanaruka London, wanakula raha za ukweli huko akija kwako ni kulala tu... unapiga simu hazipokelewi shosti upo hapo! Na mwaka huu utapiga simu sana hadi madole yaote sugu hayo mwenzako humwambii lolote kuhusu London.
Nimeufikisha kama ulivyo ubuyu wangu utajua mwenyewe uumeze ama uuteme!! Na ujue hata ukiutema huu ubuyu wa Zenji una kapilipili kwa mbali bado utakuwasha tu bibie......endelea kulala!! Tena bibiwee usije ukaniletea uchuro eti nimekosea namba.. hahahahah! Ukidhani ninmekosea namba basi na mimi nitakuuliza mheshimiwa Lucas unamjua humjui.. kama unamjua bibiwee labda ukaroge maana siku hizi ni mara kumi kwa mwezi anaenda kula vitamu London.... hahahahah unaloooo” akamaliza kuzungumza akakata simu na kuizima.
Kisha akajigalagaza kitandani akicheka kwa sauti ya juu sana. Ilikuwa usiku lakini hakujali alikuwa akiishi na wadogo zake wawili wangeanzaje kumwambia eti dada unapiga kelele tumelala.
Nafsi ya Prisca ikapata ahueni baada ya kuzungumza na yule mama huku akimrushia vijembe bila kumpa nafasi ya kujibu chochote.
Amakweli umbea ni kama tabia, utajisahaulisha halafu baadaye inarejea tena!
Prisca alikuwa merejea tabia yake.
Ni heri angeufanya usiku huu uwe wa mwisho kuusambaza umbe huo asiojua madhara yake bila kujua anaowapigia simu ni akina nani!!!
Wakati yeye anaikata simu.....
Mke wa Edwin rafiki kipenzi wa Mheshimiwa Lucas alikuwa anamuamsha mume wake kwa fujo.
Alipoamka akamuelezea kila kitu kama kilivyotokea.
“Wewe Lucas alikuaga kuwa anaenda London?” Mama Caro alimuuliza mumewe.
“Hapana na ni kawaida yake kuniaga akiwa anenda safari za mbali, taarifa niliyonayo ni kwamba wiki ijayo Caro anakuja nyumbani sina taarifa kuhusu safari yake.” Edwin alijibu akiwa amekaa kitako.
“Kwani mama Caro wewe unahisi nini hapo.... maana we nawe kwa presha za ajabu ajabu haujambo...”
“Sio hivyo mume wangu, maneno aliyozungumza huyo binti ni ya kawaida hata hayatishi lakini moyowangu umepiga kwa nguvu sana punde tu baada ya kumtaja muheshimiwa Lucas. Nikikumbuka juzi hakupokea simu yetu na wala hakujihangaisha kutupigia...”
“Hebu ngoja..naomba hiyo simu...” Edwin alichukua simu kwa mkewe, akapiga namba za Lucas zikawa hazipatikani.
Akapiga namba za mkewe simu ikaita kwa muda mrefu kabla ya kupokelewa.
“Samahani shem, nimekuharibia usingizi wako.” Alianza kuzungumza kwa utulivu na anayelazimisha furaha.
“Najaribu kumpigia Luca lakini simu yake haipatikani, kama upon aye hapo naomba niseme naye jambo ni la muhimu sana...” akazungumza na kisha kuusikiliza upande wa pili ukatoa majibu.
“Aah sawa basis hem ulale salama na samahani kwa usumbufu” akaaga na kukata simu.
“Nini amekujibu eeh! Luca yupo London? Eeh!” mama Caro akauliza huku akijawa na hamu ya kujua yalojiri.
“Yah! Ameenda London ghafla....” alijibu kinyonge Edwin!!
Mama caro akabaki kimya, Edwin naye hakuwa na la kusema.

_______
 
SEHEMU YA 8

KITENDO cha kupigiwa simu usiku ule na bwana Edwin kiliukatisha usingizi wa Christina mke wa Lucas, hakuna baya lolote alilowaza lakini badala yake alikarahika alipogundua mtu msomi kabisa kama bwana Edini anaweza kushindwa kutambua kuwa ule ni usiku na mtu amelala tena sio mtu tu bali ni mke wa mtu, licha ya hayo bado anapiga simu!!
Usingizi ulipogoma kabisa Christina aliwasha kompyuta yake akaingia katika mtandao maarufu wa ‘skype’ ili aweze kuzungumza na mumewe huku akimuona kupitia kamera ya kompyuta. Mara nyingi alipokuwa nje ya nchi walikuwa wakitumia njia hii.
Lakini hii ilikuwa mara ya kwanza kufanya hivi usiku!!
Aliingia mtandaoni na kupiga simu ile ya bure kabisa, bahati nzuri alikuta mawasiliano ya mumewe pia yapo hewani.
Simu ile ilipokelewa akamuona mumewe lakini hata kabla hawajaongea vizuri ikakatwa.
Christina akahisi kuwa ni tatizo la mtandao, akazima kompyuta yake na kujaribu kuutafuta usingizi tena.
Ile anajigeuza geuza kuusaka usingizi mara akahisi kama kuna kitu amekiona na hakipo sawa kabisa, alikaa kitako pale kitandani huku mapigo yake ya moyo yakienda mbio kabisa.
Akatulia kwa muda na hapo akahisi kuna kitu kisichokuwa sawa amekiona kwa mumewe kabla simu yake aliyopiga kwa kutumia ‘skype’ haijakatwa na kisha mumewe kupotea katika mtandao.
Christina alijaribu kupuuzia hisia zake lakini zilizidi kumsumbua kuwa kuna kitu cha ziada alikiona pale kitandani, mumewe hakuwa peke yake.
Donda la wivu likainyakua nafsi yake ya uvumilivu, vyeo kadhaa alivyokuwanavyo bungeni havikuwa na maana tena. Sasa akawa kama mtoto mdogo, akachukua simu yake ya mkononi na kubofya namba ambazo mumewe anazitumia kila anavyokuwa London.
Simu iliita bila kupokelewa, alipopiga mara ya pili simu ikakatwa tu, na mara ya tatu haikupatikana kabisa.
Christina hakuweza kulala kabisa, alilia kama mtoto mdogo, japokuwa hakuwa na uhakika kama ni kweli alichokiona ni sahihi kuwa mumewe hakuwa peke yake pale kitandani lakini suala la pili la simu kukatwa na kisha kuzimwa lilimsogeza hatua moja zaidi katika hofu ya kutapeliwa penzi lake.
Christina alijikuta akikesha bila kutarajia huku kichwa kikimuuma sana.
Yaache mapenzi yaiendeshe dunia, kama wewe hayajawahi kukuendesha basi wewe ni mfu hauishi katika dunia hii anayoishi Christina na mumewe Lucas!
Wakati Christina akiwa katika mkesha wa kuyalilia mapenzi kuna viumbe wengine wao walijikuta katika mojawapo ya mikesha mibaya kupita yote mkesha ambao hawatakuja kuupitia tena katika maisha yao!!

______

MAJIRA ya saa mbili nne usiku vijana wawili nadhifu walikuwa katika ukumbi mmoja wa starehe, walikuwa wakipata vinywaji baridi kwa chati huku wakibadilishana mawazo ya hapa na pale.
Macho yao yalikuwa yakitazama upande ambao walitakiwa kutazama wakati wote, hawakuwa pale ukumbini kwa sababu ya starehe za kawaida bali walikuwa wakitii amri kutoka kitengo cha juu yao.
Waliamua kunywa vinywaji baridi ikiwa ni geresha tu ilimradi uwepo wao pale usimtishe wala kumtia mashaka mtu yeyote yule.
Watu wote pale ndani hawakuwajali kabisa vijana walew wawili kwa kuwachukulia kuwa ni wateja kama wateja wengine waliofurika katika ukumbi huo ambao baadaye majira ya saa sita palitarajiwa kuwa na onyesho la msanii fulani wa muziki ambaye jina lake limefifia na anafanya maonyesho hovyo tena katika mazingira yoyote yale ilimradi tu kuganga njaa.
Kasoro mwadada mmoja tu ambaye yeye alikuwa anakunywa pombe kali, huyu nd’o aliwatazama kwa jicho la tofauti alihisi wale wapo pale kwa sababu zao nyingine tu na sio kupata burudani ambayo wengi waliifuata pale.
Aliamua kufikiria hivyo kuanzia awali alipofunga safari kuelekea hapo ukumbini bila kutarajia. Na sasa aliona ulikuwa muda muafaka wa kuwahoji hao vijana wawili ni kwanini wapo hapo ukumbini kinyume na mioyo yao ilivyokusudia.
Mwanadada yule aliyevalia sketi fupi maarufu kwa jina la kimini’ ikiwa na mpasuo uliolionyesha paja lake nono alipiga funda za pombe ile mfululizo hadi akaimaliza katika ile chupa.
Alifanya hivyo katika mtindo wa tarumbeta!!
Naam! Alipohakikisha kuwa anaweza kusimama wima vizuri bila kuziona nyotanyota alipiga hatua hadi maliwatoni.
Alitumia takribani dakika mbili huko, kabla hajarejea pale ukumbini akiwa peku mguu mmoja.
Alihangaika huku na kule kisha akakivua kile kiatu chenza na kukimbilia katika meza ya wale vijana.
Alikuwa mwenye hofu sana na alionyesha kupagawa.
“Kaka zangu nisaidieni...nisaidieni huyo mlevi kanichukulia simu yangu halafu anataka kunipiga..... nisaidieni kaka zangu uuuuuwi simu yangu mimi uuuuwi!” alilalamika huku akirusha mikono huku na kule.
“Tulia tulia dada!! Nani na yupo wapi?” mmoja kati ya wale vijana akamkaripia akimtuliza huku akiwa amesimama wima tayari.
Yule dada akacheza na akili yake, upesi akamshika mkonio na kumvuta huku akiwa bado anaugulia kwa uoga. Alitambua kuwa mikono yake ni laini sana, na alijua wapi pa kumshika mwanaume vizuri ili atambue kuwa ameshikwa na mwanamke laini.
Yule kijana mbiombio akafuata nyuma, akafika hadi kule msalani.
“Alikuwa hapa uuuwi simu yangu!” alilia yule dada huku akimpa nafasi kijana atangulie mbele kuangaza vizuri.
Ewala! Apewe nini kingine katika mipango yake zaidi ya kupewa kisogo namna hii katika namna aipendayo.
Yule dada akaipandisha ile sketi yake fupi kiasi kwamba nje ilibaki chupi tu iliyoonekana, sketi yote ikamezwa na kiuno, teke moja maridhawa likamtoka na kutua katika mgongo wa yule kijana kiasi kwamba likamsukuma na kumbamiza ukutani vibaya mno, mdomo ukachanika huku ukiacha damu kiasi katika ukuta, dada yule akiwa bado chupi nje akaifikia ile damu na kuifuta upesi kisha akamnyanyua kijana asiyekuwa na nguvu tena akamsukuma na kumwingiza katika choo cha wanawake!
Alijua kwa pigo lile yule bwana atabaki kugumia tu asiweze kusema walau neno moja.
Akakifunga kile choo vyema kwa kutumia kufuli jingine kabisa alilokuwa ameliandaa tayari.
Kisha akatoka na kutimua mbio kiuoga vilevile safari hii akiwa na damu katika blauzi yake, damu aliyoifuta pale ukutani baada ya kijana wa kwanza kupasuka mdomo vibaya mno.
Akatoka mbio hadi kwa kija naliyebakia pale, alifika na kumwonyesha ile damu.
“Kaka amempiga na chupa huyo mlevi Mungu weeee!! Anamuua... atamuua.... uuuuuwi!” alizungumza huku akirukaruka kama kuku aliyechichwa vibaya sasa amemtoroka mchinjaji kabla hajamaliza kumchinja!!
Alijua kwa tego lile mwanadamu wa kawaida hawezi kuponyoka, na vijana wale kwake walikuwa ni wanadamu wa kawaida tu.
Kijana wa pili hakutumia muda kufikiri, akajisahau kabisa kuwa alikuwa haitaji kujulikana yeye ni nani.
Hapohapo akatoa bastola yake kiunoni na kumwamuru yule dada amtangulize eneo la tukio.
Dada akatii huku akionyesha hofu kubwa machoni juu ya ile bunduki.
Lakini moyoni alikuwa katika kicheko akifurahia kuumaliza mchezo katika njia inayofurahisha.
Safari hii hakunyoosha niia kuelekea tena kule uani badala yake alienda katika chumbacha kuvutia sigara kilichokuwa jirani na kile choo.
Akaonyesha kwa kidole huku akionyesha uoga wake wa kike kuhusu kutangulia.
Yule bwana akatangulia akiwa makini na bunduki yake. Alipoufungua mlango, yule dada akatokwa na ngumi moja kali sana ikatua katika kisogo cha yule kijana, bunduki ikamtoka huku akitua mle ndani, nukta iliyofuata yule dada alikuwa ametanda pale ndani ameidaka ile bunduki alikuta wapo watu wawili wanavuta sigara. Akawaamuru wapige magoti kisha waangalie ukutani.
Wakatii huku sigara zikiwatoka midomoni.
“Nyie ni askari najua na sihitaji vitambulisho vyenu..... bnani amewatuma huku?” alihoji yule dada.
Askari yule akagoma kujibu!
Dada yule naye hakuuliza mara ya pili.
Akafanya kama anaondoka na kisha ghafla akaizungusha ile bastola upande wa kitako na kwa nguvu sana akambamiza nacho kisogoni yule askari aliyegoma kujibu akidhani atabembelezwa.
Huo ukawa mwisho wake.
Wale vijana ukutani aliwarukia teke la ajabu akiisambaza miguu yake yote miwili kisha kwa pamoja kila mmoja akaupokea mguu mmoja mgongoni hivyo akajibamiza ukutani na kupoteza fahamu!!
Akatoka akiiacha ile bunduki pale ndani.
Akaenda kule chooni, akaufungua mlango na kujihakikishia kuwa yule bwana hakuwa anakoroma tena bali alikuwa amenyamaza kimya tayari na damu ilikuwa imetapakaa sana pale ndani.
“Ndugu yako nimemuuliza ni nani amewaagiza kuja hapa kumfuatilia yule kijana hajanijibu nimemuacha ameenda zake kulala. Je na wewe hautanijibu!!” alimuuliza.
“Luteni Bosco!!” alijibu kwa shida sana.
“Asante wewe unazo akili nyingi sana, sasa ukienda mpe taarifa kuwa umekutana na TZ 11 na yeye anafuatilia dili hilohilo ambalo yeye luteni anafuatilia... kwa hiyo mwambie anisamehe bure!! Natetea ugali wangu!” alizungumza yule dada na kisha akatokwa na ngumi kali ikatua katika shingo ya askari yule huo ukawa mwisho wake.
Akakichukua kiatu chake, akauchukua mkoba wake mdogo na kisha akatoa blauzi nyingine na kubadilisha upesi.
Wakati anatoka akamuona mtu aliyekuwa akimfuatilia na yeye akiwa katika hatua za mwisho kutoka pale ukumbini.
Hakuwa mwingine bali alikuwa ni Manfredy Gregory ‘CHOPA’.
Tz 11 akatokwa na tabasamu hafifu kisha akaivaa miwani yake na kisha akenda mahali alipokuwa Chopa na kuanza kumbughudhi mara amalazimishe wakacheze mziki, mara amwambie kuwa anamtaka kimapenzi.
Aliyafanya yote haya ilimradi tu kumkera Chopa ili afanye maamuzi ambayo hajayapanga!
Kweli Chopa akakereka na kufikia hatua ya kuondoka hapo ukumbini ili aende katika ile nyumba ya kulala wageni aliyofikia!!!
Nini kingine tena utahitaji TZ 11 zaidi ya mambo kujipanga yenyewe namna hii??
Chopa alipotoka na yeye akatoka akipishana na watu waliokuwa wakisukumana kwenda kushangaa tukio lililotokea katika chumba cha kuvutia sigara.
_____

ILIKUWA yapata majira ya saa nne asubuhi wakati luteni mstaafu Bosco mkuu wa gereza la Ukonga alipopigiwa simu mbili zilizoachana kwa dakika chache sana.
Simu ya kwanza ilikuwa ni taarifa juu ya uwepo wa mtoto wake pale ofisini na alieleza kuwa ana shida kubwa sana ya kuonana na luteni.
Akiwa katika gari yake anapigiwa tena simu, safari hii ilikuwa ni simu ya upepo iliyofungwa katika gari lake.
Simu hii ikatoa taarifa juu ya vifo vya askari wawili katika ukumbi wa starehe.
Taarifa hii ilionekana kuwa ya kawaida sana kwake kabola hajatajiwa nambari za askari wale waliouwawa.
Moyo wake ulidunda mara mbili ya kawaida. Aliuliza mazingira ya vifo hivyo akaelezwa kuwa hawakupigwa risasi na bunduki zao wote zimekutwa salama kabisa bila kutumika walau risasi moja.
Taarifa hii ilimpagawisha sana, akamuamuru dereva aongeze mwendo kasi.
Baada ya dakika arobaini alikuwa kituoni tayari, alifikia moja kwa moja kwa mtu wa mapokezi ambaye ndiye alimpa taarifa kuwa kuna bwana mmoja alikuja kumuulizia Pocha pale gerezani. Na baada ya taarifa hiyo luteni akawaagiza vijana kumfuatilia mtu huyo wamtambue ni nani na ikiwezekana wajue ni kwa nini anamtafuta Pocha.
Luteni alimuuliza maswali lukuki yule mtu wa mapokezi ikiwa alimuuliza yule bwana jina lake, mtu wa mapokezi akakiri kuwa alimuuliza na alilinukuu pembeni kabisa.
Luteni akaliomba lile jina, akapewa jina Manfred Gregory!
Baada ya hapo akiwa anataka kuondoka mtu yule wa mapokezi akamkumbusha kuwa mwanaye alikuwa anamngoja!!
Akaenda moja kwa moja alipoelekezwa mwanaye yupo, ni katika mgahawa uliopo jirani na gereza maarufu kama hoteli ya Magereza.
Akaingia pale na kuangaza huku na kule, laiti kama isingekuwa ujasiri wa kijeshi basi angeweza kuanguka, hii ni baada ya kumuona Pocha akiwa katika mgahawa ule.
Akajipapasa kiunoni kutambua uwepo wa bunduki yake, lakini kabla hajaitoa akatambua kuwa yule binti aliyeketi na Pocha ni Sofia binti yake....
Alipiga hatua mpaka akaifikia meza ile na kuketi!
Sofia akamsalimia babake, Pocha naye akafanya hivyohivyo, Sofia alijua wazi kuwa baba yake yupo katika sintofahamu. Akamueleza kwa kifupi kilichowaleta Dar es salaam ghafla.
Akaelezea zile hisia za Pocha ambazo hata yeye Luteni alikuwa akizifahamu na ndo chanzo kikubwa cha kufanya maarifa hadi Pocha kuishi Dodoma huku waliomfunga wakiamini yupo gerezani.
“Mzee, usihoji sana maneno mengi najua unaniamini kuwa siwezikufanya jambo la kishenzi wala la kipuuzi... nahitaji kujua kitu kimoja tu je? Kuna uwezekano wa kujua kama kuna mtu aitwaye Chopa alifika hapa kumuulizia Pocha?” alihoji Sofia kwa utulivu.
Baba mtu alimjua vyema mwanaye na hapa hakuwa akiongea na mwanaye wa kawaida bali alikuwa akizungumza na mmoja kati ya wapelelezi chipukizi wanaoipenda kazi yao.
Hivyo hii ilimuondolera ile hofu alijua Pocha hawezi kuwa na ujanja wowote wa kumlaghai Sofia.
Mzee Bosco aliondoka hadi mapokezi kule na kumuhoji yule mtu wa mapokezi kama kuna mtu mwingine aliyekuja kumuulizia Pocha zaidi ya huyo Manfredy, mtu wa mapokezi akakataa kuwa hakuna mtu yeyote na huyo Manfred ndiye mtu wa kwanza kufanya hivyo tangu Pocha atolewe gerezani katika njia za kinyemela.
“Au umewahi kupata mgeni yeyote anayeitwa Chopa labda....” aliuliza mzee Bosco.
Mtu wa mapokezi akafikiria kwa kina kisha akasema hajawahi pia kukutana na jina hilo.
Mzee Bosco akarejea mgahawani na kuwaeleza alichojibiwa.
“Manfred Gregory ndiye kiumbe pekee ambaye alikuja kumuulizia Pocha na nikawaagiza vijana wangu kumfuatilia... mjinga ameua vijana wangu kama kuku...Sofia mwanangu hajatumia silaha amewaua kwa mikono na miguu yake yule mshenzi.. halafu aaaargh! Sijui nimefanya ujinga gani wale askari aaargh walikuwa vijana wadogo... huyu Manfredy ni nani Pocha?” Luteni msaatafu Bosco akamgeukia Pocha.
“Sijawahi kusikia jina kama hilo mkuu!” alijibu kwa nidhamu ya hali ya juu Pocha.
“Huyo Chopa naye umesema umehisi sijui naye ni nani?”
“Rafiki yangu wa karibu sana.... alinisaidia sana nilipokuwa gerezani, aliniepusha na mengi lakini badaye akahamishwa gereza sijui aliachiwa huru ama vipi lakini aliondolewa!!” alijibu Pocha!!
“Pocha huu si muda wa kuwatafuta marafiki zako, ujue ni kiasi gani unaweza kuhatarisha kazi yangu.....” alitaka kuendelea kuzungumza. Sofia akamkanyaga mguu.
Kisha akamnyanyua Pocha na kumweleza mzee wake kuwa atampigia simu ikiwa kuna msaada wowote watahitaji.
“Sofia!!” mzee Bosco alimuita mtoto wake wakati anataka kuondoka. Sofia akarudi upesi na kutega sikio.
“Ukifanikiwa katika pitapita zako huko kumpata huyo Manfredy sijui nani nani...namtaka akiwa hai... hai kabisa...mshenzi ameua vijana wangu wawili Sofia yaani wawili tena kwa dhihaka kubwa kabisa eti hajatumia silaha.....” Mzee Bosco alilalamika.....
Sofia akampiga begani kisha akaondoka!!
Baba yake akamsindikiza kwa macho.


___
 
SEHEMU YA 9

Nairobi Kenya.
4:00 Asubuhi

Muda wote alikuwa akiitazama simu yake kusubiri kama kuna taarifa yoyote ile kutoka Tanzania, hakuna aliyejishughulisha naye kwani kila mmoja alikuwa katika harakati za kuingia katika chumba cha mtihani pale chuoni.
Wakati wenzake wakiwaza mtihani mmoja tu yeye alikuwa yu katika dimbwi la mitihani miwili.
Mtihani wa chuo ambao haukumtoa jasho sana kwa sababu hata kama angesema asiufanye bado alikuwa na namna ya kutumia pesa na kuonekana kuwa ameufanya na kufaulu na hata kama ingeshindikana na asiwe mwanafunzi kuanzia siku hiyo bado asingebabaika katika maisha yake.
Mtihani wa pili uliokuwa ukikiumiza kichwa chake ni kitendo cha kijana mmoja raia wa Tanzania aitwaye Chopa kuwa huru tena uraiani kabla ya muda uliokusudiwa.
Sasa alikuwa akihitaji kujua hatua zote ambazo Chopa alikuwa akipitia, na taaruifa ya mwisho aliyopewa usiku uliopita ni kwamba Chopa aliingia ukumbi wa starehe lakini kuna askari waliovaa kiraia walikuwa wakimfuatilia.
Hili jambo lilimuumiza sana kichwa, na simu ya pili aliyopigiwa usiku huohuo ilimueleza kuwa aliyetoa agizo la Chopa kufuatiliwa sio taasisi bali ni mtu mmoja aitwaye Luteni Bosco, kuhusu sababu ya kwanini ameagiza hivyo huu sasa ulikuwa ni mtihani wenyewe ambao jibu lilikuwa halijapatikana.
Binti huyu mwanafunzi wa chuo alijiuliza sana kuna kitu gani kinaendelea!!
Hatimaye ujumbe aliokuiwa akiusubiri uliingia.
Ujumbe kutoka kwa Tz 11.
“ANAKABIDHI CHUMBA! NIFUATANE NAYE AU NIMFUATILIE BOSCO?” Ujumbe ulihoji.
Binti akautazama kwa muda kisha akajibu.
“FANYA YOTE!”
Halafu akaizima simu yake na kuingia katika chumba cha mtihani.
“Odongo why are you late?” sauti ya kike ya mkufunzi ilimuuliza binti huyu wakati anaingia pale darasani.
“I’m sorry!” alijibu kwa kifupi kisha akachukua nafasi yake.
Wakati anaufanya mtihani na Tz eleven naye alikuwa yupo kazini.

______

SOFIA BINTI BOSCO, licha ya umachachari wake hakuna kitu kigumu kilichokuwa kikimsumbua siku zote kama mwanzo. Alikuwa akiumiza sana kichwa na kujichukia yeye mwenyewe anapokuwa katika kuusaka mwanzo wa kitu chochote kile.
Safari hii tena alikuwa katika kuutafuta mwanzo wa mkasa huu, alisikia kuwa askari wawili waliuwawa, alisikia pia kuna bwana anaitwa Manfredy alikuja kumuulizia Pocha lakini hakulisikia jina Chopa katika mlolongo wote huu.
Na Chopa ndiye alikuwa mwanga katika mkasa huu.
“Pocha una uhakika kuwa Chopa yupo huku Ukonga?” Sofia alimuuliza Pocha baada ya akili yake kukwama kabisa katika kuupata mwanzo.
“Da’ Sofi ujue mimi sio kwamba ni Mungu najua kila kitu, zile ni hisia na hadi sasa sielewi huwa zinakuja vipi... hivyo naogopa kusema nina uhakika maana utaniuliza tena yupo wapi” alijibu Pocha kwa utulivu kabisa. Lilikuwa jibu tosha kabisa kwa Sofia na ulikuwa ukweli.
Sofia alituliza kichwa kisha akamuuliza tena.
“Umewahi kumuwaza mtu tena na mwisho ikawa kweli?”
“Ndio ni Chopa tena nilimuwazia kuhusu kuhamishwa gereza ama kuuwawa ilimradi tu niliwaza kuwa kuna mmoja kati yetu atamwacha mwenzake...” alijibu Pocha tena kwa umakini mkubwa.
“Ujue Ukonga kubwa sana hii,... tunataka kumtafuta mtu ambaye hatuna namba yake... dah!” Sofia alizungumza huku akionyesha dhahiri kuanza kukata tamaa. Ile hali hata Pocha aliigundua.
Simu ya Sofia iliuvunja ukimya ulioanza kutanda! Akaipokea na kusikiliza kwa muda kisha akaikata bila kujibu chochote.
“Baba anasema aliyewaua vijana wake anadaiwa kuwa ni mwanamke....” Sofia alisema kisha akaendelea, “Ujue babangu yule anawadharau sana wanawake sijui kwa nini, yaani hapo atakuwa amechukia sana... haamini kama mwanamke anaweza kumuua mwanaume.” Alimalizia Sofia, kisha mpango ukabadilika akamweleza Pocha kuwa babake amemuagiza eneo la tukio akatazame kwa kina nini kilichojiri.
Upesi wakarukia pikipiki katika mtindo wa ‘mshkaki’ na kutokomea.
Wakati wawili hawa wakiwa katika pikipiki kuelekea ule ukumbi wa starehe.
Tz 11 yeye alikuwa katika pikipiki pia kuelekea alipopajua yeye!!

____

SOFIA alifika eneo lile na kujitambulisha kwa baadhi ya askari, walibaki kumtazama kwa macho ya mshangao. Alikuwa ni binti mrembo wa wastani ambaye alionekana kana kwamba ni myonge na hawezi kuwa na uytaalamu wowote katika mambo magumu kama yale.
Sofia aliingia moja kwa moja katika kile chumba cha kuvutia sigara ambacho kulikuwa na maiti moja, akaitazama vizuri kisha akaenda chooni. Akamgusa gusa yule bwana baadhi ya maeneo kisha akatikisa kichwa na kuwageukia maaskari.
“Huyu bwege anajua maana ya kuua....” alisema vile kisha akaomba njia akatoka na kuanza kumpigia simu baba yake ili aweze kumueleza kiundani.
Alipiga simu ikaita bila kupokelewa, akapiga mara ya pili simu haikupokelewa pia.
Akapuuzia kuendelea kupiga kwa sababu kilichotakiwa kufikishwa ni taarifa tu na katu taarifa isingeweza kubadili ule umauti kuwa uhai tena.
Sofia alipiga hatua kadhaa hadi akafika nje alipomuacha Pocha!
Alimkuta Pocha katika hali isiyokuwa ya kawaida, Pocha alikuwa kama mwenye mawenge fulani hivi yanamsumbua kichwani.
“Sofia una uhakika kila kitu kipo salama hapa...” Pocha alimuuliza.
“Yah! Kwani kunani?”
“Aaah! Sijui nina nini mimi yaani mapigo ya moyo yako mbio sana.... sijui hata ninafumbwa kitu gani mimi... ila kuna jambo.. ila kama hapa pako salama basi sawa tuendelee huenda huko mbele kuna shida” alijibu kwa unyonge Pocha.
“Haya ngoja nimpigie mzee mara ya mwisho asipopokea mi tutakutana jioni nimpe majibu ya alichoniagiza.”
Akaingiza namba na kupiga, simu ikaita pasi na kupokelewa.
“Pocha eeh! Twende zetu....” Sofia alisema huku akianza kutangulia.
Pocha akamfuata nyuma, mwili unakubali lakini akili ikiwa imekataa kabisa kuwa sawa.

_____

Damu nzito ilikuwa ikimtoka puani na midomoni, taya zilikuwa zimelegea kiasi kwamba hakuweza kuufunga mdomo wake. Hii ikasababisha avuje udenda ulioambatana na damudamu.
Alikuwa amepiga magoti, si kwa kukusudia ama kuamrishwa na mtu la! Bali asingeweza kusimama kutoka pale alipokuwa.
Kitako cha bunduki kilikuwa kimelainisha magoti yake ambayo yalikuwa yameupoteza ule ukakamavu wake wa siku za nyuma. Alikuwa amejibu maswali yote kama alivyoulizwa lakini hiyo haikuwa sababu ya yeye kujikuta katika pona pona.
Macho yake yalikuwa yakimuangalia mwadada aliyekuwa mbele yake katikanamna ya mshangao na nyingine ikiwa ni namna ya kuomba msamaha katika namna nyingine.
Lakini tatizo lilikuwa ni msamaha kwa kosa gani?
Mwanadada yule akiwa bado na yule mzee ofisini kwake alinyanyua simu yake na kubofya nambari kadhaa, alipojaribu kupiga akagundua kuwa simu yake haina salio la kutosha.
“We babu, simu yako ina dakika za kupiga nje ya bnchi... nahitaji kama dakika moja tu!” yule binti alimuuliza yule mzee ambaye hakuwa na uwezo wa kusema lolote. Akatikisa kichwa kukataa.
“Mzee Bosco mi nakuuliza kwa sauti we unanijibu kwa kichwa aisee wazee wa siku hizi mna dharau kweli. Haya endelea na dharau zako ipo siku zitakuponza...” alizungumza yule binti kwa masikitiko makubwa.
“Halafu siku ukitengemaa vizuri afya yako waambie wakuu wako wa kazi mchezo wa kuweka kamera ambazo hazifanyi kazi waache, yaani nimetumia muda mwingi kujivalisha haya mawigi kumbe kamera hamna....wakikuuliza nani ametoa huo ushauri waambie ni TZ 11” alimalizia binti yule kisha akampungia mkono luteni Bosco na kutoweka.
Alitoka huku akiwaaga wafanyakazi wengine pale kana kwamba hakuna lolote baya lililotokea.

____

SIMU ya Sofia iliita wakati akiwa katika pikipiki, akatokwa na tusi la kawaida alilolizoea pindi anapokereka.
“Yaani mshua anazingua nimempigia muda wote hapokei halafu sasa hivi anapiga nisipopokea analalamika, oya punguza mwendo!” akamwamuru dereva wa pikipiki. Kisha akaipokea simu.
“Mzee nipo kwenye pikipiki!” alizungumza na kisha akataka kukata simu, lakini kuna kitu cha tofauti alikisikia. Alisikia kama muungurumo wa kiumbe , akasikiliza kwa makini akasikia tena muungurumo.
Akaita jina la baba yake akitanguliza cheo chake lakini hapakuwa na jibu zaidi ya muungurumo.
Sofia akaikata ile simu na kisha akamuamuru dereva abadili uelekeo na kufuata njia ya kuelekea gereza la ukonga.
Dereva akatii!!
Walipokaribia gerezani Ukonga, Sofia akamzuia dereva, akamlipa ujira wake kisha akasubiri alipoondoka ndipo akaongozana na Pocha hatua kwa hatua hadi katika ule mgahawa waliokutana awali. Akamuacha pale, kisha akiwa makini kabisa alisimama ili aweze kutoka nje.
Wakati anatoka aligonganisha macho na binti aliyekuwa anakunywa soda , japokuwa ilikuwa kwa sekunde moja tu ya kutazamana Sofia alisisimka sana kwa sababu alitambua kuwa alikuwa anatazamana na kiumbe ambaye si wa kawaida kabisa. Lakini hakupoteza muda kumfikiria kiumbe yule badala yake aliendelea na hamsini zake....
Akatoweka na kufika kule gerezani, akazifiokia ofisi za baba yake na kumkuta katibu muhtasi akiwa amejikita katika kusikiliza muziki huku akijaribu kuimba baadhi ya beti.
Sofia akamuulizia mzee Bosco.
“Yupo lakini hadi itakapotimu saa sita na nusu ndipo ataanza kuonana na watu sasa hivi ametingwa sana.. samahani eeh!” alizungumza dada yule huku tabasamu likiwa limemtawala.
Sofia alisihi kuwa ni lazima aingie ndani, akajitambulisha kuwa yeye ni mtoto wa mzee Bosco lakini katibu muhtasi yule ambaye kwa namna moja alipitia kupiga kwata katika ngazi ya kuruta alitoka upesi na kusimama mbele ya Sofia.
“Binti nitakuwasha makofi halafu hutakuwa na cha kunifanya nitakutupa selo sasa hivi. Nimesema hiyo ni amri!” alifoka yule dada.
“Na nikiivunja hiyo amri kwa sababu za usalama wa mzee wangu je?”
“Ni sisi tunaoujua usalama wa mzee wako, wewe kama ni baba yako usalama wake unaujua hukoo nyumbani not hiya” alizungumza kwa kusisitiza huku akichombeza kiingereza mwishoni.
Sofia alipiga hatua moja mbele zaidi, yule dada akajaribu kumsukuma, lakini alijikurta akiwa amesukuma gogo zito lisilotikisika, Sofia akapenya na kuufikia mlango wa mkuu wa gereza.
Akausukuma huku bunduki yake ikitoka katika kiuno na kuhamia kiganjani.
Sofia aliruka katika namna ya kubiringita sambasoti na kutua katikati ya ofisi ile, akageuka huku na kule akimaanisha kuwa yeyote atakayejileta mbele yake ni halali yake.
Alikuwa amemuona baba yake akiwa katikati ya dimbwi la damu pale ofisini kwake lakini hilo hakulizingatia kwanza, aliulinda usalama wa eneo linalomzunguka.

_____

Wakati Sofia akiwa amejikita katika kujiweka vyema dhidi ya adui yeyote anayeweza kujitokeza.
Upande wa Pocha hakuwa amekaa peke yake, bali alikuwa yu na msichana mrembo sana asiyeishiwa tabasamu usoni kwake.
Alikuwa amejitambulisha tayari majina yake bandia. Pocha naye akajitambulisha lile jina lake la Possian.
Binti yule aliingia pale kwa gia ya kumsalimia Pocha na kumsifia kuwa mchumba wake ni mrembo sana. Dada yule aliendelea kumdadisi Pocha kwa uchache ikiwa mchumba wake yule anafanya kazi hapo Ukonga ama la.
Pocha akajitahidi kukwepa kumzungumzia Sofia!!
Baada ya mazungumzo ya kama dakika tatu, binti yule aliaga katika namna ya aina yake.
“Akirejea mwambie nimempenda sana alivyonitazama wakati anaondoka... akikuuliza jina langu usiseme Getruda mwambie TZ 11” Akakishika kiganja cha Pocha na kukiminyaminya kisha akaondoka zake akimwacha Pocha akiibiaibia kuyasindikiza maungo ya nyuma ya binti huyo.
 
Back
Top Bottom