SEHEMU YA 12
CHRISTINA mkewe Lucas hakushtuka asubuhi na kuanza kulalamika kuwa anataka kuacha ubunge na kisha kwenda na mumewe London, huu ulikuwa ni mchakato ambao ulianza siku kadhaa nyuma hata kabla Lucas hajazungumza na vyombo vya habari.
Hiyo siku alipokea ugeni ambao haukuwa ugeni katika ile maana halisi ya ugeni lakini alilazimika kuuita ugeni.
Huu ulikuwa ni ujio wa Carolina Edwin ambaye alizoea kumuita mama mdogo na yeye akamuita mwanaye. Ilikuwa ni kawaida kila anapotoka uingereza kituo cha kwanza ni nyumbani kwake na kisha safari kwenda Mwanza.
Hivyo hata sasa alikuwa akipita tu, alikaa kwa siku tatu kabla ya kupanda ndege kwenda Mwanza kwa wazazi wake, ilikuwa ni siku ya pili tangu Carolina awe pale nyumbani huku muheshimiwa Lucas akiwa bado nchini uingereza.
Siku hii Christina aliamua kutoka na Caro kwenda kuogelea katika mojawapo ya fukwe za kisasa zinazosifika zaidi jijini Dar es salaam kwa utulivu uliopo katika mazingira hayo.
Walifika fukweni majira ya saa kumi jioni, alianza Christina kuogelea akimuacha Caro aliyekuwa amejikita kuvuta ‘shisha’.
Baada ya takribani nusu saa ndipo caro alipovua nguo alizokuwa amevaa na kisha kuvalia nguo maalumu kwa ajili ya kuogelea kisha akajiunga na Christina katika maji.
Ni hapa ambapo Christina alikiona kitu ambacho kilimshtua sana, alijaribu kukipuuza lakini haikuwezekana kilikuwa ni kilekile alichokiona siku kadhaa nyuma kisha kikapotea machoni mwake akibaki bila ushahidi wa kutosha.
Christina alikuwa ameona kovu katika mgongo wa Christina, kovu hili lilikuwa limejichora na kuacha michirizi inayofanana na herufi ‘C’. Kovu hili aliliona siku ile ambayo alikuwa anazungumza na mumewe kupitia mtandao wa ‘Skype’.
Hisia za uchungu zilimtawala akajikuta akitokwa na machozi, bahati nzuri maji yalionyesha ushirikiano na kuyasomba machozi yakaondoka zake.
Hakuna aliyejua kama alikuwa analia.
Ile starehe ilikomea pale, Christina akajiuliza maswa li mengi sana.
Alijiuliza inawezekana vipi mumewe ambaye ni mtu mzima kabisa aende kushiriki mapenzi na yule mtoto ambaye ni sawa na mwanaye wa kumzaa kabisa, hili lilimfadhaisha sana alipojaribu kujenga picha kuwa yupo katika mzani wa mapenzi na yule mtoto sasa muheshimiwa anachagua yupi ni bora kati yao.
Christina alikumbwa na ghadhabu akajisemea kuwa ni heri aachane na Lucas kuliko hii fedheha iliyokuwa inamkabili, lakinmi hapohapo akakumbuka kuwa kuachana na Lucas ni kumpa nafasi ya kujimwayamwaya zaidi na yule binti.
Pia alipokumbuka kuwa alikuwa hajawahi kumzalia mtoto hata wa dawa mheshimiwa Lucas nguvu zilimwishia.
Hata kangeamua kuachana na Lucas, angeenda kwa nani?? Nani angekuwa radhi kumuoa mwanamke ambaye umri unazidi kwenda halafu hana mtoto.
Hili pekee halikutosha, lililomkosesha amani kabisa ni ule ukaribu aliokuwanao na wake wa wabunge na mawaziri wengine, kama angeachana na Lucas basi ule ungekuwa mwanzo wa kuwapoteza marafiki wa hadhi yake na angetakiwa kutafuta marafiki wengine.
Msumari wa mwisho ulikuwa ni vijembe ambavyo angevipata bungeni, ikiwa atazungumza lolote ambalo lina sintofahamu basi wapinzani watajenga hoja kuwa ikiwa ndoa yake pekee imemshinda kutunza itawezekana vipi kuwatunza wananchi na kuwatendea haki?
Jingine ambalo lilikuwa na uzito pia aliloliwaza ni iwapo huyo binti atamzalia mtoto muheshimiwa Lucas ni kitu gani kitajiri??
Mawazo haya yalimvuruga sana Christina, alimsihi Caro waondoke kwa sababu kichwa kinamsumbua, akamsihi Caro pia aendeshe gari wakati wa kurudi nyumbani.
Hilo lilitimizwa wakarejea nyumbani salama.
Christina alilala akiwa na mawazo tofauti tofauti, lakini asubuhi aliamka akiwa na wazo moja aliloliona kuwa ni la busara sana.
Christina aliamua kuipigania ndoa yake huku akiamini kuwa iwapo ataipoteza basi kamwe hawezi kuja kupata ndoa kama hiyo.
Ni hapa hekaheka zake ziliposhika kasi!
Sasa alikuwa hakamatiki wala hasikiki anahitaji kuishi uingereza akiwa na mume wake.
_____
PRISCA katibu muhtasi wa Lucas katika ofisi yake kubwa iliyopo Dodoma alikuwa mtu wa kwanza pale ofisini kugundua kuwa bosi wake hakuwa na raha kabisa tangu arejee kutoka katika safari yake kisha kufika nyumbani kwake jijini Dar es salaama na sasa uwepo wake ofisini.
Kwanza hakuwa nadhifu kama ilivyokuwa kawaida yake, nywele zake zilikuwa hazijachanwa.
Muonekano wa muheshimiwa Lucas haukuwa ukimuhusu Prisca na hata katika mkataba wake wa kazi kipengele cha kuingilia mambo binafsi ya bosi wake hakikuwepo.
Lakini wambea hawahitaji mkataba ili waweze kutumia vipaji vyao, inapobidi wanafanya.
Prisca hakutaka hili limpite hivihivi, akaingia ofisini kwa bosi wake ili kumpa taarifa kadhaa za pale ofisini tangu aliposafiri.
Alipofika bafuni akajifanya kushtuka kidogo, kisha akamuuliza bosi wake kulikoni. Alikuwa hajachana nywele zake na pia alikuwa ananuka pombe!!
Lucas alimtazama Prisca kwa muda kidogo bila kusema lolote. Prisca akajiwahi kuzungumza, alivyozungumza usingeweza kusema ni mmbea.
“Samahani muheshimiwa, najua si haki yangu kujua yanayokusibu... lakini kiubinadamu nimejikuta nakosa amani kukuona katika hali hii.... samahani kama nimefanya kosa kukuuliza...” alizungumza kinyonge, na hapo akageuka ili aweze kuondoka.
“Prisca!” Lucas akamuita, akaitika kwa nidhamu ya hali ya juu. Lucas akamuomba aketi... akafanya hivyo....
“Prisca, wewe ni binti mdogo sana lakini haimaanishi kuwa wewe ni mtoto.... najua nikisema mapenzi unanielewa...” akampa nafasi Prisca ya kutikisa kichwa ishara ya kukubali.
“Basi haya mapenzi ndiyo yananifanya nipo hivi, lakini usijali kabisa nitakuwa sawa tu hivi karibuni.....”
“Mh! Ni mama anakusumbua au?” aliuliza Prisca akimaanisha mke wa Lucas.
Lucas akasita kidogo kisha akatokwa na neno ambalo lilimsababisha Prisca aone muda wa kutoka kazini haufiki ili aweze kulitoa funda lililomkaba kooni.
Akaondoka pale ofisini akiwa amezungumza mambo mengi sana na bosi wake.
Lucas hakujua kabisa kuwa pombe sio chai, ukiifakamia hovyohovyo inageuka kuwa mwanaharamu.
Akili yake ya pombe akajikuta akimuona Prisca ni mshauri mzuri sana!!
Akamwaga matatizo yake ili ashauriwe!!
Pombe zilipomwishia alijilaumu kwa kumsirikisha Prisca mambo yale lakini alimpuuzia kwa kuhisi kuwa hawezi kuzua lolote la maana ambalo litamchafua yeye.
Ama! Usiku wa giza ni heri kuliko usilolijua, usiku wa giza unakufanya utembee kwa tahadhari ili usijikwae kwa sababu unajua huu ni usiku. Lakini USILOLIJUA.........
_______
Usilolijua si sawa na usiku wa giza bali ni zaidi ya giza lenyewe.
Laiti kama usilolijua lingekuwa sawa na usiku wa giza basi Pocha na Chopa wasingeweza kufanya lolote katika usiku ule wa giza waliokubaliana kukutana.
Ilikuwa ni kawaida katika vyumba walivyokuwa wamehifadhiwa Chopa na Pocha kuna wakati ambao taa zinazimwa na kuunda giza nene sana, hata usiku huu ilikuwa vilevile.
Lakini mikono ya Pocha ina macho ya ziada haihitaji macho ya kawaida ya mwanadamu kuweza kutoa ‘loki’ za vitu tofauti tofauti. Alifanikiwa kuufungua mlango licha ya giza lile.
Akamshtua Chopa, wakaketi na kuzungumza kuhusu mustakabali wa maisha yao ndani ya vyumba vile ambavyo hawajui hata vinapatikana eneo gani ndani ya Tanzania. Na hawakujua kuwa ni baada ya vyumba vingapi wanaweza kuwa nje ya eneo lile, walitakiwa kwanza kuupata mwangaza kidogo ili wakiamua kutoka basi wasirudi nyuma.
Walizungumza mengi sana kwa sauti za kunong’ona. Kikubwa walitaka kujua nini chanzo cha yote haya, kama ilivyokuwa kule gerezani Pocha alijua ni kwa nini yupo gerezani na hata hapa anafahamu kuwa yupo kwa sababu alikuwa tu anatafutwa na Chopa.
Chopa amefanya kosa gani??
Hili lilikuwa swali zito sana lililohitaji ufumbuzi wa upesi.
Baada ya kuzungumza sana hisia zote za Chopa kuwa katika utata huu.
Hatimaye Pocha akasema hisia zake.
“Chopa kwa maelezo yako yote juu ya maisha yako ya utafutaji, mapenzi na tofauti zako na watu baadhi mimi kuna kitu nahisi hapa ambacho kipo nyuma ya haya mambo.....” akasita kidogo kisha akaendelea, “Kaka yaani hapa nisiseme eti machale yamenicheza ama vipi lakini katika majibu hata la uongo nalo jibu... mi nahisi huu ni MPANGO WA KANDO!!” Pocha alimalizia.
Kauli hii aliwahi kuisema awali kabisa wakiwa gerezani, akawa ameirudia tena kwa mara ya pili.
“Mh! Mpango wa kando? Kiaje unaufahamu huu mpango au? Maana gerezani ulinambia tena halafu haukuendelea kunieleza, Pocha tafadhali naomba unipe mwanga....”
“Ntakupaje mwanga ilihali na mimi nipo gizani, tusaidiane kulitafuta hilo jibu ambalo nd’o mwanga wenyewe kaka...” Pocha alijibu.
“lakini walau basi wewe unao huo mwanga, unahisi ni mpango wa kando.. nieleze ili na mimi niwe sawa na wewe kisha tuendelee mbele” Chopa akamsihi Pocha.
pocha akatulia kwa muda na kisha akapitia katika maelezo ya Chopa aliyotoa nayea akaelezea ambalo analihisi juu ya utata huu.
_____
Miaka kadhaa nyuma
MBEYA, TANZANIA
Wakati huu alijulikana zaidi kama Manfredy, haswaa na hili ndilo lilikuwa jina lake la kuzaliwa. Alikuwa mchapakazi, alikuwa ameajiriwa kama dereva lori lililokuwa linabeba mizigo ya viazi mbatata na mchele kutoka mjini Mbeya kupeleka sehemu mbalimbali za Tanzania ambazo zilikuwa zikihitaji sana huduma hiyo. Madereva wa barabarani wanayo tabia ya kujisifu kila mmoja akijitapa kuwa anaweza sana kuendesha gari kumpita mwenzake. Lakini kwa Manfred haikuwa hivi, alikuwa mtulivu sana aliacha kazi yake ijitangaze na kumpatia sifa.
Hakuwa na rekodi mbaya za kupinduka ama kugonga watu ama wanyama barabarani, hakuwa mlevi na lililosambaza sifa zake zaidi ni ile hali yake ya kuendesha gari kwa mwendo kasi lakini salama.
Hali hii ya kufika mapema zaidi Mbeya kisha kuingia mikoani na kisha kurudi Mbeya, wanyakyusa wakalifananisha lori alilokuwa anaendesha Manfredy kama helikopta ya mgombea uraisi mmoja wa chama cha upinzani, siku alipotua Mbeya mjini aliwaambia ile haiitwi Helikopta bali waiite Chopa inakwenda kasi kama yeye atakavyoingia kwa kasi ikulu.
Neno Helikopta likasahaulika na CHOPA likachukua nafasi, ilifikia hatua hata ndege za kawaida tu wakazi wa mbeya waliziita Chopa.
Hatimaye jina hili likahamia katika lori la Manfredy..... jina la Lori likahamia kwa Manredy wakamuita muendesha Chopa lakini hii haikufurahisha kutamka mdomoni. Wakalifupisha zaidi na kumuita Chopa.
Jina likamkaa, lile la kuzaliwa likasahaulika.
Manfredy akageuka kuwa Chopa.
Hakulichukia jina lile, alilipenda sana na kulifurahia katika nafsi yake lakini kwa nje hakusita kuwakumbusha watu kuwa Manfredy Gregory ndilo jina lake la kuzaliwa.
Maisha ni ujanja kabla hujapata!
Chopa alikuwa akibena abiria kadha wa kadha katika safari zake nyuma ya utambuzi wa bosi wake, alifanya hivi ilimradi kujipatia kipato cha ziada.
Katika pakia pakia hii kuna siku alipakia wanafunzi watatu wa kike, hawa walikuwa wana safari ya kwenda Dodoma lakini walikuwa hawana nauli ya kutosha.
Chopa alipewa taarifa hizi akazipokea katika lugha ya biashara akataja bei ya kawaida tu, baada ya muda akaambiwa kuwa asubuhi na mapema watakuwa wamefika eneo walilokubaliana.
Chopa alikuwa akiwaza kuwa watakuwa wanafunzi wa kiume, asubuhi inafika anapewa wanafunzi wa kike waliodai kuna chuo kikuu kimoja hapo Mbeya walikuwa wanasoma.
Walipozungumza ndipo Chopa akapata mustakabali, kuwa wanmgekuwa wanafunzi wa kitanzania wala wasingeweza kupanda lori lakini wale walikuwa kutoka nje ya Tanzania.
Wakiwa safarini walijitambulisha mmoja alikuwa anatoka Uganda japokuwa alikuwa mtanzania, mwingine Mnyarwanda na wa tatu alikuwa anatoka Somalia lakini wazazi wake walikuwa wakiishi Kenya.
Ni watanzania wanaojali zaidi nani atasema nini wakifanya hivi, lakini hawa hawakujali walitazama pesa walizokuwanazo katika mifuko yao.
Walizungumza mengi na kuifanya safari kuwa ya kuchangamka, Chopa akaelezea naye kwa upande wake.
Baadaye katika ongea ongea mara ikazaliwa mada kuwa madereva wa malori wanaongoza kwa umalaya, Chopa alijitetea sana lakini wale wasichana walikuwa na ushahidi mkubwa sana, Chopa alilazimika kukubaliana nao lakini akijitoa kati ya orodha ya madereva hao wahuni.
Walipokaribia Dodoma yalianza mazungumzo juu ya wapi watafikia, wawili walionekana kuwa na pa kufikia ambapo si pa uhakika lakini mmoja alikuwea njia panda hakuwa na uhakika sana kama anapotaka kufikia patakuwa sawa.
Chopa alikuwa kimya kabisa haya yalikuwa hayamuhusu.
Hadi wanafika Dodoma yule binti kutoka Rwanda hakuwa na uhakika wa ni wapi atafikia na ilikuwa ni usiku tayari.
Hapa sasa Chopa akalazimika kuzungumza, akamweleza yule dada kuwa anamrudishia pesa aliyolipia kama nauli ili aweze kutafuta nyumba ya kulipia aweze kulala.
Ule msaada wa Chopa pasipo na kuhitaji jambo klolote lile ulimstaajabisha yule dada ambaye baadaye alijitambulisha kwa jina la Nkozimakale ama kwa kifupi Nkozi.
Chopa akamwambia asijali, akaagana nao na kuwakaribisha tena pindi watakapohitaji huduma yake.
Nkozi na wenzake waliondoka wasiamini kile kilichokuwa kimetokea, dereva wa lori anakurudishia pesa uliyomlipa hakuombi namba wala kukushawishi ulale naye.
Ajabu!!
Ulipita mwezi mmoja, Chopa akiwa amesahau ile fadhila aliyofanya kwa yule dada, na si fadhila tu hata jina alikuwa amelisahau.
Ilikuwa rahisi sana kulisahau jina lile kwa sababu kila siku alikuwa na wateja wapya katika lori lake.
Siku hii akiwa jijini Mbeya maeneo ya Uyole simu yake iliita ilikuwa ni namba mpya, akapokea na kumsikiliza aliyekuwa anazungumza. Alikuwa ni mwanamke, alimjulia hali huku akimuuliza habari za siku nyingi.
Walizungumza kwa muda wa dakia moja, kisha Chopa akamsihi mpigaji ajitambulishe.
“Sijui kama utanikumbuka Chopa lakini naitwa Nkozi... Nkozimakale... yule dada...” kabla hajaendelea Chopa akadakia kiuchangamfu tayari alikuwa amemkumbuka.
Nkozi akatoa shukrani za dhati kwa usiku ule aliomsaidia bila kujalisha lolote. Chopa alimsihi asijali lolote, na kisha akamuuliza ni wapi alikuwa kwa wakati ule, Nkozi alikuwa Uyole pia.
Chopa akamsihi waonane kama inawezekana.
Nkozi akakubaliana na Chopa akamuelekeza alipokuwa hapakuwa mbali sana, Chopa akapiga hatua kadhaa hatimaye akakutana na Nkozi.
Moyo wa Chopa ulipiga kwa nguvu sana, tangu awe katika mahusiano na mpenzi wake wa muda mrefu Carolina hakuwahi kushtuliwa na mwanamke mwingine kama ilivyokuwa kwa huyu binti wa Kinyarwanda. Na hapa akakiri kuwa alikuwa anatazamana na kiumbe ambaye hawajawahi kuonana kabla.
Alikuwa amevaa sketi fupi kiasi iliyoruhusu mguu wake mweusi kuonekana vizuri na kuleta ile maana pendwa ya mguu wa bia. Alipopiga hatua kumsogelea Chopa ni kama mwili wake ulikuwa mzito kumuelemea, lakini hakuchukiza kwa jinsi alivyokuwa anatembea, badala yake alifurahisha macho ya wengi.
Pocha akiwa mmoja wapo!!
Ule mshtuko wa moyo ukazua mengine, Chopa akaona itaupendeza moyo wake akiwa karibu na Nkozi.
Kwa Nkozi naye ilikuwa hivyohivyo.
Wakapanga siku ya kukutana wazungumze zaidi.
Chopa alikuwa mwanaume kama wanaume wengine, msichana mrembo kama Nkozi unaanzaje kumueleza bayana kuwa eti unaye msichana mwingine aitwaye Carolina hivyo yeye awe katika nafasi ya pili.
Chopa akajikuta akiutapika uongo mdomoni na kuuacha ukweli moyoni. Licha ya Nkozi kumueleza kuwa hadi umri huo alikuwa amejihusisha na mapenzi mara moja tu na hakuyafurahia bado Chopa hakuwa na huruma na moyo wa Nkozi.
Nkozi kabla ya kumkubalia Chopa kuwa naye katika mahusiano alimweleza maneno ambayo Chopa aliyapuuzia lakini yalikuwa mazito sana.
“Chopa, mnamo mwaka 1994 nilizaliwa huko Rwanda, nikiutaja mwaka huo nadhani unaelewa ni kitu gani kilitokea nchini kwetu. Inasemekana mama yangu alinizaa baada ya kupigwa risasi pajani akashikwa uchungu na kunizaa kabla ya wakati na ni kwa neema zake Mungu hadi leo nipo hai. Kuna mwanajeshi mmoja wa kihutu alinisaidia kunifikisha hospitali ambapo ndio ilikuwa ponapona yangu lakini haya yote ni kwa mipango ya Mungu tu. Hivyo basi simjui baba wala mama yangu na simjui ndugu yangu hata mmoja, ninachofahamu ni kwamba watakuwa waliuwawa kwa kosa la kuzaliwa watutsi.
Nimelelewa na watu baki tu, na labda haya nd’o maisha yangu kulelewa na watu baki... hata wewe uliyenisaidia usiku ule ni mtu baki na niliyekuwa naenda kwake naye alikuwa mtu baki. Nikisema najikabidhi kwako leo Chopa elewa kwamba wewe unakuwa ndiye ndugu yangu..... sijiachii kwako kwa sababu tu nahitaji kuwa na mpenzi hapana... najikabidhi kwako kwa sababu nahitaji kuwa na ndugu walau mmoja tu. Uwe kaka yangu Chopa, uwe baba na mume kwangu.... nakusihi usiyapuuze maneno haya....mimi ni wako sasa.” Alimaliza Nkozi kisha akamkumbatia Chopa na kumpiga busu mwanana.
Na mapenzi yao yakaanzia hapo rasmi.
Kwa Nkozi likiwa ni penzi moja kwa mtu mmoja lakini kwa Chopa likiwa ni penzi moja kwa wanawake wawili. Caro anayejulikana kila kona na Nkozi anayejulikana kwa marafiki wa Mbeya pekee.
Penzi hili lilikuwa thabiti sana kwa sababu tu ubavu mmoja ulikuwa Dar es salaam na ubavu mwingine ukiwa Mbeya, akiwa Mbeya Chopa alikuwa anamjali zaidi Nkozi huku Caro akielezwa kuwa kazi zimemzidia na hawezi kuwasiliana naye mara kwa mara, na kinyume na hapo alipokuwa jijini Dar es salaam.
Mchezo huu uliendelea hadi pale Chopa alipoipoteza kazi yake baada ya mmiliki wa lori kufilisika na kuamua kuliuza lile lori.
Huu ukawa mwanzo wa penzi lile kuyumba na hatimaye kimya kikatanda baina ya pande hizi mbili.... Chopa akatabasamu akiamini kuwa Nkozi amejiongeza kivyake.
Nguvu zote zikahamishiwa kwa Carolina jijini Dar es salaam.
Lile jeraha aliloliacha katika moyo wa Nkozi bila kujua kuwa ni hatari sana kuumiza moyo wa aliyewahi kuumizwa hapo kabla.
Nkozi alikuwa mjeruhiwa mzoefu!!
______