RIWAYA; MKANDA WA SIRI
MTUNZI; HALFANI SUDY
SIMU 0674 395733
Sehemu Ya Mwisho season 1.
Ulikuwa ni mwezi wa mashaka mazito na upelelezi mkali toka katika jeshi la Polisi kwenda kwa watu wawili. Vikosi vya jeshi la Polisi vikiongozwa na Koplo Baruani viliendelea na msako wao ambao kwa sasa ulielekea kufeli, tunaweza kuuita msako uliofeli wa kumsaka kijana Martin Nguzu, jamaa anayetuhumiwa kumuua mtu ndani ya gari bandarini. Msako huo ulienda sambamba na msako wa kumsaka Mr Na na na, mzungu aliyeacha taharuki kubwa sana katika hoteli ya Grand villa. Koplo Baruani alitumia mbinu zake zote alizofunzwa katika chuo cha upolisi, CCP Moshi, koplo Baruani alitumia pia mbinu za ziada alizotunukiwa na Mwenyezi Mungu. Pamoja na kutumia mbinu hizo mbili alizozipata katika sehemu kuu mbili alizoziamini sana lakini jina la Martin Nguzu lilibaki kuwa kama msamiati mgumu ambao haukuwahi kutokea katika lugha yake adhimu ya Kiswahili. Na kuhusu Mr Na na na, ilikuwa ni sentensi tata yenye utata mwingi sana, ambao kwa mwanafunzi wa kiwango chake cha elimu hakuweza kuutatua utata huo.
Pengine alichokuwa anakosea Koplo yule kijana pamoja na Jeshi la Polisi kwa ujumla ni kufanya upelelezi ndani ya upande mmoja tu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hawakutilia maanani kabisa kuhusu upande wa pili wa Muungano, kisiwa cha Zanzibar. Upande ambao ndipo yalipokuwa majibu ya maswali yao yote.
Ilikuwa umepita mwezi mmoja na wiki kadhaa toka kifo cha Shanta wa bandarini, kijana mbabe kuliko wote bandarini, Mansour. Leo hii ilimkuta Koplo Baruani akiwa nje ya nyumba anayoishi Martin pindi akiwa jijini Dar es salaam. Nusu saa ilimuweka koplo Baruani katikati ya mlango wa nyumba ile, kasimama mithili ya sanamu la pale Posta. Alikuwa anabisha hodi bila ya kujibiwa. Pamoja na jitihada zake za kuisaka nyumba ile hadi kuipata lakini kitu ambacho alikuwa hajakifahamu bado.....Martin alikuwa anaishi nyumba ile mara chache sana akiwa jijini Dar es salaam. Mara nyingi hata akiwa Dar es salaam alikuwa analala katika hoteli mbalimbali. Sababu kuu za kuhamahama zikiwa ni hisia zake, alikuwa anazisikiliza sana hisia zake juu ya mahali pa kulala. Hisia zikimkataza anaacha, hisia zikimwambia anafanya. Koplo Baruani alivyoona kimya baada ya kubisha hodi kwa muda mrefu, aliamua kumtafuta Mwenyekiti wa mtaa wa Magomeni Mapipa ili apate ruhusa ya kuingia katika nyumba ile na kuipekua. Ilimchukua nusu saa nyingine kumpata Mwenyekiti wa mtaa. Na sasa walikuwa watu watano mbele ya mlango wa nyumba ya Martin. Walikuwa Mwenyekiti wa mtaa wa Magomeni, wajumbe wawili, shahidi mmoja na Koplo mwenyewe. Walivunja mlango wa nyumba na kuingia ndani. Ilikuwa ni nyumba ndogo yenye vyumba vitatu, bafu na sebule safi ya kisasa. Walipita chumba kimoja baada ya kingine, kwa umakini na tahadhari kubwa sana walijaribu kupekua kila sehemu waliyoihisi inaweza kuwa na lolote, lakini hawakulikuta hilo lolote. Baada ya saa moja walikaa sebuleni na kujadiliana.
"Kwani Martin amehamia lini mtaa huu?" Koplo Baruani alimuuliza mzee Nondo ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa mtaa wakiwa wamesimama sebuleni.
"Ana kama miaka mitano sasa kama sikosei.." mzee Nondo alijibu baada ya kufikiria kidogo.
"Kwani nani alikuwa rafiki yake mkubwa hapa mtaani?" Koplo Baruani aliuliza tena baada ya kuandika maelezo kidogo katika kijitabu chake. "Kwa kweli huyu kijana hajawahi kuwa na rafiki hapa mtaani, alikuwa ni mtu wa kuingia na kutoka, ukimuona leo tarajia kumuona tena baada ya miezi mitatu" Kijana mmoja aliyeitwa kama shahidi katika upekuzi ule alijibu.
"Mtu anaweza kuishi miaka mitano mtaani bila kuwa na urafiki na mtu yeyote, inawezekana kweli hiyo Mwenyekiti?"
"Ni ngumu sana Afande, lakini kwa huyo kijana anayekaa nyumba hii ni nyepesi sana, na amelithibitisha hilo, akwambialo Uledi ni ukweli mtupu" Mwenyekiti alijibu.
Baada ya kuongea hili na lile Koplo Baruani aliagana na watu wale, aliagana nao huku akiahidi kuwa atarejea tena kama atakuwa na sababu ya kurejea, pia aliwaachia namba yake ya simu ya mkononi ili wampigie pindi tu Martin watakapomuona pale mtaani. Naye alichukua namba zao. Koplo Baruani aliondoka huku akiwa bado ana maswali mengi sana juu ya mtu aitwaye Martin Nguzu lakini kwa bahati mbaya sana kwake hakuwa na wa kumuuliza.
*****
"Kumbe wewe nd'o Ayoub, Ayoub Mbembati? daaah tumefanya a big mistake, we can call it " the mistake of the year..!" Malolo alisema kwa sauti kubwa, huku moyoni mwake akiwa anatamani Ayoub aseme yeye sio Ayoub Mbembati. Lakini itatokea vipi hiko anachokitamani? Mbele yao alikuwa amesimama mtu, na alikuwa Ayoub halisi, Ayoub Bin Mbembati.
Ayoub alistuka sana kuisikia sauti ile ikiwa katika mshangao namna ile. Kumbukumbu zake zilirudi kwa kasi sana hadi mwezi mmoja uliopita, wakati alipopata wageni asiowatarajia gizani, na kuporwa mkanda wa siri bila kupenda.
"Usiwashe taa!" Ayoub badala ya kujibu swali la Malolo, ama kukili maelezo ya Malolo, yeye alikumbuka karipio la kutowasha taa alilopewa chumbani kwake gizani. Na ndipo alipoikumbuka kwamba sauti ambayo ilimpa karipio lile, sauti ambayo ilimkataza kwa nguvu asiwashe taa ya chumbani kwake mwezi mmoja uliopita ilikuwa mbele yake, sauti ileile, sauti yenye kupenda kukaripia wanyonge. Hakuwahi kulisahau karipio la sauti ile ubongoni mwake. Alilikumbuka siku zote zilizofuata baada ya karipio lile. Sauti ile ilikuwa imeshajirudia mara kadhaa katika ndoto alizoota baada ya siku ile, ilikuwa ni miongoni mwa sauti mbaya zaidi kuzisikia katika maisha yake, ilikuwa ni sauti mbaya iliyokuwa inamilikiwa na mtu aliyeondoka na mkanda wa siri katika usiku wa giza. Kamwe hakuthubutu kuisahau ile sauti hasa ikiwa katika mtindo wa kukaripia.
"Mkanda si mliuchukua nyinyi lakini..." Ayoub aliropoka akiwa katika hali ya kutetemeka. Kauli ile ilisikiwa na wote, kauli ambayo haikueleweka kabisa na yule mvuvi msindikizaji, lakini kauli ilieleweka, tena ilieleweka vizuri sana na wakina Malolo. Wote walitazamana. Waliielewa maana ya kauli ya Ayoub. Ilikuwa inamaanisha kwamba walikuwa wameenda sehemu siyo sahihi. Walishauchukua mkanda toka mikononi mwa Ayoub mwezi mmoja sasa. Na leo wameenda tena.
"Usiwashe taa!" Peter nae alikumbuka kauli ya Malolo siku ile. Sauti Iliyokuwa inamkataza Ayoub asiwashe taa.
"Labda angewasha taa siku ile, leo hii tusingesumbuka namna hii..ona sasa tumepotea maboya kizembe sana" Mawazo hayo yalipita kichwani mwa Peter. Na ilikuwa kweli, wasingewasha taa wangekuwa na taswira ya Ayoub vichwani mwao, na wangemtambua Ayoub kabla hawajahangaika na kwenda Pemba, wangemtambua pale tu walipomuona kwenye runinga tangu wakiwa Kisarawe.
Upande wa Ayoub alikuwa anatetemeka vibaya sana. Aliamini kwamba wale ndio watu aliokuwa nao katika chumba chenye giza, watu hatari sana wenye kusoma hadi mawazo ya mtu yapitayo kichwani.
"Mkanda walishauchukua sasa wamefata nini tena kwangu, bila shaka leo wamekuja kunimaliza, siku ile walifata mkanda na leo bila shaka wamefata roho yangu! Nina mkosi gani mimi?..." Inawezekana kweli kwamba Ayoub alikuwa na mkosi. Maana alikuwa amepitia na kushuhudia mambo makubwa na mazito sana katika maisha yake. Na bado mambo hayo yalikuwa yanamuandama.
"Mwendawazimu katuuza aisee..." Peter alisema kwa nguvu. Akiwa na maana kuwa Binunu kawauza kwa kuwaonesha mtu sie, lakini kauli ile ilimstua vibaya sana yule mvuvi msindikizaji.
"Hapana jamani, huyu ndiye aliyepo katika picha yenu, ni mwenyekiti wetu wa BMU, wala sijawauza, hebu iangalieni vizuri picha yenu halafu mumuangalie na huyu, au labda mniambie mapacha." Mvuvi msindikizaji alilalama.
"Shut up! Tena funga kabisa mdomo wako mchafu, hatuko katika maigizo hapa, nitakupasua tumbo lako sasahivi na kuutawanya utumbo wako hewani!" Malkia alifoka kwa nguvu huku akirusha mikono yake hewani. Akionesha jinsi atakavyousambaza utumbo wa mvuvi msindikizaji.
Jamaa aliogopa sana.
Hakutegemea kabisa kama watu wale walikuwa wakali namna ile, Mvuvi hakuweza kujizuia majimaji mepesi yasiiloweshe suruali yake, mkojo mwembamba ulimtoka bila kupenda, mkojo mwembamba ulimtoka bila kujua. Kila mmoja aliuona mkojo ule lakini hakuna aliyeujadili. Na tangu hapo wala hakuthubutu kufungua tena mdomo wake ulioitwa mchafu kuchangia chochote. Ingawa kichwani mwake kulikuwa na swali likilojirudia mara kwa mara.
"Hawa jamaa ni wakina nani?, na kuna nini kati yao na Mwenyekiti?" Alitamani sana kuuliza lakini wala hakuthubutu kabisa kulitoa swali lile nje ya mdomo wake mchafu, aliliacha likijiuliza ndani ya ubongo wake. Nani anayewaza kutamani kuuona utumbo wake ukitapakaa hewani.
Sasa Binunu aliingia katika mitaa ya Kisarawe akiwa na akili timamu kabisa. Kila kitu kilichotokea huko nyuma katika maisha yake kabla ya ile ajari mbaya ya meli kilirejea kwa kasi kubwa sana katika akili yake. Kumbukumbu zake adhimu zilizokuwa zimepotea takribani mwezi mmoja sasa zilikuwa zimerejea, kasoro vitu vichache ambavyo vilikuwa vimetokea mara ya mwisho baada ya meli ya Mv Donors kuzama. Hivyo ndivyo vitu pekee ambavyo hakuvikumbuka kabisa. Hakukumbuka baada ya ajari ile mkanda ulielekea wapi?. Alijaribu kukumbuka lakini kumbukumbu zilimgomea kabisa.
"Nakumbuka nilikaa kwenye kiti, baada ya kama ya saa moja meli ilianza kwenda mrama, kishaaaa.....yes.. lilitolewa tangazo la tahadhari, nakumbuka niliutoa mkanda baada ya tangazo lile na kuuvirigiza katika mfuko wa nailoni. Baada ya muda mfupi maji yalianza kuingia kwenye meli, nilisukumwa vibaya sana na yale maji......halafu, halafu kikatokea nini vileeeee, ah mbona nimesahau, aaah yes nimekumbuka.....nilimuona Ayoub Mbembati akiongea katika runinga....nooo sasa kwenye ile meli nilitokaje? Na mkanda utakuwa uko wapi?"
Kwa mara ya tano sasa alijaribu kukumbuka matukio yaliyotokea baada ya yeye kuingia katika meli, lakini aliishia kukumbuka hayo tu. Saa mbili sasa zilikuwa zimepita tangu Binunu akae katika msingi wa nyumba isiyoisha karibu na soko la Kisarawe. Alikuwa amekilaza kichwa chake juu ya magoti yake. Alikuwa akijaribu kuwaza upya juu ya mustakabari wa operesheni ya mkanda wa siri.
"Hii ni operesheni ya ajabu sana kuwahi kuifanya katika maisha yangu. Nilikodiwa na wakina Martin Hisia kufanya OMS bila kujua kuwa OMS ni Operesheni inayonihusu kwa asilimia mia moja. Niliingizwa katika operesheni ya kusaka kitu kinachonihusu kabisa lakini bila kujua. Kumbe ilikuwa ni operesheni ya kusaka kitu kilichopoteza maisha ya baba yangu mzazi. Operesheni ya kusaka kitu kilichoondoka na maisha ya mama yangu mzazi. Wazazi wangu walikufa kikatili sana kwa sababu ya mkanda tukiousaka katika OMS...Mkanda ule sijui utakuwa na nini ndani yake? Yaani Baba alikubali kufa kinyama namna ile lakini si kuuachia mkanda kwa watu wale wabaya, wenye nia mbaya bila shaka. Hivi mkanda huo utakuwa na nini lakini ndani yake?" Binunu sasa aliinua kichwa chake toka magotini na kuangalia mbele. Alikuwa anaangalia mbele lakini alikuwa haoni chochote kile. Alikuwa mbali sana kimawazo.
"....kwa sasa nina majukumu makuu mawili tu hapa duniani. Na majukumu hayo labda nd'o sababu ya mimi kuendelea kupumua mpaka sasa. Baada ya kuyamaliza majukumu hayo bila shaka nitakuwa nimekamilisha sababu ya mimi kuletwa Duniani. Nitakuwa tayari kufa! Najua ni majukumu mazito sana lakini lazima niyatimize, na hiyo ni kwa ajili ya wazazi wangu waliotokea kuwa wema kwangu kuliko mtu yeyote yule duniani..." Katika macho ya Binunu kulikuwa na majimaji mepesi yanatiririka alipokumbuka juu ya wazazi wake, maji yalishuka kwa kutengeneza michirizi myembamba katika mashavu yake laini.
Binunu alikuwa analia, na alikuwa analia baada ya miaka mingi sana kupita bila kulia. Hakukumbuka lini mara yake ya mwisho kulia, ingawa alikumbuka kwamba yeye alikuwa ameshawaliza watu wengi sana katika maisha yake. Na mtu wa mwisho alitoka kumliza saa mbili zilizopita.
"....nina jukumu zito sana la kulipa kisasi kwa wote waliosababisha vifo vya wazazi wangu wapendwa, pamoja na jukumu hilo zito lakini pia nina jukumu lengine zito, jukumu la kuusaka mkanda wa siri popote pale ulipo, kwa njia yoyote ile lazima niupate ule mkanda. Yaani ni LAZIMA!..." Binunu aliwaza huku neno la mwisho akijikuta amelitamka kwa sauti kubwa. Kitu kibaya sana kwake, hakuwa na kumbukumbu kabisa kama kwa mara ya mwisho mkanda alikuwa nao yeye. Alikumbuka mambo ya zamani sana na kusahau ya hivi karibuni.
Kule visiwani kina Malolo iliwafunukia kwamba walikuwa wamekosea. Walikuwa wameenda kwa mtu asiye sahihi. Lilikuwa ni kosa la kiufundi. Malolo alimpa ishara kwa siri Peter, ishara ile ya siri toka kwa Malolo ilisafiri kwa njia ya siri pia na kufika hadi kwa Malkia. Na wote watatu walielewana. Malkia alimuaga Ayoub akiwa na tabasamu tele usoni mwake. Alikuwa siye Malkia yule aliyemkoromea na kumtisha Mvuvi msindikizaji muda mfupi uliopita. Huyu sasa alikuwa mwanamke mrembo mwenye tabasamu la kirembo sana. Tabasamu lenye kuweza kumpumbaza mwanaume yeyote yule rijali, na kutoa hata asichoambiwa kutoa. Ayoub hakuwa hata na nguvu ya kuagana na watu wale. Ingawa aliliona tabasamu la Malkia lakini hakuwa hata na hisia za kupumbazwa na tabasamu lile ghali. Alibaki mdomo wazi huku akiwatazama tu wageni wake. Wale jamaa hawakujari. Walianza kuondoka huku Ayoub na Mvuvi msindikizaji wakiingalia migongo ya wababe wale watatu hadi ilipopotea katika upeo wa macho yao.
Ilikuwa ni safari kuelekea Kisarawe.
Laiti wangejua walichokuwa wanaenda kukutana nacho?
Ayoub na yule mvuvi msindikizaji sasa walibaki wanatazamana wenyewe, wakiwa hawaamini kabisa kama wamebaki salama, hawakuwa wanaelewa lengo la watu wale kuwaacha. Ulikuwa ni kama mchezo wa kuigiza wakina Steven Marashi na Ruby. Lakini ukweli ni kwamba huu haukuwa mchezo wa kuigiza. Ulikuwa ni mchezo wa kweli, wale majamaa waliondoka huku wakiwa hawajawagusa hata kucha zao wavuvi wale wawili!
Kisarawe..saa 05:08 P.M
Wakina Malkia waliwasili katika mji wa Kisarawe mida ya saa kumi na moja jioni. Walikuwa wamerudi tena katika maficho yao ya muda mfupi baada ya kukikosa walichokifata huko Pemba. Malolo alikuwa ndiye katangulia mbele wakati wanaingia ndani, mle sebuleni. Nyuma yake alikuwa anafatiwa na Peter na wa mwisho wa msafara ule wa watu watatu alikuwa Malkia, mwanamke wa kipemba hatari sana!
Alipofika tu ndani ya sebule Malolo alihisi harufu ya kifo! Harufu ya kifo cha binadamu. Haikuwa shida hata kidogo kwa Malolo kujua kwamba mle ndani kulikuwa na mwili wa binadamu, na ulikuwa unatoa harufu ya kifo. Malolo alikuwa amecheza michezo hatari mingi sana, na kukutana na harufu za vifo mara nyingi sana.
"Bloody bastard.." Malolo alisema kwa sauti ndogo sana huku kwa haraka akiitoa bastola yake kiunoni ...mwanaume alikuwa tayari kwa lolote.
Tayari kuuwa!
Tayari kufa!
Ingekuwa mimi au wewe tungerudi nyuma tena kwa hofu kubwa sana, lakini Malolo hakuwa mimi au wewe, yeye alisonga mbele akiwa makini zaidi huku mdomo wa bastola yake ukiwa umetangulia mbele, tayari kwa kuitungua hatari yoyote ile mbele yake.
Peter na Malkia walisikia sauti ya Malolo ingawa ilisemwa kwa sauti ya chini sana, pia walikiona kitendo kilichofanywa na Malolo. Moja kwa moja wakajua mambo si salama ndani ya nyumba ile, mambo si shwari maskani mwao. Nao wakatoa bastola zao viunoni. Wakati Malkia alitoa bastola moja, aliyoishika imara kwa mkono wa kulia. Peter alitoa bastola mbili toka kila upande wa kiuno chake, mikono yake yote miwili sasa ilishika bastola. Peter alikuwa anangalia kushoto na kulia kila baada ya sekunde moja, sekunde hii akiangalia kushoto, sekunde inayofuata basi aliangalia kulia. Alikuwa anapiga hatua kila baada ya kuridhika kuwa kuna usalama pande zote mbili, hatua ambayo iliruhusu na Malkia nae apige hatua lakini kwa aina tofauti. Yaani Ilipendeza sana kuwangalia. Malkia yeye alikuwa amegeuka nyuma, akiiangalia hatari yoyote itokayo nyuma yao, alikuwa anarudi kinyumenyume lakini kwa tahadhari na umakini mkubwa sana. Huku kupiga kwake hatua kulifuata baada ya hatua ya Peter, ambaye nae aliruhusiwa na Malolo. Kila mmoja alikuwa anamlinda mwenzake huku akiwa anamsaka adui. Kwa mwendo wa kunyata na kwa 'style' ile ya aina yake walifika hadi sebuleni kabisa.
Malolo ndiye alikuwa wa kwanza kumuona, alikutana uso kwa uso na uso wa Chifu huku mwili wake ukiwa umelala hovyo sakafuni karibu na meza ya runinga. Malkia alikuwa wa mwisho katika msafara ule na kumbuka kuwa alikuwa amegeuka nyuma, lakini cha kushangaza na kustaajabisha alikuwa ndiye wa kwanza kufika katika mwili usio wa uhai wa Chifu pale sakafuni.
"Chifuuuuuu" Malkia aliita kwa nguvu huku akiutikisa mwili ule lakini Chifu hakuitika. Ataitika vipi wakati hakuwa katika ulimwengu huu? Wale wanaume wawili hawakuzubaa. Walikuwa wanatanguliza bastola zao kabla ya kugeuka kila upande wakiohisi adui anaweza kutokea, vidole vyao vya shahada vikiwa katika triga tayari kwa kuifyatua hatari. Ndani ya mioyo wao walikuwa na uchungu mkubwa sana, walikuwa na hasira kali sana, walikuwa na huzuni kuu. Lakini hawakutaka kuendeshwa na hisia kama Malkia. Ilibidi wazidhibiti hisia zao ili nao wasiingie katika mikono ya adui. Ukweli ni kwamba ilikuwa inawauma sana maana kumkuta Chifu katika hali ile ilikuwa ni habari mbaya sana kwao.
"Chifu ameuwawa! Chifu, Chifuuu, nakuomba please usife Chifu, usife mpaka nitakapokuletea mkanda niliokuahidiiiiiiii....." Malkia alithubutu kusema kwa sauti yenye majonzi makuu, huku aliutikisa kwa nguvu mwili wa baridi tena uliokuwa mtupu wa Chifu. Ukimya ulikuwepo pale sebuleni uliharibiwa vibaya sana na kelele za majonzi za sauti ya Malkia.
"Shiiiiiiiiii!" Malolo alimnyamazisha Malkia huku akiwa ameweka kidole chake cha shahada cha mkono wa kushoto katikati ya mdomo wake.
"Ni hatari sana hiyo" Peter alisema kwa sauti ndogo sana. Malkia alinyamaza kulia kwa sauti, lakini hakunyamaza kulia kwa kutiririsha machozi, machozi yalimmiminika kama mtoto mdogo. Kwa mara nyingine tena Binunu alikuwa analiza mtu siku ile. Jamaa walimwangalia mwanamke yule aliyekuwa anapitia katika machungu makubwa sana lakini hakuna aliyeenda kumbembeleza, wao wenyewe walikuwa hawaijua hatma ya usalama wao mle ndani.
"Siku nitakayokufa hakika mtazikuta maiti mbili, yangu na ya huyo atakayeniuwa, nachukia sana kifo lazima nipambane sana ili kukiepuka...Chifu hawezi kufa kizembe hata siku moja!" Chifu alishawahi kuwaambia maneno hayo wakina Malolo, na Peter aliyakumbuka pale sebuleni. Na ndipo alipopata cha kufanya, alimpa ishara Malolo, na aliielewa.
Waliitekeleza.
Vijana wale wawili walianza kuingia ndani ya nyumba huku wakimuacha Malkia pale sebuleni akiwa ameulalia mwili wa Chifu. Hakika lile lilikuwa PIGO MUJA'RABU kwa Malkia. Walienda kukagua sehemu moja baada ya nyingine ili kuona kama kuna maadui ndani au labda maiti ya pili kama alivyowaahidi Chifu juu ya siku atakayokufa.
Baada ya nusu saa jamaa walikutana tena sebuleni. Wakiwa idadi ileile, watatu na mwili wa Chifu ukiwa umelala bado sakafuni ukiwa hauna uhai...huku Malkia akiwa pembeni ya mwili ule. Akiwa amekaa kitako, amenyoosha miguu yake, kaupakata ule mdoli uliokuwa unamilikiwa na Binunu, Malkia alikiwa ametoa macho akiwa anashangaa kitu kisichoonekana. Alikuwa anaongea maneno yasiyoeleweka. Amini, usiamini.....Akili ya Malkia haikuweza kustahamili uzito wa kifo cha mtu wa karibu yake sana, mtu aliyekuwa analala nae kitanda kimoja, shuka moja. Wakishirikiana kila wanachopaswa kushirikiana wanandoa. Ama kweli mapenzi ni kitu cha ajabu sana. Malkia alikuwa amestahamili maumivu mengi sana katika maisha yake, maumivu ya kuumiza sana lakini leo hii alishindwa kabisa kuvumilia maumivu ya mapenzi. Mume anauma wewe!
Ugonjwa kama aliokuwa nao Binunu leo hii ulimrudia yeye, na mdoli aupendao Binunu leo hii alikuwa anaupenda yeye. 'What goes around, comes around'
Daah! Malkia alikuwa amechanganyikiwa katika siku ileile ambayo Binunu alikuwa amerejewa na akili pamoja na kumbukumbu zake za maisha yake ya nyuma.
MWISHO WA MKANDA WA SIRI SEASON 1.