mpasta
JF-Expert Member
- Jan 17, 2011
- 917
- 1,997
Mwandishi: Badi.M.Bao
Baruapepe:badi.bao11@gmail.com
Riwaya zake mtaani: "CABO-DELGADO' na "MSAKO MWEHU"
SEHEMU-01
SURA YA KWANZA.
Ilikuwa ni adhuhuri mwanana, ikichagizwa na upepo wenye kasi ya wastani ukivuma katika maeneo ya Posta Jijini Dar es Salaam. Kila mtu alikuwa ametingwa na mihangaiko yake ya kimaisha, watu wanakimbizana huku na kule ilimradi waweze kukamilisha makusudio na malengo yao ya siku ya kimaisha waliyojiwekea.
Wakati huo huo kulikuwa na kadamnasi ya watu walikuwa wamejikusanya wamejaa pomoni ndani ya kanisa la Mtakatifu Joseph 'St Joseph Cathedral church'. Hilo ni kanisa lililopo katika Mkoa wa Dar es Salaam, Wilaya ya Ilala. Kanisa hilo la kihistoria na la kuvutia kimandhari yake lipo mkabala na 'Sokoine drive' likiangalia 'Waterfront' karibu na geti la boti zinazoelekea Zanzibar.
Mkusanyiko wa umati huo wa watu ndani ya nyumba ya ibada kwa Wakristo wa Madhehebu ya Katoliki, ulikuwa na sababu yake maalumu. Haikuwa mkusanyiko wa bure bilashi tu wa kupiga porojo na soga siku iende. Motakaa kochokocho za aghali zilikuwa zimeegeshwa nje ya kanisa, kuashiria ni tukio la linalowahusu watu walalaheri.
Walikuja kushuhudia ndoa ya kifahari kati ya Dr. Trezguet na Bi Deborah iliyotarajiwa kufungwa muda mchache ujao ndani ya kanisa hilo. Wanandoa hao tarajaji waliwasili kanisani hapo kwa ngoma na matarumbeta hadi kanisani hapo huku sherehe kabambe ya kukata na shoka ikipangwa kuchukua nafasi yake ndani ya Hoteli ya kifahari ya 'Kempisky'. Wageni maarufu na mashuhuri wa ndani na nje ya nchi, kuanzia wanamichezo, wanamuziki, na wanasiasa nao walikuja kushuhudia ndoa hiyo kwa macho yao, hasa ukichukulia ukaribu wao na Dr.Trezguet ambaye kwa umaarufu wake hamna mtu ambaye alikuwa hamfahamu au hajapata kumsikia katika nchi hii ya Tanzania.
Umaarufu wake ulitokana na kuendesha vipindi vingi vya redio na televisheni akizungumzia masuala ya Afya na Saikolojia, huku akimiliki hospitali kubwa ya kisasa Jijini Dar es Salaam. Tetesi mitaani zilikuwa zinavuma kuwa sherehe yake hiyo ya ndoa ilitarajiwa kuteketeza zaidi ya nusu bilioni na ushee huku vyombo vya habari karibia vyote vikubwa vikiwa vimetingwa na harakati za kuhabarisha watazamaji na wasikilizaji hao hatua kwa hatua ya ndoa hiyo.
Taratibu zote za ndoa hiyo kufungwa zilishakamilika, misa ya ndoa hiyo ilikaribia kukamilika huku wakiwa wameshasimamishwa mbele ya Padre pale madhabahuni tayari kwa kuunganishwa na kuwa mwili mmoja.
Huo ulikuwa ndio wakati mgumu kuliko wakati wowote katika mioyo ya wana ndoa hao. Hapo ndio sehemu ambayo kama ni kitanzi mtu anajivika mwenyewe shingoni kujinyonga, haulazimishwi na mtu wala kushikiwa mtutu wa bunduki, unatakiwa ukubali agano hilo kwa hiari yako. Dr.Trez akiwa ameulamba vazi la suti nyeusi, akionekana yu nadhifu na maridadi kabisa uso wake muda wote ulikuwa na bashasha fokofoko kuonyesha furaha aliyonayo ya kumpata mwenza, mshirika wake wa kweli katika maisha, katika shida na raha, katika mvua na jua. Maisha ya ndoa ambayo yana pande mbili kama sarafu, pande moja ni tamu kama asali na ingine ni chungu kama shubiri.
Kanisa zima sasa muda huo lilikuwa lipo kimya, kama limemwagiwa maji ya baridi vile, kila mtu anawatazama wao tu wapendanao 'Love Birds' wanaosubiri kufunga ahadi takatifu. Hadhira ile mahadhuru kanisani mule kila mmoja kichwani mwake alikuwa ana mawazo yake, wapo waliokuwa wanajiuliza na kumlaumu na kumsengenya kimoyomoyo kuwa iweje mtu maarufu na tabaka a'ali kama Dr.Trez akaoe mwanamke ambaye sio wa hadhi yake, ambaye hata sio nyota, hajulikani vizuri na kuwaacha wasichana mastaa kibao ambao anaendana nao kihadhi.
Wengine wakawa wanampongeza kwa kupiga makofi ya pongezi mioyoni mwao kwa uamuzi wa kishujaa aliouchukua wa kuamua kuchukua jiko ambalo sio maarufu hasa wakiwa na mifano hai jinsi ndoa za mastaa kibao zinavyoshindwa kudumu. Hivyo wakawa wanamtakia kheri na fanaka katika safari yake ya maisha ya ndoa aliyoichagua kuianza.
Mawazo ya Dr.Trez pale mbele ya Padri mfungisha ndoa yakaanza kuvuka milima na mabonde, yanaisasambua ndoa kwa ujumla, akawa kama vile anasubiria maneno ya Padri atakapokamilisha ndoa kwa kutamka "kwenye ndoa za kanisani hakuna talaka hivyo kwa niaba ya Mungu Baba naifunga ndoa hii kwa kuwaunganisha kuwa mwili mmoja mpaka kifo kitakapo watenganisha na hapa chini ya jua hakuna mtu yoyote atakayekuwa na uwezo wa kuivunja ndoa hii hata mimi niliyeifunga sina mamlaka ya kuivunja nimeifunga na funguo nimeshazirejesha kwa Mungu Baba yeye ndiye pekee mwenye uwezo wa kuivunja kwa mmoja wenu kufa alichounganisha mungu mwanadamu asikitenganishe-Ameen".
Kitambo chote walichokuwa wamesimamishwa maharusi hao, Bi.Harusi Debora macho yake yalikuwa yanabubujikwa na mvua ya machozi yaliyoanza kutotesha shela lake alilojifunika kichwani mwake. Waliomshuhudia wakachukulia poa wakidhania ni machozi ya furaha ya kuolewa, hasa ukichukulia katika zama zetu hizi, wasichana wanadoda majumbani mwa wazazi wao kwa kukosa waoaji. Wanaume waonjaji ni wengi kuliko waoaji, hivyo watu kilio kile cha Debora wakakichukulia ni kilio cha furaha ya ndoa. Katu hawakung'amua kuwa kilikuwa ni kilio cha shari chenye uchuro ndani yake.
Swali kutoka kwa Padri lililotupwa kwa Dr. Trez la kuulizwa kama yupo tayari kuishi na Bi. Debora kwa shida na raha, katika uzima na ugonjwa, utajiri na umaskini katika maisha yake yote, lilijibiwa kwa haraka sana swali hilo na Dr Trez akiwa na furaha sheshe. Padri akamgeuzia kibao Bi Debora akamgeukia na kumtupia swali lile lile alilomuuliza mpenzi wake. Swali ambalo kama atalijibu vyema Padri ndio atapata fursa ya kuipasisha ndoa hiyo na kuendelea na sehemu ya pili ya misa inayohusiana na ekaristi takatifu.
Roho za wahudhuriaji zikawa zipo juu juu zinagonga kama saa mbovu, matarajio yao yakiwa ni jibu la ndio ili sherehe ya ndoa ya kifahari iliyopangwa iweze kufana. Macho yote yakakodoka kodo, yakamuelekea Bi.Debora alipoanza kuulizwa na Padri yule ambaye pembezoni yake kulikuwa na bakuli la pete za maharusi ambazo walitarajia kuvishana mara baada ya ndoa kupitishwa.
"Sipo tayari kuolewa na Dr.Trezguet.....I'm sorry Aaah...Aaah...yuuleee....!" Bi. Debora alishindwa kumalizia maelezo yake akiwa amemnyooshea kidole Bibi mmoja aliyekuwa amekaa benchi la mbele kabisa. Bi.Debora alijikuta anaanguka chini kwa kishindo na kuanza kurusharusha miguu kushoto na kulia, akifafaruka, anapiga kelele kama mwehu aliyevamiwa na mapepo anazungumza mambo yasiyoeleweka mpaka akapoteza fahamu.
Zogo na vurumai mtindo mmoja likaibuka mule kanisani kila mmoja akiingilia upande wake. Hamkani mambo si shwari tena, Debora kalitia tembo maji, mambo yamegeuka kuwa segemnege. Kikosi wa watoa huduma ya kwanza ambao nao walikuwa na mualiko rasmi wakafanya juhudi za kumtoa Debora kanisani pale madhabahuni alipokula mwereka na kumkimbiza katika Hospitali binafsi ya karibu ya 'Agakhan' ili kujaribu kuokoa uhai wake.
Kila mtu baada ya tukio hilo akaanza kuropoka jambo lake, vizabizabina ukawa ndio uwanja wao huru wa kujimwayamwaya kimaneno. Wao waliovumisha kuwa Debora karushiwa jini toka Pemba na mahasidi wake waliokuwa hawataki hata kuisikia ndoa hiyo. Hivyo wakapanga mipango ya kukomesha kwa kutumia njia za kimazingara.
Wapo waliozusha kuwa Debora kagundua usiku wa kuamkia siku ya ndoa yake kuwa Dr.Trezguet ana mke na watoto wa kizungu huko ng'ambo alipokuwa anadurusu na kuishu, hivyo kakasirika kutokana na kufichwa ukweli.
Wapo 'vidinga popo' na 'habari kauzwa' waliofika mbali zaidi na hata kumvunjia heshima mama mzazi wa Dr.Trezguet. Walileta madai kuwa huyo mama ni mwanga, mchawi wa kutupwa hataki kabisa mtoto wake aoe anahofia kushindwa kuzipochoa mali za mtoto wake vizuri kama akikaliwa kichwani na huyo mkewe. Wakaenda mbali zaidi kuthibitisha madai yao kuwa ndio maana Bi.Debora baada ya kuipiga chini ndoa alinyoosha kidole cha lawama kwa mama mzazi wa Dr.Trez. Ili mradi midomo yao, na hawailipii kodi yoyote walikuwa na khiyari ya kuzungumza tani yao, vyovyote watakavyo lakini ukweli halisi wa kwanini kaipanjua ndoa hadharani alikuwa anaujua yeye mwenyewe Bi.Debora na moyo wake.
Matukio hayo yote yanavyotokea Dr.Trezguet alikuwa ameganda kama sanamu haamini kilichotokea muda mfupi kama kweli Debora, chaguo la moyo wake, ambaye hawajawahi hata kukwaruzana hata siku moja tokea waanze mahusiano yao miaka mitatu iliyopita kuwa kweli amempiga kibuti mbele ya umati wa watu. Alikuwa anawaza aibu gani isiyomithilika mbele ya umati ule na Watanzania kwa ujumla, atauweka wapi uso wake.
Machozi yalikuwa yanamtiririka bila breki, huku anajitahidi kuyafuta kwa hanchifu yake. Waandishi wetu wa habari kama unavyowafahamu kwa kupenda habari tata, wakamfuata kumhoji kutaka kujua kulikoni mpaka anamwagwa kirahisi rahisi tena mbele ya madhabahu takatifu.
Aliwapa jibu moja tu, "She is suffering from Post-Traumatic Stress Disorder (PTSD), I will fight for my LOVE" huku akawa anaondolewa kwa nguvu na wapambe wake akiwa mnyonge kutoka pale madhabahuni na kumuingiza kwenye gari lake na kutokomea zake eneo lile.
Baadhi ya wadadisi wa mambo wakapatwa na matumaini huenda ni ugonjwa huo wa "PTSD" ndio umemfanya Debora aropoke jibu baya kuwa hataki ndoa, hivyo huenda akipona atakubali kuolewa tena. Huku wakishadidia nadharia yao kwa tafakari jadidi ya kuwa kama kweli Deborah angekuwa hamtaki Dr Trezguet tangu mwanzo asingekubali kumtia hasara na kumuaibisha hadharani hivyo mbele ya umati wa watu.
Wale wapenda manyamnyam na mapochopocho ya harusi hawakutaka kulaza damu wakayafungia safari mpaka 'Kempisky Hotel' kwenda kujisosomola nayo. Wakamalizia hasira za Debora kutibua sherehe kwenye maakuli hayo. Ila chakula kingi bado kilikosa walaji hasa kutokana na wahudhuriaji wa sherehe hiyo walikuwa ni walalaheri, wale nafasi zao kimaisha. Uhalisia wa mambo ni kuwa hapo kanisani ndio ukawa mwisho wa hadithi tamu ya penzi la kusisimua la Dr Trezguet na Bi. Debora lililodumu kwenye uchumba kwa zaidi ya miaka 3.
ITAENDELEA