RIWAYA:Malaika au shetani

RIWAYA:Malaika au shetani

IAmShedeOne

JF-Expert Member
Joined
Jul 2, 2015
Posts
202
Reaction score
385
MALAIKA? Au SHETANI? (01)
Kama kawaida, mwanga unapoanza kumezwa na giza la magharibi, shughuli za utafutaji riziki kwa wengi hukoma hadi siku inayofuata. Jioni hiyo, nawe ulifunga biashara yako baada ya kupitia hesabu zako. Taabu na adha za usafiri, zisababishwazo na foleni ndefu, zinakulazimu kutembe kwa miguu badala ya kupanda daladala, pengine sababu nyingine ni ukaribu wa eneo unaloishi kwa kutokea hapo Kariakoo. Unaianza safari; mguu mosi, mguu pili.
Ukiwa maeneo ya Ilala boma; takribani nusu ya safari yako, ukamwona bwana mmoja amebarizi pembezoni mwa barabara, usawa uliokuwa ukiambaa nao katika njia yako. Watu ni wengi barabarani, kila mmoja na hamsini zake, kwa hivi, hapakauwa na sababu ya msingi ya kukushitua kumwona mtu yule.Kwa jijini Dar es Salaam, viumbe wachafu, waliochakaa na kusawajika miili yao, kutokana na sulba za kimaisha ni wengi mno, kuliko hata huyo bwana uliyemwona. Baada ya kumtazama kwa muda mrefu kadiri ulivyokuwa ukimsogelea, macho yako yakapeleka taarifa haraka kwenye ubongo kwamba mtu yule ulipata kumwona mahala. Wapi? Haukumbuki!
Ingawa hukumkumbuka, lakini kwa namna sura yake inavyokujia, yamkini ulipata kumwona kabla ya hapo. Na, huenda ulimfahamu–lakini ulimfahamu kivipi? Hilo lilikuwa nje ya milki ya kumbukumbu zako.
Ulipomkaribia, mwonekano wake ulidhihirisha dhiki na adha za kimaisha alizonazo, hivyo, kutambulika kama Ombaomba wengine warandao huku na kule kuomba pesa. Na, kwa namna ya usimamaji wake barabarani wakati ukimsogelea, ilikufunulia fikara nyingine, kwamba baada ya kukuona ukielekea usawa wake, alikuwa akikusubiri umfikie akuombe pesa.
Mbali ya kuwa ombaomba, bwana yule alitia shaka kumtazama mara mbili: rundo la nywele chafu lilijisokota kichwani mwake, uchakavu na uchafu wa nguo alizovaa, ulifanana na ngozi yake ya mwili. Mkononi alikuwa ameshika fimbo aliyoifanya kama mhimili wake wa kusimama. Ingawaje tayari magharibi ilikwisha kuingia, na kwamba joto la mchana kutwa lilimezwa na upepo na vivuli, lakini ombaomba huyo alikuwa akitiririkwa jasho jeusi, linalofumkia ukingoni mwa kichwa chake na kutengeneza mifereji myeusi pembezoni mwa mashavu yake. Juu ya hayo, sura aliukunja kiasi cha kutengeneza mfano wa matuta katika paji la uso wake, yawezayo kumhofisha ye yote ambaye angewajihiana naye.
Kwa mwonekano ule wenye kukirihisha nafsi na kuogopesha macho, ukajionea vema umpishie mbali kwa kuambaa sanjari na lami ya barabarani ili kujitanibu wowote uwezao kusababishwa naye. Wa ima, ulipoona tayari umemfikia, ukajibaraguza kutoa simu, ambayo wala haikuwa ikiita, ukaiweka sikioni kama uliyepigiwa. Yote hiyo ukikwepa asikusemeshe wala kukuomba pesa. Cha ajabu, ombaomba uliyemhofia, hakukusemesha wala kukuomba pesa, zaidi aliendelea tu kukukazia macho hadi ulipompita na kumwacha nyuma.
Ili usionekane umeiweka simu sikioni kama toi, ukajifanya kuongea. "Eeh hallow!"
Bila kutegemea, ukaisikia sauti ikikujibu toka ndani ya simu: "Hallow nini wewe? Acha kuzuga–unahangaika utafikiri umelazimishwa kutoa msaada!"
Ukapigwa na butwaa huku ubaridi wa hofu ukikutambaa mwili mzima. Kwakuwa ni kitu ambacho hukukitegemea, haraka ukaitoa simu sikioni, ukajaribu kuiangalia endapo kama iko namba iliyojipiga kwa kibahati mbaya ... Hakuna!
Simu haikupigwa wala kujipiga. Sasa kumbe nini?
Katika kutafuta ithibati ya kadhia hiyo, ukajikuta umeirejesha sikioni kuona kama ulichokisikia ni sawa au mawenge tu. Kama mchezo wa kuigiza, ile kuiweka tu simu sikioni, sauti ile ikaendelea, "Utagongwa na magari bure kwa upuuzi wako, kutoa ni moyo wala si utajiri, hujaombwa wala hujalazimishwa..."
Kabla sauti haijaendelea, kwa wahka na taharuki ukaitoa tena simu sikioni. Safari hii badala ya kuiangalia tena kama ulivyofanya awali, ukageuka nyuma kumwangalia yule ombaomba, kwa namna ulivyomtilia mashaka tangu ulipomwona, hisia zako zilikutuma kwamba huenda maajabu yale yanatoka kwake. Katika hali usiyoitegemea–a
kumwona tena–Alitoweka!
Ilikuwa ni hatua chache tu ulizopiga baada ya kumpita, sasa kutoweka kwake hata asionekane akitembea, ikawa ni kitendawili kilichokosa mteguaji. Ikawa kama uliye ndotoni, kwa maana yadhihirikayo mbele yako ni muhali kutokea katika uhalisia. Katika kuchanganyikiwa kwako, bila kujitambua ukapelekaa tena simu sikioni ukiwa kama haujaamini. Sauti ileile ilikupokea, "Huna lolote–roho mbaya tu inakusumbua. vijihela vyenyewe vya mbogamboga tu hivyo, sijui ungekuwa na pesa haswa ingekuwaje!"
Ulitamani kukimbia, miguu haikuwa na nguvu; ukatamani machozi yaakawa mbali na macho; katamani kupiga mayowe, koromea likaigomea sauti kutoka; katamani kuitupa simu, mikono ikagoma kutii maamuzi yako. Hofu ilikuvaa kuanzia kwenye kucha ya kidole cha mguu hadi kwenye unywele wa utosi.
“Au simu imeingiliwa na kirusi!” ukabaki kujisemea peke yako kama mwendawazimu.
Kila ujasiri uliotaka kujipatia haukuwa na chembe ya tija. Safari hii ulipotaka tena kuiweka simu sikioni ili umuulize huyo anayeongea ni nani, mikono yako ikaanza kutetemeka, hofu kuu ikiushambulia moyo wako. Baada ya mpambano baina ya dhamira na hisia, ukajikaza na kuipeleka sikioni. Simu ikawa kimya, hapana sauti tena.
“Kipi kinanitokea?”
Kwa kukosa majibu ya maswali yako wala ufafanuzi wa hisia zako, kama uliyefungwa mota miguuni, ukajikuta ukiondoka kwa kasi eneo lile huku ukigeuka huku na kule kuona kama yuko anayekufuatilia.
Baada ya takribani dakika thelathini, hatimaye ukawasili mahala unapoishi, Buguruni Malapa. Kabla hujaingia ndani, ukaona namna pekee ya kutafuta ufumbuzi na tiba ya msongo wa mawazo unaongeza kasi kichwani, ni kutafuta ushauri kwa kuwasimulia sahibu zako. Ukajongea hadi kijiweni kwa vijana wenyeji wa pale.
Kama kawaida ya vijiwe vya vijana; ulipowasalimu, wapo walioitika kwa shangwe, wapo walioitikia chini ya mwamba wa pua, na wapo ambao hawakuchukua taabu ya kuitikia salamu yako. Baada ya michapo uliyokuta ikizungumzwa hapo kujiweni kuisha, ndipo nawe ukapenyeza mkasa wako. Kufikia tamati ya mkasa wako, yakapatikana makundi mawili; wapo waliocheka, wakakudhihaki na kukupuuza; na wapo waliokuonea huruma wakiamini kwamba Mbu wamekusababishia Malaria kali kukupanda kichwani na kukushauri ufike kituo cha afya.
Makundi yote mawili, hayakuonesha msaada wala matumaini kwa kadhia yako. Kwa hivyo, ukaondoka kama ulivyofika. Huko nyuma ukaacha gumzo na mjadala. Kukosa kwako msaada japo wa nasaha tu, kukakupelekea kwenda kulala ukiwa umevurugikiwa kichwani.
Pengine kukosa ndugu jijini Dar es Salaam, ndiko kulikokufanya ukose pa kukimbilia. Lakini jamaa wa nyumbani kwenu, Bukoba, waishio Dar es Salaam ni wengi, na wanao umoja wa kufaana katika shida na raha, walaki siku zote umekuwa ukipuuza kujimuika nao–leo utaanzia wapi kuwafuata? Unapiga moyo konde na kukubali kusubiri kadari ya Mola.
Usiku huo, haukupata hata lepe la usingizi, usingizi uliparama kwa sababu ya moyo kuvamiwa na hofu. Taswira ya yule ombaomba ilijirudia kichwani mwako na kuitawanya sumu ya hofu kila kona ya mwili wako. Raha ilikutoka. Baada ya kitambo kirefu, hofu iliyokita moyoni muda mrefu na kuanza kuzoeleka, na taratibu ikaanza kuyeyuka kama theluji juani. Kwa hivi, kumbo la usingizi likakumba.
__________
ILIANZA kama ndoto. La, si ndoto, ni kama Jinamizi, maana hilo ndilo huwakaba watu usingizini kiasi cha kuwafanya washindwe kupiga kelele wala kupumua vizuri.
Naam, hivyo ndivyo ilivyokutokea ukiwa usingizini; ulikabwa, ukatapatapa, ukaishiwa pumzi na kuhangaika mno. Tofauti na ilivyo kwa majinamizi ambayo hukaba kwa muda mfupi, na baada ya usingizi kuparama nayo hutokomea, kwako ilizidi kipimo ukahisi kama kwamba roho inakaribia kuuacha mwili.
Tumezoea kwamba, Jinamizi hukaba usingizini tu, na usingizi ukikutoka, nalo hutoweka. Kama hivyo ndivyo; inakuwaje pale inapotokea Jinamizi likaendelea kukukaba hata baada ya kushituka toka usingizini?
Ndivyo ilivyokutokea siku hiyo, baada ya kudhibitiwa na Jinamizi kwa muda mrefu, hatimaye usingizi ukakuruka kichwani. Cha ajabu, Jinamizi liliendelea kukukaba kiasi cha kukufanya apaparike kama kuku anayechinjwa.
‘Hili sasa siyo jinamizi tena’ uliwaza. Kwa shida na maumivu ukajitahidi kufumbua macho. Kwa ulichokiona, aheri ungeendelea kukabwa kuliko kushuhudia akukabaye.
Fikra za jinamizi zikayeyuka rasmi kichwani mwako baada ya kukutanisha macho yako na yale yaliyoko kwenye sura mbaya isiyo na mvuto, yenye kutisha isiyo na wema, na yenye ghadhabu zisizo mithilika. Ni sura ya yule Ombaomba uliyekutana naye maeneo ya Ilala boma.
Ukiwa hujui kipi cha kufanya kati ya kufumba macho, kupiga kelele au kumtoa mikono yake yenye kucha ndefu na chafu shingoni mwako, Ombaomba yule alipofunua kinywa chake na kucheka kwa sauti ya juu. Kinywa kilikuwa kilichohifadhi meno machafu yaliyotengeneza rangi ya manjano na kuachia mapengo kwenye baadhi ya maeneo, kilikuwa kikitoa reha mbaya, mithili ya mzoga uliooza.
***HAYA SASA, NI MALAIKA AU SHETANI? TUTAENDELEA KESHO PANAPO MAJAALIWA
MTUNZI NI MAUNDU MWINGIZI (Mwanabalagha)
 
MALAIKA? au SHETANI (02)
Ukiwa hujui kipi cha kufanya kati ya kufumba macho, kupiga kelele au kumtoa mikono yake yenye kucha ndefu na chafu shingoni mwako, Ombaomba yule alipofunua kinywa chake na kucheka kwa sauti ya juu.

.
18814377_764910210346937_57611707920685762_n.jpg


Kinywa kilikuwa kilichohifadhi meno machafu yaliyotengeneza rangi ya manjano na kuachia mapengo kwenye baadhi ya maeneo, kilikuwa kikitoa reha mbaya, mithili ya mzoga uliooza.
Muujiza mkubwa ulikuwa kwenye meno yake ya mbele: yalikuwa kama yametengeneza vijitobo katika ncha zake. Na, kutokea kwenye vijitobo hivyo, vijidudu mfano wa funza vilikuwa vikijitokeza na kurudi ndani kadri alivyokuwa akifunua kinywa chake na kukifumba wakati akicheka. Mtu anawezaje kuishi na funza ndani ya matundu ya meno yake?
Kuhamanika kwako na staajabia hali hiyo, kukamfanya Ombaomba azidi kukucheka, japo tazamo la mtu yeyote lisingeliafiki kwamba lile kuitwa cheko. Ni cheko gani lifanyalo sura izidi kuwa mbaya namna ile? Hata anayelia huwa hawi hivyo.
"Si ulijifanya mjanja..?" Ombaomba akadhihaki.
Kwa namna alivyokukaba kooni, usingeweza kutoa sauti ya kumjibu. Wazo likaishia kupita kichwani mwako, ‘Ujanja gani sasa, Kutotoa msaada wa pesa kwa ombaomba?’
Cha ajabu, kama aliyekuwa akikusoma mawazo yako, akakushushua huku amekutolea macho, “Siyo kutokutoa msaada. Hivi, wewe una msaada wa kunipa, au mimi ndo wa kukusaidia wewe?”
Ukiwa unashangaa namna alivyoweza kukisoma kile ulichokiwaza kichwani, akaendelea, “Unakumbuka ulichonitenda? Kiumbe una roho mbaya wewe ya kumnyima nzi kinyesi!”
Ukazidiwa na mshangao. Kwamba inaonekana uliwahi kukorofishana naye, lakini haukumbuki ni wapi na kwa vipi.
"Nakuuliza halafu haujibu eenh?"
Sasa ungemjibu vipi wakati sauti haitoki?
Papo hapo, akiwa amekudhibiti hata usipate upenyo wa kujikukurua, Ombaomba akakusogezea mdomo wake hadi kwenye kiwiko cha mkono wako, kisha akakubandika jino kama sindano. Toka ndani ya jino hilo ambalo muda huo lilikuwa limechoma sehemu ya mkono wako, akawa anatoa kitu kama funza, kilichokuwa kikikuingia mkononi mwako na kukuachia maumivu makali.
‘Arrghhhh!’ kila ulipojaribu kupiga kelele, uliishia kukoroma tu kwa namna alivyokukaba koo. Baada ya kuhakikisha amekwisha kuingizia kijidudu hicho mwilini mwako kupitia mkononi, aliutoa mdomo wake na kukwambia, "Mpaka hapo tutakapokutana tena–usiku mwema."
Akakuachia na kutoweka. Ukabaki ukikohoa mfululizo hali udenda ukikutoka. Kwa taabu na maumivu, ukajiinua na kuketi kitandani huku mikono yako ingali imeshika sehemu ya shingoni mwako. Ukajipigapiga kichwani ili kuona kama uko ndotoni au La! Ukamaizi kwamba haikuwa ndoto, bali ni kweli yametokea. Maumivu yaliyokuwa yakipungua taratibu mkononi, yakakufanya ujitazame kwa uangalifu mahala ulipoumwa jino.
Ni bora hata usingejitazama kwa ulichokiona!
Macho yako yakashuhudia kitu mithili ya funza, kikimalizikia kuingia mkononi mwako kupitia tundu la sehemu ile uliyobandikwa jino. Na, kilipomalizika tu, tundu likajiziba na mwili ukarudia kama mwanzo tu – hakuna tundu–hakuna jeraha.
Kwa kihoro kikubwa, ukaruka toka kitandani na kusimama, huku ukitamani kuukimbia mkono wako mwenyewe. Nani angetulia tu hali ameona kitu kikimuingia mkononi mwake?
Mungu wangu – nimemkosea nini yule kiumbe? Ukajaribu kuusugua mkono wako, mahala pale palikoingiwa na mdudu funza; hakuna kilichobadilika. Kwa woga na hamaniko, ukaukimbilia mlango wa chumba chako–ukaufungua na kutoka. Huko nje nako, giza la kutisha likakupokea; mashaka na woga vilivyokutoa nje, vikakurudisha ndani. Ukaendelea kuhatahata na chumba; ndani uchungu, nje ukakasi. Ukiwa umesimama katikati ya chumba, mara ukasikia adhana za alfajiri–kumepa
mbazuka.
Mapambazuko hayo ndiyo yakakupa ujasiri wa kutoka tena nje na kuketi kibarazani. Kila ulichowaza na kuwazua, hakikukufikisha katika uteguzi wa kitendawili kilichokufika. Nani utakayemfikia akakuamini? Kama mwanzo tu, ulipowasimulia marafiki zako kuhusu sauti ya ajabu katika simu yako, ulkaonekana kuchanganyikiwa. Je, hili la kutokewa na mtu uliyepata kumwona hapo kabla, akakukaba koo, akakukaripia, na kama haitoshi, akakubandika jino mkononi na kukuingizia kijidudu kilichosambaza maumivu mwili mzima–utaaminika? Kibaya zaidi, kijitundu kilichobaki baada ya kijidudu kukuingia, kimejiziba chenyewe. Yuko atakayemakinika na simulizi yako?
Baada ya kuzama kwenye tafakuri ya kina, ukakata shauri la kutomwambia mtu yeyote juu ya kilichokutokea, japo moyo uliendelea kukukereketa kuuweka wazi mkasa huo kwa watu. Wapangaji wenziyo na majirani waliamka na kukukuta umebarizi hapo nje ukiwa umebarizi. Kama desturi, mkasabahiana kwa taadhima huku kila mmoja akiendelea na pilika zake asubuhi. Nuru ya jua na pitapita ya watu, vinakufariji na kukupunguzia hofu. Ukarejea ndani, na baada ya kujinadhifu mwili ukatoka kama ada, kwenda kutarazaki.
Siku hiyo, shughulini ulipwaya; hali ya furaha, amani na kujiamini vikatoweka kabisa kiasi cha kukuondolea ufanisi wako. Pamoja na kujitahidi kuzidhibiti hisia mbaya, lakini kila mara kumbukumbu zilipokurejesha usiku wa siku iliyopita, moyo ulikulipuka na kukufanya usinyae kwa simanzi. Haukuwa mkasa wa kawaida kutokea kwa kijana wa hirimu yako.
Hali ilikuwa hivyo hadi jioni ikaingia, muda wa kurejea nyumbani kupumzika ukawadia. Kishingo upande, ukafunga biashara na kuanza kuondoka. Njia ya kutoa Kariakoo kwenda Buguruni unakoishi, ni ileile ipatayo Ilala Boma ambapo ulipomwona yule Ombaomba. Pamoja na woga kukuvaa, walakini, haukuwa na namna nyingine ya kufanya, kwa sababu njia nyingine mbali ya hiyo ni ya mzunguko mkubwa mno. Ikakubidi ujikaze kisabuni na kuazimu kupita njia hiyo. Kama kawaida ya foleni ya jiji, kwa nyakati kama hizo za jioni, ikakubidi kama ilivyo kawaida yako, utembee kwa miguu. Ulitembea salama salmini, hadi ulipoanza kuyakaribia maeneo yale uliyomwona yule ombaomba na mara ikakutokea sauti ya ajabu kwenye simu, ndimo damu inakuchemka kwa mashaka, mwili ukakusisimka kwa hofu, nywele za kichwani zikajizoa kwa woga, vinyweleo vinajitutumua juu ya ngozi kwa simanzi.
Taswira ya Ombaomba akiwa amekukaba koo, huku jasho chafu likimtiririka ikaanza kukuijia. Ukajikuta ukifumba macho kwa mzizimo wa hisia mbaya kichwani. Kitendo cha kufumba kwako macho kwa hisia za hofu huku ukitembea barabarani, almanusura kikusababishie ajali.
“We bwege acha kulala barabarani!” Dereva bodaboda aliyekosa kukugonga, akakukaripia kwa maneno ya unyambi na ufidhuli.
Maneno ya dereva bodaboda huyo ndiyo yaliyokutanabahisha na kukurejesha katika umakini wa barabarani. Mfadhaiko ukakushambulia baada ya kumaizi kwamba wapiti njia wengi walibaki kukushangaa wewe. Hayo yote yanatokea ikiwa ni kituo kimoja tu kimesalia kufika mahala ulipotokewa na yule Ombaomba siku moja nyuma.
Kwanini nipate taabu yote hii!. Ukawaza huku ukitafakari hatua ya kuchukua ili kumkwepa Ombaomba.
Katika kutafuta suluhu ya mambo, ukaamua kupanda gari badala ya kupita kwa miguu eneo lile lililokuachia kumbukumbu mbaya kichwani. Bila ajizi, ukachagua moja kati ya daladala zielekeazo maeneo ya Gongo la mboto, kupitia barabara hiyo ya uhuru, ukapanda. Dalala hiyo nayo inakwenda kwa mwendo wa kinyonga, taratibu mithili ya chatu aliyevimbiwa - foleni imeuma kwelikweli. Kwa mwendo huo, inakuchukuni takribani dakika ishirini na tano, kulifikia eneo lile aliposimama Ombaomba siku iliyopita. Kumfikiria ombaomba kukakufanya uikumbuke tena ile kadhia iliyokutokea usiku; taswira ya kinywa kichafu cha ombaomba akiwa amekukaba kooni inakuijia; ile minyoo inachungulia kupitia ncha za meno yake machafu. Kwa hofu na msisimko ukajikuta ukifumba macho na kuugulia maumivu ya hisia.
Katika hali hiyo ya hisia. Ukahisi kama Ombaomba amekukamata tena tena na kutaka kukubandika jino. Bila kutaraji wala kutambua ufanyalo, ukajikuta ukipiga mayowe, “ANANIUMAAA!”
Abiria ndani ya daladala wakataharuki na kuamsha zogo, ndipo kama uliyetoka usingizini, ukazinduka, fadhaa ikakukumba; ukaangaza huku na kule, na kuona kila abiria akikushangaa na kukutazama kwa mtazamo wa wasiwasi. Wapo waliodhani umechanganyikiwa, wengine wakahisi umekumbwa na kitu kibaya. Balaa likabaki kwa abiria walioketi na kusimama karibu yake, wakikuogopa na kutaka kukuepuka, lakini kwa namna abiria walivyojaa na kubanana, hakuna aliyepata nafasi ya kukukimbia. Ili kuepuka wahka na taharuki ya abiria, ukaamua kuomba kushuka, “Konda niache hapo.”
Ingawaje hapakuwa na kituo cha dalala mahala hapo, lakini Konda aliona vyema kukushusha kama ulivyoomba ili kunusuru mkanyagano wa abiria. Kwa bahati, dalala zilikuwa haziendi kutokana foleni kushtadi barabara, hivyo, Kondakta akakufungulia mlango ili uteremke.
Ukiwa unaanza kushusha mguu chini kutoka kwenye dalala, ukagundua kwamba kumbe ndo kwanza mlikuwa mfika eneo lilelile ulipomwona yule Ombaomba jana yake, na kutokewa na sauti ya vitisho simuni. Sasa, ukajikuta ukiduaa; kushuka chini hautamani, kurudi ndani ya dalala unagwaya. Ukajikuta ukining’inia mlangoni kama wewe ndiye Kondakta. Hali hiyo, ikazidi kuwafanya abiria pamoja na Konda wazidi kukushangaa na kujitanibu nawe.
“Oya, hebu teremka bwana we!” Konda akabwata huku akikusukuma. Ukajikuta ukiteremka kama uliyechanganyikiwa.
Ukashuka huku ukiyumba kwa kusukumwa, na kubaki ukiduwaa barabarani.
“Kama hajarogwa kwa wizi wa wake za watu, basi Mbu wamemsababishia maleria,” Abiria mmoja akadhihaki.
“Mkiambiwa rudisheni vitu mlivyoiba misikitini–hamtaki!” Konda naye akakutupia maneno ya dhihaka.
“Mngechelewa kumshusha, angeanza kupiga watu humu!” Abiria mwingine akapaza sauti huku akicheka.
Maneno ya abiria kwenye daladala hayakukutaabisha kichwa. Akili yako ilimakinika na Ombaomba. Pamoja na kuangaza kwa umakini, walakini hukumwona bwana yule aliyekukosesha raha njia nzima. Ukahama upande huo wa barabara, ukaongeza mwendo na kutoweka eneo hilo.
Baada ya hatua ndefu za mashaka, hatimaye ukafika kwako ukiwa hoi bin taabani. Ukaingia ndani mwako na kujitupa kitandani kwa mchoko na mawazo. Usingizi nao haukukufanyia hiyana, ukakulaki na kukuchukua.
Kilichokutoa usingizini baada ya saa kadhaa za kulala, ni njaa ya mchana kutwa. Ukashituka na kuangalia muda: Saa nne na robo usiku. Ukasimama na kuvua viatu ulivyokuwa umelala navyo, ukabadili nguo na kutoka kwenda kupata chakula.
Baada ya chakula, ukarejea ndani ukiwa walau na nguvu mpya, ukalala. Usiku ukapita bila ya bughudha za ombaomba wala rabsha za ndotoni. Siku hiyo, walau uliamka na amani kwamba yale mauzauza yamekwisha, na kwamba unaendelea na maisha yako kama kawaida.
Mizunguko ya utafuta ilimalizika kama iwavyo siku nyingine, ukarejea nyumbani salama bin salmin. Mchezo ukakaanza baada ya kumaliza kupata chakula na kupanda kitandani kulala. Ndani ya mkono wako wa kushoto, maumivu makali mfano wa sumu ya nyoka yalianza kutambaa kwa kasi. Kitu mfano wa funza kilikuwa kikitembea ndani kwa ndani na kuacha uchungu usiosemekana. Fikara na hisia, vikakurejeshea kumbukumbu ya kile kilichokuingia mkononi kupitia jino la Ombaomba. Kadiri muda ulivyokuwa ukiyoyoma, ndivyo maumivu yalivyozidi kukumaliza. Mdudu aliyekuwa akikutembea mkononi, aliambaa kuanzia chini ya bega mpaka karibu ya kiwiko–. Uzalendo ukakushinda–ukaanza kulia.
Kwa mchomo wa maumivu, ukatamani kuita watu, walakini hunacho cha kuwaambia. Nani atakuamini? Kukosekana japo ushahidi wa kijitundu kilichopitisha hicho kijidudu kisambazacho sumu mwilini, kingefanya usisikilizwe. Na, suala la kwanini haukuwaeleza watu kama ulivamiwa na jitula ajabu usiku, lingekunyima haki ya kueleweka. Hapo awali, hukutazama mbali, ukaamini hakuna madhara makubwa, hivyo, ukalifuga tatizo moyoni.
Ujasiri ulikufanya ujikaze huku ukilia kwa sauti hafifu, lakini kadiri maumivu yalivyokuwa yakiongezeka, ndivyo sauti ikaanza kupanda, kilio cha uchungu na maombolezo kikawafikia wapangaji wenziyo na kuwafanya waje kukugongea mlango. Ukajizoazoa kitandani, ukautwaa mlango na kuwafungulia, kisha ukajibwaga sakafuni na kuendelea kuugulia maumivu huku ukiwa umeushikilia mkono kama kwamba unayazuia maumivu yasisambae mwilini.
“Muga!” mama mwenye nyumba akaakuita, “umeumwa na mdudu?”
“Bora hata angeniuma,” ukamjibu huku jasho la uchungu na maumivu likikutiririka, “ameniingiia kabisa mkononi!”
Mama mwenye nyumba, pamoja na wapangaji wenziyo, waliojumuika chumbani mwako, walikumbwa na taharuki. Na badala ya kukusaidia, wakaanza kukuhofia. Vihoro na alama za mshangao vikajidhihirisha kwenye nyuso zao.
“Mbona hatukuelewi Muga?” Salum mdananda, kijana aliyepanga chumba cha pili kutoka cha kwako, akaakusaili huku akikuinamia. Ukatamani kuwasimulia, walakini maumivu makali hayakukupa pumzi za kutosha kufanya hivyo. Badala yake, ukaazidi kulia kwa uchungu.
Wakaamshwa majirani, wajuvi wa dawa za kuondosha sumu za wadudu mfano wa Nyoka, Nge, Tandu, nk. Kuamshwa kwa majirani, kukaaongeza idadi ya watu chumbani mwako.”
“Enhee, amekuuma wapi?” mmoja kati ya wazee walioleta dawa, alikusaili.
Ukatamani kumwambia kwamba hakukuuma, bali alikuingia mwilini, lakini hilo litachukua muda na kucheleweshea tiba–ukamwonesha mkononi, huku ukiendelea kulia.
Si tu kwamba dawa hazikufaa kitu, bali kadiri walivyokuwa wakikupaka dawa, ndivyo sumu ilivyozidi kutambaa ndani kwa ndani na kuzalisha maumivu mara dufu. Kwa uchungu ukajikuta ukiwaondoa wasikuguse. Hilo nalo likawashangaza majirani na wapangaji wenziyo.
“Ja–ma–ni nau–mia–” Kila ulipohitaji kuelezea namna maumivu yanavyozidishwa na dawa zao, kauli haikufika mwisho kwa maumivu.
Majadiliano ya wakubwa, yakapitika kwamba uwahishwe hospitali. Na, kwakuwa hapo unapoishi si mbali na hospitali ya Amana. Mzee Lawalawa, mmoja wa majirani, akajitolea gari yake, ukapandishwa kwa kubebwa, na msafara wa kuelekea hospitali ukaanza.
Kilichowastaajabisha madaktari ni kauli kutoka kwa wapangaji wenziyo kwamba, kuna mdudu amekuingia mwilini, kutokana na maelezo yako ya awali. Kesi nyingi huwa mni tu kuumwa na mdudu mwenye sumu, na si mdudu kuingia mwilini kupitia sehemu isiyo na tundu. Kama kawaida ya matabibu, matibabu yakaanza.
Taarifa za maradhi zinawafikia nduguzo mjini Bukoba. Kwa uzito wa aina ya ugonjwa, hawakufanya zohali, walijikusanya na kuianza safari ya kuja jijini Dar es Salaam. Pia, taarifa zikawafikia watu wa Bukoba waishio Dar es Salaam, walakini wakagoma kujumuika nawe, kwa sababu tangu awali uligoma kujumuika nao wakati wakianzisha umoja wa kusaidiana.
Majira ya saa kumi na mbili jioni, waliowasili kutoka Bukoba ni; mama yako, Bi Mwanakatwe; dada yako, Shella; Na, kaka yako, Kamugisha. Wakati huo, ule uchungu usababishwao na sumu ya kijidudu ndani ya mkono, ulikuwa umepungua, maumivu yakabaki kwa mbali.
Salum Mdananda na mzee Lawalawa, wakawapokea nduguzo na kuwapa kwa muhtasari, taarifa za tangu hali ilivyobadilika usiku hadi kufikia muda huo. Nduguzo pamoja na mama yako, wakawashukuru waungwana wale kwa namna walivyoshughulika hadi muda ule.
Baada ya kumalizana na akina mzee Lawalawa, mama yako alikusogelea, na kuanza, “Pole sana, unaendeleaje kwa sasa?”
“Ahsante mama, naendelea vyema, namshukuru Mungu.”
Shella akadakia kwa wahka, “Haya, ilikuwaje hasa na kipi kimekukumba?”
“We nawe, hata hatujajuliana hali!” Muganyizi akamshushua Shella.
“Ni vyema akatusimulia mapema kama hali yake imetulia, kuliko kukaa tu halafu hali ibadilike ashindwe hata kuzungumza!” Shella akasema.
Ukajiinua kitandani na kuketi, kisha ukaanza kusimulia mkasa mzima, tangu awali ya mkasa wa Ombaomba na sauti ya ajabu, hadi akhiri ya usiku wa uvamizi wa Ombaomba chumbani kwako. Simulizi za kubandikwa jino na kuingiziwa kijidudu, iliwaacha hoi nduguzo, kila mmoja akiingiwa na ubaridi wa hofu.
“Hapa, kuna namna, si bure,” bi Mwanakatwe akasema, “na sioni haja ya kuendelea kupoteza muda hapa hospitali!”
“Kabisa!” Kamugisha akayasadiki maneno ya mama yake.
“Mwiba uingiliapo ndipo utokea. Kamwe, uchawi hautolewi hospitali,” bi Mwanakatwe aliendelea. “Leo hii, nitakwenda kwa Nyahinga kumuelezea.”
Nyahinga, mama wa rika la bi Mwanakatwe. Ni mganga wa kuogopwa kutoka Bukoba japo anaishi Dar es Salaam. Amejitengenezea umaarufu mkubwa kwa uwezo wake wa kupambana na wachawi na kuwaangamiza. Makazi yake ni Gongo la Mboto.
Bi Mwanakatwe na Nyahinga, walifahamiana tangu enzi za utoto wao huko Bukoba, kabla ya Nyahinga kuhamia jijini Mwanza na baadaye Dar es Salaam kwa shughuli zake za kiganga. Kwa fikra za bi Mwanakatwe, zilizoungwa mkono na watoto wake, tatizo linakwenda kuhitimishwa na mtaalamu wao.
Ilitokea kama bahati, pale bi Mwanakatwe alipokwenda kuomba ruhusa kwa madaktari, kumwondoa mwanawe hapo hospitali ili kumtibu kienyeji, alikubaliwa. yamkini madaktari nao, walikuwa njia moja kutoa ushauri kama huo, baada ya kusikia kisa cha mdudu wa ajabu aliyemo ndani ya mkono wa mgonjwa.
Nyote kwa pamoja mkaondoka hospitalini hadi kwako. Baada ya kufika nyumbani, majirani na wapangaji wenziyo wakaajumuika kukujulia hali. Walipokwisha, wakasambaa kila mmoja na shtighali zake za dunia. Baada ya kupata chakula na maji ya kuoga, kwa kutumia gari ya Kamugisha, mkaianza safari ya kuelekea Gongo la Mboto kwa Nyahinga.
__________
BAADA ya Nyahinga kukuoneni, kwa bashasha na taadhima, akawaacha wateja, akatoka kumlaki shoga yake, “Oh, Mama Kamu, karibu sana shoga yangu–sikujua kama mko nje, nisingalikuweka muda wote huo ndugu yangu!”
“Aah, usijali swahiba, ndivyo kazi inavyotaka hivyo,” bi Mwanakatwe akajibu.
“Kweli unenayo, lakini si kwa mtu kama wewe bwana–we ni mwanafamilia!”
Baaada ya kupokeana; bi Mwanakatwe akakutambulisheni nyote kwa Nyahinga.
“Hata ningekutana nao barabarani, haki vile, nisingaliwakumbuka. Niliwaacha wangali wadogo mno,” Nyahinga akasema. “Kama huyu Muga ndo alikuwa mwembamba kama chelewa!”
Nyote mkacheka kwa pamoja.
“Na huyo ndo ametufanya kwako muda huu,” bi Mwanakatwe akaanzisha mjadala.
“Kumbe–basi vyema–karibuni!”
Kabla bi Mwanakatwe hajasimulia chochote, mabadiliko ya hali yako yakaanza kutoa picha ya tatizo lililokupelekeni hapo. Mdudu akaanza kutambaa mithili ya moto mkononi mwako na kukuachia sumu kali ya maumivu kiasi cha kukufanya uanze kulia na kuomboleza kwa uchungu. Hali ika tafrani, Nyahinga akashirikiana na wasaidizi wake kukutuliza kwa ufundi wa kiganga bila mafanikio. Hila zote zikamwisha Nyahinga, bila ya kuweza kuzuia maumivu wala kujua kiini cha tatizo.
Zinaletwa dawa za kupaka–hazikufua dafu! Dawa za kunywa–hazikufaa kitu! Maumivu makali mtindo mmoja!
Mara, Nyahinga akapandisha mizimu, na kuanza kuongea lugha zisizoeleweka kwa mtu wa kawaida. Wasaidizi wake ambao walikuwa wakimsaidia kusikiliza maelekezo ya mizimu, nao ghafula wakapandisha mizimu. Nyumba ikakuwa ya mizimu–utulivu ukavurugika–hakuna wa kutafasiri wala kuwaelewa mizimu waliopanda vichwani mwa wataalamu. Almanusra wazimu umpande bi Mwanakatwe.
*****
MTUNZI; MAUNDU MWINGIZI (Mwana Balagha)
 

Attachments

  • 18814377_764910210346937_57611707920685762_n.jpg
    18814377_764910210346937_57611707920685762_n.jpg
    12.9 KB · Views: 97
MALAIKA? au SHETANI? (03)
18767936_765511990286759_5726442326676391561_n.jpg

Mara, Nyahinga akapandisha mizimu, na kuanza kuongea lugha zisizoeleweka kwa mtu wa kawaida. Wasaidizi wake ambao walikuwa wakimsaidia kusikiliza maelekezo ya mizimu, nao ghafula wakapandisha mizimu. Nyumba ikakuwa ya mizimu–utulivu ukavurugika–hakuna wa kutafasiri wala kuwaelewa mizimu waliopanda vichwani mwa wataalamu. Almanusra wazimu umpande bi Mwanakatwe.
Hali hiyo ilidumu kwa takribani nusu saa kabla ya mizimu kumruka Nyahinga, na kustaajabu kuona wasaidizi wake nao wakiwa wamepandisha mizimu vichwani. Akawasikiliza huku akiwahoji hadi walipomaliza na kuruka.
Utulivu ukarejea kwa wastani.
“Fanya upesi, kalete nghusha,” Nyahinga akamwagiza msaidizi wake, “lete ile nyekundu!”
Nghusha ni dawa ya mitishamba, ambayo aghalabu hufungwa kwa kuzungushwa kwenye kitambaa chekundu au cheusi.
Ngusha Ilipofika, Nyahinga akakufunga mkononi na kuanza kukupunga huku akiimba nyimbo za kiganga kwa lugha ya kihaya. Alifanya hivyo huku akikuzunguka mduara hadi maumivu yalipopunguza kasi na kwisha kabisa.
“Uuh!” bi Mwanakatwe, aliyejifunga kipande cha kanga kiunoni, akatweta. Pembezoni mwako, Shella akajifuta jasho. Nyumba nzima ilikuwa kimya.
“Nimemwona,” Nyahinga alisema.
Nyote mkamgeukia.
“Bora umemwona mwenyewe–hiyo ndiyo hali halisi ya mwanao,” bi Mwanakatwe akamjibu.
“Sina maana hiyo,” Nyahinga akakazia. “Nimemwona huyo kiumbe anayemsumbua!”
Nyote mkamakinika na taarifa hiyo.
“Ulimfanya nini huyo kiumbe?” Nyahinga akakuhoji.
“Sina kumbukumbu ya kumfanyia ubaya wowote mtu yeyote!” ukajibu.
“Ndiye huyu mwenye nywele chafu na meno mabovu?” Nyahinga akakuuliza huku akiangalia kwenye kioo chake.
Ili kutafuta ithibati ya mambo, Nyahinga akakusogelea na kukuonyesha mtu aonekanaye kwenye kioo.
“MAMAAA!” Ukajikuta ukipiga kelele za uoga, baada ya kuiona sura ya yule Ombaomba kwenye kioo. “Ndiye huyo!”
Akakirejesha kioo chake juu ya ungo, kkabaki mkitazamana.
“Twende huku!” Nyahinga akasema huku akikushika mkono na kukuinua.
Akakuingiza kwenye chumba kingine. Ni chumba chenye mwanga hafifu; michoro ya majiniwatu na viumbe wa ajabuajabu, mafuvu ya watu na wanyama, nk. Katikati ya chumba hicho kuna kitanda cha kamba; vile vitumikavyo kuoshea maiti.
“Panda hapo kitandani!” Nyahinga akakuamuru.
Nitapandaje ilhali miye si maiti? Ukajiuliza.
Baada ya kijitafakari, ukaafiki kishingo upande. Ile kupanda tu na kujilaza kitandani hapo, Nyahinga akaanza kupiga ngoma zilizokuwamo humo chumbani, kwa nguvu huku akiimba. Mara ukaanza kuhisi kizunguzungu, mara macho mazito kuona, kisha kitu kama usingizi kikayazidia nguvu macho yako. Na hapo ikaanza kama ndoto kichwani…
__________
MKIWA maeneo ya Magomeni Mapipa, jijini Dar es Salaa, wewe na sahibu yako, mlikutana na bwana mmoja, dhalili wa hali na dhaifu wa afya, akakusogeleeni kwa haraka na kukutakeni pesa. Taashira ya ufukara ilijishajihisha maungoni na mavazini mwake.
Pengine kutokana na kuchoshwa na wimbi la Ombaomba maeneo yako ya kazi, ukampuuza fakiri yule. Walakini, bila kutegemea, rafiki yako akatoa noti ya shilingi elfu kumi, na kumpa.
“Wewe, pesa yote hiyo unampa ya nini?” ukamzuia rafiki yako.
“Ah, mwache tu. Inaonekana ana hali ngumu sana!”
“Utaweza kusaidia Ombaomba wa mji wote?” ukahoji, “Kungejua mpaka kufika jioni huwa wamekusanya pesa nyingi mno hawa, kuliko hata wewe mfanyabiashara, wala usingetaabika nao.”
Ukiwa umemzuia rafiki yako, ukatoa sarafu ya shilingi mia mbili na kumpa huyo Ombaomba badala ya ile elfu kumi.
Kwa ghadhabu na uchungu, Ombaomba akatoa msonyo mrefu, huku akikukata jicho la hamaki.
Hukujali. Zaidi, ukamkaripia, “Unachagua pesa? Katafute za kwako!” ukamgeukia rafiki yako na kumwambia, “Tuondoke zetu!”
Mkaondoka na kumwacha Ombaomba akiendelea kukutazama kwa chuki na hasira. Kila ulipogeuka nyuma, ulimwona Ombaomba akiwa vilevile, amesimama palepale, bila kutikisika –akikutazameni. Hakuondoka pale, hadi mlipofika mbali zaidi ya upeo wa macho yenu kumwona.
Hukuwa na na mashaka wala tafakuri juu yake, kwa kutambua Ombaomba kama yule hano lo lote la kukufanya.
Siku nyingine, ikiwa imekatika miezi kadhaa tangu ulipomtindikia riziki yule Ombaomba, ukiwa unatokea kazini kwako majira ya saa kumi na mbili jioni kwa miguu, ndipo ukakutana tena na Ombaomba yuleyule, akiwa amesimama maeneo ya ilala…! Kumbukumbu ziligoma kurejesha mkanda wa tukio la awali lililokukutanisha naye kwa mara ya kwanza.
__________
GHAFLA, ukashituka usingini, ukatoka kitandani huku ukitweta na kutaka kukimbia. Kumbukumbu ya mkasa wa namna ulivyokutana na yule Ombaomba vilijidhihirisha ndotoni, ukiwa kitandani kwa mganga.
Nyahinga akakushika mkono, kisha mkatoka nje na kujumuika na ahli yako, wamejiinamia. Baada ya kuketi, Nyahinga alisema, “Haya, tayari Muga amekwisha kumkumbuka mtu wake.”
Wote wakakutazama kwa mshangao. Nyahinga akamalizia, “Sasa, tueleze hatua kwa hatua, namna ulivyokutana na mtu yule.”
Bado ulikuwa ukistaajabia ufundi wa Nyahinga kuweza kukurejesha kumbukumbu za matukio yaliyopita, kwa kukulaza juu ya kitanda cha kuoshea maiti, na kukupigia ngoma za kiganga. Bila kufanya ajizi wala zohali, taratibu ukaanza kusimulia kuanzia 'alif mpaka yee'.
Pamoja na kujaribu kuonesha namna ambavyo hukudhamiria uadui na Ombaomba yule, lakini kwa simulizi ile, ulistahiki kulaumiwa kwa kitendo cha dharau, choyo na jeuri uliyomwoneshea, tena kwa pesa isiyo ya kwako.
Baada ya ukimya kutuama kufuatia kuhitimika kwa simulizi ya mkasa wako, Nyahinga akaendelea, “Tuna kibarua kigumu cha kumtambua kiumbe huyo–maana bila ya kutambua tunapambana na nani, itakuwa kazi ya bure bileshi. Kiumbe hicho, kilichojivika umbile la kibinaadamu, hakioneshi asili yake; si mtu, si jinni, si mzimu.”
“Sasa, kama kiumbe hicho si katika jamii ya wanaadamu, majini wala mizimu–kumbe ni nini hasa?” Kamugisha akahoji.
“Ndiyo nikasema, hilo liko nje ya uwezo wetu; yawezekana ni Shetani au hata Malaika, maana hao ndiyo viumbe wasiokamatwa na ramli za kiganga wala kichawi. Kama ni shetani, basi tutapambana yae kwa msaada wa Mungu; na endapo kama ni Malaika, hilo tutamwachia Mungu mwenyewe kwani ndiye huwatuma Malaika wake kwa lile alitakalo yeye!” Nyahinga akajibu kwa unyonge na kukata tamaa.
Baada ya mjadala, tiba zikaendelea kwa wastani, hadi ulipotimu muda wa chakula cha mchana. Mkajumuika kupata chakula, na baada ya chakula tu, Nyahinga akakuelezeni, “Hapa, inatakiwa tutoe kafara.”
“Kafara ya nini?” bi Mwanakatwe akahoji.
“Kwanza, tutaandaa sadaka ya chakula kwa watoto na wasiojiweza. Kisha, tutatupa sadaka ya pesa kwa watoto pekee. Watoto ni wasafi tamthili ya Malaika, kwa hivyo, kwa kuwatumia wao kama ngao yetu ya kuombea msamaha, asaa tukasamehewa. Na ikawa mwisho wa dhila hii kwa Muga.”
“Tawire,” bi Mwanakatwe alijibu.
“Jumamosi ndiyo siku nzuri kufanya kafara hilo. Tutahitaji kumwaga damu ya mnyama, na mnyama mwenyewe ni vyema akawa Kondoo kwa sababu ya upole na ukimya wake, huenda ikawa sababu ya kulituliza baa hili. Kimsingi, hatuna uwezo wala sababu ya kupambana na kiumbe hicho cha ajabu, tutapaswa tu kukiomba msamaha. Tutakwenda makaburini usiku, bila kujali kama hali ya Muga itakuwa imebadilika na kuwa mbaya au laa, huko makaburi, tutamchinja kondoo huyo na kisha tutamzika kwenye kaburi.”
“Baada ya kafara hiyo ya makaburini, siku ya Jumatatu ndipo tutakapotoa sadaka ya chakula, kisha mtakwenda njia panda, kupasua nazi na kutupa sadaka ya pesa!”
“Bora salama tu fundi,” bi Mwanakatwe alisema.
“Nasikitika kukuambieni jambo moja,” Nyahinga akaanza tena. “Maelekezo niliyopewa na mizimu ni kwamba, kwanza ni lazima nazi hiyo ipasuke kwa pigo moja tu, hakuna kurudiarudia, hivyo, mpasuaji ambaye ni Muga mwenyewe, atapaswa kutumia nguvu kwa kuielekeza nazi kwenye kitu kigumu kama vile jiwe. Nazi ikishapasuka, ni lazima mtu aiokote na kuila–na mwokotaji wa kwanza, atatakiwa awe ni wa jinsi ya kiume.”
“Mnh, nani huyo atakayeokota nazi na kuila?” Shella aliuliza.
“Mbona wako wengi tu; kuna watoto wasiojua lolote, kuna wehu wasio na akili timamu, na wako hata walimwengu wenye dhiki kali. Hayo yakifanyika kikamilifu, maana yake kafara itakuwa imekubalika na kuanzia hapo, Muga atakuwa amepona. Lakini, endapo kama nazi haitovunjika, au ikavunjika halafu mtu wa kwanza kuiokota akawa ni wa jinsi ya kike, basi mjue kafara imeshindikana, na mzimu wangu hautokuwa na uwezo tena wa kupambana!”
Maneno hayo yakazalisha simanzi zaidi moyoni kuliko faraja, ukawatembezea macho yako wote mle chumbani, kisha nawe ukauliza. “Kwahiyo baada ya kupasua hiyo nazi huko njiapanda, itatubidi kukaa maeneo hayohayo kabla hatujarejea tena huku kwako mpaka atakapopatikana mtu wa kuiokota na kuila?”
“Swali zuri, huku kwangu hamtakiwi kurudi tena. Ikitokea mmefanikiwa, mumshukuru Mungu na muelekee kwenu, sitahitaji malipo ya kazi hii kwa sababu nimeifanya kwa ajili ya shoga yangu. Na, ikitokea hamkufanikiwa, mkatafute mganga mwingine,” Nyahinga alifafanua, “pia suala la kumsubiri mtu atakayeokota nazi hiyo, ni la lazima ili muondoke mkijua kama kafara imekubalika, au sivyo. Juu ya hayo, hampaswi kumzuia wala kumwelekeza mtu yeyote kwenda kuokota nazi.”
Siku ya Alkhamisi mkaimaliza nyumbani kwa Nyahinga, halikadhalika na Ijumaa. Hatimaye siku ya Jumamosi ikatimu, maandalizi yakafanyika. Mkanunua kondoo kama mlivyoagizwa, mkawa tayari kusubiri giza liingie mwende makaburini.
“Tutakwenda watu watatu tu: Muga, mimi na msaidizi wangu,” Nyahinga alisema.
Muda ulipotimu mkaondoka nyumbani, na kuelekea makaburini.
__________
KAMA kawaida, mazingira ya makaburini hasa katika nyakati za usiku, hutisha na kuogofya mno. Mliingia katika viwanja vya makaburi mkiwa watatu kama mlivyoondoka nyumbani. Nyote mlijifunga vipande vyeusi vya kaniki katika mtindo wa lubega.
Baada ya nyimbo za kiganga kumalizika, Nyahinga na msaidizi wake wakamshika Kondoo, ukaamriwa umchinje kwa kukilengesha kichwa chake kwenye chungu cheusi kilichokuwa na dawa yake ili damu ichuruzikie humo. Ukafanya hivyo, na zoezi likakamiliza.
“Haya, kunywa!” Nyahinga alikuamuru unywe ile damu ya kondoo iliyochanganyika na dawa kwenye chungu. Ukatii.
Damu iliyobakia ilitumika kuchorea maandishi kwenye nazi utakayokwenda kuipasua njia panda kama ulivyoelekezwa awali.
Hali ambayo haukuitegemea, mlikuta kaburi likiwa tayari limekwishachimbwa bila ya kumtambua mchimbaji; ukatakiwa umzike kondoo yule, ukafanya hivyo bila kusaidiwa na mtu yeyote.
“Weka hicho chungu juu ya kaburi,” Nyahinga alikuelekeza.
Ulipomaliza kukiweka, akasema: “Omba msamaha kwa ulichomtendea yule Ombaomba, kisha Muombe Mungu akunasue kwenye mkosi huu!”
Wakati ukimalizia kufanya kama ulivyoelekezwa, ukashuhudia kile chungu kikizama chenyewe kaburini taratibu na kupotelea humo.
“Dalili njema; tuondokeni, mwiko kugeuka nyuma!” Nyahinga alihitimisha, na papo hapo mkaanza kutoka nje ya uga wa makaburi. Ngwe ya kwanza ikakamilika bila ya rabsha zozote.
Mama na nduguzo wakafurahi kukuona umerejea salama salmini. Mkaendelea kuwapo nyumbani kwa Nyahinga mpaka ilipotimu siku ya Jumatatu.
“Kusanyeni noti mojamoja: ya shili miatano, ya elfu moja, ya elfu mbili, ya elfu tano na ya elfu kumi, kisha, endapo kama hiyo nazi itavunjika bila tabu hapo utakapokwenda kuipasua, ndipo na hizi pesa mtazitupa papo,” Nyahinga akakuelekezeni huku akikupeni nazi moja iliyochorwa maandishi kwa damu ya kondoo. “Kazi hii, mkaifanye saa kumi na moja jioni. Isiwe kabla wala baada ya hapo. Nakutakieni kila la kheri!”
Baada ya kutoa shukrani na kuagana kwa kutakiana kila la kheri, mkafungasha kila kilicho chenu, mkaondoka na kurejea nyumbani kwako. Mkiwa huko, kichwani mwako ulijawa na mawazo lukuki, nduguzo walijaribu kukufariji, bi Mwanakatwe naye alijikita kwenye maombi kila mara.
“Kwa sababu zoezi lililobakia ni dogo, hakuna tena sababu ya kuandamana pamoja kwenda kutafuta njia panda,” ulisema wakati mkijiandaa. “Mama na Shella ninyi mtatusubiri tu, nitakwenda na Kamugisha.” Ulihitimisha kwa sauti ya ushawishi na upole.
Haikuwa rahisi kumshawishi bi Mwanakatwe akubali kukuacha uende peke yako, huku akiamini huenda hali yako ikabadilika ghafla ukiwa huko, na kuzuwa dhahma mbele ya kadamnasi. Ila kwa kushirikiana na na nduguzo, hatimaye akaafiki.
Muda ulipoanza kujongea, mkatoka wewe na Kamugisha na kuingia kwenye gari yenu ndogo tayari kuianza safari … safari ya matumaini.
Maeneo hayo unayoishi wewe, ziko njia panda nyingi mno, lakini haukutaka kuzitumia hizo kwa kuogopa vijicho vya walimwengu wanaokufahamu. Mkaenda hadi mitaa ya Tabata ambako mlikutana na njia panda nyingi pia ambazo ungeweza kukidhi haja yako. Huko nako tatizo kubwa likawa ni wingi wa watu hasa kwa muda ule wa saa kumi na moja ambapo baadhi wanatoka makazini huku wengine wakiendelea kujitafutia riziki.
Wakati mkiendelea kukimbizana na muda, kwa mbali ukaanza kuhisi maumivu mkononi, hofu ikakita moyoni mwako, mashaka ya zoezi yakaanza kukuandama.
***

MTUNZI; MAUNDU MWINGIZI (Mwana Balagha)
 
Kamugisha mbona lete stori acha kuibania
 
Nzuri lkn kuna watu huku jf wanakera wanaleta stor hawamalizii km mjukuu wa chief si muwe km mrembo shunnie jaman
 
Nina Udhuru Nitaweka Muda Wowote Kuanzia Hivi Sasa
Imebaki Sehemu Ya MOJA TU!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom