MAGNUM22
Sehemu 8
GOLDEN TULIP
SAA NANE USIKU, hoteli ya Kimataifa iliyojengwa kando kando ya Barabara ya Toure ilikuwa kwenye hali ya utulivu. Magari mengi yalikuwa maegeshoni na ni walinzi tu walikuwa wakipita huku na huko kuhakikisha usalama wa vyombo hivyo. Gina akaongoza gari mpaka katika maegesho ya hoteli hiyo.
“Tunawapataje?” Gina akamuuliza Amata huku akizima injini ya gari hilo.
“Tutatumia Soviet Method, kwani picha ya yule mwanamke huna?” Amata akamtupia swali Gina.
“Ipo!” Gina akajibu.
“Sawa, ichukue twende nayo,” Amata akamwambia Gina huku tayari keshafungua mlango na kuteremka nje. Gina naye akateremka na kumfuata, hatua zao zikawafikisha katika meza ya mapokezi ya hoteli hiyo. Katika ofisi hiyo kulikuwa na wanadada wawili waliovalia nadhifu na kupendeza kwelikweli.
“Karibu sana Golden Tulip, nikusaidie nini?” mmoja wa wale wadada ambaye beji juu ya kifua chake ilimtambulisha kama Esther Kwimba akawakaribisha.
“Asante sana, sisi ni maafisa uhamiaji tumekuja hapa tunamtafuta mtu huyu… je mmewahi kumuona? Akamwambia mrembo yule huku akimwonesha kitambulisho cha kazi hiyo. Mwanadada yule akachukua kitabu cha leja na kukiweka tena mezani.
“Alikuwapo hapa, lakini amecheck out, likizo yake imekwisha!” akajibu. Amata akamkazia jicho kana kwamba bado hajarizika na jibu hilo, “huamini au?” akaongeza swali.
“Si kwamba siamini, ila nataka unambie ni saa ngapi ametoka na nani?” Amata akampiga swali mwanadada yule. Akafunua kitabu cha wageni na kutazama mpaka kwenye jina lile, Angela Queen.
“Angela Queen, amecheck out saa 11 jioni ya leo,” akajibu mwanadada yule.
Kamanda Amata akamtazama Gina, “tumemkosa?” mwanamke huyo akauliza huku akiweka mkono wake shavuni kwa masikitiko.
“No!” Amata akajibu, kisha akaaga na kutoka na Gina mpaka kwenye gari.
“Hatuwezi kumkosa, kama ametoka saa kumi na moja ina maana kwamba ndege yake ni saa moja usiku au saa kumi na mbili jioni ….”
“Ikizidi sana saa mbili usiku,”
“Yes! Kwa maana hiyo hatuna budi kutazama kama kuna ndege ya kutoka nje ya Tanzania mida hiyo,” Amata akamwambia Gina. Gina hakutaka kuchelewa akainua simu na kupiga kwa Lulu kutaka kujua kama kuna ndege yoyote ya kutoka nje ya Tanzania, jibu ambalo alilipata ni kuwa ‘hakuna’. Akamtazama Amata kwa nukta kadhaa kisha akamwambia, “Atakuwa humuhumu nchini”.
“Usiseme nchini, kwa kusema hivyo ndiyo unazidi kumpoteza, sema humuhumu jijini…”Amata akaongezea.
“Wapi sasa?”
“Sijui!” akamjibu huku akijiegemeza kitini na mkono wake ukishikwa kichwa, ukimya ukatawala kwa nukta kadhaa kati ya wawili hawa.
“Gina!”akaita, “sasa naweka nguvu zangu kwa asilimia tisini kwa mwanamke huyu na hao wenzake, mchezo wanaufanya unanitia mashaka, naihisi hatari mbaya sana siku ya kesho,” akamwambia.
“Yaani…. Kama sijakuelewa flani hivi,” Gina akaonesha mashaka katika hilo.
“Nasema, hawa jamaa sasa inabidi tuwafungie kazi, naanza kuhisi hatari siku ya kesho,” akarudia kusema.
“Kwa hiyo!”
“Yaani hapa tulipofikia yatupasa kutoa taarifa panapohusika ili kuanzia asubuhi ulinzi uwe mkali kila kona. Akamwambia Gina huku akifunga mkanda wa gari lake. Tayari jogoo wa kwanza alikwishawika, huyu kwenye mila zetu tungemchinja kwa sababu kafanya hivyo kabla ya wakati.
“Kumekucha, twende tukalale,”
“Unataka cha asubuhi?” Amata akamtania.
“Toka hapa!!!!” akamwambia huku akiwasha gari na kuyaacha maegesho hayo taratibu.
* * *
SIKU ILIYOFUATA
PAMABAZUKO LA SIKU HII lilimkuta Kamanda Amata na Gina kitandani, ni sauti ya kengele ya mlango ndiyo iliyowakurupusha katika usingizi wao.
“Aaaaaaaahhhhhhhh!” Gina akainuka na kutwaa koti lake lililoshonwa kwa kitambaa kizito cha taulo. Akavuta droo na kuchukua bastola yake ndogo akaifutika katika mfuko wa ndani huku mkono wake ukiwa huko, akatoka chumbani na kuelekea sebuleni. Akafika na kuufungua mlango macho yakagongana na kijana muuza maziwa ambaye anamfahamu, daima huja kumletea bidhaa hiyo.
“Leo mbona umewahi sana?” akamwuliza.
“Nina safari saa tatu asubuhi ndo maana nimekuetea mapema, hata hivyo nilijua kuwa umetoka maana niliona gari inageuza hapa getini,” yule kijana akamwambia.
“Gari?”
“Eee gari moja ya bei mbaya sana, nyeusi hivi… lakini ilivyonipita kwa mbele nikaona kuna wazungu watatu…”
Gina akatahayari kwa maneno hayo, akajiuliza juu ya gari hilo, hakulijua.
“Ok! Labda walipotea njia!” akamwambia na kumshukuru, kisha akamwambia asubiri kidogo, akaingia ndani na kumletea shilingi elfu ishirini kama nauli kwa safari kwa kuwa kijana huyu huwa anamsaidia mara nyingi hata kazi za hapo nyumbani. Mara baada ya kurudi ndani akamkuta Kamanda Amata akiwa tayari ndani ya suti safi.
“Vipi baba?” akamuuliza.
“Vipi?! Kazi mama, unajua leo ni siku ngumu sana, by the way kijana anasema ni gari gani lilikuja?
“Ee mwanaume hupitwi, wivu tu, yaani ushakuja kusikiliza…”
“Ndiyo, lazima nijue nini kinazungumzwa,” Amata akajibu huku akifunga vifungo vya mikono ya shati lake.
“Ninapata wasiwasi, anasema kuna gari jeusi lilikuwa na Wazungu watatu ndani yake, nina wasiwasi kwa sababu huyu tunayemsaka hata pale uwanja wa ndege alitumia gari jeusi…”
“Hata Chiba alituambia kuwa anahisi wapo watatu,” Amata akamwambia, “kwa hiyo wamekuja mpaka nyumbani, wamepajuaje? Walikuwa wanatufuatilia?” akaongeza maswali yaliokosa majibu.
“Vaa tuondoke! Haraka!” Kamanda akamwambia Gina na ni nukta hiyo hiyo simu yake ikaita kwa fujo, akaichuku na kuitazama, Chiba.
“Ndiyo kaka!” akaitikia.
“Jiangalieni nahisi mpo hatarini, kwa usalama tokeeni mlango wa nyuma,” akamwambia kupiti asimu hiyo. Dakika ishirini baadae, Gina naye akawa tayari, safari ikaiva.
“Tutokee mlango wa nyuma!” Amata akamwambia Gina, naye hakubisha, wakatumia njia hiyo kutoka nje, wakakodi taksi na haraka wakaingia katikati ya jiji. Breki ya kwanza ilikuwa ofisi ndogo. Madam S alikuwa tayari ndani ya ofisi hiyo, zaidi ya yeye safari hii kulikuwa na mgeni mwingine zaidi, Inspekta Simbeye.
“Nilijua tu kuwa muda huu mtaingia, haya hatuna muda wa kupteza…” akawaambia huku akiwataka kuketi.
“Kumekucha na siku yetu ni hii, kwa ushirikiano wetu tutaweza kuzuia jaribio la mauaji ambalo lina tetesi ya kutokea,” Madam S akasema.
“Mauaji?” Amata akauliza.
“Ndiyo, Simbeye alikuwa hapa,”
Inspekta Simbeye, akiwa ndani ya nguo za kiraia, lakini mkononi mwake kukiwa na simu ya upepo, alikuwa ofisini hapo dakika chache tu zilizopita. Ni mara chache sana ya Inspekta huyu wa kudumu kuja katika ofisi hii, kazi zao daima hufanyika mahala popote wanapochagua.
“Amepata hii meseji…” akampa simu Amata.
“Tunajua, mnatufuatilia,
lakini mjue kuwa tumejipanga na
tutatekeleza azma yetu,
lazima Somali Land iwe huru.
Tunahitaji Ardhi ya mama zetu,”
Ni sisi Freedomfighter!”
Kamanda Amata, akairudisha simu ile kwa Madam S, “ndiyo tunawafuatilia, na leo hii tutawatia mkononi,” akamalizia kusema.
“Mh! Wajitangaza sasa,” Gina akasema.
“Wameona tayari mmegundua nyayo zao,” akajibu, “sasa nataka niwape mpango kazi wa kufanya,” akaongeza.
Madam S akajikohoza kusafisha koo, “tatizo hatujui ni wakati na saa ngapi na ni njia gani watu hao watatekeleza mpango wao,” akawaambia.
“Yes!!” wakajibu kwa pamoja.
“Good sasa mpango wa kwanza ni kuzuia mkutano kuanza saa tatu, tukague ukumbi mzima kama kuna mlipuko au kitu chochote ambacho kitahatarisha uhai wa mtu. Pili tukiruhusu mkutano ufanyike tuhakikishe tumekagua gari zote za viongozi hao kabla hawajapanda kuja ukumbini, na ukaguzi wa kila mtu anayeingia ukumbini, asiruhusiwe mtu kuingia na simu, saa, wala chochote kile cha mawasiliano au chuma. Naongeza kuwa viongozi wote wasile chakula wala kunywa maji kutoka katika hoteli hiyo…” Madam S akatoa muongozo wa kwanza, akamgeukia Simbeye.
“Inspekta nimemwambia kuwa ninathitaji vijana wake wa kikosi maalumu kuanza kuweka ulinzi kwenye ukumbi huo sasa, ili kuzuia mtu yeyote kuingia ndani ya eneo la ukumbi huo,” akawaambia. Baada ya hapo akachukua simu maalumu ya ofisi na kupiga mahala fulani pa siri, akatoa angalisho la kuzuia mkutano huo kwa muda. Hakutaja muda gani ila alieleza hilo na kutaka kuonana na Mkuu wa Itifaki ya mkutano huo haraka iwekanzvyo.
“Kamanda Amata, hakikisha unategua kitendawili hikl ndani ya dakika chache zijazo kwa kombat ya aina yoyote, Chiba utakuwa na Amata, lakini wewe unajua ni nini cha kufanya, fuatilia hii meseji ujue imetoka wapi nahitaji ndani ya dakika chache tu uwe umenipa jibu. Gina nataka ufanye kazi ndani ya ukumbi wa mkutano kwa siri, hakikisha hutambuliki kwa yeyote, najua unajua nini cha kufanya.
* * *
Madam S alikutana na Mkuu wa Itifaki katika ofisi yake ndani ya jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani. Hakikuwa kikao bali ni kupeana maagizo juu ya nini cha kufanya katikma mkutano huo.
“Unajua kuzuia mkutano kwa muda usiojulikana tunajenga picha mbaya sana katika uso wa kimataifa, kuna wajumbe wa Commoniwealth na UN na jumuia nyingine kubwa ambazo kwazo sisi hutegemea mengi. Sasa wanajua saa mbili tunatakiwa ukumbini then mnachelewesha mambo, Wazungu hawa watatasusa mkutano…” akazungumza bwana yule aliyetuna kitini kama chatu aliyemeza mbwa.
“Achana na Wazungu, mambo ya Afrika lazima yaamuliwe na yafanywe kiafrika, mkutano umeahirishwa kwa sababu za kiusalama, kuna tetesi za umwagikaji wa damu katika mkutano huu, inaonekana wewe wapenda litokee siyo?” madam S akamwambia huku akiwa tayari kainuka kitini.
“Si napenda litokee, bali mambo ya kiitifaki hayaendi hivyo mama,” akamwambia.
“Sasa ni hivi, kikao kitaanza itakapotangazwa, na ikiwezekana, hakitakuwepo kwa kabisa au tutabadilisha ukumbi,” Madam S akamwambia.
“Kubadilisha ukumbi?” akauliza huku naye akijitahidi kusimama kuonesha msisitizo lakini tumbo lake likamzuia kufanya hivyo. Wakati huo Madam S tayari alikuwa keshafungua mlango anaondoka.
Katika mahoteli yote ambayo wageni wale walifikia kulikuwa na ulinzi mkali sana, askari wenye sare na wasio na nazo walikuwepo, kila mmoja akiwa ametingwa na kile anachotakiwa kufanya. Hali ilikuwa tete, vijana wa Usalama wa Taifa walikuwa hai hai kujaribu kugundua mpango huo kila eneo muhimu ambalo walilihisi, lakini kazi ilikuwa ngumu.
Asubuhi hiyo hiyo, Gina alitinga katika ukumbi wa mkutano kama alivyotakiwa kufika, katika lango kuu la kuingia katika eneo la ukumbi huo, aishuhudia askari wa FFU na baadhi wa JW wakiwa wameweka ulinzi mkali, waandishi wa habari na watu wengine ambao tayari walikuwa wamewasili, wakatakiwa kukaa mbali kidogo na eneo kwa kuwa kuna kazi iliyokuwa ikifanyika.
“Akuna cha bomu wala nini,” akasikika mtu mmoja akisema.
“Basi tu, tunataka kuonekana tuko makini na usalama hamna chochote, walishindwa Angola na Ivori Coast kuzuia mauaji ya viongozi itakuwa sisi….” Mwingine aisikika, huyu ni kati ya wale Watanzania wanajidharau na kutokujiamini. Barabara kadhaa zilifungwa tayari kuruhusu wageni wa mkutano huo kuwasili muda wowote.
Kati ya watu waliokuwa katika kundi la waandishi wa habari, alikuwapo Amanda Keller akifuatilia kila kitu kwa ukaribu kabisa. Na taarifa zote ambazo zilipatikana hapo, zilifika kwa Martin na Fredy moja kwa moja. Hakuna mtu ambaye alimjua mwanamke huyo kuwa ni ‘kidudu mtu’ kati ya watu hao, na kutokana na mchanganyiko wa waandishi Wazungu kwa Waafrika haikuwa rahisi kumjua.
* * *
Ndani ya hoteli ndogo ya Kunduchi Beach huko Kunduchi, Martin na Fredy walikuwa wakipata kifungua kinywa huku wakisika mengi kutoka kwa Amanda.
“Wanafikiri sisi ni wajinga kufanya kazi yetu kwa wazi hivyo?” Fredy akamuuliza Martin.
“Sisi ni profesheno, yani nitamtungua huyo jamaa mpaka wenyewe watashangaa, salama yao ni kuachia ambacho tajiri wetu anataka,” Martin akamjibu Fredy huku akiweka kikombe cha kahawa kinywani na kupiga funda moja kwa mruzi.
“Wanafanya ukaguzi kama kuna mlipuko wowote….”
“Hah! Hah! Hah! Hah! Waache wafanye mazoezi maana hakuna watakachopata…” Martin akazungumza, “ni risasi moja tu basi ambayo wanatakiwa kuitafuta na si bomu au kemikali au sumu ya kwenye chakula, na risasi hii ninayo mimi peke yangu tu, na ndiye ninayejua ni wakati gani wa kuiruhusu ifanye kazi yake, na wasipoangalia watakufa wao, tena kifo kibaya,” akamwambia Fredi huku mkononi akiirusharusha risasi moja kubwa.
Upande wa pili, Chiba alikuwa ndani ya gari lake akiendesha taratibu huku akijaribu kufuata mawasiliano fulani ambayo aiyahisi si ya usalama sana. Kutoka ndani ya gari hilo aliweza kusikia sauti ya Amanda ikipeleka taarifa mahali fulani. Alichokuwa anafanya yeye ni kufuata wapi mawimbi hayo yanaelekea kwa kuangalia nguvu yake kawenye chombo hicho. Sasa alikuwa tayari maeneo ya Tangi Bovu na signal ilimwonesha kuwa upande huo wa Bagamoyo ndiko mawimbi hayo yanakwenda.
“Nina uhakika wa kuwatia mkononi muda si mrefu, huyu mwanamke yupo huko mjini ila sijajua ni eneo gani, na inaonekana anajua information zote,” Chiba akamwambia Amata kwa kifaa chake maalumu ambacho hakiingiliani na mawasiliano yoyote ya huko duniani.
“Ngoja nijaribu kumgundua kama nitafanikiwa maana inaonekana anajua sana kujibadili,” Amata akamjibu Chiba, “na ukigundua ni wapi walipo, naomba unijulishe usifanye kitu, ili tuje tuwatie displin na wajue kuwa sisi si watu wa mchezo mchezo,” akaongeza kusema huku akiwa mita chache kutoka Hoteli ya Kepinski Kilimanjaro ambapo Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye ni Rais wa Ganbia pamoja na marais wengine walifikia mahala hapo. Ulinzi wa hapo haukuwa wa kawaida, kila aliyeingia alikaguliwa mpaka maeneo nyeti kabisa ya mwili wake.
* * *
Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa akakutana kwa siri na Mkuu wa Itifaki, mara hii ndani ya Ikulu, yaani makao makuu ya Rais wa nchi.
“Mheshimiwa, sasa tunaweza kuruhusu shughuli ziendelee, vijana wanasema usalama upo mwingi tu, hakuna walichokigundua kibaya,” yule Mkurugenzi akamwambia Mkuu wan chi huku mwanaitifaki yule akitikisa kichwa kuafikia hayo.
Baada ya kutafakari kwa sekunde kadhaa, akawataka kusubiri, akawaacha sebuleni na kuingia ndani katika chumba chake cha siri, akainua simu yake na kupiga namba fulani, akampata Madam S ambaye yeye ndiye aliyekuwa na usemi wa mwisho wa Rais huyo.
“Hali ikoje huko?” akamuuiza.
“Vijana hawajagundua chochote kibaya, nimewapa taarifa watu wa usalama na itifaki kuwa sasa shughuli inaweza kuendelea lakini ulinzi ndiyo kitu cha muhimu sana,” akamjibu.
“Sawa! Asante, nategemea hautakuwa mbali na eneo,” akamwambia.
“Bila shaka, na nitaongeza minzi wa siri kwa mgeni wetu kwa kuwa siamini mtu zaidi ya viajan wangu tu,” Madam S akamwambia.
“Fanya hivyo,” Rais akamwambia na kukata simu.
Saa nne kamili, waandishi wakaruhusiwa kuingia ukumbini na wageni wengine, wakapangwa mahala pao tayari kwa mkutano huo. Dakika kama ishirini baadae, ving’ora vikasikika na gari za bei mbaya sana zikaingia mfululizo katika eneo la ukumbi huo na kuegeshwa mahala salama kabla vingozi kuruhusiwa kushuka. Walinzi maalumu kutoka nchi ambazo marais wao walikuwapo waizingira magari hayo pande zote, huku masikioni mwao wakiwa na vifaa maalumu vya mawasiliano. Hakuna aliyejua ni nani wanayewasiliana naye, ilikuwa siri yao. Saa nne na nusu wote kwa pamoja wakafungua milango na kuwateremsha viongozi hao kisha kuwaingiza ukumbini humo, lakini kati ya wote hao, rais wa Gambia ambaye ndiye haswa mwendesha mkutano hakuwapo. Yote haya Amanda alikuwa akiyaona yote na kuwapa taarifa watu wake.
Kule Kunduchi, tayari vijana wale walikuwa wakijiandaa kuondoka kuelekea mjini tayari kwa kazi waliyotumwa. Martin akiwa chumbani kwake, akafunga kila kilicho chake tayari kwa safari na Fredy vivyo hivyo. Baada ya kila kitu kukamilisha wakaweka kila kitu ndani ya gari na wao kujipakia tayari kwa safari.
Chiba alifika katika hoteli hiyo na kupishana na gari lile getini pasi na kulichunguza sana, akaingia na kuegesha la kwake ndani kisha akateremka mpaka mapokezi. Alikuwa na uhakika kabisa kwamba mawasiliano hayo yametoka hapo.
“Karibu Kunduchi Beach Resort!” akakaribishwa na kijana mmoja mrefu mwenye asili kama ya Kisomai hivi.
“Asante sana, ninauliza mwenyeji wangu kama nimemkuta,” Chiba akamwambia huku akitoa picha na kumwonesha. Yule kijana akaichukua na kuingalia mara moja tu, akamrudishia kisha akatikisa kichwa kushoto kulia.
“Vipi?” Chiba akauliza.
“Dah! Kaka umejipatia dodo nini…. Maana wanawake hawa Wakizungu ni wagonjwa sana wa mapenzi ya kiafrika….” akasema.
“Kajilengesha mwenyewe mi nifanye nini, kuna mwanaume anayekataa mwanamke wa Kizungu, kwa mfano wewe angeamua kukupa, ungekataa?”
“Aaaaa brazaaa si unajua tena, bahati za wachache hizo, nikiipata siiachi,”
“Sasa je! Chumba chake kiko wapi?”
“Namba 50, Impala!” akamjibu. Chiba akavuta hatua mpaka upande wa vyumba na kukagua mpaka akakipata hicho akitakacho. Akapiga jicho katika tundu la ufunguo, hakuna ufunguo, akili ya kwanza ikamwambia kuwa ndani humo hakuna mtu. Akatazama huku na kule yuko peke yake eneo hilo, akachukua funguo yake na kuipachika, akanyonga mara mbili kitasa kikakubali tekenyo hilo, ukafunguka. Chiba akakaribishwa katika chumba kipana cha mviringo kilichobeba samani za thamani.
Bila shaka hii ni suit! Akawaza na kuingia ndani taratibu kisha akaufunga mlango nyuma yake. Akaitazama saa yake na kuizungusha kwenye pete ya juu, akasubiri kama sekunde kumi hivi hakuna chochote. Akachukua kifaa chake cha mawasiliano na kuwasiliana na Amata, akampa taarifa kuwa yupo chumbani kwa mwanmke huyo. Kamanda Amata akampa ‘go ahead’. Chiba akapekua hapa na pale, akainua hiki na kile, katika meza moja akakutana na kadi sakima ndogo kabisa ‘micro chip’ akaitazama kwa mahaba na kuichukua kwa uangalifu mkubwa, akaipachka katika simu yake na kuhamisha mafaili yote katika simu hiyo, kisha akaichomoa na kuirudisha mahala palepale. Akafungua moja baada ya jingine kusoma japo vichwa vya mafaili hayo. Lakini wingi wake haikuwa rahisi kumaliza yote hayo. Akaendelea kupekua hapa na pale na ndipo akakutana na begi moja dogo, alipolifungua, akakutana na nwele bandia kama sita hivi za aina tofauti na midomo bandia, nyusi, kope mpaka mboni za macho.
Mshenzi huyu, ndo maana anatusumbua si ajabu hata wanaume wake nao hujibadili! Akawaza na kuviacha kama alivyovikuta. Katika kuendelea kupekua pekua hakukuta kitu zaidi, akaamua kutoka ndani ya chumba kile akakifunga na kurudi kaunta.
“Ah mara hii?” yule kijana akauliza.
“Hapana, nitarudi muda si mrefu kuna vitu nachukua nje hapo,” Chiba akajibu huku akielekea garini, akawasha na kuondoka. Akiwa njiani akaegesha mahala na kuchukua simu yake.
Inawezekana kuna faili za kushughulikia haraka kabla sijafika mjini! Akawaza, kisha akafungua ile simu na kupekua mafaili mengi mengi, lakini haya hakuwa na mvuto nayo ijapokuwa yalikuwa ni ya mipango mingi mingi tu. Katika karibu na kukata tama akakutana na faili moja lililoandikwa Magnum 22, kwanza akalipuuza, lakini baadae, akaamua kutazama nini kilichopo ndani yake. Hakuamini macho yake, taarifa za mipango yote ya mauaji zilikuwa humo, ijapokuwa hazikueleza mengi yaliyopita, ila zilieleza mpango mkakati wa mauaji ya Dar es salaam, na wakati gani wa kufanya mauaji hayo. Chiba alihisi jasho likimtiririka kwapani, lakini kilichompa faraja ni kuwa wauaji wanasubiri hatima ya mktano huo ndipo wauae endapo ombi lao litakuwa limekataliwa. Akaitupa simu yake kitini na murudisha gari barabarani kisha akaondoka kwa kasi sana kuelekea mjini. Akatazama saa yake, tayari ilitimu saa sita kasoro robo, akainua simu yake na kumpigia Amata.
“Nakupata Chiba!” Amata akaipokea.
“Mkutano umefikia ratiba gani sasa?” akamuuliza.
“Wapo kwenye speech ya mwisho, Mkuu wa Nchi anashukuru ugeni huo…” Amata akajibu kwa kuwa hata yeye alikuwa akisikiliza kupiti chombo maalumu, na hakuwa mbali na eneo hilo.
“Agenda ya Somali Land, imetengwa au la?”
“Chiba mbona unaniuliza maswali ambayo yananitatanisha?” Amata akaongea kwa ukali.
“Just nijibu…”
“Imekataliwa, na wamesema haiwezekani kuwa hivyo!” Amata akajibu.
“Sasa….”
“Chiba kikao kimeisha, ngoja nicheki nini kinaendelea…”
“TSA 1 muuaji atatumia Magnum 22 mpango wao ni kumdungua Rais wa Gambia kutokea juu ya ghorofa la TPSA, wakati wa kupiga picha ya pamoja,”
“What? Chiba!” Amata akaita huku akifungua mlango wa gari na kuubamiza, akainua macho kutazama ghorofa lile, hapo ndipo akagundua kuwa ni kweli kutoka juu ya jingo hilo unaweza kumpata kirahisi mtu akiwa katika mlango mkuu wa ukumbi ule.
* * *
Kwenye gari ambalo ndani yake kulikuwa na Fredy na Martin, walikuwa wakipata kila kitu kutoka katika mkutano huo. Amanda kutoka ndani ya ukumbi wa mkutano alikuwa akiwapeperushia mawasiliano yote, kila kilichokuwa kikizungumzwa na kuamuliwa. Mara baada ya agenda za mkutano kwisha, ikafuata hotuba fupi ya shukrani kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama mwenyeji kuwashukuru wageni hao. Ni wakati huo Gina alipokuwa tayari kamhisi mwanamke yule aliyejipachika katikati ya wanahabari wa kimataifa, aliporudisha macho tena, hakumwona. Gina akahisi kupata ganzi na tayari viongozi walikwishamaliza mkutano, sasa walikuwa wakipeana mikono tayari kwenda nje kwa ajili ya picha ya pamoja.
“Wamekataa, hatuna budi kutekeleza tunalopaswa,” Fredy akamwambia Martin.
“Umeona mwenyewe jinsi jamaa wanavyotuandama, wamegundua nyayo zetu, tunapotoa mguu nao wanakanyaga…”
“Sekunde tano mbele yao tupo salama, na hakika hizo tano tutakamilisha kila kitu…”
“Amanda!”
“Nimeshamwambia jinsi ya kutoroka…” Fredy bakajibu.
Martin akateremka garini na mkoba wake, akavuka barabara na kulipita jingo la kwanza kisha akaingia lile la pili la TPSA, akaingia kwenye lifti na kwenda juu kabisa, huko akakiendea kibanda kidogo ambacho kilikuwa na mitambo yote ya kuongozea lifti hiyo, akaiharibu na kuzima umeme ndani ya jingo hilo. Harakaharaka akafungua mkoba wake na kuchomoa vipande vitatu vya bunduki, akaviunganisha kwa haraka na kuiweka tayari, risasi moja akipachika ndani ya bunduki hiyo, Magnum 22 riffle, akafyatua miguu yake na kulala chini kimya huku akijifunika tambara ambalo lilifanana rangi na sakafu ya eneo hilo na kuruhusu mdomo tu wa buduki kutokeza nje. Jicho lake likiwa tayari kwenye lensi yenye nguvu kabisa alikuwa akiwaona viongozi wale wakitoka nje huku ulinzi maduhubuti ukiwa umewazunguka. Kila alipojaribu kumuweka kwenye shabaha yule anayemtaka watu walikuwa wakipita hapa na pale na kumpoteza shabaha.
“Shabaha ngumu Fredy!” Martin akamwambia Fredy kwa chombo chao cha mawasiliano.
“Five seconds Martin,” Fredy akamjibu.