Logikos
JF-Expert Member
- Feb 26, 2014
- 12,513
- 19,569
Utangulizi
Maisha matamu sana, haya ni maneno ambayo nisingeweza kuyatamka miaka ishirini iliyopita, sikujua cha maisha wala uzuri…, na si mimi tu wengi tulikuwa kwenye dhahama hizo…Nasogea kwenye bustani na kuketi napigwa na upepo mzuri naona wanafamilia wakitembea kutoka makwao kuelekea sokoni kwa ajili ya matumizi yao… kwa mbele kidogo naona vijana wanasubiri usafiri (kuna basi la umeme linapita kila baada ya dakika tano) ili waelekee sehemu ya uzalishaji kujipatia kipato chao…, ingawa ni saa kumi na mbili jioni lakini katika huu mji uzalishaji hufanyika kwa masaa 24.
Naangalia kwa mbali nyumba yangu ninayoishi, sio mimi tu kila mkazi wa hapa anayo makazi, majengo ya nyumba ni ghorofa nne zenye nyumba nne kwenye kila ghorofa yaani jumla nyumba 12 kwa kila jengo.
Nyumba na mazingira ni masafi…, lazima yawe masafi ukizingatia kuna watu wa kufanya usafi na kwa kufanya hivyo wanajipatia kipato… Hizi nyumba (apartment blocks) kwa haraka haraka unaweza kudhani ni makazi ya watu pekee, lakini ukiangalia kwa karibu ni viwanda!!! Kwenye kila jengo kwa juu kuna solar panels zinazokusanya nishati ya jua, kila tone la mvua ikinyesha pia linakusanywa na kuhifadhiwa kwa matumizi, vyoo vyote vya nyumba zote vimeunganishwa na uchafu wake unapelekwa sehemu unahifadhiwa kwa muda na baadae unatumika kama mbolea kwa mazao yasiyo ya chakula yaliyopo huko nje ya huu mji ambao umezungukwa na miti ya misitu.
Kila nyumba ina sehemu za kutupia uchafu tofauti tofauti baada ya matumizi, wasafishaji hupitia huu uchafu na mabaki ambayo mwisho wa siku hutumika tena kutengenezea bidhaa nyingine yaani kwa ufupi kila uchafu wa kitu kimoja ni malighafi ya kingine.
Maji ya kuoga na kusafishia vyombo na nguo nayo hayapotei bure ndio haya yanamwagilizia hizi bustani na haya maua ambayo yananiburudisha hapa nikiwa nimepumzika… Aahh Maisha Matamu sana.
Kwa mbali naona migahawa ya kutosha nikitoka hapa niende nikajipatie mlo wangu, sina tatizo wala woga wa kulala njaa au kukosa milo mitatu nina bili ya chakula bora kwa mwezi mzima…, aahh huenda ukasema sasa si ni gharama kwanini usipike mwenyewe lakini utagundua kwamba gharama ya kula nje ni ndogo kuliko hata kujipikia…
Ninachukua simu yangu na kuangalia ukurasa wa kazi kwa mwezi huu ili niweze kupata kipato changu cha dola 600 nilitakiwa nifanye kazi kama masaa 30 tu kwa mwezi yaani kama lisaa limoja kwa siku, ila mimi niliamua kufanya kwa wiki sasa nimepumzika. Nina wiki kama mbili za kupumzika mke wangu yeye nadhani ameamua kufanya kidogo kidogo.
Watoto wangu wawili wote wapo Chuo baada ya kumaliza Sekondari ambapo walisoma na kupata elimu ya vitendo, ingawa elimu sio bure lakini gharama zote zinatoka kwenye kipato changu na mke wangu. Nina nyumba ambayo tumekuwa tukiilipia kutoka kwenye vipato vyetu. Nimeshamaliza mkopo wa hiyo nyumba ambao haukuwa na riba. Nadhani baada ya miaka mitano nitastaafu, mafao yangu ya uzeeni yatanipatia stahiki zangu zote za kuweza kuishi, na nyumba ambayo tumeshailipia tukiamua mimi na mwenza wangu tunaweza kuiweka sokoni ili jiji liweze kuinunua sababu nitakuwa na uamuzi wa kuhamia kwenye nyumba za wazee wanzangu ambapo kuna uangalizi mzuri zaidi.
Naangalia watoto wakiwa kwenye baiskeli zao wanaendesha huku wakifukuzana kwa furaha… kwa mgeni wa huu mji anaweza kushangaa kwa kutokuona magari wala parking nje ya nyumba zaidi ya vituo vya mabasi!!! Sio kwamba hakuna magari kwenye huu mji bali magari yote yanapaki nje ya mji yaani parking zipo nje na hayaruhusiwi kuingia ndani kuepusha msongamano. Hapa mjini barabara ni za watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na mabasi ya jamii.
Ukizingatia huu mji wa watu takribani elfu 50 wenye nyumba za makazi 833 na familia 10,000. Umbali wa kutoka kwenye nyumba ya mbali kabisa mpaka katikatika ya mji ni mwendo wa kutembea au kuendesha baiskeli basi utaona hakuna haja ya kutegemea usafiri binafsi wa gari, ukizingatia mabasi yanapita kwenye barabara nje ya kila nyumba kila baada ya dakika tano…. Kweli Maisha ni Matamu Sana…
Sio kwamba kwa wapenda magari hawana wala hawawezi kupata, bali kwenye sehemu ya kutokea na kuingilia mjini kuna parking ya magari kila mgeni au mwenye gari huyapaki huko na sio kuingia nayo mjini, vilevile kuna mpango wa kukodi magari. unachagua gari lolote unalotaka na unaweza kulikodi na kulitumia iwe kwa masaa, siku miezi au muda wowote ule na Jiji ndio linahakikisha ufanyaji kazi na ufanisi wa hilo gari.
Natembea polepole kuelekea kujipatia mlo wa jioni, nilishapiga simu nadhani leo natuchukua take away nikalie nyumbani au sijui nimpigie mke wangu na watoto tukutane huko huko tukapate chakula..., ngoja nitawauliza tufanye maamuzi.
Nadhani hapa unaweza ukashangaa iweje Machinja mimi Masikini naongelea utajiri huu mkubwa wa kwangu na jamii yote hii inayonizunguka ?
Kupata majibu inabidi nirudi nyuma miaka kadhaa, nikikumbuka kweli nilikuwa nimekata tamaa! Nilikuwa Machinga Masikini katika lindi la masikini wenzangu, Nilikuwa sina kipato cha uhakika, nafukuzwa kila kona, sina makazi wala malazi, bila mafao ya uzeeni sikujua nikizeeka nigekuwa mgeni wa nani, nguvu zangu ndio zilikuwa mtaji wangu na lishe yangu duni ilikuwa ni suala la muda tu kabla hata nguvu hazijanitupa mkono.
Itaendelea...
Get Your Free Copy