mzaramo
JF-Expert Member
- Sep 4, 2006
- 6,371
- 5,183
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
NA: George Iron Mosenya
"Nimekosa magoli zaidi ya 9000 katika maisha yangu, nimepoteza mechi zaidi ya 300 katika maisha yangu, niliaminiwa mara 26 kuwa nitaipa timu yangu ushindi lakini nikashindwa. Nilishindwa tena na tena na tena katika maisha yangu NDIO MAANA NIKAFANIKIWA- Michael Jordan, mchezaji wa zamani wa mpira wa kikapu."
NA HII NI SEHEMU YA KWANZA
HALI haikuwa shwari katika kota za polisi maeneo ya Mabatini jijini Mwanza,shida ya maji ilisababisha baadhi ya maaskari kwenda kazini pasi na kuiloweka miili yao panapo maji. Umeme nao uliwalazimu wengi wao kuzipiga saluti huku nguo zao zikiwa hazijanyooshwa.
Hii haikuwa shida sana kwa kundi kubwa.
Majira ya saa tatu kasorobo gari la maji liliwasili, lilikuwa ni agizo la serikali baada ya vilio kuwa vingi kutoka kwa wafanyakazi hawa watiifu.
Akina mama wakatoka nje na kuikimbilia ile gari na kujikuta wameunda foleni ya kutisha huku kila mmoja akimuhimiza mwenzake asiruhusu mtu kuingia mbele yake kwani kila mmoja ana haraka na anayahitaji sana hayo maji.
Kama ilivyo ada, panapo shida ustaarabu husafiri kwenda mbali.
Akinamama watu wazima walikuwa wakipigana vikumbo haswa, huyu anamsukuma mwenzake aliyesukumwa naye anasukuma.
Ilikuwa ni vita ya kimyakimya.
Mwanamke mmoja mkimya alikuwa anatokwa jasho kutokana na kusimama muda mrefu katika ile foleni. Alikuwa akiitumia kanga yake kujipangusa lile jasho huku moyoni akilaumu sana kampuni inayohusika na usambazaji maji jijini humo kutokana na kushindwa kurekebisha tatioz hili lililoendelea kudumu hadi kwa siku kumi.
Wakati anapanga foleni mbele yake walimtangulia watu wasiopungua thelethini, lakini sasa walibaki takribani saba. Akapata ahueni na tumaini jipya likazaliwa katika moyo wake wa subira.
Macho yake yakiwa yanatazama mbele muda wote mara akagutushwa na mguso wa kusisitizwa katika bega lake. Akageuka...
"Naomba unijazie hizi ndoo mbili foleni yako ikifika." Sauti kavu ya kike ikamweleza, akashindwa kuelewa kuwa lilikuwa ombi ama amri.
"Mama, nenda ukapange foleni tafadhali." Akajibu kwa mkato kisha akapiga hatua mbele baada ya foleni kusogea.
"Kwani ukinijazia utapungukiwa nini, watu wengine wana roho mbaya kama nini... ndoo mbili tu!" Mama mtaka kutekewa maji akabwatuka.
"Kha! we shangazi vipi, we mwenzetu ushakoga unanukia pafyumu hapa, sie twanuka jasho halafu unataka urahisi tu. Ebwaneee kapange foleni huko..." Sasa mwanadada akajibu jeuri.
"Na nitachota kabla yako, malaya mgeni wewe..." Akabwatuka huku akiondoka zake kama aendaye kupanga foleni.
Yule binti akatamani kuendeleza shari lakini mmoja kati ya wanawake waliosikia mtafaruku huu akamwonya kuachana na ile shari.
Akatii!
Baada ya dakika mbili anamwona yule mama akiongoza njia kuelekea katika bomba.....
Macho yakamtoka pima asiamini kuwa ni kweli yule mama mnukia manukato anachota kabla yake, hasira zikajijenga katika moyo na kichwa chake.
Kweli akateka ndoo mbili. Akajitwika moja kichwani na nyingine ikaning'inia katika mkono wake wa kuume. Kisha kusudi kabisa akajipitisha mbele ya hasimu wake ambaye alikuwa akisota bado katika foleni.
"Kinyamkera utangoja mpaka miguu izame tumboni..." Neno chafu likamtoka yule mama.
Uvumilivu ukampiga chenga mwanadada akachomoka katika foleni akamvamia yule mama, ndoo ikamtoka kichwani na ile ya mkononi ikatua chini.
Ukafuata ugomvi mkubwa kati ya mama mtu mzima na mwanadada. Mwanadada alikuwa hodari akamrarua vyema yule mama mtu mzima huku akimpa zawadi ya kapu la matusi.
"Wewe Janeth wewe.... mke wa Inspekta huyo. Mungu wangu eeh! umefanya nini sasa... ungevumilia Janeth. Tumeshamzoea huyu hapa kota mbona sisi... ndo tabia zake."
Janeth akabaki kuduwaa, yaani kuwa mke wa inspekta ndo awe na tabia kama hizo. Janeth hakuwa akielewa sawa juu ya hivyo vyeo, kwake ikawa kama ndoto tu.
Baada ya saa moja kupita askari wawili wakafika kota za polisi mabatini wakamkamata Janeth ambaye alikuwa akiishi peke yake kwa wakati huo baada ya kaka yake ambaye ni askari kusafiri na mkewe kwenda kijijini.
Akawekwa rumande kwa siku nne!
Ilikuwa ni mara yake ya kwanza, hivyo aliteseka mwili na akili.
Alitoka akiwa amekonda mno.
Akapewa onyo kali juu ya kosa lake la kumshambulia mke wa Inspekta.
_____
KILA aliyekuwa nje alimwona Janeth alivyokuwa anapepesuka, kijana mmoja akawahi kumpokea tofauti na wengine waliobaki kusikitika bila kutoa msaada.
Akamfikisha hadi ndani, akatoka nje na kumletea maji ya kuoga, kisha akamkaribisha chai.
Baada ya huduma hizi Janeth akachangamka kidogo. Wakazungumza mawili matatu kisha kijana akajitambulisha wakati anataka kuaga.
"Naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu"
"Lipi jina lako, Konstebo ama Martin. Maana umeanza Martin ukasita kisha ukaanza na Konstebo...." Janeth akahoji.
Martin akatokwa na tabasamu hafifu kisha akamfafanulia Janeth kuwa Konstebo sio jina bali ni cheo katika jeshi la polisi.
Hakumweleza kuwa ni cheo cha chini kupindukia...
______
JIJINI Dar es salaam hali ya hewa ilikuwa tulivu lakini joto halikutoroka liliendelea kuweka kambi jijini humo.
Joto hili halikuyaathiri maji ya bahari ya hindi, hivyo watu walijazana katika fukwe mbalimbali kwa ajili ya kupambana na joto hili linalokera.
Katika ufukwe maarufu wa Koko mamia walikuwa wamejitosa katika maji wakijaribu kuzisahau shida zao kwa kuogelea.
Kijana mmoja alikuwa pembezoni akitazama watu wanavyoshindana kuyakata mkaji kwa mbwembwe. Alifurahia kutazama zaidi kuliko na yeye kujumuika katika maji yale.
Si kwamba alikuwa hajui kuogelea la! Maamuzi tu...
Na vile alikuwa mgeni jijini Dar hakutaka kuleta ujuaji aje aibiwe nguo zake aishie kudhalilika kwa kutembea nusu uchi na nguo za kuogelea barabarani.
Wakati anaendelea kutazama waogeleaji hakuacha kuangaza fahari nyingine ya macho.
Mabinti warembo wa Dar es salaam!
Alikiri kuwa hayakuwa maneno matupu, ni kweli ni warembo mno. Urembo ambao unaweza kusababisha mwanaume kukiuka viapo vyake....
Katika kutazama vivutio hivi likapita kundi la watu watatu. Mwanaume mmoja na wanawake wawili.....
Akaisikia sauti ambayo haikuwa ngeni sana katika masikio yake. Akasimama wima na kuanza kufuatilia kundi lile ili aweze kuona ni nani anayezungumza sauti ile.
Akaongeza mwendo na kulifikia lile kundi. Kishya akapiga moyo konde na kuwasemesha....
Wakasimama!
"Samahani.... kuna sauti naifananisha kati yenu." Akarusha kete yake.
Wakacheka!
"Ehee! sauti yako dada, si ngeni kabisa katika masikio yangu. Sijui kama tumewahi kuonana..."
"He! kaka, wenzako wanafananisha sura wewe unafananisha sauti, utajuaje labda uliisikia kwenye Televisheni ama huduma kwa wateja..." Akajibu kwa nyodo kiasi.
"Au ndo yaleyale anayoyasema mama yenu... mnafanana misauti hiyo hatari..."
"Eti kaka labda ulimsikia Zubeda ukadhani ndo mimi..." akajazia dada yule mrefu na aliyeumbika vyema hasa hasa miguu yake.
"Mimi naitwa Nguzu, Martin Nguzu. Sijui kama umewahi kulisikia jina hili." Akajaribu kujitambulisha huenda atakumbukwa.
"Samahani kaka, sijawahi kusikia hilo jina hakika." Alijibu kiupole.
"Labda umewahi kukaa Mwanza. Huku Shamaliwa, Igoma ama Nyegezi..." Alizidi kutafuta uthibitisho.
"Mh! kaka huyo mtu unamdai ama maana si kwa kulazimisha huko. Huu ni msako haswa..." Dada wa pembeni akachombeza.
"Hebu ngoja, kwanini tuandikie mate...." Dada aliyefananishwa akasema kisha akachukua simu yake akabofya na kuweka sikioni.
"Eh! Da Zuu kuna mtu kakufananisha huku...." Aliongea huku anacheka.
"Anaitwa Zungu sijui nani..."
"Naitwa Nguzu..." alirekebisha upesi Martin.
"Anaitwa Nguzu, hebu ongea naye bwana. Maana alivyotuganda looh!" Akampasia simu Martin Nguzu.
"Habari, naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu..." Akafanya utambulisho kama alivyowahi kufanya jijini Mwanza kwa mwanadada aitwaye Janeth lakini huyu wa sasa ni Zubeda.
Maongezi yalichukua takribani dakika moja kabla simu haijarejea mikononi mwa dada aliyefananishwa.
"Ndiye.." akashusha pumzi martin huku akitabasamu.
"Kumbe ni askari looh! ningeshangaa mlugaluga tu aje kuhangaika na watu asiowajua." Hatimaye yule mwanaume akazungumza. Mwanaume aliyekuwa pamoja na mabinti hao.
"Amesema nikupatie nambari yangu umtumie sasa hivi anipigie." tabasamu halikujipa likizo katika midomo yake pindi alipokuwa akiyatamka hayo.
Ikawa hivyo. namba ikatumwa lakini hakupigiwa simu...
Usiku wa saa nne simu yake ikaita...
Alikuwa ni Janeth ambaye kwa sasa anajulikana kwa jina la Zubeda.
Ni miaka mitatu ilikuwa imepita tangu waonane mara moja tu jijini Mwanza. Wamekutana tena jijini Dar es salaam!
Maisha ya Martin yalikuwa tulivu bila ubaya na mtu.
Huenda yangedumu katika utulivu huu kwa miaka mingine mingi, lakini kukutana na Janeth aitwaye Zubeda kwa sasa ikawa ni safari nyingine ya kutisha!