Riwaya konki: Adili na Nduguze

Riwaya konki: Adili na Nduguze

SURA YA 8.

Mrithi wa Mji wa Mawe


Baada ya kwenda mbele hatua chache Adili aliona mlango mdogo. Kizingitini pake palikuwa na ngazi iliyoongoza juu. Alipopanda vidato vichache aliona dalili za mtu au watu walioishi mle. Kwanza alikuwa akipanda kwa kusitasita, lakini sasa dalili zile zilimvuta akafululiza kupanda. Aliendelea mpaka orofani. Alifuata zilikoongoza dalili mpaka akafika kulikokuwa na chumba kidogo. Mlango wake ulikuwa wazi, kwa hivi aliingia ndani. Huko aliona pazia la hariri lililotariziwa kwa vito vya dhahabu, lulu na yakuti linaning'inia mbele yake. Fusuai hizo zilimeremeta kama nyota. Dalili alizoona ziliendelea nyuma ya pazia hilo. Alijipa moyo mkuu akafunua pazia. Alipofanya hivyo macho yake yaliona mlango wa tarabe.


Mlango huo ulikuwa mzuri sana. Mbao zake zilikuwa za mpingo, nazo zilinakshiwa kwa johari na pembe. Mtu yoyote angaliona mlango huo angalistaajabu sana. Adili alibisha hodi akaingia katika chumba kikubwa. Chumba chenyewe kilikuwa kimepambwa vizuri sana. Katikati yake palikuwa na meza na kiti. Msichana wa fahari alikuwa amekaa kitako pale juu ya kiti. Usonwake ulikuwa umetukuka. Kwa uzuro uliokuwa haumithiliki. Bila shaka yeye alikuwa malkia wa wazuri katika dunia nzima. Libasi alizovaa zilikuwa nzuri na za thamani kubwa sana. Katika miji yote mingine aliyopata kufika katika safari zake, Adili alikuwa bado kukutana na mtu yeyote mwingine aliyevaa libasi nzuri kama zile.


Kama uzuri ulio peponi wamejaaliwa malaika; karibu uzuri wote ulio duniani alijaaliwa msichana huyo. Uzuri wake ulikuwa haulingani kwa uzuri na mwanamke mwingine yeyote aliyesifiwa kuwa mzuri katika zamani zake. Msichana mwenyeww alikuwa anasoma kitabu kitakatifu. Matamko yake yalikuwa kama mafuatano ya muziki. Moyo wa Adili ulitekwa na mapenzi ya tamasha hiyo. Akili yake ilipotea na nuru ya macho yake ilizimika kitambo. Ile ilikuwa mara ya kwanza mshale wa mapenzi kupenya moyoni mwake. Ulipenya katikati ya moyo wake. Haukuacha nafasi ya mapenzi ya mwanamke mwingine. Licha ya Adili hata mtu mwingine aliyekuwa hajui mapenzi angalikutana na mwanamke huyo moyo wake ungalitekwa pia.


Akili ya Adili iliporudi alimwamkia mwenyeji wake. Mwenyeji aliyeamkiwa hakuitikia tu, lakini alitaja jina la aliyemwamkia vile vile akamkaribisha kwa furaha. Adili alimwuliza alilijuaje kina lake, yeye alikuwa nani na miujiza gani iliyopita pale hata viumbe wa mji mzima wakageuka mawe. Bila ya kusema neno msichana aliondoka akaenda kuchukua kiti. Alikiweka karibu yake akamwomba Adili kukaa kitako. Mwendo aliotumia katika kwenda na kurudi wakati wa kuchukua kiti ulichukua pumzi zoye za Adili. Alikwenda kwa hatua za kupendeza , na mikono yake ilipunga kama upepo. Uzuri wake wa fahari ulikuwa na madaha makubwa. Chumba chake kilikuwa kama mahali pa faraja panapotafutwa na wanadamu.




Miguu ya msichana

Na mwendo aliokwenda,

Adili alipoona

Moyowe ulimshinda.


Alikuwa na miguu

Mfano wa charahani,

Wala ulimwengu huu

Hajatokea kifani.


Alipendeza hatua

Wakati alipokwenda,

Chini viatu vyalia

Mithali kama kinanda.

Alikwenda kwa madaha


Mwanamke mwenye enzi,

Yaliyompa furaha

Kila mwenye kubarizi.
 
Dhuluma kubwa ni kukosa kunitag kwenye mwendelezo huu, nilikuwaga nasikia tu ADILI NA NDUGUZE wala sikutaka kujisumbua kujua inahusu nini.... sasa nimeshikwa na nitanunua kitabu wasome wanangu kwa lazima.
 
Dhuluma kubwa ni kukosa kunitag kwenye mwendelezo huu, nilikuwaga nasikia tu ADILI NA NDUGUZE wala sikutaka kujisumbua kujua inahusu nini.... sasa nimeshikwa na nitanunua kitabu wasome wanangu kwa lazima.
Utakuwa umefanya vema sana mkuu. Hii riwaya ina mafunzo muhim mnoo ukiisoma kwa utulivu utastaajabu mwandishi alivyo mbunifu kwa kiwango cha kustaajabisha kabisa.
 
Natenga laki 4 nitakuja Dar mwezi wa 8 hiyo ni kwa ajili ya vitabu tu awamu ya kwanza.
 
SURA YA 9

Mji Ulivyogeuka Mawe


Sasa msichana alieleza kwamba yeye alikuwa binti mfalme, na jina lake lilikuwa Mwelekevu. Baba yake, Mfalme Tukufu alikuwa yule aliyeonekana kitini katika halmashauri ya madiwani wanaume. Mama yake, malkia Enzi, alikuwa yule aliyeonekana katika halmashauri iliyohudhuriwa na madiwani wanawake. Ufalme wao ulikuwa na utukufu na nguvu nyingi. Labda dola yao ilikuwa ya kwanza duniani iliyokuwa na miji laki moja. Isipokuwa, Fahari, mji uliogeuka mawe, miji mingine ilizama baharini. Raia chini ya bendera yao walikuwa lukuki. Mawaziri walikuwa laki tano. Kila waziri alikuwa na umati wa watu. Amirijeshi mmoja alikuwa na majemedari elfu moja na sufufu ya majeshi. Hazina za nchi zilikuwa na mali zisizohesabika kama machimbo ya Tanganyika.


Ulimwengu uliajabia dola yao kwa ushujaa wa askari na kwa busara ya mawaziri wao. Walakini, juu ya sifa hizo, mfalme, malkia na raia walikuwa waabudu mizimu. Mizimu yao ilikuwa miti. Miti yenyewe ni ile iliyogeuka mawe ukutani. Kabwere, Mganga na imamu wa mizimu hiyo alivuta mioyo ya watu wote. Siku moja asubuhi mfalme na malkia walikwenda katika halmashauri zao, kila mmoja akakaa juu ya kiti chake. Madiwani walikuwa wamewazunguka kabla ya kuanza kazi zao za desturi; mtu mmoja ambaye hakujulikana alikotoka alisimama ghafula mbele ya mfalme akajitangaza kuwa aliitwa Mrefu.


Mrefu alikuwa mwujiza katika viumbe. Alikuwa na miguu mikubwa na mapaja manene, kiuno cha utambo na kifua kipana na shingo yake ndefu ilichukua kichwa kikubwa. Mabega yake ya mraba yalining'iniza chini mikono iliyokuwa na nguvu kama manjanika. Kwa kimo cha kukithiri alitembea baharini bila ya kuguswa na maji magotini, akafikia vilele vya milima kwa mikono yake. Aliweza kukamata ndovu chini au nyangumi baharini akamwoka kwa jua mbinguni. Sauti yake ilikuwa kama radi kwa wepesi wake wa ajabu wa kuzunguka dunia nzima kwa sekunde moja, alionekana kama kiumbe kilichoumbwa maalum kuokoa kitu motoni, baharini au katika hatari nyingine.


Mrefu alimwambia Tukufu kuwa mfalme ni naibu wa Mungu duniani. Kwa hiyo , ufalme ni amana kubwa. Amna hiyo ilitaka uangalifu mkubwa kwa sababu ni dhima bora iliyowekwa mikononi mwa wanadamu. Wajibu wa kwanza wa mfalme ni kuwa mwadilifu katika matendo yake. Kila tendo, jema au baya , ni mfano kwa raia wake. Kwa sababu ya maisha ya milele ibada ya mizimu ilikuwa maangamizi , na uimamu wa kabwere ujinga mtupu.


Tukufu alimtazama msemaji akasema kwa ukali, "Nini kilichokujusurisha kusema upuuzi, Mrefu? Kama kwa sababu ya urefu ubongo wako umeyeyuka kwa jua, kaa kitako chini ya kivuli cha mizimu yetu utaburudika. Kama umerogwa, Kabwere atawakomesha waliokuroga. Riziki ya wanadamu hutoka mimeani. Kwa sababu hiyo, mimi na kaumu hii twaabudu miti. Funga ulimi wako, bwana. Usipofunga hasira ya mizimu itakuwa juu yako. Tafadhari jiokoe."


Mrefu alionya , "Hapana haja ya jibu la haraka. Tumia wakati upendao wa kufikiri. Nimesema neno la Mungu. Mungu hachelei tisho la mwanadamu, kazi ya mikono yake mwenyewe. Neno takatifu gumu kufahamika, lakini lina tija kwa wajisumbuao kulifasiri. Kila msaada nitakupa wa kulifasiri."


Tukufu hakujali onyo hili akaamrisha kushikwa kwa Mrefu aliyekuwa hasogeleki wala hashikiki. Uwezo usio hadhari ni kileo kibaya sana. Siku ile ilikuwa ya tisho na msiba, ole na maangamizi makubwa. Kwa laana iliyotamkwa na Mrefu, miji mingine yotw ya dola hii iligharika, na kila kiumbe kilichokuwa na maisha katika Fahari kiligeuka jiwe.


Hili lilipotokea Mwelekevu alikuwa darini anachungulia nje kwa dirishani. Toka pale aliweza kumwona Mrefu na kusikia maneno yake. Hakupendelea kushindwa kwa baba yake. Hapana mtoto apendeleaye hili . Walakini, mapendeleo yakiachwa mbali, nuru ya fikira humulika mno siku zote juu ya kweli kuliko uongo, na juu ya haki kuliko dhuluma. Nuru hii ndiyo iliyomwokoa Mwelekevu katika maangamizi yale ya kutisha. Na tangu siku ile aliamini kuwa onyo la bure likikataliwa huleta majuto ya milele.


Hayo yalipokwisha jiri Mrefu alimpa binti mfalme chuo kitakatifu alichomsifia kuwa bora kuliko vitabu vyote vya duniani vikichanganywa pamoja. Kwa matumizi mengine, Mrefu aliomba mkomamanga uote. Mkomamanga huo ulizaa komamanga moja kila siku. Kila chembe katika komamanga hilo ilikuwa chakula na kinywaji mbalimbali. Kwa mti ule wa ajabu binti mfalme aliweza kuishi maisha ya faraja. Mwisho alionywa kuwa siku ya kuona mti ule umezaa matunda mawili ajue Adili, mwokozi wake amefika. Hilo ndilo lililomjulisha siku ile kuwa mgeni wake alikuwa si mtu mwingine ila Adili.


Usemi wa binti mfalme ulimwonyesha Adili kuwa turufu huenda kwa mchezaji siku zote. Laiti asingalikwenda wenziwe walikoogopa akatafuta tafuta asingalikutana na bahati ambayo hakutazamia kuja katika ndoto zake . Alishukuru akamchukua binti mfalme pamoja na tunu bora alizoweza . Katika tunu zake yalikuwemo pia makomamanga mawili ya ajabu. Hayo yalikomesha kiu na njaa katika merikebu yao kwa muda wa siku kadha wa kadha.


Adili aliyageukia manyani akayauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea. Manyani yaliziba nyuso zao kwa viganja vya mikono yao kwa aibu.
 
SURA YA 10

Kutoswa kwa Adili


Nahodha na mabaharia walimshangilia Adili kama mtu wa bahati ya peke yake, na kuwa mtu mwingine yeyote kati yao angalifuatana naye kwenda walikoogopa , asingalikutana na bahati ile kubwa. Adili aliwashukuru wote akisema kwa furaha mkulima alikuwa mmoja siku zote, lakini walaji wengi. Pato lake lilikuwa pato lao vile vile.


Aligawa tunu zake katika mafungu manne yaliyokuwa sawasaw. Fungu la kwanza alimpa nahodha, na kila ndugu yake akapata fungu moja. Fungu lililobaki lilikuwa lake mwenyewe. Hili aliligawa tena katika mafungu mengi, kila baharia akapata sehemu yake. Isipokuwa ndugu zake, watu wote chomboni walishukuru wakamwombea heri. Nyuso za ndugu zake zilionekana zimekunjamana na macho yao yaliiva. Alifahamu hawakuridhika kwa sababu ya choyo chap kikubwa.


Aliwataka radhi akawaambia kuwa ingawa mafungu yao yalikuwa madogo, lakini wao walikuwa ndugu zake. Mali yake ilikuwa mali yao katika maisha na mauti. Palikuwa hapana sababu ya kukasirika.

Wakati alipokuwa akisema na ndugu zake stahani, Mwelekevu alikuwa amekaa ngamani na jahazi inakwenda moto mmoja.

Sasa Hasidi na Mwivu walimwuliza Adili nia aliyokuwa nayo juu ya bibi yule mzuri aliyempata katika mji wa Mawe.

Aliwajibu kuwa wakifika salama janibu nia yake ilikuwa kumwoa.

Hasidi aliomba kuwa angalifurahi kama angalimwoa yeye bibi yule.

Mwivu kadhalika alinasihi kuwa angalipenda kumwoa yeye.

Kwa kusikitika, lakini kwa imara kabisa, Adili alijibu kuwa kama walitaka neno jingine lolote katika miliki yake angaliwapa, ila hakufikiri kuacha mkono wa bibi yule kuguswa na mru mwingine katika ndoa ila yeye mwenyewe. Wao walimtaka lakini yeye alimpenda zaidi. Walakini wakirudi Janibu atawatafutia mabibi wawili wazuri. Gharama yote itakuwa juu yake. Arusi zao na yake zitakuwa siku moja , fungate na furaha yao itakuwa moja.


Ndugu zake walihoji kama mume mmoja katika Afrika aliweza kuoa wake wengi, na mke mmoja katika Asia alipata kuolewa na waume kadhaa, isingalikuwa vema kama ndugu watatu wa Janibu wangalishiriki uzuri wa mke mmoja?


Adili alibisha kuwa kulikuwa na mambo yaliyofaa na yaliyokuwa hayafai kushiriki. Ndoa ilikuwa jambo moja katika yale yaliyokataa ushirika. Ushirika katika ndoa ulipasa wanyama na ndege. Mtu alitukuzwa mno kuliko mnyama. Huchukiza akiishi katika maisha duni. Ilipasa watu wa wakati ujao katika Afrika, Asia na Janibu kuishi katika maisha bora ya utu, na kuifanya dunia mahali pa kiasi, sio ulafi na uchafu. Mwanamume hakukusudiwa kuwa fahali wa kila mtamba, wala mwanamke kuwa tembe la kila jogoo.


Ushirika wa ndoa ulipofanikisha na uvundo wa kuchukiza duniani, ndugu zake walinyamaza kimya kama walioridhika, lakini moto ulikuwa ukiwaka mioyoni mwao. Usiku Adili alipokuwa amelala na jahazi inakwenda mbio kwa pepo za omo, ndugu zake walikuwa macho. Mawazo mabaya hurusha usingizi. Kuzinduka kwake usingizini Adili alijiona amechukuliwa hangahanga. Kufumbua macho aliona ndugu zake wamemfunga kifati. Mmoja alimshika kichwani na mwingine miguuni. Koo yake ilisongwa sana. Aliwauliza kwa pumzi nyembamba aliyoweza kuvuta neno walilotaka kumtendea.


Alijibiwa , "Huss, fedhuli wee! Wauliza neno ulijualo. Koma sasa! Tumesalitika na mapenzi ya mwanamke aliyeko chomboni. Tumekushauri kumwoa shirika. Umekataa. Huna budi kufa."

Alitoswa baharini kama kitu kilichokuwa hakifai.


Adili aliyageukia manyani akauliza kama yaliyosemwa yalitokea au hayakutokea. Manyani yaliziba nyuso kwa viganja vya mikono yao kwa aibu.
 
Wakuu wadau wa hii riwaya, leo nimekwama mwenye chochote anisaidie ili ninapoangalia mechi ya stars nipate japo nyama choma na kinywaji.
Namba hii 0753142156.

Riwaya hii nitaitype mpaka iishe hapa hapa jamvini.
 
Wakuu wadau wa hii riwaya, leo nimekwama mwenye chochote anisaidie ili ninapoangalia mechi ya stars nipate japo nyama choma na kinywaji.
Namba hii 0753142156.
Riwaya hii nitaitype mpaka iishe hapa hapa jamvini.
Huu nimtandao gani mkuu nijuze iliniweze kufanya mazingira kwa wakala
 
Wakuu wadau wa hii riwaya, leo nimekwama mwenye chochote anisaidie ili ninapoangalia mechi ya stars nipate japo nyama choma na kinywaji.
Namba hii 0753142156.

Riwaya hii nitaitype mpaka iishe hapa hapa jamvini.

Stars ishatoka sasa rudi kwenye mambo ya msingi, au bado umekwama kiuchumi..!!
 
Back
Top Bottom