Riwaya: Kibiritingoma

Joined
Oct 4, 2023
Posts
58
Reaction score
61

Alikuwa mrembo wa sura, mwenye umbo la kuvutia na sauti ya kuburudisha. Akawa mashuhuri kama fedha, na adimu kama almasi.

Sifa hizi, akazitumia kama fimbo, alipokutana na wanaume wenye tamaa kali ya ngono; alipokaribishwa kwenye dunia ya ukahaba.

Kisha, akakutana na huyu.
Kijana msomi, mwenye uwezo wa kucheza na kompyuta na mitandao.
Kwa pamoja, wakaanzisha biashara haramu, iliyowatajirisha kisha baadaye ikawafikisha kando ya kinywa cha mauti...

BIashara ya kuwauzia watu dhambi zao, kwa gharama yoyote waliotaka. Ni biashara gani hii?

Na kwa vipi, iwafikishe mautini?

Ungana nami kwenye mkasa huu wa aina yake, uliotungwa na mwandishi mbarikiwa, Godlove Kabati
 
KIBIRITINGOMA
Imeandikwa na, GODLOVE KABATI
Kwa udhamini wa, MAJIVU YA FASIHI
WhatsApp: 0763204351

SEHEMU YA KWANZA...



Dhamiri ni kweli.
Humsuta mtu hasa pale anapotembea njia isiyo sahihi. Humkumbusha mtu kuwa, japokuwa hajakamilika, bado anahitaji kuufukuzia ukamilifu kwa juhudi zake zote.


Jua zuri la kupendeza, lilionekana likichomoza kutokea upande wa Mashariki wa anga. Mwanga wake mzuri wa dhahabu uliufukuza mwezi ambao nao ulitii bila shuruti na kuanza kufifia mawinguni.
Ndege wa angani wakaanza safari zao za siku zote kila ilipofika mida kama hii, wakaimba na kufanya fujo za kila namna. Ni hizo fujo na kelele za nyimbo zao, vilivyowaamsha wanadamu ambao walikuwa bado wameyakumbatia malazi yao.
Kulikuwa kumekucha...ilikuwa ni alfajiri.

Naam,
Hata mwanaume huyu alikuwa mmoja kati ya wale waliokuwa bado wameyakumbatia malazi yao alfajiri hii. Yeye akiwa bado ameunatisha mwili wake juu ya godoro hili laini kwa gundi ya ajabu.
Gundi inayowatesa wale wapenda usingizi. Uzembe!
Ni uzembe tu, wenye chembechembe za uchovu, uliomfanya mwanaume huyu aendelee kujilaza kifudifudi palepale kitandani, akiwa ndani ya shuka jepesi lililokuwa na joto la haja. Sio kwamba amesinzia la! Ila kaamua tu, kulifaidi joto la asubuhi lililochanganyikana na uchovu kisha likapigiliwa msumari mzito na uvivu.
Uchovu? Kwa nini uchovu?
Usiku uliopita alikuwa na shughuli nzito mno ambayo imemfanya aendelee kujilaza palepale kivivu.
Uchovu huuhuu ukamfanya ajihisi mzito sana walau hata kujigeuza ili alale chali.
Haya, afungue macho basi ili aione dunia, akashindwa!
Badala yake akalivuta shuka na kujikunyata akijiviringa zaidi ndani yake. Ingezuka vita ya tatu ya dunia kama mtu angempokonya shuka hili muda huu.

Alizisikia kwa mbali sauti za ndege wanaoimba kwa furaha kuikaribisha siku hii mpya.
Akawaza kuhusu furaha yao,
"...Hawapandi, hawavuni na wala hawaweki ghalani lakini baba wa mbinguni huwalisha hao....je nyinyi si bora kupita hao?..." Akajaribu kurejerea mstari huu katika maandiko matakatifu.
Akasonya baada ya kugundua kuwa yeye sio ndege, hivyo hana namna yoyote ile ya kujilinganisha nao.
Kitendo cha kukumbuka kuwa amerejerea mstari mtakatifu tu, akamkumbuka Mungu,
akalikumbuka kanisa, akamkumbuka mke wake wa ndoa, akaikumbuka familia yake aliyoiacha nyumbani.
Kisha mara moja akaikumbuka shughuli nzito iliyojaa laana aliyoifanya usiku uliopita.

Naam,
Ni kwa mara ya tano sasa amediriki kutoka nje ya ndoa na kukutana na binti huyu. Kwa pamoja wameshiriki, juu ya vitanda tofauti tofauti, kwenye hoteli tofauti tofauti, katika siku tofauti tofauti—kuisulubu amri ya sita.
Akapata sononeko la moyo. Alikuwa na donda ndugu lililogoma kupona. Akamfikiria tena mke wake...hakupenda kuisaliti ndoa yake.
Lakini ukorofi na fujo za mke wake, vilivyoilizokithiri ndizo zilizopageuza nyumbani kwake kuwa kama jehanamu ndogo.
"Mama Junior!...ni kwa nini lakini?"

Akazungumza yeye na nafsi yake,
Akajilaumu peke yake,
Ameoa tayari ana mke,
Lakini bado anajihisi mpweke.


Mara akakurupushwa na rabsha ndani ya chumba kile, zilizosababisha ukelele fulani ambao haukumkera...na hapo macho yake yakakubali kufunguka.
Akajitahidi kukipindua kichwa chake, akijipindua kama nyoka pale juu ya kitanda kilichoshirikiana na joto kumshikilia asiamke.
Macho yake yakagota juu ya umbo la mwili wa kike uliokuwa umesitiriwa ndani ya taulo fupi lililolowana kiasi, likiwa limefungwa maridadi kifuani na kuacha wazi mabega yake huku likijitahidi kuyaficha mapaja laini yaliyonona na lisiweze.
"Huyu hapa huyu..."
Akatamka na nafsi yake kwa mara nyingine,
"Huyu nd'o amekuwa faraja ya moyo wangu...yaani dah! Mama Junior, umenifanya nilale na malaya?" Akazidi kujiuliza na kujijibu mwenyewe.

Ni wazi kuwa binti huyu alikuwa ametoka kuumwagia maji mwili wake. Na sasa huyu hapa ametazamana na kioo kipana kilichobandikwa kwenye kabati, amempa mgongo tu huyu mwanaume na mara binti huyu akafanya tukio ambalo lilisababisha hali ya uchangamfu pale chumbani.

Taratibu bila papara akalifungua taulo lile fupi na kubaki kama alivyokuja duniani, maungo yake yote yakabaki wazi!
Lile jotoridi pale kitandani likaanza kuongezeka. Likazidi na kuiyeyusha ile gundi yote ya uchovu. Bwana huyu akachangamka na kukaa mkao wa kula ili macho yake yasiyo na pazia yafanye jukumu lake la kila siku.

Mwili uliobarikiwa ngozi laini, ulikuwa umelowanishwa kwa tembe chache za maji. Kama embe bichi mwituni.
Rangi yake asili iliyokataa daima kueleweka kama ni nyeusi, machungwa au ile ya maji ya kunde ikaonekana iking'ara. Hii haikuwa ngozi yenye rangi bandia iliyotegemea vipodozi wala kemikali ili ing'ae.

Binti akalikamata taulo lile na kuanza kuupapasa mwili wake taratibu, akijipangusa tembe zile za maji. Alikuwa ni kama anapiga deki.
Mboni za macho ya huyu kiumbe aliyekuwa kitandani yakazidi kufuatisha tu kila kiungo kilichofikiwa na huduma ya taulo lile. Kwa kila kiungo akakifanyia uchambuzi wa kisanii.
Mwinuko wa milima miwili yenye ukubwa wa kadri iliyokuwa na bonde katikati yake, ikibebwa na mapaja manono angavu yaliyojazwa nyama na yakajazika, sambamba na miguu mizuri ya kike iliyonyimwa michubuko ya aina yoyote ile.

Hivi ni miguu tu? Akakagua tena kama kuna mchubuko au kipele chochote kile juu ya mwili wa huyu binti; Kama kingekuwepo basi kitakuwa kinapitia dhuluma na aibu ya upweke kwa kukaa mahali isiyostahili.

Kiuno chake chembamba,
Ngozi laini isiyo na magamba,
Yavutia kwa macho waweza kuilamba,
Yote hii kazi ya muumba.


Taulo lilipohamia mbele hakuweza kufanya uchambuzi wake. Na hilo likamsononesha upya.
Akapitia mateso kuamini kuwa binti huyu amemaliza kujikausha mwili wake.
"Hivi kweli huyu ndiye nilikuwa naye usiku kucha?" Akajiuliza.
Kila siku alizidi kumuona mpya kabisa machoni mwake, hakuwahi kuuzoea uzuri wake.

Binti huyu akainua mguu wake na kuuweka juu ya stuli ndogo. Taratiibu akaanza kuipakaa ngozi laini ya mwili wake mzuri kwa mafuta.
Juu ya mwili wake laini,
Mijongeo ya vidole kwa umakini,
Kajipakaa toka juu mpaka chini,
Akitazamwa tokea pale juu kitandani,
Na dume kubwa la nyani,
Kwa macho yenye huzuni.


Katikati ya miguu ya mwanaume kulikuwa na askari ambaye daima alikaa chonjo kukabiliana na hali za hatari kama hizi. Tayari alikuwa amesimama wima kwa ukakamavu.
"Amekosa nini huyu binti?"
Likawa swali gumu ambalo daima alijiuliza tangu alipomtia mrembo huyu machoni kwa mara ya kwanza. Alikuwa na urembo wa kutosha kabisa kumfanya shetani aungame makosa yake yote kisha aamini kuwa yupo Mungu anayeishi, muumba wa kila kitu kizuri.
Lakini ajabu!
Mrembo huyu ni changudoa, kahaba, malaya, dada poa ama waweza kumuita KIBIRITINGOMA!
Asingekosa mwinyi mwenye pesa za kutosha kumuoa au hata kumfanya hawara.
Ukute ana mikosi!
Au ana laana kutoka kwa wazazi wake..
Kwani ana wazazi kweli huyu?

Ilikuwa ni foleni ya maswali ambayo iliendelea kujipanga akilini mwa bwana Didas Ambrozi; mkurugenzi wa kampuni, baba wa familia, mzee wa kanisa na mzee wa busara aliye muungwana kama alivyojulikana na jamii.
Kila wadhifa aliokuwa nao, ulitosha kabisa kumfanya aone aibu kutoka nje ya ndoa na kununua makahaba. Mara mia hata angekuwa na hawara wa nje lakini kahaba?! Hakika alikuwa amepiga hatua ndefu sana ya kujitafutia aibu.

Lakini kwake yeye, aliitazama hii aibu kwa jicho la tofauti kabisa. Wakati nyinyi mnamuona huyu binti kama kahaba na changudoa, yeye alimuona kama hawara au mchepuko wa pembeni!
Kila aliposhambuliwa na vurugu na masimango ya mke wake, aliifuata faraja yake na tulizo kwa huyu binti. Alionjeshwa asali, yeye akaamua kuchonga mzinga kabisa.

Bwana Didas Ambrozi akajikohoza kidogo,
"umeamkaje Bebe." Kwa sauti yenye kitetemeshi akatoa salamu ile akiwa na matarajio kuwa labda binti huyu aitwaye 'Bebe' atamuoena aibu na kujisitiri.

Lakini haikuwa hivyo, kwa nini ajisitiri?
Hakuna alama yoyote ile ya mwili wake isiyojulikana na mwanaume huyu. Wameshakutana kimwili zaidi ya mara nne, wakibadilishana bidhaa ambazo kila mtu alihitaji kutoka kwa mwenzie.
Bebe alihitaji fedha na Bwana Didas alihitaji ladha ya tunda la mti wa katikati. Kwa Didas ikiwa ni burudani lakini kwa Bebe ilikuwa ni kazi iliyoachana kwa sentimita chache sana na neno 'biashara'!

"Salama tu Daddy...vipi wewe!" Kwa sauti changamfu iliyojaa huba, Bebe akamjibu akiwa amemtazama Didas huku sura yake ikivaa tabasamu lenye bashasha. Hapa yakazuka mafumbo mapya kabisa, yaliyohitaji uchambuzi wa kisanii.

Sauti yake ya kinanda,
Nyepesi nyororo iso na inda,
Tamu kama soda ya Mirinda,
Kutoka kinywani mwa huyu kinda,
Bwana Didas ikamshinda!


Macho yake yakagota kwenye sura yake.

Kasura kake kazurii,
Kamefinyangwa kwa umahiri,
Anatabasamu kwa desturi,
Tabasamu tamu la alfajiri,
Utataka kumtazama adhuhuri,
Hutochoka mpaka alasiri,
Si utani Bebe alikuwa zaidi ya neno 'mzuri'!


"Eeer...mi mzima! Naona leo umewahi kuamka aisee!" Akajitahidi kulazimisha tabasamu usoni mwake, akafanya jitihada za kusimama huku akimficha askari wake aliyekuwa tayari kupigana asubuhi hii.
"Mh...jamani Daddy, sa ulitaka nilale mpaka saa ngapi. Nina kazi nyingi zinanisubiri asubuhi hii mwenzioo"
Bebe akamjibu kwa sauti ileile ya madeko akianza kuvaa nguo zake za ndani moja baada ya nyingine. Mwisho akamalizia na kigauni kifupi chekundu kilichokataa katakata kuyafunika yale mapaja yake yaliyokuwa na uwezo wa ajabu wa kuamsha ashiki ya dume lolote lile rijali.

Bwana Didas akajinyoosha huku akipiga mwayo mrefu, mkono wake wa kulia ukahamia kiunoni, na ule wa kushoto ukakipapasa kitambi chake chepesi kisha akarejea upya juu ya kitanda na kuketi.
Bado macho yake yako kwa Bebe.
Umbo lake matata likijisanifu vyema ndani ya kigauni kile kilichoung'ang'ania mwili wake kwa kuubana kiasi.

Bebe akachukua pochi yake ndogo na kupiga hatua zake kwa madaha, miguu yake ikijikata kwa mwendo wa paka 'catwalk' mpaka pale juu ya kitanda na kuketi kando ya Bwana Didas.
Viganja vyake laini vikavikamata viganja vigumu vya Didas na kuanza kuvitomasa katika namna upole na kubembeleza.

"Daddy..."
Akamtazama usoni kwa macho ya kusinzia, Katika namna ya kurembua,
Kwa sauti ya kichokozi,
Akalitaja jina kwa mapozi,
Ambalo siku zote liliyapoza maumivu yote ya moyo wa Didas Ambrozi.


"Niambie mrembo..." Didas akamjibu kwa upole...tayari ameshalainishwa akalainika.
"Mi nd'o naondoka hivyo..." Soni ikauvamia uso wake akazihamisha mboni zake mpaka kwenye vile viganja alivyokuwa anacheza navyo.
Didas akashusha pumzi kwa nguvu kisha akauruhusu mkono wake wa kulia umzunguke Bebe na kumkumbatia.
"Asante sana kipenzi...umeugeuza usiku wangu wa jana kuwa sawa na sikukuu!Nimefurahi sana." Akatamka kwa mahaba huku akiusaili uso wa Bebe uliobarikiwa uzuri.
"Mmh jamani kwelii?..." mrembo akauliza kwa sauti ya kinanda.
"Haswaa...na laiti kama ningekuwa na uwezo ningekufanya mke wangu wa pili. Ni vile tu dini yangu hainiruhusu." Didas akatema cheche.
Bebe akaishia kuguna bila kusema neno. Ukimya wake ukamruhusu Didas aendelee kutumia vyema uwanja wa mazungumzo.

"Kuna swali nataka nikuulize Bebe...kama hautojali lakini." Akameza funda jepesi la mate kwa woga.
"Uliza tu"
"Uum...utaishi haya maisha mpaka lini Bebe?!" Akaweka pumziko na kumkazia macho usoni, macho yaliyohitaji majibu.
Bebe akatazama sakafu na kuufyata mdomo wake mdogo, akabaki kimya.

Didas akaendelea,
"Wewe ni msichana mrembo sana. Na najua fika kuwa hili unalijua, hata kioo ulichokuwa unakiangalia muda mfupi uliopita hakikukudanganya. Lakini ni kwanini unafanya hii biashara?!" Akamuongezea swali jingine bila kujibiwa lile la kwanza. Bado Bebe aliendelea kubaki kimya.

"Nisikilize Bebe...nataka niyabadilishe maisha yako. Huu mwili wako haukuumbwa ili uishi kwenye madanguro, nataka nikupe jumba kubwa la kifahari ukae, uishi kwa raha. Ngozi yako hii mama, haikufumwa ili ipigwe na vumbi mpenzi, wala miguu yako haistahili adhabu ya kutembea zaidi ya hatua kumi mama yangu. Nitakupa gari la kutembelea. Sipendi kukuona unaishi hivi mrembo..."
Wakiwa wametazamana uso kwa uso, Didas akiwa amekishika kidevu cha Bebe kilichochongoka kama embe. Akaendelea kumshawishi Bebe akubaliane na ombi lake la siku nyingi. Aachane na biashara hii ya kujiuza na aishi kwa kutulia akihudumiwa na yeye mwenyewe.

Bebe akayalegeza macho yake makubwa na kurembua kimahaba akauondoa taratibu mkono wa Didas kwenye kidevu chake. Akatumia mkono wake kukishika kidevu cha Didas kilichoota ndevu nyingi mithili ya 'steelwire' akakisogeza karibu na akaivamia midomo yake kwa papi za midomo yake.
Kilichofuata ni kitendo cha kubadilishana mate kwa sekunde kadhaa.

Kisha Bebe akaondoa midomo yake na kumtamkia kwa ukaribu,
"Daddy...Uko tayari kumuacha mke wako kwa ajili yangu?!... Uko tayari kuandikisha mali zako zote kwa jina langu?!...Uko tayari kunioa kwa ndoa ya kifahari...Ndoa itakayofanyika kwenye fukwe za Uarabuni?! Nijibu Daddy uko tayari?!..."
Maswali yake yakageuka shubiri kinywani mwa Didas. Yalikuwa machungu mno...hakuweza kuyajibu na akaishia kuguna.

"Hayo yote nimehaidiwa na wanaume tofauti sijui ni nani mkweli na nani mdanganyifu. Lakini wote wamenipatia sifa zilezile. Kama unazonipatia wewe." Akatamka akisimama taratibu.
"Kila mmoja amenihaidi pete ya ndoa. Lakini wote hawa wanajua fika kuwa mimi sifai kuwa mke wa mtu. Nimzalie watoto, niwe mama wa familia...mnalijua hilo kabisa! Kwanza ni mwanaume gani timamu atakubali kumuoa malaya?!" Akaliacha swali lake lielee hewani. Likamfanya Didas aone aibu na kutazama chini. Jibu alilolipata lilimfanya ajione sawasawa na kuwa uchi hadharani.

"Sitaki kufungwa kwenye gereza la pete. Sitaki nipitie mateso ya pingu za maisha.Furaha yangu ni pesa! Ndoa yangu ni pesa, ninachokitaka ni pesa tu, pesa mezani!" Akatamka huku akiunyoosha mkono wake kwa Didas ambaye alielewa alichokimaanisha.

Upesi huku akitetemeka akalipekua suruali lake na kuibuka na waleti. Akahesabu noti kumi na tano nyekundu na kumpatia Bebe.
Bebe akazihesabu na kushangaa,
"Eh? Kilo na nusu?!" Akauliza Bebe baada ya kuona kazidishiwa ujira.
"Eeh..wala usiwaze...chukua zote hizo!" Akajibu kwa kigugumizi Didas. Kijasho chembamba kikianza kumvuja makwapani.

Bila kujibu kitu Bebe akazisukuma kwenye pochi yake, akainama na kuachia busu la hewani kuelekea usoni kwa Didas, aliyelazimisha tabasamu.
"Bye bye Daddy...mpaka kesho tu utakuwa umenisahau tayari!"
Akageuka nyuzi mia tatu sitini kwa maringo, na kupiga hatua kuondoka pale chumbani.
Viatu vyake vya kuchuchumia vyenye visigino vilivyoinuka, vikaifanya marumaru ya sakafu ile iziimbe sifa zake.

Nyama zake za makalio zikipata mtikisiko,
Sakafu chini ya viatu vyake ikalia ko!ko!ko!,
Nyuma yake akaacha masikitiko,
Didas akabaki na masononeko,
Hawezi kulipikia peke yake hili jiko,
Kumbe wapo wengi wale wavuta kiko,
Wenye nasaba bora wanaomzidi mshiko,
Labda atumie hirizi na mazindiko,
Lakini ye mzee wa kanisa, ushirikina kwake mwiko!


"Aiseee!" Ikamtoka bwana Didas, hakuamini anachokiona. Kifurushi kilichosheheni kila aina ya baraka ya uumbaji nd'o kileee kilikuwa kinamuacha peke yake chumbani. Bebe alikuwa ni tafsiri halisi ya 'complete package' ya neno 'mwanamke mzuri'.
Alikuwa amemzoea Bebe. Lakini kila siku alimuona mpya.
Akaachwa chumbani mle akifanya tafakuri. Bebe alimuachia sentensi tata mno iliyomdai aiandikie insha yenye kichwa,
"NDOA YA MWANAUME TIMAMU NA CHANGUDOA!"
Hakika alipewa darasa huru. Darasa la bure. Akarejerea upya kulitafakari neno la Mungu.

*****

Nje ya hoteli hii ndogo...Bebe akasimama na kuvuta hewa safi kwa sekunde nne. Upepo mwanana ukamlaki na kuuburudisha mwili wake kwa kumpepea.
Naam, ilikuwa siku mpya!
Akatabasamu na kuifungua pochi yake, akahesabu upya noti zile huku akiuhisi ushindi moyoni mwake.
Upesi akazitenga noti tano na kuzifutika kwenye sidiria yake, huenda hizi zilikuwa za ziada.
Akaitazama simu yake aliyokuwa ameiamuru iwe bubu kwa kuiseti katika 'silent mode' usiku kucha. Akakuta jumbe nyingi na simu nyingi zilizomtafuta bila mafanikio.
Zilimtafuta nyingi lakini ni moja tu iliyokuwa na umuhimu kuliko zote.
MADAM SALLY!
Ndivyo alivyohiifadhi.
Akaipigia upesi akiwa tayari kupokea lawama, matusi, shutuma na malalamiko yote.
Na kweli! Hakukuwa na salamu.
Mvua ya matusi ya nguoni na lawama ilimnyeshea kutokea upande wa pili.

"Madam, madam...calm down madam! Nd'o nilikuwa nakuja jamani. Kanikamia huyo, hakutaka niondoke haraka!" Akajitetea.
"Kwa hiyo unataka kusema umempa na 'Cha asubuhi au?'...we ruka ruka tu huko. Ukitapeliwa shauri yako!"
Sauti ile kavu ya kike ikafoka.
"Nakuja jamani madam nipo njiani hapa!"
"We hata usipokuja...ili mradi hela yangu inifikie huku mie!"
Simu ikakatwa.
Bebe akatazama kulia na kushoto, akapunga mkono kumuita dereva bodaboda. Kisha akapanda huku akimpatia maelekezo ya wapi anapokwenda. Pikipiki ikachochewa moto, ikaviringisha matari yake na kuondoka.
Nyinyi hamkuwepo,
Lakini acheni mimi niwasimulie...Hakika Bebe hakufanania hata kidogo na kupanda bodaboda. Huenda bwana Didas Ambrozi alikuwa sahihi, akampa fursa lakini Bebe akaikataa na kuendelea kuyakumbatia maisha yaliyozidi kumparua kwa makucha makali.
Kwa nini akatae?
Hata mimi sijui,
Maana ukiona mtu anatema asali kwa nguvu kisha akakimbilia kulamba pilipili, tena kwa hamu kubwa, lipo jambo! Hakika lipo jambo. Tena sio jambo dogo!

Itaendelea...
 
KIBIRITINGOMA
YA: Godlove Kabati
Chini ya udhamini wa: MAJIVU YA FASIHI
WhatsApp: 0763204351


SEHEMU YA PILI


Chimbuko la jamii yoyote ile huanzia kwenye ngazi ya familia.
Familia ni kitovu cha taifa, na ni chemichemi ya tamaduni zote zinazolijenga taifa.
Nguzo za familia zinapoyumba, ni rahisi sana maadili ya jamii kuporomoka na kuzua janga kwa taifa.
Japokuwa malezi ya watoto katika familia ni jukumu mama la wazazi yaani baba na mama,
Hilo halizuii mchango wa jamii kwenye malezi ya watoto wetu.
Malezi ni ya kwetu sote...



Anaitwa Frolida Pasko,
Walioona kuwa ndimi zao zitapata taabu sana kulitaja jina lote hili, wakamuita Frola ili kuokoa muda.
Hakutegemea kupachikwa jina jingine katika maisha yake. Mpaka pale alipoianza shughuli hii ya ukahaba na kutumika kingono ili apate pesa.
Alivutia sana kwa urembo wa sura yake, wale waliokuwa wajuvi wa misemo na lugha, wakadai kuwa ati ana sura ya upole na adabu kama ya mtoto mdogo. Wanaoijua ile lugha iliyokuja kwa ndege wakasema ana 'baby face', wakamuita 'baby'. Waswahili wakafunga kazi kwa kumuita 'Bebe'.
Naam,
Muite kwa majina ya Frolida na Frola wakati wa mchana. Lakini anapokuwa kazini, anavaa wajihi mpya kabisa...hapa muite Bebe!
Jina la Bebe likajizolea umaarufu mkubwa, yale mengine yakazikwa kwenye kaburi la sahau.

Malezi?!
Alilelewa ndio, tena na wazazi wawili, baba na mama. Yeye akiwa mtoto wa pekee.
Jinamizi la umasikini liliiwinda familia yao usiku na mchana, likapanua mdomo wake mkubwa na kunyoosha makucha ili kuwaangamiza.

Baba yake mzazi, mzee Pasko; hakuwa na kazi maalumu ya kueleweka. Kila siku aliamka asubuhi kisha huyoo anaondoka, anakoelekea hapajulikani. Na aliporudi usiku alikuwa akiyumba na kutoa maneno machafu na yenye aibu.
Alikuwa mlevi wa kupindukia, aliyezifanya baa,vilabu na vijiwe vya pombe za kienyeji kuwa kama nyumba za ibada. Huko aliudhuria asubuhi, mchana na jioni. Alipokosa bia, alizikumbatia pombe za kienyeji.
Pombe zikang'ang'ania kila sarafu yake, zikakamata kila noti yake. Akayasahau majukumu yake kwenye familia kama baba.
Hakuwa na mahusiano na pombe tangu zamani lakini marafiki zake aliofanya nao kazi kwenye kampuni ya ulinzi, ndio hawa waliomsogeza kwenye meza za vilabu na baa mbalimbali. Wakazitambulisha chupa za pombe na bia kwake, wakazinadi kuwa zina uwezo wa kuufukuza msongo wa mawazo na kuleta utulivu wa nafsi.
Ni nani asiyeupenda utulivu wa nafsi?
Umaskini na taabu viliyafinyanga maisha ya Pasko na familia yake, vikamsuta na kumuonyesha kuwa yeye sio baba bora.
Akaikaribisha pombe kwa mikono miwili, akaionja mara ya kwanza na kufinya uso wake kwa ukakasi na uchungu aliouonja, akaambiwa ni kawaida hiyo kwa mtu anayeanza pombe kwa mara ya kwanza.

Akajikaza,
Taratibu...katika namna ya ajabu, uchungu ukageuka kuwa utamu, utamu ukasafiri kooni ukasafisha umio na kutulia tumboni mwake. Baada ya dakika chache tu akahisi faraja ambayo hakuwahi kuihisi popote pale maishani mwake.
Ni hapo, aliposaini mkataba wa maisha na pombe. Akaivisha pete na pombe ikawa kama mke wake wa pili.

Kuvaa miwani ikawa tabia yake ya moja kwa moja...na alipozoea kwenda kazini akiwa amevaa miwani, waajiri wake wakamuachisha kazi mara moja.
Hapo akazidisha mapenzi yake kwa pombe... kwa nguvu zake zote, akili zake zote na moyo wake wote.
Akawa mzigo nyumbani. Wakati anaotegemewa alete chochote kitu, yeye akawa anategemea akute chochote kitu.
Kijiti cha jukumu la kulea familia kikahamia kwa mama moja kwa moja. Kazi zake ndogondogo za kuuza nyanya,vitunguu na mbogamboga zikawa kama jicho lake pekee alilolitegemea kuilisha familia yake.
Aliitwa Bi Devotha;
Mwanamke ambaye tumbo lake lilibarikiwa kumleta duniani mtoto mmoja pekee.
Frolida!

Bahati mbaya kwake, hakufanikiwa kupata uzao mwingine, ama mtoto wa kiume kama alivyodai mzee Pasko. Hili likawa doa katika ndoa yake, lililosababisha vurugu na kutoelewana kila kukicha, hasahasa pale Bwana Pasko aliporudi nyumbani akiwa kapandwa na pepo chafu la pombe za kienyeji.
Aligeuka mbogo, akavurumisha matusi na lawama kila kukicha. Leo hii atadai watoto halafu kesho atadai mtoto wa kiume.

Chumba chao kidogo kiligeuka ulingo wa ndondi kila usiku wa manane. Majirani waliuingilia ugomvi huu mpaka pale walipochoka na kuanza kuuchukulia kama ni sehemu ya maisha ya kila siku ya familia hii, wakaanza kuyazoea.
Mazoea...mazoea yakajenga tabia, hakuna hata mmoja aliyechukua hatua.
Mpaka ilipohitimu ile siku ambayo bwana Pasko alikuja akiwa na hasira aliyoiokota kilabuni baada chupa yake kupigwa teke na walevi waliokuwa wakigombana.
Siku hii alirejea akiwa amevimba kwa hasira. Anatamani kurarua kiumbe hai chochote atakachokikutana mbele yake. Hakugonga mlango, akaupiga teke kwa nguvu, ukaitika kwa kuteguka kwenye bawaba na kuvunjika kisha akaingia ndani kwa jazba.
Mke wake aliposimama mbele kumuuliza sababu ya kuuonea mlango ule legevu, akampiga bila huruma na kumjeruhi kwa kipande cha panga butu lenye kutu tumboni.
Akaogopa sana baada ya kushuhudia namna damu inavyofumuka kwa fujo kutoka tumboni kwa mkewe. Pombe yote iliyomhadaa kuwa itamfariji, ikamsaliti na kuyeyuka kichwani kwake.Akaogopa!
Akaamua kutafuta uelekeo na kukimbia kadri miguu yake ilivyoweza kumbeba.

Ukelele usio wa kawaida ukawafanya majirani watoke nje kutazama ni nini kimejiri. Mazoea hayakuchukua nafasi wakati huu.
Bi'Devotha alikuwa hoi...Frola akiipunga mikono yake hewani, macho yakimtazama mama yake pale chini, machozi mengi usoni.
Ilitisha, iliogopesha, ilisikitisha na kuhuzunisha sana kutazama.

Upesi akawahishwa hospitalini kupatiwa matibabu. Na msako mkali dhidi ya bwana Pasko ukaanza. Alitafutwa kwa muda mrefu sana bila mafanikio. Alipotea na kutokomea kusikojulikana.
Huku nyuma, mkewe akabaki hospitalini akipatiwa matibabu. Matibabu ambayo gharama yake isingeweza kukidhiwa na binti peke yake abadani.
Huu mpira ukapigwa pasi kwa jamii yake ya karibu.
Ndugu, jamaa na marafiki wakajichanga mpaka pale walipoweza...lakini wangeweza mpaka wapi?!
Familia kama hii, iliyoishi kwenye mitaa korofi iliyomezwa na umaskini, njaa, maladhi, uhuni, ubakaji, umbea, wizi na vurugu za kila aina. Wangepata wapi hao ndugu na jamaa wa kutosha kulipia matibabu ya bi.Devotha?!

Tiba yake ikafanyika kwa kipimo kilichostahili malipo yaliyotolewa...mpaka pale kitanda cha hospitali kilipomchoka.
Bi'Devotha akahamishiwa nyumbani kwake, kidonda chake kikiwa bado hakijapona vyema.
Hakukuwa na namna, ilitakiwa ahudumiwe palepale juu ya godoro lake lililozizoea chaga mbovu ambazo hazikupenda bugudha ya aina yoyote ile ama sivyo, zinavunjika katika wakati usio na jina.
Baada ya muda fulani, magonjwa ya ajabu ajabu yakaanza kumshambulia. Maumivu ya kidonda yakaikaribisha homa kali na mateso kwenye mwili wa mama yule.

Ule msemo wa asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu, ukamvamia Frola katika namna ya tofauti. Sio kwamba hakuwahi kufunzwa na mamaye, la hasha!
Alifunzwa na kufunzika...lakini sasa alihitajika apate darasa la ulimwengu. Maana kwa wakati huu majukumu yote ya familia yalimgeuzia macho yeye.
Darasa la ulimwengu likamdai ada kubwa, akiwa kidato cha tatu tu. Akaanza kuugawanya muda wake wa masomo na kumtazama mgonjwa. Akaamua aache masomo ili achague moja, ndipo akaanza biashara ndogondogo ili apate fedha za kumhudumia mama yake na kupata chakula.
Naam,
Ulimwengu haukuwa na huruma kwa huyu binti wa miaka kumi na nane, Frolida Pasko akasulubiwa na maisha. Akaulaani sana ulimwengu, akamlaumu sana Mungu aliyeruhusu yeye azaliwe kwenye familia yenye baba aina ya mzee Pasko.
Jahazi la maisha yao likayumba...wakala kwa taabu, wakavaa kwa taabu na wakalala kwa taabu...sahau kuhusu kusoma, sahau kuhusu majaribu aliyokutana nayo Frola mitaani kutoka kwa wanaume na vijana wenye uchu wa ngono.

Usiku mmoja ulioambatana na mvua za rasharasha sambamba na radi zenye ngurumo za kutisha. Familia hii duni, iliyosahaulika kwenye mgao wa bahati na furaha, ilikuwa imejihifadhi chini ya paa lilelile lenye mabati yenye kutu yanayogongana daima, kukiwa na hali ya upepo wenye fujo.

Kwa mwangaza hafifu wa kibatari kilichokuwa kinakata viuno baada ya kufyonza mafuta bila haya, Frola alikuwa amempakata mama yake.
Ule ukimya wa 'shetani amepita' ndio ulitawala. Kisha ghafla,
"Frolida binti yangu..."
Sauti ya kufifia, iliyolazimishwa kutoka kinywani mwa Bi Devotha ilitamka kwa upole.
"Abee mama."
Akajibu, akiwa ameyaruhusu mapaja yake yatumike kama mto wa kulalia, amekipakata kichwa cha mama yake...mikono yake ikijaribu kumliwaza mama huyu ambaye mwili wake umekataa katakata kuuacha urembo wake wa ujanani, japokuwa ulionekana kuwa umepitia suluba na uchovu wa kutosha kuukaribia uzee.
"Nisameheni sana mwanangu,
Najua kuwa nakuchosha, nimekuwa mzigo kwako binti yangu. Haikutakiwa uishi haya maisha hata kidogo!"
Akakatishwa mara moja,
"Mama...mama usiseme hivyo mama. Wewe sio mzigo kwangu bhana...Na hata siku moja hautakuja kuwa mzigo kwangu mama!" Kwa sauti ya kudeka, Frola akamfariji huku mkono wake ukitambaa taratibu kichwani mwa mamaye. Bado huyu alikuwa ni mama yake, kwa nini asideke? Mtoto hakui mbele ya mama.

"Haya sio maisha niliyotaka uishi mwanangu, sio kabisa! Lakini baba yako...kho!kho!kho!"
Kikohozi kikamvamia, upesi kikombe kilichojaa maji kikasogezwa, Frola akamnywesha mama yake kwa taabu.

"Niliwahi kuwa binti kama wewe enzi zangu. Niliwahi kuwa mrembo kama ulivyo wewe.
Pale kijijini kwetu, niliweza kuwazuzua vijana wengi sana, ambao walinitamani sana kimapenzi. Wazazi wangu wakanikanya na kunizuia kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi katika umri ule.
Nilianza kwa kuwaelewa mpaka nilipokutana na Pasko. Huyu akanifanya nisahau makanyo yote ya wazazi wangu, nikampa moyo wangu wote, nikampenda kwa kila namna inayostahili kuitwa upendo wa kweli. Sikujua...kumbe nilimkumbatia shetani mwenye mapembe saba kichwani na mkia mrefu.

"Akanilubuni na kwa mara ya kwanza nikakutana na mwanaume kimwili. Ilikuwa mara ya kwanza lakini haikuwa ya mwisho, tukazini tena na tena. Nikapata mimba na akanishawishi nizitoe mara kwa mara ili tusigundulike kwa urahisi.
Zilikuwa mbio za sakafuni tu...na tulipoishia ukingoni tulikuwa tumechelewa sana. Niligundulika baada ya kukamatwa nikiwa kwenye jaribio la kutoa mimba.
Hali ikawa zaidi ya hatari, wazazi wangu wakageuka mbogo.
(Anakohoa)

"Baba alinipiga sana akitishia kuniua, nikaogopa na kukimbia. Huko nyuma, akaagiza watu wanitafute. Woga ukanizidia, ukali wa baba niliuelewa kwa maneno na vitendo. Ili kuitafuta salama yangu, nikajitahidi kumuepuka kadri niwezavyo.
Giza la usiku nalo likaanza kuiinamia ardhi katika namna ya kutisha.
Sikuwa na kimbilio, zaidi ya kuelekea kwa
Pasko, ambaye naye alikuwa katika harakati za kutoroka pale kijijini, hofu ikionekana waziwazi usoni mwake. Akanishurutisha kuwa tutorokee jijini Dar, akidai kuwa huko anao ndugu na jamaa watakaoweza kutupa hifadhi kwa siku chache akiwa anaweka mambo yake sawa.
Ni hapo nilipoanza kuuona waziwazi uongo wake aliokuwa ameuvisha nguo hapo kabla.
Kuwa ana biashara zake nyingi huko mjini na nyumba ya kuishi.

"Bila kufikiria mara mbili, nikakubali huyo shetani anidanganye kwa mara ya pili. Usiku wa siku hiyo hiyo Pasko akanitorosha. Chozi la kwaheri likanitoka nilipokuwa nakiaga kijiji changu cha nyumbani.
Tulifika Dar-es-Salaam tukiwa hoi baada ya ugumu wa safari,iliyokuwa ya kubangaiza.
Ajabu na kweli!
Ile Dar niliyokuwa nasimuliwa na baba yako pale kisimani, haikuwa kama nilivyoikuta.
Mara moja, jiji likanipokea na ugumu wa maisha, ulioanza ukaanza kunisigina bila huruma.
Mpaka wewe unazaliwa mwanangu...kho! Kho! Kho!"

Kikohozi kikamzidia...
Mara hii alikohoa sana kama aliyekabwa na kitu kigumu kooni. Frola akaruka na kusogeza kikombe cha maji, akamnywesha kwa taabu kabla hajatulia tena na kuhema juujuu.
"Frola..." akamuita, bado koo lake liko vitani na pumzi zinazopishana kwa nguvu.
"Abee mama."
"Nife leo, nife kesho mwanangu.
Kuwa makini sana na wanaume! Hata siku moja, usimwamini mwanaume.
Fanya yote lakini tambua kuwa wanaume ni watu wabaya." Na hapo kikohozi kikamvamia upya kwa fujo.

Akashindwa kuendelea na Frola akampumzisha juu ya kitanda. Anatetemeka kwa baridi japo tembe za jasho zilionekana kuulowanisha mwili wake.
Frola akayaandaa malazi yake pale juu ya sakafu ya baridi, na kujitanda kwa shuka jepesi kuusubiri usingizi ambao ungejileta wenyewe wakati ambao ungefaa.
Hali ya hewa huko nje ilitisha sana, ngurumo za radi na miale ya kushtukiza vilizidi kuikoleza historia ya usiku huu na kuufanya uwe wa kukumbukwa zaidi kwenye maisha ya Frola.

Na kweli!
Ulikuwa ni usiku wa kihistoria haswaa..
Alipoamka asubuhi hakuamini kile ambacho macho yake yalikishuhudia.
Bi. Devotha, mama yake kipenzi...alikuwa marehemu.

Angejaza mapipa kwa machozi, angetamka kila aina ya laana, angeulalamikia ulimwengu...lakini asingeweza kuurejesha uhai wa mama yake.
Hakukosea yule aliyetamka kuwa,
"Gharama ya maisha itamhusu marehemu mwenyewe, lakini gharama za mazishi ni ya wale waliobaki duniani...hii haitamuhusu marehemu moja kwa moja".
Na kweli, mwili wa Bi.Devotha ulirejeshwa upesi mavumbini japo katika namna ya tofauti. Jamii ikachukua jukumu la kuusindikiza mwili wa marehemu kaburini. Ulikuwa msiba wa kushangaza hakika, huu ulipingana na ile methali ya wahenga unaodai kwa kila msiba una mwenziwe.

Kama mtu angetaka kuifahamu tofauti kati ya kuzikwa na kufukiwa ardhini, basi angejionea mwenyewe katika msiba huu mubashara.
Hakukuwa na ndugu wa karibu zaidi ya Frola peke yake. Akaachwa katika shimo la majonzi akiwa mkiwa, yatima ambaye chuki za maisha magumu ya dunia na laana zake vyote vilikuwa vimejiandaa kumshambulia kwa uchu.

Dunia ikamuinamia, akapoteza tumaini la maisha. Kama lilivyo jani la mti lidondokavyo kutoka kwenye tawi lake, mzee Pasko alipotea moja kwa moja. Achana na kutojulikana alikimbilia wapi, jamii ilimsahau moja kwa moja.
Huruma pekee aliyoonewa Frola, ni kusikitikiwa tu, maana hali aliyoachwa nayo haikupe
Frola akashika hatamu za uongozi wa familia hii mpya inayohusisha mtu mmoja tu. Yeye mwenyewe akiwa baba na yeye mwenyewe akiwa kama mama pia.
Pesa kiduchu za rambirambi zilizokusanywa zisingemtosha kulisukuma gurudumu la maisha yake. Mtoto huyu wa kike akaamua kujifunga kibwebwe na kutafuta shughuli yoyote ile...

Mradi mkono uende kinywani,
Hana wa kumlisha abadani,
Alishaitupa kalamu zamani,
Usishangae kutomuona shuleni,
Binti kibwebwe kiunoni,
Kafunga aingie vitani,
Kupigana na adui gani,
Nani mwingine zaidi ya umaskini?

Akaanza kwa kufanya kazi kwenye migahawa kadhaa, lakini huko hakudumu sana kabla hajasumbuliwa na wateja wa kiume wa migahawa hio.
Hawa walimhusudu katika namna ya kugombea na kushabikia kuhudumiwa na yeye peke yake. Wakamsifia kwa urembo wake na haiba yake nzuri, wengine wakaanza kumtongoza.
Ni usiku mmoja tu, ulitosha kabisa kumkaribisha kwenye dunia mpya.
Siku hii alichelewa kurudi nyumbani baada ya kuhudumia wateja kwenye mgahawa ule mdogo aliokuwa ameajiriwa.
Hakujua kama alikosea kona au alipita kwenye kona hio katika muda usio sahihi. Yeye alishtukia ameparamiwa na kuzibwa kinywa kwa nguvu. Kisha akaburutwa mpaka kwenye jumba ambalo halijamalizika ujenzi wake.
Bila salamu wala kujitambulisha, vijana watatu mashababi walioonekana kuwa walimpania kwa muda mrefu, wakamvamia na kumbaka kwa zamu.
Frola alilia sana akihitaji msaada na hakukuwa na msaada wowote ule kwa ajili yake usiku huu eneo lile.
Baada ya kukidhi haja zao za kimwili, vijana wale waliokosa utu wakayeyuka gizani. Wakamuacha pale Frola akiwa hajielewi. Hawakutaka kujua amezirai? Amekufa? Hawakujali, ili mradi wamemaliza haja zao basi.

Fahamu zilimrejea Frola akiwa kwenye chumba cha matibabu hospitalini. Hakujua amefika pale vipi, hakujua amelala pale kwa siku ngapi. Alichokiona ni dripu iliyofungwa kwenye mkono wake wa kuume na akagundua kuwa kuna tabasamu lipo pale kando yake likimtazama.
Mwanamke mmoja mnene wa kadri, aliyevaa mavazi ya gharama kiasi na kuukamilisha urembo wake kwa vipodozi vilivyoigeuza rangi ya uso wake kutoka kwenye asili yake mpaka kuwa mwekundu.
"Pole kipenzi!..."
Alitamka akiwa bado anatabasamu. Tabasamu kama hili alikuwa amewahi kuliona mahala...aliliona wapi?
Mama mzazi!
Lilikuwa tabasamu kama la marehemu mama yake. Tabasamu la upendo.
Halafu ghafla akaukumbuka unyama aliotendewa na wale vijana madhalimu.
Chozi likamdondoka Frola.

"Pole mamy...daktari atakuja hivi punde!"
Akatamka huku akifanya jitihada za kumfunika Frola kwa shuka lile jeupe.
"Niite madam Salome...ama waweza kuniita Madam Sally."
Akajitambulisha kwa mara ya kwanza maishani mwa Frola.

*****

Mara ya kwanza na mara moja tu!
Na ni huyu akawa mama mpya kwa Frola, mama aliyesababisha apate jina jipya kabisa la Bebe.
Ni huyuhuyu,
Madam Sally amempigia simu na kumuuliza ni wapi alipo mpaka muda huu.
Na kwake ndiko anakoelekea...


Itaendelea....
 
KIBIRITINGOMA
yake: Godlove Kabati
Kwa udhamini wa MAJIVU YA FASIHI

SEHEMU YA TATU


Aliutazama mlango wa geti lile kwa hofu, akashusha macho yake taratibu mpaka kilipo kitasa. Akasita kukipindua.
Akashusha pumzi ndefu ili kujirejeshea ari ya kujiamini.
Kisha,
"Ngo! Ngo! Ngo!..."
Akagonga mlango ule. Hakuna kauli yoyote ile ya kumkaribisha iliosikika.
Akagonga tena bila kujibiwa. Akajaribu kuusukuma mlango ule na kweli ulikuwa wazi.
Akazama ndani.
Mlinzi wa mahala pale aliyetegemea awe wa kwanza kumpokea alikuwa mbali sana kimwili.
Amechutama akiegama kwenye ukuta, uso wake ameuficha kwa kofia pana, kama aliyezirai...anakoroma. Alikuwa amechotwa na usingizi mzito. Silaha yake duni ya siku zote alikuwa ameitelekeza mbali naye, rungu dogo.
"Lo! Maskini mzee wa watu!".
Bebe akatumia sekunde kadhaa kumtazama kwa masikitiko kabla hajamsogelea na kumgusa kidogo katika namna ya kumshtua.
"Mzee Baraka!...we mzee Baraka!"
Mlinzi yule mzee akakurupuka, akachupa na kuliokota rungu lake.
Upesi akawahi pale getini, almanusura amchote Bebe na kumbwaga chini. Bebe akapepesuka hewani lakini mara akajiwahi na kupata mhimili .
"Khaa! Wewe..."
"Naam...samahani sana! Samahani..po-pole!" Mlinzi akiwa amebaa akawahi kuomba radhi. Pumzi zinapishana kwa kasi puani mwake, hofu, woga na wasiwasi vimemvamia kwa pamoja.
"Ina maana umechoka namna hiyo kweli mzee wangu?" Bebe anajikun'guta vumbi na kujiweka sawa.
Mzee huyu ambaye alionekana kuwa na umri wa kutosha kabisa kuwa na mabinti wenye umri sawa na Bebe kama wawili au zaidi, akajipangusa kijasho chembamba kilichoanza kulowanisha paji lake la uso.
"Ha-hapana mwanangu, ni uchovu tu, nimekesha usiku kucha. Na-na huu nd'o muda wangu wa kupumzika." Akajitetea.
"Mmh...babu nd'o uache geti wazi?"
Mzee akawahi kukagua mlango mdogo wa geti lile kuhakikisha alichoambiwa, kisha akajikuna kichwa chake bila kuwashwa. Alipogeuka nyuma ili ajitetee tena akajikuta yuko peke yake, tayari Bebe alikuwa anazihesabu hatua zake kuelekea ndani ya jengo hili kubwa la kifahari lililokuwa kimya likiwatazama.
Akaingia ndani yake, kama aliyemezwa hivi. Huku nyuma akamuacha mzee aliyekuwa na mawazo mengi sana juu ya mustakabali wa kibarua chake.


********

"Yaani ndani ya masaa yote hayo, umepata laki moja tu?!" Sauti ya kike iliyoshiba ubabe, ilikoroma.
"Mteja mmoja tu Madam!" Akajibiwa kwa sauti nyingine ya kike, hii ilikuwa nyepesi inayotangaza huruma.
"Hapana Bebe! Kuna kitu hakiko sawa hapa. Wewe sio wa kuniletea kiasi kidogo namna hii! Uliv'onambia utakesha huko mpaka asubuhi nikadhani utapata hata laki na nusu hivi au mbili kabisa! Sasa hii nini hii? Nakupasulia ngapi hapa?" Akalalamika.
Hakujibiwa moja kwa moja, zaidi Bebe aliviringisha macho yake makubwa na kutazama pembeni katika namna ya kususa.

"Wewe ni moja kati ya wasichana ninaowaamini sana, na thamani yako ni ya juu. Wewe sio wa laki moja kabisa! Au umeanza kuniibia? Eh? Niambie Bebe...umeanza kunizunguka?" Safari hii akasimama na kumtazama Bebe usoni, mikono yake kiunoni, amemuinamia kisharishari.
Bebe bado ametazama pembeni, anaonesha kukereka.

Madam akarejea tena juu ya sofa na kuketi. Akaikusanya mikono yake juu ya kifua chake kipana na kuikunja katika namna ya kuibebanisha.
"Ulikuwa wapi Bebe?", akamuuliza kwa sauti ya polepole akiwa amemtazama kwa macho ya kumpima.
Bebe akaugeuza uso wake taratibu na kumtazama Madam usoni kimya bila kunena lolote.
"Nilitaka kukupatia kazi, ukanambia una mteja wako binafsi...na ukaniambia kuwa ana fulusi. Kwahio hapa nikupe fote utaridhika kweli?"
"Madam Sally, we nipe chochote kile mi nitaridhika tu! Alikuwa vibaya kiuchumi...nimegombana naye sana lakini kwa vile nafahamiana naye nd'o ikawa kama hivyo." Bebe akajibu kwa ufasaha na kweli, akaeleweka.
"Sawa!" Ikamtoka Madam Sally.
Akatenga noti sita nyekundu na kumpatia noti nne Bebe.
"Kha! Madam vipi tena, mgao gani huu?" Bebe akapigwa na butwaa.
"Nafsi yangu inanisuta kuwa umepewa mia hamsini. Na hizo hamsini umezificha Bebe, sitaki nikukague. Unafahamu mwenyewe!"
Madam Sally akajibu kwa kujiamini.

Kanuni yao ya mgawo wa asilimia ilikuwa ni ileile ya siku zote, yeye anachukua arobaini na sitini zinachukuliwa na binti husika. Na hata sasa, machale yake yalimtaarifu kuwa Bebe ameficha elfu hamsini na alichokifanya yeye ni kufuata kanuni.
"Nimezificha wapi? Wapi Madam? Niambie..." Bebe akalalamikia mgawanyo ule.
"Unataka nikuonyeshe zilipo eh?"
Madam akasimama na kukivamia kifua cha Bebe kwa nguvu.
Bebe akiwa hajategemea tukio hilo, akajitahidi kumzuia bila mafanikio.
Noti tano zikaibuliwa kutoka kwenye sidiria ya Bebe, iliyopekeuliwa kwa mikono shupavu ya Madam Sally.

"Haya hiki nini?"
"Lakini-lakini...hio ni bonasi yangu Madam. Kanizidishia yeye mwenyewe!" Akiwa na sauti ya kilio, Bebe akajiweka kwenye nafasi iliyodai haki yake iliyopokonywa.
Madam Sally akazitupa noti zile juu ya meza ndogo ya kioo.
Zilikuwa zimekunjwakunjwa na kupoteza ule unyoofu wake.
"Nimewalea mabinti wengi sana Bebe. Nimeshuhudia tabia nyingi sana, wapo niliowaamini kama wewe na wapo waliogeuka wasaliti, wakawa nyoka wenye vichwa saba. Hakuna ujanja wowote ambao unaweza kufanya ukawa mgeni kwangu.
Nina uzoefu wa kutosha Bebe...naweza kukutazama tu na nikagundua umelala na wanaume wangapi kwenye usiku tuliokubaliana unaenda kwa mwanaume mmoja."
Akaweka kituo akiusanifu uso wa Bebe, ambaye alikuwa ameruhusu machozi mepesi yaulowanishe. Jambo lililouzidisha urembo wake.
Madam Sally hakuyajali machozi yake, akaokota pakti la sigara na kuchagua mojawapo.
"Ni katika michezo na ujinga wa namna hii, ambao nyie mnaona kama unjanja. Mabinti wanaoanza kuniibia huwa nawapoteza!
Sitaki kuwaza kuwa hata wewe utaingia kwenye hili kundi Bebe...sitaki!"
Tayari sigara iko kinywani mwake. Bebe akaokota kiberiti na kukiwasha, Madam akasogeza kinywa chake na mwale wa moto ule wa kiberiti ukaichoma sigara ambayo ilijibu kwa kutoa moshi.
"Asante!" Ikamtoka Madam Sally.
Akazikusanya fedha zote na kumpatia Bebe.
"Sidhani kama nimekuonea...lakini kwa vile unataka fedha, haya mrembo hizo hapo!"

Bebe akapigwa na butwaa. Bado alikuwa haelewi ni kwa namna gani Madam Sally amekubali kumpatia kiasi chote kile hivihivi.
"Madam lakini-" akakatishwa.
"Ulisema ni mteja wako...sijakutafutia mimi. Basi kula kilicho chako binti. Sawa eh?!" Madam akamjibu huku akizidi kupambana na sigara ile ambayo ni kama alikuwa anaivuta kwa hamu kubwa.
Bebe akazikusanya fedha zile kutoka pale mezani huku mikono ikimtetemeka, kisha akamtazama Madam usoni.
Alikuwa mwanamke wa shoka haswaa, mwili wake wenye umbo kubwa ambalo liko katikati ya unene na wembamba.
Mwonekano wake ambao daima ulimfanya aonekane kama aliyekula chumvi nyingi na hapohapo ukamfanya aonekane kama anayeukimbia uzee kwa nguvu zake zote.
Mikono yake shupavu iliyozoea kupambana na suluba za maisha ilichora mishipa ya damu ilioelekea kufanana na mizizi juu ya ngozi yake.
Ni huyuhuyu Madam Sally, aliyekuwa mama mlezi wa Bebe kwa kipindi chote hiki cha miaka miwili na nusu tangu wamekutana.
Mama mlezi?
Mlezi gani huyu anayeunga mkono ukahaba?
Yumkini ana malezi ya tofauti.

"Asante Madam!" Ikamtoka Bebe na akasimama na kupiga hatua kingonge kuelekea kilipo chumba chake.
"Halafu Bebe!" Akaitwa.
"Leo usiku mimi na wewe tutakuwa wote pale Club! Mwambie hivyohivyo Sharon na Kulusumu!" Madam akatamka.
"Sawa Madam!"

******

Muite Madam Sally,
Kama ukitaka kulitaja jina lake kwa ufasaha basi muite Salome.
We muite hivyo tu ataitika, hakuwa na majina mengine ya ziada. Labda alikuwa nayo lakini hakutaka yajulikane.
Waswahili wa mitaa ya Sinza walimjua kwa jina hilo tu.
Ni Club yake maarufu iliopatikana palepale Sinza Mori... iliyojulikana kwa jina la LE CLUB GRANDE, iliyompatia jina la heshima. Watu wakaanza kumuita Madam.

Umiliki wake wa club hiyo kubwa ya kisasa, ulikuwa ni fumbo kwa wakazi na wale waliopenda kujiburudisha mahali hapo.
Hakuna aliyehoji na hata hivyo maneno yalikuwa mengi sana chini ya meza.
Yeye hakujali!
Alikuwa na mitego yake ya siri katika eneo hilohilo la LE CLUB GRANDE.
Biashara ya kuuza mabinti warembo na makahaba kwa matajiri wenye fedha!

Aliwakusanya kwa wingi popote kule walipokuwa kwenye mitaa maarufu ya jiji la Dar-es-Salaam. Aliwachagua kulingana na vigezo vyake yeye mwenyewe.
Aliwaahidi matunzo na haki zote za binadamu; Mavazi, chakula na malazi.
Akawaahidi kuwatafutia soko la wanaume wenye fedha waliohitaji huduma ya ngono.
Kisirisiri aliwasiliana nao kwa njia za siri akafanikisha biashara hii haramu.
Akaliendesha danguro hili katika namna ya kipekee.
Jina lake likapata sifa miongoni mwa wale waliofahamu ni kitu gani kinaendelea pale LE CLUB GRANDE.
Wakamtunuku cheo cha Madam!
Na yeye akawapa kilicho bora.

Ni usiku fulani ambao alikuwa kazini kwenye mawindo ya mabinti wake, akiwa na mabinti kadhaa wajuvi wa mitaa ya Dar.
Na siku hii saa saba usiku, walikuwa Manzese katika mitaa ya mwanzoni tu.
Mabinti wakaomba udhuru wakatafute mahala pa kujisitiri kwa haja ndogo. Madam akawasihi wavumilie maana hatari ya kuvamiwa na vibaka ilikuwa njenje, hakufanikiwa kuwashawishi. Wakashuka kutoka kwenye gari lake, wakihaidi hawakawii kurudi na hata hivyo hawaendi mbali.
Baada ya dakika moja, akasikia yowe!

Mmoja kati ya binti wale alikuwa akipeperusha mikono yake hewani. Ulikutwa mwili wa binti aliyekuwa hoi ndani ya jumba bovu. Hali yake ilitisha! Mavazi yake yamechanika na yu nusu uchi akiwa hajitambui.
Akafanya wema wa kumuwahisha kwenye kituo cha afya.

Baada ya siku kadhaa, hali ya binti huyu ilikuwa njema na baada ya maongezi ya hapa na pale, wakafahamiana.
Madam Sally akabeba jukumu la kumsaidia binti huyu kama mwanae.
Frola akahamia nyumbani kwa Madam, akapatiwa kazi ya uhudumu pale pale LE CLUB GRANDE .

Kama mtego tu,
Baada ya muda kidogo Frola akaleta malalamiko kwa Madam kuwa anasumbuliwa na wateja wakimtaka kimapenzi.
Madam akatabasamu na kumueleza kuwa avumilie tu na baada ya muda mambo yote yatakaa sawa.
Uvumilivu huu ambao ulitegemea binti Frola ale mbivu, ukamletea mbichi na kumlazimisha azile kwa nguvu.
Bila kuelewa akakutana na mwanaume mmoja aliyekuwa anaongea maneno matamu kama asali.
Huyu akamshawishi akashawishika!
Kamlainisha akalainika!
Mwisho wa siku tunda lake likalika!
Akalipwa pesa, pochi yake ikafurika!

KARIBU KWENYE MCHEZO!
Frola akakaribishwa rasmi kwenye maisha ya ukahaba.
Madam akamuweka mbele ya kioo,
Kisha akaliinamia sikio lake la kulia na kumtamkia taratibu,
"Unamuona huyo hapo mbele?
Huyo ni mrembo ambaye amezaliwa kula mema ya hii nchi.
Huyo amezaliwa kula matunda ya uhuru wa hii nchi.
Amepewa uzuri kama silaha yake ili aishi kwa usalama kwenye hii dunia. Anastahili kila kilicho kizuri hapa duniani.
Na ni kitu gani kizuri hapa duniani kuliko hela?!"
Yalikuwa maneno ya kishujaa kutoka kinywani
mwa Madam Sally.

"Wewe ni mrembo sana Frola.
Urembo haudumu milele mwanangu. Ipo siku utazeeka na urembo wako utafifia kama jani kavu. Na ukizeeka kabla haujaufaidi urembo wako utakuwa umefanya dhambi kubwa chini ya jua.
Hiyo dhambi yako haitasameheka kabisa!
Urembo wako ni zawadi!
Itumie ukingali nao bado!
Wewe ni mali, wewe ni hela!" Akamaliza na kuondoka akimuacha palepale mbele ya kioo.

Frola akamtazama yule Frola mwingine ambaye alikuwa pale kwenye kioo. Ni kama naye alikuwa anamweleza,
"Wakati ni sasa. Urembo haudumu milele shauri yako!"
Katika namna ya ajabu, Frola akabobea kwenye ukahaba wa viwango vya juu.

Kazi ilikuwa rahisi sana,
Madam Sally anawasiliana na mabwanyenye wanaohitaji huduma ya makahaba. Hawa wanamlipa yeye kwanza kisha anawatumia mrembo waliemchagua.
Baada ya kazi, noti nyingine nyingi, safi, zilizonyooka, zinagawiwa kwa mrembo aliyetoa huduma siku hiyo.
Kisha ile sitini kwa arobaini inaemda kufanyika huko kwenye danguro.

Maisha yakaenda hivi kwa muda mrefu sana. Hakuna aliyedhani kama yatafikia mwisho, hela ilijenga kiota kwenye miguu ya Madam Sally na warembo wake.
Labda ingeendelea kuishi milele kama asingekutana na huyu Frola wa kuitwa Bebe.
Labda asingemuokoa kabisa usiku ule.
Hakujua!
Hakujua....



ITAENDELEA..
 


KIBIRITINGOMA
Ya: Godlove Kabati
Kwa udhamini wa MAJIVU YA FASIHI
WhatsApp: 0763204351


SEHEMU YA NNE


Usipotumia uwezo wako kuitimiza ndoto yako, wapo watakaoutumia uwezo wako kuzitimiza ndoto zao.
Na baada ya kukutumia, hawatakuacha uende mbali. Watahakikisha unabaki kwenye mduara wao ili wazidi kukutumia tena na tena.
Watakuonyesha mafanikio utakayoyafikia kama tu utakuwa chini yao na kuwatumikia. Na wewe daima utazidi kuzunguka kwenye duara lilelile daima.
Akili kichwani mwako!

Na hii ni sehemu ya nne...




Ulikuwa ni usiku wenye hekaheka.
Jambo ambalo sio ajabu hapa jijini Dar-es-Salaam. Labda kwa mgeni jijini.
Lala wewe tu! Lakini kwa wengine, nd'o kwanzaa kumekucha.
Bado watu wanautafuta mkate wao wa kila siku, tena katika namna tofautitofauti.
Naam!
Huu ni muda muafaka kwa wale waliofanikiwa kuupata mkate wao, kuja kuipa miili yao pole kwenye kumbi na maeneo mbalimbali ya starehe.
Kwenye hayo maeneo mbalimbali, yapo machache yaliyosifika kwa ubora wa huduma zake. Kuanzia mapambo, burudani ya muziki, vyakula na vinywaji mpaka wahudumu.
Lakini LE CLUB GRANDE, ilikuwa kwenye anga la peke yake miongoni mwa kumbi hizo chache.

Ni nani asingevutiwa na zile taa nzuri zenye rangi mchanganyiko 'disco lights' zinazomeremeta?
Eneo pana la wazi, kubwa lililozungukwa na ukuta,
Vyakula na vinywaji vyote vitamu, si ajabu ukila mpaka ukajing'ata. Miziki ya kila ladha ipo hapa. Rhumba, reggae, amapiano hata ngoma za kikongo utasakata.
Tembea kote lakini ukifika hapa, hakika pengine utapakataa katakata.

Uchangamfu!
Ni moja kati ya sifa lukuki za klabu hii kubwa.
Na leo hii Jumamosi ambayo kwa wengi ilikuwa 'wikendi', palikuwa pamejaa na kuchangamka.
Kila mtu alikuwa na sababu yake ya kuchangamka na kufurahi. Huyu angefurahishwa na muziki, yule vinywaji, na huyu mwingine mapambo.
Huyu wa mapambo tusimshangae! Ni haki yake kufurahi bwana.
Lakini kuna hili kundi la wale waliofurahia kutazama watu wengine, watawachambua kuanzia walivyovaa, wanavyotembea, wanachokula ama wanachokunywa. Kisha watakipa daraja chakula chao na kupitia hicho watachagua thamani ya huyu mtu wanayemtazama.
Wamdharau au wamuheshimu, watajua wao!

Lakini miongoni mwa hawa watazamaji na wachambuzi, lilizaliwa kundi kubwa la wanaume ambao walikuwepo pale kwa dhumuni moja tu.
Kuwinda mabinti!
Macho yao hayakutulia. Walipepesa huku na huko wakimuona mmoja wao tu, haraka macho yao yatahamia kwenye maumbile yake halafu watamuhukumu kwa kumfuata ili wakauze lugha zao.

"Oya D ,una uhakika kuwa anafanya kazi hapa lakini?!" Ilisikika sauti changamfu.
"We tulia Jeifoo...mimi huwa sikosei mzee. Hili nd'o chimbo lake we sikilizia tu, muda sio mrefu utamuona kwani saa ngapi hapo?"
"Sa'hivi?...Saa nne na nusu!"
"Enheee...sasa tulia, hii nd'o mida yenyewe hii."

Yalikuwa maongezi ya vijana wawili waliokuwa mawindoni katika klabu hii. Jumanne aliyejulikana kama Jeifoo (J4) pamoja na Dotto aliyependelea kuitwa 'D'. Yupo mtu waliyekuwa wanamtafuta na meza yao ilitosha kabisa kulielezea hili. Ilijitofautisha na meza nyingine nyingi kwa kubeba chupa mbili za bia na glasi mbili pekee.

Ghafla ukumbi ukalipuka kwa shangwe. Baadhi ya watu wakasimama huku wakipunga mikono yao hewani kwa furaha. Ilikuwa ni kama kuna ugeni ambao kama haukusubiriwa kwa hamu basi kuna mtu maarufu ambaye ameingia ukumbini pale.
Sauti ya muziki ikaongezwa maradufu na mshehereheshaji wa bendi ya siku hio akapaza sauti yake,
"O yeah, finally! Mama la mama...mama lao, jike la shoka! Mabibi na mabwana...si mwingine ni Madaaam!...Madam Sally Salome!"
Shangwe likazidi maradufu, likasindikizwa na sauti ya mdundo wa muziki. Jambo lilizozidisha uchangamfu mahali hapa.
"Madam! Madam! Madam!..." ziliendelea kuvuma.

"Enhee...sikia sasa Jeifoo. Em sogea!" Mmoja kati ya vijana wale akamsogeza karibu mwenzie aliyeitwa kwa jina la J4(Jeifoo). Wakiwa wamesimama, wakajaribu kuchuchumia ili waone yanayoendelea.

"Yule maza niliyekwambia wanamuita Madam yule...nd'o huyo hapo anayeshangiliwa sasa!" Akipambana na kelele za shangwe zile, akamnong'oneza J4 sikioni mwake.
J4 akamkazia macho mwanamke yule mwenye umri wa makamo, akijaribu kumlinganisha na taarifa fulani fulani alizozisajili kwenye ubongo wake.
Madam Sally akasogea moja kwa moja mpaka jukwaani, akapewa kipaza sauti.
"Kama kawaida! Hapa ni chemchemi ya burudani! Kula, kunywa, furahi!"
Akaondoka kwa mbwembwe, umati ukimshangilia sana kwa shangwe.

"Kwa hio unataka kusema huyo nd'o anasimamia shoo nzima au?" J4 akamuuliza D kwa sauti kubwa ili asikike pia.
Mwenzie akatikisa kichwa huku akiyumbayumba katika namna ya kufurahia burudani ya bendi ile.
"Na ni huyuhuyu anayewamiliki hao wasichana akiwemo huyo ambaye tunamtafuta!" D akatamka kwa kujiamini. Wakarudi kuketi na kuusubiri muda wao wa mawindo ufike.
Chupa zao zikawa tupu ndani ya dakika chache tu. Akaja mhudumu mrembo kuziondoa chupa zile na akauliza kwa tabasamu murua kama wanahitaji huduma ya ziada.
J4 na D wakatazama kwa kuibia kisha wakamjibu kuwa kama wakihitaji watamuita tu. Ni heri walitamka maneno haya, maana hata fedha zilizokuwepo mifukoni mwao ni za kuhesabu tu. Hapa hawakuja kuburudika, walikuwa na jambo lao.

Mhudumu yule akaanza kuhesabu hatua zake kuondoka kwenye meza ile. Upesi ishara zikatembea baina ya J4 na D kwa kasi kama umeme.
"Oyah, tumuulizie huyuhuyu, itakuwa anamfahamu!" J4 akamkonong'oneza D.
Mara ghafla,
"Da-dada..samahani, tunakuomba mara moja!"
Akaitwa tena kutokea pale pale kwenye meza aliyotoka.
Taratibu kwa mwendo wa madaha, kiuno chake chembamba kikipepea huku na kule akawafikia na kurejesha upya tabasamu lake usoni. Hii ni namna yao ya kipekee na nidhamu ya kuwahudumia wateja, waliyofunzwa katika klabu hii.

"Bila samahani!" Mwanya ukaonekana kinywani mwake, alipotamka maneno haya.
"Uum...samahani, sijajua kama una haraka lakini natamani nizungumze na wewe japo kwa dakika moja tu. Tafadhali..."
Nani huyu mwingine kama sio D?
J4 akaamua kuwa mtazamaji tu.
Muhudumu yule akalikoleza tabasamu lake na kuketi kando ya D,
D akajikohoza kidogo na kulazimisha tabasamu.
"Naam, naitwa Brown sijui we nani mwenzangu."
"Naitwa Sharon!" Binti akajibu kwa sauti ya kubembeleza iliyojaa uchangamfu. Hapa akazidi kumpandisha D mizuka.
"Ooh jina lako mbona zuri hivyo...ulijichagulia mwenyewe au?"
"Mmh..hapana! Kwa nini?" (Anacheka)
"Zuri sana aisee..na hongera jina lako linakufanana kwa uzuri!" D akazidisha mbwembwe.
Mbwembwe zake zikawa kero kwa J4 ambaye alitaka aende moja kwa moja kwenye pointi ya msingi.
"Naam, kuna mhudumu mmoja hivi hapa namtafuta. Uuum silifahamu jina lake, lakiniii ni mrembo mrembo hivi kama wewe...
Si mrefu sana, wala si mfupi sana..." D akaanza kuzunguka.
"Anaitwa Bebe!...Bebe nd'o jina lake!" J4 akaamua kuingilia kati. Jambo lililomfanya D ajichekeshe na kuomba radhi.
Yule mhudumu akashusha pumzi na kuwakagua J4 na D nyusoni mwao. J4 akiwa makini na D akijichekesha.
"Yupo..lakini kwema?" Akahoji.
"Aah dada...kwani sie tunaonekana kama wakorofi? Yule ni rafiki yetu tu tunataka tumsabahi, hivyo tu!" J4 naye akachonga tabasamu la uongo usoni mwake.
Binti akashusha tena pumzi zake na kusimama akiangaza huku na huko.

"Yule pale! Ngoja nikawaitie..."
"Ha-haamna shida sister...acha tu tutamuita wenyewe. Mbona hamna shida, we nenda tu tusikusumbue!" Wote wawili wakaruka na kumchangamkia.
"Mmh sawa!" Akaguna.
"Nadhani naweza kuondoka kama hakuna shida nyingine..." lile tabasamu lililokuwa usoni mwake likafifia. Na sasa yu tayari kuondoka.
"Uum naweza kupata mawasiliano yako tafadhali?" D akamuwahi na kumpatia simu yake ili anakili namba zake.
Kitendo cha kuombwa nambari za mawasiliano kikamrejeshea tabasamu lake la mwanzo.
"Mh za nini tena?" Akajibu huku akiwa ameipokea tayari na vidole vyake vimeanza kuchezacheza juu ya skrini ile ya simu-janja.
"Aah Sharon we naye....kwa hiyo hautaki niisikie sauti yako tena au?" Huyu ni D kwenye moja na mbili.

Wakati huu J4 alikuwa mbali sana. Macho yake yalimakinika kwenye kile kiwiliwili cha mwili ulioinama kuhudumia wateja, waliyeoneshwa na mhudumu huyu, Sharon.
Aliliona umbo matata lenye mwondoko wa kiwango cha nyota tano, lililomilikiwa na mhudumu huyu aliyempa mgongo. Kwa harakaharaka tu, angemtafsiri kuwa ni mrembo. Aliwatazama mamwinyi waliokuwa wakihudumiwa naye namna mate yanavyowadondoka walipokuwa wanamkagua binti huyu.

Umakini wake wote ukachotwa kwa binti yule. Kumtazama kwa nyuma tu ilikuwa ni burudani tosha na kumsubiria ageuke lilikuwa ni tukio kubwa ambalo macho yake yalilisubiri kwa hamu, sawa na muumini aliyefunga mchana kutwa aisubiliavyo adhana ya jioni akale futari.
Naam,
Hata yeye alisubiri ageuke tu ili aione sura yake kwa mara nyingine tena, baada ya kuiona mara moja tu kwenye picha ya mtandaoni.

Mara ghafla, binti yule akageuka!
Macho ya J4 yakatiwa ukungu, ikawa ni kama eneo lile anamuona yeye tu. Kwa mara ya kwanza maishani mwake, macho ya J4 yakaishuhudia kazi tukufu ya sanaa ya uumbaji wa Mungu.
Mdomo wake ukabaki wazi, akapigwa na butwaa.

"Oa Jeifoo...Oa Jeifoo!" Akashtuliwa na D asimsikie.
"Oa vipi unaangalia nini mzee? Umeona mali mpya nini?" D akamuuliza akijaribu kukagua upande ule ambao J4 ametazama.
Alipogeuka tu na yeye akaungana naye kwenye huu msafara.
Wote wawili wakamtazama.

"God bless Africa!"
J4 akahamishia mikono yake kichwani kwa mshangao. D naye alibaki kukikuna kidevu chake chenye ndevu chache zilizokosa rutuba. "Hii nd'o maana halisi ya kisu kikali kaka...yaani hapa aisee!" Akamalizia J4, huku akiketi vyema kwenye kiti chake.
"Enhe nd'o yeye sasa huyo halafu ni kama anakuja huku." D akaweka nukta ili wamtazame kwa ukaribu zaidi. Hili ndilo lilikuwa windo lao haswaa.

Ni yule yule Bebe!
Akakatiza karibu na meza yao kwa madaha, mwendo wake ule ule maarufu kama 'catwalk'. Harufu yake murua ya manukato ikazivamia pua za J4 na D na kuwaachia mateso.
Huku nyuma, mtikisiko wa nyama zake zilizompa umbo namba 8 zikawa kama msumari wa mwisho kwenye jeneza la urembo wake.
Msumari huuhuu ukamchoma J4, akashika kifua chake.

"Oyah bro!" J4 akatamka huku akisimama.
Bado macho yao yanamsindikiza Bebe mpaka alipoingia ndani ya kaunta.
"Vipi unamfata au sio wa levo zako..." sauti ya D iliyojaa kicheko ikamuuliza J4.
"Em ngoja nikajaribu! Lakini dah, ngoja tuone..." hakueleweka.
Akatembea moja kwa moja kuelekea ilipokuwa kaunta.
Ile hali ya kujiamini aliyokuwa nayo ikaanza kuporomoka kwa kasi. Akakagua huku na huko na macho yake yakanasa tena kwa Bebe kama sumaku.
Wakati huu Bebe alikuwa akipakia vinywaji kwenye tenga lake kuvipeleka kule alikoagizwa.

J4 akasogea karibu na njia ambayo ni lazima tu angekutana naye asma la watapishana. Mapigo ya moyo wake yakaanza kwenda kasi.
Woga ukamvamia, na ili asionekane kama mwenye aibu,
Akaiwasha simu yake ya mkononi na kuipekua pekua bila mpangilio. Mara aende kwenye faili la picha mara atoke, mara aingie kwenye orodha ya majina ya watu atoke. Alikuwa amekamatika haswaa.
Huyu ni binti aliyekuwa anamuwinda kwa siku nyingi bila mafanikio, mara baada ya kukutana na picha yake kwenye mitandao ya kijamii na kuzisikia habari zake.
Leo hii ni huyu hapa mbele yake...mwili wake ukapigwa ganzi.
Akarudisha simu yake mfukoni baada ya kugundua kuwa anaelekea kwenye nusu-uwendawazimu kama sio kuwehuka kabisa.

Akazubaa pale kaunta akimtazama Bebe kwa muda mrefu. Jambo hili likamfanya agande kwa dakika kadhaa bila kujua la kufanya.
"Karibu bro!...Nikuandalie kinywaji gani?"
Mhudumu mwingine aliyekuwa mule ndani ya kaunta akamkaribisha kwa bashasha.

J4 akashtuka na kujiweka sawa,
"Uum...naomba Vant moja hapo!" Akatamka kwa kujiamini. Akatoa noti moja ya shilingi elfu tano ya kitanzania. Ilikuwa noti pekee aliyokiwa nayo mfukoni, na labda ingemsaidia kama nauli usiku huu. Yeye akaitumia ili asionekane mnyonge mbele ya Bebe.
Huyu ni mwanaume!

Akapewa chupa ile ndogo na kabla hata hajaanza kuipunguza. Bebe huyooo, akaondoka tena.
Namna gani!
J4 naye akasimama na kinywaji chake kuelekea uelekeo uleule sawa na Bebe. Lakini akajihadhari sana asigundulike kama anamfatilia. Akachagua kubaki nyuma yake, tena kwa mita za kutosha, akizuga kuwa bize na simu yake na mkono mwingine na chupa ndogo ya kinywaji kile kikali.

Upande mwingine, D alikuwa anaifatilia hii sinema ambayo kwake ilikuwa ya kuchekesha.
Akakumbuka viapo na tambo za J4 kuwa akimtia machoni tu huyo mlimbwemde wa kuitwa Bebe, hatachelewa kumsaini kama mpenzi wake mpya.
"Duh! Huyu dogo ataishia kula kwa macho tu."D akasema na nafsi yake.
"Hapo kanunua mzinga ili aoshe, halafu hana nauli! Mmh...yangu macho tu."
Akaweka kituo na kuegamia kiti chake, kicheko chepesi kikamtoka baada ya kumuona J4 anarejea, uso wake ukiwa umesawajika.
Hakuna alichokuwa ameambulia, zaidi ya kuwa mpenzi msindikizaji.

Usiku mchangamfu, uliopambwa na burudani ukaendelea pale LE CLUB GRANDE.
Saa sita kasorobo usiku!


********

Ni shughuli hizi za kiofisi pekee zilizoibana ratiba ya bwana Didace Ambrozi. Yeye kama mkurugenzi wa kampuni hii kubwa ya usindikaji wa vyakula na vinywaji hapa nchini, CHIVIHI & KABATI COMPANY LIMITED.
Daima meza yake ilijaa mafaili na nyaraka lukuki zilizoisubiri saini yake tu ili shughuli nyingine ziendelee.
Atasaini bila kuzipitia nyaraka hizi?
Hapana.
Ilimbidi azipekue, azichambue na afanye milinganyo kwenye mizani ya faida na hasara kabla ya kuidhinisha shughuli yoyote ile.

Asubuhi ya Jumatatu hii, meza yake ilikuwa vilevile kama alivyoiacha Ijumaa iliyopita, kama alivyomwelekeza karani wake ampangie nyaraka zote.
Ikamlaki kwa bashasha, ikiwa imepangwa vyema.

Kama kawaida yake akaanza kwa sala fupi, kisha akaketi na kuanza kupekua faili moja baada ya jingine.
Akaiona karatasi ambayo alikuwa akiichorachora na kuandika vitu ambavyo havieleweki. Akaguna,
'Nini hiki?' Akajiuliza.
Lakini hakukaa muda mrefu kabla hajamkumbuka Bebe.
Naam, ni yeye aliyekuwa akiongea naye jioni ya siku ile kwenye simu na bila kuelewa akajikuta amechorachora maandishi yale juu ya karatasi, kama tu yalistahili kuitwa maandishi.

Hapohapo akaachana na nyaraka,
Akaegamisha mgongo na kichwa chake juu ya kiti chake kikubwa cha kuzunguka. Akaenda huku na kule, fikra zake zikiwa kwa Bebe tu.
Akaifikiria sura yake nzuri na utukufu wa urembo wake wote.
Halafu ajabu!
Akakumbuka kuwa eti naye ni kahaba anayeishi kwenye danguro, tena kwa kulelewa!
Bwana Didace Ambrozi akasikitika sana.
"Maskini..." Akatamka.
"Halafu naye, akili yake imeshafungwa minyororo ya utumwa. Eti ameridhika na hali aliyo nayo." Akatikisa tena kichwa chake.
"Lazima nitamsaidia tu. Siwezi kumuacha apotee kwenye msitu wa ukahaba! Kama atazikataa fedha zangu, basi hatozikataa fursa nitakazompatia zimuinue!" Aliyatamka haya akiwa analichora neno BEBE juu ya karatasi ile.

Mara simu yake ya mezani ikaita, akajinyoosha kabla hajaipokea. Alikuwa ni karani wake, aliyemtaarifu kuwa meneja wa masoko anahitaji kuwasiliana naye.
"Vipi nimuungamishe na wewe bosi?", sauti ile ya kike, changamfu yenye nidhamu ikamuuliza.
"Naam, muunganishe! Halafu Tessy..."
"Abee Bosi!"
"Niandalie kahawa hapo...na kama kawaida usisahau kuweka cocoa, sukari iwe ya kusikilizia!" Akaamrisha.
"Hamna shida Bosi!"

Baada ya sekunde chache simu yake ikaita na aliyekuwa hewani ni meneja masoko.
"Habari za Asubuhi mkuu!" Akasalimiwa.
"Salama tu kaka...habari yako Mr. Atumanya Kiiza!"
"Kwema mkuu...nisijue huko kwenu."
"Kwema. Naam...nakusikiliza!"
"Uum..samahani mkuu kuna mswada tuliutuma kwako hapo tangu Alhamisi iliyopita. Nadhani utakiwa umeuona!"
"Mswada kutoka wapi huu...idara ya masoko au?" Didace akauliza huku akipekua nyaraka zilizokuwepo mezani pale.
"Naam mkuu...faili namba CVK/345/7..." Hakumaliza.
"Naam nimeliona!" Didace akamkatisha.
"Eeh mkuu tunatarajia kufanya utekelezaji kuanzia wiki hii. Nadhani ukilipitia utaona tulichokijadili kwenye kikao chetu mkuu!" Akatamka kwa nidhamu.
"Bila shaka Mr. ATM, bila shaka, nitalipitia upesi." Akamtamkia na kumuita kwa jina ambalo alilitumia kiutani tu.
Wakaagana na macho yake yakavutiwa na mada mbalimbali zilizokuwepo kwenye mswada ule.

Ulikuwa ni mpango mkakati wa kuongeza ubunifu wa matangazo ya bidhaa zao hasa kwenye vipindi vya televisheni kubwa za hapa nchini.
Mr. Didace Ambrozi akaketi vyema kwenye kiti chake na kuusoma mpango huu, tena kwa umakini mkubwa.
Kwenye ukurasa wa mapendekezo,
Kulikuwa na hoja ya kufanya usaili wa kumtafuta binti mrembo atakayeweza kusimama mbele ya kamera na kuigiza tangazo la bidhaa zao.

"Mungu wangu!" Bwana Didace alianza kuuhisi ushindi moyoni mwake. Akalitazama neno BEBE alilokuwa amelichora juu ya karatasi ile.
Hii ilikuwa ni nafasi ya dhahabu aliyokuwa anaisubiri kwa muda mrefu.

Ni kweli Bebe hakuwa na elimu ya kutosha, mpaka amuweke kwenye ofisi mojawapo ndani ya kampuni ile.
Wala hakuwa na ujuzi wa kazi yoyote ile ya kiofisi hata ya kufanya usafi tu, hata hivyo hili la Bebe kufanya usafi halikumfanana.
Kwake alilitafsiri kama kitendo cha kukufuru kazi tukufu ya Mungu aliyoifanya kwenye mwili wa Bebe.
Lakini hili la kumtafuta mrembo wa kufanya promotion (matangazo) ya bidhaa halikuhitaji vyeti vya darasani.

Bwana Didace akasimama na kushangilia kwa nguvu akitupa ngumi zake hewani. Akafumba macho na kumuona Bebe akiwa kwenye majukwaa makubwa ya mitandao na media kubwa hapa nchini.
Akaziona bidhaa za kampuni hii zikinunuliwa kwa wingi.
Akayaona matangazo na mabango makubwa pale jijini yakiwa na picha zenye lile tabasamu angavu la Bebe.
"Bahati iliyoje kwa mabango haya kumiliki sura yenye urembo usiopimika kama ile?" Akajiuliza.

Akarudi na kuketi upya juu ya meza yake mara moja akamwaga wino wake juu ya ule mswada huku akitabasamu.
Karani wake akagonga mlango, akamruhusu aingie ndani.
Alikuwa kabeba kisinia cha udongo chenye jagi na kikombe kidogo pamoja na jagi maridadi.

"Hii hapa mkuu!" Akatamka kwa nidhamu.
"Enhe vipi na wewe kikombe chako kiko wapi?"
Akamuuliza huku furaha yake ikionekana waziwazi.
"Nani mimi?" Binti yule mwenye nidhamu akauliza kana kwamba mule ofisini alikuwepo kiumbe hai mmoja tu.
"Ah, mi nishakunywa Bosi..." akajiwahi.
"Kaa hapa tunywe pamoja bwana...utachangamka lini wewe? Enhe?" Akamshurutisha kwa uchangamfu. Binti yule akaenda na kurudi akiwa na kikombe chake kisha akaketi bila kujiamini.

"Tessy! Mbona huniulizi mama? Eh? Niulize kwa nini nimekupa hii ofa!" Didace Ambrozi amechamngamka.
"Mh..kulikoni tena?" Binti akauliza akiwa na aibu.
"Hahahahahaha!" Kicheko cha ushindi kikamtoka Didace. Hili likazidi kumshangaza sana binti huyu.
"We furahi tu mama yangu...muda sio mrefu chapa ya bidhaa yetu inaenda kuwa ya moto sokoni. Tutauza mnoooo! Hahaha!"

Huenda cheko lake lilibeba matumaini. Huenda alikuwa na imani kubwa na mambo yatakayozaliwa na mswada huu aliousaini.
Kwake ilikuwa ni vita ambayo alianza kuuona ushindi wake akilini, na silaha yake aliyokuwa nayo aliiamini kwa asilimia zote.
Hakujua kuwa silaha aliyo nayo hajaizoea vya kutosha.
Akasahau ule msemo usemao kuwa, silaha usiyoizoea usiiamini!




ITAENDELEA.....
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…