Mpelelezi aliyekuja alikuwa ni mwanamke na alikuja akiwa peke yake. Alikuwa amevaa shati la kijivu la mikono mifupi na suruali. Alikuwa hajachomekea na nilihisi ni kwasababu sehemu ya shati iliyoning’inia ilikuwa ni kwaajii ya kuficha bunduki, pingu au chochote kile alichokuwa amebeba. Alikuwa na uso wa mviringo uliojaa nywele. Hakuwa amevaa urembo wowote. Hata pete tu hakuwa nayo. Nilikadiria umri wake kuwa kwenye miaka ya thelathini na tano kupanda juu. Labda arobaini mwisho. Alikuwa ni mwanamke wa kuvutia. Nilivutiwa naye mara tu nilipomuona. Alinionesha kitambulisho chake. Kilikuwa kina namba za ofisini kwake na namba yake ya simu. Kilikuwa pia kina barua pepe yake. Alilitamka jina lililokuwa kwenye kadi yake hiyo. Jina lenyewe lilikuwa ni Theresa Lee. Alikuwa na asili ya Asia. Nilihisi kutokana na jina lake la Lee.
Alianza kuongea, “Unaweza kuniambia ni nini haswa kilichotokea?”
Aliongea kwa sauti ya upole, huku akiwa kaziinua kope zake. Unaweza kuniambia? Unaweza? Kama vile, unaweza kustahimili kuniambia? Nilitabasamu, kidogo. Katikati ya New york ni sehemu ambayo mauaji yapo kwa asilimia chache sana. Na hata kama Theresa alikuwa ameshuhudia kesi za mauaji tangu siku ya kwanza alipoingia ofisini, bado nilikuwa namzidi kuona maiti kwa wingi. Tena kwa idadi kubwa tu. Na kusema kweli yule mwanamke kwenye treni sio kwamba maiti yake ilikuwa imeharibika sana, hapana. Nilikuwa nimeona maiti zenye kutisha kuliko ile.
Kwahivyo nilimwambia kila kilichotokea, kuanzia kule mtaa wa Bleecker, kuja zile pointi kumi na moja, namna nilivyojaribu kuokoa jahazi, yale maongezi, bunduki na hatiame kujiua kwa yule mwanamke.
Theresa Lee akataka tuiongelee orodha ya zile pointi kumi na moja.
“Tunayo hiyo orodha,” Alianza kusema. “Ninadhani inapaswa kuwa siri.”
“Imekuwa wazi takribani miaka ishirini sasa,” Nilimwambia. “Kila mtu anaijua. Sio siri tena.”
“Wewe uliionea wapi?”
“Israeli,” Nilijibu na kuongeza. “Kipindi ambacho imemalizwa tu kuandikawa.”
“Inawezekana vipi”
Kwahivyo nikaanza kumtajia historia yangu. Kwa ufupi. Jeshi la marekani, miaka kumi na tatu ya polisi wa wanajeshi, kuwa kwenye kitengo cha uchunguzi, huduma niliyofanya karibu ulimwengu mzima, jumlisha vikazi vya hapa na pale hadi pale nilipopunguzwa na jeshi.
“Ulikuwa afisa tu au cheo gani?”
“Cheo kikubwa cha Meja.” Niijibu.
“Na sasa hivi unafanya nini?”
“Nimestaafu.”
“Mbona umri wako bado sana.”
“Niliamua nile maisha nikiwa bado kijana.”
“Na unahisi unakula maisha kweli?”
“Sio sana.”
“Na jana usiku ulikuwa unafanya nini? Huko Bleecker?”
“Nilienda kusikiliza muziki.”
“Na ulipopanda treni ulikuwa unaelekea wapi?”
“Nilikuwa naenda kutafuta chumba mahali popote au labda ningeenda kuchukua basi.”
“Uende wapi?”
“Popote.”
“Kama utalii au?”
“Ndiyo.”
“Kwani unaishi wapi?”
“Siishi popote. Mimi naenda popote nitakapotaka.”
“Begi lako liko wapi?”
“Sina begi.”
Watu wengi wakifika hapo huwa wananiuliza maswali yasiyo na msingi, Lakini Theresa hakuniuliza. Baadala yake macho yake yalibadilika na akabadilisha mada, “Ninashangaa kuona orodha ilikuwa haipo sahihi. Nilidhani ilitakiwa kuwa asilimia miamoja sahihi.”
Aliongea kwa kuniaminia. Kama vile ambavyo askari mmoja angeongea na askari mwenzie.
“Ilikuwa haiko sawa kwa sehemu ndogo tu, lakini kwenye kujiua ilikuwa ipo sawa.” Nilijibu.
“Ni kweli, lakini ilikuwa ukweli nusu tu.”
“Ni bora ukweli nusu kuliko uongo mtupu.” Nilijibu halafu nikaongeza swali. “Mmekwishafahamu chochote kuhusu huyo mwanamke?”
“Bado. Lakini tutapata chochote muda sio mrefu. Wananiambia kwenye tukio wamepata funguo na waleti. Naamini vitatoa mwanga. Lakini kuna kitu bado sielewi kwanini alivaa koti.”
Nilisema, “Mimi pia sijui.”
Theresa alikaa kimya, kama aliyekwazika. Nilianza kuongea, “Haya mambo kila siku yanatakiwa kufanyiwa mamboresho. Binafsi nahisi tuongeze pointi ya kumi na mbili kwa wanawake.”
“Wazo zuri.”
“Na kuna kitabu nilisoma kinasema kuwa ile sehemu kuhusu kukuta bikra mbinguni ni tafsiri iliyokosewa. Inamaanisha ni kitu chenye sukari. Maziwa na asali.”
“Unataka kuniambia wanajilipua kwa sababu ya maziwa na asali?”
“Sina hakika.”
“Wewe ni mtaalamu wa lugha?”
“Hapana! Ila naongea Kiingereza,” Nilisema. “Na kifaransa. Halafu kwanini mwanamke anayejilipua atakake bikra? Unajua maandiko mengi matakatifu yametafsiriwa vibaya. Haswahaswa sehemu ambazo mabikra wamehusishwa. Hata ukiangalia Agano jipya kwa mfano. Kuna watu wanasema Mariam alikuwa ni mama kwa mara ya kwanza, sio bikra. Ninaamini waandishi wakifufuka watacheka sana kuona kilichoandikwa sasa hivi.”
Theresa Lee hakutoa oni lolote. Baadala yake aliuliza, “ Upo sawa?”
Nilichukulia swali lake kama anauliza pengine nilikuwa nahitaji ushauri wa daktari kutokana na nilichokishuhudia. Labda pengine kuongea sana kwangu kulimfanya ahisi nimechanganyikiwa. Lakini nilikuwa nimekosea.
“Nipo sawa,” Nilimwambia.
“Mimi ningekuwa wewe ningekuwa ninajuta sasa hivi kwa kumfuata yule mwanamke. Pengine wewe ndiye ulisababisha kifo chake. Labda ungemuacha angebadilisha maamuzi yake.”
Tulikaa kimya kwa muda baada ya hiyo kauli halafu akatokea askari mwingine aliyetingisha kichwa kumuita Theresa. Waliongea kwa sauti ya chini ambayo sikuweza kung’amua maneno. Theresa alikuja tena na kuniomba niongozane naye kwenye chumba cha mahojiano.
“Kwanini?” Niliuliza.
“Ndiyo utaratibu.” Alinijibu. “Ili tuchukue maelezo yako yachapwe jarada lifungwe.”
“Sina uhuru wa kukubali au kukataa?”
“Usianze ubishi,” Theresa aliniambia. “Kumbuka kuna ile orodha ya pointi kumi na moja na wewe ni shahidi. Tunaweza kuamua kukuweka tu ndani hadi uote mvi na ufe. Kwahivyo usijaribu kuleta usumbufu usio na sababu.”
Niliinua mabega juu na kumfuata hadi kwenye gari yake. Ilikuwa ni Ford Victoria, na uwezo wake lazima nikiri ulikuwa mzuri. Ilitupeleka mpaka kituoni kulipokuwa na hiyo ofisi ya mahojiano. Tuliingia na kupanda ngazi za juu. Tulipokifikia chumba alikifungua na kunipisha niingie ndani kwanza. Alipohakikisha nimeingia aliufunga mlango kwa nje na kuniacha ndani peke yangu. Nilikaa humo peke yangu kwa dakika ishirini hadi Theresa alipoufungua tena mlango.
Awamu hii hakuwa peke yake. Alikuwa amembatana na bwana mmoja hivi aliyekuwa amebeba faili. Aliliweka faili mezani na kumtambuisha yule bwana kama askari mwenzake. Aliniambia jina lake lilikuwa ni Dochery. Aliniambia yule Dochery alikuwa na maswali kadhaa ya kunihoji.
“Maswali yapi?” Niliuliza.
Kwanza akaanza kwa kunipatia kahawa na nitumie bafu kuoga. Nilikubali vyote. Dochery alinisindikiza hadi sehemu ambayo nilitumia kuoga, niliporudi kulikuwa na vikombe vitatu vya kahawa mezani. Nilichukua kikombe kimoja cha kahawa na kukionja. Kahawa ilikuwa ipo poa sana. Theresa na yule Dochery walichukua vikombe viwili vilivyokuwa vimebaki.
“Embu anza tena kusimulia mkasa mzima ulivyokuwa,” Theresa alisema.
Kwahivyo nilianza upya. Ndani ya dakika tano tulianza kulijadili suala zima tena. Kama watu watatu wanaofanya kazi pamoja. Halafu ghafla hali ikabadilika.
Dochery aliuliza, “Ulijisikia vipi?”
Niliuliza, “Nilijisikia vipi kuhusu nini?”
“Kipindi anajiua?”
“Nilifarijika angalau alikuwa haniui mimi.”
Dochery alianza kusema, “Sisi ni kitengo cha mauaji. Lazima tuchunguze chanzo cha kesi yeyote kujua kama kuna utata wowote. Nadhani unaelewa.”
“Utata kama upi?” Niliuliza.
“Tunahakikisha kama hakuna zaidi ya kinachoonekana kwa macho tu.”
“Hakuna zaidi. Alijipiga risasi mwenyewe.”
“Hayo umesema wewe.”
“Hakuna aliyekuwa kwenye ile treni atakuambia tofauti na ninachokuambia.”
Dochery alisema, “Huwa kuna mambomambo hapo katikati.”
“Unanihisi vinginevyo?” Nilisema.
“Ndiyo. Labda wewe ndiye uliyempiga risasi.”
Theresa Lee aliniangalia kwa jicho la huruma. Nikasema, “Sikumuua mimi.”
“Basi labda ilikuwa ni bunduki yako.”
“Haikuwa bunduki yangu. Ile bunduki ni mzigo mkubwa sana na sina begi la kuibebea.”
“Wewe una umbo kubwa la mwili. Suruali yako inaweza ikawa na mifuko mikubwa.”
Theresa Lee akanitazama tena kwa jicho la huruma. Kama anayeniambia, pole unapitia haya yote.
“Hiki ni nini? Unajifanya askari mwerevu, au unaonyesha ulivyo askari mjinga?”
“Unasema mimi ni mjinga?”
“Umethibitisha hilo wewe mwenyewe. Kama nilimpiga mimi sasa hivi ningekuwa nimefungwa pingu. Ningekuwa nimechukuliwa alama za vidole na usingenipeleka bafuni kuoga halafu ukabaki nje. Lazima ungekuwa na mimi kila sehemu.”
“Siwezi kufanya hivyo mpaka nithibitishe uliua kweli.”
“Kwani watu wa hospitali wanasemaje?”
“Bado hatujapata taarifa kutoka kwao.”
“Lakini mashahidi wengine walikuwepo.”
Theresa alitikisa kichwa kukataa, “Hawana msaada wowote. Hawakuona kilichotokea.”
“Lazima waliona.” Nilisema.
“Mgongo wako ulikuwa umewakinga. Halafu, walikuwa hata hawaangalii kinachoendelea. Halafu wengi wao walikuwa wamesinzia na hawajui hata Kiingereza. Kwahivyo maelezo yao yalikuwa hayana msaada wowote.”
“Na yule jamaa fulani aliyekuwa mbele yangu. Mbona alikuwa macho. Na alionekana kama raia wa Marekani na anajua Kiingereza?”
“Jamaa yupi?”
“Alikuwa abiria namba tano. Alikuwa kavaa chinos na tisheti ya golfu.”
Theresa alilifungua faili lake. Alipopitisha mach akatikisa kichwa kidogo. “Hakuna abiria wa tano. Treni ilikuwa na abiria wanne tu, ukiweka na huyo mwanamke.!”