SEHEMU YA NNE
Tulitazamana kwa muda usiopungua sekunde kumi (10). Nilinyanyuka pale nilipokuwa nimekaa. Nilianza kumsogelea. Hakukuwa na cha kuogopa. Hata hivyo, bado ningeweza kufa hata kama ningekuwa umbali wa hatua thelathini sawa na ambavyo ningekufa kama ningekuwa umbali wa inchi moja kutokea ambapo yule mwanamke alikuwa amekaa.
Nilimpita yule mwanamke mwenye asili ya Kihispania aliyekuwa mkono wa kushoto. Nilimpita pia yule jamaa aliyekuwa amevaa tisheti ya NBA kwenye mkono wangu wa kulia. Nilimpita na yule mwanamke mwenye asili ya Afrika Magharibi aliyekuwa amekaa mkono wa kushoto kwangu. Alikiwa bado amelala.
Abiria namba nne alikuwa bado ananiangalia kadri nilivyokuwa nikielekea alipokuwa amekaa. Bado mikono yake alikuwa ameiweka kwenye begi. Nilisimama hatua sita kutoka alipokuwa amekaa.
Nilisema, “Ninachokifikiria juu yako naomba kisiwe kweli.”
Hakujibu chochote, ila midomo yake ilicheza. Mikono yake pia ilianza kucheza ndani ya begi.
“Naomba nione mikono yako?”
Bado hakujibu chochote.
“Mimi ni polisi,” nilidanganya. “naweza kukusaidia."
Bado hakujibu chochote.
“Tunaweza tukaongea juu ya hili suala lako.”
Hakujibu chochote bado.
Kwavile nilikuwa nimeshikilia machuma kwaajili ya abiria wanaosimama niliyaachilia. Kufanya hivyo kulinifanya nionekane mdogo. Mtu wa kawaida tu ambaye sitishi. Nilibaki nimesimama tu. Sikuwa na chaguo. Yeye alihitaji nusu sekunde tu ili aweze kufinya kitufe cha bomu. Mimi nilikuwa nahitaji zaidi ya sekunde mia tatu kumzuia asifanye jambo lolote la hovyo. Pengine ningeweza kumnyanganya begi kwa nguvu na kumsukuma aanguke chini lakini nisingesaidia chochote kwa sababu kabla ya mimi kuufikisha mkono wangu mahali alipokuwa ameshika begi basi angekuwa alishabonyeza kitufe cha kuruhusu lilipuke zamani sana.
Hakukuwa na tumaini lolote.
Niliwaza labda nimtoweze uwezo wake kwa kumpiga ghafla kwa nguvu kichwani kwa pigo moja safi ili apoteze fahamu, lakini hesabu zangu zilikataa. Hata kama ningekuwa mwepesi na kasi kiasi gani, umbali aliokuwepo haukuwa rafiki kwangu mimi kurusha ngumi itakayompata vyema na kumjeruhi kabla hajabofya swichi ya bomu. Lazima angeniwahi. Hakuna ubishi juu ya hilo.
“Naweza kukaa karibu yako, “ Nilimuuliza.
“Hapana. Usinisogelee.” Alijibu huku akiwa bado ananiangalia machoni.
Sauti yake ilikuwa kavu. Hakukuwa na lafudhi ya kigeni kwenye maneno yake. Nilihitimisha kuwa ni Mmarekani, lakini lafudhi peke yake haitoshi kumfanya mtu awe mmarekani. Angeweza kuwa raia wa nchi nyingine yeyote ile. Kwa ukaribu nilikuwa namuona vizuri zaidi. Kutokana na maneno yake sikutikisika au kupiga hatua yeyote. Nilibaki nimetulia, lakini midomo yangu ilifunguka.
“Umechelewa,” Nilianza kuongea. “Sasa hivi sio muda sahihi.”
Mikono yake ilicheza ndani ya begi.
“Nahitaji kuona mkono wako mmoja tu, tafadhali.”
Ghafla treni ilisimama. Niliyumba kidogo halafu nikarudi kusimama wima. Akili yangu iliniambia ni vyema nikazishikilia zile chuma kwa sababu walioziweka hawakuwa wameziweka kwa bahati mbaya. Nilipotulia nilimuangalia halafu niliendelea kuongea.
“Nioneshe mkono mmoja.”
Hakujibu chochote tena. Pia hakuwa ananiangalia machoni wakati huu. Alikuwa anaangalia kiunoni kwangu. Kwa kuwa kitendo cha kushika zile chuma kulifanya shati langu linyanyuke juu kidogo, hivyo alama za kovu liliko kwenye kiuno changu zilionekana. Ilikuwa ni kidonda kilichotokana na mlipuko mkubwa wa bomu huko Beirut, ambapo nilikuwa umbali wa yard 50 tu kutokea eneo la mlipuko. Leo nilikuwa Yard 33 tu kutoka alipokuwa amekaa yule mwanamke.
Alirudisha macho yake usoni kwangu tena. Nilijua nini kinafuata. Watu wengi baada ya kuliona hilo kovu huwa wananiuliza nililpata vipi jeraha kubwa kiasi hicho. Sikutaka aniulize hilo swali, hivyo kabla hajaongea nilianza kuongea.
“Nioneshe mkono wako mmoja.”
“Kwanini?” Aliniuliza.
“Kwa sababu hauhitaji miwili yote kuwemo humo.”
“Sasa nikikuonesha utafaidika nini?”
“Sijui,” Nilimjibu.
Kusema kweli sikuwa najua nilikuwa nafanya nini. Kwanza mimi sio mtaalamu wa mateka. Nilikuwa naongea tu ilimradi. Jambo ambalo siyo haiba yangu. Kikawaida mimi ni mtu mkimya sana, lakini sikuwa tayari kufa ikiwa ninaweza kukiepusha kifo kwa kuongea. Labda ndiyo maana nilikuwa ninaongea. Huwa inashangaza sana namna mtu anavyofanya vitu pale ambao anakuwa kati kati ya mdomo wa mauti.
Yule mwanamke alichezesha mkono wake. Nilimuona akiongeza nguvu kwenye kitu alichokuwa amekishikilia ndani ya begi lake kwa mkono wa kulia halafu akautoa nje mkono wake wa kushoto taratibu. Ulikuwa mkono mdogo wa wastani. Mishipa ilikuwa inaonekana juu yake. Kucha zake pia zilikuwa zimekatwa vyema na hakuwa amevaa pete au urembo wowote mkononi mwake. Hivyo nilijua alikuwa hajaolewa na alikuwa hana hata mchumba. Baada ya kutoa mkono kwenye begi aliugeuza niuone upande wa pili. Hakuwa ameshika chochote, lakini ulikuwa mwekundu kwa sababu ya joto.
“Ahsante.” Nilisema.
Alitikisa kichwa kukubali halafu akauweka mkono wake kwenye siti iliyokuwa jirani na yeye. Treni ilianza kutembea tena. Baada ya sekunde kadhaa ilipita chini ya daraja. Kulikuwa na giza sana.
“Nioneshe kilicho ndani ya begi lako.” Nilisema baada ya treni kutoka kwenye giza na kuuona mwanga.
“Kwanini?”
“Nahitaji kujua.”
Hakujibu chochote.
Hakufanya muondoko wowote.
Alikuwa bado anatafakari nini cha kufanya. Nilimuingilia kati kati ya mawazo yake. “Sitokichukua hicho kilichomo ndani ya begi lako. Nakuahidi. Nia yangu ni kukiona tu. Basi.”
“Sioni sababu yeyote kwanini unilazimishe kuona kilicho kwenye hili begi.” Aliongea hatimaye
“Huoni sababu yeyote?” Nilimuuliza.
“Ndiyo.”
“Sikiliza. Mimi ninahusika kwenye huu mpango. Lengo la mimi kutaka kuona ni nataka kujua kama kila kitu kipo sawa, sijui kama unanielewa? Na kama hakipo sawa nikirekebisehe kwaajili ya matumizi ya baadae. Sasa hivi sio muda mzuri.”
“Lakini si ulisema wewe ni askari?” Aliniuliza.
Nilibaki nababaika, lakini hatimaye nilipata jibu la kumpatia. Sio zuri sana ila niliamini angeridhika nalo.
“Ndiyo. Lakini nilisema naweza kukusaidia pia. Haukumbuki?”
Alikaa kimya.
Treni ilianza kupunguza kasi. Niligeuka nyuma. Sio kwa kupenda, ili nilijikuta tu. Sekunde chache baadae niligeuka tena kumuangalia yule mwanamke. Mkono wake ulikuwa unacheza cheza tena ndani ya begi kama mtu aliyekuwa anataka kutoa kitu.
Nilibaki namuangalia tu. Hatimaye begi liliachia kile kilichokuwemo na aliunyanyua mkono wake wa kushoto. Nukta chache baadae, Mkono wake wa kulia pia ulitoka kwenye begi.
Hakuwa na betri la bomu. Hakukuwa na nyaya nyingi zilizoungwa wala swichi na wala vyote vinavyohusiana na bomu.
Kulikuwa na kitu kingine kabisa cha ajabu na tofauti kabisa. Nilitetemeka. Sio kwa uoga, bali kwa mshtuko.
SEHEMU YA TANO:
BOFYA HAPA.