SEHEMU YA SITA
Treni ilisimama. Tofauti na mwanzo, sasa hivi milango haikufunguka. Labda kuna mtu alikuwa amebonyeza kitufe cha hadhari au labda kondakta alikuwa amesikia mlio wa ile bunduki. Vyovyote vile, nilichokuwa najua kwa wakati ule ni kuwa milango ya treni haikufunguka. Lilikuwa ni jambo zuri kwa sababu ni bora kumfungia kichaa mwenye bunduki ndani ya gari kuliko kufungua akakimbia. Pengine walihisi labda kuna mtu alikuwa anaua watu huku nyuma ndiyo maana milango ilibaki imefungwa.
Mpenzi msomaji, huwa iko hivi, Bunduki kubwa kama Magnum 357 ilitengenezwa mwaka 1935 na kupachikwa jina la Magnum. Hiyi Magnum ni kilatini kinachomaanisha kubwa. Hivyo hata risasi inayokaa kwenye hii bunduki inatakiwa kuwa kubwa sana. Kikawaida wakati ambao risasi hutoka kwenye hii bunduki moto huwa unawaka kwa sababu ya Oxygen na mkwaruzano ulio hewani na ndiyo maana mwanga wa moto huonekana bunduki inapopigwa. Lakini kwa kesi kama ya abiria namba nne na namna alivyokuwa amejifyatua risasi huwa inapita kwa kasi na kuacha tobo kubwa huku ule moto ambao ulitakiwa kuwaka baada ya risasi ukifuatilia nyuma kwa nukta chache. Hivyo huwa unasambaa chini ya ngozi na kuzilipua nyama nyama au kulifunia kabisa fuvu kama ndizi iliyomenywa.
Ndicho nilichokuwa nakiangalia mbele yangu. Uso wa yule mwanamke ulikuwa kama tambala bovu lililochanika huku nyama zenye damu zilikuwa bado zinaning’inia. Nguvu ya ile risasi ilikuwa imetoboa shimo kuanzia usawa wa mdomo wake kuelekea juu kutafuta eneo la kutokea ambapo ilisambaratisha ubongo na fuvu lake kwa sehemu kubwa. Kwa namna moja au nyingine alikuwa amepoteza kichwa na akili zake. Na uhai. Mwili wake ulikuwa umelegea. Kidole chake cha shahada kilikuwa bado kimejikunja kama vile kilikuwa bado kimeshika trigger, licha ya kuwa bunduki lake halikuwa mikononi mwake. Ilikuwa imemponyoka baada ya kujifyatua.
Sauti ya ule mlio wa bunduki bado ilikuwa akilini mwangu. Nyuma nilizisikia sauti za ukimya wa abiria wenzangu. Pua yangu ilianza kuhisi harufu ya damu zilizokuwa zinatoka kwenye mwili wa yule mwanamke. Nilijivuta nikasogea mbele nikaanza kukagua begi lake. Halikuwa na kitu. Niliusogelea mwili wake nikafungua zipu. Hakukuwa na kitu isipokuwa blauzi nyeupe aliyokuwa amevaa kwa ndani.
Nilijivuta nikasogea hadi kilipokuwa kifaa cha kuitia tahadhari. Nilisogea karibu na maiki nikaanza kuongea.
“Mauaji. Kuna mtu amejipiga bunduki.”
Baada ya kusema hivyo akili yangu ilitulia na kufurahi. Sio kwa sababu ya kile alichokuwa amekifanya yule dada, hapana. Ilikuwa ni kwa sababu tulikuwa tupo salama kwa sasa ukilinganisha na kama ingelikuwa ni bomu.
“Mauaji.” Nilisema tena baada ya ukimya na kukosa jibu kutoka kwa kondakta. Sikuwa nataka kusubiri hadi wakati ambao kitengo cha usalama, hiyo ni NYDP pamoja na SWAT, wajikusanye ndiyo milango ifunguliwe. Hilo lingechukua muda mrefu sana.
Baada ya dakika moja sauti ilisikika kwenye spika za matangazo. Alikuwa ni konda.
“Abiria wote mnatakiwa kubaki kwenye siti zenu. Kutokana na tukio lililopita muda sio mrefu, milango itabaki imefungwa kwa dakika chache kwa sababu za kiusalama.”
Alikuwa anaongea taratibu. Nilihisi labda alikuwa anasoma hayo maneno kutoka mahala fulani. Kwanza, sauti yake ilikuwa kama ya mtu anayetetemeka na ya kukwaruza kwaruza. Pili, haikuwa na ukawaida ndani yake.
Niliporidhika nilijivuta hadi kwenye kiti kilichokuwa hatua tatu kutokea pale maiti isiyokuwa na akili wala kichwa ikiwa imelala.
Ingelikuwa ni muvi, Vitengo vyote vya usalama na askari polisi wangekuwa wamefika eneo la tukio nukta chache tu baada ya mlio wa bunduki. DNA ingekuwa imekwisha hakikishwa na walio nyuma ya hilo tukio wangekuwa wamekwisha kukamatwa na kusomewa mashtaka pamoja na hukumu zao. Lakini haya yalikuwa ni maisha halisi. Ulipita muda mrefu kabla usalama wafike.
Maaskari sita waliingia ndani ya treni. Walikuwa wamevaa kofia na sare zao. Niliwakadiria walikuwa wapo kwenye patrol usiku huo. Wote tuliinua mikono yetu juu baada ya kuwaona. Sijui kwanini, lakini wote tuliinua mikono yetu juu.
Askari mmoja alibakia mlangoni kuziba nafasi, wengine watatu walienda hadi ilipo kuwepo maiti ya yule mwanamke halafu wakasimama hatua kama sita kutokea ilipokuwa maiti ya yule mwanamke. Hawakuahangaika kuangalia kama ana viashiria vyovyote vya uhai ndani yake kwa kusikiliza mapigo ya moyo kwenye mkono wake wa kushoto. Hawakuweka kioo mbele ya pua zake ili kujua kama alikuwa bado anapumua. Nilihisi ni kwa sababu mbili. Moja, Alikuwa amekufa hata kwa jicho la kawaida. Pili, alikuwa hana pua au niseme TOINYO kutokana na uimara wa shaba aliyokuwa amejipiga.
Askari ambaye alionekana kuwa mkubwa kwao aligeuka nyuma. Alikuwa amekasirika kidogo, lakini alijitahidi kuweka sura ya kawaida.
“Nani shahidi wa hili tukio.”
Hakuna aliyejibu. Sio mwanamke mwenye asili ya Kihispania, wala jamaa mwenye shati ya NBA, hata yule wa ki-Africa. Wote walikuwa wamekaa kimya. Pointi namba nane, Angalia mbele tu. Kama haumuoni mtu, basi na yeye hakuoni. Hata jamaa mwenye tisheti ya golfu alikuwa kimya tu.
“Alitoa bunduki kwenye begi akajipiga nayo kichwani.” Hatimaye niliongea.
“Hivyo tu.” yule askri alihoji tena.
“Ndiyo au hapana.” Nilimjibu.
“Kwanini?” Yule askari aliuliza.
“Sijui. Nitajua vipi?”
“Wapi na saa ngapi?”
“Humu humu kwenye treni. Sina hakika kuhusu muda.” Nilimjibu.
Yule askari aliandika kitu kwenye karatasi. Alihitimisha ile maiti ni matokeo ya kujipiga risasi mwenyewe. Hata hivyo, barabara za gari moshi za chini zilikuwa ni jukumu la NYPD. Hivyo hii kesi ilikuwa ni jukumu lake – Hilo halina ubishi.
Alitikisa kichwa halafu akasema, “OK. Wote shukeni kwenye gari hadi pale nje ambapo tutachukua majina na anuani zenu pamoja na maelezo kidogo.”
Baada ya kutupa maelekezo alibonyeza radio call yake. Alianza kutaja namba za siri fulani ambazo sikuzielewa. Nilihisi labda alikuwa anaita sekta ya matibabu na dawa. Baada ya hapo ingekuwa ni jukumu la wenye usafiri kufanya usafi kwenye gari lao. Haikuwa kazi ngumu. Niliwaza. Hata hivyo ilikuwa bado ni usiku sana kuwa asubuhi.
Tulitoka ndani ya lile gari moshi na kujikusanya pembezoni kidogo. Askari wengi walikuwa wameanza kufika eneo la tukio. Dakika tano zilipita kabla ya gari la wagonjwa mahututi kufika. Waliokuwa ndani ya gari la wagonjwa walishuka na kuingia ndani ya gari moshi. Sikuweza kuona nini kiliendelea huko ndani.
Huku nje askari waliendelea kupita na kuhoji watu. Yule askari kiongozi wa doria ile ya usiku alikuja kwangu. Mimi ndiye nilikuwa nimejibu swali lake ndani ya treni hivyo alinipa kipaumbele cha kuhojiwa wa kwanza. Aliponifikia alinichukua kuniongoza hadi kilipokuwa kituo cha stesheni cha polisi. Aliniweka kwenye chumba f’lani cha mahojiano. Tulipokaa alianza kwa kuniuliza jina langu.
“Michael Kichaka.” Nilisema.
Aliliandika kwenye karatasi yake bila kusema chochote. Alipomaliza kuandika alisimama akaelekea ulipokuwa mlango. Nilijua kwanini alikuwa anataka kuondoka. Alikuwa anamsubiria mtu. Nilikuwa najua alikuwa anamsubiria nani. Sio kwa jina au sura, ila kwa cheo. Alikuwa anaondoka hadi hapo atakapokuja mpelelezi kwaajili ya kunihoji. Hilo halikuwa na ubishi.