Riwaya Kali; Briefcase

Riwaya Kali; Briefcase

RIWAYA; BRIEFCASE
MWANDISHI; HALFANI SUDY
WhatsApp 0674 395733

Sehemu Ya Nne

Haikuwa safari ndefu. Saa mbili na dakika kumi alifika Vikindu getini. Alisimama wakati akifikiria aanzie wapi kumtafuta James Luganda. Alex alitumia dakika tano kuzungukazunguka pale stendi, akimtafuta mtu angalau mwenye kuonekana mwenyeji wa eneo lile, hakumwona. Alipoangalia, akakumbuka kitu.

"Hawa dereva bodaboda wanaweza kumfahamu"

"Mambo vipi kaka" Alex alimsalimia dereva bodaboda mmoja.

"Safi tu kaka, wapi? Unaenda Malela au Vianzi" Dereva bodaboda aliuliza.

"Hapana kaka, kuna jamaa mmoja nilikuwa namuulizia" Alex alisema.

"Anaitwa nani?" Dereva bodaboda aliuliza.

" Anaitwa James Luganda" Alex alisema.

"Mimi simfaham. Ngoja nimuite Ras tumuulize, yeye ni mwenyeji zaidi yangu" Yule dereva bodaboda alisema.

Akaitwa Ras na kuulizwa kama anamfahamu James Luganda.

"Mmmh mimi simfahamu John. Lakini kule karibu na ofisi ya serikali za mitaa kuna mzee anaitwa mzee Luganda ila ana mtoto wa kike anafanya kazi Saluni anaitwa Lilian. Labda watakuwa wanafahamiana John" Ras alisema.

Moyo wa Alex uliripuka kwa furaha. Alikumbuka katika kitambulisho cha James Luganda kilionesha amejiandikia katika ofisi ya serikali za mitaa.

"Nipeleke" Alex alisema harakaharaka.

"Haina shida ni buku tu" Ras alisema huku akiwasha pikipiki yake.

"Naenda kutatua utata wa briefcase" Alex aliwaza akiwa juu ya pikipiki.

"Ni nyumba ile nyeupe." Ras alimuonesha Alex nyumba ya mzee Luganda, naye aliondoka bila ya kuona kama alimpeleka sehemu sahihi ama sivyo.

Kuondoka kwa Ras ilikuwa furaha kwa Alex. Alitaka kufanya uchunguzi wake mwenyewe bila bughudha ya mtu. Aliisogelea ile nyumba kwa mwendo wa taratibu. Alifika barazani, alisimama kidogo kisha akaizunguka ile nyumba mara mbili. Nyumba ilikuwa kimyaa. Alirudi tena barazani na kupiga hodi. Hakujibiwa. Alipiga tena, kimyaa. Sasa aliita huku akigonga mlango, bila kutegemea mlango ulifunguka lakini hodi haikuitikiwa. Bila kufikiria Alex aliingia ndani huku akiita hodiii.
Lilikuwa kosa la mwaka!!!

Alex alifika kwenye sebule pana yenye harufu mbaya. Macho yake yalishuhudia picha za kutisha ambazo hajawahi kuziona tangu azaliwe, huku pua yake ikikaribishwa na harufu kali ya damu!! Alex alibaki akiwa amesimama wima, mapigo ya moyo yakipiga kwa nguvu kama yanataka kutoka nje ya kifua chake. Jasho la ghafla lilimpata huku uwoga wa kutupwa ukidhihirishwa machoni mwake. Sio tu ilikuwa mara yake ya kwanza kukutana na maiti zilizouwawa kikatili namna ile, ilikuwa ni mara yake ya kwanza pia kukutana na maiti katika umri wake wa miaka ishirini na tano. Alibaki amepigwa na bumbuwazi kwa dakika tano, wakati dakika ya sita inaingia ndipo alipopata wazo la kurudi nyuma na kukimbia. Alirudi stendi na kupanda gari la kuelekea Mbagala rangi tatu, siku ilianza vibaya sana tofauti na jana yake ilivyoanza vizuri kule Posta.

***

Taarifa za vifo vya mzee Luganda na mkewe zilianza kusambaa taratibu. Majirani wawili walioenda kuwasalimu wazee hao ndio waliotoa taarifa kituo cha Polisi cha Vikindu, Polisi wa Vikindu walipoona namna mauaji yalivyofanyika waliwataarifu wenzao wa Mkuranga, ndipo Inspekta Jasmin, askari mgeni katika kituo cha Mkuranga alipopewa kazi ya kuchunguza kesi hiyo.

Watu walikuwa wamejaa katika nyumba ya mzee Luganda. Watoto wake wote wawili walikuwa wameshafika msibani. Nje makundi ya watu wakiongea tetesi mbalimbali juu ya kifo kile cha kinyama walichofanyiwa wazee wawili.

Mara, gari ya Polisi ya Mkuranga iliwasili. Nyuma walishuka askari Polisi watatu wakiwa wamevaa sare za jeshi hilo. Mbele alishuka dereva na askari wa kike aliyekuwa amevaa sare safi za jeshi la Polisi. Watu wote waliwapisha askari wale, na macho ya watu wengi wakimwangalia yule askari wa kike aliyetangulia mbele.

"Wapo wapi ndugu wa marehemu?" Inspekta Jasmin aliuliza alipofika ukumbini.

"Sisi" James na dada yake Lilian walijibu. Na wazee wengine wawili nao walijibu. Wakati huo miili ikiwa imefunikwa tu kwa kanga pale sebuleni.

"Nawahitaji watu wa kwanza kuziona hizi maiti" inspekta Jasmin alisema.

"Ni wale pale majerani zetu" James alisema huku akiwaonesha kwa kidole majerani wawili.

"Nitawahitaji kituo cha Polisi kwa ajili ya kutoa maelezo" Inspekta Jasmin.

"Sawa" Wale wazee walijibu kwa uwoga.

"Afande Adrian zichunguze hizo maiti na kuzipiga picha, kisha tafuta watu wanne wa kuja kuzitoa hizi maiti kabisa" Inspekta Jasmin aliamrisha.

"Sawa afande" Adrian alijibu huku akipiga saluti.

"Poleni sana ndugu zangu kwa msiba huu. Kupoteza wazazi au ndugu wawili kwa mpigo na jambo baya sana. Sisi kama jeshi la Polisi tunawaahidi kuwakamata watu wabaya waliofanya mauaji haya, ingawa tutahitaji msaada wenu sana kama ndugu katika upelelezi" Inspekta Jasmin alisema.

"Sawa afande, tutawapa ushirikiano wote mtakaouhitaji ili kuhakikisha aliyewakatili wazazi wangu anakamatwa" James alisema wakati Lilian alikuwa analia.

"Ninyi tutaenda pamoja pia kituoni kwa maelezo" Inspekta Jasmin aliwaonesha James na Lilian. "Pamoja na ndugu wawili hapo. Hivyo tutaondoka watu sita, sawa?"

"Sawa" Wote waliitikia.

"Nimemaliza afande" Adrian alisema.

"Haya vijana kazibebeni zile maiti. Bebeni kwa umakini" Inspekta Jasmin alisema.

Vijana wawili walienda kubeba maiti ya kwanza, na wale wengine walibeba maiti nyingine. Wakati maiti ya mzee Luganda ikinyanyuliwa ndipo kitambulisho kilichokuwa kimemganda mgongoni kilidondoka katika dimbwi dogo la damu.

"Kitambulisho!!" James alisema.

"Hebu kilete hapa hiko kitambulisho afande Adrian. Hakikisha haukishiki kwa mkono" Inspekta Jasmin alisema.

Kwa kutumia mkono wenye 'glove' afande Adrian alikichukua kile kitambulisho. Akampa Inspekta Jasmin ambaye naye alikuwa amevaa 'glove' mkono mmoja. Akakishika vizuri kitambulisho kile na kukisoma. Akabaki amekishika vilevile.

Watu wote walikaa kimya.

"Tumepata pa kuanzia uchunguzi wetu. Muuaji yeyote yule hawezi kufanya mauaji bila kuacha ushahidi nyuma yake. Twendeni" Inspekta Jasmin alisema. Na watu sita, pamoja na wale askari walitoka nje na kuelekea hospitali ya wilaya ya Mkuranga kisha kituo cha Polisi, ambapo mahojiano ya wale watu sita juu ya mauaji ya mzee Luganda na mkewe yalifanyika.

Watu wa kwanza kuhojiwa walikuwa ni wale majerani wawili. Ambao walielezea namna walivyoingia kwa mara ya kwanza mle ndani na kuzikuta maiti. Pia walielezea namna mzee Luganda na mkewe wakivyoishi na majerani pale mtaani kwao.

Baadae waliingia wale ndugu wawili, ambao walikuwa ni kaka zake na mke wa mzee Luganda. Nao walieleza jinsi wanavyowafahamu wazee wale ndani ya familia.

Kisha akaingia Lilian Luganda, akiwa analia isivyo kawaida.

"Pole sana dada kwa msiba mzito" Inspekta Jasmin alisema.

"Ahsante sana dada" Lilian alisema huku akijifuta machozi ambayo yalikuwa yanaendelea kutoka.

"Kaa kwenye kiti dada. Usilie dada yangu ndio mitihani ya dunia" Inspekta Jasmin alisema. Lilian alikaa kwenye kiti akiwa anatazamana na Inspekta Jasmin.

"Naitwa Jasmin. Ndiye askari ninayesimamia hii kesi ya kuuwawa kwa ndugu zenu. Wewe unaitwa nani? Na una uhusiano gani na marehemu?" Inspekta Jasmin aliuliza huku akiandika katika karatasi iliyokuwa juu ya meza.

"Naitwa Lilian Luganda. Ni mtoto wa pili wa mzee Luganda"

"Kumbe ni wazazi wako, pole sana Lilian" Inspekta Jasmin alisema.

"Nashukuru dada" Lilian alijibu.

"Wewe unaishi pale nyumbani na wazee?" Inspekta Jasmin aliuliza.

"Ndio naishi nao pale" Lilian alijibu.

"Mnaishi watu wangapi mle?" inspekta Jasmin aliuliza.

"Tulikuwa tunaishi watu watatu. Mimi, baba na mamaaa" Lilian alisema na kuanza kulia tena.

"Nyamaza Lilian, jikaze, nijibu maswali yangu ili tumpate mtu aliyewauwa baba na mama yako ili naye ahukumiwe" Inspekta Jasmin alisema.

Lilian alianza kufuta machozi tena.

"Hebu nambie hali ilikuwaje nyumbani kwenu kuanzia jana asubuhi hadi leo"

"Hali ilikuwa nzuri tu afande. Jana mimi niliamka saa moja asubuhi na kujiandaa kwenda kazini, wakati namaliza kujiandaa mama alinifata chumbani. Tulisalimiana na nilimuaga kuwa naenda kazini. Nilirudi kazini saa kumi na mbili jioni. Nilifika nyumbani na kumkuta baba akiwa barazani akisikiliza redio, nilimsalimia na kuingia ndani. Nilikutana na mama sebuleni akitoka nje, naye nilimsalimia. Nikaenda ndani kubadili nguo kisha kwenda jikoni kupika chakula cha jioni. Nilipomaliza kupika, nilienda sebuleni, ambalo niliwakuta baba na mama wakiangalia TV. Niliungana nao, hadi saa mbili usiku, tulikula na mimi nilienda ndani kulala nikiwaacha baba na mama palepale sebuleni.

Leo niliamka saa moja asubuhi. Nilijiandaa kwenda kazini, nilipomaliza nilienda kugonga chumbani kwa mama, nilimsalimu na kumuaga kuwa ninaenda kazini. Saa mbili kama na nusu hivi alikuja dereva bodaboda wangu anaitwa Ras pale saluni kwangu, akanitania kwamba kuna jamaa amempeleka nyumbani kwa ajili ya kuleta posa. Tukataniana akaondoka zake. Saa moja baada ya kuondoka Ras ndipo nilipopigiwa simu kwamba nirudi nyumbani mama anaumwa. Niliporudiiii....." Lilian alishindwa kumalizia. Aliangua kilio kikubwa akiombeleza kifo cha wazazi wake.

"Pole sana Lilian" Inspekta Jasmin aliacha kuandika na kumwangalia Lilian. Ndio ukubwa huo, lazima uzikabili changamoto kama hizi kwakuwa wewe ni mtu nzima" Inspekta Jasmin alisema.

"Inaniuma sana Afandeee, baaaba jamaniii, oooh mama mmeondoka nyote kwa pamojaa, mmetuacha wakiwa!" Lilian alilia kwa majonzi.

Akiwa bado analia Inspekta Jasmin alimtupia swali.

" Nani unahisi atakuwa kawauwa wazazi wako?"

Lilian Luganda alinyamaza ghafla na kumwangalia yule askari wa kike, katika maswali yote hili hakulitegemea.

"Hakuna mtu ninayemhisi moja kwa moja afande, ingawa huyo mgeni aliyempeleka Ras nina mashaka naye" Lilian alijibu huku akimshangaa askari yule pamoja na kumueleza kuhusu mtu yule bado hajang'amua kitu.

Inspekta Jasmin aliandika, kisha akarusha swali lengine tofauti.

"Kaka yako anafanya kazi gani?"

"Sasa si atakuja mwenyewe na kumuuliza. Mbona ananiuliza maswali yasiyonihusu"Lilian aliwaza kichwani mwake.

" Alikuwa mhasibu katika kampuni ya A&B, lakini kwasasa sifahamu maana aliacha kazi pale " Lilian Luganda alijibu huku akianza kuona askari yule anamuuliza maswali ya kipuuzi.

"Umeolewa?" Inspekta Jasmin aliuliza tena.

"Hapana sijaolewa" Lilian alijibu huku akionekana kukereka na maswali yale.

"Unamfaham mtu anayeitwa Alex Manda?" Bila kujari Inspekta Jasmin aliendelea kuuliza.

"Hapana ndio nalisikia leo jina hilo" Lilian alijibu.

"Hujawahi kuwasikia wazee wako hata siku moja wakilitaja jina hilo?" Inspekta Jasmin aliuliza tena.

"Hapana, ndio nalisikia hapa kwa mara ya kwanza" Lilian alijibu tena.

"Nashukuru sana kwa ushirikiano wako. Mwambie kaka yako aingie" Inspekta Jasmin alisema na Lilian alitoka nje taratibu.

Dakika mbili mbele aliingia kijana wa kiume. Alikuwa kijana mrefu aliyejazia kimazoezi. Macho yake yalikuwa hayatulii mahali pamoja huku sura yake ikionesha hofu kwa mbali. Inspekta Jasmin aliyaangalia yote hayo kwa jicho moja tu na kuyaona.

Kijana alifika na kukaa kitini. "Habari yako kaka" Inspekta Jasmin alimsaliamia wakati kijana akikaa.

"Nzuri afande" Kijana alijibu kwa sauti nzito.

"Naitwa Jasmin. Ni askari ninayefatilia kifo cha wazazi wenu kama nilivyojitambulisha kule nyumbani kwenu. Sijui wewe unaitwa nani?" inspekta Jasmin alijitambulisha na kuuliza swali.

"Mimi naitwa James Luganda. Mtoto wa kwanza wa mzee Luganda" James alisema.

"Wewe unakaa pale nyumbani?" Inspekta Jasmin aliuliza swali analolijua jibu lake.

"Hapana. Mimi nimepanga huko Bunju. Nilihama pale nyumbani miezi sita iliyopita" James alijibu.

"Kwanini ulihama pale nyumbani kwenu?" Inspekta Jasmin aliuliza.

"Nilihama tu kwa lengo la kuanza maisha yangu mwenyewe" James alijibu.

"Sio ulihama baada ya kupata kazi mpya yenye maslahi zaidi?" Inspekta Jasmin aliuliza.

"Nilijua tu. Najua Lilian amekwambia hivyo lakini hiyo siyo sababu" James alijibu.

"Kwasasa unafanya kazi gani?" Inspekta Jasmin aliuliza.

James alikaa kimya.

"Usinambie huijui kazi unayoifanya?" Inspekta Jasmin alikazia.

"Ni Mhasibu katika kampuni ya R.M" James alijibu huku akiogopa.

"Ananidanganya" Inspekta Jasmin aliwaza.

"Una muda gani tangu uajiriwe kwenye hiyo kampuni?" Inspekta Jasmin aliuliza.

"Ni mwaka wa tatu sasa" James alijibu

"Ananidanganya Lilian alinambia miezi sita" Aliwaza Inspekta Jasmin.

"Lini ulihama kutoka kampuni ya A&B na kuhamia RM?" Inspekta Jasmin aliuliza.

James alibabaika vibaya sana. Hakujiandaa na maswali namna hiyo kwakuwa hakutegemea kabisa kuulizwa maswali kuhusu yeye badala ya wazazi wake. James alitoa kitambaa mfukoni na kujifuta jasho. Muda uleule Inspekta Jasmin alipeleka kombora lingene.

"Unamfahamu Alex Manda?"

James Luganda macho yalimtoka pima mithili ya kijusi kabanwa na mlango. Kama maswali yale yalimtoa jasho, hili la sasa lilimtoa mkojo kabisa. Jina la Alex Manda lilikuwa ni swali zito sana kwake.

"Unamfahamu Alex Manda?" Inspekta Jasmin alirudia swali.

James Luganda alibaki kimya.

"Nakuuliza kwa mara ya tatu, unamfahamu Alex Manda?" Inspekta Jasmin sasa alibalika.

James Luganda hakujibu.

Je nini kitatokea? Tuwe wote katika sehemu ijayo.
 
RIWAYA; BRIEFCASE
MTUNZI; HALFANI SUDY
SIMU 0674 395733

Sehemu Ya Nne

James alibabaika vibaya sana. Hakujiandaa na maswali namna hiyo kwakuwa hakutegemea kabisa kuulizwa maswali kuhusu yeye badala ya wazazi wake. James alitoa kitambaa mfukoni na kujifuta jasho. Muda uleule Inspekta Jasmin alipeleka kombora lingene.

"Unamfahamu Alex Manda?"

James Luganda macho yalimtoka pima mithili ya kijusi kabanwa na mlango. Kama maswali yale yalimtoa jasho, hili la sasa lilimtoa mkojo kabisa. Jina la Alex Manda lilikuwa ni swali zito sana kwake.

"Unamfahamu Alex Manda?" Inspekta Jasmin alirudia swali.

James Luganda alibaki kimya.

"Nakuuliza kwa mara ya tatu, unamfahamu Alex Manda?" Inspekta Jasmin sasa alibalika.

James Luganda hakujibu.

"Afande Adriiian!!" Inspekta Jasmin aliita kwa nguvu. Adrian aliingia na kupiga saluti.

"Mweke lock up huyu, nitamuhitaji baadae" Inspekta Jasmin alisema.

Afande Adrian alimchukua James Luganda na kumpeleka selo. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza James kuwekwa selo. Aliogopa sana.

"Nenda hospitali kafatilie ripoti ya uchunguzi wa kidaktari uniletee hapa. Halafu waruhusu hao ndugu wa marehemu wakauchukue miili ya marehemu. Waambie James bado tunaendelea naye na mahojiano" Inspekta Jasmin alisema.

"Sawa afande" Afande Adrian aliitikia, alipiga saluti na kutoka nje.

***

Ndani ya selo alikutana na watu watatu. Baada ya kama dakika ishirini waliingizwa watuhumiwa wengine watatu. Wakituhumiwa kwa kesi mbalimbali. James Luganda alikuwa amejipweteka kwenye kona moja ya selo, selo yenye harufu ya uvundo na vitu visivyoeleweka, huku ukutani kukiwa na michoro mbalimbali.

Nje ya selo, katika ofisi ya Inspekta Jasmin, kulikuwa na kikao cha watu wawili. Inspekta Jasmin na afande Adrian.

"Sasa Adrian, kwa mujibu ya maelezo ya hawa watu, kuna watu wawili wa muhimu sana kuwasaka. Bila shaka watu hao ndio watakuja kumaliza utata. Watu hao ni dereva bodaboda mmoja wa pale Vikindu, jina lakini kamili hatuna ila jina lake maarufu ni Ras. Mtu mwingine muhimu katika upelelezi huu ni Alex Manda, kijana ambaye kitambulisho chake kimekutwa eneo la mauaji" Inspekta Jasmin alisema.

"Huyo Alex Manda naye anaishi Vikindu?" Afande Adrian aliuliza.

"Inavyoonesha haishi pale. Kitambulisho chake kinaonesha amejiandikisha katika kituo cha huko Mbagala maji matitu. Hivyo chukueni na hii picha ili mkasake huko" Inspekta Jasmin alisema.

"Sawa Afande" Adrian alijibu.

"Fanyeni huo msako kwa haraka na umakini mkubwa. Tunataka tuimalize hii kesi haraka iwezekanavyo" Inspekta Jasmin alisema.

"Nimekuelewa afande" Adrian alijibu. Alipiga saluti na kutoka nje.

**SURA YA TATU**

NYUMBA moja iliyokuwa maeneo ya Mikocheni kulikuwa na kikao. Watu watano waliizunguka meza moja ya vioo iliyojaa vinywaji mbalimbali. Watu wote walikuwa wamevaa suti za gharama kudhihirisha uwezo wao kifedha. Sura zao zikionesha kuwa walikuwa wameridhika na maisha.

"Nashukuru sana wajumbe kwa kufika. Hiki ni kikao cha dharura. Kitakuwa tofauti kabisa na vikao vyetu vya kawaida. Tofauti kiutaratibu na mpangilio. Ngoja niende moja kwa moja kwenye mada maana hatuna muda mrefu wa kukaa hapa, ni hivi kuna tatizo dogo limetokea huko Vikindu nyumbani kwa wazazi wa James Luganda." Mzee mmoja mfupi mweusi alisema.

"Kumetokea nini tena nyumbani kwa JL?" Mzee mwengine mwembamba aliuliza. Alizoea kumwita James Luganda kwa kifupi.

"Jana asubuhi tulimtuma Fred sokoni Tandika mahali anakufanyia biashara yule kijana Alex. Nia yetu ilikuwa ni kumpeleleza Alex kama bado atakuwa na nia ya kufatilia mambo yetu. Fred alienda na kuchagua pea tano za viatu na kumwambia Alex kuwa atazifuata baadae. Alex aliuweka pembeni ule mzigo. Fred alirudi Posta na kumpigia simu Alex kwamba amletee vile viatu. Nia ni kumleta Alex karibu na jengo la RITA kuona atafanya jambo gani baada ya kuliona jengo lile. Alex alifika Posta na ule mzigo. Alimkabidhi Fred. Alitoka nje, alikuwa anataka kuondoka lakini aligairi, alielekea katika jengo la RITA!!" Mzee mfupi mweusi alinyamaza.

"Haa! Kumbe ana wazimu Alex, kashindwa kuvumilia baada ya kukaa mbali na sisi?" Mwanamke pekee aliyokuwa katika kikao kile alisema.

"Hakuweza mama Mwagito, na hilo ndilo tukilolitaka. Alex aliingia mle mjengoni na kuanza kupeleleza. Kwa bahati mbaya wakati anapanda juu waligumiana na James Luganda katika ngazi, na kwa bahati mbaya James alidondosha kitambulisho" Mzee mfupi mweusi alisema.

"Usinambie Alex alikiokota" yule mzee mwembamba alisema.

"Nakwambia Alex alikiokota na zaidi alianza kupeleleza James Luganda ni nani?. Hayo tuliyatarajia na tulishajipanga kumweka Alex kwenye mtihani kwa kuwatumia wazazi wa James Luganda" Mzee mfupi mweusi alisema.

"Sasa tatizo likuwapo?" Kijana mwengine mweupe aliuliza.

"Tulifanikiwa kila kitu. Ila tatizo James Luganda yupo kituo cha Polisi na hajatoka mpaka sasahivi" Mzee mfupi mweusi alionesha palipo na tatizo.

"Sasa hapo tatizo lipo wapi Don? James amefiwa na wazazi wake, lazima utegemee James Luganda atatakiwa Polisi kwa mahojiano" Mama Mwagito aliuliza.

"Walichukuliwa watu sita kwenda kutoa maelezo Polisi. Cha kushangaza sasa watu watano wameruhusiwa huku James Luganda akibaki ndani. Na mpaka sasa tunajiuliza ni ni kimembakisha James Luganda kule ndani? Hiyo ndio sababu ya sisi kama kamati ya ulinzi tuwe hapa muda huu" Mzee mfupi mweusi alisema.

"Mbona hii ishu ndogo sana. Watume watu Mkuranga wakapeleleze sababu ya James Luganda kubaki ndani. Wakapeleleze haraka na kuleta majibu katika kamati hii kesho asubuhi" Fred alisema.

"Hakuna tatizo. Hilo limepita. Ishu nyingine ni kuhusu Alex Manda. Tayari ameshaingia katika kundi letu kwakuwa tayari yupo katika mtihani. Leo ataenda kuelezwa majukumu yake" Mzee mfupi mweusi alisema.

"Kazi nzuri sana Don. Tutahitaji na faili kuhusu Alex Manda naye kesho asubuhi" Mama Mwagito alisema.

Kikao hiko cha watu watano kilifungwa. Huku Don akiachiwa jukumu la kutafuta vijana wa kufanya kazi.

***

Alex Manda alikuwa anazurura tu Mbagala rangi tatu. Akili yake ilikuwa imechanganyikiwa isivyo kawaida. Picha za maiti za mzee Luganda na mkewe bado zilikuwa zimemtawala kichwani.

" Hakika kuna watu makatili sana hapa duniani. Mtu anamchinja mwenzake mithili ya kuku! Mzee Luganda amechinjwa na kichwa chake kikiwa kinaning'inia pale shingoni sana. Yule mkewe sasa, wamemwacha na majeraha mabaya sana tumboni. Wamekufa vifo vibaya sana wale wazee" Alex alikuwa anawaza huku akielekea Mbagala maji matitu. Leo, aliamua kutembea kwa miguu.

"Kuna watu makatili sana hapa duniani. Wazee wale watakuwa na kosa gani liliwafanya waadhibiwe namna ile. Ni picha mbaya sana kuonwa na macho yangu. Kuna siri kubwa sana juu ya vifo vile. Kesho lazima niende Vikindu ili nijue undani wake. Nikiwa eneo la tukio nitapata tetesi tu kwanini watu wale wameuwawa" Alex alikuwa anawaza hayo akiwa njiani kuelekea nyumbani. Ndipo ghafla gari ya Polisi ilifunga breki miguuni mwake. Askari watano waliruka kule nyuma na bunduki zao mkononi. Midomo ya bunduki yote ilikuwa inakitazama kichwa cha Alex. Alex alikuwa anatetemeka. Hakujua kwanini askari wale walimvamia namna ile. Hakuwa mtuhumiwa, na wala hakuwa na rekodi yoyote mbaya ya kihalifu.

"Ni yeye! Ni yeye afande Adrian!" Askari alisema kwa mbwembwe huku akikiangalia kitambulisho mkononi mwake.

Afande alishuka mlango wa mbele wa gari ya Polisi. Akiwa kafura kwa hasira. " Upo chini ya ulinzi Alex. Unatuhukiwa kuwauwa bwana na bibi Luganda wa Vikindu...." Akili ya Alex iliishia hapo. Masikio yake hayakusikia maelezo ya mbele ya afande Adrian.

"Iweje atuhumiwe yeye katika mauaji yale? Polisi wamejuaje kama yeye alienda Vikindu nyumbani kwa mzee Luganda" Hakutafakari mara mbili. Alibebwa juu juu na kutupwa nyuma ya gari ya Polisi. Askari wengine walidandia lile gari na gari lilitiwa moto. Alex alikuwa amekamatwa.

Saa moja mbele afande Adrian alikuwa anamkabidhi Alex Manda mbele ya Inspekta Jasmin.

"Tumefanikiwa kumpata Ras na Alex Manda. Ras haikuwa kazi ngumu, tulienda na kumchukua pale Vikindu katika Kijiwe cha bodaboda. Ila Alex kidogo kasumbua. Tulienda katika ofisi za serikali za mitaa Mbagala maji matitu. Uzuri wake Alex alikuwa amepanga nyumbani kwa Mwenyekiti. Alimtambua na kutupeleka mara moja. Tulipofika na kuwauliza majirani kama Alex yupo, tulijibiwa kwamba alikuwa hajarudi tangu alivyotoka asubuhi. Tulikaa saa mbili kumsubiri. Hakurudi. Ndipo tulipoamua kwenda doria huku tukichukua namba ya Mwenyekiti atujulishe pindi atakaporudi. Wakati tunarudi njiani taa zetu za gari zilimlika mtu, na mimi moja kwa moja nilihisi ni Alex kwakuwa sura yake ilikuwa imeshaganda kichwani baada ya kukiangalia hiki kitambulisho mara nyingi sana. Tulimpakia Alex Manda ambaye ni huyu hapa mbele yako" Adrian alisema kwa kirefu.

"Kazi nzuri sana. Umefanya kazi kubwa na kwa wakati" Inspekta Jasmin alisema.

"Ahsante sana afande. Lakini pia ni jukumu langu afande" Adrian alijibu.

"Ni kweli afande. Sasa Adrian nataka uwe sehemu ya mahojiano nitakayomfanyia Alex. Moja kwa moja ninakujumuisha katika kesi hii hadi tutakapopata ufumbuzi. Funga mlango na tuanze kazi" Inspekta Jasmin alisema na Adrian alienda kufunga mlango.

Je nini kitaendelea?

Kwa wanaotaka kumuunga mkono mwandishi simulizi hii inapatikana WhatsApp 0674 395733 kwa sh 2000 tu.
 
Aisee we jamaa story zako zinakatisha tamaa, zinachelewa sana kiasi cha kupoteza morali Mkuu
 
Back
Top Bottom