HUBA LA MISS TANZANIA-PART 23
️[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586]
"Ooh my God.....looh salaleee...! picha yangu kabisaaa au mtu anayefanana na mimi?" aliuliza kwa mshtuko Shebby baada ya kusimuliwa na Sada juu ya ujio wa mtu wanayemhisi ni afisa usalama, ambaye alikuwa hana asili wala fasili mtu huyo machoni mwao. Mtu huyo alikuwa si mwingine bali ni Kachero Manu alikuwa amefika kazini kwao RAJA SAFARI TOURS kufanya taftishi na baadhi ya watumishi wa hapo. Kilichomleta hapo kwenye kampuni hiyo ni kujaribu kufanya taftishi kama muuaji wa Profesa Kaganda ndio huyo huyo muuaji wa Bwana Pateli! Taftishi ambayo ilizaa matunda asiyoyategemea kwa Kachero Manu. "Ni sura yako wewe nakufahamu vizuri sibahatishi na sijaja hapa kuleta maneno ya mkahawani au kwenye vijiwe vya kahawa" Sada alikazia maneno kwa ukali akionyesha kutopendezewa na ubishi wa Shebby. "Nisamehe bestito sijakusudia kukubishia, haya tuyaache kwanza, ehee...! Akasemaje sasa huyo jamaa kuwa nimefanya tukio gani? " aliomba msamaha Shebby huku akiendelea kumdodosa Sada. "Kapita kuhoji kila mtu pale kazini huku anamuonyesha picha yako, sasa Mzee Sheni yule mpishi wako uliyekuwa unaenda nae mbugani karopoka maneno ya sumu hata yasiyohusu, sijui oooh...! Ulikufukuzwa kazi kwa sababu mkichangia bibi na Bosi wetu marehemu Pateli, hapo ndio huyo mgeni akavutika na udaku wa Mzee Sheni kaondoka nae ofisini katokomea kusipojulikana... kila mtu anasikitika juu yake yule Mzee sijui ataacha lini taarifa za lolololo, zitakuja kumponza siku za usoni" alizidi kupasua maneno Sada bila mficho kwa Shebby bila kuelewa kuwa amemfaa vilivyo. "Naanza kuogopa sasa mie nimefanya kosa gani mpaka nasakwa kwa udi na uvumba! " alijisemesha kwa huzuni Shebby hali ya kuwa anajua kila kitu kinachoendelea. "Dalili zinaonyesha ni usalama wa taifa huyo mtu, maana kaja na gari zao nyeusi zile" alizidi kuweka tashididi ya mazungumzo yake. Shebby sasa taharuki ilimkamata vilivyo, alitambua sasa polisi wameshafika mbali kwenye uchunguzi wao wa mauaji ya mfululizo kuanzia kwa Bosi Pateli na Profesa Kaganda. Hivyo akizubaa kidogo tu itakula kwake atashindwa kutekeleza kisasi chake kwa Dr.Sonko. "Inabidi bestito Sada unipe hifadhi nyumbani kwako la sivyo nitaumbuka! " alivunja ukimya Shebby kwa Sada akiomba auni ya ulinzi. Sada alivuta pumzi ndefu baada ya kusikia maneno yake ya Shebby. "Unanipa mtihani mzito sana Shebby, maana hujaniambia umefanya nini mpaka unatafuta, lakini pia hata mie unanipa mashaka unaonekana mambo yako kiuchumi sasa yapo bambam unasukuma ndinga la gharama huenda kuna tukio zito umefanya unatafutwa!" Sada alitikisa kiberiti kwa Shebby huku akionyesha kama hatokubali kirahisi. Lakini uhalisia wa mambo Sada alikuwa anampenda kwa dhati Shebby alikuwa hawezi kupindua kwa chochote atakachomwambia. Kwa zaidi ya miaka 6 tokea wamefahamiana, Sada alikuwa moyoni anaungua kwa joto la mapenzi kwa Shebby, na ndio maana alipoona kuna mtu anamsaka Shebby alishindwa kujizuia kutokumpa taarifa. Miaka yote alikuwa anajipa moyo ipo siku tu, huenda Shebby atamtakia kuwa anampenda. Aliposikia Shebby amenasa kwenye huba la Miss Tanzania na kishatangaza ndoa, aliugua karibia mwezi mzima, yu mahamumu hoi bin taabani hajiwezi kitandani. Alipopata nafuu na kurudi kazini alianza kuzoea kuwa Shebby ndio kapuruchuka sio wake tena, lakini walipoonana siku Shebby amekuja kuchukua barua yake toka kuzimu pale ofisini, ugonjwa wake wa huba kwa Shebby ukaibuka upya. Meseji cha chombezo zile za umeamkaje, umeshindaje na za usiku mwema zilikuwa hazikauki katika simu ya Shebby toka kwa Sada. "Hata wewe Sada, mwandani wangu huniamini unaniona kama mimi ni mjuba nishakua mtu wa ovyo sasa nani ataniamini tena?" alijifaragua kujilalamisha mbele ya Sada huku akijivika usoni mwake huzuni kubwa na kujitia kuinama chini. "Baby.....usinidhanie vibaya, sikuwa na nia mbaya nikihofia tu nikataka unitoe wasiwasi mimi nakuaminia zaidi ya asilimia 100% huwezi kuniingiza matatizoni" alijibu Sada huku moyoni akiwa na mlipuko wa furaha wa kuitwa mwandani na Shebby kwa mara ya kwanza kwa muda wa miaka 6. Shebby akawa anachekea tumboni kwa namna alivyomnasa kiulaini Sada kwenye mtego wake wa kumpa hifadhi mpaka anaitwa 'baby'. Maana alifahamu fika sasa msako dhidi yake wakimkosa nyumbani kwake, utahamia kwenye mahoteli na nyumba za kulala wageni hivyo hatokuwa salama kabisa. Kimbilio pekee ambapo ni salama palibaki nyumbani kwa Sada na ingekuwa ngumu kwa vyombo vya usalama kuleta hisia kuwa Shebby yupo nyumbani kwa Sada." Nilikuwa nataka kushangaa sana kama na wewe Sada ni rafiki mnafiki yule mkia wa fisi, ambaye wakati wa shida anakuepa kama mkoma vile" alizungumza Shebby kwa kujiamini huku anamalizia 'Ice-cream' yake kushushia mlo wake kabambe. Wakaendelea kusogoa hadithi moja mbili tatu huku wakijiandaa kuondoka kuelekea nyumbani kwa Sada huku furaha ya Sada ikiwa ni sheshe kama kumsukuma mlevi akijua fika Shebby akifika kwake vibwanga na vitimbi atakavyomfanyia hawezi kupindua kwake.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586]
Ulikuwa ni usiku mbichi wa saa 2:30 usiku katika maeneo ya 'Mbezi Juu-Kwa Pembe' siku hiyo ya Jumamosi,Kachero Manu alikuwa ndio kwanza anaegesha kwenye eneo la maegesho la 'LIBRA SOCIAL HALL' gari yake aina ya 'Toyota Crown Royal Saloon' rangi ya maziwa. Aliegesha eneo ambalo hatapata usumbufu pindi atakapohitaji kuliondoa gari lake kwa haraka hasa ukichukulia siku hiyo ni ya mwishoni mwa juma, kadamnasi ya watu walikuwa wamefurika kuja kustarehe mpaka che. Ilikuwa dalili zinaonyesha ndani ya ukumbi ule kulikuwa kuna tafrija ya harusi inafanyika. Wahudhuriaji walikuwa wanazidi kumiminika huku wakiwa wamevalia mavazi yao nadhifu huku wakionekana wana furaha kubwa. Ghafla wakati Kachero Manu anajiandaa kuvuka upande aingie kwenye moja ya mashine za kutolea fedha zilizopo hapo hapo 'LIBRA SOCIAL HALL' usafiri wa Bwana na Bibi harusi ulikuwa unaingia. Fahari ya macho ikabidi Kachero Manu akodoe macho kuwaangalia wapendanao hao waliokuwa ndio wanashuka kwenye gari yao ya kifahari huku Bibi harusi akionekana kupendeza mpendezo wa Shamsi Matlai. Wakawa wanatembea masi masi kwa mwendo wa pole kuingia ukumbini mule,huku nyimbo mbalimbali za muziki zkipigwa kuchagiza uingiaji wao ndani ya ukumbi. Kachero Manu akapuuzia kuendelea kufuatilia yasiyomhusu akavuka ng'ambo ya pili na kuingia kwenye moja ya mashine ya kutolea fedha ya katikati inayomilikiwa na benki ya NBC, huku yasari kwake kulikuwa na mashine ya benki ya NMB na yamini kwake kuna mashine ya benki ya CRDB, na zote zilikuwa na watu wanachukua fulusi zao wakafanye mapochozi ya usiku huo kwenye starehe zao za mwishoni mwa juma. Akachukua kiasi cha pesa anachohitaji kisha akatoka na kuifuata barabara ya giza ya upande wa kulia kama alivyoelekezwa nyumbani kwa Shebby. Alitembelea kwa mwendo wa mashi mashi kwa takribani robo saa, mpaka akakutana na kibanda umiza kimejaza watu kibao wanashuhudia mchuano wa mechi za ligi kuu ya uingereza kabumbu uwanjani wachezaji wanamenyana katika runinga. Akapita na hamsini zake na hamna hata mmoja hata aliyegeuka kumtazama yeye. Alivyoenda mbele zaidi akaanza kuteremka bonde kushuka chini kwa mbali akawa ameziona nyumba nga'mbo ya pili zimejitenga. Akaenda mubashara kwenye baiti mojawapo ya kati kati ambayo ni duka la kuuza bidhaa ndogondogo. Alipofika dukani, alikuta wateja wanahudumia bidhaa mbalimbali za mahitaji yao ya siku, akazuga nae pia ni kama mhitaji wa bidhaa huku macho yake yote yanakodoa nyumba ya pili yake ambayo ndio nyumba haswa anayoishi Shebby. Alimuona mama mmoja yupo nje ya kibaraza anachoma maandazi. Akafanya maamuzi ya kumvaa yule kumuulizia kama Shebby yupo kwenye baiti. "Mama shikamoo...mimi ni mgeni wa mpangaji mwenzenu Shabani Zomboko sijui nimemkuta? " aliuliza Kachero Manu kwa yule mama. "Marhaba mwanangu, wala sifahamu maana huyo Shebby kutoka kwake na kurejea kwake anajuaga mwenyewe, labda umpigie simu au pita moja kwa moja na veranda hiyo chumba chake kimejitenga peke yake utakiona tu! " alijibu yule bila kumtazama usoni Kachero Manu huku akiweka maandazi mapya ya kuchoma kwenye karai linalochemka mafuta ikiwa ni ishara hana haja ya maswali zaidi yupo kikazi zaidi. Kachero Manu akajiongeza akaanza kutembea na veranda huku akigusa kiunoni kuhakikisha mguu wa kuku wake upo salama tayari kwa kutumika kama ikibidi. Kwa bahati baiti yote ilikuwa kimya kasoro chumba kimojawapo kulikuwa na muziki unapigwa kwa sauti ya chini. Akafika kwenye kile chumba kilichoungana na sebule alichopanga Shebby akakuta taa zimezimwa ishara ya kwamba hamna mtu ndani. Akaanza kubisha hodi kujiridhisha kama kweli hamna mtu. Aligonga kama mara tatu ukimya ukawa umetamalaki. Akaangalia muda kwenye saa yake ya mkononi, saa ikasoma ni saa 3:15 usiku juu ya alama. Himahima akachomoa mkungu wa funguo zake malaya mfukoni akaanza kukorokochoa kwa funguo hizo kwenye kitasa hicho cha mlango. Funguo wa tatu kujaribisha ukakubali kukifungua kitasa kile sasa mlango ukawa umefunguka. Haraka haraka akaingia ndani na kuurudishia mlango ule bila kufunga tena na ufunguo, alijua hatopoteza wakati mrefu. Akawasha kurunzi yake ndogo ya kumuwezesha kupata nuru ya kutosha kumuongoza chumbani mule huku mkono mwingine ukiwa umebeba bastola tayari kwa kushughulika ikibidi. Alipotupa macho kwenye sebule ile kwa haraka haraka hakuona chochote kitakachokuwa msaada kwake akaamua aelekee chumbani kwa Shebby. Kwa bahati alipokanyaga tu zulia la kujifutia miguu akahisi kama kuna kitu kigumu chini yake. Akanyanyua zulia lile akaona funguo mbili moja kubwa na nyingine zimeunganishwa kwa silsila nyembamba. Akatabasamu kwa jinsi mambo yanavyokwenda bambam. Akafungua mlango wa chumba kile akaingia bila hata kuubugaza mlango kwa pupa yake aliyokuwa nayo. Alipomulika kurunzi kitandani akakuta picha zimezagaa pale kitandani akasogelea na kuokota picha mojawapo. Ilikuwa ni picha ya Profesa Kaganda ikiwa imewekwa alama ya vema kuonyesha tayari ameshashughulikiwa. "Shabaaashi...! Huyu ndio muuaji asiyejulikana maluhuni mkubwa Shebby utanitambua mimi ni nani! " alijikuta anaropoka kwa sauti ya taratibu. "Tupa silaha yako chini na nyoosha mikono juu" ilikuwa ni sauti ya kama muungurumo wa radi katika masikio ya Kachero Manu huku mtutu baridi wa bastola ukiwa umegusa sikio lake la kushoto. Alishtukizwa kwa namna asiyoitarajia hata kidogo mpaka akajilaumu kwa kutochukua tahadhari ya kutosha. Bila ubishi wowote akatupa chini bastola yake na kunyoosha mikono yake, likawa ni kosa la kujutia la pili kwa Kachero Manu. Mtu yule aliyemuweka chini ya ulinzi akamnukiza puani kwa kitambaa, hanchifu kilicholowa kemikali. Pale pale Kachero Manu akajikuta anaishiwa nguvu na kuanguka chini puuuh kwa kupigiza kichwa kwenye tendegu la mguu wa kitanda kama papai lililoiva sana. Akapoteza fahamu chumbani mule mwa Shebby.
[emoji811][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586]