Gereza la Kifo - 52
Mtunzi - HAMISI KIBARI
ILIPOISHIA
Aliketi kwenye sofa ndefu pale sebuleni na kuendelea kusoma magazeti yaliyokuwa chini ya meza ndogo. Akiwa anaendelea kusoma magazeti yale ya nyuma, ghafla mawazo yake yalihamia kwa mwanae mchanga ambaye kwa sasa alikuwa akilelewa na mama yake Walari kule kijijini kwao baada ya kuchukuliwa kutoka kituo cha kulelea watoto wasio na wazazi ambako alipelekwa na wauguzi wa hospitali ya Bulibuli.
Alijikuta akitamani kumuona mwanae huyo mdogo haraka. Sasa akajipangia kwamba ikiwezekana kesho yake aende kijijini kwao kumuona mwanaye huyo mchanga ambaye wakati akikamatwa na hadi kufungwa, alikuwa hajamtia machoni.
Wakati akiwa katika lindi kali la mawazo, Walari alishituka pale aliposikia mtu anagonga mlango.
Endelea...
Wakati huo ilikuwa saa moja na kitu usiku. Giza lilikuwa limeshatanda kila sehemu.
Mariamu, alitoka kasi kuelekea mlangoni kufungua. Sekunde chache baadaye, watu waliokuwa wanagonga hodi waliingia. Alikuwa Nurdin na mkewe, mama Hadija.
Wote walipatwa na bumbuazi walipofika sebuleni na kumkuta Walari akiwa maeketi huku akitabasamu baada ya kuwaona.
Tena mama Hadija alitaka kupiga kelele akidhani ameona mzimu kama siyo msukule.
"Vipi, mbona mmeshikwa na mshangao.
"Ni wewe kweli, Walari, au tunaota," akauliza Nurdin akiwa bado kasimama katikati ya sebule huku bodo uso wake ukionyesha mshangao mkubwa.
"Ni mimi jamani. Ketini tuongee. Ni hadithi ndefu."
Ukiona miujiza ndiyo hii. Ni wewe kweli Walari?" Mama Hadija naye akauliza akiwa bado anatetemeka. Inaonekana dhahhiri alipatwana mshtuko mkubwa.
"Jamani kaeni chini tuongee. Mlipitia hospitali, siyo?"
"Ndiko tunakotoka na..."
"Najua mmeambiwa nimekufa, siyo?" Akadakia Walari akimkata kauli Nurdin.
"Ndiyo, tuliambiwa umekufa. Tumekwenda hadi chumba cha kuhifadhia maiti kuthibitisha, tukakuta jina lako kwenye kitabu cha watu waliokufa. Hivi sasa tulikuwa tunapanga namna tutakavyoshughulikia mazishi yako, na hasa tulikuwa hatujui taratibu za kuzika mtu aliyefia jela. Je, gereza litatupa tumzike wenyewe ama inakuwaje," akasema Nurdin akiwa anaketi kwenye kochi moja mkabala na lile alilokuwa ameketi Walari huku sasa uso wake ukichangamka.
Baada ya wanandoa hao kuketi, huku mama Hadija akionekana bado ana utando wa mkanganyiko kwenye uso wake, Walari alianza kusimulia kilichotokea.
Alielezea namna alivyofuatwa na mfanyakazi wa Masunju, ambaye pia ni hawara yake na kumweleza mpango aliousikia wa kumuua. Akawaeleza namna msichana huyo alivyomsikitikia hadi akaamua kwenda kumweleza ili kama anaweza kufanya lolote kujinasua na kifo afanye hivyo.
Akawasimulia namna alivyohangaika hadi alipoonana na mhudumu wa chumba cha maiti na kufanikisha mpango wa kumtorosha wodini baada ya kufanya udanganyifu kwamba kafa.
"Tena ilikuwa bahati Nyamagwila kuwahi kidogo, kwani dakika chache baada ya kunipiga sindano ya usingizi na kuonekana nimekufa, wale watu wa magereza wakawa wamefika. Walipoambiwa nimekufa wakaamini. Niamshukuru saa Mwenyezi Mungu," akasema Walari.
Nurdin na mkewe sasa walimwelewa Walari na nyoyo zao zikatulia, lakini swali sasa likawa namna Walari atakavyoishi katika hali hiyo.
"Sasa utajificha wapi ili isifahamike kwamba hujafa? Kwa sababu inatakiwa upotee angalau kwa miaka miwili hivi," akahoji Nurdin.
"Cha msingi ilikuwa kuokoka kifo. Hilo tutalipanga baadaye," akajibu Walari.
*************************************
Hatimaye kulikucha Walari akiwa nje ya gereza kwa kutoroka. Hiyo ilikuwa ni siku ya Jumatatu, siku ambayo rufaa ya Walari ilikuwa inakuja kwa hukumu.
Ingawa alikuwa na uhakiwa wa asilimia nyingi za ushindi, lakini ilikuwa inawezekana pia kushindwa rufaa yake. Swali, alilokuwa akijiuliza ni endapo akishindwa rufaa yake huku akiwa ametoroka gerezani angeishije?
“Lakini la msingi ni hili lilitokea, la kujiokoa na kifo. Hayo mengine nitayakabili kadri yatakavyokuja,” alijisemea.
Asubuhi hiyo, Madenge Marare, ambaye tayari alikuwa ameshaelezwa na Nurdin kuhusu Walari kutoroka wodini, alipitia nyumbani hapo ili waandamane kwenda mahakamani, na pia alikuwa na hamu ya kuongea mawili matatu na Walari.
Mama yake Walari, yeye walipanga kukutana naye huko huko mahakamani.
Mwanamke huyo ambaye alikuwa amelazimika kuuza baadhi ya mashamba yake ili kugharimia rufani ya Walari, huku Madenge na Nurdini wakimpiga jeki, alikuwa hana habari yoyote kuhusu Walari kutoroka jela. Hata hivyo, Mama Walari alijikuta akibaki na sehemu kubwa ya fedha hizo baada ya Wakili kusema angelimtetea Walari bure kabisa.
Alfajiri siku hiyo ya Jumatatu, Walari alikuwa ametaka kwenda kijijini kwao, ili kuwaeleza wazazi wake kilichotokea na kumuona mwanae mchanga, lakini Nurdin na mkewe wakamzuia kwanza.
Wakamwambia kwamba ilitakiwa kwanza ajifiche sana, wakati wakitazama upepo unavyokwenda kwani anaweza kuonekana na kushitakiwa kwa kosa la kutoroka gerezani, hasa ikizingatiwa hawakujua hukumu ingekuwaje.
Madenge Marare alipowasili kwa Nurdin asubuhi, yeye alikuwa na mawazo mchanganyiko. Alipongeza hatua ya Walari kujinasua na kifo lakini akaonya asionekane kwani inaweza ikafahamika na hata kuandikwa kwenye vyombo vya habari, hali inayoweza kusababisha ajikute na kesi nyingine.
"Kama zingefanyika juhudi za wewe kuepuka kifo lakini ukawa bado hospitali au hata gerezani ingekuwa kitu kizuri sana kwa sababu leo naamini kwa asilimia 100 utashinda rufaa na kuwa mtu huru... Lakini hakuna neno, hata kilichotokea si kibaya kwa vile kilikuwa lazima kifanyike kuokoa uhai wako," akasema Marare.
Baadaye Marare na Nurdin waliondoka kwenda mahakamani kusikiliza rufani ya Walari kwa kutumia pikipiki. Walari alibaki nyumbani hapo akisikilizia kitakachotokea huko mahakamani.
Saa nane na nusu mchana, Walari alikuwa akitoka kwenye chumba cha wageni ambako alikwenda kujipumzisha baada ya kuhisi usingizi. Haukupita muda, mama yake aliingia akiwa ameandamana na Madenge Marare.
Uso wa mama yake ambao ulikuwa unaonyesha furaha wakati wanafunguliwa mlango na Mariamu, ulisinyaa kidogo baada ya mama huyo kumtia mwanae machoni. Hii ni kutokana na afya mbaya aliyokuwa nayo bado. Lakini mwalimu huyo mstaafu alijikuta akumkumbatia mwanae kutokana na kuhakikisha kwamba yule aliyekuwa mbele yake ni mwanae ambaye kuna wakati aliamini ni mtu atakayefia jela.
Baadaye Marare alimpa mkono Walari na kumpongeza wakati mama yake akiwa ameshindwa cha kuongea kutokana na furaha. Nurdin alikuwa amepitia kazini kwake baada ya hukumu.
"Hongera sana ndugu yangu. Ingawa taarifa za mahakama zimeonyesha umekufa, lakini hakimu aliendelea kutoa hukumu ya rufaa yako na kukupa ushindi. Umeshinda rufaa yako, kwa hiyo, ingawa wewe unajulikana kama mfu lakini uko huru," akasema Marare.
"Hakimu amesema nini wakati akisoma hukumu?"
"Amesema mwenzie wa mahakama ya mwanzo alikosea sana katika hukumu yake, kwa sababu kwa jinsi alivyopitia mwenendo wa kesi ulivyokuwa, kulikuwa hakuna ushahidi wa kukutia hatiani kwa makosa ulioshitakiwa nayo. Isitoshe hakimu pia ameshangaa adhabu uliyopewa kwamba ilikuwa kubwa sana, kwani yalikuwa ni makosa madogo tu yenye adhabu ya kifungo kisichozidi mwaka mmoja, kulipa faini ama vyote kwa pamoja," akajibu Marare.
"Asubuhi nilisikitikia kitendo chako cha kutoroka ukiwa bado uko jela," akaanza kusimulia Marare," lakini pia nimeona manufaa yake. Kuna kila dalili kwamba Masunju angekata rufaa kupinga hukumu ya leo kama kusingekuwa na taarifa kwamba umekufa."
"Ndugu yangu Marare, kwa kweli wewe pamoja na Nurdin, na mama yangu, ninawashukuru sana kwa jinsi mlivyopigana kiume hadi kuniokoa na kifungo cha uonevu. Isingekuwa juhudi zenu ningefia jela. Kwa kweli sina maneno mazuri ya kuelezea namna ninavyowashukuru," akasema Walari.
"Wala usijali. Hili lilikuwa jukumu letu na kwa kweli kama tusingelitekeleza tusingekwepa lawama. Sisi sote tuna furaha kuona tumefanikisha kitu tulichokipigania," akajibu Marare.
"Vipi, waandishi wa habari hawakuwepo mahakamani. Wasije kesho wakaandika kwamba nimekufa," akauliza Walari.
"Niliona waandishi wawili pale mahakamani, lakini hawajui kama kulikuwa na hii kesi ya rufaa, kwa hiyo tumejitahidi kuwakwepa. Hakuna mwandishi aliyeingia kwenye chumba cha mheshimiwa hakimu wakati wa hukumu," akajibu Marare.
"Vipi, Masunju alifika kortini kusikiliza hukumu?"
"Alikuwepo ofisa mmoja wa magereza ambaye ndiye nilimsikia nje akiongea na wakili wao kwamba kulikuwa hakuna haja ya kumkatia rufaa mtu ambaye keshakufa," akajibu Marare.
"Nina mashaka, Masunju anaweza akawaambia jamaa wa gazeti la Upekuzi kwamba nimekufa."
"Ngoja tusubiri Jumamosi tuone litatoka na nini," akajibu Marare.
Itaendelea...