Gereza la Kifo - 45
Mtunzi - HAMISI KIBARI
ILIPOISHIA
Akina Nurdin na mama yake hawakuamini macho yao kwa jinsi Walari alivyokuwa ameisha. Alikuwa medhoofika mithili ya mtu anayeugua ugonjwa hatari wa ukimwi.
Hali yake kiafya ilikuwa inatisha kiasi kwamba alionekana kama mtu anayeweza kufariki dunia muda si mrefu. Walari aliwapungia mkono akina Nurdin akiwa amemshika bega yule askari muungwana huku akilazimisha tabasamu baada ya askari wale kugoma kumruhusu kwenda kusalimiana kwa karibu na ndugu zake hao.
Mama yake alibubujikwa machozi kwa jinsi kijana wake alivyokuwa amekonda na hata Nurdin alitoa kitambaa mfukoni na kufuta machozi.
Mama huyo na akina Nurdin hawakujua kabisa kilichokuwa kimemkabili Walari huko jela na kila mtu akaonekana kusononeshwa sana na hali yake.
Endelea...
Baada ya kuingia mahakamani, ndugu zake hao ndipo wakapata nafasi ya kwenda kuongea naye kwenye benchi alikowekwa na askari wakati mahakama ikimsubiri hakimu aje.
Madenge alimuuliza kilichomsibu hadi kuwa na afya mbaya kiasi kile.
Walari akajibu haraka kwamba alipelekwa chumba cha mateso ambako alikumbwa na malaria kali pamoja na kuhara damu, ugonjwa ambao hadi muda ule ulikuwa ukimsumbua.
Kabla hawajaongea mengi, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kanda, Waduku Wesai, aliingia, kisha Walari akatakiwa apande kizimbani. Lakini kutokana na hali yake kuwa dhaifu, hakimu aliagiza mkata rufani aletewe kiti pale kizimbani.
Karani wa mahakama, akiwa ameketi kwenye meza ndogo mkabla na wakili wa Walari katika ukumbi wa mahakama iliyokuwa na watu wachache waliohudhuria, alimweleza Hakimu kwamba kesi hiyo ilikuwa imekuja kwa rufaa.
Baadaye alisimama Wakili akasema kwanza kabisa anamtaka Hakimui akemee vikali uongozi wa gereza kwa kumtesa mteja wake na kujaribu kueleza kwa kifupi na husuani kutompeleka hospitali.
“Mheshimiwa hakimu, katika hali ya kawaida mgonjwa kama huyu alipaswa kuwa hospitali lakini mteja wangu anatokea katika chumba cha mateso ya kutengenezwa ili kumkomoa, inatia uchungu sana,” alisema Wakili akitoa kitambaa mfukoni na kufuta machozi.
Baada ya hakimu kuitikia ombi hilo na kuwakemea vikali watu wa magereza alianza kusikiliza sababu za rufaa na kabla ya hapo akaagiza baada ya kutoka hapo mfungwa yule apelekwe hospitali.
Wakili Dickson Mafuru alimwambia Hakimu Wesai kwamba mahakama ya wilaya ilikosea katika kesi iliyokuwa ikimkabili Walari, kwanza kwa kutoa adhabu ambayo hailingani na kosa na pia kosa lenyewe lilikuwa la kubambikwa.
Wakili yule akasema kulikuwa hakuna ushahidi wowote ulioonyesha kwamba mshitakiwa aliingia kwenye kiwanda cha sabuni na mafuta kwa lengo la kufanya uhalifu na hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kwamba mshitakiwa alidhamiria kuongea na mfungwa.
Isitoshe, akasema, kiwanda kile kwa sasa kimebinafsishwa na hivyo si eneo la jeshi moja kwa moja kama ilivyodaiwa kwani menejimenti inayokiendesha si ya kijeshi na hata bodi ya Wakurugenzi.
"Kwanza haieleweki ni kwa vipi kiwanda ambacho asilimia kubwa kinamilikiwa na watu binafsi, kiwe kinalindwa na wafanyakazi wa serikali, yaani askari magereza, na zaidi ya hapo wafungwa nao wanakwenda kufanya kazi hapo. Hapa kuna walakini, mheshimiwa."
Wakili alimwambia Hakimu kuwa mfungwa ambaye anakaribia kumaliza muda wake, hata ambaye hajamaliza, ni kawaida sana kumuomba mpita njia sigara kama ilivyokuwa kwa Walari.
"Mbona mimi huwa ninakutana na wafungwa wengi kisha wananiomba pesa huku wakiwa wanalindwa. Sheria ya kutozungumza na mfungwa ilikuwa na maana ya usalama tu kwa wafungwa na hatujaonyeshwa namna mteja wangu aliyekuwa akijipitia njia, alivyotaka kuhatarisha usalama.
"Mteja wangu alimpa mfungwa huyo pesa kuonesha uungwana wake tu, tena alifanya hivyo mbele ya askari aliyekuwa getini na ambaye hakuchukua hatua yoyote.
"Sijui kwa nini upande wa mashitaka haukumleta huyu askari aliyekuwa getini siku ya tukio. Bila shaka walijua kuwa angeua kesi yao ya kumbambikia mteja wangu," akasema Wakili Mafuru.
Wakili alimwambia Hakimu kwamba miezi michache kabla ya kukamatwa, mteja wake alikuwa amekwaruzana kidogo na mkuu wa gereza na ndiyo maana akambambika kesi hiyo na kwamba kama mteja wake angepewa nafasi angeithibitishia mahakama kuhusu ugomvi wao huo kwa ushahidi.
Baada ya kusema vile wakili alimuomba Hakimu atengue uamuzi wa mahakama ya wilaya na kisha, kwa vile inawezekana ilikuwa si rahisi hukumu kutolewa haraka, mteja wake apewe dhamana.
"Mheshimiwa, ninaamini mteja wangu atashinda hii rufaa na ndio maana ninaomba apewe dhamana wakati akisubiri hukumu," akasema wakili.
Mwendesha mashitaka ambaye alikuwa anasimama upande wa gereza alisimama na kupinga Walari kupewa dhamana. Upande huo wa mashitaka pia ulitaka mahakama itupilie mbali rufaa hiyo kwa vile haina hoja za msingi.
Wakili Mafuru akasimama tena na kusema kwa vile upande unaolalamikiwa katika shauri hilo haujatoa sababu zinazoeleweka kwa nini mteja wake asipewe dhamana akamtaka Hakimu atupilie mbali hoja zao na kumpa haki mteja wake ambayo alidai ilikosekana kupatikana katika mahakama ya mwanzo.
Hakimu Mkazi Waduku Wesai ambaye alikuwa akimfahamu Walari kwa vile wakati akiandikia gazeti la Waraka wa leo alikuwa akiripoti sana habari kutoka kwenye mahakama yake, aliinama chini na kuandika kwenye jalada la kesi lililokuwa mbele yake.
Huku kimya kikitanda mahakamani, Hakimu hatimaye aliinua uso wake: "Kama nilivyosema awali, mkata rufaa ana hali mbaya kiafya na hivyo narudia kuwaagiza askari magereza kumpeleka hospitali akatibiwe.
Kuhusu uamuzi wa dhamana ya Walari na hukumu yake, hakimu alisema yote atayatolea uamuzi siku tano zijazo.
"Hii ni kesi fupi na mwenendo wa kesi ulivyokwenda huko mahakama ya wilaya unaonyesha mambo machache kabisa. Kwas asa ninaagiza mkata rufani apelekwe hospital na hapa aletwe kama atakuwa na nguvu, Jumatatu ijayo asubuhi," akasema Hakimu Waduku Wesai.
Wakati akiahirisha kesi hiyo hadi siku tano zijazo hakimu alirudia tena kuwamuru maofisa wa magereza kuhakikisha wanampeleka Walari hospitali.
Baada ya kesi kuahirishwa askari wale walihakikisha kwamba hawampi Walari muda wa kuwasiliana na ndugu zake, wakamchukua moja kwa moja hadi gerezani.
Huko gerezani, Walari alifikishiwa selo ambako alivuliwa nguo za kiraia na akavalishwa sare zake za kifungwa ambazo angalau zilikuwa hazijachanika sana kulinganisha na wafungwa wengine, kisha akapelekwa hospitali. Alifurahi kuona agizo la hakimu limetekelezwa.
*** *** *****
Saa sita mchana, siku ya Jumamosi, Walari alishituka usingizini. Alihisi amebanwa na haja ndogo lakini alipepesa macho kwenye wodi ile ya wagonjwa wa kiume ambamo kulikuwa na wafungwa wengine saba, hakumuona askari. Alitaka askari amfungue pingu alizokuwa amefungwa kitandani ili ajisaidie.
Baadaye aliona wauguzi wanakuja kumchukua mfungwa mwenziye mmoja ambaye alikuwa amefariki dunia asubuhi hiyo.
Jumamosi hiyo alikuwa anajisikia vizuri kiasi, ingawa mwili ulikuwa bado hauna nguvu. Karibu usiku mzima na mchana huo alikuwa hajaharisha. Hakujua kilichokuwa kimemsaidia, kama ni zile dawa alizopewa na Mujora James au dawa alizokuwa ameanza kupewa hospitalini hapo.
Kwa siku mbili za nyuma alizokuwa amelazwa, Walari alikuwa akihudumiwa vizuri na muuguzi waliyewahi kuishi naye jirani. Siku ya kwanza Jestina, ambaye inaonekana si msomaji wa magazeti, alishituka sana kugundua kuwa Walari amefungwa jela. Ndipo Walari akamsimulia kisa kizima ambacho kilimsikitisha sana muuguzi huyo.
Wakati yule mfungwa aliyekufa alipokuwa akishughulikuwa na wauguzi tayari kwa kuwekwa kwenye toroli maalumu la kubebea maiti ambalo limefunikwa kila sehemu, ili kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, Walari alimuona Nyamagwila, yule mhudumu mkuu wa chumba cha maiti cha hospitali hiyo akija.
"Nyiye (wauguzi) nipeni haraka huyo maiti wenu nimhifadhi kisha niende zangu kutafuta lunch (chakula cha mchana). Mtu nasikia kafa nusu saa iliyopita lakini mbona mnanichelewesha?" Akafoka Nyamagwila akiwa amesimama karibu kabisa na kitanda alichokuwa amelazwa Walari.
Walari alitaka ageuze sura yake ili kukimbia macho ya Nyamagwila ambayo yalikuwa yakimtazama, lakini akawa amechelewa kwani mhudumu huyo wa chumba cha maiti sasa alikuwa anamsogolea zaidi huku akimtumbulia macho.
Je, nini kitaendelea? usikose kufuatilia mkasa huu wa kusisimua na kusikitisha...