Riwaya: Chokoraa

RIWAYA: CHOKORAA
MTUNZI: George Iron Mosenya


SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA


George hakuwahi kukutana na dhahama hii ya usumbufu. Lakini huu ulikuwa usumbufu wa maajabu, usumbufu usiokuwa na maneno ndani yake.
Usumbufu wa vitendo.
Mara huyu avae hivi mara yule arembue jicho. Ilimradi shaghalabaghala.
Mwanaume akajikaza!!

Lakini atajikaza mara ngapi iwapo usiku ule uvumilivu ulimshinda akataka kumbaka Isha??
Hata kama hakumbaka sasa ana ujauzito.
Hata George ni mwanadamu!!

****

MAJI ukiyavulia nguo sharti uyaoge. Mwanaidi alikuwa ameamua kupigana kwa ajili ya watoto yatima na wasiokuwa na makazi. Watoto ambao wameugeuza mtaa kuwa makazi yao. Watoto waliobandikwa jina nchini Kenya wakiitwa ‘chokoraa' jina ambalo linatumika sasa afrika mashariki kwa ujumla.
Kadri mwanaidi alivyoikamata pesa ndivyo alivyoona kuwa haitoshi katika harakati zake. Alitakiwa kufikiri zaidi anapata vipi pesa nyingi zaidi ili aweze kutimiza alichonuia katika akili yake.
Sasa alikuwa amefanikiwa kuikamata akili ya diwani na alikuwa amechota pesa nyingi.
Jambo la kwanza lilikuwa kumpeleka mama George katika huduma ya afya.
Huku aligharamika kiasi kikubwa cha pesa ikiwemo ya kuwahonga madaktari ili wasipeleleze zaidi alikumbwa na nini hadi kufanyiwa upasuaji mbovu namna ile.
Kwa hili alifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Jambo jingine alilolifikiria kwa wakati uliopita na sasa alilitendea kazi ni kuhusu kutafuta nyumba kubwa.
Madalali wa mjini wakachukua pesa yao na nyumba ikapatikana.
Nyumba ya vyumba viwili pamoja na sebule.
Maisha mapya!!

Frida akaanzishwa kliniki. Kwa ajili ya ile mimba yake isiyokuwa na baba.
Mwanaidi akawa mlezi rasmi wa familia.

****
WIVU wa mapenzi. Hauchagui kaliba yoyote katika jamii. Maskini anao, tajiri anao vilevile.
Usiombe wivu ukauteka moyo wako. Waweza kujikuta unafanya mambo ambayo mjukuu wako akisimuliwa atakiri kuwa bibi ama babu yake alikuwa na wazimu. Si bure!!
Huwezi kutambua kama una wivu, wivu humfanya mtu awe mjingamjinga na kujiona anayofanya ni sahihi.
Ule wivu ulioiondoa roho ya mwanadada Emiliana. Sasa ulikuwa unashambulia na kuigalagaza roho nyingine katika mazingira mengine.
Huyu alikuwa anahangaika muda mrefu lakini hakuweza kulalamika popote kwa kuwa tu hakuwa na ushahidi wa kumpa uhuru wa kuongea.
Je? Ushahidi unajileta wenyewe? Jibu ni hapana. Ushahidi hutafutwa.
Binti huyu akalazimika kuutafuta ushahidi, kimya kimya kama alivyofanya marehemu Emiliana kwa mume wake mtarajiwa Kasuku.
Mitego aliyokuwa ameitega ili imnase ushahidi sasa ilikuwa imetoa majibu aliyoyasubiri. Majibu yaliyomkera na kumfanya ajute kufanya upelelezi ule.
Kichefuchefu kikamshika. Akatamani kutapika lakini hakutapika.
Akawahi limao lake akakikabiri.
Njiani aliona maluweluwe. Hakuamini alichokiona, lakini alijilaumu kwa nini alikitafuta.
Hakuitikia salamu ya mtu yeyote yule. Alitembea akiyumba huku na kule, akaufikia mlango wa chumba chake akaufungua. Akajitupa kitandani. Akamngoja adui yake aweze kurejea amkabili.
Mwanzoni hakuhisi usingizi kabisa lakini alikuja kushtuka asubuhi.
Adui alikuwa anamalizia kufunga mkanda wa suruali yake aende kazini.
Alitaka kumzuia lakini akajikuta anaagwa. Hakujibu!!

Subira yavuta heri endapo yule hasira ambaye majibu yakle ni hasara atakuwa likizo.
Lakini siku hii hasira alikuwa amejikunyata katika moyo wa mwanadada huyu. Hivyo subira akawa ameondoka zake.
Hakuweza kuikabili hasira hii.
Aliona yule bwana wake anachelewa kurejea akaamua kutoka mwenyewe aweze kumfuata. Alitegea mida ile ya siku iliyopita, alitegemea kumuumbua.
Akiwa njiani anakutana na kundi la akina dada.
Alikuwa anawafahamu wawili kati yao.
Hasira zikachachamaa. Akawakabili. Akawasimamisha.
"We malaya George ni nani yako?"
"Malaya? Nani Malaya..na George yupi?" alijibu kwa kiburi binti mnene mfupi.
"Nakuuliza George ni nani yako. Yule mwalimu." Alitoa maelezo ya ziada.
"Mwalimu wangu kwani vipi? Unataka namba yake? Kakujaza mimba nini?" alijibu kwa dharau. Wenzake wakacheka.
Sasa akakumbwa na msukumo wa hasira isiyosimulika. Akamvamia yule aliyetoa majibu yale. Akaanguka naye chini. Akaanza kumshambulia na makucha.
Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Wale wasichana wawili wakajiunga kumtetea mwenzao.
Kibao kikamgeukia yule binti. Ambaye alijuta kuzaliwa chokoraa na kisha kuitwa Isha. Akaijutia ile mimba aliyopewa na George.
Majuto hayo yakawa na thamani yake.
Akaupata msaada.

****


George, akiwa darasani siku hii alikuwa anawaza juu ya msichana wa kitanga ambaye alikuwa katika wakati mgumu sana kukabiliana na hisia hizi. Hisia za ajabu.
Alikuwa anajiuliza aliwahi lini kukumbana na hisia hizi.
Alipoumiza kichwa sana akamkumbuka Frida. Siku ya kwanza walipoonana wakati anasoma chuo kikuu.
Upendo!!
Aliamini alikuwa anampenda.
Lakini kikwazo kikubwa kilikuwa ni Isha. George alitambua kuwa licha ya kwamba anaishi na Isha bila kuwa na mipango yoyote ya mbeleni. Lakini alikuwa amembebea mtoto wake.
George aliogopa kujihusisha na msichana mwingine kwa kuhofia kumjaza msichana mwingine mimba kisha kuongeza wimbi la watoto wa mitaani.
Hakutaka kabisa kuhusika katika tatizo hili. Kwani yeye alikuwa katika harakati za kulipunguza tatizo na si kulitawanya kama hivi anavyowaza.
Binti huyu wa kitanga aliyekuwa kidato cha tano. Alikuwa na kila kigezo cha kuitwa mrembo. Lakini hili halikuwa na maana kubwa kwa George. Na alilipuuzia mpaka siku ambayo alichelewa kutoka kazini baada ya mabinti watatu kumsihi awasaidie maswali kadhaa ya somo la hesabu.
Kati ya mabinti hawa alikuwemo binti wa kitanga.
Baada ya kumaliza kufundishana, mabinti na mwalimu waliongozana njia moja.
Marafiki wawili wakapeana ishara. Mara George na Lisa wakabaki peke yao. Marafiki wawili wakifuata kwa nyuma.
Aliyesema mapenzi yalizaliwa Tanga huenda hakukosea.
Lisa akaanza kufanya yale aliyoyajua. Ilimradi tu kumtega bwana George.
George ni mwanaume na macho yake hayana pazia. Kilicho chema machoni naye kwake pia kilikuwa chema.
Akajisahau kama ni mwalimu. Akauvaa ujana.
Yaliyotokea, yaliwafanya waonekane kama wapenzi wa saiku nyingi.
Wakati yanatokea. Lilikuwepo jicho la mwanadada mjamzito Isha likifuatilia kwa ukaribu.
Isha hakutaka kuwavamia kwa wakati ule.
Akaachana nao akawahi nyumbani.

George alipoachana na Lisa alijutia alichokifanya. Japo hakikuwa na madhara yoyote, sawa lakini ni kosa kukamata kiuno cha msichana hadharani. Walionitazama watanionaje? Hata Isha angenifikiriaje?
Mimi ni mwanaharakati. Sitakiwi kuwa dhaifu!!
Nikirudi nyumbani nitamshirikisha Isha juu ya jambo hili. Najua atanishauri vizuri. Alijisemea George.
Hapo alikuwa katika basi akielekea nyumbani kwa akina Sakina. Kwa ajili ya somo la usiku.
Ilikuwa bora huku alipotoka kuliko hapa anapoelekea maana mitihani ilikuwa inamkabili.

Usiku aliporejea Isha alikuwa amesinzia fofofo.
Hayakufanyika mazungumzo yoyote yale.
Asubuhi kama ilivyo ada alitakiwa kuwahi kazini.
Alimuaga Isha. Lakini hakujibiwa.
Hakujali, aliamini ni mang'amung'amu ya usingizi.

Sasa ni jioni anakumbwa na mshtuko. Yule binti aliyemuacha kitandani. Akiwa katika lindi la usingizi.
Anakutana naye akiwa hana fahamu. Amezungukwa na wanafunzi wakimshangaa tumbo lake kubwa likiwa nje.
George anapigwa na butwaa kukutana na Isha katika hali ile.
Hapakuwa na haja ya kujiuliza maswali mara mbimbili. Hakuwepo wa kuyajibu.
Zikachukuliwa hatua.
Isha akapelekwa katika kituo cha afya kilichokuwa jirani.
George badala ya kwenda nyumbani kwa akina Sakina, aliandamana na gari la walilokodi kumpeleka Isha hospitali.
Hali tete!!

****

Seba Sebastian, diwani aliyaekuwa na nia ya kuwania tena kiti cha udiwani alikuwa anafurahia kila hatua aliyokuwa anapitia kwa wakati huu. Habari aliyoinunua kwa bei mbaya sasa ilikuwa inampa faraja.
Katika pitapita zake huku na kule aliweza kuzisikia tetesi juu ya bwana Dembele na shughuli zake za kuuza madawa.
Lakini kati ya hawa wote hakuna hata mmoja ambaye alikuwa na uhakika juu ya anachokizungumza.
Hali hii ilimpa faraja Seba na kujiamini kabisa kuwa ni yeye pekee anayehodhi habari ile.
Alihitaji sasa kuifanyia kazi. Asingeweza kwenda peke yake kufanya maamuzi haya. Yule mwanamke wake mbichi kabisa ambaye alikuwa anamuandaa kuwa mke wake baadaye ilikuwa lazima ashirikishwe.
Seba alikuwa na mke na watoto lakini bado alikiuka maadali ya dini yake akaweka nyumba ndogo.
Nyumba ndogo hii aliitunza tangu ikiwa shuleni. Alimlipia ada na kumgharamia kila kitu na sasa alikuwa amemaliza chuo kikuu. Alimchukulia seba kama baba yake wa kumzaa, wazazi wake wote walifariki kitambo na hakuwahi kuwatambua.
Walipishana sana umri kwa kiasi kikubwa lakini angefanya nini binti yule iwapo alikuwa anahitaji huduma za mzee Seba?
Hakuwa na ujanja.
Kwa kuwa Seba alikuwa na elimu duni. Alikumbwa na kihoro akaketi meza moja na mtoto wake huyu ambaye anamuandaa kuwa mke wa pili. Akamfungukia kila kitu juu ya habari aliyoinunua.
Habari kuhusu Dembele.
Binti alisikiliza kwa makini sana.
Kisha akachukua nafasi ya kutoa ushauri.
Akamshauri avute subira kidogo, uchaguzi ukikaribia ndipo amuumbue bwana yule.
"Yule mtoto hawezi kuiuza tena habari hii?" Seba aliuliza.
"Akiiuza bado itamchafua bwana Dembele na atakuachia kiti..tena hiyo itakusaidia sana maana hautakuwa na hatia yoyote na hawezi kukuwekea kisasi." Alijibu kwa utulivu, usomi ukichukua nafasi.
Seba akakolea.
"Sikukosea kukuchagua." Alisifia mzee huyu kisha akamkumbatia na kumbusu shavuni.
Siku ikaisha. Mzee seba alilala katika nyumba aliyompangia binti huyu.
Asubuhi akaondoka na kuiacha ile siri ikiwa sio siri tena.
Alijisahau kuwa hakuna siri ya watu wawili.
Kitita cha pesa kiliachwa mezani kama sumaku ya penzi. Asidanganyike na wajanja wa jiji akamsaliti.

****

MWALIMU wa kike hakuwa na amani hata kidogo moyoni. Mshawasha wake wa kumuona George ulikuwa unamwadhibu.
Siku hiyo alitambua kuwa lazima itakuwa siku ya kipekee kwake.
Siku ya kumshawishi kitu George.
Maajabu George kuchelewa kazini.
Dakika, masaa yakakatika. Bado George hakuonekana na hapakuwa na taarifa yoyote ile. Kibaya zaidi hakuna aliyejua nyumbani kwake.
Suzi akakosa amani. Jambo alilobeba moyoni lilikuwa linamsumbua sana.
Jioni ikafika, bado George hakuonekana.
Suzi akamlaani George kimoyomoyo kwa kutomiliki simu ya mkononi wakati uwezo alikuwanao.
Suzi hakuamini kabisa kama ataweza kupata usingizi katika hali hii ya mawazo. Lakini angefanya nini? Akaamua kuondoka huku amani ikizidi kumkimbia. Alimuhitaji sana George.

Wakati Suzi akihangaika kumuwaza George. Wakati huo George alikuwa akihangaika huku na huko kulipia pesa za matibabu.
Hakuwa na pesa ya kutosha kutokana na kuwaazimisha waalimu wenzake pesa pamoja na kulipia kodi ya nyumba. Sasa pesa ilihitajika.
Si kwamba hakuwa na akiba ya pesa nyingine la!!
Pesa ilikuwepo lakini anayefahamu pesa zilipo alikuwa amepoteza fahamu.
Isha alikuwa mtunzaji wa pesa nyingine katika njia ya kibubu, ambacho alifahamu mwenyewe ni wapi anakihifadhi.

Mwanaume alitakiwa kuchukua maamuzi. Akafikiria kukimbilia katika familia ya Dembele, moyo ukasita. Alihofia kujibiwa vibaya maana Sakina hakuwa anatabirika.
Suzi !!
Jina hilo likashambulia kichwa cha George. Akamkumbuka binti huyo mhitimu wa chuo kikuu ambaye kwa muda huo wa kutafuta kazi alikuwa anafundisha masomo ya ziada pia.
Suzi licha ya kuwa mwalimu na yeye alikuwa katika mpambano na wanafunzi wengine wengi wanaomuwinda George kimapenzi.
Aliwahi kumkaribisha George nyumbani kwake mara mbili lakini hakufanikiwa kumteka kimapenzi.
Suzi alikuwa akimuhitaji sana George. Lakini mazungumzo kati yao yalileta huzuni kubwa. Japokuwa maisha ya Suzi yalikuwa vyema kutokana na kutunzwa na diwani. Bado alibakia kuwa yatima, aliyepata adha ya uyatima utotoni pekee.
Historia ya George na mipangilio kabambe aliyokuwanayo katika kuwaokoa yatima na chokoraa ilimkosha Suzi na kuahidi kuwanaye bega kwa bega
Walihitaji pesa kufanikisha harakati hizi.
Pesa hiyo ilikuwa kikwazo na sasa pesa hiyo inayohitajika inamsukuma George kwenda kwa Suzi.

Suzi hakutegemea ujio wa George. Akiwa na kanga moja pekee alimkumbatia George kwa nguvu. Na ghafla akambusu. George akajilazimisha kutabasamu.
Suzi akaketa hovyo mbele ya George ambaye hakuwa na furaha.
"Una nini Gee"
" Acha tu…..Suzi kuna tatizo. Dada yangu mmoja amefikwa na tatizo. Yupo hospitali mi sina kitu nahitaji sana msaada wako we fanya kuniazima..halafu…"
"Mimi na wewe hatuazimani. Shilingi ngapi inahitajika. Pole sana G najua ni kiasi gani una upendo wa dhati kwa chokoraa na yatima"
George akataja kiwango cha chini kabisa. Akapewa mara mbili yake.
"George ukitoka huko hospitali pliiiz usiache kuja kuna jambo zito kwa faida yangu na yako. Usiache hata kama ni usiku vipi?" Suzi alimsisitiza George wakati anatoka.
George akakubali.
Akatoweka upesi kuwahi hospitali. Hakuamini ingekuwa rahisi kiasi hicho kukomba pesa kwa Suzi.
Kichwani aliamini kuwa Suzi alimhitaji usiku huo kwa ajili ya mapenzi tu hapakuwa na jipya lolote.
"Ameninunua tayari sina ujanja." Alikiri kwa sauti ya chini akiwa peke yake.

***SUZI ameipata siri ambayo anahitaji kumshirikisha GEORGE….Siri juu ya DEMBELE…….Siri ya kuuza madawa ya kulevya. KWANINI ANAHITAJI KUTOBOA SIRI HII??? Na je itakuwa na manufaa ama itazua majanga kwa chokoraa hawa??

***ISHA katika matatizo…..wivu umemsukumia pabaya…..sasa yu hoi hospitali.

***MWANAIDI, FRIDA NA MAMA GEORGE….Harakati zinaendelea.



muuza ubuyu ram culbby mbalu BPM Jullie Z Khantwe Excel ladyfurahia Igunga Moja
 
Duh! Sijui George atarudi tena kwa Suzi...., sijui kama ataambiwa hiyo siri au ndo wataishia kwenye mapenzi...., yani sijui yani....!!
 
George, natamani siku moja ukutane na mwanaidi na frida, Pole isha wivu umekuponza umeambulia kupigo
 
RIWAYA: CHOKORAA
MTUNZI: George Iron Mosenya



SEHEMU YA ISHIRINI NA NANE

Suzi akaketi hovyo mbele ya George ambaye hakuwa na furaha.
"Una nini Gee"
" Acha tu…..Suzi kuna tatizo. Dada yangu mmoja amefikwa na tatizo. Yupo hospitali mi sina kitu nahitaji sana msaada wako we fanya kuniazima..halafu…"
"Mimi na wewe hatuazimani. Shilingi ngapi inahitajika. Pole sana G najua ni kiasi gani una upendo wa dhati kwa chokoraa na yatima"
George akataja kiwango cha chini kabisa. Akapewa mara mbili yake.
"George ukitoka huko hospitali pliiiz usiache kuja kuna jambo zito kwa faida yangu na yako. Usiache hata kama ni usiku vipi?" Suzi alimsisitiza George wakati anatoka.
George akakubali.
Akatoweka upesi kuwahi hospitali. Hakuamini ingekuwa rahisi kiasi hicho kukomba pesa kwa Suzi.
Kichwani aliamini kuwa Suzi alimhitaji usiku huo kwa ajili ya mapenzi tu hapakuwa na jipya lolote.
"Ameninunua tayari sina ujanja." Alikiri kwa sauti ya chini akiwa peke yake.


Aliwasili hospitali na hali ya Isha ilikuwa vyema tofauti na awali lakini daktari hakuwa na furaha na mafanikio haya ya kumrejesha Isha katika hali ya awali.
George alipowasili alikaribishwa kuonana na daktari.
"Naona ameamka!!" George aliongea huku akimtazama daktari aliyelilazimisha tabasamu.
Daktari alimpa maelezo ya kitaalamu George huku akimsisita kuwa na jasiri. Kauli ya kutakiwa kuwa jasiri ilimshtua George lakini hakutia neno.
"Mgonjwa wetu anatakiwa kufanyiwa upasuaji….upasuaji wa haraka sana. Hivyo hapo zinahitajika pesa kiasi. Mwenyewe hajui kuhusu hilo. Ana furaha na tusingeweza kumwambia chochote. Mtoto aliyembeba amefia tumboni, na tumejaribu kumchoma sindano ya maji ya uchungu haijafanya kazi na kama isipofanya kazi masaa ishirini na nne mbele hakuna ujanja zaidi ya kumfanyia upasuaji. Na masaa ndo haya yanayoyoma." Daktari alijieleza kwa marefu na mapana. George alikuwa amekodoa macho, hakujua lolote kuhusu maji ya uchungu, alichotambua pale ni kuwa damu yake si hai tena. Imetoweka.
Hakuweza kuzungumza. Daktari aliendelea kuwa muongeaji mkuu.
Hitimisho likawa kumfanyia upasuaji Isha.
Kwa kuwa ilikuwa hospitali binafsi, huduma hii ililipiwa. Tatizo la pesa halikuwepo.
Asubuhi Isha hakuwa yule Isha mwenye tumbo kubwa tena. Hakuwa na mimba. Kisu kilipenya na mtoto ambaye hajatimiza siku zake akatolewa akiwa mfu.
Aliomboleza kwa muda, akabembelezwa akatulia.
Aliendelea kubaki palepale hospitali kwa ajili ya kufanya mazoezi mepesimepesi ya kumrejesha katika hali ya kawaida.


****


Msongo wa mawazo ulimhangaisha George. Hakutamani kulala katika kitanda alichokuwa analala na Isha.
Alijiona ni mtu mwenye mikosi kila siku. Alizaliwa katika mazingira na ajabu akakulia katika raha yenye mashaka.
Alimpoteza Frida na sasa Isha yu matatizoni.
Siku hii akaenda kuimalizia nyumbani kwa Suzi.
Huku aliamini wanaweza kubadilishana mawazo.
Alimkuta Suzi anaandaa chakula jikoni. Wakasalimiana kisha akaketi kumngojea Suzi amalize kupika.
Wakati chakula kikiwa mezani mazungumzo yaliendelea. Tofauti na George alivyodhania kuwa Suzi yupo kimapenzi tu.
Hali ilikuwa tofauti. Suzi akamueleza George kuwa pesa imepatikana. Pesa ya kufanya harakati za kumkomboa chokoraa na yatima.
George akaweka umakini na kumsikiliza Suzi. Naye bila hiana akazungumza yote aliyoambiwa na hawara yake ambaye ni diwani.
"Kwa hiyo?" George aliuliza.
"Tunatakiwa kumuuzia huyo Dembele habari hii kwa bei mbaya." Suzi alimwambia George. Kisha akaongezea "Kwa kuwa anahitaji sana kuheshimika katika jamii na hakuna apendaye kwenda jela. Basi lazima ainunue taarifa hiyo ambayo ni ya muhimu kwake kuliko sisi."
Suzi akaeleweka. Wakapanga mikakati ya siku gani wakutane na Dembele.
Suzi asingeweza kwenda kuonana na Dembele, walifanya hivyo ili kumpoteza diwani asijue ni nani aliyeiuza siri hiyo.
Wakakubaliana hiyo siku iwe baada ya siku mbili.


Mtafutaji hachoki na akishachoka ujue kapata. Usemi huu ulitenda kazi siku ambayo Dembele alimkabidhi George kitita. Alifanya hivyo upesi kwani George alitishia kuwa iwapo atagoma kuinunua basi atawaruhusu wanaoimiliki taarifa hiyo waitumie wanavyotaka.
Mwanzoni Dembele alitaraji kumpatia pesa George kisha kumfuatilia na kumwondoa duniani lakini baada ya kusikia kuwa wapo watu ambao wapo nyuma yake alifadhaika na kumuacha kama alivyo.
Lakini alijiweka makini sana naye.
Alitulia akitunga sheria ya ni kwa jinsi gani atazitwaa roho zilizohifadhi siri hii.
Baada ya siku kadhaa Sakina alirejea shuleni na huu ukawa mwisho wa George kufika katika nyumba ile mara kwa mara.


****


PESA mwanaharamu, George hakutegemea kuzikamata kwa uwingi kiasi kile. Uwingi ule ukampagawisha.
Kwa akili ya kibinadamu akamsahau Isha kwa muda.
Akiwa mtaani mara akalikumbuka kumbatizi la mtoto wa kitanga, Lisa. Hakika lilikuwa kumbatizi maridhawa ambalo hajawahi kulipata. Kucha za bandia zilizojipenyeza na kumfinyafinya zilimpatia hisia fulani ya ajabu.
Akaitamani tena ile hisia ijirudie. Na itajirudia vipi kama sio kumtafuta Lisa?
George akaingia kinyemela eneo la Mchikichini, akafanikiwa kumpata Lisa mtoto wa kitanga.
Akasahau kabisa kuwa anaye mgonjwa hospitali.
Alihitaji kukumbatiwa, lakini hakutaka iwe hadharani.
Akajikongoja akalipia chumba katika nyumba ya kulala wageni.
Lisa ambaye alikuwa anamtamani George siku nyingi akaiona nafasi hiyo ni ya kipekee kwake kutimiza haja zake.
Wawili ndani ya chumba. Uwezo wao wa kufikiri ukiwa umesahauliwa majumbani kwao, hapa vichwa vilikuwa wazi kabisa.
Walichokifanya, wanakijua wao. Na hawakujutia maana kiliwafurahisha.
Mtoto wa kitanga aliyefunzwa kisha akauongezea ufundi binafsi, akamnyanyasa George ipasavyo.


Waliagana asubuhi ya siku iliyofuata. George hakukumbuka hata kumuuliza yule binti ni kwa nini hajarejea nyumbani kwao angali hakuaga.
Asubuhi hii George akiwa na zigo la pesa alifika nyumbani kwa Suzi ambaye alikuwa amemuuza rasmi diwani bila kujali lolote baya litakalomtokea.
Furaha yao ya kuzipata zile pesa nayo ikaishia pabaya.
Suzi akaitumia fursa hiyo kumshawishi George.
George akashawishika, japo alikuwa amechoka sana lakini akajikaza kisabuni akajivinjari na binti huyu.
Katika haya yote hakuna aliyejali kama wametumia kinga ama la.
George akaanza kujisahau kama yeye ni mwanaharakati.
Akamsahau na Isha!!


****


MWANAIDI alikuwa amejiegesha katika kitanda cha futi sita kwa tano kilichopo katika nyumba ya kulala wageni maeneo ya Magomeni jijini Dar es salaam.
Alikuwa akihesabu masaa ili aweze kupata taarifa juu ya jambo ambalo alikuwa amelifanya kwa uangalifu.
Tabasamu lilikuwa linachanua katika midomo yake huku akiona kila jambo likienda sawia. Alifurahia kumiliki pesa nyingi na alikuwa anafurahia kijana aliyemuagiza mahali kwa ajili ya kwenda kuchukua pesa nyingine.
Huyu aliyeagizwa aliaminiwa sana na mwanaidi hivyo hakuwa na mashaka kabisa.
Muda ulizidi kwenda bila majibu yoyote. Mbaya zaidi yule kijana aliyetumwa hakuwa na simu hivyo mawasiliano yalikuwa magumu.
Mwanaidi alianza kuingiwa na hofu lakini kwa mara ya kwanza katika maisha yake akaipuuzia hofu hiyo. Akayapuuzia machale yaliyokuwa yakimcheza kuwa huenda kuna jambo lilikuwa limeharibika.
Kosa kubwa sana!!
Ndio ni kosa kubwa sana lililofanywa na Mwanaidi. Ni heri angeyaheshimu machale yake.
Mlango wa chumba chake uligongwa kwa utaratibu.
Akauliza nani mgongaji, sauti ya kiume ikajibu.
Mwanaidi akacheka kidogo. Alicheka huku akiyalaumu yale machale kuwa yalitaka kumpoteza kwa siku ile. Akauendea mlango na kuufungua.
Hakutegemea kama ingekuwa rahisi kiasi hicho wala kuwa ngumu kiasi hicho kilichotokea.
Mwanaidi bila silaha yoyote anatiwa mikononi mwa wanaume wawili. Kisha mmoja anamtazama kwa macho makali yaliyojaa chuki.
Mwanaidi ana kwa ana na bwana Dembele!!
Yule mnyanyasaji aliyemteka kwa nia ya kumtumikisha biashara ya madawa ya kulevya.
Mwanaidi alipojaribu kufurukuta alikutana na mkono imara, ukalisalimia shavu lake. Maumivu yakatambaa chozi likamtoka.
Dembele akatabasamu. Mwanaidi akatukana kwa kikabila chao.
Mwanadada jasiri na mwanaharakati wa ukweli sasa yu mikononi mwa watu wabaya. Hana silaha, na hawezi kujinasua.
Bwana Dembele aliyekuwa amevaa suti aliingiza mkono ndani ya suti kisha akachomoa bastola akamuonesha Mwanaidi.
"Ukileta fujo tu nasambaratisha hicho kichwa chako." Onyo likatolewa, Mwanaidi akahisi ubaridi baada ya kuiona ile silaha. Mkojo ulikuwa unapenya.
Kama vile hakuna chochote kinachoendelea. Mwanaidi akiwa na yule kiijana aliyemuagiza kwa bwana dembele kumuuzia siri walipitishwa mapokezi na safari yao ikaishia katika gari aina ya Pajero, ilikuwa na vioo vyenye utando mweusi.
Mwanaidi matatani!!
Umahiri wake katika kuchepuka kutoka mazingira magumu ukawa katika kikomo.
Usiku huo wakajikuta katika vyumba viwili tofauti. Mwanaidi chumba chake na yule mjumbe chumba chake.
Mwanaidi alitakiwa kufanya jambo moja tu kwa ajili ya uhai wake.
Kumuelekeza bwana Dembele mahali alipo mama George na Frida.
Kupatikana kwa watu hawa kisha kuondolewa uhai ilikuwa njia pekee ya bwana dembele kujiweka mbali na hatia. Kinyume na hapo ni lazima angekuwa hatiani na jina lake lingechafuka sana.


****


Isha alikuwa anafanya mazoezi ya mwisho na mgonjwa mwenzake ambaye walikutana siku hiyo. Kitu kilichowafanya wazoeane kwa siku moja ni kwamba kila mmoja alikuwa amefanyiwa upasuaji na kila mmoja alikuwa anatolewa siku hiyo. Mama na mwana walikuwa wamechoka na sasa walikuwa wanapiga soga za hapa na pale.
Wote walikutana wakiwa waongeaji sana.
Waliongea sana huku kila mmoja akimngojea ndugu yake aweze kuja kumchukua.
Maongezi yakaisha na muda ukazidi kwenda kasi.
Sasa kigiza kilianza kuingia, isha akashangazwa sana na ukimya wa George na huyu mama naye akalalamika kuwa mwanaye amekawia sana kuja kumchukua.
Majira ya saa mbili usiku hali bado ilikuwa vile vile hakuna ndugu aliyejitokeza.


Wakati Isha anawaza George kuja kumchukua, George alikuwa katika gari la mama mtu mzima akielekea anapopajua yeye mwenyewe, wakati huo mama huyu aliyekuwa akimngojea Mwanaidi aje kumchukua…binti shupavu alikuwa matatani na ni kauli yake pekee inatakiwa ili awe huru ama aangamie peke yake.,
Mwanaidi anatakiwa kuwafichua Frida na mama George ili uhai wake uende mbele kwa dakika kadhaa.
Mwanaidi matatani!!
George stareheni!!
Isha na Mama George hawafahamiani. Hawajui kuwa watu wanaowasubiri wapo katika wakati gani huko walipo.
Harakati zinamchukua na kumtesa Mwanaidi, starehe zinamtwaa na kumpelekesha George.
Kizungumkuti!!


muuza ubuyu ram culbby mbalu BPM Jullie Z Khantwe Excel ladyfurahia Igunga Moja Samaya
 
Mmh! mbona shughuli sasa, haya ngoja tusubiri tu manake hapa hata utabiri ni mgumu kwa sasa
 
Kuna watu Mungu amewajalia vipaji vya utunzi, hii story yaani mtu huwezi hata kutabiri mwisho wake.
 
RIWAYA: CHOKORAA
MTUNZI: George Iron Mosenya




SEHEMU YA ISHIRINI NA TISA




Wakati Isha anawaza George kuja kumchukua, George alikuwa katika gari la mama mtu mzima akielekea anapopajua yeye mwenyewe, wakati huo mama huyu aliyekuwa akimngojea Mwanaidi aje kumchukua…binti shupavu alikuwa matatani na ni kauli yake pekee inatakiwa ili awe huru ama aangamie peke yake.,
Mwanaidi anatakiwa kuwafichua Frida na mama George ili uhai wake uende mbele kwa dakika kadhaa.
Mwanaidi matatani!!
George stareheni!!
Isha na Mama George hawafahamiani. Hawajui kuwa watu wanaowasubiri wapo katika wakati gani huko walipo.
Harakati zinamchukua na kumtesa Mwanaidi, starehe zinamtwaa na kumpelekesha George.
Kizungumkuti!!


****


Ilikuwa kama bahati tu. Bahati ya mtende kuotea jangwani.
Siku nyingine, mahali pengine George anaingia katika mtego wa maajabu. Mtego ambao hakujua autegue vipi. Na kwa nini awaze kuhusu kuutegua wakati aliufurahia mchezo huo?
Akiwa anatokea kufundisha darasa la jioni pale mchikichini anakutana na kiumbe ambaye alikuwa ameyahifadhi macho yake nyuma ya vioo vwa miwani nyekundu ambayo ilikuwa kubwa sawasawa na uso wake.
George hakuamini kama ni yeye alikuwa anaitwa, akageuka nyuma kutazama kama kuna mtu zaidi yake.
Hapakuwa na mtu!! Akaitikia wito.
Aliposogea karibu na ile gari akaanza kuitambua kwa mbali ile sura.
"Shkamoo mama." Alisalimia. Lakini kama ilivyokuwa siku ya kwanza hakujibiwa tena.
Wakachangamkiana kwa michapo ya hapa na pale.
Akaombwa apande garini. Akabweteka akapanda.
Gari ikaanza kuondoka. George akiwa ametilia maanani kuchungulia paja lililoachwa wazi la yule mwanamama. Hakujali ni wapi anapelekwa. Kwanza alikuwa ameshikwa na matamanio tayari.
Geti likafunguliwa wakaingia ndani.
Nyumba ilikuwa tulivu sana tofauti na awali ambavyo ilizoeleka.
"Vipi hawapo nini?" aliuliza George.
"Yap wametoka na baba yao"
Alijibu yule mwanamke huku akikishika kiganja cha George na kukiminyaminya. Joto likapenya na kumsisimua.
George akapagawa!!


Alikuwa ndani ya nyumba ya bwana Dembele na alikuwa mikononi mwa mke wa Dembele. Mama sakina!!
Mama wa kiarabu.


Hapa hawakudumu sana, yule mama wa kiarabu akachukua alichohitaji kutoka chumbani, kisha akarejea garini wakatoweka tena.
Mama Sakina alikuwa amechoshwa na tabia za mume wake za kumnyima haki yake ya ndoa. Ulikuwa umekatika mwezi mzima tangu mume asitishe huduma hiyo. Na hakutoa sababu yoyote ya kuwa katika hali hii. Siri alibaki nayo pekee moyoni akijua ni kipi kinachomkabili. Alikuwa na msongo wa mawazo juu ya siri yake kuvuja.
Ujio wa George kama mwalimu wa mwanaye ulimfanya ajikute katika kumtamani kijana huyu. Kila alipojaribu kutafuta upenyo wa kumueleza, alikuwa na mtoto wake na mbaya zaidi hawakuruhusiwa kutoka nje familia nzima hivyo alikuwa anaikosa nafasi.
Ilikuwa jambo la kushangaza siku ambayo Dembele alibadilika na kuwa kama yule wa zamani. Akaichukua familia nzima kasoro mkewe ambaye alidai hayupo sawa kiafya. Hiyo ilikuwa janja yake tu kumkomoa mume wake huyo kwa ubinafsi aliokuwa amemfanyia kwa mwezi mzima.
Familia nzima ilipotoweka. Mama Sakina aliingia garini naye akatoweka pia.
Alikuwa na nia ya kwenda kumtembelea rafiki yake kwa lengo la kunywa naye pombe kwa kufuru na furaha ya kuwa huru tena.
Safari yake ikaishia pale alipomuona George. Sasa amemchukua garini wamefika na kuondoka nyumbani kwa Dembele.
Mwisho wa safari yao ukawa katika hoteli yenye hadhi ya juu sana. Chumba kikubwa kabisa kinachojumuisha sebule. Ni humu walifikia.
George ametamanika japo hawezi kusema.
Mama Sakina anagundua madhaifu hayo.
Hakuna mazungumzo.
Wakajibwaga sebuleni. Mama na mwana katika penzi zito.
Hakuna aliyejali kwa mara nyingine kuhusu kinga.
George akafurahia penzi la mama mtu mzima. Mke wa Dembele.
George hakuwa anatambua ni katika hatari kubwa kiasi gani anajiweka.


Majira ya saa sita usiku, mama wa kiarabu anaitazama saa yake na kumsihi George waondoke kwani hawezi kulala nje ya nyumba yake bila mumewe kupewa taarifa. George hana kipingamizi.
Wanajiandaa na kukiacha chumba hicho katika upweke mkubwa sana. George anaelekea upande ambao mama Sakina haelekei, hivyo wanaagana huku yule mama akimpatia George kiasi cha pesa kwa ajili ya nauli. George aliipokea huku akitabasamu kwani hakuwa katika uhitaji wa ile pesa.
George alibaki kusimama akitafakari aelekee upande upi.
Hospitali!!
Akakumbuka kuwa Isha alitakiwa kutoka hospitali siku hiyo.
Japo hakushtuka sana lakini alihisi hatia ikimtafuna. Sasa akaangaza uwezekano wa kupata usafiri aweze kufika hospitali.
Aliamini kuwa Isha atakuwa amekasirika lakini atamsamehe kwa namna yoyote.
Akapata teksi!! Safari ya kuelekea hospitali ikaanza.


Wakati George anaanza safari ya kuelekea hospitali, jemedari wa kike alikuwa amepokea kipigo kitakatifu hatimaye akajikuta anaimba kwa kurudiarudia kuhusu kutambua walipo Frida na yule mama George.
Dembele akiwa amechemkwa na hasira baada ya kufurahishwa na wimbo huo wa Mwanaidi alimchukua katika gari lake kisha wakaelekea mahali alipopataja kuwa Frida na Mama George wanapatikana.
Hospitali. Hapa ndipo walipoanzia.
Hapakuwa na mtu aliyetajwa na Mwanaidi. Dembele akachukia kudanganywa. Akataka kumpa kipigo kingine Mwanaidi lakini akajirudi na kumuhoji zaidi.
Sasa walitakiwa kwenda kumchukua Frida.


****


Isha licha ya kumkasirikia George kwa kuchelewa kufika eneo la hospitali kumchukua. Alikuwa na sharti la kumsamehe.
"Kuna mama tunaondoka naye…"
"Mama yupi?" George aliuliza.
Isha akamuelezea yule mama ambaye mwenyeji wake hadi wakati huo alikuwa hajafika. George hakutaka kumkera Isha na aliuhitaji msamaha ili kujivua hatia iliyokuwa inamkabili. Akakubali!!
George alimchukua Isha pamoja na yule mama. Wakaingia katika taksi aliyokodi.
Muda wote yule mama ambaye awali alikuwa mchangamfu sana sasa alikuwa kimya na kama anafanya tafakari ya jambo zito.
Isha alijitahidi kumsemesha lakini hakuonyesha ushirikiano.
"Mama ulikuwa unaumwa nini?" hatimaye George alianzisha mazungumzo.
"Oparesheni mwanangu…ilikuwa inanisumbua walinishona vibaya."
"Ohoo!! Pole sana mama." Alijibu George huku akiliona jicho la kuibia ibia kutoka kwa yule mwanamke.
George hakupendezwa na kitendo hicho cha kuangaliwa kiwiziwizi. Alimhisi vibaya yule mama lakini hakuwa na la kufanya kwa kuwa Isha alikuwa amependekeza waondoke naye.
Walifika nyumbani usiku sana. Isha akalala kitandani na yule mama. George akajiegesha chini kwenye mkeka.
George akiwa katika mawazo yake mbalimbali yaliyohangaisha kichwa chake alikatishwa na maongezi yaliyonoga kutoka kwa Isha na yule mama kitandani.
Mazungumzo haya yalikuwa mfano wa filamu ambayo George aliwahi aidha kuhadithiwa hapo kabla ama aliwahi kuiona.
Ilikuwa ni filamu juu ya bwana ambaye anahusishwa na usafirishaji na uuzaji wa madawa ya kulevya. Yule mama alikuwa anasimulia sio tu kwa kuwa anaifahamu bali naye alikuwa muhusika mkuu katika filamu ile.
George hakuamini kama amelala chumba kimoja na muhusika wa filamu anayoifahamu.
"Kuna binti huyo…..yaani sijui nisemeje tulikutana naye hapahapa Dar, kisha tukapoteana baadaye ndiye aliyekuja kuniokoa. Wale watu wangeniua, halafu sikuwa peke yangu kuna binti mwingine walimleta ana mimba huyo. Iliniuma sana kutambua kwamba na yeye atafanyishwa kazi kama mimi. Sikuwa na la kumsaidia. Lakini huyo binti aliyekuja kutuokoa sijui hata nimuelezeeje sijui ni malaika?" mama aliendelea kutiririka. Isha alikuwa anasikiliza huku anasisimka mwili.
"We hili tumbo unaona lipo sawa sasa hivi. Lilikuwa halitamaniki mbona. Walikuwa wanafungua na kufunga, wanafungua na kufunga." Simulizi iliendelea.
George akakosa ustahimilivu. Akaamua kujumuika katika mazungumzo.
"Mama!!" George akaita. Yule mama akasisimka ghafla kusikia lile jina. Akaketi.
Ama kwa hakika damu ni nzito kuliko maji. Na mama kamwe hawezi kumsahau mwanaye. Mama akamuita George, kijana akamsogelea. Isha akawa mtazamaji.
Mama akamshika sura yake kisha akaiminyaminya.
Akamshika mikono.
George akashangaa na kutaka kujitoa katika mikono ile.
"Wewe ni mwanangu." Alisema yule mama bila kusita. George akashangaa tena bila kusema neno lolote. Mara maneno ya kusikitisha yakaanza kumtoka yule mama, akaanza kumueleza George juu ya maisha yake ya utotoni. Akiyazungumza hayo alikuwa amemkumbatia mwanaye.
George akajisikia yupo katika mikono salama.
"Alinifanya mimi kilema. Akatoroka na wewe." Alimaliza kuzungumza akaanza kulia. George aliamini yale maneno kwa asilimia hamsini na nyingine hamsini hakuamini. Lakini alipogusiwa juu ya Mwanaidi, Frida pamoja na mama huyu kuwahi kufika mahali alipokuwa anaishi alianza kuamini.
Alipoulizia juu ya Mwanaidi na kuelezwa juu ya kutoonekana kwake. George akajishtukia kuwa ile siri aliyoiuza kwa bwana Dembele alikuwa amemuuza pia chokoraa mwenzake. Mwanaidi!!
Hali ikawa tete!! Usingizi ukapaa.
Hasira ya mama yake kufanyishwa kazi haramu ya kusafirisha madawa. Ukatili wa bwana Dembele kunyanyasa yatima ikarudisha upya moyo wake uliokuwa umeyumba.
Uchungu ukamshika.
Jemedari wa kiume akauvaa u-George wake wa awali akaingia vitani.
Alihitaji usiku huohuo kuonana na Mwanaidi pamoja na Frida. Lengo likiwa kumtia hatiani bwana Dembele siku inayofuata kwa kosa la kunyanyasa na kuua.
Safari ya usiku ule ikashindikana kutokana na Isha kugoma kubaki peke yake nyumbani. Wakaamua kufanya kila kitu siku inayofuata.
Laiti kama wangejua kuwa bwana Dembele naye yupo katika mawindo. Wangeiendesha oparesheni yao usiku huohuo. Kwani ni usiku huohuo, Frida alitiwa mikononi mwa mashetani hawa.
Dembele alitamani kuziondoa roho hizi lakini alihofia kuwa kubaki kwa ile roho ya mama George kungemletea matatizo na angekabiliwa na hatia nyingine kubwa zaidi iwapo mama huyu atafanikiwa kutoa ushahidi.
Frida ambaye hakuwa amejeruhiwa akahifadhiwa mahali asipopajua akiwa ametenganishwa na Mwanaidi ambaye alikuwa hoi.


Asubuhi George na jopo lake hawakukuta mtu nyumbani kwa Mwanaidi. Mlango ulikuwa umerudishiwa na chumba kilikuwa tulivu.
Na Frida naye hakuwepo!!
Tatizo jingine jipya.
George akawa anasumbuliwa na hatia ya kuwauza chokoraa wenzake, hakujua aanze vipi kujieleza mbele ya jopo lake ili aweze kueleweka.
Hapa, George akaamua kuchukua maamuzi binafsi. Maamuzi ya kupambana na Dembele.
Alitaka kufika na kumkabili ana kwa ana, hakujua Dembele ana hatari kiasi gani.
Akaondoka bila kuaga. Akafika nyumbani kwa Dembele.
Bahati nzuri alimkuta.
Maelezo yake ya hasira yakamwingiza hatiani. Akatiwa mikononi mwa mtu huyu hatari.


George alikuwa ni mtoto wa mama, maisha aliyokulia ya kudeka deka katika familia ya mzee Emmanuel ambaye yupo jela akitumikia kifungo chake yalimfanya asiwe jasiri sana. Kipigo kidogo alichokipata kilimfanya awataje Isha na mama yake mahali walipo. Kwa kuonyesha uoga wake alimtaja hadi Suzi. Yule binti ambaye ana mahusiano na diwani.
Faida kwa Dembele.
Akauona ushindi ukija mezani mwake.
Nikishawachukua hawa naua!! alijiapiza huku akiandaa safari ya kwenda kuwakamata.


Maelekezo ya George hayakuwa yameyumba hata kidogo. Yalikuwa maelekezo yaliyonyooka sana.
Isha na Mama George wakakamatika kirahisi kama kuku wa kizungu. Hata Suzi naye hakusumbua katika kukamatwa.


Hatimaye Dembele akatabasamu. Ndiyo, lazima atabasamu maana alikuwa ameshinda vita. Mashahidi wa uhakika wote alikuwa nao kibindoni.
Nani mwingine wa kumsumbua?
Hakupata jibu la ni nani wa kuweza kumsumbua.


***ISHA, GEORGE, MWANAIDI, MAMA, SUZI, FRIDA. Wote wapo mikononi mwa Dembele.
Je? ni nani wa kuziokoa roho hizi zinazopigania uhuru na furaha ya CHOKORAA. AU NDIYO MWISHO WA HARAKAT???

muuza ubuyu ram Toplady mkereketwaa culbby mbalu BPM Jullie Z Igunga Moja
 
Last edited by a moderator:
Dah!!harakati zinafikia ukingoni au mapambano.ndo yanazidi..songa nayo..
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…