Riwaya: Barua Kutoka Jela

Riwaya: Barua Kutoka Jela

RIWAYA: BARUA KUTOKA JELA
MTUNZI: IBRAHIM GAMA


SEHEMU YA KUMI

Hivyo mara kwa mara alipokuwa anaongea kupitia vyombo vya habari, kuelezea maendeleo ya wagonjwa, Inspekta Jamila alikuwa anamuona kupitia kwenye Luninga!
Ndiyo maana hata alipoiona picha yake katika Albam ya marehemu Hamida, mara moja alimtambua!
Lakini kabla hajaongea na Dokta Masawe, kimaajabu na kiulaini anamuona pia Geradi Mwaipopo ambaye yeye alikuwa akimtafuta kwa Udi na Uvumba! Ambaye picha ya sura yake ilinaswa kwenye macho ya marehemu Kiyarwenda Mwemezi Baada ya kufanyika vipimo vya kitaalam.
Hakika Mungu ni Mkubwa kwani hakutegemea watu wale kama wangekuwa na uhusiano! Duh ama kweli usilolijua ni kama usiku wa kiza!
Inspekta Jamila akiwa pale alipo, alimuona yule Dada aliyemletea vinywaji, akiwahudumia Dokta Masawe na kundi lake, akaangalia saa yake na kuona ni saa sita kasoro dakika tano za mchana.
Dokta Masawe aliangalia saa yake kisha akawa anaongea jambo na wenzake, ambalo Inspekta Jamila kwa umbali aliokaa, hakuweza kuwasikia wanachoongea.
Mara bila ya kutarajia Inspekta Jamila alimuita yule Dada Muhudumu, na alipofika pale akamtuma akamwambie Dokta Masawe kuwa, yule mgeni wake wa saa sita ameishafika kitambo yupo pale anamuhitaji! Na yule dada kama umeme akawasilisha ujumbe ule kwenye meza ya Dokta Masawe walioijaza kwa nyama za kuchoma na pombe! Na wote waliokuwa wamekaa katika meza ile wakageuka kumtazama Inspekta Jamila.
ndipo Inspekta Jamila alipoiona sura ya Geradi Mwaipopo kwa ufasaha na uwazi kabisa, kwa haraka haraka aliwatupia macho na wale jamaa wawili lakini hakuambua kitu, kwani hakuweza kumtambua hata mmoja kati ya wale wawili!
Na nukta chache baadae Dokta Masawe alikuwa amehamia katika meza ya Inspekta Jamila wakawa wanatazamana uso kwa uso mdomo kwa mdomo!
“Ndiyo Bi Jenipha habari za tokea muda ule?” alianzisha mazungumzo Dokta Masawe, huku akilikariri lile jina la Jenifa!
Inspekta Jamila ilibakia kidogo tu aangue kicheko, kwani yeye alishasahahu lile jina alilomuongopea Dokta Masawe.
“Nzuri tu Dokta Masawe, pole na kikao. Je! wale waheshimiwa uliokuwa nao, ni miongoni mwa wajumbe katika kikao chako?”
Inspekta Jamila aliongea huku akijichekesha.
“Wewe umejuaje? Watu hawa ndiyo wanaoniweka mjini na muda huu nikawa napata kilaji hapa!”
Alijibu Dokta Masawe, na Inspekta Jamila akatambua kuwa mtu anayeongea nae , ni mualifu anaejiweka katika kivuli cha udaktari.
Ila ana kazi nyingine ya ziada tena ya haramu, inayompa pesa nyingi zinazomfanya awe jeuri na kulewa wakati wa kazi!
“Kumbe nimepatia, basi nipe zawadi yangu.”
Inspekta Jamila akazidi kujizoesha kwa Dokta Masawe ili awe naye Karibu, na hatimaye aendeleze kazi yake iliyomfanya awe pale wakati ule.
“Ehee Lete habari zako, kwani sina muda mrefu nataka kutoka, kuna sehemu nakwenda kumuhudumia mgonjwa.”
Dokta Masawe alianzisha Mazungumzo.
Inspekta Jamila, bila ya kupanga alijikuta akiongea hivi.
“Dokta Masawe Samahani sana tena sana, kwani nina mdogo wangu, amepatwa na matatizo amekuja yupo nyumbani kwangu, hivyo ninahitaji msaada wako umuhudumie!”
Inspekta Jamila aliongea kwa sauti ya upole, huku akiwa macho yake ameyalegeza, na kwa kuwa macho ya Inspekta Jamila tokea asili yake tayari yasharembuliwa! Basi alivyoyalegeza, loo Salale utadhani macho ya mtoto mchanga aliepatwa na ugonjwa wa Degedege!
Na hata kama ungekuwa mgumu kiasi gani, kwa macho yale uzalendo ungekushinda lazima!
Na ndivyo ilivyotokea kwa Dokta Masawe! Akaingia katika mtego wa Inspekta Jamila.
“Do pole sana bibie, je huyo ndugu yako amepatwa na matatizo gani?”
Aliuliza Dokta Masawe huku akionyesha huruma na moyo wakusaidia!
“Yeye amepigwa Risasi na Polisi na risasi imebaki mwilini kwake! Lakini pia imemvunja bega alikuwa katika harakati za kutafuta maisha unajua tena vijana Dokta, hivyo akiwa na wenzake, wameshafanikiwa kupora pesa, wakatokea askari wa doria na kuanza kutupiana risasi, na yeye ikampata risasi ya bega, lakini alifanikiwa kuwatoroka polisi na kuondoka!”
Inspekta Jamila, alisema maneno hayo huku akimtazama Dokta Masawe usoni mwake, na kuendelea.
“Hivyo tafadhali sana Dokta Masawe nakuomba nisaidie kama itawezekana, nitakupa kiasi chochote cha pesa ukiweza kufanikisha jambo hili tafadhali Dokta, tafadhali. Niokoe katika kadhia hii!”
Inspekta Jamila sasa aliuwa kabisa, kwani mtego huo ukinasa, moja kwa moja atakuwa analipigia mstari jibu lake tu kwamba, Dokta Masawe ana uhusiano na wahalifu, wakiwemo Geradi Mwaipopo na wenzake!
Hivyo inawezekana, majambazi kuwa wanamtumia Dokta Masawe katika maswala kama haya, kwani majambazi wanapopigwa risasi, hawaendi katika hospitali za Serikali kwa kuhofia kukamatwa na polisi, Lakini huwa wanatibiwa katika hospitali za watu binafsi au madaktari huenda na vifaa vyao katika nyumba za majambazi hao, na kuwatibia kisha kupewa pesa nyingi sana kwa kitendo hicho!
“Duh Dada unanitisha kidogo, kwani hatujazoeana kabisa, unawezaje kuniambia kitu kama hicho, na wewe nani kakwambia kama mimi nashughulika na vitu hivyo! Yaani unaniweka katika wakati mgumu na sina amani hata kidogo!”
Dokta Masawe alikuwa yupo njia panda, Pesa anaitaka, lakini pia anaogopa kwani hamtambui huyu Dada asije akawa ni askari akaingia katika matatizo, ukizingatia leo hiyo hiyo alitembelewa na askari tena wa kike!
Inspekta Jamila muda wote tokea afike Dokta Masawe alikuwa haishi kuchezeachezea simu yake mara kwa mara kama mtu aliekuwa limbukeni wa simu!
Dokta Masawe baada ya kujiumauma, mwisho wa yote akamwambia yule mwanamke mrembo aliyekuwa mbele ya macho yake, mwenye pua ya upanga iliyochongoka mithili ya pua ya kisomali, ambaye akimwita kwa jina la Jenipha akasema.
“Sawa nimekuelewa na kwa sababu yako nitaifanya kazi hiyo kwa moyo mmoja, na kijana atarejea katika hali yake ya kawaida! Je umeniandalia kiasi gani?”
“Kwa kweli Dokta Masawe kwanza nakushukuru sana kwa moyo wako wa huruma, kuhusu pesa inabidi utaje wewe Dokta, kwani wewe ndiyo mtendaji ila usinigonge sana kwani ndugu yangu atakuletea Tenda kutoka kwa jamaa zake ili nao uwe unawatibia wanapopatwa na matatizo kama yake!”
Inspekta Jamila alizidi kumtega yule Dokta dhalimu ambaye hadi kufikia pale, alikuwa anamchukia vibaya sana!
“Kwanini Dokta unafikiria kunitajia bei, inamaana hujawahi kuwatibu wagonjwa wa namna hiyo?! Kama umeshawahi wewe nipe bei kama hao ulizowapa siku za nyuma!”
Inspekta Jamila aliyasema hayo huku akiendelea kuchezea simu yake!
Dokta Masawe alikohoa kidogo kisha akasema.
“Nakuwa mzito kusema kiasi cha pesa kwa sababu sijamuona mgonjwa mwenyewe nikaweza kumkagua, ili kwanza nijue hiyo risasi imemchuna tu, au imeingia kwenye nyama, lakini pia nijue risasi ya bunduki gani iliyomuathili ndiyo ningeweza kukwambia bei kwa urahisi. Hao ambao tayari nimekwisha watibia Hospitalini kwangu na wengine majumbani mwao wote kwanza niliwaona kisha baada yakuwafanyia uchunguzi, nikawapa bei na kuwashughulikia!”
Dokta Masawe alikuwa anaeleza kitaalam namna anavyofanya kazi yake kwa ufasaha, na kuendelea.
“Labda kwako tuseme hivi, itabidi tukubaliane moja kwa moja hata kama mgonjwa sijamuona kwa kiasi cha shilingi Laki Tano!”
Inspekta Jamila alishusha pumzi nzito kwa jibu lile kwani Dokta Masawe alimthibitishia kuwa ndiyo zake, hivyo kwa kuwa yeye alikuwa yupo kazini, alikubali bila hata kulilia hali!
“Sawa Dokta nimekubali, kwani pesa kitu gani bwana, pesa zinatafutwa! Hasara Roho pesa makaratasi!”
“Thatha Bwana Mathawe ndiyo umehamia moja kwa moja kwa huyu bibie hadi jamaa dhako umetuthahau?!”
Ilikuwa ni kauli ya mmoja kati ya wale jamaa alioingia nao Dokta Masawe, na mara moja Inspekta Jamila mapigo ya moyo yakaanza kumwenda mbio!
Kwani aliikumbuka kauli ya Bwana Masudi, yule jirani yake Mwaduga, alipomwambia kuwa.
“Nilimsikia akiongea kwa kithethe, tunatho Elfu tatu tupeleke kwa macheni”
Leo akiwa na Dokta Masawe anamsikia jamaa akiongea kwa kithethe, na hata wasifu wake alioambiwa na Masudi, hakika unashabihiana nae.
Huyu bwana ni katika wale watu wawili, ambao Inspekta Jamila, hakuweza kuwatambua awali.
Inspekta Jamila Pia akafikiri kuwa, wale jamaa huenda ikawa ndiyo waliopanda Taxi ya Mwaduga pale katika barabara ya Namnani! Hapo mapigo ya moyo yakazidi kumuenda mbio, huku damu ikimchemka!.
Inspekta Jamila aliinua simu yake juu kuelekea kwa yule Jamaa wa Kithethe huku akiwa anacheka hadi jino la mwisho linaonekana,huku akiendelea kuchezea simu akamwambia yule bwana kithethe.
“Huo wivu sasa unaouleta, kama unaona Dokta anafaidi basi njoo na wewe ukae!”
Hatimae kwa jibu lile wote watatu wakaangua kicheko.
Dokta Masawe alimjibu yule bwana; “Nakuja sasa hivi kwani namalizia malizia maongezi ya mwishomwisho!”
Na yule jamaa akamwambia, “Mimi thikuonei wivu, ila ulithema kuna thehemu unatakiwa thaa nane, na hivi thatha ni thaa thaba na nuthu”
Baada ya kusema hayo mzee wa kithethe akarudi kwa wenzie kwenda kuendelea na makulaji!
Dokta Masawe na Inspekta Jamila wakakubaliana kesho jumanne baada yakutoka Muhimbili katika “Clinic” yake wakutane maeneo ya Ilala Amana, ili waongozane hadi nyumbani kwake Inspekta Jamila, ambaye Dokta Masawe alimtambua kwa jina la Jenipha, ili akatoe huduma kwa mgonjwa.
Baada ya kuafikiana, Dokta Masawe, aliondoka katika meza ile, na kurudi katika meza ya maswahiba zake.
Inspekta Jamila akifurahia kuwa mtego wake umenasa vizuri na hasa umekuwa ni MTEGO WA PANYA kwani huingia aliyekuwepo na asiyekuwepo! Au labda niseme ilikuwa jiwe moja kwa ndege watatu!
Inspekta Jamila akaendelea kunywa kinywaji chake cha ofa baada ya kile alichoagiza kwa pesa yake kukimaliza.
Huku macho yake yakiwaangalia wale jamaa waliokuja na Dokta Masawe, mara akamuona Dokta Masawe ameinuka na kuagana na jamaa zake kisha akatoka nje ya hoteli na kutokomea kusikojulikana.
Inspekta Jamila alingoja kama kiasi cha dakika tatu toka kuondoka kwa Dokta Masawe, aliinuka katika kiti alichokalia na kwenda chooni huku akipita Karibu kabisa na meza ya wale jamaa, kisha ule mkono uliokuwa umeshika simu yake, akawanyooshea mkono na kuwapungia akiwapa salamu, huku nao wote wakiwa wanamtazama na walimuitikia salamu yake huku wakiwa wamepigwa na ganzi kwa mshangao! Wakistaajabia urembo wake.
Geradi Mwaipopo alikuwa yupo tofauti na wenzake, kwani yeye aliitazama ile simu ya Inspekta Jamila, kisha akamkazia macho ya udadisi mkuu!
Inspekta jamila, yeye akapitiliza moja kwa moja hadi katika vyoo vya wanawake na kuingia chooni.
Ilimchukua kama dakika tatu hivi akiwa kule chooni, alipotoka nusura aanguke kwa mshangao, kwani sehemu waliokuwa wamekaa kina Jeradi Mwaipopo, sasa ilikuwa na viti vitupu!
wale jamaa walishatoka eneo lile.
Inspekta Jamila alimuona yule muhudumu wa kike akiondosha chupa zilizokuwa zimezagaa kwenye meza ile!
Inspekta Jamila kwa mwendo wa haraka alitoka nje ili awawahi watu wale, na hatimae awafatilie kusudi iwe rahisi kuwatia mkononi mwa Sheria.
Alipotoka nje akaiona gari moja aina ya Toyota Mark II nyeupe ikiingia barabarani kuelekea maeneo ya Kagera ikiwa inatoka katika sehemu ile ya hotel!
Kitendo bila kuchelewa, Inspekta Jamila aliwahi kwenye gari yake ili awafatilie wale wahalifu, lakini alipofika usawa wa gari yake, ilibidi akae chini kwa jinsi alivyochoshwa!
Tairi la mbele upande wa dereva wa gari yake lilikuwa limelala chini lina pancha!
“Nooo! Haiwezekani.”
Hatimaye Inspekta Jamila, alipata nguvu na kutoa kauli.
Inspekta Jamila, alikuwa hakubaliani na hali aliyoiona katika gari yake.
Tairi za gari yake, zilikuwa mpya kabisa, tena ni TUBE LESS hivyo hata kama angekuwa amekanyaga msumari tairi lisingelala mapema kiasi kile!
Akiwa pale chini kwenye kikuta akiwa amekaa, aliishuhudia ile gari ikipotea machoni mwake,huku naye akiwa amekata tamaa!
Mara walitokea jamaa wawili waliokuwa wanaosha magari katika eneo lile, wakamwambia Inspekta Jamila.
“Vipi sister unayo jeki na spana tuchakarike chap chap?”
Inspekta Jamila akawaangalia wale jamaa na kuridhika kwamba siyo watu wabaya, akapatana nao bei ili wambadilishie tairi wamuwekee tairi la akiba.
Inspekta Jamila akainuka pale alipokuwa na kuuendea mlango wa gari yake, ili afungue apate kutoa jeki na spana yakufungulia tairi, akasikia sauti kutoka kwa wale jamaa ikimwambia.


“Tulia hivyo hivyo Inspekta Jamila! Kwani kujaribu kubisha ni sawa kabisa na kusaini kifo!”
**MASSAWE anahusika vipi na matendo ya kiovu??
**JAMILA matatani vijana aliowaamini wamemteka na kutishia uhai wake….nini kitaendelea???


Jagarld Jullie Z Sangomwile Khantwe Mr Rocky Gunda66 Himidini VAN HEIST BPM ABUBAKAR SHEKAU NYIROmamsapkhan born again pagan princetx Ennie mcubic jonnie_vincy slim5
 
Nafatilia kila hatua asante sana Cusuist
 
Last edited by a moderator:
Ooh maskini inspector nazidi kumuhofia shoga yk dkt zahala. Huenda anakuchomesha
 
ukuje huku mpendwa, kuna kitu kimeekwa ram
 
Last edited by a moderator:
Hii kazi ya udetective inahitaji ujasir mkubwa sana vinginevyo unaweza kuikimbia
 
Dah, kazi zingine hizi zataka moyo,huyu mwaipopo ni jambazi lililobobea,pole jamila najua kufa hufi lakini cha moto utakiona..!

Pamoja sana mkuu Casuist
 
Last edited by a moderator:
Dah, kazi zingine hizi zataka moyo,huyu mwaipopo ni jambazi lililobobea,pole jamila najua kufa hufi lakini cha moto utakiona..!

Pamoja sana mkuu Casuist
 
Last edited by a moderator:
Dah, kazi zingine hizi zataka moyo,huyu mwaipopo ni jambazi lililobobea,pole jamila najua kufa hufi lakini cha moto utakiona..!

Pamoja sana mkuu Casuist
 
Last edited by a moderator:
Hii story tamu jamani..casuist uwe unatupia walau sehemu 2 kwa mpigo..
 
RIWAYA: BARUA KUTOKA JELA
MTUNZI: Ibrahim Gama


SEHEMU YA KUMI NA MOJA

Hatimaye Inspekta Jamila, alipata nguvu na kutoa kauli.
Inspekta Jamila, alikuwa hakubaliani na hali aliyoiona katika gari yake.
Tairi za gari yake, zilikuwa mpya kabisa, tena ni TUBE LESS hivyo hata kama angekuwa amekanyaga msumari tairi lisingelala mapema kiasi kile!
Akiwa pale chini kwenye kikuta akiwa amekaa, aliishuhudia ile gari ikipotea machoni mwake,huku naye akiwa amekata tamaa!
Mara walitokea jamaa wawili waliokuwa wanaosha magari katika eneo lile, wakamwambia Inspekta Jamila.
"Vipi sister unayo jeki na spana tuchakarike chap chap?"
Inspekta Jamila akawaangalia wale jamaa na kuridhika kwamba siyo watu wabaya, akapatana nao bei ili wambadilishie tairi wamuwekee tairi la akiba.
Inspekta Jamila akainuka pale alipokuwa na kuuendea mlango wa gari yake, ili afungue apate kutoa jeki na spana yakufungulia tairi, akasikia sauti kutoka kwa wale jamaa ikimwambia.
"Tulia hivyo hivyo Inspekta Jamila! Kwani kujaribu kubisha ni sawa kabisa na kusaini kifo!"
Mmoja kati ya wale jamaa wawili alimwambia Inspekta Jamila huku mkononi akiwa ameshikilia Bastola aina ya Chinise.
Inspekta Jamila alisikia maneno yale yakimuingia hadi kwenye damu, huku akiwa amemuelekezea mgongo yule jamaa anaemuamrisha maneno yale.
Inspekta Jamila alitaka kugeuka, lakini jamaa aliikoki ile bastola huku akimwambia.
"Stop! Mkononi kwangu nina silaha ya moto, na ndani yake kuna risasi nane hivyo,sitosita kuitumia kama tu utaleta ukaidi. sikiliza ujumbe wangu kwa makini, na nitakuacha huru uendelee kupumua! Kwani maisha yako nimeyashika yapo mkononi mwangu!"
Wakati jamaa mmoja amemtuliza Inspekta Jamila, yule mwengine alitoka mbio akaingia katika gari iliyokuwa imeegeshwa jirani kabisa na gari ya Inspekta Jamila akaiwasha na kuiweka mkao wa kutoka!
"Elekea kwenye hiyo gari na upande, kisha nikupe ujumbe wangu huku gari ikiwa inatembea, nikishamaliza kukupa ujumbe wangu na ukaukubali nitakuacha huru na hai, ila kama utaendelea kukaidi kama tulivyokuagiza katika walaka mfupi kule Muhimbili, nitayakatiza maisha yako Inspekta!"
Moyo wa Inspekta Jamila ukapiga Pah huku ukimuenda mbio! Alichofanya nikuelekea katika ile gari huku damu ikimchemka, na jamaa akimfatilia kwa Karibu nyuma yake.
Alipofika katika mlango wa ile gari, aliangalia mle ndani ya gari nakumuona mtu mmoja tu aliekaa nyuma ya usukani ambae ni yule jamaa aliejifanya muosha magari, gari waliyokuwa wanaiosha ndiyo iliyofunguliwa mlango ili aingie!
Hapo kulitokea kitu mbacho hakuna aliekitegemea katika wale jamaa.
Inspekta Jamila aliinama kama anaetaka kupanda ile gari, na yule jamaa aliemshikia bastola nyuma yake, akasogea Karibu zaidi ili aingie pamoja nae.
Inspekta Jamila kwa wepesi wa ajabu alirusha teke aina ya OSHIRO na kuipangusa ile bastola mikononi mwa yule jamaa, na ile bastola iliruka juu!
{OSHIRO ni teke la kisigino linalopigwa kwa kuzunguka ukiwa umempa adui mgongo.}
Yule jamaa akiwa amefadhaishwa kwa kitendo kile, akaruka juu ili aidake ile bastola.
Na hilo lilikuwa ni kosa la mwaka kwake, Inspekta Jamila alirusha teke lingine, safari hii akipiga teke aina ya MAIGERI na kumpata yuje jamaa katika kifua usawa wa chembe, na yule jamaa akatupwa nyuma kama gunia nakuanguka kwa kishindo akidondokea kisogo!
{MAIGERI ni teke linalopigwa kwa unyayo wa chini ya vidole vya mguu ukiwa unatazamana na adui}
Inspekta jamila kwa kasi ya ajabu, aliitoa bastola yake mgongoni kwa mkono wake wa kushoto, na kuikoki wakati huohuo akiidaka ile bastola ya yule baradhuli kwa mkono wake wa kulia, akawa na bastola mbili mikononi mwake!
Inspekta Jamila aliichanua mikono yake ikawa kila mtu katika wale jamaa wawili anatazamana na mdomo wa bastola.
Moja akiielekeza magharibi, na nyingine upande wa mashariki kwa namna walivyokaa wale watekaji wake!
Yule jamaa aliekuwa ndani ya gari, alipoona mambo yamegeuka akakanyaga mafuta kwa nguvu, na gari ile aina ya Toyota Chesser Automatic yenye Silinda sita iliondoka kasi huku ikichimba eneo lile ikiwacha vumbi la hali ya juu!
Inspekta Jamila sasa kwa mikono miwili ambayo imekamata bastola mbili, alijitupa chini kama Mkizi akilala kifudifudi huku akizielekeza zile bastola kule kwenye ile gari na kufyatua risasi mfululizo zilizopiga kwenye tairi za gari ile, na akaishuhudia gari ile ikiruka juu na kupinduka juu chini! Huku ikiwa imeshaingia katika barabara ya morogoro ikawa Boneti la gari ile ikipanda kikuta kinachotenganisha barabara, na Buti lake likiwa barabarani huku Magurudumu yake yakizunguka hali ya kuwa yapo juu!
Kilichofatia ni mtafaruku na fadhaa ya hali ya juu kwa wakazi wa maeneo yale, kwani watu walikuwa wanakimbia hovyo huku wakipiga kelele, pia wapo waliokuwa wanakimbilia ili waone kilichotokea.
Inspekta Jamila akamgeukia yule jamaa pale chini, akapiga goti na kumuelekezea zile bastola mbili zilizokuwa mikononi mwake, akamuona yule jamaa anakohoa damu tena mfululizo.
Inspekta Jamila akaingiza mkono katika mkoba wake uliokuwa unaning'inia begani muda ule, akatoa simu yake na kubonyeza tarakimu kadhaa kisha baada ya kupokelewa simu ile alisema.
"Specil order nipo manzese Aljentina hapa, Friends corner hotel ongeza nguvu tafadhali, kuna wahalifu nimepambana nao."
Baada yakusema yale akakata simu na kumsogelea yule jamaa pale chini, huku watu wakiwa wamejaa eneo lile, akairudisha simu yake katika mkoba wake kisha akaitoa risasi iliyokuwa Chemba tayari kwa kufyatuka kutoka katika bastola ya yule jambazi pale chini pamoja na magazine yake, akaitumbukiza katika mkoba wake.
Akabakiwa na bastola moja tu sasa akamnyooshea yule mtekaji wake na kumwambia.
"Safari yetu ya pamoja bado ipo! Ila itabidi tusubiri gari nyingine, kwani yangu ina pancha na ile yenu imepinduka!"
Kiasi cha dakika tano baadae Gari aina ya Land Rover 110 Difender mbili za polisi, huku mitutu ikiwa mikononi ziliwasili eneo lile, na tafrani ikaanza upya kwani watu walikuwa wanakimbia hovyo eneo lote likajaa hekaheka tupu.
Inspekta Jamila akatoa maelekezo kwa wale askari wa Doria Kenda, na mara moja yule jambazi alisombwa msobemsobe akarushwa ndani ya ile gari ya polisi huku afande mwingine akishughulikia kubadilisha tairi katika gari ya Inspekta Jamila.
Kule katika Barabara ya Morogoro, askari wa usalama barabarani walikuwa wanayaongoza magari kupita, huku simu za upepo zao zikiwa zinawasaidia kuwasiliana na watu wa "Break Down" ili kuja kuiondosha ile gari iliyopata ajali.
Yule jambazi alietaka kutoroka na gari, baada yakuona wamedhibitiwa, alikuwa anatolewa chini ya uangalizi wa askari polisi, kwani alikuwa amenaswa na usukani wa gari ile.
Inspekta Jamila akamuendea yule Jambazi aliepambana nae pale alipolala ndani ya gari ya polisi na kumwambia.
"Kabla hatujaendelea na safari yetu, itabidi upelekwe hospitali kwanza, ukishapata uzima safari yetu kama kazi itakuwepo!"
Dakika tano baadae Inspekta Jamila aliondoka eneo lile akielekea ofisini kwake, huku zile Gari mbili za askari polisi moja ikiwa imebeba majeruhi wawili ikiwakimbiza katika hospitali ya taifa ya muhimbili na nyingine ikimsindikiza Afande jamila!
Namna gari zile zilivyokuwa zikiondoka, na wale askari walivyokuwa wananing'inia huku bunduki zao aina ya SMG walivyozidhibiti mikononi mwao, raia walijikuta wakishangilia kama wapo mpirani vile!
Huku nyuma magari matatu aina ya Land Rover 109 yalikuwa yanakuja kwa kasi eneo lile ili kuwahi Tenda ya kuinua na kuivuta ile gari iliyopata ajali, zilikuwa ni "Break Down!" Na hiyo ilikuwa ni saa nane na robo ya mchana mbuzi anakula majani.
*******
Saa kumi na moja ya jioni, Inspekta Jamila alikuwa ameketi katika kiti ofisini kwa "IGP" akimpa maelezo ya kazi yake kama alivyoelekezwa na bosi wake huyo.
"Afande kuna jambo linaniumiza kichwa, kwani leo ikiwa ni siku ya kwanza tu kuanza rasmi kufatilia kesi hii nimegundua kwamba kuna watu ambao tayari wana taarifa ya mimi kuishika kesi hii! Na wanajaribu kunitisha nisiendelee kuifanya kazi hii, kazi ambayo ina heshima kubwa kwangu katika maisha yangu ya uaskari."
Inspekta Jamila alikuwa anaongea kwa hisia ya hali ya juu sana, huku akionekana mzuka kumpanda.
"Hasa yule ----- aliepelekwa hospitali, yule anajua kila kitu kwani ameshanithibitishia mimi mwenyewe pale alipojaribu kuniteka!"
"IGP" alikuwa kimya akimsikiliza kijana wake,lakini bado akiendelea kumshangaa! kwani Inspekta Jamila alikuwa anajiamini na nimtendaji mzuri.
"Sasa Afande hebu nipe taarifa kwanza namna ilivyokuwa, kisha kujulikana kuwa wewe ndiyo mwenye kesi hii tutajadili mwisho wa ripoti yako."
"IGP" alimwambia Inspekta Jamila. Nae Inspekta Jamila akamuhadithia kila kitu, toka asubuhi matukio ya kikazi aliyopambana nayo, hadi kufikia wakati ule walipokuwa wamekaa katika ofisi ile!
"IGP" alikuwa akimsikiliza kijana wake huku akisisimkwa na damu katika baadhi ya maelezo ya kijana wake.
Inspekta Jamila baada ya kumaliza kutoa ripoti yake, "IGP" alikuwa katika tafakari nzito, kisha akasema.
"Umesema ulikuwa ukiwarekodi kupitia simu yako yenye uwezo wakupiga picha za video, na wale wahalifu wote umepata sura zao, kazi nzuri sana kijana."
"IGP" alimpongeza Inspekta Jamila kwa ujasiri na kuweza kufanikisha kuwatambua wahalifu wale, lakini pia wale aliowatia mbaloni!
"Sasa kuna kitu kimoja nataka uwelewe kutoka sasa kuwa, kwa vyovyote vile wale majambazi wameshakugundua kuwa wewe ni askari tena hatari kwao!
Hivyo hata Dokta Masawe kwa kuwa ana mawasiliano na wale jamaa kuna uwezekano mkubwa tukampoteza, hivyo itabadi leo usiku atiwe mbaloni ili tuweze kuwakamata na wahalifu wenzake!"
"IGP" alikuwa anachangia mawazo yake baada yakupata ripoti kutoka kwa kijana wake.
"Sawa kabisa mkuu, pia naomba mkuu yule kijana aliopo mahabusu Mwaduga Dingo, ufanyike mpango wa haraka aachiwe ili aje kuwatambua wale jamaa niliowapiga picha."
Inspekta Jamila alitoa pendekezo kwa mkuu wake wa kazi.
"Kijana Mwaduga nilishaongea na mkurugenzi wa mashtaka kila kitu, na kesho kutwa siku ya jumatano, mkurugenzi amenambia, atamuondolea mashtaka yanayomkabili, hivyo ataachiwa huru."
"IGP" alihitimisha suala la Mwaduga Dingo.
Inspekta Jamila na mkuu wake wa kazi walipanga mikakati ya namna ya kushinda kesi ile kwa ushahidi usio na chembe ya shaka, kisha wakaletewa chakula mlemle ofisini wakala, walipomaliza kula ilikuwa imeshatimu saa mbili za asiku!
"Sasa wewe nenda ukapumzike kazi nzuri sana uliyoifanya katika siku ya leo, na kama ulivyopendekeza katika ripoti yako, Afande Kubuta awe ndiyo askari utakaeshirikiana nae, hilo litakamilika na usiku huu yeye ndiye atakaekwenda kumkamata Dokta Masawe nyumbani kwake."
"IGP" akaagana na Inspekta Jamila ambae alikuwa amechafuka na amechoka, huku yeye akiinua simu na kumtafuta Afande Kubuta na kumwita ofisini kwake usiku uleule!



**MAIGERI na OSHIRO zimemuokoa Inspekta dhidi ya watu wabaya…..
***USHAHIDI unazidi kupatikana…
NINI KIMEJIFICHA NYUMA YA PAZIA..
USIKOSE MUENDELEZO

Jagarld Jullie Z Sangomwile Khantwe Mr Rocky Gunda66 Himidini VAN HEIST BPM ABUBAKAR SHEKAU NYIROmamsapkhan born again pagan princetx Ennie mcubic jonnie_vincy slim5 MAVUNO mp anold amoneyazan
 
Ya leo fupi sana Casuist tuwekee nyingine tafadhali
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom