Riwaya - Balaa

Riwaya - Balaa

SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA SABINI

Masaa matano ndani ya gari yake aina ya Toyota corolla yalitosha kumfikisha mpelelezi mahiri nchini Tanzania, Daniel Mwaseba katika mji mdogo wa kitalii, Kilwa Masoko. Mji ambao kwa sasa ulikuwa umechafuka kwa matukio mauji ya kutisha sana pamoja na upotevu wa maiti katika hospitali ya wilaya ya Kilwa, iliyopo katika mji wa Kilwa Kivinje, kilometa chache tu toka mji wa Kilwa Masoko. Daniel Mwaseba alitafuta hoteli nzuri ya kupumzika kabla hajaanza shughuli, miongoni mwa shughuli ngumu zaidi alizowahi kuzifanya Daniel Mwaseba katika kuitetea Tanzania dhidi ya hila zote za watu wabaya. Hoteli ya kitalii ya Kimbilio nd'o lilikuwa jibu lake. Hoteli iliyokuwa kandokando mwa bahari ya Hindi, katika fukwe nzuri na safi za pwani ya Jimbizi ama JB kama wenyeji wa Kilwa walivyozoea kuziita. Katika hoteli hiyo Daniel Mwaseba alipokelewa kwa ukarimu wa hali ya juu. Kama zilivyo mila na desturi za watu wa Kilwa. Mhudumu wa kike aliyevaa sare za hoteli hiyo, sketi fupi ya bluu isiyofika katika magoti na shati safi jeupe. Mhudumu huyo alimpeleka Daniel Mwaseba katika chumba safi na kikubwa, namba 53 alifanikiwa kusoma namba pale mlangoni wakati akiingia ndani ya chumba hiko, waliingia ndani na yule Mhudumu aliyejitambulisha kwa jina la Irene. Irene alimuelekeza Daniel vitu mbalimbali kuhusu chumba kile kisha akaondoka. Alivyobaki peke yake Daniel Mwaseba akajilaza chali katika kitanda kipana cha kitanda kile. Akiwa amelala pale kitandani maandishi yote yaliyoandikwa na mwandishi asiyejulikana jina katika gazeti la Shupavu yalijirudia katika kichwa chake.

Siku nzima Daniel Mwaseba aliimaliza pale Kimbilio hoteli. Alipata kila alichokihitaji katika hoteli ile.
Jioni alienda katika fukwe nzuri ya jimbiza aliyokuwa anaisikia sifa zake, hakuwahi kufika katika fukwe hiyo ingawa alishawahi kwenda mara kadhaa Kilwa, alipigwa na upepo mwanana wa bahari. Hakuwa na haja ya kwenda kutembea mjini, alikuwa anaujua sana mji wa Kilwa. Alishakuja katika harakati zake nyingi sana za kipelelezi. Alitulia ufukweni hadi giza lilivyoanza na kurudi katika hoteli aliyofikia.

Siku iliyofuata ilikuwa ni siku ya balaa sana katika mji wa Kilwa Masoko. Wanafunzi mia moja wa shule ya Msingi Masoko hawakujulikana walipoenda. Ilikuwa balaa hasa. Mji nzima wa Kilwa ilikuwa ni vilio. Vilio toka kwa wazazi wa watoto waliopotea, vilio toka kwa ndugu wa watoto waliopotea. Jeshi la polisi wilayani Kilwa liliingia tena kazini angalau tu kupata fununu tu kwa kilichotokea kwa watoto hao mia moja wa shule ya Msingi Masoko. Hadi jioni haikupatikana fununu yoyote. Taarifa ilikuwa ileile. Kwamba watoto mia moja hawatolala majumbani mwao usiku ule. Watalala wapi, lilikuwa swali gumu ambalo jeshi la polisi na wazazi wa watoto hao hawakuwa wanaweza kulijibu.

Siku hiyo mbaya ikapita, ikaja siku nyingine mpya. Baada ya siku tatu tangu watoto wapotee katika shule ya Msingi Masoko. Hakukuwa na taarifa yoyote juu ya watoto wale waliopotea. Siku hiyo ya tatu ikaja na jipya, watoto kumi na saba toka katika shule ya Sekondari Kilwa walipotea. Matukio yote hayo yalifikia sikio la Daniel Mwaseba na kumfanya Daniel Mwaseba atabasamu. Tabasamu la kishujaa akijua kwamba kazi aliyokuwa anaipenda zaidi hapa duniani imeanza...


ITAENDELEA MUNGU AKIPENDA
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA SABINI NA MOJA

Sasa askari walijigawa kulinda shule zote za mjini Masoko. Na wazazi wengine waliingiwa na uwoga sana, hawakuruhusu watoto wao waende shule. Kuruhusu mtoto kwenda shule ilikuwa ni sawa na kumpoteza kabisa!
Vilio ndani ya Kilwa vilizidi na kupaa zaidi, vikafika hadi nje ya mipaka ya Tanzania. Umoja wa mataifa kupitia shirika lake la watoto wakatoa kauli, na kuitaka Serikali ya Tanzania kuongeza nguvu katika kuwasaka wauaji hao. Marejani nayo ikatoa kauli, na kulaani pia vitendo hivyo vya kinyama. Hadi sasa watu wa Kilwa wakiwa hawajui chanzo cha mambo hayo kutokea.
Mji ulipoa, watu wakiishi kwa woga kuu. Watu wazima waliogopa, watoto wadogo waliogopa! Uwoga ulioathiri hadi shughuli za kiuchumi za Kilwa. Wakubwa waliogopa kwenda makazini, watoto waliogopa kwenda shuleni.

Wakati ulinzi ukishamiri katika shule zote za Msingi na Sekondari Kilwa. Polisi wakigeuka walinzi wa shule, kundi la Six Killers walibadirisha aina ya pigo sasa. Walevi saba walitoka majumbani kwao jioni lakini hawakurejea kwao usiku wa manane kama ilivyo ada yao. Walipokuwa wanarejea majumbani kwao usiku baada ya kulewa, njiani walidakwa na Six killers na kupelekwa porini ngome. Six Killers walikuwa wanahitaji mioyo, iwe ya watoto, iwe ya wakubwa, iwe ya walevi ama ya wazima.

Kwa bahati mbaya kabisa, miongoni mwa walevi waliokamatwa usiku ule mbaya ni mama Kindumba, rafiki kipenzi wa Mwanasheria mlevi.

Ilikuwa ni wiki kadhaa tangu Mwanasheria mlevi kutoonekana katika kilinge chao cha ulevi. Ilikuwa huzuni kwa walevi wote kutoonekana kwa Mwanasheria mlevi. Huku lawama zote zikiienda kwa jeshi la polisi ambao ndio walimchukua kwa mara ya mwisho. Lakini pamoja na kutoonekana kwa Mwanasheria mlevi, walevi hawakuacha kunywa pombe. Waliendelea kunywa pombe huku wakimlilia Mwanasheria mlevi. Hakuna hata mlevi mmoja aliyewaza kwenda kituo cha polisi kujua hatma ya Mwanasheria mlevi. Wao wenyewe walikuwa wanajihisi wakosefu. Waende kituo cha polisi halafu....

Ikaja usiku huu, usiku ambao walevi saba walipotea katika mazingira ya kutatanisha. Ukiwa ni muendelezo wa kupoteza kwa wanafunzi. Six killers walifanya kazi kwa umakini mkubwa sana, kila Mlevi alikamatwa kwa namna yake. Huku mama Kindumba akiwa mlevi wa mwisho kukamatwa usiku ule.....

ITAENDELEA MUNGU AKIPENDA
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU! 0757 633010

SEHEMU YA SABINI NA MBILI

Mama Kindumba alitoka kilabuni saa nane ya usiku. Alikuwa na furaha sana, alikuwa kalewa barabara, akiimba nyimbo yeye mwenyewe na kucheza yeye mwenyewe. Alikuwa anakata mitaa usiku wenye giza nene bila wasiwasi wowote. Watu husema pombe hupunguza uwoga kwa mlevi, inawezekana ikawa kweli maana mama Kindumba hakuwa na uwoga wowote usiku ule. Nyimbo zikizoimbwa kwa sauti ya kilevi na mbwembwe za kilevi zilikoma alipokutana na Bedui, Moja wa Six Killers. Pombe zote ziliishia hapo, nyimbo ziliishia hapo. Kwanza aliona Kivuli kirefu cheusi, kisha kivuli hiko kilirusha kofi moja la nguvu toka katika mkono ulioshiba wa wa Kivuli, mkono uliochanganyika na dawa za kulevya ulimlaza Mama Kindumba usingizi nzito. Mama Kindumba alilala katika mtaa wa Kariakoo pale karibu na ukumbi wa Hall fear na kuamka katika pori la Ngome. Na mama Kindumba kukamilisha idadi ya walevi saba waliotekwa siku hiyo.

Mpelelezi Daniel Mwaseba ilikuwa ni sawa na askari Polisi wa kituo cha Polisi Masoko. Kila alipojaribu kuweka mtego wake kuwatega wahalifu kundi la Six killers waliutegeua mtego wake. Wakina Don Genge walikuwa wajanja sana walibadiri aina ya watu wanaowateka mara kwa mara. Wakati wanawateka wanafunzi wa shule ya Msingi Masoko, siku ya pili yake Daniel Mwaseba alienda kulinda katika shule ya Msingi Mnazimmoja. Lakini Six killers hawakwenda kuteka tena wanafunzi wa shule ya msingi, walibadiri mbinu, walienda kuteka wanafunzi wa shule ya Sekondari Kilwa. Wakati Daniel Mwaseba alienda kulinda shule ya Sekondari Mtanga, kundi la six Killers walibadiri tena mtindo walienda kuwateka walevi.
Daniel alikuwa anatabasamu kila tukio linavyotokea, ishara kwamba alikuwa anakasirika sana. Huyo ndiye Daniel Mwaseba hutabasamu kila mambo yanavyokuwa mazito.

Kwa upande wa kundi la Six killers kwao ilikuwa ni furaha, vifijo na nderemo. Walikuwa na mateka wengi sana. Sasa walitulia katika kambi yao wakiwa na uhakika wa kupata mioyo kumi tano kwa siku kadhaa.

Mwezi ukapita, bila tukio lolote lile la kushangaza katika mji wa Kilwa Masoko wala mji wa Kilwa Kivinje. Baadhi ya watu walianza kusahau matukio ya kutisha yaliyotokea mwezi mmoja nyuma. Watu walianza tena kutembea usiku. Baadhi ya askari Polisi pia walisahau kasheshe iliyotokea mwezi mmoja nyuma. Lakini wazazi na ndugu wa watu waliotekwa hawakusahau kabisa, waliomboleza kila siku juu ya upotevu wa ndugu zao. Wao walikuwa na mawazo sawa na mpelelezi mahiri nchini Tanzania, Daniel Mwaseba, ambaye hakuwa amesahau juu ya vifo na upotevu wa watu kiajabu wa raia wema na alikuwa kazini kila jua lililokuwa linachomoza.....

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA SABINI NA TATU

Hatimaye Daniel Mwaseba sasa alikusanya taarifa za kutosha juu ya sakata hii, na kuingia kazini rasmi.
Jioni moja ilimkuta Daniel Mwaseba katika baa ya Tiga Tisa. Baa ileile iliyokuwa chanzo cha kifo cha Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya Kilwa. Pale Tano alipoikosa shabaha yake ambayo ilikuwa ni Mwanasheria mlevi na kumuua Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa. Daniel Mwaseba hakwenda kunywa katika baa ile. Daniel Mwaseba alikuwa kazini. Alikuwa makini kwa kila kilichoendelea pale Tiga Tisa, alijua lazima atapata kitu kitakachompeleka hatua nyingine katika upelelezi wake. Naam, Daniel Mwaseba alishakusanya taarifa za kutosha. Taarifa ambazo zilizomjurisha kwamba, kwa mara ya mwisho Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa alikuwa katika baa hiyo kabla mauti hayajamfata hadi nyumbani kwake. Bila shaka Israel mtoa roho alitoka naye hapo, hivyo ndivyo Daniel Mwaseba akivyoamini.

Hiyo ndio sababu pekee iliyompeleka Daniel Mwaseba katika baa ya Tigatisa. Alikaa kwenye kona moja, iliyokuwa gizani kidogo lakini ilimuwezesha kuona watu wote wanaoingia na kutoka katika baa ile maarufu Kilwa.

Saa nne alikaa pale baa ya Tiga Tisa. Hakukuwa na kitu chochote cha kukitilia shaka. Baa ilikuwa na ushwari wake uleule alioukuta tangu alivyoingia.

'Mvumilivu hula mbivu'

Saa sita ya usiku katika baa ya Tiga Tisa aliingia mtu mmoja mrefu, mtu ambaye Daniel Mwaseba alimtilia shaka kidogo. Alikuwa jamaa mmoja mwenye mwili uliojengeka kimazoezi, alikuwa amevaa vest nyeupe huku chini akiwa amevaa pensi fupi aina ya timberland. Pamoja na ujabari uliokuwa unaonekana katika mwonekano wake lakini alikuwa anachemenea mguu mmoja. Sifa hizo hazikumfanya Daniel Mwaseba astuke sana, mpaka pale Mhudumu wa baa ile alivyomkonyeza Daniel Mwaseba...

ITAENDELEA MUNGU AKIPENDA
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA SABINI NA NNE

Daniel alishaenda katika Baa hiyo mida ya jioni na kumuhoji Mhudumu wa Baa ile. Mhudumu aliyemthibitishia kuwa anamtambua mtu anayemuhisi kuwa ndiye alimuuwa Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya Kilwa. Mhudumu alimwambia kuwa alimtilia shaka mtu huyo pindi tu alivyoingia katika Baa ile. Mhudumu alianza kumpeleleza mtu yule kwa siri. Ingawa Mhudumu hakuwa mtaalamu wa wahalifu, lakini macho ya mtu yule yalimjulisha kwamba yule jamaa alikuwa Mhalifu! Aliyashuhudia macho mabaya ya jamaa yule yakimwangalia Mwanasheria mara kwa mara. Na pindi tu Mwanasheria alivyopanda gari lake na kuondoka, na yule jamaa naye aliondoka.

Zilipokuja taarifa kwamba Mwanasheria kauwawa kwa kisu nyumbani kwake, yule Mhudumu alimtilia shaka sana yule mtu aliyemwona akimwangalia Mwanasheria kwa jicho baya. Lakini hakuwa na mtu sahihi wa kumueleza.

Upelelezi wa polisi ulikuwa wa ajabu sana. Hawakwenda kabisa kupeleleza mahali ambapo Mwanasheria alionekana kwa mara ya mwisho (Tigatisa). Mhudumu yule aliwasubiri askari waje pale angalau awaambie anachokifahamu kuhusu kifo cha Mwanasheria, lakini polisi hawakwenda. Naye hakuwa na amani ya kwenda kituo cha Polisi kueleza hisia zake, kwanza zilikuwa hisia tu. Mhudumu alikaa na dukuduku moyoni mpaka leo hii jioni alivyokuja askari huyu kijana, Daniel Mwaseba. Baada ya Daniel Mwaseba kumchokonoa Mhudumu yule Mhudumu alimueleza kila kitu Daniel, na kumuhakikishia kuwa anamtambua huyo mtu endapo atatokea tena katika baa ile. Ingawa Mhudumu alisema huyo mtu hakuja tena katika baa ile tangu usiku wa tukio lile. Daniel Mwaseba hakuwa na wasiwasi, alimwambia Mhudumu kuwa atakuwa anaenda Baa kila siku. Na siku atakayoyokea tu huyo jamaa amkonyeze, kwa bahati nzuri siku ileile Tano alienda TigaTisa, na Daniel Mwaseba ndipo alipokonyezwa na yule Mhudumu.

Daniel Mwaseba pale alipokaa alimuona vizuri sana Tano. Bila wasiwasi wowote Tano alichagua meza moja iliyokuwa tupu na kukaa. Yule Mhudumu alienda Kumsikiliza Tano. Kisha alirudi tena kaunta kuchukua alichoagizwa. Daniel Mwaseba alimshuhudia Mhudumu akipeleka bia mbili katika meza ya yule jamaa, kisha akaondoka. Daniel Mwaseba alinyanyuka pale alipokaa na kuifuata ile meza aliyokaa Tano...

ITAENDELEA MUNGU AKIPENDA
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA SABINI NA TANO

Ghafla, Tano aliushuhudia ugeni asioujua katika ile meza yake. Tano alimwangalia kwa umakini mkubwa sana yule kijana mgeni aliyeivamia meza yake bila kukaribishwa. Yule kijana nae ( ambaye sisi tunamtambua kama Daniel Mwaseba) alitulia tuli, kama hakuwa amefanya jambo lolote lile ajabu. Baada kama ya dakika moja ya ukimya, Daniel alimuita Mhudumu wa Baa ile kwa kutumia ishara ya mkono. Mhudumu alienda kwa mwendo wa taratibu akiwa anatetemeka, alijua anaitwa ili akayaeleze pale yote aliyomwambia Daniel Mwaseba jioni ya siku ile. Lakini haikuwa hivyo, alipofika pale Daniel alimuagiza maji makubwa ya baridi aina ya Kilimanjaro. Wakati Mhudumu akienda kuchukua maji. Ndipo Daniel alijitambulisha kwa yule jamaa mwenye mwili wa kibabe.

"Naitwa Daniel Mwaseba.." Alivyolitaja tu hilo jina, kwa kutumia macho yake makini ya kipelelezi, Daniel Mwaseba aliona mstuko alioupata yule jamaa, ulikuwa mstuko mkubwa ulioiacha sura yake ikiwa katika hali ya kutahayari. Bila shaka Tano hakutegemea kabisa kukutana na mtu mwenye jina kama lile.
Kabla Daniel hajaongeza kitu chochote, Mhudumu aliyaleta maji ya Kilimanjaro makubwa aliyoyaagiza Daniel Mwaseba. Akayaweka juu ya meza pamoja na glasi ya wastani. Mhudumu aliondoka huku uwoga ukitapakaa hadi katika mwendo wake.
Daniel Mwaseba alifungua ile chupa kubwa ya Kilimanjaro, akamimina maji nusu katika glasi, akanywa funda moja dogo. Alitulia akiyaruhusu maji yale ya baridi kupenya katika koo lake. Aliyefanya hayo yote kwa umakini mkubwa sana. Kuhakikisha yule jamaa hafanyi ujanja wowote ule.
Kwa upande Tano hakuwa tayari kabisa kulisikia jina la Daniel wakati ule. Mara nyingi sana alishazisikia sifa na umahiri wa Daniel Mwaseba katika mapambano. Kwa bahati mbaya zaidi alikuwa amekutana na Daniel Mwaseba akiwa mgonjwa, mgonjwa wa goti aliloumizwa na Dokta Yusha. Tano alijutia kitendo cha kuachana na wenzie kimoyomoyo, wangekuwa wote labda wangeweza kumkabili Daniel Mwaseba na kumzidi mbinu. Tano alitafakari kwa kina afanye nini ili anusurike katika kisanga kile, lakini hakupata, akili ilikuwa inagoma kabisa kuwaza. Kila akiwaza akili ilikuwa inamrudisha palepale mezani na mbele yake alikuwa anatazama na mpelelezi mahiri nchini Tanzania, Daniel Mwaseba....

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA
 
Itaendelea kesho mjukuu usikae mbali na JF.....Jaman maoni na ushauri unaruhusiwa...kutabiri matukio ya nayofuata pia ruhusa
 
Mh bora aliwaacha wenzie tano anaweza kukamatwa na kufichwa wenzie wasijue alipo
 
Itaendelea kesho mjukuu usikae mbali na JF.....Jaman maoni na ushauri unaruhusiwa...kutabiri matukio ya nayofuata pia ruhusa

Simulizi tamu sana mkuu,sema kuna errors ndogondogo,mfano ktk sehem ya kwanza makubaliano yalisema mioyo 12 kwa siku...ila mbele ukaanza kusema ni 15

But all in all nimeipenda,maana mwanzo nilivyoona title yake nkahic labda ni ile hadithi ya "USIKU WA BALAA" nilikuwa naikubali sana ile
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA SABINI NA SITA

"Unaitwa nani mwenzangu?" Daniel aliuliza kwa sauti yake ya upole yenye kuonesha urafiki.
Jamaa hakujibu, alikaa kimya kama hajaulizwa kitu.
"Usinilazimishe nitumie nguvu kijana, nina nguvu za kukufanya chochote!" Sasa Daniel alisema kwa ukali kidogo.
Tano alimwangalia tu Daniel Mwaseba, huku akitafuta namna sahihi ya kutoa bastola yake iliyokuwa kiunoni kwake.
"Huwezi kuniwahi kwa bastola yako iliyopo kiunoni"
Daniel alikijibia kitu ambacho Tano alikuwa anakiwaza tu kichwani kwake. Tano alistuka sana! Licha ya kusomea saikolojia ya wahalifu Daniel Mwaseba alikuwa na kipawa cha kutambua vitu vinavyopita katika kichwa cha Mhalifu.
Daniel hakuujari mstuko wa Tano wa Six Killers. Yeye aliuliza swali lengine kabisa .

"Kwanini ulimuua Mwanasheria?"
Tano hakujibu kitu, aliendelea kuwa bubu.
"Naona umeshindwa kunijibu hapa tukiwa kama rafiki, sasa utanijibu mahala pengine tukiwa kama maadui"
Daniel Mwaseba alichomoa bastola na kumuonesha Tano kwa siri sana. Hakuna mtu mwengine wa pembeni aliyeweza kuiona ile bastola kwa jinsi alivyooneshwa zaidi ya Tano mwenyewe.
"Hii bastola nzuri sana, halafu ina kiwambo cha kuzuia sauti. Naweza nikakufumua kichwa chako kimyakimya bila mtu yoyote kutambua sababu ya kichwa chako kutawanyika! Naomba ufuate nitakachokuelekeza"
Uso wa Tano ulistuka sana kutokana na kauli ya kitisho toka kwa Daniel Mwaseba.
"Nyanyuka taratibu na utoke nje ya baa hii, nakuomba twende kirafiki, ujanja wowote ule utakaoufanya inamaanisha unakitafuta kifo chako kwa nguvu!"
Tano aliishiwa ujanja, hakuwa na chochote cha kufanya, alikutana na mjanja wa wajanja, alitoka nje taratibu huku akifuatwa kwa nyuma na Daniel Mwaseba kwa umakini mkubwa sana.

Safari yao iliishia katika nyumba ya kulala wageni aliyofikia Daniel Mwaseba, pembezoni mwa bahari ya hindi, Kimbilio lodge. Huku njiani wakitembea kama marafiki wa kweli. Watu waliopishana nao njiani bila kuhisi hatari yoyote kati ya watu hawa wawili, laiti wangejua vitu vilivyokuwa vinazunguka katika vichwa vya watu hao wawili...

ITAENDELEA MUNGU AKIPENDA
 
Back
Top Bottom